Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zaytun Seif Swai (6 total)

MHE. ZAYTUN S. SWAI Aliuliza:-

Kutokana na changamoto za vyanzo vya mapato hususan katika Halmashauri zilizo nje ya miji kumekuwa na uwiano usio sawa wa utoaji wa mikopo.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta njia ya kuweka uwiano sawa wa mikopo hiyo bila kujali mapato ya Halmashauri husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hutolewa kwa kuzingatia kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019. Halmashauri inatakiwa kutenga na kutoa asilimia 10 ya fedha za makusanyo ya ndani katika kipindi husika kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu baada ya kuondoa vyanzo lindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa sheria hii ni asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa kwenye Halmashauri husika ambayo yanatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine kutokana na fursa zilizopo. Hivyo, kiwango cha mikopo inayotolewa kinategemea uwezo wa makusanyo wa Halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka hususan baada ya kuwepo kwa sheria ambapo mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 26.1 mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 42.06 mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo Serikali inatambua changamoto zinazotokana na utaratibu huu na itaendelea kuuboresha ili kuongeza tija na kufikia malengo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo hii.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupima na kuchimba visima virefu Mkoani Arusha hasa Wilaya ya Longido katika Vijiji vya Noondoto, Matale, Wosiwosi na Ngereani ambapo kuna uhaba wa vyanzo vya maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kutokana na Wilaya ya Longido kuwa na uhaba wa vyanzo vya maji hasa chemichemi, Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali ikiwemo kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi na kuchimba visima virefu, ambapo katika Kijiji cha Matale B, uchimbaji wa kisima unaendelea kupitia Bajeti ya mwaka 2020/2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Noondoto, kinapata huduma ya maji kupitia mradi wa maji wa Kijiji cha Elang’atadabash unaohudumia vijiji vitano vya Elang’atadabash, Sokoni, Olchonyorokie, Noondoto, Losirwa na Naadare. Katika Kijiji cha Wosiwosi kisima kilichochimbwa, maji yake yalibainika kutofaa kwa matumizi ya binadamu kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha madini chumvi ukilinganisha na kiwango kinachokubalika.

Mheshimiwa Spika, hivyo, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itatumia vyanzo vya Mto Engaresero kutekeleza mradi wa kufikisha maji Kijiji cha Matale na Wosiwosi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kijiji cha Wosiwosi, tumeweka bajeti ya kujenga bwawa litakalosaidia mifugo na wananchi.

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ngereani kinapata huduma ya maji kupitia Mradi wa Maji Tingatinga Ngereani. Serikali itaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Longido wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kutumia vyanzo mbalimbali vitakavyoonekana vinafaa ikiwemo mito, visima na mabwawa.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-

Je, Serikali ina mikakati gani dhidi ya vitendo vya Ukatili vinavyofanywa kwa wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa tatizo la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutokomeza ukatili huo. Moja ya hatua hizo ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022. Mpango huu wa miaka mitano unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, jitihada nyingine ni pamoja na kuanzishwa kwa Kamati 16,343 za Ulinzi na usalama wa wanawake na watoto kwenye ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zina jukumu la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Pia kuanzishwa kwa madawati 420 ya Jinsia na watoto katika vituo mbalimbali vya Polisi nchini ambayo huwezesha wahanga wa ukatili kuripoti aina mbalimbali ya ukatili wa kijinsia.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imewezesha kutungwa kwa Sheria za Msaada wa Kisheria Na.1 ya mwaka 2017. Sheria hii inatoa fursa kwa wanawake waliofanyiwa unyanyasaji au kudhulumiwa kupata haki zao kupitia vyombo vya usimamizi wa sheria.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa Mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili, sheria zilizopo pamoja na kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka uwiano sawa wa mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani bila kujali mapato ya halmashauri husika ili kusaidia wanufaika wa mikopo wanaoishi nje ya miji wapate fursa sawa na wanufaika wa mijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura ya 290 kifungu cha 37(a) na Kanuni zake za mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa Sheria ya mikopo ya asilimia 10 ya wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ni asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri baada ya kuondoa mapato lindwa. Hivyo kiwango cha mikopo kinatokana na uwezo wa makusanyo ya halmashauri husika. Halmashauri zimeelekezwa kutoa fursa sawa za mikopo kwa vikundi vyote vilivyokidhi vigezo vilivyopo ndani ya halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo hii ni sehemu tu ya mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi iliyopo nchini, na Serikali itaendelea kuiboresha kadri itakavyohitajika.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -

Je, ni lini akina Mama zaidi ya 300 waliokuwa Wafanyakazi wa Kiwanda cha Kiliflora Wilayani Meru watalipwa stahiki zao baada ya Kiwanda hicho kufungwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Zaytun Seif Swai, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mgogoro uliopo baina ya wafanyakazi na mwekezaji wa Kampuni ya Kiliflora Ltd. Hivyo, Serikali ilifuatilia mgogoro huo na kubaini kuwa Tanzania Investment Bank (TIB) ilirejesha fedha iliyokopesha kwa kuuza mali za Kiliflora Ltd zilizowekwa dhamana ili kulipa deni la mkopo uliochukuliwa na Kampuni. Hivyo, kisheria Wafanyakazi wanapaswa kulipwa na Kampuni ya Kiliflora kwa kuwa kilichofanyika ni ufilisi kabidhi na siyo kufunga kampuni. Mfilisi Kabidhi (Receiver and Manager) ni tofauti na Mfunga Kampuni (Liquidator).

Mheshimiwa Spika, aidha, wafanyakazi wa Kiliflora Ltd, Wilson Samwel na Wenzake 502 walifungua Kesi ya Labor Na. ARS/ARM/305/2020, 152/2020 dhidi ya Kampuni ya Kiliflora Ltd na Frank Mwalongo ambaye ni Mfilisi Kabidhi ambayo ilianza kusikilizwa tarehe 30/10/2020. Shauri hili lilikwishatolewa maamuzi na Mahakama kwamba, masuala ya madai ya wafanyakazi yanapaswa kufanyiwa kazi na Kampuni ya Kiliflora Ltd maana haijafilisiwa kama ilivyoonekana kwenye taarifa za BRELA kwamba, Kampuni bado ipo hai.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea kuhimiza mmiliki wa shamba la Kiliflora kuwalipa akina mama hao. Nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Viwanda vya Kusindika Maziwa katika Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Arusha ni moja ya mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa maziwa ambapo unazalisha takriban lita 30,550,500 kwa mwaka. Mkoa wa Arusha una jumla ya viwanda 18 viwanda ambavyo ni vikubwa na vidogo vya kusindika maziwa vilivyosajiliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo uliosimikwa wa kusindika maziwa kwa viwanda tajwa ni kiasi cha takriban lita 43,789,200 kwa mwaka. Lakini hata hivyo, usindikaji halisi ni lita 6,315,400 kwa mwaka. Maziwa mengi hayaingii kwenye soko rasmi na kushindwa kupelekwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa, kutokana na ukusanyaji mdogo wa maziwa yanayozalishwa na wafugaji katika maeneo hayo. Jambo linaloathiriwa na ukosefu wa mifumo mizuri ya ukusanyaji wa maziwa (collection centres).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kushirikiana na sekta binafsi kuendelea kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya kukusanyia maziwa ili viwanda vyote vipate maziwa ya kutosha katika mkoa wa Arusha na mikoa mingine nchini, yenye uzalishaji mkubwa wa maziwa. Hii itasaidia kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.