Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Martha Festo Mariki (20 total)

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nampongeza Naibu Waziri wa Maji kwa kutoa majibu mazuri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imekuwa ikitenga pesa nyingi sana kwenda katika miradi mbalimbali katika Mkoa wetu wa Katavi na miradi hiyo huonekana kwamba haikidhi kutokana na ongezeko kubwa la watu katika Mkoa wa Katavi hususan Wilaya ya Mpanda. Je, ni lini Serikali itatoa maji kutoka chanzo cha uhakika cha Ziwa Tanganyika ili kukidhi mahitaji ya maji ya watu katika Mkoa wetu wa Katavi hususan Mji wa Mpanda ambao unaongezeko kubwa sana la wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kutokana na Serikali ilitenga fedha nyingi sana kwenda katika Mradi wa Mamba katika Wilaya ya Mlele, Jimbo la Kavu na mradi huo umekamilika, lakini mradi huo umekamilika kwa kuacha baadhi ya vijiji vingi sana kupata maji. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kuja kufanya ziara katika Mkoa wetu wa Katavi, kujionea jinsi gani Serikali imetenga pesa nyingi, lakini mradi huo umeonekana uko chini ya kiwango kwa baadhi ya vijiji vingi sana kutokupata maji? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Lugangira, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Swali lake la kwanza, lini Serikali itatumia Ziwa Tanganyika kupelekeka maji katika Mji wa Mpanda na Mkoa wa Katavi? Wizara imeshakamilisha usanifu wa miradi yote mikubwa ambayo itatokana na maziwa yetu makuu, ikiwemo Ziwa Tanganyika. Hivyo, kwa mwaka ujao wa fedha tunatarajiwa kuanza kazi hizi endapo kadri namna ambavyo tutakuwa tunapata fedha ndivyo namna ambavyo miradi hii ya Maziwa Makuu itakuwa inatekelezwa. Hivyo, hata kwa Mkoa wa Katavi nao tutauangalia kwa jicho la kipekee kabisa kwa umuhimu wake na niendelee kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kutoka Mkoa wa Katavi hasa Mheshimiwa Martha akiwa Mbunge wa Viti Maalum ameweza kuwajibika mara nyingi sana kufuatilia suala hili na sisi kama Wizara hatutamwangusha Mheshimiwa Martha pamoja na Wabunge wote wanaotoka ukanda ule.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anasema mradi umekamilika lakini baadhi ya maeneo maji hayatoki, anatamani mimi niweze kufika huko. Nimwahidi Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili la Bajeti, tutapanga pamoja ratiba ambayo itakuwa rafiki kwetu sote ili niweze kufika Mpanda nijionee na kabla ya mimi kusubiri hadi Mwezi Julai huko, nitaagiza wahusika pale tuna Managing Director wa Mamlaka ya Maji.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tuna RM wa pale, nitawaagiza waanze kufuatilia ili mpaka mimi nitakapokuwa naelekea huko kwa ajili ya ziara ikiwezekana wawe wameshafanya marekebisho na maji yaweze kutoka. (Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni hitaji la wananchi wa Kitulo la kuitangaza hifadhi hiyo kama kivutio ambacho kiko nchini kwetu; na kwa kuwa, hitaji hilo linafanana sana na hitaji la wananchi wa Katavi la kuitangaza Katavi National Park ambayo ina vivutio vingi sana vya asili vya utofauti akiwepo twiga mweupe anayepatikana kipekee sana katika Mkoa wetu wa Katavi:-

Je, Serikali ina mikakati gani mipya ya kuitangaza hifadhi hiyo ili iweze kufahamika ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Naibu Spika, ahsante. Serikali ina mpango wa kuipaisha hifadhi ya Katavi kwa kuzingatia bajeti iliyopo kwenye mwaka wa fedha wa 2021/2022. Eneo hili ni eneo zuri sana kwenye upande wa utalii.

Mheshimuwa Naibu Spika, hivyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Martha kwamba Serikali inatambua mchango wa Hifadhi ya Katavi na kwamba ni eneo zuri sana kwenye kuhamasisha utalii. Hivyo, tutajitahidi sana pamoja na maeneo mengine yote yaliyoko Tanzania ambayo yana vivutio kuhakikisha kwamba tunayatangaza ili tuweze kupata watalii wengi na kufikia namba ambayo imekusudiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Stalike – Kibaoni yenye urefu wa kilometa 71 ni ahadi ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na tayari barabara hiyo imeshafanyiwa upembuzi yakinifu.

Swali langu kwa Serikali: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami katika barabara hii, ukizingatia Mkoa wa Katavi ni moja kati ya mikoa michache sana ambayo bado haijafanikiwa kuunganishwa Mkoa na Mkoa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara hii ni muhimu na Mkoa wa Katavi upo kwenye mchakato wa kupata barabara za lami. Kama nilivyosema, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, bajeti yetu inaanza kujadiliwa tarehe 17 na tarehe 18 hapa Bungeni. Nitapata fursa ya kuwatajia barabara ambazo tumetangaza kwa mwaka huu na mwaka wa fedha ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie katika barabara muhimu ambazo zinajengwa kwa kiwango cha lami ni pamoja na kuunganisha Mkoa wa Katavi na maeneo mengine. Ahsante sana.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, kwanza naanza kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa kuitangaza hifadhi yetu ya Taifa ya Katavi lakini nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Swali la kwanza ilikuwa ni ahadi ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, mwaka 2019 ya kujenga hoteli ya Kitalii katika Mkoa wa Katavi katika Kata ya Magamba, ili hoteli hiyo iweze kuwavutia zaidi watalii kwa kupata malazi yaliyo bora na malazi yanayoridhisha. Je, huo mpango wa kujenga Hoteli ya kitalii katika Kata ya Magamba ambapo tulishatenga eneo umefikia wapi Ukizingatia hoteli hii itakwenda kuibua fursa nyingi kwa vijana wanaozunguka katika Mkoa wa Katavi kuweza kuapta ajira? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Katavi vikiwepo vijiji vya Mwamapuri, Chamalindi, Ikuba, Starike, Mangimoto, na Kibaoni vijiji hivi kwa muda mrefu vimekuwa havinufaiki na ujirani mwema kwa kupata miradi ya maendeleo kupitia TANAPA. Je, Serikali inatoa tamko gani ili vijiji hivi viweze kunufaika na hifadhi hiyo ukizingatia vijiji hivyo ndivyo vinavyotunza hifadhi hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Maliki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la hoteli ya kitalii kujengwa katika hifadhi ya Katavi ni kweli Hayati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, aliahidi katika ziara zake kwamba kujengwe hoteli ya kitalii katika hifadhi ya Taifa ya Katavi. Mpango huo umeshapangwa na kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2021/2022 mpango huu tumeuweka na hoteli hii ya kitaifa itaanza kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu ujirani mwema, ujirani mwema ni kweli Serikali imekuwa ikisaidia vijiji vyote vinavyozunguka maeneo ya hifadhi ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Katavi lakini kwa mwaka wa fedha 2021 tulikuwa na changamoto ya Korona hivyo tulishindwa kuhudumia haya maeneo ya hifadhi kama ambavyo Serikali imekuwa ikipanga. Lakini nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili sasa tunaenda kulitekeleza katika mpango wa fedha wa mwaka 2021/2022 vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi za Taifa, ujirani mwema utaenda kutekelezwa kwa kiwango cha juu, ahsante, (Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itakamilisha kupeleka umeme katika vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, vijiji ambavyo viko katika Kata ya Kakese, Kijiji cha Kamakuka, lakini katika Kata ya Mwamkulu vijiji kama Saint Maria, Kawanzige, Mkwajuni na Ikokwa, lakini katika Kata ya Kakese, Kijiji cha Songebila? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Katavi kwamba vile vijiji vyote alivyovitaja kikiwemo cha Saint Maria ambayo nimekisia vizuri vyote viko katika mpango wa REA III Round II na tayari mkandarasi ameshaaza kazi katika maeneo hayo tunamshukuru kwa sababu yeye na Mheshimiwa Pinda wamekuwa wakifuatilia na tunahakikisha kwamba kabla ya Disemba mwakani tayari vijiji hivyo vitakuwa vimepata umeme kwa ile programu tuliyoiweka ya mkandarasi kuhakikisha anapeleka umeme katika muda huo.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa vigezo vinavyowakwamisha vijana wetu wa Kitanzania hususan waliopo katika mikoa inayopakana na nchi jirani ikiwemo Mikoa ya Katavi, Kigoma na mingineyo ni pamoja na ucheleweshwaji na upatikanaji wa namba za NIDA.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutokutumia kigezo hiki wakati vijana wanapokuwa wanatumia ajira ili kuwawezesha vijana wetu waweze kupata ajira kwa kuwa mchakato huo bado haujakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili; ni kwanini sasa mfumo wa NIDA usiunganishwe na mfumo wa RITA wa vyeti vya kuzaliwa ili kuwawezesha Watanzania pale tu mtoto anapozaliwa aweze kupata cheti kimoja kinachounganisha kuonyesha kwamba huyu ni raia kwa kuzaliwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa kwa kuwa umefika wakati ameona umuhimu wa wananchi hasa wa mkoa wake kufanyiwa haraka katika kupata vitambulisho huku akiwa anajua kwamba vitambulisho kwa sasa NIDA ndiyo kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba sasa nianze kujibu swali la kwanza, kwamba, je, Serikali sasa haioni haja ya kuondosha hiki kigezo cha NIDA ili sasa mambo mengine yaweze kuenda yakiwemo ya vijana kuweza kupata ajira?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba tumeamua kuweka kigezo hiki ili kuweza kuwajua ni nani wenye sifa na nani wasiokuwa na sifa; na tumeamua kukiweka kigezo hiki ili kuona kwamba nani ambao wana Utanzania na nani ambao hawana Utanzania. Sasa kwa kusema moja kwa moja kigezo hiki kukitoa basi ni jambo ambalo linahitaji procedure, twende tukakae na watu wa utumishi na taasisi nyingine. Nimwambie tu Mheshimiwa kwamba jambo hili tunalichukua na tutakwenda kuona namna ya kulifikiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kikubwa kingine ninachotaka niseme ni kwamba, na hapa nataka nitoe agizo lakini pia nitoe wito kwa mamlaka hii inayosimamia; kwamba kwa sasa tuone namna ya kuwapa zaidi kipaumbele vijana ambao wanakwenda kutafuta ajira ili waweze kupatiwa hivi vitambulisho kwasababu tumeona na tumegundua kwamba kweli hii imekuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na yote hayo nichukue fursa hii niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba bado kuna wilaya vitambulisho vipo wenyewe hawajaenda kuvichukua, sasa matokeo yake tunaendelea kupata lawama. Tunataka tutoe wito tuwaambie Waheshimiwa Wabunge kwa kushirikiana na viongozi wengine huko wa Chama na Serikali muwaambie watu waende wakachukue vitambulisho vyao. Yapo maeneo vitambulisho vipo lakini hawajaenda kuvichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba, kwanini sasa tusiunganishe RITA na NIDA. Lengo na azma ya Serikali siku zote ni kuhakikisha kwamba wanatengeneza muunganiko wa mfumo ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi. Sasa kuunganisha RITA na NIDA si tatizo, Serikali ipo tayari kuunganisha mifumo lakini kuziunganisha taasisi nadhani ni jambo ambalo tunahitaji tukae sasa tufikirie tuone namna bora ya kuziunganisha hizi. Ni kweli zote ni taasisi za Serikali lakini zinao utofauti katika muundo na katika majukumu yake. Kwa hiyo nalo hili pia tutalichukua tuone namna ambavyo tunaweza tukaenda tukasaidia wananchi. Nakushukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Hospitali ya Mkoa wa Katavi inao upungufu mkubwa sana wa Madaktari Bingwa akiwemo Physician na Daktari Bingwa wa Watoto, pia Mkoa mzima Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake yupo mmoja tu.

Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge, kwanza hospitali yao ni mpya inayojengwa sasa, lakini ni kweli kwamba siyo tu kwa Mkoa wa Katavi bali upungufu wa Madaktari Bingwa uko karibu nchi nzima, ndiyo maana unaona kuna mkakati unaofanywa kuongeza Madaktari Bingwa. Nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge tuangalie la kufanya. Kwa sababu najua kuna Daktari wa Watoto aliyekuwepo pale alipelekwa Songwe, sasa tutaona ni nini kinafanyika ili kurekebisha hayo yaliyotokea. Ahsante.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza, naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini ripoti ya CAG mwaka 2020/2021 imeonesha kwamba fedha hizi zimekuwa nyingi zikipotea kutokana na kutorejeshwa ipasavyo: Je, Serikali inatoa tamko gani kuhakikisha fedha hizi zinarejeshwa ili ziweze kuwanufaisha wanufaika wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika mwaka wa fedha 2020/2021 na miaka ya fedha ya nyuma ya mwaka wa fedha huo, kulikuwa na kasi ndogo ya urejeshaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10, na Serikali ilitambua changamoto hiyo, tukachukua hatua; kwanza, kwa kuongeza usimamizi na uratibu wa mikopo pamoja na marejesho ya fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, nilijulishe Bunge lako Tukufu sasa kwamba mwenendo wa marejesho wa fedha hizi kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 umeongezeka kwa takribani asilimia 84 sasa ikilinganishwa na miaka nyuma ambayo ilikuwa chini ya asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kusimamia marejesho ya fedha hizi ili mfuko huu uendelee kuzunguka kunufaisha vikundi vingine.

Mheshimiwa Spika, nitoe tamko kwamba Wakurugenzi wa halmashauri zote kote nchini wahakikishe wanakopesha asilimia 10 kwa makundi yale kadri ya sheria, na wahakikishe wanarejesha fedha zile ili ziendelee kuwanufaisha wananchi wengine. Ahsante sana.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini bado kumekuwa kuna changamoto kubwa hususan kwa shule shikizi ambazo zilipata msaada kupitia maswala la UVIKO pamoja na kupitia Kapu la Mama.

Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na shule hizo kupatiwa walimu ikiwa shile hizo zimesajiliwa lakini nyingi zina mwalimu mmoja mmoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, pamoja na kuonekana kwamba kada ya walimu imekuwa ikiajiri sana walimu wakike lakini kwa Mkoa wa Katavi imekuwa ni tofauti. Katika Mkoa wetu wa Katavi kuna changamoto kubwa sana ya walimu wa kike katika shule za Sekondari; mfano katika shule ya Majalila, shule ya Mwamapuli ambapo shule hizo zimekuwa hazina kabisa walimu wa kike.

Je, Serikali inatoa tamko gani ili Watoto wetu waweze kupata mahitaji ambayo mtoto wa kike anayapata akiwa na mwalimu wa kike shuleni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua uwepo wa vituo shikizi ambavyo vinasaidia shule mama. Tulishatoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wote mikoa nchini kuhakikisha kwamba wanafanya msawazo na sehemu ya msawazo huo ni pamoja na kupeleka walimu kwenye hivo vituo. Kwa hiyo nirudie tena jmabo hili litekelezwe kama ambavyo Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais- TAMISEMI amekwishalitolea maelekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu walimu wa kike Mkoa wa Katavi kukosekana, tumelipokea ili tulifanyie kazi kwa kuongeza idadi ya waalimu katika ajira zinazofuatia, na katika maeneo ambayo kuna walimu wengi tutafanya msawazo vilevile kuwapeleka katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha, ahsante sana.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe ikiwepo ultrasound pamoja na x-ray? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mariki Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ukosefu wa vifaa tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe lakini hospitali zingine za Halmashauri na vituo vya afya ni kipaumbele cha Serikali nimuhakikishe Mheshimiwa Mbunge katika bajeti hii inayokuja lakini watumishi ambao wanaajiriwa katika mwaka huu wa fedha tutakipa kipaumbele kituo hiki cha afya na Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ahsante kwa Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali.

Je, Mheshimiwa Waziri unatuhakikishia pamoja na usanifu huo wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kuleta katika Mkoa wetu wa Katavi. Je, usanifu huo utaambatana pamoja na ufungaji wa mita za uhakika ambazo zitaenda kuondoa tatizo la ubambikizwaji wa bili kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi? Ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Dada yangu Martha kwa kazi kubwa anayoifanya katika Mkoa wa Katavi, kwa kweli ni kielelezo chema kwa ajili ya kuwapigania wananchi wa Katavi kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie kwamba tumepewa maelekezo mahsusi na Mheshimiwa Rais kuhakikisha tunatumia rasilimali toshelevu kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Nimhakikishie kwamba tunapokwenda katika bajeti hii 2022/2023 na asubiri katika bajeti yetu ya Wizara yetu ya Maji tumejipanga katika kuhakikisha tunakwenda kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika ili wananchi wa Katavi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, pili ni juu ya suala zima la malalamiko ya bili za maji. Wizara ya Maji tumeendelea kufanya mageuzi makubwa sana na hata katika wiki yetu ya maji tumeshaanza kuweka mifumo katika kudhibiti, pia katika kuhakikisha tunamaliza tatizo hili la maji kabisa la bili, tumeona kabisa kizuri huigwa tunaona sasa ni muda wa kutumia teknolojia zilizopo kwa kuanzisha prepaid meter kwa maana ya mita za maji (LUKU) ili kuhakikisha kwamba tunaondokana na tatizo la hili la maji.

Mheshimiwa Spika, tumesharuhusu wadau mbalimbali wameshaweza kufunga ili kuweza ku-study na muda si mrefu tutatoa maelekezo kwa ajili ya uanzaji wa hizo mita za maji(LUKU). Ahsante sana.(Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini katika Mkoa wetu wa Katavi changamoto bado ni kubwa sana. Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika vituo vya afya pamoja na Hospitali za Wilaya, lakini hospitali hizo zinashindwa kufanya kazi kama hadhi ya Hospitali ya Wilaya na badala yake kufanya kazi kama zahanati kutokana na upungufu mkubwa sana wa watumishi katika hospitali zetu za Wilaya za Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nijue, zipi hatua za haraka za Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaweza kupata watumishi ili waweze kupata huduma zilizo bora? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Katavi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatambua upungufu uliopo katika hospitali ndani ya Mkoa wa Katavi, lakini katika kupitia utaratibu ambao Serikali imeuweka kupitia mifumo ambayo tumeianzisha ndani ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, ambapo mojawapo ni pamoja na HR Assessment System, tumeweza kugundua hilo tatizo. Pia kwa kupitia mifumo ya upangaji wafanyakazi, tumeshaliona jambo hilo na ndiyo tumeahidi kupitia bajeti hii inayokuja ambayo tutawasilisha mbele ya Bunge lako hapa, kwamba hilo jambo la upungufu wa watumishi katika Mkoa wa Katavi nalo pia ni moja kati ya jambo tunalokwenda kulishughulikia.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kibaoni – Majimoto – Inyonga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, Katavi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilishatolewa ahadi na ipo kwenye Ilani. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, tuone bajeti tutakayopitisha, naamini kuna mapendekezo ya kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami, kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Tabora, ahsante.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Zaidi ya miaka kumi Mkoa wa Katavi umekuwa hatuna gari la Zimamoto.

Je ni lini Serikali italeta gari la Zimamoto katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika,Mkoa wa Katavi unalo gari moja la zimamoto lakini tunatambua kwamba ni bovu na liko kwenye matengenezo. Tutakachofanya ni kuharakisha matengenezo ya gari hili, ili angalau liweze kurejeshwa Katavi liweze kutoa huduma stahiki, nashukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa. Je, ni lini mradi wa umwagiliaji wa Mwamapuli uliopo Halmashauri ya Mpimbwe utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ukisoma katika kitabu chetu cha kwenye bajeti kiambatisho Na. 6, kimeelezea skimu ambazo tunakwenda kuzifanyia kazi kwa maana ya ujenzi kwa mwaka 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, skimu ya Mwamapuli yenye hekta 12,000 Wilaya ya Mpimbwe ni sehemu ya utekelezaji wa ujenzi wa katika mwaka wa fedha unaokuja. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge skimu hiyo inakwenda kutekelezwa.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, wananchi wa Mkoa wa Katavi hususan wa eneo hili wamekuwa wakizunguka umbali mrefu kupitia Eneo la Mpanda mpaka Inyonga kutokana na kwamba barabara hii kipindi cha masika imekuwa haipitiki kabisa.

Swali la kwanza; je, Serikali haioni sasa umuhimu wa haraka wa kufanya ujenzi wa barabara hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali inafanya ujenzi wa Barabara ya kutoka Mpanda – Uvinza mpaka eneo la Lulafe. Je, ni lini Serikali itakamilisha kilometa zilizobaki mpaka Uvinza ili tuweze kuunganishwa na wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwa ujenzi wa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii aliyoitamka ni kilometa hizo 60 ambazo zinahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini Serikali iliona umuhimu kwanza kwa kuanza ujenzi wa Daraja la Kavuu ambalo lilikuwa la chuma sasa tunakwenda kuweka zege na kazi hii inaendelea. Katika mwaka wa fedha sasa tutakamilisha hizo kilometa zilizobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwa Barabara hii ya Mpanda – Uvinza; barabara hii ipo na mkandarasi anaitwa CHICO na tayari tumeanza ujenzi wa kiwango cha lami kilometa 25 na tunategema kwamba mkataba huu utaisha baada ya mwaka mmoja na miezi sita. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo hayo yote, kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kutekeleza mradi huu na utakamilika kwa wakati, ahsante. (Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ni azma ya Serikali kukuza kilimo nchini. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuwapa kipaumbele kwenye mikopo wanafunzi ambao wanachaguliwa kwenda kusomea masomo ya kilimo hususan katika kampasi zilizopo pembezoni mfano kampasi ya Mizengopinda ya sasa hivi ina zaidi ya miaka mitatu ambayo imejikita zaidi katika kutoa elimu ya nyuki?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa sasa katika Mkoa wa Katavi tuna hiyo kampasi moja. Serikali haioni kuna umuhimu wa kuongeza kamapasi nyingine ili kupanua wigo wa elimu katika Mkoa wetu wa Katavi kwa kuongeza kampasi kama vyuo vya afya pamoja na vyuo vya uhasibu? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Mariki Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza anataka kufahamu mkakati wa Serikali juu ya mikopo. Naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge Serikali imekuwa ikiongeza kiwango au kiasi cha mikopo kwa wananfunzi wa elimu ya juu. Kwa takwimu zilizopo kwa mwaka 2021/2022 tulitenga na kupeleka jumla ya bilioni 570 kwa ajili ya wanafunzi hao. Mwaka 2022/2023 tulipeleka zaidi ya bilioni 554 hela ya kawaida lakini tulikuwa na vile vile bilioni tatu kwa ajili ya Samia Scholarship lakini katika bajeti yetu vile vile tumeweza kutenga jumla ya bilioni 738 kwa ajili ya mikopo katika mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba Serikali imejipanga na kujizatiti kuhakikisha kwamba wanafunzi wetu wanapata mikopo kwa wakati wake.

Mheshimiwa Spika, tuna kozi za vipaumbele ikiwemo na hiyo aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge kozi za sayansi lakini zile za uhandishi, kozi za udaktari na kozi hizi za kilimo pamoja na masuala ya nyuki kwa ujumla wake ndizo ambazo tunazizingatia katika utoaji wa mikopo katika kipindi kijacho.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anataka kufahamu utaratibu gani Serikali itatumia kuongeza idadi ya vyuo. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Uwepo wa kampasi hii unaweza ukasaidia katika kuongeza aidha ndaki au shule nyingine katika kampasi hii. Kwa sababu tukumbuke hata hiyo University of Dar es Salaam wakati inaanzishwa ilianza na kozi moja lakini imeweza kupanuka mpaka hivi sasa ina kozi mbalimbali. Kwa hiyo, hata kozi hizi hapo baadae tutaangalia uhitaji na namna gani ya kuweza kuangalia kozi nyingine za kuanzishwa katika kampasi hii, nakushukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika hatuna kabisa Kituo cha Polisi, lakini wananchi wa Wilaya hiyo wameonesha juhudi kwa kuanzisha ujenzi wa kituo cha polisi kwa kujenga msingi. Je, ni lini Serikali itaunga juhudi hizo kwa kutupatia pesa ili tuweze kukamilisha kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuahidi Mheshimiwa Mariki kwamba, tunatambua umuhimu wa kuwa na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya na vituo vingine kwenye Tarafa husika katika Wilaya ya Tanganyika. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, tumeshaongea hata na Mbunge wa Jimbo kwamba, kwenye bajeti yetu ijayo tutaona uwezekano wa kuwachangia ili waweze kujenga kituo hicho, tumuombe Mwenyezi Mungu liwezekane liweze kutekelezwa, nashukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini katika Mkoa wetu wa Katavi katika Jimbo la Nsimbo tuna x-ray ambayo Serikali imetupatia lakini x-ray hiyo imeshindwa kufanyakazi kutokana na kwamba hatuna mtaalam wa mionzi.

Je, ni lini Serikali itatupatia mtaalam wa mionzo ili x-ray iweze kufanyakazi kwa kuwahudumia wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili; katika Wilaya ya Tanganyika Kata ya Ilangu wananchi ususani kinamama wajawazito wamekuwa wakifata huduma mbali sana kutokana na kwamba hawana kituo cha afya; je, ni lini Serikali itatujengea kituo cha afya katika Kata hiyo ya Ilangu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Martha Mariki, la kwanza hili la wataalamu wa mionzi, hivi karibuni katika mwaka huu wa fedha Serikali imeajiri watumishi wa kada ya afya 8,000 na tayari katika matangazo yale wakati yanatolewa ilikuwa tunatafuta watalamu wa mionzi ya x-ray 69. Lakini nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba katika ajira hizi walipatikana watumishi 61 tu na hizi nafasi nyingine zilizosalia tutazitangaza upya ili kuweza kuwapata watalam hawa wa mionzi na tuweze kuwapeleka maeneo mbalimbali nchini ambapo Serikali imewekeza fedha nyingi katika ununuzi wa vifaa tiba ikiwemo mitambo ya mionzi na kule Nsimbo napo tutapaangalia kwa ajili ya kuwapeleka watalamu hawa wa mionzi.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la Kituo cha Afya katika Kata ya Ilangu iliyopo kule katika Wilaya ya Tanganyika, tutatuma timu ya watalaam kwa ajili ya kwenda kufanya tathimini katika Kata ya Ilangu, kuona idadi ya watu waliokuwepo pale na vile vigezo vinavyotakiwa vya umbali kwenda kufata huduma ya afya na kadhalika na baada ya tathimini hiyo kufanyika tutapata taarifa katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kuweka katika mipango yetu kuhakikisha kwamba wananchi wa Kata ya Ilangu wanapata huduma ya afya iliyobora kwa kupata kituo cha afya.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kutenga bilioni tano kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivi, lakini, pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba inaboresha elimu nchini hususan elimu ya sekondari kwa upande wa sayansi. Nidhahiri kabisa katika Mkoa wetu wa Katavi bado kuna upungufu mkubwa sana wa walimu hususan walimu wa kike na walimu wa sayansi. (Makofi)

Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na Mkoa wa Katavi ambao una upungufu mkubwa, ikiwepo shule ya Mwangaza ina mwalimu mmoja tu wa sayansi na Shule ya Rungwa ambayo ina zaidi ya wanafunzi 1500 lakini haina kabisa walimu wa sayansi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Je, Serikali inaongeza jitihada gani kuhakikisha kwamba ina boresha elimu ya sayansi hususan kuhakikisha watoto wa kike wanakwenda kuongezeka na kupata elimu ya sayansi nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Martha Mariki na hili la kwanza la upungufu wa walimu Mkoani Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kuhakikisha inaondoa upungufu wa walimu katika maeneo yote nchini ikiwemo Mkoa wa Katavi; na katika Mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali iliajiri jumla ya walimu wa sayansi 6,949.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka huu ambayo inatekelezwa ya 2023/2024 Serikali imetenga ajira kwa ajili ya kupunguza upungufu wa walimu wa sayansi. Tunaendelea kuratibu na wenzetu wa Ofisi ya Rais, Utumishii li kuweza kupata vibali vya kuweza kuajiri walimu hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu swali la pili la Mheshimiwa Martha Mariki linalohusu jitihada za Serikali; Serikali hii, hasa utashi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, alihakikisha kwamba tunakwenda kujenga shule za wasichana za sayansi katika kila mkoa. Awamu ya kwanza, Mheshimiwa Rais alitoa fedha kwa ajili ya kujenga shule kumi kwenye mikoa kumi na awamu ya pili kuna fedha bilioni 48 imekwenda kwenye mikoa 16. Hii yote ni kuhakikisha kwamba watoto wa kike wanapata elimu iliyobora na elimu ya sayansi katika mikoa yote. Hivyo, awamu ya kwanza jumla ilienda bilioni 40 na awamu ya pili bilioni 48.