Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Martha Festo Mariki (10 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kuniona. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema. Kipekee sana napenda kuwashukuru baba na mama yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini mimi kama binti na kama kijana kuweza kuwawakilisha akinamama wa Mkoa wa Katavi. Pia napenda sana kuwashukuru akinamama wote wa Mkoa wa Katavi na UWT kuanzia ngazi ya Mkoa mpaka Taifa. Pia kipekee naomba nimshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyoendelea kuchapa kazi na jinsi anavyoendelea kulipeleka Taifa letu la Tanzania mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisoma sana hotuba ya Mheshimiwa Rais, hotuba hii imebeba maono na dira ambayo inaonyesha ni jinsi gani Tanzania itakwenda mbele katika uchumi endelevu; kutoka uchumi wa kati mpaka uchumi wa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana nijikite katika sekta ya afya. Naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa jinsi ambavyo inaendelea kupambana kuhakikisha kwamba huduma za afya zinaboreshwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii adhimu kuiomba sana Wizara ya Afya, watuboreshee Hospitali ya Wilaya ambayo kwa sasa inatumika kama Hospitali ya Mkoa wa Katavi, kutokana na kwamba mkoa wetu una fursa nyingi sana ikiwemo kilimo, biashara ambazo zinasababisha kuwepo na mwingiliano wa watu wengi. Hivyo, tunaomba sana Serikali yetu sikivu itusikie kwa kutuboreshea Hospitali ya Mkoa wetu wa Katavi ili iweze kuwahudumia wananchi wanaoingia kwa wingi kufuata fursa nyingi za kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda sana nichukue nafasi hii katika kuchangia suala la kilimo. Katika hotuba hii Mheshimiwa Rais ameelezea kuhusu suala la kilimo kwamba atahakikisha kinasonga mbele katika nchi yetu ya Tanzania. Nikiwa kama mwakilishi wa akinamama Mkoa wa Katavi, wananchi wamenituma kwamba katika sekta ya kilimo, kumekuwa na sintofahamu kuhusiana na wakulima wetu. Wakulima wamekuwa na changamoto ambapo wanailalamikia Serikali kuhusu mambo ya Stakabadhi ghalani. Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuja mkoani kwetu alisema Mkoa wa Katavi wakulima wake hatujakidhi vigezo vya kuungwa katika Stakabadhi Ghalani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sekta ya kilimo iweze kutoa maelekezo na tamko: Je, wananchi wa Mkoa wa Katavi tumefikia hadhi ya kuungwa katika Stakabadhi Ghalani? Kama sivyo, basi waweke utaratibu ili wananchi wetu wa Mkoa wa Katavi ambao ni wapiga kura wetu waliotuamini sana waweze kuondokana na sintofahamu hiyo, kwa sababu wanategemea sana kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuchukua fursa hii kuipongeza Wizara ya Elimu kwa jinsi ambavyo inaendelea kupambana. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi ambavyo anapeleka elimu yetu mbele kwa kutoa elimu bure kuanzia form one mpaka form four. Katika Mkoa wetu wa Katavi nasi tungependa kuwa na vyuo vingi kama ilivyo katika mikoa mingine. Vyuo hivyo vimwezeshe mtoto wa kike katika Mkoa wa Katavi aweze kwenda kupata elimu kwa ukaribu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nawakaribisha sana Waheshimiwa wenzangu mje mwekeze katika Mkoa wa Katavi wenye fursa nyingi zikiwemo za kiutalii na kilimo. Karibuni sana, Katavi imenoga jamani, karibuni. (Kicheko/Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi katika wizara hii ya Ulinzi.

Kwanza napenda kuipongeza Wizara hii kwa kazi kubwa inayoifanya kwa kuhakikisha Taifa linakuwa salama muda wote. Tunatambua uzalendo wao kwa Taifa hili na sisi kama wawakilishi wa wananchi tutakuwa nao bega kwa bega.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na pongezi hizo tuna changamoto katika Mkoa wa Katavi wa mgogoro baina ya jeshi na wananchi wa Mpanda Manispaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro umekuwa wa muda mrefu sana, namuomba sana Mheshimiwa Waziri kupitia Serikali watoe tamko kwani wananchi hao wamekuwa wakifanya shughuli za maendeleo katika maeneo hayo kwa muda mrefu kutokana shughuli za jeshi katika eneo hilo imesababisha mgogoro na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali itoe tamko ili wananchi wajue hatima yao kwani mpaka sasa wananchi hawajui nini hatima ya mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia jioni hii ya leo. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema. Kipekee naishukuru na kuipongeza sana Wizara ya TAMISEMI kwa jinsi ambavyo inasaidia kina mama kupata mikopo ya asilimia 10 ambapo ni asilimia 4 kwa vijana; asilimia 4 kwa kina mama; na asilimia 2 kwa walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimesoma na kuuelewa sana Mpango huu wa Maendeleo wa miaka mitano. Naomba sana nijikite kuishauri Serikali kuangalia namna ambavyo inaweza kuwasaidia akina mama na vijana hawa kwa kuwaboreshea kutoka kwenye asilimia zile 4:4:2 na kuwapa asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyoelewa, kina mama ndiyo wanaoweza kuibeba jamii na ndiyo wanaobeba familia katika kuzihudumia. Hivyo naiomba sana Serikali sasa ione kuna umuhimu wa kina mama hawa ambao pia ndiyo waaminifu wakubwa katika upigaji wa kura, kina mama hawa ambao wamekibeba Chama cha Mapinduzi kwa kuwa waaminifu kwa kupiga kura nyingi sana za ndiyo kwa rahisi wetu Dkt. John Pombe Magufuli, sasa ni wakati wa Serikali yetu sikivu ione umuhimu wa kuiboreshea kina mama hawa kutoka kwenye mkopo wa asilimia 4 na kuwapa asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Serikali yetu sikivu iweze kutoa elimu ya kutosha, elimu wezeshi kwa kina mama hawa ili waweze kunufaika na mikopo hii. Kuna baadhi ya maeneo kina mama kweli wamekuwa wakiomba mikopo na kupewa mikopo hii lakini mikopo imekuwa haiwanufaishi kutokana na kwamba elimu wanayopewa ni ndogo. Mfano, kina mama wanaojitolea katika kazi za za kufuga nyuki, napenda sana Serikali yetu sikivu iweze kutoa elimu wezeshi kwa kina mama hawa ni namna gani wataweza kufuga nyuki ili waweze kunufaika wao lakini waweze kutoa wigo wa ajira katika jamii zinazowazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana napenda nijikite katika kuzungumzia Wizara ya Maliasili. Niiombe sana Serikali yetu sikivu, sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi tunayo Katavi National Park, naiomba sana Serikali yetu sikivu ili kuendana na Mpango huu wa Maendeleo ituboreshee barabara katika maeneo yale ya hifadhi ili kuwawezesha watalii wanaokuja Katavi kuweza kupita kwa urahisi zaidi. Tumeona kipindi cha masika ambacho ndicho kipindi wanyama wanapatikana kwa wingi, kipindi ambacho utalii ungefanyika kwa wingi kule Katavi, barabara hazipitiki na hivyo kuwazuia watalii wengi kuvutiwa kuja Katavi National Park. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba sana Serikali yetu sikivu kuiboresha hifadhi hii kwa ku—promote kwa kutoa matangazo mbalimbali ili watu wote duniani waweze kuifahamu Katavi National Park. Katavi National Park ni hifadhi pekee yenye Twiga mweupe. Natamani sana Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wenzangu muifahamu Katavi National Park, ni hifadhi ambayo ina vivutio vingi sana. Hivyo, Serikali ikiboresha miundombinu katika hifadhi hii itaweza kupata mapato makubwa lakini tutaweza kwenda kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi wakiwepo vijana wanaozunguka mkoa ule. Pia itawasaidia kina mama kwa kuwawezesha kutengeneza curio shop ambapo wataweza kuuza vinyago mbalimbali kwa watalii lakini kutoa fursa mbalimbali za kibiashara ikiwepo mama ntilie kupika na kuwahudumia watalii wanaokuja katika hifadhi hii ya Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kutoa shukrani zangu za dhati kwa jinsi Serikali inavyoendelea kutuhudumia wananchi wa Katavi kwa kutupa miundombinu katika maeneo mbalimbali lakini kutupa ulinzi na kuhakikisha hali ya amani ipo katika Mkoa wetu wa Katavi. Hivyo naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee naendelea sana kuwashukuru akina mama wa Mkoa wa Katavi kwa jinsi ambavyo wameniamini mimi kama mwakilishi wao kuja kuwawakilisha. Nawaahidi sitawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi katika Wizara hii muhimu sana kwa maisha ya wananchi wangu wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha anakwenda kumtua ndoo mama kichwani. Katika mwaka mmoja sasa Mheshimiwa Rais ameonesha njia nzuri ya jinsi ya kupambana na kutatua changamoto ya maji katika nchi yetu na sisi kama wawakilishi wa wanawake tutaendelee kumpatia ushirikiano wa dhati ili kutimiza azma yake ya kuwatua ndoo kinamama wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Juma Aweso, Waziri wa Maji kwa kazi kubwa anayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kuhakikisha huduma ya maji inapatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, lakini nimpongeze Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kwa kazi kubwa wanayoifanya, ukweli kazi inafanyika na inaonekana. Pia nimpogeze Naibu Waziri mwanamama shupavu Mheshimiwa Maryprisca kwa kazi kubwa anayoifanya kuwasaidia akinamama wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kumpogeza Mheshimiwa Waziri lakini bado kuna changamoto ndogo ndogo zilizopo katika Mkoa wa Katavi. Lengo la Serikali ni kufikisha maji kwa mijini asilimia 85 na vijijini kufikia asilimia 60, lakini kwa Mkoa wa Katavi bado ile azma ya Serikali bado haijafikia.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha changamoto za maji katika Mkoa wa Katavi, kumekuwa na kukatikakatika kwa maji, inafikia hatua mwezi mzima maji hayapatika katika baadhi ya maeneo, lakini wananchi wamekuwa wakiletewa bill kubwa za maji na kubambikiwa bill za maji kutokana na mita kutokuwa za uhakika. Nashauri Mheshimiwa Waziri zifungwe mita za uhakika na ziwe na uwazi mkubwa ili wananchi wetu wawe na uelewa kusoma bill zao.

Mheshimiwa Spika, ilikutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Katavi lazima mradi wa ziwa tanganyika ufanyike kwa haraka ndio utakuwa mkombozi mkubwaa wa wananchi wa Mikoa Kigoma,wakatavi na Rukwa. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo katika Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini kipekee sana, ninampongeza sana Mheshimiwa Jumaa Aweso, Waziri wetu wa Maji na dada yangu, Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, kwa jinsi wanavyoendelea kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mpanda ni mji ambao upo katika Makao Makuu ya Mkoa wetu wa Katavi. Mji huu wa Mpanda una fursa nyingi sana zikiwemo fursa za kilimo, kiutalii na kimadini. Lakini Mji wetu huu wa Mpanda una changamoto sana ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naiomba sana Serikali kwanza kwa kuipongeza kwa jinsi ambavyo wameonesha jitihada zao katika kuhakikisha Mji huu wa Mpanda unakwenda kupata maji ya uhakika ili kuweza kuwakomboa wananchi wake. Naishukuru sana Serikali kwa kutuletea Mradi wa Ikorongo Na. 01, lakini wakaona haitoshi, Mradi wa Ikorongo Na. 01 ulivyokuwa hautoshelezi kwa maji wakatuletea Ikorongo Na. 02. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali kupitia Waziri wa Maji, ije ifanye ziara katika Mkoa wetu wa Katavi ili iweze kuangalia, je, hizi pesa Serikali ilizozitenga na kupeleka fedha hizi katika Mkoa wetu wa Katavi, je, value for money ipo katika miradi hii ya maji? Maana kumekuwa kuna ubabaifu, wanafunga mabomba maeneo mengine maji hayatoki, lakini baadhi ya mabomba yamekuwa yako chini ya kiwango yanapasuka na hivyo kupoteza fedha nyingi sana za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe sana kaka yangu, Mheshimiwa Jumaa Aweso, aje katika Mkoa wetu wa Katavi kuhakikisha kwamba anafanya ziara ili aweze kwenda kushughulika na wale wote wanaokwenda kucheza na pesa za Serikali. Hususan tukiangalia kabisa maji ni uhai na wananchi wa Mkoa wa Katavi wengi wanahitaji maji ili tuweze kufikia ile azma ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; niiombe sana Serikali kwa kuwa imeleta miradi mbalimbali ya maji katika Mkoa wetu wa Katavi na maji hayo yameonekana hayatoshi, niwaombe sana Serikali kipo chanzo cha uhakika sana cha Ziwa Tanganyika. Na kutoka Mji wetu wa Mpanda mpaka lilipo Ziwa Tanganyika ni sawa na kilometa 120. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo niiombe sana Serikali kutoa maji katika chanzo cha uhakika ambacho ni Ziwa Tanganyika ili kwenda kumkomboa mama kwa kumtua ndoo kichwani. Mama zetu wamekuwa wakipata taabu sana katika Mkoa wetu wa Katavi kuhangaika kutafuta maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo sasa jamani ni wakati wa kumuaminisha mama wa Mkoa wa Katavi na wa Tanzania kwa ujumla kwamba Serikali yetu Sikivu inayoongozwa na mama yetu Samia Suluhu, kwamba yukotayari kuwatua ndoo kichwani akinamama wa Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Jumaa Aweso, akinamama wa Mkoa wa Katavi wanalalamika sana wenyewe ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa kubambikiziwa bills zinazotokana na maji. Niwaombe sana Wizara ya Maji ikiwezekana kwa nini tusitumie utaratibu kama wa luku; kama luku, mtu anakwenda ananunua units zake anatumia umeme na anakuwa habugudhiwi na mtu ni kwa nini tusifanye utaratibu huu katika suala la maji? Mtu anunue units zake za maji atumie maji, zinapokwisha zikate ili kuondokana na usumbufu wa watu kubambikiziwa bili kubwa za maji ambayo hawajayatumia. Maana kumekuwa kuna maeneo mengine unakuta maji hayajatoka hata miezi miwili lakini bado bili za maji zinakuja, sasa bili hizi zinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri akashughulike sana na watendaji kwani watendaji wamekuwa wakikwamisha sana Wizara hii ya Maji. Kaka yetu, Mheshimiwa Jumaa Aweso, amekuwa akijitahidi sana na Wizara hii ni ngumu kwa kweli, Wabunge wote tunafahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Jumaa Aweso akashughulike na watendaji katika Wizara ya Maji kuanzia ngazi ya mkoa, akaangalie kule changamoto ni nini kinachokwamisha. Serikali imekuwa ikitenga pesa, inapeleka pesa lakini bado maji yamekuwa yakikwama katika maeneo mengi, wananchi wake hawapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Eng. Maryprisca Mahundi na Mheshimiwa Waziri. Niwaombe sana muendelee kuchapa kazi, msife moyo, tunafahamu Wizara hii ina changamoto nyingi lakini kwa kuwa ninyi mama yetu Samia Suluhu amewaamini na amewaweka hapo, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu mzidi kutatua changamoto ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Jumaa Aweso; kwa kuwa Mji wetu wa Mpanda ambao uko katika Mkoa wa Katavi hivyo katika miji ile 28 itakayokwenda kunufaika, niwaombe sana Mji huu wa Mpanda tunahitaji maji, ni mji ambao una fursa nyingi sana za kibiashara, mji ambao unakusanya watu wengi sana wanaohitaji kufanya mambo ya kibiashara katika mji wetu. Niwaombe sana tupate maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Katavi tuko chini ya miguu yenu, tunawaomba sana mtuangalie katika hiyo miji 28 jamani na sisi mtupe kipaumbele. Mji wetu umesahaulika kwa muda mrefu, Mkoa wetu wa Katavi umekuwa nyuma kwa mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe katika suala la maji wananchi wa Mkoa wa Katavi tunawaomba sana mtuangalie katika ile miji 28 itakayonufaika na mradi kutoka India basi na sisi mtupe kipaumbele ili twende kuendelea na uzalishaji wa mazao, mambo ya kiutalii ambayo yako katika Mkoa wetu wa Katavi. Suluhisho ni kupata maji ili wananchi wale waendelee kuchapa kazi na kuongeza pato katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii, naunga mkono hoja, naomba tupitishe bajeti ya Wizara ya Maji. Ahsanteni. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu, Wizara ya Afya. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipekee sana napenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa jinsi ambavyo ilivyotutendea mambo makubwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kuhakikisha kwamba, imetekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kutupatia hospitali kila wilaya, iliahidi na ilitekeleza. Wananchi wa Mkoa wa Katavi wanasema ahsante sana Serikali ya Awamu ya Tano iliyopita, lakini kipekee tunamshukuru sana Mama yetu Samia Suluhu kwa jinsi ambavyo anaendelea kuchapa kazi na kuhakikisha kwamba, huduma za afya nchi nzima zinaboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Katavi kwanza tunatoa shukrani za dhati kipekee kwa kupata zahanati nyingi na vituo vya afya katika Mkoa wetu wa Katavi. Tumepatiwa zahanati za kutosha, lakini vituo vya afya vya kutosha katika Mkoa wetu wa Katavi katika wilaya zetu mbalimbali. Lakini changamoto kubwa tuliyonayo wananchi wa Mkoa wa Katavi katika wilaya zetu tumepatiwa vituo vya afya, lakini vituo vile vya afya tuna ukosefu mkubwa sana wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Katavi takribani mkoa mzima tuna upungufu wa watumishi katika kada ya afya takribani asilimia 72 ambapo watumishi tulionao ni sawa na asilimia 28. Kwa jinsi Mkoa wetu wa Katavi ulivyo na muingiliano wa watu wengi utaona watumishi hawa ni wachache sana kuhakikisha kwamba, wanaenda kutatua changamoto katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Katavi wanapata huduma zilizo bora katika afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wananchi pia wa Mkoa wa Katavi katika vituo vyetu vya afya kuna upungufu sana wa vifaa tiba. Tuna upungufu wa vifaa tiba takribani asilimia 60, ambao sisi tunao ni kama takribani asilimia 40. Tunaiomba sana Wizara ya Afya waweze kutupatia watumishi ili waweze kwenda kutatua changamoto katika vituo vyetu vya afya kwa kuhakikisha wananchi wetu wa Mkoa wa Katavi wanaenda kuhudumiwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wananchi wa Mkoa wa Katavi tunaomba sana Serikali yetu sikivu, Serikali yetu tukufu, huduma ya MSD tunaomba katika Mkoa wetu wa Katavi iweze kuboreshwa. Serikali imekuwa ikitenga pesa kwa ajili ya dawa katika Mkoa wa Katavi, lakini MSD wanatuambia baadhi ya dawa hakuna. Sasa tunaomba sana Wizara ya Afya wahakikishe kwamba, wananchi wa Mkoa wa Katavi tumakwenda kupata dawa ili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kupata huduma iliyo bora katika kuhakikisha kwamba, afya zao zinaenda kuwa safi ili waweze kwenda kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi pia wa Mkoa wa Katavi tunasema asante sana Serikali yetu kwa jinsi ambavyo imeona umuhimu ikaamua kutujengea hospitali ya Mkoa wa Katavi ambayo kwa jinsi ninavyoiona ile ramani, jinsi ilivyokaa niiombe sana Serikali, hospitali ile isitumike kama hospitali ya Mkoa hospitali ile kwa ramani jinsi inavyoonesha inafaa kuwa hospitali ya rufaa. Ukiangalia mwananchi wa Mkoa wa Katavi tunatumia gharama kubwa sana kwenda kufuata rufaa katika Mkoa wa Dar-es-Salaam katika Hospitali ya Muhimbili, lakini kwenda Ikonda pia ni mbali sana, lakini ukiangalia kwenda Bugando ni mbali sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Katavi wamekuwa wakitumia gharama nyingi sana kufuata rufaa katika mikoa hii ambayo ni mbali sana na ukizingatia miundombinu yetu katika Mkoa wa Katavi bado ni mibovu. Hivyo, niiombe sana Serikali kwa kuwa, walitenga hela katika Hospitali hiyo ya Mkoa wa Katavi ambayo ina hadhi kabisa ya kufanywa kuwa hospitali ya rufaa au hospitali ya kanda kwa watu wanaotokea katika mikoa hiyo ya Katavi.

Niwaombe sana Serikali, hospitali hiyo ilikuwa ikabidhiwe Januari tarehe 21. Sasa niwaombe tunaiuliza Serikali, ni kwa nini mkandarasi sasahivi hayuko site na hakuna kitu chochote kinachoendelea katika hospitali ile? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ile hospitali ni muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi, lakini kwa wananchi wa mikoa ya jirani, jirani zetu pale watatumia hospitali ile kama ya rufaa ili kuondokana na adha ya kufuata hospitali za rufaa ikiwepo Ikonda, ikiwepo Muhimbili, ambapo ni gharama kubwa nyingi sana. Niwaombe sana Serikali yetu Sikivu, tunaomba hospitali hii iweze kumalizika, ili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kupata huduma iliyoboreshwa kwa ukaribu ili waweze kuchapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizingatia Mkoa wetu wa Katavi wananchi wale ni wazalishaji wazuri sana wa kilimo wanahitaji huduma iliyo bora, lakini ukizingatia Mkoa wetu wa Katavi Rais wetu aliyepita, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliona umuhimu wa mkoa ule akaamua atajenga bandari, alisema kwamba, atajenga bandari na bandari imeshaanza kujengwa. Kuna bandari inayojengwa Wilaya ya Tanganyika ambayo inaenda kutuunganisha na wananchi wa Kalemii, Kongo, ambako kuna dhahabu nyingi sana. Hivyo yote hiyo naeleza haya ili muweze kuona umuhimu wa hospitali ile kuweza kumalizika, ili iweze kutibu wananchi wengi sana wanaokuja katika Mkoa wetu wa Katavi kuhakikisha fursa nyingi sana za uchumi zinaenda kunyanyuliwa katika Mkoa wetu wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, niiombe sana Serikali hospitali ile ni muhimu sana wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaihitaji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo napenda kuchangia katika Wizara ya Afya, niwaombe sana, kumekuwa na sintofahamu akinamama wanapoenda kujifungua. Mama zetu wanapoenda kujifungua wanakutana na ghadhabu sana wanaambiwa kwamba, wanatakiwa wachangie damu, ila hata pale wanapopata watu wa kwenda kuwachangia damu wanaambiwa kwamba, ile mifuko ya kuchangia damu inauzwa, takribani wanatoa mpaka 16,000/=. Niwaombe sana Serikali waangalie jambo hilo aikinamama ni waaminifu sana na akinamama wana upendo mkubwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Serikali muweze kuwaangalia akinamama hawa waweze kwenda kujifungua. Ikiwezekana kama Serikali ilivyosema akinamama watajifungua bure, basi kweli waende kutekeleza hiyo kwa vitendo. Akinamama wa Mkoa wa Katavi na akimama wa Tanzania nzima tuhakikishe kwamba, wanajifungua salama na wanajifungua kwa bei nafuu, ikiwezekana ni bure kabisa kama Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu jinsi alivyotuahidi. Hivyo, niiombe sana Serikali kupitia Wizara ya Afya mjitahidi jamani, akinamama wa Mkoa wa Katavi wanahitaji huduma iliyoboreshwa ili kuhakikisha akinamama wanajifungua na kuzaliana, tuweze kwenda kuzaliana tuongeze nguvu kazi katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, niiombe sana Wizara ya Afya, kutokana na huu upungufu ambao umeonekana ni mkubwa sana, hapa nitazungumzia Hospitali yetu ya Wilaya ya Mpanda ambayo kwa sasa inatumika kama Hospitali ya Mkoa. Hospitali ile jamani ina ufinyu sana wa maeneo kiasi ambacho kwamba, hata upasuaji imekuwa ni kitendawili kufanyika maeneo yale. Niwaombe sana Wizara ya Afya wakati tunasubiri hospitali hii ya rufaa iweze kukamilika niwaombe sana waiboreshe hiyo Hospitali yetu ya Wilaya ya Mpanda ambayo inabeba wagonjwa wengi sana, waiboreshe kwa kuangalia kukarabati miundombinu, lakini kuleta vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoeleza hivi hata huduma tu ya CT-Scan katika Mkoa wetu wa Katavi haipo. Niwaombe sana Wizara ya Afya mtuangalie wananchi wa Mkoa wa Katavi. Naongea hivi kwa uchungu sana mtuangalie kwa sababu, mama zangu na baba zangu wanapata tabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo napenda kuchangia katika Wizara hii ya Afya niwaombe sana. Kwa kuwa, Serikali yetu imeahidi wazee watapata huduma bure, niwaombe sana mtuboreshee wazee waweze kupata huduma iliyo bora na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya kilimo. Kwanza naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wanaendelea kushughulikia matatizo yanayojitokeza katika Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajikita moja kwa moja kwenye suala la masoko. Mkoa wangu wa Katavi, wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa asilimia kubwa sana wamekuwa wakitegemea kilimo. Lakini wanazalisha mazao mengi, masoko yamekuwa ni tatizo na ukizingatia kwamba pembejeo zimekuwa na bei sana. Katika Mkoa wetu wa Katavi huwezi kuamini, gunia la kilo 100 linauzwa hadi shilingi… (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tusikilizane, tupunguze sauti. Tumsikilize Mbunge mwenzetu. Huyu anaitwa Mheshimiwa Martha Mariki na anafunga ndoa hivi karibuni sana, kwa hiyo… (Makofi/Vigelegele)

Zile kadi za michango Mheshimiwa hakikisha zinafika kote. Endelea kuchangia.

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nasema wananchi wa Mkoa wa Katavi hususan akina mama maana jambo lolote katika Taifa hili linapokuwa suala ni gumu sana sana lazima limguse mwanamke yeyote wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa maana kuwa, katika Mkoa wangu wa Katavi akina mama na akina baba wa Mkoa wa Katavi wamekuwa wakizalisha mahindi kwa wingi lakini masoko yamekuwa ni mtihani. Gunia la kilo 100 limekuwa likiuzwa mpaka shilingi 18,000. Hapo tunamuumiza sana mkulima huyo ukizingatia pembejeo zimekuwa zikiuzwa bei sana. Hivyo, niiombe sana Serikali kupitia Wizara yetu ya Kilimo waweze kumtamfutia mwananchi huyu masoko ya uhakika ili tuhakikishe mkulima huyu tunamkomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili nitakalozungumzia ni suala la irrigation schemes. Katika Mkoa wetu wa Katavi tuna maeneo ambayo ni potential yakiwepo maeneo kama ya Mwamapuli, Mwamapuli tuna takriban hekta 13,600 ambazo zinaweza kukubali kilimo cha umwagiliaji. Hivyo, niiombe sana Serikali katika Mkoa wetu wa Katavi hususan eneo la Mwamapuli ambalo ni potential sana kwa kilimo cha mpunga, Mkoa wa Katavi umekuwa maarufu sana kwa kulima mpunga ambao ni first class ambao hata nchi za jirani zimekuwa zikija katika Mkoa wetu wa Katavi kuja kukusanya mpunga huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, niiombe sana Wizara ya Kilimo katika eneo la Mwamapuli tuweze kuwekeza kwenye irrigation schemes ili mwananchi wa mkoa huo aweze kulima, yani tufanye bandika bandua ili tuweze kumkomboa mwananchi na Taifa letu liweze kupata uzalishaji ulio bora. Wananchi wa Mkoa wa Katavi tunalima mpunga ambao ni first class na nikuambie tu Mkoa wetu wa Katavi mchele unaotoka pale ni mchele ambao ni first class, mchele wa kienyeji. Mchele ambao ukiupika lazima jirani asikie harufu kwamba ni mchele wa kienyeji uliopikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, niiombe sana Serikali tuwekeze eneo hili ili mwananchi yule aweze kulima na Taifa letu liweze kuingiza mapato kupitia kilimo. Niiombe sana Serikali yangu Sikivu na tukufu. Tukiwekeza katika kilimo tutakuwa tumemkomboa mwananchi kwani kilimo ni uti wa mgongo na wananchi wengi wa maeneo yale wanategemea sana kilimo hivyo tuwekeze hasa katika uchimbaji wa mabwawa makubwa ambayo tukiwekeza katika mabwawa makubwa yatasaidia katika kilimo hicho kikubwa na pia akina mama wa Mkoa wa Katavi watafanya kilimo cha mbogamboga na hivyo tutakuwa tumemgusa mwanamke wa Mkoa wa Katavi kwa kulima pia mbogamboga kwa kutumia umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, niiombe sana Serikali, kwa kuwa muda ni mchache pia tuna maeneo mengine kama eneo la Kalema. Kalema ni eneo ambalo ni potential, hivyo niiombe Serikali tukiwekeza katika eneo hilo tutaweza kufanya kilimo chenye tija. Ukizingatia kwamba katika eneo la Kalema kumekuwa kuna miradi ya kimkakati ikiwepo ujenzi wa bandari ambao unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tukitumia kilimo tukazalisha kwa wingi na tukatumia bandari yetu ambayo tunajengewa na Serikali yetu Sikivu katika maeneo haya ya Kalema, tutaweza kwenda kufanya biashara na majirani zetu wa Kongo Kalemi kwa kupeleka mazao yetu kwa kutumia bandari hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Serikali imetuhakikishia kwamba tunaenda kujengewa meli za kusafirisha mizigo. Hivyo, niiombe sana Serikali tukiwekeza katika kilimo tutakwenda kumkomboa mwananchi na Serikali yetu itaingiza mapato na Taifa letu litaenda kusonga mbele. Pia, tutakuwa tumemsaidia kijana wa Kitanzania kwa kuweza kupata ajira nyingi sana zitakazotokana na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo kwa unyenyekevu mkubwa ninaiomba sana Serikali kupitia Waziri wa Kilimo aweze kutusaidia wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kufanya uwekezaji katika maeneo ambayo ni potential ili Serikali yetu iweze kumsaidia mwananchi kujikomboa. Wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaipongeza sana Serikali kwa juhudi zao wanazoendelea kupambana ili kuhakikisha kwamba tunatatua matatizo ya wananchi. Hivyo, wananchi wa Mkoa wa Katavi tunaamini Serikali yetu Sikivu itatusaidia kwa kuweza kuwekeza katika maeneo hayo ambayo ni potential.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema. Kipekee sana napenda kumpongeza Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Medard Kalemani na Naibu wake kwa jinsi ambavyo wanaendelea kufanya kazi kwa umakini mkubwa na nampongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee sana naipongeza sana Serikali yangu Tukufu kwa kutekeleza mradi wa Mwalimu Nyerere. Mradi huu utakwenda kuleta tija na mapinduzi makubwa sana katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza Serikali kwa ajili ya mradi wa REA. Katika Mkoa wetu wa Katavi wananchi wanaipongeza sana Serikali kwa jinsi ambavyo imeleta umeme katika vijiji mbalimbali. Hata hivyo kuna maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme huu. Hivyo, niiombe sana Serikali kupitia Waziri wetu Mheshimiwa Medard Kalemani vijiji hivi viweze kupata umeme huu ili kuleta tija kwenye uzalishaji katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, vijiji hivi ni pamoja na Vijiji vya Mwamkulu. Kata ya Mwamkulu inaongoza sana kwa uzalishaji wa mpunga lakini kwa masikitiko makubwa bado haijaweza kupata umeme. Hivyo kumekuwa na changamoto katika mashine zile za kukoboa mpunga wananchi wamekuwa wakikwamisha na umeme.

Mheshimiwa Spika, pia katika Kijiji cha Kakese na chenyewe kina uzalishaji mkubwa sana wa mpunga lakini hakina umeme. Baadhi ya vijiji ambavyo pia havina umeme ni pamoja na Vijiji vya St. John, St. Maria, Mkwajuni na Ikokwa. Tuiombe sana Serikali yetu sikivu…

SPIKA: Vyote viko katika Wilaya gani?

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, viko katika Wilaya ya Mpanda, Jimbo la Mpanda Mjini lakini ni Pembezoni, Kata ya Mwamkulu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika Wilaya hiyo Mpanda maeneo ya Ulila kuna Kijiji cha Usense na chenyewe hakina umeme, maeneo ya Ugala, Kambuzi na Litapunga. Tunaiomba sana Serikali vijiji hivi viweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Katavi kwa muda mrefu sana tumekuwa tukitumia umeme wa generator. Upo mkakati wa kuleta umeme wa Gridi ya Taifa lakini tunaomba sana Wizara iweze ku-push na kuhakikisha kwamba mradi huu unaenda kukamilika kwa muda uliopangwa ambapo umeme huu ambao unatokea Sikonge kupitia Inyonga umepangwa kukamilika mwezi Septemba.

Mheshimiwa Spika, pia ombi letu sisi wananchi wa Katavi, wananchi wa Wilaya ya Mpimbwe wanasema kwamba kwa kuwa mradi huo utakwenda kukamilika kule Inyonga na Inyonga mpaka Mpimbwe ni takribani kilomita 135, wanaomba kuungiwa line ili umeme uweze kutoka Inyonga kwenda Mpimbwe. Kwa kuwa hiyo ni wilaya moja na ni karibu sana tungeomba sana na wananchi wa Mpimbwe waweze kuungiwa line hiyo ili umeme uweze kutoka Inyonga na kufika Mpimbwe. Kwa kuwa wananchi wa Mpimbwe wamekuwa wakipata adha kubwa wanatumia umeme wa gridi ambao unatokea Zambia kupitia Rukwa na umeme huo umekuwa ukikatika mara kwa mara kutokana na matumizi kuwa makubwa. Hivyo, tunaiomba sana Serikali yetu sikivu kuhakikisha kwamba mkakati huu unaenda kukamilika na wananchi wa Mpimbwe, Inyonga na Katavi yote wanapata umeme ili waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kukatikakatika kwa umeme limekuwa ni changamoto kubwa ambayo pia imekuwa ikiwakwamisha sana baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Katavi hususani vijana wenzangu ambao wamekuwa wakijikita katika shughuli za uchomeleaji. Hivyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maliasili. Kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wameendelea kufanya kazi vizuri katika Wizara hii. Hata hivyo, kipekee sana nampongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uchache wa muda, moja kwa moja nitaanza kwa kuchangia kwa Mkoa wangu wa Katavi kuhusiana na suala la TFS kutokana na tozo mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitoza kwenye vitu vinavyotengenezwa kwa mbao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Katavi, TFS wamekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa wananchi. Huwezi kuamini, mfano mwananchi anaponunua kitanda chake pale Mpanda Mjini na anataka akipeleke katika Wilaya ya Mlele, Halmashauri ya Mpimbwe, kumekuwa na tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kama double payment.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, juzi tu hapa kuna wananchi ambao wamenunua vitanda vyao na meza Mpanda Mjini na wanavipeleka katika Halmashauri ya Mpimbwe. Vitanda hivi, huyu mtumiaji anakuwa ameshalipia na amepata risiti lakini wanavyopita kwenye mageti wanatozwa tena pesa na watu wa TFS wakiambiwa tena walipie gharama za vitu hivyo. Hii imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aje ashughulikie suala hili kuangalia tozo hizi, ikiwezekana ziondolewa kwani wananchi hawa wamekuwa wakipata adha kubwa na watu hawa wa TFS. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa kuna migogoro mbalimbali baina ya wananchi na TFS kwa mfano, katika Wilaya ya Mlele Kata ya Kamsisi; kumekuwa na mgogoro mkubwa baina ya watu hawa na mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakichomewa nyumba zao, wananchi wamekuwa wakichomewa mazao yao, lakini pia TFS hawa wamediriki kabisa kuwachomea hata maduka wananchi, wananchi hawa wamefanyiwa ukatili, mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu na Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukimwambia mara nyingi na hata Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa anafahamu suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali yetu sikivu iweze kushughulikia mgogoro huu ili wananchi hawa waweze kuishi kwa amani, kama tunavyojua ardhi haiongezeki, lakini wananchi wanaongezeka, tuombe sana tuangalie mgogoro huu, ikiwezekana kabisa tuumalize mgogoro huu kwani wananchi hawa wamekuwa wakipata adha, mama zangu na baba zangu wa Kijiji cha Kamsisi, Kata ya Utende, maeneo ya Ilunde na Ilela wamekuwa wakichapwa sana, wakiadhibiwa, wakiambiwa kwamba wanaingilia maeneo ambayo ni ya mapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri waje washughulikie suala hili, ikiwezekana waje katika Mkoa wetu wa Katavi,waweze kufanya ziara, waje wawasikilize wananchi, wasiwe wanasikiliza tu watendaji wakati mwingine imekuwa ikipotoshwa. Hivyo, waje wafanye ziara kule wajihakikishie wajue je, mwenye kosa ni mwananchi au wenye kosa ni watu hawa wa TFS. Niwaombe sana Wizara wafanye ziara kule ili waweze kujua nini chanzo cha tatizo hili na ikiwezekana tulimalize ili wananchi wetu waweze kuishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kumekuwa kuna tatizo la kubambikiziwa kesi. Watu wa TFS wamekuwa na tabia ya kuwambambikizia kesi wananchi wale wanaoizunguka Katavi National Park. Sasa tunachotaka wananchi wale wa Katavi waweze kufurahia kuwepo kwa Katavi National Park hifadhi ambayo Mwenyezi Mungu ameibariki na siyo waone ni kero kuwa karibu na hifadhi hiyo. Wamekuwa wakibambikiziwa kesi mbalimbali, wakiambiwa kwamba wengine wamekutwa na nyara za Serikali, wengine wamekutwa sijui na nyama za pori kama hizi za Nyati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aje katika maeneo hayo atafanye ziara aangalie kesi hizo hasa zile ambazo zimekuwa hazina vithibitisho, ikiwezekana ziondolewe. Wananchi wa vijiji hivi wamekuwa wakihangaika, wananchi wa Vijiji vya Majimoto, Mamba, Chamalendi na Mwamapuli wamekuwa wakiteseka sana. Hivyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afanye ziara Mkoa wa Katavi, tunataka wananchi wa Mkoa wa Katavi wafurahie kuwepo kwa Katavi National Park na siyo hifadhi hiyo iwabugudhi wananchi. Wananchi tunawapenda na hifadhi pia tunaipenda kwa sababu inatuingizia mapato. Tunachotaka tu ni kwamba migogoro hiyo ikiwezekana iishe na hasa hiyo migogoro na kesi ambazo hazina uthibitisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI. Moja kwa moja niende kwanza kwa kuimpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameendelea kufanya kazi kubwa katika Taifa hili lakini kwa jinsi ambavyo ametugusa sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kutupatia hospitali za wilaya katika kila halmashauri. Sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi tumebahatika kupata hospitali zenye level ya wilaya katika kila halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hopsitali hizo za wilaya ambazo tunazo katika halmashauri zetu hospitali nyingi zinashindwa kufanya kazi kwa masaa 24 kutokana na upungufu mkubwa sana wa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hospitali kama hospitali ya Halmashauri ya Msimbo lakini Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika lakini Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe, Hospitali ya Wilaya ya Mlele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hizi kwa kweli zina operate kwa level ya zahanati. Kama Serikali ni lazima tuhakikishe kwamba fedha hzi nyingi zilizowekezwa na Serikali katika hospitali hizi zinaenda kutumika vizuri kwa kupeleka watumishi ili wananchi waliokusudiwa waweze kupatiwa huduma iliyobora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Katavi kwa upande wa upungufu wa watumishi kwa upande wa afya pamoja na elimu. Tunaupungufu wa watumishi kwa asilimia 56.18. Kwa upande wa Wilaya ya Tanganyika tunaupungufu wa asilimia 66, katika Wilaya ya Mlele tuna upungufu wa asilimia 61 upande wa Nsimbo tuna asilimia 63.2, upande wa Mpanda Mjini tuna upungufu wa asilimia 36.1 na upande Mpimbwe tunaupungufu wa asilimia 69.1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu huo ni mkubwa na wananchi wanakutana na adha mbalimbali kutokana na kwamba wanashindwa kupatiwa huduma Serikali iliyokusudia kwa kujenga hospitali hizo za wilaya katika Mkoa wetu wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naipongeza Serikali kwa kuleta pesa nyingi katika kuwekeza katika vituo vya afya pamoja na zahanati. Katika Mkoa wetu wa Katavi tuna zahanati nyingi ambazo Serikali imeziwekeza, hadi hivi ninavyoongea kuna zahanati zaidi ya 16 ambazo zimeshindwa kufuguliwa kutokana na upungufu mkubwa sana wa watumishi na kufikia mwezi wa Sita tutakuwa na zahanati zaidi ya 26 ambazo zinashindwa kufunguliwa kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vituo vya afya, kuna vituo vya afya ambavyo vimejengwa ikiwepo Ilunde, Majimoto, Mwamapuli, Gulamata na kwa upande wa Kibaoni. Zahanati hizi na vituo vya afya nyingi zinashindwa kufanya huduma ya upasuaji na matokeo yake wagonjwa wengi wakienda pale wanapatiwa tu paracetamol. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali kupitia Wizara hii ya TAMISEMI, kwa kuwa tumepata ajira 21,000. Tunaomba wananchi wa Mkoa wa Katavi tuweze kukumbukwa tuangalie wanaopata adha hapa sana sana ni mama zangu wa Mkoa wa Katavi. Unakuta kituo kama hiki Kituo cha Afya cha Kibaoni, cha Kasansa na Majimoto, vinashindwa kufanya huduma ya upasuaji. Sote tunaelewa wakina mama wengi wanapoenda kujifungua kuna wengine wanatakiwa wafanyiwe upasuaji lakini zahanati hizi na vituo vya afya havifanyi huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Waziri wa TAMISEMI aliangalie kwa jicho la pili suala hili wananchi wa Mkoa wa Katavi waweze kupelekewa watumishi ili waweze kuhudumiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambapo nilikuwa napenda kulichangia, katika ajira na usawa, natokea katika mikoa ambayo ipo pembezoni. Mfano Mkoa wetu wa Katavi, kuna Mkoa wa Kigoma lakini kuna Mkoa kama wa Lindi. Watumishi wengi wanapopangiwa maeneo haya wanashindwa kuja kufanya kazi kutokana pengine na miundombinu ambayo hawaijawa supported. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara iweze kuboresha mazingira ya walimu pamoja na watumishi hususan wa afya ili wanapokuja kupangiwa katika maeneo haya waweze kufanya kazi katika mazingira yaliyobora ili wasiweze kutukimbia. Kwa kweli unakuta wafanyakazi wanapopangiwa katika mikoa hii kwa mfano Mkoa wangu wa Katavi unakuta mtu amepangiwa eneo la Gulamata lipo upande ule wa Mishamo. Ni eneo ambalo ni mbali usipomuwekea miundombinu mizuri, mtumishi huyu lazima ataomba kuhama aweze kuhamia maeneo mengine. Ila tukiwawekea mazingira rafiki na mazuri lazima watumishi hawa watakaa waweze kufanya kazi na kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilikuwa napenda kuchangia ni kuhusiana na kuboresha kitengo cha wakaguzi wa ndani. Katika kuboresha kitengo hiki cha wakaguzi wa ndani linaweza likamsaidia sana CAG. Kitengo hiki kimekuwa kwanza hakitengewi bajeti ya kutosha lakini pia wanakosa uhuru kutokana na kwamba wanafanya kazi kubwa ambayo wanakuwa wanamuangalia Mkurugenzi aweze kuwapatia mafuta lakini wanamuangalia Mkurugenzi ndio aweze kuwapatia magari ya kwenda kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Serikali waboreshe kitengo cha wakaguzi hawa wa ndani ili waweze kudadavua na kutoa madudu yote ya pesa zinazoliwa katika halmashauri zetu. Tukiwawezesha hawa wakaguzi wa ndani kwa kweli kazi kubwa itafanyika katika halmashauri zetu na fedha zote zinazopelekwa na Serikali ziitaweza kusimamiwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi naunga mkono hoja.(Makofi)