Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saada Mansour Hussein (2 total)

MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pia nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, je, ni njia zipi kama Serikali mnazitumia kuwajulisha wale ambao hadi leo hawajapatiwa vitambulisho vyao kwenye vituo vya NIDA?

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatambua kuwa kwenye ofisi za NIDA kuna uhaba wa watumishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Saada Mansour Hussein, lakini pia nataka kutumia fursa hii kumpongeza sana kwa kazi nzuri na kubwa ambayo anaifanya katika Mkoa wa Kaskazini ya kuhakikisha kwamba akina mama au wananchi, lakini zaidi akina mama na watoto wanaishi katika mazingira mazuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni njia zipi ambazo tunazichukua kama Serikali kuhakikisha kwamba wale ambao hawajaenda kuchukua vitambulisho vyao taarifa zinawafikia.

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nichukue fursa hii, niwashukuru wananchi na viongozi kwa kuwa wametambua kwamba bado kuna baadhi ya wananchi hawajaenda kuchukua vitambulisho vyao mpaka muda huu, badala yake wanakaa wanalaumu Serikali. Kwa hiyo kikubwa ambacho nataka niseme ni kwamba, zipo njia nyingi ambazo huwa tunazitumia kuwafikishia ujumbe au taarifa kwamba vitambulisho vipo na waje.

Mheshimiwa Spika, ya kwanza; huwa tunawatumia ujumbe mfupi, kwa wale ambao namba zao zipo hewani zinapatikana. Pia huwa tunawapigia simu kabisa kuwajulisha. Vile vile kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya na kupitia Ofisi za Masheha na Watendaji huwa tunatoa taarifa hizo ili wananchi ambao wameshatengenezewa vitambulisho vyao, lakini hawajaenda kuvichukua, waende wakavichukue.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nikiri kwamba, bado tuna changamoto ya rasilimawatu katika Ofisi zetu za NIDA, lakini nimwambie Mheshimiwa aendelee kustahimili, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kupitia NIDA tupo katika mchakato wa kutengeneza mazingira ya kuajiri vijana, lengo na madhumuni, shughuli za NIDA ziweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni hatua gani zilizochukuliwa na Serikali hadi sasa kwa wote waliohusika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YANCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saada Mansour Hussein kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, watuhumiwa wa mauaji haya yaliyotokea Zanzibar, wote walikamatwa na kesi zao zinaendelea mahakamani. Nakushukuru sana.