Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Martha Festo Mariki (13 total)

MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji Mkoa wa Katavi ni asilimia 70. Serikali kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mpanda inatekeleza miradi miwili ya maji ambayo ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji na imeshaanza kutoa huduma ya maji. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa banio, ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilomita 24 kutoka katika chanzo cha maji Ikolongo II na ujenzi wa tenki la lita milioni moja kwa ujumla wa mradi, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa Manispaa ya Mpanda ambapo mji huo ni miongoni mwa miji 28 itakayonufanika na utekelezaji wa mradi wa maji kupitia fedha za mkopo kutoka Serikali ya India. Kazi hii inatarajiwa kuanza hivi karibuni na itachukua miezi 24. Aidha kupitia RUWASA utekelezaji wa miradi 30 unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021. Miradi hii, ikikamilika jumla ya vijiji 138 vya Mkoa wa Katavi vitakuwa na huduma ya maji ya uhakika, hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kufanya kazi za maendeleo.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Katavi ili iweze kupata watalii wengi na kuongeza mapato. Aidha, Hifadhi ya Taifa Katavi imekuwa ikitangazwa kupitia vyombo vya habari vilivyopo ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Katavi iliandaa Mpango Mkakati wa Kukuza Utalii kwa Mkoa wa Katavi mwaka 2019 ambao umesaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza Hifadhi ya hiyo na mikakati mingine inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na Kuvitangaza vivutio vilivyomo ndani ya hifadhi ikiwa ni pamoja na wingi wa Viboko, Simba na Twiga weupe. Vilevile Wizara ina mkakati wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa Katavi kupitia tovuti na mitandao ya Kijamii yaani Instagram, Facebook na Twitter lakini pia kuimarisha miundombinu ya barabara ndani ya Hifadhi husika ili kurahisisha kufikika kwa maeneo ya vivutio ndani ya Hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuitangaza Hifadhi hii kupitia chaneli maalum ya Tanzania Safari Channel, lakini pia kusimika mabango kwenye mikoa ya jirani kama vile Mbeya, Songwe, Tabora na Kigoma. Serikali pia inaandaa safari za mafunzo kwa wanahabari, mawakala na wadau mbalimbali wa utalii kwa lengo la kuwapa fursa ya kuvielewa vivutio vya utalii na kuvitangaza ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mwingine ni pamoja na kujenga sehemu ya malazi ya bei nafuu kwa ajili ya wageni wa ndani na nje ya nchi, na pia kuandaa video au filamu na machapisho mbalimbali na kuyasambaza kwa wananchi na mabasi ili kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Katavi;

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuzitangaza Hifadhi za Taifa kupitia maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ili kuwezesha kupata wawekezaji na watalii. Ni imani ya Serikali kwamba jitihada zinazoendelea kufanywa za kutangaza vivutio hivyo katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi zitaendelea kuzaa matunda na hivyo kuwapatia wananchi wa Katavi na Taifa kwa ujumla manufaa stahiki.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi kwa kuwa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inaendelea kutekeleza mpango kazi wa kuzalisha vitambulisho, na inatarajiwa ifikapo Agosti, 2021 wananchi wote waliotambuliwa na kupewa namba za usajili watakuwa wamepatiwa vitambulisho. Aidha, mpango huu unalenga kuzalisha vitambulisho kwa awamu kwa kila wilaya, ambapo kwa kipindi cha kuanzia tarehe 14 Januari 2021 hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2021 Mamlaka imefanikiwa kuzalisha na kusambaza vitambulisho 7,148,971 katika wilaya 73 nchini. Tanzania bara wilaya 63 na Zanzibar wilaya 10, na kazi ya uzalishaji inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Mei, 2021 Mamlaka imefanikiwa kugawa namba za utambulisho kwa wananchi 11,737,021 Kutokana na mfumo wa NIDA kuunganishwa na mifumo mingine ya taasisi za Serikali na binafsi. Aidha, wananchi wanaendelea kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kama vile huduma za kifedha, kufungua biashara, kupata namba ya mlipa kodi (TIN), kupata hati za kusafiria, umilikishaji ardhi na kusajili laini za simu kwa kutumia namba za utambulisho wakati wakisubiri kupatiwa vitambulisho vyao vya taifa. Nakushukuru.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na mikoa jirani ya Kigoma, Rukwa na Tabora ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na jitihada za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma ambapo ujenzi wa barabara ya Mpanda – Ifukutwa - Vikonge yenye urefu wa kilometa 37.65 umekamilika kwa kiwango cha lami. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 sehemu ya barabara ya Vikonge – Mishamo Junction yenye urefu wa kilometa 62 imetengewa shilingi milioni 3,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali kupitia TANROADS iko katika hatua za mwisho za mchakato wa zabuni ya kumpata mkandarasi wa ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mikoa ya Katavi na Rukwa, ujenzi wa sehemu za Sumbawanga – Kanazi urefu wa kilometa 75, Kanazi – Kizi – Kibaoni kilometa 76 na Mpanda – Sitalike kilometa 36.5 kwa kiwango cha lami umekamilika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 4,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kibaoni – Sitalike yenye urefu wa kilometa 71. Serikali kupitia TANROADS iko katika hatua za mwisho za mchakato wa zabuni ya kumpata mkandarasi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa Mikoa ya Katavi na Tabora, utekelezaji wa barabara ya Tabora – Ipole – Koga – Mpanda yenye urefu wa kilometa 359 ni kama ifuatavyo; Tabora – Sikonge yenye urefu wa kilometa 30 ujenzi umekamilika; sehemu ya Usesula – Komanga yenye urefu wa kilometa 108 na barabara ya kuingia Mji wa Sikonge yenye urefu wa kilometa 7.5; sehemu ya Komanga – Kasinde yenye urefu wa kilometa 108 na barabara ya kuingia Mji wa Inyonga kilometa 4.8; sehemu ya Kasinde – Mpanda kilometa 108 na barabara ya kuingia Mji wa Urwira yenye urefu wa kilometa 3.7 ujenzi wake umekamilika. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaongezea mkopo akina mama wajasiriamali wa Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri za Mkoa wa Katavi zimekuwa zikitoa mikopo ya uwezeshaji kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kuzingatia sheria na kanuni za utoaji mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri za Mkoa wa Katavi zilitoa jumla ya mikopo ya Shilingi milioni 980 sawa na asilimia 105 kwa vikundi 124 vyenye jumla ya wanufaika 850. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 halmashauri za mkoa huo zimepanga kutoa mikopo hiyo yenye jumla ya Shilingi bilioni 1.45 sawa na ongezeko la kiasi cha Shilingi milioni 470.

Mheshimiwa Spika, halmashauri zitaendelea kuongeza kiwango cha mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kulingana na ongezeko la makusanyo ya mapato ya ndani. Ahsante sana.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutatua changamoto ya uhaba wa walimu katika shule za pembezoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa ajira ili kukabiliana na upungufu wa walimu shuleni, unaotokana na walimu kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa, kufariki na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa. Tangu mwaka 2018/2019 hadi mwaka 2021/2022, Serikali imeajiri jumla ya walimu 26,598 wakiwemo walimu 16,640 wa shule za msingi na walimu 9,958 wa shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina hakikisha walimu wanaajiriwa na kupangwa katika shule zenye uhitaji zaidi, hususan zilizoko maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020 Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliboresha mfumo maalum wa maombi ya ajira na upangaji wa walimu ujulikanao kama Teachers Allocation Protocol. Kupitia mfumo huo, shule zenye upungufu mkubwa wa walimu hususan zilizoko vijijini hubainishwa, ambapo walimu huomba ajira moja kwa moja kwa kuchagua shule husika iliyopo katika mfumo. Aidha, Ofisi ya Rais – TAMISEMI imetoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara kufanya msawazo wa walimu kutoka shule zenye ziada na kuwapeleka katika shule zenye upungufu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri walimu kulingana na mahitaji na upatikanaji wa fedha ili kukabiliana na uhaba wa walimu hususani katika maeneo ya pembezoni.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa kutoa Maji Ziwa Tanganyika na kuyapeleka Mkoa wa Katavi?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya huduma ya upatikanaji wa maji Mkoa wa Katavi ni asilimia 71 kwa Vijijini na asilimia 60 kwa Mjini. Katika kuboresha huduma ya maji Serikali imeanza kutekeleza miradi ya maji kwa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 mradi unaoendelea kutekeleza ni Mradi wa Maji Karema katika Wilaya ya Tanganyika utakaohudumia vijiji vya Kapalamsenga na Songambele.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kutumia Maziwa Makuu kunufaisha wananchi waishio karibu na vyanzo hivyo ikiwemo wananchi wa Mkoa wa Katavi uliopo karibu na Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali itaajiri Mtaalam Mshauri wa kufanya usanifu wa kina wa ujenzi wa miundombinu wa chanzo cha maji (intake) chenye uwezo wa kuzalisha maji mengi kutoka Ziwa Tanganyika na kuwezesha wananchi wa Wilaya za Tanganyika, Mlele, Mpanda na maeneo ya karibu kunufaika na chanzo hicho.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Watumishi katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi wa Mkoa wa Katavi kila mwaka kwa kuendelea kutenga Ikama na Bajeti kama inavyopitishwa na Bunge lako. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali ilitenga nafasi 522 za kada mbalimbali kwa Mkoa wa Katavi na katika mwaka wa fedha ujao (2023/2024) tunakusudia kutenga Ikama ya ajira mpya 914 kwa Mkoa wa Katavi iwapo Bunge lako likiridhia na kuipitisha Bajeti ya Serikali iliyopendekezwa.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga barabara ya Kibaoni – Majimoto hadi Inyonga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Majimoto hadi Inyonga yenye kilometa 162. Hadi sasa jumla ya kilometa 9.3 zimejengwa kwa kiwango cha lami sehemu ya Inyonga kilometa 4.2 na Majimoto kilometa 2.6 na Usevya kilometa 2.5 ambapo ni Makao Makuu ya Halmashauri ya Mpimbwe. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa sehemu iliyobaki, ahsante.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha matawi ya Vyuo Vikuu vya Umma katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imelenga kupanua na kuboresha huduma za jamii ikiwemo Elimu ya Juu ili kufikia maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na azma hiyo, Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation – HEET wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021-2026 inatarajia kujenga kampasi mpya 14 za Vyuo Vikuu katika mikoa ambayo haina Taasisi ya Elimu ya Juu ukiwemo Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Spika, Kupitia Mradi wa HEET, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetengewa jumla ya shilingi bilioni 18.4 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi mpya katika Mkoa wa Katavi Wilaya ya Mlele, Halmashauri ya Mpimbwe. Kwa sasa kazi zinazoendelea katika kampasi hiyo ni tathmini ya athari za kimazingira na Jamii yaani environmental and social impact assessment na mchakato wa kumpata mshauri elekezi unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni 2023 na baadaye mkandarasi wa ujenzi, nakushukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya vifaa tiba katika Hospitali za Wilaya zinazojengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali ilitenga shilingi bilioni 7.1 kwa ajili ya vifaa tiba vya kinywa/meno na macho kwa hospitali 71. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 15.5 kwa ajili ya vifaa tiba kwenye hospitali 31 zinazoendelea na ujenzi kila moja imetengewa shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali zote nchini ili kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawaajiri vibarua wapatao 20 ambao wamefanya kazi Shirika la Reli Mkoa wa Katavi kwa miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango uliofanywa na vijana wa Kitanzania ambao wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya reli ikiwemo ukarabati wa njia ya reli katika Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania inaendelea kuwatumia vijana hao katika miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa njia ya reli na imekuwa ikiwahimiza vijana hao kujiendeleza ili kuwa na sifa ya kuajiriwa katika utumishi wa umma kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma. Kupitia utaratibu huo vibarua wawili wamejiendeleza na kuajiriwa na wengine wanaendelea kuhamasishwa.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kwa maabara ya sayansi katika shule za Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mpango wa kuboresha elimu ya sekondari katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga shilingi bilioni 5.148 kwa ajili ya kununua vifaa vya maabara ili viweze kusambazwa katika shule za sekondari kote nchini ikiwemo shule za Mkoa wa Katavi. Ununuzi wa vifaa hivyo upo katika hatua za mwisho kulingana na taratibu za manunuzi.

Aidha, katika Mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilipeleka vifaa vya Maabara katika Shule za Mbede, Usevya, Mizengo Pinda, Mamba, Chamalendi, Kasansa, Kabungu, Karema, Mpandandogo, Kandamilumba, Mwese, Kapalamsenga na Homera zilizopo kwenye Mkoa wa Katavi.