Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Alex Raphael Gashaza (17 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Wizara hii ni Wizara Mtambuka, ni Wizara nyeti, ni Wizara inayolitangaza Taifa, ni Wizara inayotangaza fahari za Taifa, ni Wizara ambayo ina umuhimu wake. Najua wachangiaji waliotangulia wamechangia mambo mengi na nitasisitiza katika mambo kadha wa kadha. Nianze tu kwa kujikita kwenye bajeti yenyewe, nikimpongeza Waziri Mwenye dhamana kwa hotuba nzuri aliyoitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii kulingana na umuhimu wa Wizara hii naweza nikasema kwamba upo upungufu hususan katika bajeti ile ya maendeleo kulinganisha na changamoto ambazo zinakabili Wizara hii. Ningeomba na ningeshauri kwamba kiasi kilichotengwa kwa ajili ya maendeleo kiongezwe ili kuweza kukabiliana na changamoto ambazo Wizara hii inakabiliana nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwanza kwenye upande wa utalii. Waliotangulia pia wamesema juu ya promotion katika sehemu hii ya utalii. Naweza nikasema kwamba promotion bado haijafanyika kwa kiasi cha kutosha, hasa promotion kwa utalii wa ndani. Ukijaribu kuangalia Watanzania walio wengi leo ambao angalau wana ufahamu, zaidi ya milioni 30 hawajui fahari, hawajui rasilimali za utalii ambazo tunazo sisi Watanzania. Kwa maana ya kwamba ni wengi ambao hawapati access kuingia kwenye vile vivutio vya utalii. kwa hiyo tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tuna-promote utalii wa ndani ili kuweza kuongeza pato katika sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia tunavyo vyanzo vingi ambavyo hatujavitumia vizuri ili kuweza kuongeza utalii. Vyanzo hivyo ni pamoja na fukwe ambazo tunazo katika bahari kuu, ukianzia Tanga, Dar es Salaam ukashuka mpaka Mtwara zipo fukwe nzuri ambazo tungezitumia vizuri zingeweza kuongeza utalii na kuongeza pato la Taifa. Kwa mfano, ukienda Maputo Msumbiji unaweza kuona jinsi ambavyo wamejaribu kutumia fukwe zao na zinaingiza pato kubwa la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia bado yapo maeneo ya asili ambayo hatujayatumia vizuri. Ukienda kwa mfano, Iringa kwenye zile palace za Ki-chief kwa Chief Mkwawa, leo inatumika kama kituo cha utalii. Kuna aliye-raise hoja ya mjusi mrefu duniani ambaye alitoka Tanzania na akapelekwa Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwakumbushe Watanzania pia kwamba katika harakati kama mnakumbuka wakati ule wa Vita vya Maji Maji hata Chief Mwenyewe Mkwawa mnakumbuka kwamba baada ya kuuawa kichwa chake kilichukuliwa kikapelekwa Ujerumani. Lakini tarehe 9 Julai, 1954, Kichwa chake kilirudishwa Tanzania na kikawekwa mahali maalum kama makumbusho kwenye palace ya Chief Mkwawa pale Iringa Kalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kupitia Wizara hii, kichwa cha Chief Songea ambacho nacho pia kilipelekwa Ujerumani ni wakati sasa wa kupaza sauti na kukirudisha, ili kusudi kiwekwe kwenye museum na hatimaye kiweze kuwa kituo cha utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna miundombinu pia ambayo haitoshelezi, haikidhi hususani katika maeneo ya utalii kwenye Wizara hii. Kwenye kitabu cha bajeti wameeleza juu ya kuongeza vifaa kwa ajili ya (patrol) ya doria kupambana na majangili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki wakati mwingine kufika kwenye maeneo ya utalii ni ngumu; niombe pia waweze kuongeza ndege kwa ajili ya shughuli yenyewe ya utalii, kwa sababu mahali pengine barabara hazipitiki, huwezi kwenda kwa magari. Kwa hiyo, wajaribu kuongeza pia ndege kwa ajili ya shughuli hizo za kitalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Jimboni kwangu, kwa sababu muda siyo rafiki. Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina takribani game reserve mbili. Kuna Game Reserve ya Burigi yenye hekta 13500 na kuna Game Reserve ya Kimisi ambayo ina takribani hekta 35,000. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba katika hifadhi hizi Jimbo langu la Ngara na Halmashauri yangu ya Ngara hainufaiki na chochote. Burigi Game reserve iliingizwa kwenye gazeti la Serikali tangu mwaka 1959, lakini mpaka leo ile tozo ambayo inatakiwa kurudishwa Halmashauri ya asilimia 25 kutokana na shughuli za uwindaji zinazofanyika haijawahi kutumwa hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Game Reserve ya Kimisi vivyo hivyo imekuwa gazetted tangu mwaka 2005, mpaka leo haijawahi kutolewa hata senti tano. Mbaya zaidi Kimisi Game Reserve sasa imekuwa ni kama kichaka cha majangili, wanaonufaika katika Kimisi Game Reserve ni wageni kabisa tofauti na Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa hii Kimisi Game Reserve unaanzia Rusumo boda unashuka kwenda Karagwe jirani kwa ndugu yangu Innocent Bashungwa. Kuna Kijiji cha Kashasha kule ni mpakani na Rwanda, upande wa Rwanda ni wananchi wanaishi pale. Game reserve yao ya Kagera iko ndani na ndiyo game ambayo wanaitegemea sana kwa upande wa Rwanda kwa ajili ya kuingiza kipato kama utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Tanzania unapovuka mto tu unaanza na pori na kule kuna wanyama, kule kuna ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo, kuna maziwa kama Ziwa Ngoma ambalo ziwa lile nafikiri halijawahi kufanyiwa utaratibu wa uvuvi au wa uwindaji mzuri. Kuna viboko wanaibiwa mle, tena wanaibiwa na watu kutoka Rwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kambi moja ya Wanyamapori iko Rusumo pale lakini nashindwa kuelewa wanafanya nini? Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri pamoja na changamoto iliyoko ya mifugo iliyoko mle ndani, lakini niseme kwamba changamoto ni usalama wa maeneo yale na mipaka yetu ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kama ambavyo upande wa Rwanda wamefanya kutengeneza kama Buffer Zone ambayo wananchi wanakaa wanaendesha shughuli za kilimo, basi na upande huu mwingine kwa ajili ya kuimarisha usalama, tuweze kuangalia namna gani tunaweza kuitumia ardhi ile kwa ufasaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina vivutio vingi vya kitalii. Tuna maporomoko ya Mto Rusumo, mto unaotenganisha Rwanda na Tanzania. Maporomoko yale ni maporomoko ambayo tukiyatumia vizuri ni kivutio kizuri sana cha kitalii. Bahati nzuri eneo lile ni eneo ambalo sasa lina miradi mikubwa. Kuna mradi wa umeme unaozalishwa pale, kuna daraja kubwa la Kimataifa ambalo limefunguliwa juzi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, kuna maeneo ambayo tukiyatumia tunaweza tukainua pato hususani katika sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna vilima vinaitwa vilima vitatu. Hivi vilima vitatu vinaunganisha nchi tatu ambazo ni washirika wa Afrika Mashariki, Tanzania, Rwanda na Burundi. Vilima vile ni kituo kizuri kinachoweza kuwa kituo cha kitalii kama Wizara hii inaweza ikawekeza katika eneo lile. Pia bado tuna pango ambalo lilikuwa linatumika kama root ya kupitishia watumwa wakati wa utumwa. Pango ambalo ni underground, unatembea kilomita tano uko ndani ya pango. Lile limegeuka kuwa ni pango kwa ajili ya maficho ya majambazi. Hili likiandaliwa vizuri, likatunzwa vizuri ni eneo ambalo linaweza likawa ni zuri sana kwa ajili ya kivutio cha utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo kadha wa kadha ambayo ningeweza kushauri. Kama nilivyotangulia kusema kwamba, Wizara hii ina changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na changamoto ya ujangili, naomba Serikali sasa ifanye mipango mikakati ya dhati kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inadhibiti hali hii ya ujangili, pia migogoro inayojitokeza ya wakulima na wafugaji. Pamoja na kwamba tumeshauri kuwa Wizara zote ambazo zinaingiliana ziweze kukaa pamoja na kuweka mipango ya pamoja, naomba ufanyike utafiti wa kuona ni namna gani ambavyo ardhi hizi, misitu hii, reserve hizi…
Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kwa mara ya kwanza ili niweze kutoa mchango wangu katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kuwepo katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Kumi na Moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukue nafasi hii pia kwa sababu nimesimama kwa mara ya kwanza kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara ambao wameniamini na kunipa nafasi hii; kwani hii ni mara ya nne nagombea; na wananchi wa Ngara wamekuwa na imani, Jimbo la Ngara limeshinda kwa kishindo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepata kura nyingi, Mbunge wa CCM amepata kura nyingi tofauti ya kura 18,000 dhidi ya Mpinzani wa CHADEMA, lakini pia Madiwani wote wa Kata 22 ni wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuonyeshe ni jinsi gani ambavyo wananchi wa Jimbo la Ngara lakini na Watanzania kwa ujumla walivyo na imani na Chama cha Mapinduzi na Serikali yake. Nachukua nafasi hii pia kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais. Sikupata nafasi ya kuchangia, lakini ni hotuba ambayo ilijaa weledi ambayo ilileta matumaini mapya kwa Watanzania.
Nachukua nafasi hii pia Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa Mpango huu ambao mmeuleta mbele yetu ambao pia unaleta matumaini. Ndugu zangu mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nje ya Bunge hili nilikuwa nikiangalia yaliyokuwa yakiendelea, wakati mwingine nilikuwa nachelea kujua kwamba ni nini, hususan upande mwingine. Ndungu zangu, ninajua kwamba maendeleo ni mchakato. Miaka 54 inayotajwa kwamba ni miaka 54 ya Uhuru ni muda mrefu, naamini ukilinganisha na yaliyofanyika ni mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanasahau kwamba tayari wanayo zaidi ya miaka 29 tangu mwaka 1992, lakini mpaka leo huwezi ukapima. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika kuchangia mpango huu. Vipo vipaumbele ambavyo vimeainishwa katika Mpango huu ikiwa ni pamoja na kipaumbele cha kilimo, kipaumbele katika Sekta ya Madini. Naomba niwarejeshe katika Mpango huu hususan katika ukurasa ule wa 34. Naanza kuchangia upande wa Utawala Bora. Nina uhakika kwamba huu nao ni msingi katika kutekeleza Mpango huu na msingi ambao unaweza ukatupeleka katika mafanikio katika Mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua zimekuwepo jitihada kubwa na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais alijaribu kuangalia akaona kwamba upande huu ni lazima tuushughulikie, ndiyo maana ameanza kuboresha sekta hii upande wa TAKUKURU kama chombo ambacho kinaweza kikasimamia na kuhakikisha kwamba pia utawala bora unafanyika, Mahakama na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze dhahiri kwamba pale ambapo Serikali itaweza kwenda sawasawa na kusimamia Mipango hii kwa umakini kwa kuzingatia Utawala Bora nina uhakika kwamba tunaweza kufanikiwa. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais kwa kutambua kwamba ipo mianya ambayo inasababisha tusiweze kupata mapato vizuri, lakini kwa lengo la kutaka kuimarisha utawala bora kwa maana ya kuziba mianya ya rushwa, kwa makusudi na kwa dhamira ya dhati akasema kwamba lazima sasa aanzishe Mahakama ya Mafisadi ya kushughulikia mafisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mkakati mahususi ambao utakapoenda kutekelezwa tuna uhakika kwamba Tanzania mpya itaonekana na Mpango huu utaweza kutekelezwa kwa umakini. Kwa sababu kwa kuziba mianya ya rushwa maana yake ni kwamba pia makusanyo ya Serikali yataweza kuongezeka. Makusanyo yatakapoongezeka, maana yake ni kwamba mipango hii itaweza kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaaminishe Watanzania na ninyi mtakubaliana na mimi kwamba kazi ya kiongozi ni kuonyesha njia na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tayari ameonyesha njia kwamba anayo dhamira ya dhati ya kuonyesha kwamba makusanyo yanapatikana, anayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba mipango hii inatekelezeka. Tunaongelea siku 100 za utendaji kazi wake, lakini matokeo tumeyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongeze Baraza la Mawaziri ambalo ameliunda, kwa sababu kwa kipindi hiki kifupi cha miezi miwili, mitatu tumeona matokeo ya kazi wanayoifanya Mawaziri hawa. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuwapongeza kwa sababu hii inaonyesha mwelekeo tunakokwenda kwamba itaweza kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika suala zima la madini. Tunajua kwamba eneo hili ni eneo ambalo ni nyeti na ambalo tuna uhakika na kuamini kwamba likisimamiwa vizuri linaweza likaendelea kuboresha na kuinua uchumi wa Tanzania.
Katika jimbo langu la Ngara yako madini adimu, madini ya Nickel, madini ambayo yanaifanya Tanzania iingie kwenye ramani ya dunia kuwa na deposit kubwa ya Nickel duniani kama siyo ya kwanza itakuwa ni ya pili. Ndiyo maana naunga mkono ujenzi wa reli ya kati pamoja na reli inayotoka Dar es Salaam kuja Isaka, kwenda Mwanza, Tabora, Kigoma, lakini pia mchepuko wa kutoka Isaka kuja Ngara ili kusudi mradi huu uweze kutekelezeka na nickel hii iweze kusafirishwa kwa ajili ya kupelekwa sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tunategemea kwamba ni mkubwa lakini ambao wananchi wa Ngara kwa muda mrefu wamekuwa wakiuangalia kama tumaini lao kwa ajili ya kusababisha ajira. Tangu mwaka 1973/1974 exploration ilianza. Tulitegemea miaka ya 2010/2012 kwamba mradi huu ungeanza lakini mpaka sasa hivi haujaanza. Kulikuwepo na excuse ya kwamba hakuna umeme. Nampongaza Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Profesa Muhongo, na timu yake akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wamejitahidi kuhakikisha kwamba sasa umeme unasambazwa katika Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongea na Meneja wa Kanda, TANESCO mchana huu akahiadi kwamba tayari Ngara inaunganishwa kwenye grid ya Taifa na bahati nzuri kwa Mpango ambao unaanza Januari mwaka huu, Ngara imepewa kipaumbele kwenye kuunganishwa kwenye grid ya Taifa. Bado pia tuna mradi mkubwa wa umeme katika maporomoko ya Rusumo, mradi ambao unashirikisha nchi tatu; Rwanda, Tanzania na Burundi. Kwa hiyo, naamini kwamba Ngara itaweza kupata umeme wa kutosha na ni eneo ambalo linaweza likawekezwa. Naomba mgodi huu wa Kabanga Nickel uangaliwe na uweze kuanza mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye suala la afya. Tuna hospitali moja tu ya Wilaya ambayo inahudumia zaidi ya watu takriban 400,000 lakini kipo Kituo cha Afya ambacho tangu mwaka 2006 Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara iliweza kuomba kupandishwa kuwa hospitali na Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka 2008 alitangaza kiwa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeandika barua mara kadhaa kwa ajili ya kuomba usajili wa kituo hiki kiweze kuwa hospitali; ni hospitali inayotegemewa kwa sababu ina vigezo vyote vya kuitwa Hospitali na barua ya mwisho ilikuwa ni ya mwaka 2013. Nimebahatika kukutana na Naibu Waziri wa Afya na amekubali kulishughulikia hili, naomba liweze kushughulikiwa haraka iwezekanavyo ili kuweza kunusuru afya za wana-Ngara ili Hospitali hii ya Nyamiaga iweze kutambulika kama hospitali na iweze kupata mgao ili iingizwe kwenye bajeti kwa ajili ya kuhudumia wananchi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni pamoja na Kituo cha Murusagamba ambacho Mheshimiwa Rais alishatangaza rasmi kwamba sasa kianze kupanuliwa kwa ajili ya kuwa hospitali kulingana na jiografia ya Jimbo la Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze pia katika suala la maliasili. Tunajua kwamba Halmashauri zina vyanzo vyao vya mapato. Kwa mujibu wa Sheria ya Maliasili, Jimbo la Ngara lina hifadhi mbili; Hifadhi ya Burigi na Hifadhi ya Kimisi. Hifadhi ya Burigi imeingizwa kwenye gazette la Serikali tangu mwaka 1974; Kimisi imeingizwa kwenye gazette la Serikali mwaka 2005. Kwa mujibu wa sheria hiyo kuna tozo ya asilimia 25 ambayo inatakiwa ingie kwenye Halmashauri kama own source, lakini kwa miaka yote hiyo kwa hifadhi zote hizi mbili hakuna hata senti tano ambayo imeingia kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri husika kwamba tozo hii ya asilimia 25 ianze sasa kuingia kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, lakini pia hata arrears kwa miaka yote hiyo ambayo haikuweza kutolewa kama tozo kwa ajili ya kuimarisha Halmashauri ya Wilaya ya Ngara iweze kutolewa kwa ajili ya kuongeza pato la Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nangana na waliotangulia, kwamba lazima retention hii iweze kukusanywa kwa ajili ya kuweka kwenye mfuko…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Gashaza, ahsante.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya na uzima kuwepo ndani ya jengo hili.
Pili, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi, kwa sababu tangu Mkutano wa Tatu umeanza nilikuwa sijapata nafasi ya kuchangia, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake na timu nzima kwa hotuba nzuri ambayo wameilata mbele yetu, hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja anatambua umuhimu wa nishati hii ya umeme kwamba ni nyenzo muhimu katika maendeleo na mageuzi ya kiuchumi katika nchi yoyote ile. Kila Idara, kila sekta na kila Wizara inaguswa na Wizara hii, kwa maana hiyo ni cross-cutting Ministry. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na nishati ya umeme, katika Wilaya yangu ya Ngara Jimbo langu la Ngara, nina kila sababu ya kuipongeza Wizara hii na kumpongeza Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika Jimbo langu la Ngara. Amenitembelea Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo ametembelea Naibu Waziri, ametembelea Waziri Mkuu katika kuzindua Mradi wa Orion Holland ambao utazalisha megawatt 2.5 kitu ambacho nina amini kwamba kinafungua fursa kwa wananchi wa Jimbo la Ngara na kwa Taifa kwa ujumla kuleta maendeleo na hasa katika sekta ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niendelee kukupongeza kwa jitihada zinazoendelea sasa kwamba kufikia mwezi wa nane mwaka huu Wilaya yetu ya Ngara itakuwa imeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, kwa hiyo, kuendelea kutupa fursa ya kuwa na umeme wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, Wilaya ya Ngara ni Wilaya ambayo mradi mkubwa ambao ninaweza kusema ni mradi ambao upo kwenye zile miradi ya flagship project ya umeme wa maporomoko ya Rusumo ambapo umeme huo utazalisha takriban megawatt 80, kati ya hizo megawatt 27 zitakuwa upande wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo kwamba wananchi wa Jimbo la Ngara wanafurahi na wanakupongeza kwa jitihada hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kwamba sasa tutakuwa na umeme wa kutosha ndani ya Jimbo la Ngara, kwa kuzingatia kwamba kwa sehemu kubwa tuna vijiji takribani 49 ambavyo mpaka sasa hivi havijafikiwa umeme, lakini kwa uhakika kwamba kufikia mwezi wa nane mwaka huu tutakuwa na umeme wa kutosha, wanataraji kwamba REA III sasa iweze kugusa vijiji vyote na vitongoji vyote takribani 240 ambavyo vimebaki ili kusudi umeme huu uweze kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye upande wa madini. Mheshimiwa Waziri anatambua kwamba Wilaya ya Ngara ni Wilaya ambayo ina madini mengi ambayo yanaweza yakaleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa Tanzania. Wilaya ya Ngara ina madini ya nickel na ndiyo maana hata katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ile reli ya kati wameelekeza kwenda Keza. Keza iko Ngara ambapo kuna madini ya nickel. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini haya ni madini ambayo kwa Tanzania yanaifanya Tanzania i-rank nafasi ya tatu duniani kwa kuwa na deposit kubwa ikitanguliwa na Russia pamoja na Canada. Kumekuwepo na vikwazo ambavyo vimepelekea mgodi huu wa nickel usianze, mgodi ambao umeanza utafiti tangu miaka 1973. Nina uhakika wengi wetu humu walikuwa hawajazaliwa, lakini mpaka leo mgodi huo haujaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu miaka 2002 kumekuwepo na ahadi kwamba mwaka kesho tutafungua, mwaka kesho tutafungua mgodi, lakini mpaka sasa hivi bado mgodi huo haujafunguliwa. Kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano umeeleza vikwazo vitatu ambavyo vilikuwa vinaonesha kwamba mgodi huu ili uweze kufunguliwa ni lazima vikwazo hivyo viwe vimeondolewa. Ni pamoja na kikwazo cha umeme, kikwazo cha miundombinu ya usafiri na kikwazo cha bei kwenye Soko la Dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikwazo hivyo viwili naweza kusema kwamba vimeondoka kwa sababu umeme sasa ambao tunategemea kuwa nao katika Wilaya hii ya Ngara ni umeme wa kutosha kuendesha mgodi huo na wananchi vijiji vyote wakapata umeme kwa matumizi ya majumbani na hata kwa matumizi ya viwanda vidogo vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mawasiliano kulingana na bajeti kwamba reli ya kati sasa kwa standard gauge ndani ya miaka mitatu, minne ijayo kwa maana kufikia mwaka 2019 yawezekana tayari reli hii ikawepo.
Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba madini haya muhimu na ambayo yanaweza yakaleta mabadiliko ya uchumi katika nchi yetu, inaonekana kama vile inasahaulika sahaulika kwamba madini hayo yapo na mradi huu upo. Kwa sababu hata kwenye kitabu hiki cha bajeti haikuonesha kwamba mradi huo unafikiriwa. Ndiyo maana hata wawekezaji katika mgodi huo (Barrick) leo ukiangalia hakuna shughuli zozote zinazoendelea pale mgodini, pamoja na kuomba retention ya miaka mitano kwa maana ya mwaka 2015 kwenda 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgodi haujengwi kwa siku moja, haujengwi kwa miaka miwili au miaka mitatu; tunahitaji kuona kwamba kunakuwepo na msukumo na kampuni hii ambayo inahusika pale iweze kuweka nguvu tuone jitihada. Sasa hivi wame-abandon site, hakuna kinachoendelea. Tunahitaji kuona jitihada zinazofanywa na Wizara hii kwa maana ya Serikali kuhakikisha kwamba wanapeleka miundombinu inayotakiwa, iende sambamba na jitihada zao katika kufanya maandalizi. Tunajua kufanya fidia siyo chini ya miaka miwili, wananchi hawajafidiwa.
Kwa hiyo, naomba Wizara iweze kusukuma kampuni hiyo ianze maandalizi ya ujenzi wa mgodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia katika Wilaya ya Ngara kuna madini ya manganese. Ipo kampuni ambayo sasa inafanya utafiti na uchimbaji pale. Nilikuwa najaribu kuteta na Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwamba mazingira yalivyo ya shughuli inavyofanyika, inahitaji wakajiridhishe. Tuna mashaka kwamba pengine hawakufuata taratibu na sheria za utafiti na uchimbaji. Barua ambayo mwekezaji huyu ameandikiwa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kanda Maalum, ni kwamba ni lazima awasiliane na Halmashauri na afuate taratibu na sheria za Halmashauri. Hakuripoti Halmashauri na mpaka sasa hivi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara imebidi kumwandikia barua kusitisha ili tuweze kupata ufafanuzi. Ninaamini kwamba hilo wataweza kulifuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye gesi. Baada ya kugundua gesi nchini Tanzania, imeonekana kwamba sasa ni tumaini la Watanzania wengi kwamba gesi hii itaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi na gesi hii maeneo mengi ndani ya nchi hii tunaitegemea ili iweze kusaidia kwa kuzalisha nishati ya umeme lakini pia hata kwa matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kuishauri Wizara hii ni kwamba tujaribu kuangalia ni namna gani ambavyo tunaweza ku-establish substations ambazo zitatumika kwa ajili ya kusambaza gesi hii katika maeneo mbalimbali ikiwezekana kutenga substations hizi kikanda ili kusudi wananchi wote waweze kunufaika na gesi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba yapo makampuni kadha wa kadha ambayo yako tayari kuja kuwekeza kwa maana ya kutumia gesi hii na kufanya uzalishaji wa umeme. Kuna kampuni kutoka Uturuki, kuna kampuni kutoka maeneo mbalimbali ambao wanatamani waingie Tanzania kwa ajili ya kutumia gesi hii. Tunapoweza kukaribisha makampuni hayo, nina uhakika kwamba yataweza kutusaidia katika kuzalisha umeme wa kutosha kutokana na gesi na kusambaza kwa wepesi zaidi na kuweza kuleta mabadiliko mazuri ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye madini ambayo ni unique, madini ya Tanzanite. Kwa muda mrefu tumekuwa tukipiga kelele kwamba inakuwaje Tanzanite ambayo ni madini yanayozalishwa Tanzania peke yetu tunakuja kujikuta kwenye Soko la Dunia Tanzania tuko nyuma; eti nchi kama Kenya na South Africa ndio ambao wanaonekana kuuza na kuteka soko la Tanzanite! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatutia aibu. Hebu niombe Wizara husika iweze kujikita na kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukawa na umiliki wa Tanzanite kama fahari ya Tanzania na madini ambayo yanaweza yakainua uchumi wa Tanzania na kuleta manufaa kwa watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika hili, hata kama ni kutafuta wataalam wa kufanya utafiti ili kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukarejesha heshima ya madini haya, kama nembo ya Taifa hata kwa jina lenyewe kwamba ni Tanzanite kwa maana ya kwamba ni madini yanayopatikana Tanzania tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kwamba Wizara hii imejipanga na ndiyo maana hata katika bajeti yake imeonesha jinsi ambavyo matumizi kuelekea kwenye bajeti ya maendeleo imepewa kipaumbele kikubwa, asilimia 94. Zaidi ni pale ambapo nimefarijika kwamba katika fungu hili la maendeleo takribani asilimia 68 ni bajeti ya ndani ni fedha za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha kwamba ni rahisi na tutaweza kufanikiwa kutekeleza miradi hii ambayo tumeipanga kwa sababu ya own source kwa maana ya kwamba ni pesa za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimtie moyo Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini; unajua wakati mwingine unapoenda kufanya kitu kizuri wengine hawakubali, ndiyo maana mtu mmoja akasema kwamba don’t focus on barriers or obstacles, always focus on your destiny.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba Wizara hii chini ya Profesa Muhongo, mmeamua kuleta mabadiliko makubwa ndani ya nchi hii kwa sababu viwanda vitapatikana kutokana na nishati ya umeme, huduma bora za afya zitapatikana kutokana na nishati ya umeme kwa maana ya kutumia mitambo, Ultra Sound na CT-Scan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ubora wa huduma ya afya kwa Mtanzania inatokana na nishati ya umeme. Just keep on, usibabaike, songa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia taarifa za Kamati hizi mbili, Kamati ya UKIMWI na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kupongeza Kamati hizi kwa kazi nzuri walioifanya na niwapongeze waliotangulia kuchangia. Mengi wameyagusa, mimi nijielekeze tu kwanza kwenye suala la elimu.
Mheshimiwa Mwenekiti, kama wengine walivyotangulia kusema hakuna namna ambavyo Taifa lolote lile linaweza kuendelea kama bado halijaweza kuelimisha watu wake. Kwa kutambua kwamba kupitia elimu ndipo unapoweza kuwa na rasilimali watu iliyo bora na zaidi hasa katika kujenga msingi. Ukijaribu kuangalia rasilimali hii muhimu tunaanza kuipoteza kuanzia darasa la saba, tunakuja sekondari kwa maana kidato cha nne pale ambapo tunajikuta tumehamasisha, tumejenga shule nyingi za kata tukitegemea watoto wetu waweze kupate elimu hii na waweze kuendelea hadi vyuo vikuu lakini kwa matokeo kwanza ya mwaka huu ya kidato cha nne unaweza ukaona ni rasilimali kiasi gani ambayo itabaki nyuma huku vijijini ambayo ni nguvu kazi vijana kama hatukuweka mpango mahsusi kwa ajili ya kuona ni namna gani ambavyo rasilimali hii tunaweza tukaiboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamejaribu kuweka mpango wa kuanzisha vyuo vya VETA. Niombe mpango huu usiwe katika karatasi tu, uwe ni mpango unaotekelezeka, vinginevyo kama tutaendelea kupoteza rasilimali hii muhimu, kila mwaka vijana wetu wanamaliza kidato cha nne, zaidi ya 60%, 70% wanabaki vijijini, hawana ujuzi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza rasilimali hii muhimu na hasa ukizingatia tunajipanga sasa Taifa hili liweze kuwa linajenga uchumi kuelekea kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda. Hakuna namna tunaweza kufaulu kama tusipoweza kuiandaa hii rasilimali muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na huduma zinazotolewa katika shule zetu, kuna kitu ambacho napenda Kamati wajaribu kuangalia. Sijui maeneo mengine lakini katika Jimbo langu la Ngara mara kadhaa kumekuwepo na tatizo la radi hususani katika maeneo ya shule. Mwaka jana tulipoteza wanafunzi watatu katika shule ya sekondari Kanazi kwa kupigwa na radi, lakini pia katika Kata ya Nyamagoma tulipoteza wananchi watatu kwenye familia moja ambao wako karibu na shule ya msingi na maeneo kadha wa kadha. Kwa hiyo, niombe…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja za Kamati zote mbili.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijalia kuiona jioni hii ya leo. Pia, nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya kusimamia Kanuni na Sheria za Uendeshaji wa Bunge. Mungu akutie nguvu na akupe afya ili uendelee kukalia Kiti hicho mpaka tunapomaliza Bunge hili la Bajeti, tarehe Mosi, Mwezi wa Saba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango, Naibu Waziri wa Fedha na timu yao kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kuandaa mpango huu wa Bajeti ya Mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii iliyofanyika ni kubwa na hii kazi imefanywa na binadamu. Yamkini kukawepo na upungufu sehemu, lakini kwa sehemu kubwa, mambo makubwa yamefanyika na ambayo kwa hakika yanatupa dira na mwelekeo wa kuwa na Tanzania ya tofauti, Tanzania ya viwanda, Tanzania ya uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na eneo la maji na umwagiliaji, sehemu ambapo wachangiaji wengi waliotangulia kama si Wabunge wote wanagusia eneo hilo kwa sababu ndilo eneo ambalo sasa linamgusa kila Mtanzania na ndilo eneo ambalo lina kero kubwa kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamejitahidi sana katika kuweka bajeti kwa ajili ya kutekeleza miradi hii kama ambavyo hata wakati wa uwasilishaji wa Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji alisema kwamba, tunahitaji sasa kwa miaka mitano ijayo kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukamwondolea adha huyu mwana mama Mtanzania anayeishi kijijini kubeba ndoo ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili niseme bado ipo kazi kubwa ya kufanya na niungane mkono na waliotangulia kuchangia kwamba, katika kuondoa kero hii au tatizo hili, lazima tufanye maamuzi, sisemi kwamba, ni maamuzi magumu, lakini tuzingatie ushauri ule ambao kila mmoja anaposimama anajaribu kuutoa. Ili kuondoa kero hii, lazima tujibane na tutafute ni mahali gani ambapo tunaweza tukapata fedha kwa ajili ya kuongeza kwenye Mfuko huu wa Maji hususan maji vijijini na si kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane mkono na waliotangulia kwamba tozo ya sh.i 50/= kwa kila lita kwenye mafuta, hebu tujaribu kufanya uamuzi huo tuipeleke kule ili tuongeze Mfuko huu na tuweze kutatua kero hii. Nasema hivi kwa sababu mifano iko hai, ukiangalia hata katika bajeti iliyotengwa nina uhakika kwa maka wa fedha 2016/2017, hata viporo ambavyo bado havijakamilika hatuwezi kuvikamilisha kwa bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kwenye Jimbo langu la Ngara, kwa miradi ile ya vijiji 10 tu, mkataba ulikuwa ni bilioni tano nukta, mpaka sasa hivi Wakandarasi wameshalipwa bilioni mbili nukta sita, maana yake bado bilioni mbili nukta tano. Kwenye Bajeti hii, Fungu la Maji lililoenda kule ni bilioni mbili tu ambayo haitoshelezi hata kuwalipa Wakandarasi kama watamaliza miradi ile. Kwa maana hiyo, mwaka 2016/2017 hakuna miradi mingine itakayofanyika pamoja na kwamba kuna Kata nyingi ambazo zina tatizo la maji ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ngara Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana nasema kwamba, lazima tuzingatie tuone ni namna gani tunavyoweza kuongeza kwenye Mfuko huu wa Maji hususan maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa sababu kauli mbiu ni kuwa na Tanzania ya Viwanda, lazima kuwe na uzalishaji na uzalishaji huo unatoka mashambani na huko ndiko waliko Watanzania, wananchi walio wengi takribani asilimia 70, ambao wanafanya shughuli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri hata Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwenye hotuba yake ya Bajeti amekiri kwamba, hapo kuna changamoto kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna namna ambavyo tunaweza tukaleta mabadiliko ya viwanda kama hatutajikita na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji ili tuweze kulisha viwanda vyetu na ili tuongeze uzalishaji, ni lazima tuingie kwenye kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu kuna mabonde makubwa takribani hekta 5,000 na zaidi. Wizara ilishafanya survey ikaonekana yapo mabonde matano makubwa ambayo yakifanyiwa kilimo cha umwagiliaji yanaweza kubadilisha uchumi wa wana Ngara, lakini kuongeza pia pato la Taifa. Kwa sababu kundi hili linapokuwa maskini, linapokuwa halizalishi, maana yake halilipi kodi, kwa maana hiyo inazidi kuvuta hata wale wachache wanaolipa kodi, GDP ya Taifa inashuka kwa sababu ya kundi hili ambalo halijaangaliwa kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa Bigombo - mradi wa umwagiliaji, ambao ulikuwa ukamilike tangu mwaka 2013. Mradi ule kama ungekuwa umekamilika ungeweza kuzalisha tani nyingi sana za mazao kutoka kwenye kilimo cha umwagiliaji, lakini kwenye Bajeti hii bado haikutengewa fedha pamoja na kwamba mradi ule umefikia kwenye asilimia 80. Badala yake zimetengwa bilioni karibu mbili kwa ajili ya mabonde mengine mawili kwa kufanya upembuzi yakinifu na detailed design kwa ajili ya kuja kuanzisha haya mabonde mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Mheshimiwa Waziri kwamba katika eneo hili, kwa sababu tayari lipo bonde ambalo mradi ulishaanza na uko kwenye asilimia 80 basi, kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya kwenda kwenye upembuzi yakinifu kwa mabonde mengine kiweze kuhamishiwa hapo ili kumalizia huo mradi na wananchi wa Ngara waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sheria ile ya Kodi, imejaribu kueleza juu ya kuondoa msamaha wa kodi hususan kwa ile Pay As You Earn kwa wafanyakazi. Ukijaribu kuangalia dhamira ya Serikali ni njema kuhakikisha kwamba, inapunguza ile kodi kutoka kwenye digit mbili na kubakia kwenye digit moja. Ukiangalia kwenye Bajeti hii…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi hii na kunijaalia uzima na afya, lakini pia nichukue nafasi hii kumshukuru Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu Wizara hii, Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi kwa kazi kubwa wanayoifanya na nzuri. Tunajua zipo changamoto kadha wa kadha ambazo huwezi kuzikwepa.

Nichukue nafasi hii pia kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano kwa kazi ambayo inafanyika chini ya Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza na miradi ya maji, Wabunge wengi wamelalamika kuona jinsi ambavyo miradi mingi ya maji ambayo imeanza kwa muda mrefu hasa miradi ile ya vijiji kumi, imechukua muda mrefu kukamilika. Niombe kwa sababu hili limejitokeza pia hata kwenye Jimbo langu la Ngara, miradi ile ya vijiji kumi bado mpaka sasa hivi haijakamilika. Niombe kwamba sasa tuweke nguvu kubwa katika miradi hii ambayo tumewekeza fedha nyingi takribani shilingi bilioni 5.1 kwenye Wilaya yangu ya Ngara iweze kukamilika ili wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, sambamba na miradi hiyo ya vijiji kumi, kuna vijiji viliongezwa kufikia 13 ambavyo ni vijiji vya Kabalenzi, Murugarama na Kumbuga Kata ya Nyamagoma. Vijiji viwili kati ya hivyo vipo kwenye programu inayoendelea na miradi inakaribia kukamilika. Kipo kijiji cha Kumbuga, Kata ya Nyamagoma, vilichimbwa visima vitatu tangu mwaka 2014 wakamaliza kuchimba lakini pampu hazikufungwa wala DP hazikujengwa ili kuwafikia watumiaji. Kwa hiyo mradi ukatelekezwa. Niombe sasa kwamba mradi huu wa kijiji hiki cha Kumbuga ambapo wananchi wanahangaika, wanatembea zaidi ya kilometa 16 kwa maana ya kilometa nane kwenda na kurudi kufuata maji, mradi huu ukamilike, zinunuliwe pampu zifungwe na DP zijengwe ili wananchi waweze kupata huduma za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba hili litafanyika kwa sababu mmeniongezea pia miradi ya vijiji vitatu; Kijiji cha Mrugina, Mkariza Kata ya Mabawe na Kijiji na Kanyinya Kata ya Mbuba. Kwa maelekezo yaliyotolewa ni kwamba mradi huu wa Kumbuga utaunganishwa kwenye vijiji hivyo, niombe basi kwa sababu tayari wataalam wako site kwa ajili ya kufanya survey kwenye vijiji hivi vitatu na baada ya hapa watatengeneza BOQ kwa ajili ya kutangaza tender, niombe kijiji hiki cha Kumbuga kisisahaulike, kiunganishwe ili iweze kufanyishwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka jana aipotembelea Ngara tuliomba pump akatupatia shilingi milioni 13, tukaomba shilingi milioni 24 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji mjini, tukapewa. Vile vile akatupatia shilingi milioni 75 kwa ajili ya eneo la K9 ambapo kuna kiteule cha Jeshi pamoja na shule mbili za sekondari. Mradi huu unaendelea vizuri, wameshafunga pump, umeme umeshafika kwa hiyo tunaamini kwamba wananchi wataanza kunufaika muda si mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kuna mradi mkubwa ambao niliomba wa kutumia chanzo cha Mto Ruvuvu na kutumia kilele cha mlima Shunga ambao ndio mlima mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera ambapo yakijengwa matenki makubwa pale yanaweza yakapeleka maji kwa mtiririko na kwa gharama nafuu Wilaya nzima ya Ngara, Biharamulo, Karagwe kuendelea mpaka hata Mkoa wa Geita kwa maana ya Mbogwe, Bukombe mpaka Chato. Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikifuatilia juu ya hili, nishukuru kwa ushirikiano ambao umenipa na Katibu Mkuu na niliahidiwa kwamba zitatengwa shilingi milioni 200 kwa ajii ya kuanza usanifu.

Mheshmiwa Spika, hata hivyo nimejaribu kuangalia kitabu cha bajeti nimeona fedha za jumla, kwamba kwenye Jimbo langu la Ngara wamenitengea shilingi bilioni 1.7, kati ya hizo shilingi bilioni 1.05 ikiwa ni fedha za ndani. Hakuna mchanganuo lakini nitaomba Waziri atakapokuja kuhitimisha basi unipe ufafanuzi kama hizi shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuanza usanifu wa mradi huu zitakuwa ziko kwenye fungu hili ili angalau niweze kupata amani na wananchi wa Jimbo la Ngara waweze kuamini kwamba sasa tatizo la maji likuwa historia katika Wilaya yetu ya Ngara na Wilaya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona katika ukurasa wa 195 katika miradi ile itakayotekelezwa katiak mikoa 17 ukiwemo Mkoa wa Kagera ni Mradi wa Rusumo ambao umeelezwa hapa. Mradi huu najua kwamba utatekelezwa katika vijiji vitano; vijiji vitatu vya Kata ya Rusumo ambavyo ni
Nyakahanga, Mshikamano na Kasharazi na vijiji viwili Kata ya Kasulu ambavyo ni Rwakalemela na Nyakariba na hapa imeonesha kwamba fedha hizi zilizotengwa, takriban shilingi bilioni moja ni kwa ajili ya mikoa hii 17.

Mheshimiwa Spika, nitaomba Waziri atakapokuja kufanya majumuisho basi niweze kuelezwa kwamba kwenye mradi huu wa Rusumo ambao utatekelezwa kwa ubia wa Serikali na NELSA ni kiasi gani ambacho tumekuwa tumetengewa kwa ajili ya kuanza kufanya feasibility study, detailed design na kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mhandisi mshauri.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye umwagiliaji, nchi ya Misri wanatajirika na uchumi unakua kwa kasi kutokana na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Bonde la Mto Nile. Mto Nile asili yake inatokewa kwetu huku Ngara, mto Kagera na Ruvuvu ambayo inapoungana ikaingia kwenye Ziwa Victoria, ndiyo inaenda kutengeneza mto Nile kule, sisi huku mito hii hatujaitendea haki. Sasa naomba kwamba kwenye upande wa umwagiliaji tuwekeze hapo.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia scheme ya umwagiliaji nchi nzima tumeshatumia tu asilimia 1.6 kwa hekta zaidi ya milioni 29 ambazo zinaweza zikafanya kilimo hiki. Niombe kwamba tuweze kutumia fursa hizi ili kuweza kuinua uchumi kwa kutumia scheme za umwagiliaji. Ipo scheme ya umwagiliaji ya Bhigomba ambayo ilishaanza tangu mwaka 1913, ilitakiwa ikamilike 2014, ilianza mwaka 2013 ikamilike 2014. Ilitumia gharama ya shilingi milioni 715 ambayo ilitakiwa kukamilisha mradi, lakini mpaka sasa hivi huo mradi haujakamilika, umetekelezwa. Ukienda kufanya tathmini sasa hivi, kwa tathmini iliyofanyika mwaka juzi inaonekana inahitajika karibuni shilingi milioni 185 ili kukamilisha mradi huo. Niombe kwamba sasa Wizara ya Maji kuukamilisha mradi huu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba mwezi uliopita tumepokea delegation kutoka Kuwait Fund kwa ajili ya kuangalia bonde la Mhongo, ili kuanza usanifu wa scheme ya umwagiliaji katika bonde hili. Niombe kwa sababu tunazo fursa, tuna zaidi ya hekta 5,000 katika Wilaya yetu ya Ngara ambapo tukiweza tuzitumie kwa scheme hii ya umwagiliaji. Kuna scheme tano ambazo tayari Serikali tulishaziingiza kwenye mpango.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tulitengewa bilioni mbili kwa ajili ya scheme ya umwagiliaji ya Mgozi, Kata ya Mbuba na Mhongo, Kata ya Bukirio lakini fedha hizo hazikutoka. Scheme ya umwagiliaji kwenye bonde hili la Mgozi hata kwenye bajeti hii ya mwaka huu haikuwekwa. Kwa hiyo niombe, kwa sababu ni fursa ambazo zinaweza zikainua uchumi wa wananchi wa Jimbo la Ngara ambao zaidi ya asilimia 80 ni wakulima basi tuwekeze hapo ili kusudi tuanze scheme hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba yapo mazao ambayo unaweza kulima katika maeneo ya kawaida, lakini yapo mazao ambayo huwezi kulima kwenye highlands, inatakiwa yalimwe kwenye maeneo ya mabonde ambapo unaweza ukafanya umwagiliaji na Ngara tumejipanga kwa sababu yapo mazao ambayo tunaendelea kufanyia utafiti ambayo tunaamini tukipata kilimo hiki cha umwagiliaji unaweza ukatumia hekta moja ukawa tajiri kama mazao haya ni kama vile stevia na chia seeds, Waheshimiwa wanajua kwamba tunaweza tukainua uchumi wa wananchi wetu, vile vile tukaboresha hali ya lishe na tukachangia Pato la Taifa. Kwa hiyo, niombe tuwekeze kwenye scheme za umwagiliaji ili kusudi tuweze kuinua kipato cha wananchi wetu na pia tuinue uchumi wa Watanzania, ikiwa ni pamoja na kupata malighafi za kulisha viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niunge mkono uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini, hii itakuwa ni suluhishi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba maji ni tatizo nchi nzima kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuchangia wameeleza. Natambua jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji kama mahitaji muhimu.

Maji ni kila kitu. Bila kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za maji katika maeneo yetu, hata baadhi ya mipango mingine ya maendeleo kwa ajili ya nchi yetu yanaweza yakakwama. Maji ni viwanda, maji ni kilimo, maji ni afya, maji ni mazingira na maji ni uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana mkono na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kusema kwamba bajeti hii ya Wizara iweze kuongezewa fedha angalau kuweza kufikia bajeti ya mwaka 2016. Ni kwa nini nasema hivi? Kwa bajeti ya mwaka unaoishia sasa 2016/2017, katika Jimbo langu la Ngara nilikuwa nimetengewa shilingi 2,000,045,000 kwa ajili ya mradi wa maji, kukamilisha miradi ambayo ilikuwa ikiendelea na ikiwezekana kuanzisha miradi mipya. Mpaka dakika hii ninavyoongea ni shilingi milioni zisizozidi 400 ambazo zimeshapelekwa kati ya shilingi 2,000,045,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye umwagiliaji zilikuwa zimetengwa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu katika mabonde mawili; Bonde la Mgozi na Bonde la Mhongo, lakini mpaka dakika hii hakuna hata senti moja ambayo imekwenda kule. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba ni vizuri tukaangalia kuongeza bajeti hii ili tuweze kuangalia mahali ambapo bado panahitaji kupata huduma hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji ukurasa wa 122, amekiri kupungua kwa rasilimali za maji katika maeneo mbalimbali; lakini ameendelea akakiri kwamba yapo maeneo ambayo yana maji mengi na maeneo mengine hayana maji. Nashauri kwamba kama kuna maeneo ambayo yana rasilimali kubwa ya maji, basi maeneo haya yaweze kupewa kipaumbele kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji na vyanzo vya maji viimarishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba usambazi wa maji ni endelevu kulingana na ongezeko la idadi ya watu, lakini tukishajenga katika maeneo yale ambayo tunaamini kwamba vyanzo ni reliable, maji ni mengi halafu tukaendelea kusambaza taratibu kwa kadri tunavyopata fedha, tutaweza ku--cover maeneo mengi ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkutano wa sita, niliuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji nikasema Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina vyanzo vingi vya maji. Tuna mito miwili, Mto kagera na Ruvuvu ambayo haikauki; ni maji mengi ambayo yakitumiwa vizuri yanaweza yakasambazwa kwenye mikoa mitatu, Mkoa wa Kagera, Geita na Shinyanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na jiografia ya Jimbo la Ngara kwamba liko kwenye mwinuko wa juu, actual ni kati ya mita 1,200 mpaka 1,800, kiasi kwamba ukiweza kuweka chanzo cha maji pale ukajenga matenki makubwa, tuna mlima mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera. Unaweza ukapeleka maji kutoka pale kwa mtiririko kwa gharama nafuu ukasambaza katika mikoa hiyo mitatu niliyoitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme na naendelea kusisitiza Mheshimiwa Waziri kwamba ajisumbue na siyo kujisumbua ni kutekeleza wajibu wake kwamba tunapomaliza Bunge hili, hebu atume team yake ya wataalam kufika Jimbo la Ngara waone vyanzo vilivyopo. Bahati nzuri Naibu Waziri, TAMISEMI tarehe 30, Desemba mwaka 2016 alifika katika Jimbo la Ngara akaona, nikamwonesha mito ile, nikamwonesha mlima huo, nikasema ukitumia vyanzo hivi tutatatua tatizo kubwa la maji katika eneo kubwa la nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado yapo maeneo ambayo mengine hayahitaji pesa nyingi, lakini unakuta ni kero ya muda mrefu. Kwa mfano, kuna eneo la K9 ambalo nimekuwa nikiomba maji kwa muda mrefu, linahitaji shilingi milioni 26 tu kwa ajili ya mtambo wa kusukuma maji na
kusaidia jamii ya wananchi waliopo pale. Kuna taasisi mbalimbali; Sekondari mbili, Kambi ya Jeshi na wananchi walioko pale. Ikipatikana shilingi milioni 26 mtambo unapatikana, unasukuma maji, kero inaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa umwagiliaji, hakuna namna ambavyo tunaweza tukaongeza uzalishaji kama tusipoweza kuboresha scheme za umwagiliaji. Jimbo la Ngara ni jimbo ambalo lina utajiri wa mabonde oevu na tayari kuna mabonde matano ambayo yaliainishwa na Serikali kwa ajili ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bonde moja lilishaanza scheme ya umwagiliaji; Bonde la Bigombo tangu mwaka 2012. Mradi huu ulikuwa ukamilike 2013, lakini mpaka sasa hivi mradi ule haujakamilika na inaonekana hata Wizara imesahau kabisa kwamba mradi huo upo kwa sababu Mkoa wa Kagera ni wilaya mbili tu; ya Muleba na Karagwe ambayo imeonesha kutengewa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Jimbo la Ngara kwenye mradi huu wa Bigombo hakuna hata senti iliyotengwa na wala haiko hata kwenye program, maana yake ilikuwa imesahaulika. Kwa hiyo, naiomba Wizara kwa sababu tayari tumeshawekeza pesa shilingi milioni 715 zilitengwa kwa ajili ya mradi huu na karibu zote zimesha-exhaust lakini bado mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara husika iweze kufuatilia na kuona ni namna gani ambavyo inaweza ikakamilisha mradi huu kwa sababu tumesha-dump pesa pale na wananchi wanahitaji kunufaika na mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara na nimeanza na Mhandisi wa Maji wa Wilaya, kwamba lazima tutengeneze profile za maji katika maeneo yetu. Najua kwamba jiografia inatofautiana hata kwenye Halmashauri zetu kati ya kijiji na kijiji, kati ya kata na kata. Kuna mahali unaweza ukatumia scheme ya maji ya mtiririko, kuna mahali huwezi, inabidi utumie visima.

Mheshimiwa Naibu Spika,asa tukitengeneza profile hizi, tukajua kwamba mahitaji ni nini kwenye kila kijiji na kata, uwezekano wa scheme ipi itumike katika maeneo hayo, tukawa na profile hii na pengine tukawa hata na makadirio roughly itaweza kutusaidia katika kupanga na kuonesha vipaumbele ili kusudi kile kinachowezekana, kama ni kijiji kina scheme ya kisima, shilingi milioni 20 au 30 zinatosha, basi hilo lifanyike na ndipo hapo ambapo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja, lakini naomba kwamba suala la kuongeza bajeti ya Wizara hii lizingatiwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kunipa nafasi ili niweze kuchangia mada hii ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwanza kuipongeza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba sekta hii ambaYo ni sekta muhimu inapiga hatua na kuweza ku- support sekta zingine ambazo zinategemea kilimo kama Sekta ya Viwanda, Mazingira na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia vitabu hivi viwili, kitabu cha Hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na kitabu cha Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya Kilimo, Mifugo na Maji, nimefarijika kutokana na malengo ambayo yapo katika bajeti hii. Pia nimefarijika zaidi baada ya kuona kwamba utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais, zinaendelea kudhihirika kwa vitendo hususani pale ambapo wameendelea kuondoa zile kodi za kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka Mkoa wa Kagera Wilaya ya Ngara, sisi ni wakulima wa zao la kahawa, kwa muda mrefu sana zao la kahawa limekuwa na bei chini kutokana na tozo nyingi. Zilikuwepo kodi 26 sasa zimeondolewa kodi 17; naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais na Wizara ya Kilimo kwa kazi hii nzuri. Vile vile nipongeze hata kwa kodi ambazo zimepunguzwa kwenye Sekta ya Mifugo, kodi saba zilizoondolewa zitafanya maboresho katika sekta hii ya mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango mizuri ambayo imeainishwa katika kitabu hiki cha bajeti katika kuboresha sekta hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini kutokana na bajeti hii kuwa ndogo napata mashaka kidogo katika utekelezaji wa baadhi ya malengo ambayo yamewekwa katika mpango huu wa utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kunapokuwepo na ufinyu wa bajeti na inapotokea kwamba sasa hata pesa hazipelekwi kwenye miradi ya maendeleo inavyotakiwa, athari ni kubwa na zinaonekana katika maeneo mengi. Kwa mfano tumeshuhudia kwamba upo upungufu kwa mfano wa watumishi hususan Wagani katika maeneo mbalimbali, tumeshuhudia upungufu wa bajeti katika vituo vya utafiti, tumeshuhudia kuwepo na upungufu wa fedha hususan katika kuboresha miundombinu katika sekta ya mifugo kwa mfano ujenzi wa malambo, ujenzi wa majosho na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kwamba katika utekelezaji sasa wa bajeti hii, pamoja na kwamba kuna ufinyu huu, kuna upungufu huu, nina uhakika kama tutaweza kusimamia vizuri na tukaenda kulingana na jinsi ambavyo tumeweka vipaumbele, tunaweza tukapiga hatua, sina mashaka kwa sababu dalili naziona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari ambazo nimezisema, kwa mfano kwenye vituo vya utafiti kuna mahali ambapo mpaka sasa hivi kwenye vituo vya utafiti kama kituo cha Naliendele, baadhi ya watumishi ambao wamestaafu hawajaweza kupata stahiki zao hususani kama pesa kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao, lakini bado pia, watumishi wanapostaafu replacement ya watumishi wengine inakuwa ni tatizo kutokana na ufinyu wa bajeti. Kwa hiyo niwaombe katika maeneo haya ambayo ni muhimu Serikali iweze kuyaangalia na kujikita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jitihada za Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Naibu Waziri, na watendaji wao. Binafsi upande wangu katika Jimbo langu la Ngara, wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa na ndiyo maana nasema kwamba, ili tuweze kuinua sekta hii ya kilimo pamoja na kuzalisha mazao ya chakula lakini ni lazima pia tuangalie uzalishaji wa mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu kubwa tunaangalia mazao ya chakula kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na chakula cha kutosha, lakini tunapokuja katika suala la kuinua kipato cha mwananchi na kuinua uchumi wa nchi hii kupitia sekta ya kilimo, lazima tuangalie uboreshaji katika mazao ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mazao ambayo tumeyazoea korosho, kahawa, pareto, pamba na kadhalika; lakini yapo mazao mengine ambayo hatujayazoea Tanzania lakini ni mazao ambayo yamefanya vizuri katika nchi zingine na ambayo yameweza kuinua uchumi mkubwa katika Mataifa hayo. Ndiyo maana katika jitihada zangu binafsi kama Mbunge wa Jimbo la Ngara za kuangalia fursa zilizopo, na kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, tumeamua kuanzisha zao jipya la Stevia, ambalo ni zao linalofanya vizuri duniani sasa. Naishukuru Wizara kwa ushirikiano wanaonipa kwamba tayari sasa tunaingia kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii kama nilivyoomba wakati ule kwenye swali langu la nyongeza, kwamba kituo cha Maruku ambacho kitafanya utafiti kwa kushirikiana na Kampuni ya East Africa Stevia and agro investment kwenye zao hili la Stevia basi bajeti iweze kutengwa kwa ajili ya kituo hiki cha Maluku na utafiti huu uweze kufanyika katka Jimbo la Ngara. Ni pesa kidogo tu ambazo haziwezi kuzidi milioni 20 kwa kuanzia kwa ajili ya utafiti huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mifugo. Sekta hii ni sekta muhimu, lakini ni sekta ambayo imekumbana na changamoto nyingi. Katika Wilaya yangu ya Ngara tuna mifugo mingi, tuna ng’ombe takribani 70,000, mbuzi wasiopungua 190,640, nguruwe takribani 20,000 na kondoo zaidi ya 75,000 lakini hatuna lambo hata moja, yaani bwawa la kunyweshea mifugo. Kwa hiyo hii inakuwa ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo ambayo ilikuwa inachungiwa kwenye hifadhi za Burigi na Kimisi sasa mifugo hiyo inaingia vijijini ambako hakuna huduma hizi za mabwawa na malambo, kwa maana hiyo vyanzo vya maji ambavyo ndivyo vinavyotumiwa na wananchi kwa ajili ya matumizi ya kawaida vinazidi kuharibiwa kutokana na mifugo hii, ambayo ni mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho ya bajeti yake aweze kuangalia ni namna gani ambavyo wanaweza wakatenga kiasi fedha kwa ajili angalau ya kuweza kuchimba hata malambo manne basi kwa sababu tuna tarafa nne basi kwa kuanza angalau Malambo manne ili kila tarafa iweze kupata lambo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ngara naweza nikasema ni lango la kuingilia na kutoka kwenye Nchi za Maziwa Makuu, lakini pia ni Jimbo ambalo lina fursa nyingi. Kama nilivyotangulia kusema na ambavyo nimesema wakati nachangia kwenye Wizara ya Maji, niipongeze Wizara kwamba baada ya mchango wangu wameangalia kwa makini na tayari bonde la Murongo limetengewa fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu, ambalo liko katika Kata ya Bukililo. Pia Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye taarifa ya Kamati hizi mbili. Niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwanza kupongeza kazi ambazo zimefanywa na Kamati hizi mbili kwa mapendekezo na ushauri ambao wameweza kuutoa kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye Kamati hii ya Kilimo, Mifugo na Maji hasa katika upande wa mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona changamoto ambazo baadhi ya mazao ya biashara ambayo Watanzania ndio tumekuwa tukitegemea kama zao la kahawa, soko limekuwa ni changamoto kwa sababu pia bei imekuwa haipandi na hii ni kutokana na kodi nyingi ambazo zimekuwepo. Pamoja na kwamba Serikali imejitahidi kupunguza, lakini bado kwa kweli mazingira ya uzalishaji wa zao la kahawa na soko na bei bado haijawa nzuri, hususan kwa wakulima wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na zao hilo la kahawa, tumeona maboresho ambayo yamefanyika kwenye zao la korosho na tumeona jinsi ambavyo bei imekuwa ikipanda kwenye korosho. Pamoja na kwamba kumetokea changamoto hiyo ya baadhi ya watu kutokuwa waaminifu na kutaka kuvuruga soko letu, lakini naamini kwamba Serikali itaweza kufuatilia hususani katika uchambuzi huu ambao ulifanyika kwenye mzigo uliokuwa umeuzwa nje na kukuta kwamba kuna uchafu kama mchanga na mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapaswa kujua kwamba kwa kadri tunavyoendelea, yapo mazao mengine ya biashara ambayo yamefanya vizuri duniani na kama ambavyo tunajaribu ku-adapt teknolojia mbalimbali kulingana na mabadiliko ya teknolojia, nafikiri ni wakati muafaka pia kuweza ku-adapt hata katika teknolojia ya kilimo ambayo inaweza ikatusaidia kuweza kuinua kipato cha wananchi walio wengi zaidi asilimia 75, lakini pia ambayo inaweza ikasaidia kuendana na kauli mbiu na sera ya Taifa ya kuwa na uchumi wa kati na uchumi wa viwanda kwa kuanzisha mazao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe wakati wa Bunge la Bajeti lililopita niliwahi kusema kwamba lipo zao linaitwa stevia ambalo linaonekana linafanya vizuri duniani, nikaomba tuanze kufanya utafiti wa zao hili kwa kushirikiana na center ya Utafiti ya Maruku, Mkoa wa Kagera. Naishukuru Wizara ya Kilimo ambao wamekuwa wakinipa ushirikiano kuhakikisha kwamba zoezi hili linafanikiwa, pamoja na kwamba changamoto bado yako kwenye bajeti, lakini naiomba sasa kama ambavyo tulifanya wasilisho la utafiti wa zao hili Wizara ya Kilimo mapema mwaka 2017, basi waweze kupeleka fedha katika Kituo cha Maruku kwa ajili ya kuhakikisha kwamba utafiti huu unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mazao kadha wa kadha. Leo kuna zao kama chia seeds, wengine wanaita super food, ni zao ambalo linafanya vizuri duniani na ambalo katika hali ya kawaida linaweza likabadilisha uchumi wa wananchi wa kawaida, kwa sababu ni zao la muda mfupi, lakini ni zao ambalo linahitajika, pia ni medicinal kwa maana ya kwamba linaweza likaboresha afya ya Watanzania, lakini pia likaboresha uchumi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Kilimo kwamba tayari wanaendelea kunipa ushirikiano na muda siyo mrefu tunaamini kwamba tutapata kibali kwa ajili ya kuingiza mbegu kwa ajili ya kufanya na utafiti wa zao hili ili kuinua uchumi wa wananchi wa Ngara, lakini na wananchi wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna namna tunavyoweza kufanya miujiza kubadilisha maisha ya wakulima wa kawaida tusipowekeza kwenye suala la kilimo na kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kwa sababu kumekuwepo na mabadiliko ya tabia nchi, mara kwa mara tunajikuta tunaenda tofauti na matarajio katika misimu yetu ya kilimo.

Kwa hiyo, naomba tuwekeze zaidi katika kilimo cha umwagiliaji. Hatujafanya vizuri, ukiangalia ni kwamba, ni asilimia 1.6 tu ambayo tumefanya kwenye sekta hii ya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuwekeze katika miradi ambayo tayari imeanzishwa, kama mradi wa Bigombo kwenye Wilaya yetu ya Ngara ambayo takribani sasa miaka mitatu iliyopita ulitakiwa uwe umekamilika, lakini haujakamilika mpaka sasa hivi na tumeshatumia fedha nyingi zaidi ya shilingi milioni 715 na miundombinu inaanza kuchakaa wakati haijaanza kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tujikite katika kilimo cha umwagiliaji ili kuboresha maisha ya Watanzania, lakini pia kuandaa mazingira ya kupata malighafi kwa ajili ya kulisha viwanda vyetu ambavyo tunakazana navyo kwa ajili ya kuvianzisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii iko migogoro ambayo imekuwa ikiendelea katika sekta hii, migogoro ya ardhi ni pamoja na mipaka; mipaka kati ya wilaya na wilaya, kijiji na Kijiji, mipaka kati ya maeneo ya ufugaji na kilimo.

Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Afya. Niungane na Wabunge waliotangulia kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, lakini pia kazi kubwa wanayoifanya Waziri na Naibu Waziri na watendaji wao wa Wizara katika kuboresha afya za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi yamefanyika katika Jimbo langu la Ngara hasa katika kuboresha afya za wananchi wa Ngara ikiwa ni pamoja na kuboresha vituo vya afya Musagamba Mabawe, lakini pia hata upatikanaji wa dawa kabla ya hapo wananchi wa Jimbo la Ngara walikuwa wanaenda kutibiwa Burundi haya wa kata za mipakani lakini leo imekuwa ni vice versa kwamba kuna wanaotoka upande mwingine kutaka kuja kupata huduma upande wetu. Kwa hiyo, napongeza Serikali na Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo bado zipo changamoto, tuna vituo vinne katika Wilaya ya Ngara kati ya kata 22, lakini kipo Kituo cha Afya Lukole ambacho kituo hiki ni miongoni mwa hivyo vituo vinne. Hiki kituo kilikuwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Lukole wakati wakiwepo wakimbizi wa Burundi, majengo yaliyojengwa katika kituo kile ni majengo ambayo mengi yalijengwa kwa tofali za tope kwa hiyo siyo majengo ya kudumu lakini ni kituo ambacho kinahudumia watu zaidi ya elfu ishirini na tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Mheshimiwa Waziri Ummy, Naibu Waziri Dkt. Ndugulile mmefanya kazi kubwa kwangu, lakini niombe hili nalo tuliangalie kwa macho mawili kwamba hiki kituo nacho tuweze kukiboresha ili kiwe kwenye hadhi kwa sababu kinatoa huduma ka wananchi wa Jimbo la Ngara hata Jimbo jirani la Bihalamuro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi upo kwa kiasi kikubwa kwenye sekta hii ya afya, kuanzia kwenye hospitali ya Nyamiaga, vituo hivyo vinne na kwenye zahanati. Niombe kwamba sasa kwa watumishi hawa ambao wanaenda kuajiriwa, watumishi 16,000 kwenye bajeti ya mwaka huu, idara ya afya basi mtufikirie.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado pia kuna baadhi ya watumishi waathirika hususan katika Hospitali ya Murugwanza, Dada yangu jana aliiongelea na mimi nalisisitiza hili kwa sababu wapo watumishi 49 ambao wakati wa uhakiki wa vyeti siyo makosa yao, waliondolewa kwenye payroll wakati hawakuwa na kosa na bado wakarudishwa. Wengine wanadai miezi kumi, wengine wanadai arrears za mishahara yao miezi sita, saba kwa namna tofauti, niombe hilo liweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mpango wa bima ya afya kwa watu wote, hii inaweza kuwa ndiyo suluhisho kwa ajili ya kuondoa double standard na kuwahudumia watu kwa usawa. Ni nia njema ya Serikali na niombe hili lifanyiwe haraka na Wabunge tupo tayari kwa ajili ya kuendelea kuhamasisha ili mpango huu uanze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipo Kituo cha Afya katika Kata ya Nyakisasa, kituo hiki kilianzishwa kwa nguvu za wananchi, lakini pia kwa kutumia Mfuko wa Jimbo; yapo majengo ambayo ambayo hayajaweza kutosheleza kuwa kituo cha afya, lakini tunaamini ikiwekwa nguvu kidogo kituo kile kinaweza kikafunguliwa kulingana na jiografia ya hali ya Ngara, kituo hiki ni muhimu na tunakihitaji. Niombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja ulifikirie hilo katika vituo ambavyo unaweza ukaviongezea fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwenye upande wa lishe. Lishe katika hali ya kawaida inaonesha kwa mujibu wa takwimu kwamba Tanzania tuna lishe duni ni watatu Afrika, lakini ni wa kumi duniani, unaweza ukaona ni jinsi gani ambavyo kuna changamoto hiyo. Pamoja na kwamba Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) wameonesha ni jinsi gani ambavyo wamefanya jitihada katika ku-control hata vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyotokana na udumavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kwamba twende zaidi tujaribu kushirikiana hata na Wizara ya Kilimo kuona ni namna gani tunavyoweza kuhamasisha baadhi ya mazao ambayo yanaongeza lishe. Kwenye ukurasa ule wa 89 kwenye kitabu hiki cha hotuba ya Waziri wameonesha ni jinsi gani ambavyo wanajaribu kutoa chanjo kwa asilimia kubwa kwa watoto chini ya miaka mitano kwa matone ya Vitamini A.

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vyakula lishe kama viazi lishe ambavyo vina Vitamini A nyingi ya kutosha ambavyo tukihamasisha ulimaji wa viazi lishe (orange sweet potato) vinaweza vika-cover eneo ambalo tunatumia gharama kubwa kwa ajili kuwachanja watoto hawa kwa matone ya Vitamini A. (Makofi)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hizi mbili zilizoko mbele yetu za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya na uzima na ambaye amenipa nafasi hii. Pia, niungane na wananchi wa Jimbo la Ngara, Watanzania, wanajumuiya ya UDOM kuonesha masikitiko yangu makubwa kumpoteza kijana Paschal Deogratius Mboyi, ambaye amefariki dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana huyu mwaka jana akiwa Chuo Kikuu cha UDOM aliandika kitabu chake cha Diwani ya Pakacha Limetoboka, kitabu ambacho nilimkabidhi nakala yake Waziri wa Elimu na ilikuwa katika mchakato wa kuona namna gani kinavyoweza kuingizwa kwenye syllabus kwa sababu ni vijana wachache sasa ambao wana vipaji. Kwa hiyo, niungane na Watanzania wote kusikitika kwa ajili ya kumpoteza kijana mahiri huyu katika wakati wa ujana na alikuwa na maono makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wanaopongeza, aisifuye mvua maana yake imemnyea, imemnyeshea au imemnyea yote sawa. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya. Mvua hii ya kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Rais, mimi na wananchi wa Jimbo langu la Ngara imetunyeshea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata takribani bilioni 1.4 kwa ajili ya upanuzi wa vituo viwili vya afya, Kituo cha Afya Murusagamba, Kituo cha Afya Mabawe, kwa maana ya milioni 400 kwa ajili ya miundombinu, milioni 300 kwa ajili ya vifaatiba, milioni 700 kwa kila kituo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata milioni 226 kwa ajili ya miradi ya maji ya vijiji 10, lakini Mheshimiwa Rais mwenyewe mwaka jana alitupatia milioni 13 cash wakati amekuja Ngara kwa ajili ya kununua pump ya maji na milioni 24 tumepata kwa ajili ya maboresho ya huduma za maji. Mwaka jana huo nilimwomba mradi mkubwa wa maji kutoka kwenye vyanzo vya mito, Mto Ruvuvu, Mto Kagera na Mlima Shunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwenye bajeti inayokuja ya maji, kwa taarifa niliyonayo, tunategemea kupata karibu milioni 200 kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu wa mradi huo. Nina kila sababu ya kumpongeza, kuwapongeza Watendaji wa Serikali kwa maana ya Waziri, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye elimu. Wengi wamechangia na wamesema kwenye elimu, lakini mimi nitaomba nijikite pia kwenye upande wa elimu maalum na watoto wenye vipaji maalum. Nichukue nafasi hii kwanza kuwashukuru Watanzania ambao wamemuunga mkono kijana wetu Anthony ambaye amesambaa kwenye mitandao ya kijamii nchi nzima na nje ya nchi, anatoka Jimboni kwangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wote ambao wameshiriki katika kuchangia kumwezesha ili kijana huyu ambaye ameonekana kuwa na kipaji maalum aweze kuendelezwa. Kwa namna ya kipekee pia, nimshukuru Ndugu Isaack Msuya, ambaye amekubali kumchukua kwenye shule yake anayoimiliki ya Mwanga kumsomesha kijana huyu, pia, wadau wote ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika kumchangia mtoto huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto. Najua kwamba, tumekuwa na shule zenye vipaji maalum, shule hizi ni za sekondari japo nazo pia hazitoshi kama vile Mzumbe Sekondari, Kilakala, Weruweru, Ilboru, Kibaha, shule zisizozidi saba, lakini hatuna shule za msingi, sidhani kwenye record, nimejaribu kupitia kwenye mitandao ku-google, lakini sijaona kuna mahali ambapo tuna shule za msingi zenye vipaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hizi za msingi ndizo ambazo zinaweza kulea watoto hawa ambao wana vipaji maalum na tukawekeza kwenye watoto hawa ili kusudi tuweze kuwa na wataalam waliobobea wanaoweza kuleta mabadiliko pia ya kweli na kwenda sawa na kasi ya Mheshimiwa Rais kuwa na uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwamba hii ni changamoto sasa, hivyo tuangalie uwezekano wa kuanzisha shule zenye vipaji maalum, sambamba pia na shule kwa watoto wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kwa watoto wenye ulemavu hasa katika kupata elimu ni kubwa. Nilikuwa nikizunguka kwenye Jimbo langu, wapo watoto takribani mia mbili na kitu ambao wako vijijini na kila nilipokuwa nikipita wanauliza wazazi kwamba, kuna mkakati gani kwa ajili ya kuboresha au kuwapatia elimu hawa watoto wenye ulemavu. Tunayo Shule ya Msingi Murugwanza ambayo imeanza programu hii japo katika mazingira magumu, lakini niombe Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukaunga mkono jitihada hizi ambazo zimeanza katika Jimbo la Ngara, hususan katika shule ya msingi Murugwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende upande wa TARURA. TARURA naiunga mkono kwa asilimia 100. TARURA iliundwa kwa maksudi thabiti ya kutaka kuboresha huduma za miundombinu ya barabara kwenye vijiji na miji. Kumekuwepo na ulinganifu kuona jinsi ambavyo Halmashauri zetu zilikuwa zinasimamia programu hii ya matengenezo na ukarabati wa barabara na jinsi ambavyo TANROADS wamekuwa wakifanya. Ukijaribu kuangalia asilimia 30 ambayo Halmashauri ilikuwa ikipata ndiyo hiyo ambayo TARURA nao wanapata, sasa sitegemei kwamba, kuna kiti kinaweza kikafanyika tofauti kama hatutaweza kuongeza bajeti.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na mchango wangu utajikita zaidi katika sekta ya uwekezaji. Kabla sijaanza kutoa mchango wangu, nichukue nafasi hii kwanza kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba nchi yetu imepiga hatua hususani katika sekta hii ya uwekezaji na ndiyo maana hata taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba Tanzania tumepiga hatua. Kwa mfano, Africa investment Index inaonyesha jinsi gani ambavyo Tanzania tumepiga hatua na kufikia namba 13 katika nchi 54 za Afrika. Pia ukiangalia hata katika taarifa ya Where to Investment in Africa inaonyesha jinsi ambavyo tumepiga hatua hususani katika kuvutia uwekezaji na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna namna ambavyo tunaweza tukapiga hatua na kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda kama hatutajipanga vizuri na kuona ni namna gani ambavyo tutaweza kwenda katika uwekezaji huu. Kuna kauli inayosema kwamba, we have to learn from the past for future. Tutakumbuka kwamba baada ya uhuru chini ya Rsis wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, baada ya uhuru alijikita kuona ni namna gani ambavyo tunaweza sasa tukakimbizana kuinua uchumi wa Tanzania kupitia sekta hii ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini zipo changamoto nyingi ambazo tumejifunza baada ya kuona baadhi ya viwanda ambavyo tulikuwa navyo wakati huo vilikumbana na changamoto kadhaa wa kadhaa. Awamu hii ya Tano tunapokuja kuwekeza zaidi na kuweka nguvu katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda kama injini ya maendeleo kufikia uchumi wa kati, naamini tumejifunza changamoto ambazo zilitukwamisha wakati ule. Nimpongeze Rais kwa sababu yeye sasa amekuwa ni mbeba maono mapya katika kuwekeza kwenye sekta hii ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tulizokutana nazo baada ya uhuru ni rasilimali watu kwa maana ya wataalam walikuwa wachache, miundombinu ya umeme kwani maeneo yaliyokuwa yameunganishwa kwenye gridi ya Taifa yalikuwa ni machache mno lakini sasa kwa sababu ya maono ambayo anayo Mheshimiwa Rais ndiyo maana tumeanza kujenga msingi ili kuhakikisha kwamba tunapoingia sasa kwenye uwekezaji katika sekta ya viwanda hatukumbani na vikwazo tena. Tunaona jinsi ambavyo amethubutu kuanzisha mradi mkubwa wa umeme (Stiegler’s Gorge) kwenye Bonde la mto Rufiji, tunaona jinsi ambavyo tunaboresha bandari kwa sababu hizi ni fursa ambazo zitatuwezesha sasa kuweza kuingia kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna neema kwamba Tanzania kijiografia sehemu kubwa tuko kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi na ndiyo maana tukaona ni vyema kuanzisha Maeneo Maalum kwa ajili ya Uwekezaji (EPZ, SEZ) na ndiyo njia pekee ambayo inaweza ikatupeleka kuwa na uchumi wa viwanda. Kwa mfano, nchi za China na India, zimepata uhuru kutoka kwa Wakoloni miaka inayofanana, miaka ya 1949. Baada ya kupata uhuru tu ndani ya miongo sita waliangalia ni namna gani sasa ambavyo uhuru wao watautumia kwa ajili ya kuboresha uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hizi zilianza kuwekeza kwenye Maeneo haya Maalum (EPZ, SEZ) kwa maana ya Export Processing Zones na Social Economic Zones kwa lengo la kutaka kuinua uchumi wao. Hiki ndicho ambacho kimeweza kuwafanya waweze kukimbia kwa haraka. Leo China ni nchi ya pili duniani katika uchumi unaokua kwa kasi. Ni ukweli usiopingika kwamba sasa hivi katika sekta ya viwanda, China inaongoza ikiwa ni pamoja na India. Tukiangalia mifano pia hata ya nchi za Bara la Asia (Indonesia, Malaysia na Korea ya Kusini) nao pia kupitia mifumo hii ya uwekezaji wameweza kupiga hatua kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na mapendekezo ya Kamati ya Sheria lakini pia na taarifa za Kamati ambazo zipo katika sekta hii kwamba lazima tuweke nguvu sasa katika kuwekeza na lazima tuangalie ni namna gani ya kuweza kuendelea kupanua maeneo haya ya EPZ na SEZ. Maeneo yametengwa, najua yapo na ni machache na bado kumekuwepo na changamoto ambazo zinakabili maeneo haya lakini lazima tuangalie ni namna gani sasa tunavyoweza kuendelea kupanua maeneo lakini pia tukiendelea kuboresha na kuondoa vikwazo vya fidia ili kusudi maeneo haya yaweze kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapowekeza katika uzalishaji wa viwanda ni lazima tuangalie masoko ya vile tunavyovizalisha. Najua kwamba yapo masoko ya aina mbili, soko la ndani na la nje. Tunapokwenda kwenye ushidani wa soko la nje lazima tuangalie ni mazingira gani ambayo yanawezesha masoko ya nje kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoamini, kama tutakuwa tumeweza kuendelea kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji, tukaendelea kuita au ku-attract wawekezaji wenye tija ambao uwekezaji wao huo utatupa faida kwa maana ya kuongeza mitaji, kuwa na akiba ya fedha za kigeni, kutoa ujuzi kwa maana ya kwamba tuta-attract na ujuzi kwa sababu wanatoka kwenye mataifa ambayo yamefanikiwa basi itatuwezesha katika kufanya exportation ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kushindana kwenye soko la nje. Kwa hiyo, lazima yote haya kuyaangalia na kujipanga kuona kwamba sasa ni wawekezaji wa aina gani pia ambao tunawaalika kuwekeza ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji wa aina yoyote unaoweza kufanyika, uwe uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, sekta ya kilimo na sekta ya madini ni lazima tushirikishe idara au sekta mbalimbali. Sekta muhimu katika uwekezaji huu ni pamoja na sekta ya ardhi. Najua kwamba upo mpango wa miaka 20 (2013 - 2033) wa matumizi ya ardhi. Mipango hii inatakiwa iende sambamba kwa sababu kama tutakuwa hatujaweza kutekeleza mpango huu wa matumizi ya ardhi na tukaainisha maeneo ambayo tunahitaji kuwekeza na tuwekeze nini kwa maana ya vipaumbele, tutajikuta tunashindwa kufanikiwa na tunakutana na vikwazo. Ndiyo maana nikasema kwamba lazima tuangalie sasa tunaweka vipaumbele katika uwekezaji upi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ninukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kwenye Mkutano wake wa kwanza anahutubia Bunge baada ya uchanguzi wa mwaka 2005. Alijaribu kueleza mafanikio ambayo yamepatikana kutoka na awamu zilizopita. Akasema wakati Awamu ya Pili kulingana na hali ya uchumi ilifikia mahali Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Pili, Mzee wetu Mwinyi ikabidi aanze kuruhusu sasa watu waingize mitumba kulingana na hali ya uchumi tukaingia kwenye biashara ya nje. Kwa hiyo, wakati wa kuruhusu Mzee akaitwa Mzee wa Ruksa, akasema kwamba hata nzi na mbu waliingia baada ya kufungua madirisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa naomba niseme kwamba ni vyema tukachukua tahadhari kwa sababu lazima tuwe na vipaumbele kwamba tunataka tuwekeze kwenye nini. Kwa mfano, tunapotaka tusema tuwekeze kwenye viwanda lazima tujue raw material zinapatikana kutoka wapi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako, muda wako ndiyo huo umeisha.

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwakunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Ni ukweli usiopingika kwamba Wizara hii ni nyeti na inafanya kazi kubwa ya kuwahudumia Watanzania takribani milioni 55. Tunashukuru kwa ajili ya usalama na utulivu uliopo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya watu milioni 55, watu wana tabia na akili tofautilakini ukiangalia jinsi ambavyo Wizara hii kupitia Jeshi lake la Polisi imeweza kudhibiti hali ya uhalifu ndani ya nchi hii, tuna kila sababu ya kuwapongeza. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri, Makamishna Jenerali wa Uhamiaji, Jeshi la Magereza na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kwa kazi kubwa ambayo kwa kweli wameweza kuifanya, tunawapongeza na Mungu awabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Wakati wote hauwezi ukafanya kwa asilimia 100, we always do to optimum. Kwa hiyo, kwa jitihada ambazo zimefanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kuhakikisha kwamba utulivu na amani unapatikana kupitia Wizara hii ya Mambo ya Ndani, tuna kila sababu ya kusema wamefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba changamoto hazikosi, kwenye Jeshi la Polisi kama wengine ambavyo wamesemakwamba zipo changamoto hususan katika uwezeshaji wa Jeshi letu la Polisi kutekeleza majukumu yao kulingana na hali ya kijiografia ya nchi yetu na ukubwa wa nchi yetu. Tunajua kwamba resources, kwa maana ya rasilimali ni kidogo, hasa rasilimali watu lakini pia hata vitendea kazi. Tunamshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo anaendelea kuguswa kwa namna ya kipekee ili kuiwezesha Wizara hii kutekeleza majukumu yake.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto ya malazi, kwa maana ya nyumba za Askari wetu, ipo changamoto hata ya matumizi ya kila siku kwa maana yabills za umeme, na maji. Niombe Wizara ijaribu kuangalia maeneo ambayo kwa kweli kuna madeni makubwa kama ambavyo Kamati imeweza kushauri, basi waangalie ni namna gani wanaweza kupunguza madeni hayo kwenye maeneo ambayo madeni ya umeme na maji yapo ikiwa ni pamoja na Wilaya yangu ya Ngara. (Makofi)

MheshimiwaMwenyekiti,lakini pia tunajua kwamba jiografia zinatofautiana, kwamfano, Wilaya ya Ngara iko mpakani, tunapakana na nchi mbili ambazo hali ya usalama wakati mwingine inakuwa si tulivu na katika mipaka yetu kunakuwa na changamoto ya mwingiliano na wageni kutoka nje. Hii inatokana na kwamba Wilaya ya Ngara kwa muda mrefu ime-host wakimbizi, tangu miaka ya 1959. Kwa hiyo, Wilaya ya Ngara ni Wilaya ambayo sasa hata wageni kutoka nchi jirani wameshaizoea kutokana na kwamba wameishi kwa muda mrefu wakiwa wakimbizi, kwa hiyo, hata wanapokwenda ni rahisi kurudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe vituo vya polisi ambavyo sasakwa jitihada za wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Mkoa, tumeanza kujenga kwenye maeneo hasa kata za mpakani, basi Wizara ione namna gani inavyoweza kutuongezea nguvu kwa ajili ya kukamilisha vituo hivyo. Vituo hivyo ni Mkanizi, Mluvyagira, Murubanga, Keza na maeneo mengine.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,Wilaya ya Ngara ina vituo viwili vya pamoja, OSBP (One Stop Border Posts) kwenye mpaka Rusumo tunapopakana na Rwanda na mpaka wa Kabanga tunapopakana na Burundi. Kituo hiki cha OSBP- Rusumo, tunahitaji kuwa naCCTV Cameras, hakuna, ukienda upande wa Rwanda kila ofisi ina CCTV Camera, kwetu pale hakuna hata moja, kwa hiyo, kiusalama ni changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,lakini pia tumepita pale na Kamati ya LAAC kuangalia kituo hiki, tunazo scanners mbili, scanner kwa ajili ya passengers na kwa ajili ya luggage’s. Scanners zile zinahitaji moto mwingi wa umeme, wakati mwingine hazifanyi kazi, kwa hiyo, upekuzi unafanyika manuallykiasi kwamba kiusalama si hali nzuri, tunahitaji kuboresha maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda upande waJeshi la Magereza, tuna changamoto kubwa hasa Wilaya yangu ya Ngara, kwanza hawana gari, hata wanapokuwa na wagonjwa kuwasafirisha kuwapeleka hospitali ni tatizo lakini hata kuwapeleka wafungwa kwenye shughuli inakuwa ni gumu, hasa inapokuwa maeneo ya mbali. Kwa hiyo, tunahitaji tupate garikwa ajili ya Jeshi letu la Magereza katika Wilaya yetu ya Ngara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni pamoja pia na msongamano wa wafungwa/mahabusu magerezani. Wapo mahabusu ambao hawana sababu ya kuendelea kukaa mle kwamuda mrefu kutokana na kesi zao walizo nazo. Wengine kesi zao zina dhamana, kwa hiyo, tukiweza kuharakisha kufanya upelelezi au wakapewa dhamana wakawa nje wakawa wanahudhuria mahakamani, inaweza ikapunguza msongaman. Kwa hiyo, niombe hilo nalo liweze kufuatiliwa na kuangaliwa kwa umakini hii ikiwa ni pamoja na wahamiaji haramu ambao anakamatwa na kuwekwa ndani kwa muda mrefu. Kama inabainika kwamba ni wahamiaji harama hakuna sababu ya kuwahifadhi na kuwagharamia chakula na kadhalika, ni afadhali tukawarudisha kwa sababu wengi wanatokea nchi za jirani, Rwanda na Burundi, ambayo ni just walking distance, kutoka Ngara Mjini kwenda borders hizo zote, hazizidi kilomita 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nikienda upande wa Uhamiaji, tunatambua kwamba Sheria ya Uraia wa Tanzania ya mwaka 1995, Sura ya 357 na kama ilivyorejewa mwaka 2002 lakini na Kanuni zake za mwaka 1997, zinaeleza kwamba raia wa Tanzania wanatambuliwa kwa aina tatu: Uraia wa Kuzaliwa;Uaraia wa Kurithi lakini na Uraia pia wa Kuandikishwa. Utambuzi huu unazingatia vipindi mbalimbali vya uongoziwa nchi hii. Kuna uraia kabla nabaada ya uhuru,kabla ya mapinduzi na baada ya mapinduzi na baada ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wanasema ignorance of the law is not excuse lakini tunahitaji kuendelea kutoa elimukwa wananchi wetu na wakati mwingine kuweza kuhakikisha kwamba haya makundi matatu ya uraia yanajulikana katika jamii. Wakati mwingine hata zinapotolewa taarifa kwamba kuna baadhi ya wahamiaji haramu, unajikuta watu wengine wanapata usumbufu kumbe wako katika categorieshizi na hawapaswi kutuhumiwa kama siyo raia lakini ni kutokana nakwamba elimu hii ya uraia kwa wananchiwalio wengi hususan maeneo ya vijijini na hasa maeneo ya mipakani haipo. Kwa hiyo, tuombe Jeshi letu la Uhamiaji wajaribu kujisumbua hasa katika maeneo ya mipakani na vijijinikutoa elimu ya uraia ili kuweza kujua nani anakuwa raia na nani si raia na kwa sababu zipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru Mheshimiwa Waziri mwanzoni mwaka huu ulifanya ziara katika Wilaya yangu ya Ngara, tumekuwa waathirika wakubwa hususan katika suala zima la uraia. Kuna wapiga kura wangu wengine wanashindwa hata kutembea kwenda Kahama lakini kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ile ya Kwanza, Uhuru wa Kuishi, Mtanzania anayo haki ya kuishi mahali popote. Wakati mwingine wananchi wanashindwa kutembea kwa kuhofu kwambaakionekana sehemu fulani …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gashaza, ahsante sana. (Makofi)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Maji. Niungane na Wajumbe waliotangulia kuwapongeza viongozi wetu; Waziri wa Maji, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri, Katibu Mkuu - Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu - Eng. Kalobelo, Wakurugenzi wa Wizara kwa maana ya Mkurugenzi Mkuu ma Mkurugenzi Msaidizi, Eng. Christian na watendaji ambao wako chini yao kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niipongeze Serikali kwa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini, Mijini na Usafi wa Mazingira (RUWASA). Tunaamini kwamba hii itakuwa ni suluhisho pia katika kuharakisha kupeleka huduma ya maji vijijini kama ambavyo tumeona mafanikio tulipoanzisha TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuanzisha ni kitu kimoja na ufanisi ni kitu kingine. Tumeona kuna upungufu wa watumishi; ili RUWASA waweze kufanya kazi vizuri lazima kuongeza watumishi lakini watumishi wenye sifa na ambao ni makini. Ili RUWASA waweze kufanya kazi yao vizuri na Mfuko wa Maji Taifa ni lazima kuongeza fedha ili waweze kutekeleza miradi ya maji kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jinsi ambavyo Mfuko wa Maji wa Taifa jinsi ambavyo wameweza kufanya vizuri, asilimia 67 ya miradi iliyotekelezwa imetokana na fungu ambalo liko kwenye Mfuko huu. Kwa hiyo, kwa kutenga fedha za kutosha kwenye kwenye Mfuko hii, itapelekea kutekeeza miradi mingi ambayo imekwama. Niungane na Wajumbe waliotangulia kusema kwamba shilingi 50 iongezwe; inatoka kwenye mafuta, mitandao ya simu, inatoka wapi, jambo la msingi ni tuongeze fedha katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwashukuru. Tumepokea shilingi milioni 208 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kulipa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya vijiji 10, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika Jimbo langu naweza nikagawa makundi ya miradi katika sehemu tatu, kama sio nne; miradi ya vijiji 10 ambayo imechukua sasa zaidi ya miaka mitano haijakamilika. Tumeomba shilingi milioni 400 certificate kwa ajili ya kulipa wakandarasi waendelee kumalizia miradi hii. Niombe Wizara hizi fedha zilipwe haraka iwezekanavyo ili waendelee kukamilisha miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa miji sita katika Mkoa wa Kagera. Ni mradi ambao ulianza kusanifiwa na Mhandisi Mashauri tangu miaka ya 2014. Huyo Mhandisi Mshauri akashindwa kuendelea na kazi akawa terminated. Nawashukuru kwamba sasa amepatikana Mhandisi Mshauri mwingine amesharipoti site tangu juzi. Kwa hiyo, niombe azingatie mkataba wa miezi nane ambao amepewa ili mradi huu uweze kutekelezwa kwa sababu uta-cover eneo la Mji wa Ngara Mjini lakini pia na vijiji saba ambavyo vimeongezwa; Vijiji vya Mrukurazo, Nyakiziba, Nterungwe, Buhororo, Kumtana, Kabalenzi na kadhalika. Kwa hiyo, niombe kwamba usanifu wa mradi huu uweze kufanyika kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mradi wa vijiji vitano. Nishukuru Wizara kwamba tayari mmetoa go-ahead, no objection kwamba waanze kutangaza. Vijiji vya Mkalinzi; Mrugina, Kata ya Mabawe; Kanyinya, Kata ya Mbuba; Kumbuga, Kata ya Nyamagoma; na Ntanga. Naomba tunapoanza kutekeleza bajeti Julai basi taratibu zote ziwe zimekamilika ili vijiji hivyo ambavyo vina adha ya maji viweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe kwenye fungu hilo kwa sababu tuna chanzo cha Mto Ruvubu na kutumia Mlima Shunga ambao ndiyo mrefu kuliko milima yote Mkoa wa Kagera, vipo vijiji katika kata hilo ambapo ndipo maji na mlima uliopo. Vijiji vya Kenda, Kagali na Mlengo visiachwe katika mpango huu, viongezwe ili wananchi ambao wapo katika eneo hilo wasiachwe nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, kwenye Mto huohuo wa Ruvubu na mlima huohuo ambao mradi huu ulikuwa ndiyo suluhisho kwa ajili ya vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara. Kwa sababu Mhandisi Mshauri atakuwa yuko site kwa ajili ya kuanza kusanifu mradi huu na chanzo ni hichohicho na mlima huohuo ambao utaweza kusambaza maji kwa mserereko wilaya nzima na hata nje ya wilaya. Ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais wakati namwomba mwaka juzi, 2017, alivutiwa kwa sababu alikuwa anaona ni mradi mkubwa unaweza ukatoa huduma kwa Wilaya ya Biharamulo, Wilaya ya Kakonko, tena wakati ule nilisema unaweza ukaenda mpaka Bukombe na Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mradi huu muuchukulie kama mradi mkubwa ambao unaweza ukatoa suluhisho kwa maeneo mengi ambayo hayana vyanzo vya uhakika vya maji. Kwa hiyo, niombe katika bajeti hii, huu mradi wa Mheshimiwa Rais ambao tulimuomba uende sambamba na huu mradi wa miji sita kwa sababu chanzo ni hichohicho na sehemu ya ku-supply ni hiyohiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka kwenye mlima huu upo mlima mwingine mkubwa ambao kimo chake kutoka usawa wa bahari ni kama mita 1,400 hivi, huu wa Shunga ni 1,820, kwa hiyo huu Mlima wa Msumba ambao upo katika Kata ya Nyakisasa, Tarafa ya Rulenge, unaweza ukasambaza maji kwa mtiririko baada ya kupokea maji kutoka kwenye mlima huu kwa vijiji vyote vya Tarafa ya Rulenge na Tarafa ya Mrusagamba lakini ukapeleka hata Wilaya jirani ya Kakonko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe mradi huu Wizara muuangalie kama ni mradi mkubwa unaoweza ukatatua changamoto ya maji katika Wilaya ya jirani pia. Mhandisi Mshauri kama anao uwezo basi ni afadhali hii anayoifanya sasa hivi ya usanifu wa mradi wa miji sita aweze kuongezewa phase two kwa ajili ya kuendelea na usanifu wa mradi huo mkubwa wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ambao unaweza ukawa ni suluhisho kwa maeneo hayo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeona jitihada za Wizara kwenye Wilaya ya Temeke, hususan maeneo ya Kurasini, pale ambapo tayari mmeshalipa nafikiri zaidi ya shilingi milioni 600 kama fidia kwa ajili ya kutengeneza sewage system. Naomba tu-adopt sasa technology mpya ya recycling. Kwa sababu bado ku-discharge maji machafu kupeleka ziwani au kwenye mito ni kuendelea kuchafua mazingira lakini tunaweza tukaendelea kufanya recycling ukawa ni mkakati mahsusi kwenye majiji, miji na halmashauri za miji kwa sababu hata haya maji safi na salama yanatokana na maji machafu tu isipokuwa tunayafanyia treatment yanakuwa safi na salama. Kwa hiyo, tukiandaa sewage systems, mahali pa kupokea yale maji machafu halafu tuka-recycle tutajikuta kwamba tunaendelea kutunza mazingira lakini pia na kutunza maji. Hata kama itakuwa ni miaka mingapi ijayo tutakuwa na uhakika kwamba hatupungukiwi maji kwenye vyanzo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niendelee kuwapongeza Wizara na niombe tuzingatie haya ambayo Kamati imeshauri kwa sababu Kamati ya Bunge ndiyo Bunge. Kwa hiyo, haya ambayo wameshauri, kama hii ya kuongeza fedha ili kuondoa changamoto hii ya fedha kwenye Mfuko huu wa Maji tuizingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishauri kwamba Wizara hii ya Maji lazima ifanye kazi sambamba na Wizara zingine; Ofisi ya Makumu wa Rais (Mazingira) na Wizara ya Ardhi ili kuhakikisha kwamba tunatunza vyanzo vya maji. Tunapotunza vyanzo vya maji maana yake ni kwamba tunaendelea kuwa na uhakika wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepitisha Sheria ya Watumiaji wa Maji, yapo maeneo ambayo lazima tuwe makini tunapoanza kutekeleza sheria hii hasa kwenye vyanzo kwamba watu wawe mbali na vyanzo vile vya maji. Hata kama kuna mahali ambapo pipes za maji zimepita, kuna umbali ambao hakuna shughuli za kibinadamu zinazotakiwa zifanyike katika maeneo hayo. Ni vizuri wakati tunaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo lakini wananchi waelimishwe zaidi ili waweze kujua sheria hizi na waweze kuzingatia ili wawe ndiyo watunzaji wa miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya PAC.Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa nafasi ili kuweza kusimama kwa ajili ya kuchangia. Pili, nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi mingi katika Halmashauri zetu. Miundombinu katika Sekta ya Afya na Sekta ya Elimu tumeona kazi iliyofanyika, tunaipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo ambayo nitapenda kusisitiza kama ambavyo tumeweza kuyaeleza katika taarifa yetu, baadhi ya Halmashauri na niseme kwa wingi zaidi ya asilimia 50 kuna maeneo ambayo yamepelekea kuweza kupata hoja za ukaguzi kwa mfano eneo la ku-dispose mali za Serikali kwenye Halmashauri zetu hususan magari chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi hoja zimekuwa zikijirudia mara kwa mara na hazipatiwi ufumbuzi, lakini katika kutafakari kwa kina tumekuja kugundua kwamba yawezekana kuna changamoto hususan katika suala zima la sheria ya ku-dispose mali hizi, kwa sababu inachukua muda mrefu kwanza kukamilisha mchakato huu wa ku-dispose na hata Halmashauri wanapoanza initiative za kuandika barua kwa ajili ya kuomba kibali, kibali kinachelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika,vile vile tumekuja kugundua kwamba pengine Halmashauri kwa sababu wao ndio wanapaswa kumgharamia Mhakikimali Mkuu wa Serikali au timu yake inayokuja kufanya assessment, basi Halmashauri wanaona hakuna sababu kwa sababu wanagharamikia baada ya kuuza fedha zinaenda Hazina na sio lazima kwamba zirudi kwa ajili ya kusaidia ama kununua gari nyingine kwa ajili ya ku-replace kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipendekeze kwamba katika kipengele hiki ni vizuri tukaangalia kama kikwazo ni sharia, basi tuone namna gani ambavyo unaweza ukaletwa Muswada kwa ajili ya kurekebisha sheria hii ili kuwaondolea mzigo mkubwa Halmashauri ambao wanaamua sasa kuacha magari yanakuwa grounded na Serikali inaendelea kupata hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ya pili ni kuhusu miradi hii inayotekelezwa na force account na hii inatokana na upungufu wa watumishi ambao wapo katika Halmashauri zetu. Serikali naipongeza kwamba wanaonesha jitihada za kuongeza watumishi hususan kwenye Sekta ya Elimu na Afya lakini kwenye upande wa uhandisi bado kasi ya kupeleka/kuajiri watumishi hao ni ndogo kiasi kwamba sasa usimamizi wa miradi hii ambayo inakuwa ikitekelezwa kwenye Halmashauri zetu inakuwa ni shida. Wapo ma-engineer natechnicians ambao wapo mitaani hebu na wenyewe sasa kutokana na umuhimu kwamba Serikali inapeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hii basi tuongeze pia idadi ya kuajili wataalam katika maeneo haya ili kusudi tuweze kupima ile value for money. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ukijaribu kuangalia wakati tunatekeleza miradi ya MMEM mwaka 2000/2001, tulikuja kukutana na changamoto hii kwamba tulianza kujenga madarasa kwa wingi maeneo yote nchi nzima lakini kwa sababu usimamizi ulikuwa ni mdogo tumejikuta kwamba madarasa mengi yaliyojengwa leo hayatamaniki wakati ni muda mfupi. Kwa hiyo, ili tusiendelee kufanya makosa yaleyale ndio maana nashauri kwamba Serikali tuongeze idadi ya kuajiri hususan wataalam katika sekta hii ya uhandisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikielekea kwenye upande wa makusanyo, niipongeze Serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI kwamba kwa sehemu kubwa kwa kweli wamefanya kazi kubwa baada ya kupeleka POS 7,227 kwenye Halmashauri zetu. Kupeleka POSni jambo moja lakini pia kukusanya mapato inavyotakiwa ni jambo lingine kwa sababu unaweza ukapeleka POS lakini POS zile wakazi-locate kwenye vyanzo ambavyo sio reliable yaani vyanzo ambavyo havina mapato ya kutosha na zile POS zingine ambazo zimekuwepo na zimekuwa zikifanya udanganyifu zinapelekwa kwenye vyanzo vile ambavyo ndio kuna makusanyo makubwa na kukawepo na leakage kama ambavyo tumefanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kama ambavyo Mbunge aliyechangia Mheshimiwa Komanya alisema kwamba ni afadhali zile POS ambazo zilikuwa zikitumika ambazo udhibiti wake sio rahisi basi zitolewe na Halmashauri hizi kwa sababu bei ya kununua POS hizi ambazo sasa zimedhibitiwa na kisasa bei imeshuka karibu kwa asilimia 75, basi walazimishwe kununua hizi POS mpya ambazo ni rahisi kuzidhibiti na hatimaye iwe rahisi sasa kuweza kuzungumza mfumo mzima wa makusanyo ili Halmashauri ziweze kuongezewa makusanyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusisitiza kwenye upande wa stahiki za Madiwani. Tunamalizia muda lakini wapo Madiwani katika maeneo mengi wanadai Halmashauri zao posho zao lakini pia hata makato ambayo yamekuwa yakikatwa kwenye mikopo yao haipelekwi kwenye mabenki lakini pia hata huduma ya bima wamekuwa wakikatwa lakini hazipelekwi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda uliobaki ni mdogo, tuombe kwamba Waziri mwenye dhamana na Serikali waweze kufuatilia kuhakikisha kwamba kwenye Halmashauri Madiwani hawa wasiondoke na madeni, wakati mwingine inakuwa ni ngumu kuweza kuja kudai baada ya kuwa wamemaliza muda wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo ya kuchangia na naunga mkono taarifa hizi za Kamati ya LAAC na Kamati ya PAC. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati. Niungane na Wabunge wenzangu waliotangulia kupongeza viongozi wetu Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wa Wizara hii kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya; tumepiga hatua kubwa. Ukijaribu kuangalia kulingana na taarifa coverage mpaka sasa hivi vijijini ni karibu asilimia 84 kwa maana ya kwamba kati ya vijiji 12,268 ni vijiji takribani 1990 tu ambavyo havijafikiwa na umeme na ambavyo nina uhakika kwamba 2020 basi tutakuwa tumefika maeneo yote hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika nikienda kwenye mradi wa REA hususan REA awamu ya tatu zipo changamoto ambazo tunaziona hususani katika speed kwa wakandarasi ambao wamepata zabuni hizi. Niombe katika Wilaya yangu ya Ngara usimamizi wa karibu kwa mkandarasi uweze kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama tulivyokuwa tumeanza kwamba tupeleke umeme kwenye maeneo kutokana na uhitaji ambapo kuna huduma za kijamii kama shule, afya n.k. Niombe kwamba katika Jimbo langu la Ngara kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ulipokuja; umeshakuja zaidi ya mara tatu; nimekuwa nikikulilia kwamba vile vijiji ambavyo vina huduma hizi, kama Kata ya Bukiriro kwa maana ya kijiji cha Bukiriro, Kijiji cha Mururama kwenda Kigarama, Mrusagamba Tanga, Kumbuga; kwa sababu ya umuhimu na huduma zilizoko kule tunahitaji kupata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vipo vijiji ambavyo vilipitiwa na umeme REA II lakini hakuna umeme unaopatikana; kwa mfano Kijiji cha Kenda ambapo line ya kutoka Ngara Mjini kwenda Lusumo boda ilipita pale na ukafanyika uharibifu; kwa maana ya kwamba kuna mazao yaliyokatwa lakini watu hawa hawajaunganishiwa umeme; sawa na Kijiji cha Kata ya Mabawe, Kijiji cha Murugina ambapo pia ulipita line kubwa lakini mazao kama kahawa yalikatwa na bado mpaka sasa hivi wananchi hawa hawajaunganishiwa umeme basi tuweze kuwafikiria hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwamba tuliunganishwa kwenye grid ya taifa mwaka wa jana lakini mpaka sasa hivi takribani mwaka mzima huduma ya umeme imekuwa ni shida kutokana na msongo wa umeme unaokuja kuwa mdogo, ambao mara kadhaa umekuwa ukikatikana hata kushindwa kukidhi kutoa huduma. Hii imeathiri hata huduma ya maji kwa sababu pampu zinazotumia umeme kusukuma maji zimekuwa haziwezi kufanya kazi vizuri na hivyo kusababisha adha ya ukosefu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi wa njia ya kusafirisha umeme mradi wa kutoka Rusumo kuelekea Nyakanazi. Line hii ni line ambayo imepelekea kwamba sasa wananchi wanaopitiwa na mradi huo hawajapata fidia mpaka sasa hivi. Mwaka jana kulikuwa na commitment ya Serikali kwamba kufikia mwezi wa tano mwaka jana wangekuwa wamepata fidia lakini mpaka sasa hivi wananchi hawa wa Kijiji cha Kafua, wananchi wa maeneo ya Benako kwenda mpaka Rusumo hawajapata fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mradi tunaoendelea nao katika Jimbo la Ngara ambao ni mradi wa nchi tatu, mradi wa maji wa Rusumo. Mradi huu umekuwa na changamoto kubwa kwa sababu wapo wananchi ambao mpaka sasa hivi ni mwaka wa tatu mradi umeanza hawajapata fidia. Kila ambapo wamekuwa wakijaribu kudai haki hiyo kumekuwa na uzungushwaji hususani Kampuni ya NELSAP ambao wanahusika moja kwa moja katika kuhakikisha kwamba watu hawa wanapata fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri katika hili ajaribu kufatilia kwa karibu ili wananchi ambao wanadai fidia katika mradi huu waweze kupata stahiki yao. Ipo athari kubwa ya milipuko katika eneo hili la mradi ukizingatia kwamba wanapochoronga kwa ajili ya kutengeneza tanel kumekuwepo na mtikisiko mkubwa. Awali ilikuwa ifanyike light blastaling lakini sasa hivi ilipofikia takriban mita 380 ambazo zinatakiwa zichorongwe kwa heavy blasting kuna athari kubwa ambayo itajitokeza na athari ambayo haikuonekana wakati wa kuandaa visibility study na detail design.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba katika vikao ambavyo Mheshimiwa Waziri unahudhuria, vikao vya mawaziri wenye dhamana muweze kuangalia ni namna gani ya kuhakikisha kwamba watu wanapata fidia lakini pia kuangalia namna…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti kuu ya Serikali na hali ya uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nichukue nafasi hii kuwapongeza viongozi wetu; Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mipango, Naibu Waziri, Dkt. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Mlinga alipokuwa akichangia alijaribu kuonyesha jinsi ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyofanya kazi katika kutekeleza Ilani. Wenzetu walijinasibu kwamba hiyo ni Ilani yao lakini naomba niwarejeshe kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kuanzia ukurasa ule wa 36 – 80, kwa maana ya Sura ya Tatu inaeleza jinsi ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaenda kuboresha huduma na miundombinu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, reli, kuimarisha huduma za usafiri wa anga na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza Ilani ya Uchaguzi. Kama walivyosema kwamba walichokifanya ilikuwa ni ku-copy na ku-paste mtakumbuka wakati wa uzinduzi wa kampeni mwaka 2015, walisema kwamba Ilani yao wananchi wataikuta kwenye website, hawakuwa na Ilani mezani. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Kwa hiyo, nimeona hili niliweke wazi ili kujua kwamba tunatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2015-2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba ifikapo 2025 tunafikia uchumi wa kati. Ili tuweze kufikia uchumi wa kati, ni lazima kujikita kuwekeza katika sekta nyeti ambazo zitatufanya tuweze kutoa ajira kwa wingi pia tuweze kukuza kipato cha Taifa na cha mtu mmoja mmoja. Lazima tuwekeze kwenye sekta ya kilimo kwa sababu hakuna namna ambavyo tunaweza tukawa na uchumi wa viwanda kama hatujawa na uwekezaji mzuri kwenye sekta ya kilimo, hatujatengeneza mazingira rafiki ya kufanya biashara, hatujaweza kuwa na vyanzo vya mitaji kwa maana ya kuwa na mikopo ya bei nafuu. Kwa hiyo, nipongeze Serikali kwamba katika mpango wake wa bajeti hii ya 2019/2020 wamejaribu kuangalia maeneo yote hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba katika sekta ya kilimo tumefanya vizuri kwa maana ya kwamba ni miongoni mwa sekta ambazo zimechangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 28.2 lakini bado unaweza ukaona kwamba tuna fursa kubwa ya kuongeza pato la Taifa kupitia sekta hii ya kilimo kwa sababu yapo maeneo ambayo tulitakiwa tuweze kuyafanyia kazi hususani eneo la umwagiliaji ni asilimia isiyozidi 6 tu kwenye maeneo yanayofaa kwa ajili ya umwagiliaji ambayo tumeweza kufanya. Kwa hiyo, bado tunayo nafasi, ukizingatia kwamba kuna mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaathiri hali ya upatikanaji wa mvua na hali ya ardhi ni vizuri sasa tukajikita kwenye kilimo cha umwagiliaji ili maeneo haya yaliyobaki takribani hekta karibu 20,000 zinazofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji tujikite huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuendelea lazima pia tuwe na Taifa ambalo limeendelea na ili tuweze kuendelea lazima tuwekeze kwenye elimu, hususani elimu ile ambayo itamwezesha pia mtu mmoja mmoja kuweza kujiajiri. Leo tunaona jinsi ambavyo vijana wanamaliza chuo kikuu na kushindwa kujiajiri. Najua kwamba katika michepuo tunayoenda nayo sasa ya masomo ya sayansi, kilimo na biashara lakini nishauri kwamba katika kuboresha elimu tujikite pia katika vocational training kwa maana ya kuboresha na kupanua wigo wa kuwa na vyuo vya VETA. Pamoja na kwamba Serikali imeweza kuonyesha jitihada na kuboresha vyuo vya FDC’s kwa maana ya vyuo vya maendeleo ya Taifa takribani 54 lakini bado havitoshelezi. Kwa hiyo, nashauri kwamba tuendelee kupanua wigo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata katika masomo yale ya kawaida kwenye zile taasisi ambazo ni za sanaa na sayansi, kwa sababu tunalenga kutengeneza elimu ambayo itamfanya mwananchi au vijana wetu waweze kujiajiri basi tuone uwezekano wa kuingiza somo la entrepreneurship katika kila tahasusi. Kwa mfano, badala ya masomo ya sanaa kwa maana ya HGL, HGK unaweza ukasema HEL au HEG, hizi tahasusi zipo katika nchi za East Africa Community kwa mfano Rwanda, Uganda na Kenya. Masomo haya yanawasaidia angalau anayemaliza kidato cha nne, kidato cha sita hata chuo kikuu kuwa na basic ya somo la entrepreneurship ambalo litamfanya aweze kupambana na hali yake anapokuwa akisubiri suala la ajira anaweza akajiajiri mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye upande wa miundombinu, miundombinu ya barabara na reli ni muhimu sana kwa ajili ya kuongeza au kuinua uchumi wa Tanzania. Nipongeze kwa jitihada za kuanza ujenzi wa reli ya Standard Gauge ambayo itatoka Dar es Salaam kuja Isaka na matawi yake kwenda Tabora – Msongati - Mwanza pia kwenda Keza - Kigali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, reli hii ni muhimu hususani katika eneo la Ngara ambapo kuna deposit kubwa nickel, kama reli hii ikijengwa na mgodi wa Nickel ukaweza kuanza utaweza kufanya reli hii iwe na tija kwa sababu mzigo utakaosafirishwa ni mkubwa na ambao unaweza ukasaidia katika kuhakikisha kwamba deni ambalo tunakuwa tumekopa kwa ajili ya ujenzi wa reli hii basi liweze kurudishwa kwa haraka kutokana na biashara ambayo tutakuwa tukiifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye upande wa feeder roads ambazo ziko chini ya TARURA, barabara hizi ni muhimu. Tunajua kwamba tunapowekeza kwenye kilimo, maeneo ya kilimo yako vijijini na ambako tunahitaji barabara safi na bora kwa ajili ya usafirishaji wa mazao kuyapeleka sokoni. Kwa hiyo, niombe kwamba katika maeneo ya Halmashauri zetu TARURA iweze kusimamia na kuangalia barabara ambazo ni za kipaumbele kwa kushirikiana na Halmashauri zetu ili kusudi barabara hizi ziweze kuboreshwa na hatimaye wananchi waweze kunufaika na uwekezaji katika barabara hizi kwa ajili ya kusafirisha mazao yao kupeleka sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata soko la mazao yao yameanzishwa masoko ya mipakani. Ngara ni miongoni mwa Wilaya ambayo iko mpakani mwa Rwanda na Burundi na lipo soko ambalo lilianzishwa la mpakani la Nzaza tangu mwaka 2013 lilipoanzishwa mpaka leo bado halijakamilika. Tunaomba miradi hii ambayo imeanzishwa kimkakati kwa lengo la kutengeneza masoko ya ndani basi iweze kukamilika ili wananchi waweze kupata maeneo ya kuweza kuuza biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)