Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Alex Raphael Gashaza (8 total)

MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-
Jimbo la Ngara ni miongoni mwa Majimbo tisa ya Mkoa wa Kagera yenye tatizo kubwa la maji safi na salama katika vijiji vyake vingi; na Jimbo hili lina utajiri mkubwa wa vyanzo vya maji vikiwemo Mto Kagera na Mto Ruvubu pamoja na mlima mrefu kuliko yote ya Mkoa wa Kagera (Mlima Shunga) ambao kitako chake kinagusa hii mito yote miwili kiasi kwamba yakijengwa matenki makubwa kwenye kilele cha mlima huu, maji yanaweza kusambazwa kwa mtiririko Vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara, Biharamulo, Karagwe, Kyelwa na Chato:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia mito hii miwili ili kumaliza kabisa tatizo la maji katika maeneo yote tajwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mji wa Ngara una uhaba wa maji kama ilivyokuwa miji mingine iliyoko ndani ya Mkoa wa Kagera. Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba, imemwajiri Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni katika miji mitano iliyopo katika Mkoa wa Kagera na mji mmoja katika Mkoa wa Geita. Miji hiyo ni Ngara, Biharamulo, Kayanga/Omurashaka, Kyaka/Bunazi, Muleba katika Mkoa wa Kagera na Chato katika Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa ya upembuzi yakinifu uliofanywa na Mhandisi Mshauri huyo, Mto Kagera na Mto Rubuvu itakuwa ni mojawapo ya vyanzo vya maji vitakavyotumika katika Mji wa Ngara. Miji mingine itapata maji kutoka katika vyanzo vyenye uhakika vilivyopo katika Wilaya hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mhandisi Mshauri anaendelea na kazi ya usanifu wa kina na kuandaa makabrasha ya zabuni. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2017. Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Serikali itatenga fedha za ujenzi kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili ambayo imeanza kutekelezwa Julai, 2016.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-
Maporomoko ya maji ya Rusumo yanapatikana katika Jimbo la Ngara nchini Tanzania na Wilaya ya Kirehe nchini Rwanda kwenye mpaka wa Tanzania na Rwanda na maporomoko haya yanaweza kuwa kivutio kizuri cha kitalii.
Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti katika eneo hili ili liweze kurasimishwa kwa ajili ya shughuli za kitalii ili kuongeza pato la Wilaya na Taifa kupitia sekta hiyo ya utalii?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa maporomoko ya maji ya Rusumo yaliyopo Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, yana uwezo wa kuwa kivutio kizuri cha utalii katika Kanda ya Ziwa Victoria. Wizara iliwahi kutembelea eneo hilo na kushauri kuwa linaweza kutembelewa kama kivutio. Maeneo mengine yanayoweza kujumuishwa katika maporomoko hayo kama kivutio ni maeneo ya hifadhi za Burigi na Kimisi, Bioanuwai ya pekee katika katika misitu ya asili ya Minziro, mapango ya watumwa katika Kata ya Kenza na maporomoko ya maji katika Msitu wa Rubare pamoja na maji ya moto katika Msitu wa Mutagata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iko tayari kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kufanya utafiti unaoweza kuendeleza na kurasimisha maporomoko hayo na mandhari yake kuwa kivutio cha utalii kitakachoongeza pato la Wilaya na Taifa kwa ujumla.
MHE. ALEX R. GASHAZA Jimbo la Ngara lina mifugo mingi hususan ng’ombe na mbuzi, lakini kuna tatizo kubwa la maeneo ya kunyweshea mifugo kwa maana ya malambo/ mabwawa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Je, ni lini Serikali itaanza uchimbaji na ujenzi wa malambo/mabwawa kwa ajili ya kunyweshea mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwanza napenda kumpa pole sana rafiki yangu, Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, mpiganaji, Mbunge wa Ngara kwa maafa yaliyowapa Wanangara, lakini pia naomba kujibu swali sasa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Ngara ina mifugo mingi ambapo pia hali hii inasababishwa na mifugo kuhamia kutoka nchi jirani bila kufuata utaratibu. Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha Wilaya ya Ngara ina ng’ombe wa asili 70,000, ng’ombe wa maziwa 2,872 na mbuzi wa asili 190,000, mbuzi wa maziwa 169,000 na kondoo wa asili 14,600.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na Serikali ili kukabiliana na upungufu wa maji kwa mifugo. Serikali imekuwa ikitekeleza mkakati wa kujenga malambo ya maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mengi nchini tangu mwaka 2001/2002 kwa kupitia bajeti ya Wizara na kupitia miradi shirikishi ya kuendeleza kilimo katika Wilaya ya Ngara pia katika miradi iliyoibuliwa na jamii yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika juhudi hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kupitia ufadhili wa TASAF Awamu ya Tatu, inatarajiwa kujenga mabirika manne ya kunyweshea mifugo katika vijiji vya Magamba, Mumuhamba, Munjebwe na Nterungwe. Aidha, mradi unajenga bwawa moja katika kijiji cha Kasulo na miradi yote ya maji ya mifugo hadi kukamilika itagharimu jumla ya shilingi 135,569,900. Ujenzi wa malambo yote umekamilika, kilichobakia ni ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifugo. Jumla ya watu takribani 685 watafaidika na miradi hii.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-
Barabara ya Nyakahuwa – Rulenge – Murugarama yenye urefu wa Km 85 imeahidiwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami sambamba na barabara ya Nyakahuwa – Murusagamba tangu kipindi cha kwanza cha uongozi wa Awamu wa Nne lakini mpaka sasa barabara hizo hazijatengenezwa:-
Je, ni lini barabara hizi ambazo ni kichocheo cha maendeleo kwa Tarafa za Murusagamba, Rulenge, Kabanga na Jimbo la Ngara kwa ujumla zitaanza kutengenezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba nijibu swali la Mhehimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali kuzijenga barabara za Nyakahuwa-Kumubuga – Murusagamba (km 34) na Kumuguba – Rulenge – Murugarama (km 75) kwa kiwango cha lami ipo pale pale. Tayari Serikali imeanza mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kupata fedha za kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hizi utakaogharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika zipo katika hatua ya mwisho za ununuzi. Mradi huo utahusisha pia ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Rulenge – Kabanga Nickel (Km 32)
Mheshimiwa Spika, wakati maandalizi hayo yakiwa yanaendelea, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) itaendelea kuzifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hizi ili ziweze kupitika majira yote mwaka. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 454.74 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Nyakahuwa- Kumubuga – Murusagamba na shilingi million 457.3 kwa ajili ya maengenezo ya barabara ya Kumubuga – Rulenge – Murugarama.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo na tatizo kubwa la hali ya usalama katika Jimbo la Ngara tangu mwaka 1993 kutokana na kuwa mpakani mwa nchi za Rwanda na Burundi ambapo kuna mwingiliano mkubwa wa wageni/wahamiaji haramu kutoka nchi hizo.
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha Kanda Maalum ya Kipolisi katika Wilaya ya Ngara ili kudhibiti hali ya usalama?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi katika Kata ya Mabawe, Muganza, Kirushya, Mtobeye, Mbuba na Nyakisasa?
(c) Kwa kuwa Jeshi la Polisi Wilayani Ngara lina gari moja tu zima na lingine bovu bovu, je, ni lini Serikali itatupatia angalau magari mawili, moja kwa ajili ya Tarafa ya Rulenge na la pili kwa ajili ya Tarafa ya Murusagamba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alex Gashaza, Mbunge wa Ngara lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hali ya usalama katika Jimbo la Ngara kwa sasa imeimarika ikilinganishwa na miaka iliyopita. Wilaya ya Ngara imepakana na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Serikali imeweka mikataba ya ujirani mwema na nchi za Rwanda ambapo Jeshi la Polisi hufanya doria za pamoja mipakani.
Mheshimiwa Spika, kuna changamoto katika mipaka yetu na nchi ya Burundi inayotokana na kukosekana kwa amani katika nchi hiyo na kupelekea watu kuvuka mipaka. Aidha, Jeshi la Polisi nchini limeanzisha vituo vya ulinzi shirikishi ili kujenga uhusiano wa pamoja na wananchi ili kuimarisha hali ya usalama katika eneo hilo. Kwa sasa hali ya usalama katika eneo hilo imeimarika na hakuna haja ya Serikali kuanzisha Kanda Maalum ya Kipolisi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la uhaba wa vituo vya Polisi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Ngara na katika Kata za Mabawe, Muganza, Kirushya, Mtobeye, Mbuba na Nyakisasa. Aidha, katika Kata ya Muganza kitajengwa Kituo cha Polisi eneo la Mkalinzi kwa nguvu za wananchi ambapo katika Kata za Mabawe, Mtobeye, Mbuba na Nyakisasa Polisi hutoa huduma kupitia Vituo Maalum vya Operesheni vya maeneo ya Murugyagira, Rulenge, Kabanga na Bugaramo. Hata hivyo, Serikali itajenga vituo vya polisi katika maeneo hayo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-

Zamani kulikuwa na maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya Mifugo na Kilimo katika kutekeleza Sera ya Matumizi Bora ya Ardhi, lakini idadi ya watu inavyoongezeka, maeneo hayo yanavamiwa na kusababisha migogoro:-

Je, Serikali ina mpango gani juu ya kuanzisha Skimu ya Ufugaji bora na kilimo cha kisasa ili kuepukana na migogoro ya wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hapo awali yalikuwepo maeneo mengi yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya wafugaji nchini ambayo kwa sasa yamepungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la shughuli za kijamii kama vile kilimo, makazi na shughuli nyingine za kiuchumi. Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali nchini imetenga maeneo ya malisho kuyagawa kwenye vitalu na kuyatoa kwa wafugaji kwa ajili ya malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jukumu la kuanzisha “Scheme” za ufugaji wa kisasa unaozingatia kanuni za ufugaji wa kisasa, Serikali kupitia Wakala wa Mafunzo ya Mifugo Nchini (LITA) imeandaa mpango kabambe wa kuanzisha “Incubation Youth Center “ambapo vijana waliohitimu Vyuo vya katika ngazi ya Cheti na Diploma watapata fursa ya kuanzisha miradi ya ufugaji kwa vitendo kwa muda maalum chini ya wakala na watakapohitimu watakuwa na fursa nzuri ya kujiajiri kupitia ufugaji. Pia, watakuwa na fursa ya kuanzisha mashamba ya mfano katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imezindua rasmi mafunzo rejea kwa Maafisa Ugani na Wafugaji kuhusu ufugaji bora nchini nchi nzima. Mafunzo hayo yanakusudiwa kutolewa kwenye Halmashauri zote nchini na yameanza kutolewa katika Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara ambapo wafugaji 750, Maafisa Ugani 32 walipata mafunzo rejea na katika Wilaya ya Kaliua, Mkoa Tabora mafunzo rejea yalitolewa kwa wafugaji 438 na Maafisa Ugani 33.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo hayo yamejikita katika uboreshaji wa Kosaafu za mifugo, udhibiti wa magonjwa, matumizi sahihi ya madawa na viuatilifu, uboreshaji wa viuatifu, uelewa wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Sekta ya Mifugo ili kuepukana na migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Aidha, mafunzo yanalenga kuwaongezea wafugaji maarifa kwa kuwapatia teknolojia mpya ili kuhamasisha Ufugaji wa Kisasa na Wakibiashara nchini. Mpango huu unalenga kuongeza uzalishaji wa malighafi zitokanazo na mifugo yenye viwango bora ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya nyama maziwa na ngozi vinavyoendelea kujengwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na juhudi hizo, Wizara imeendelea kuhamasisha wafugaji kuanzisha maeneo ya kuzalisha malisho bora ili kuongeza uzalishaji. Pia Wizara imeanzisha mashamba darasa ya mfano 365 katika maeneo mbalimbali nchini ili kuchochea wafugaji kujifunza na kuzalisha mbegu na malisho.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-

Katika Jimbo la Ngara wapo wachimbaji wadogo wa madini ya Manganese katika Kata ya Murusagamba, Kijiji cha Magamba na tayari wamepata soko la madini hayo nje ya nchi ikiwemo India, Afrika Kusini na Uturuki:-

Je, Serikal iko tayari kutoa kibali kwa wachimbaji hao kuuza madini hayo yakiwa ghafi kutokana na kwamba hakuna mitambo ya uchenguaji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imendelea kusimamia Sekta ya Madini kikamilifu kwa kuhakikisha shughuli za uchimbaji na biashara ya madini zinafanyika kwa kufuata sheria na taratibu za nchi ili rasilimali hiyo iweze kutoa mchango kwa Serikali kupitia malipo ya tozo stahiki za madini na pia itoe fursa ya ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Madini na kwa kuwa rasilimali hiyo siyo jadidifu (non renewable), mwaka 2017 ilifanya marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na kutunga sheria mpya ya Mali na Urithi wa Asili (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act, 2017) ambayo imerasimisha umiliki wa rasilimali madini kwa Taifa. Kupitia sheria hizo, Serikali imetoa zuio la usafirishaji wa madini ghafi pamoja na makinikia nje ya nchi ili kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini nchini ambayo itatoa fursa ya ajira kwa Watanzaia na pia kutekeleza dhima ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia changamoto inayowakabili wachimbaji wadogo wa madini ya viwandani yakiwemo madini ya manganese, Serikali inakamilisha utaratibu unaotumika katika kipindi cha mpito hasa kwa wachimbaji wadogo waliokuwa wamezalisha madini yao na kulipia tozo zote za Serikali kabla ya zuio hilo.
MHE. ALEX R. GASHAZA aliuliza:-

Wakati wa Mkutano wa Bunge wa Bajeti niliwasilisha Orodha ya Vijiji 11 vinavyohitaji kujengewa minara ambavyo ni Chivu, Runzenze, Kigina na Ntoboye Kata ya Ntoboye, Murubanga, Kititiza, Kumubuga Kata ya Nyamagoma, Kijiji cha Mukalinzi Kata ya Muganza na Kijiji cha Ruhuba Kata ya Mbuba:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa minara hiyo ili kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa vijiji hivyo hasa ikizingatiwa kuwa vijiji hivyo viko pembeni mwa Jimbo na hali ya usalama katika maeneo hayo siyo nzuri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Ngara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Kata za Ntoboye, Nyamagoma, Muganza na Mbuba zipo pembezoni mwa Jimbo la Ngara. Katika Kata ya Mbuba, vijiji vya Kumwendo, Mbuba na Kanyinya tayari vimepata mawasiliano. Pia Kata ya Muganza Kijiji cha Mukabu kimepata huduma ya mawasiliano pia. Aidha, Kijiji cha Mukalinzi utekelezaji wa upelekaji mawasiliano utakamilika mwezi Septemba mwaka huu 2019 ambapo ruzuku ilitolewa kwa Kampuni ya Viettel au Halotel.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Chivu, Runzenze, Kigina na Ntoboye Kata ya Ntoboye, Murubanga, Kititiza, Kumubuga Kata ya Nyamagoma na Kijiji cha Ruhuba Kata ya Mbuba vitafanyiwa tathmini kwa kuangalia mahitaji halisi na kisha kuingizwa katika orodha ya miradi itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2019/2020.