Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zaytun Seif Swai (5 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na vilevile naomba niwashukuru wananchi wangu wa Mkoa wa Arusha hususan kinamama wa Mkoa wa Arusha kwa kuniamini kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili. Nawaahidi wananchi wangu hususan kinamama wa Arusha sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa, naomba nishukuru familia yangu wakiongozwa na mama yangu mpendwa mama Sifa Swai, mume wangu na mtoto mpenzi Alina. Wote hawa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakinishauri vyema jinsi gani ya kuwaongoza wananchi wetu na vilevile wananiongezea busara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hotuba ya Rais, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala la elimu. Serikali imefanya mambo makubwa sana kwenye awamu zilizopita kwenye suala la elimu na yote haya imeyafanya kwa sababu inatambua umuhimu wa elimu na mchango wake mkubwa katika uchumi wa Taifa letu. Kutokana na umuhimu huu, Rais ameeleza mambo mbalimbali yanayohusiana na elimu katika hotuba yake na majawapo ikiwa ni kuanzisha shule za sayansi za watoto wa kike katika kila mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi ni mnufaika wa elimu iliyotolewa bure na Serikali katika masomo haya ya sayansi na hisabati. Kwa hiyo, natambua vizuri changamoto wanazozipata watoto wa kike katika masomo haya na naipongeza Serikali kwa kuamua kuanzisha shule hizi ili kutatua changamoto zile. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, naomba niishauri Serikali, suala la shule za sayansi ni muhimu sana na linatakiwa lichukuliwe kwa umuhimu wake. Shule hizi zinahitaji umakini mkubwa kwenye kuziendesha. Kwa kuanza zinahitaji kuwa na ubora wa hali ya juu, maabara zenye viwango vya juu na walimu wenye uwezo mkubwa wa kuwafundisha wanafunzi hawa. Vilevile shule hizi zinahitaji nyezo mbalimbali kama vitabu na kadhalika. Kwa hiyo, naiomba Serikali isikurupuke kwenye suala hili, iliangalie kwa umakini na tuhakikishe shule hizi zinajengwa kwa umakini wa hali ya juu tukizingatia hayo mambo niliyotaja ili basi lengo la Serikali liweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi sote ni mashuhuda, tumeshuhudia jinsi halmashauri zetu zinavyopata shida sasa hivi kujenga madarasa na kutafuta madawati katika shule mbalimbali na wananchi wetu pia wanalalamika kwa sababu michango ni mikubwa kusaidia maendeleo haya. Kwa hiyo, naiomba Serikali suala hili la ujenzi wa shule za sayansi kwa watoto wa kike isilichukulie juu bali ilichukulie kwa umakini na tulianze suala hili mapema tusisubiri mpaka mwisho wa miaka mitano ili tuweze kuzijenga shule hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile niongelee suala la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kutokana na mapato ya halmashauri. Tumeona jitihada kubwa sana za Serikali inazofanya kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kupitia mikopo isiyokuwa na riba na mikopo mingine yenye riba nafuu na vilevile kupitia mifuko na program mbalimbali zilizoanzishwa na Serikali. Mikopo hii ya asilimia 10 inatolewa kulingana na mapato ya halmashauri husika na sisi sote tunajua kwamba halmashauri zote hazilingani kimapato. Kwa hiyo, formula hii haizingatii halmashauri zenye changamoto ya vyanzo vya mapato. Mikopo hii isiwe ni adhabu kwa wanufaika walioko vijijini na sehemu zenye changamoto za mapato. Naiomba Serikali iweze kuangalia formula hii kwa undani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatolea mfano mdogo tu, hauwezi kulinganisha mapato ya Ilala, Kinondoni na halmashauri za Ngorongoro, Longido au Monduli na sehemu zingine za vijijini. Kwa hiyo, tunaomba Serikali yetu iangalie fomula hii na iweze kugawa mikopo hii kwa usawa. Suala hili pia litapunguza gap lilipo la umaskini wa vijijini na mijini ambapo nadhani ndiyo lengo kubwa la Serikali yetu, tupunguze gap la umaskini lililopo kwa sasa vijijini na mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nichangie kwenye sekta ya maji. Nashukuru Mheshimiwa Rais bado anatambua kuna changamoto nyingi za maji, hususan vijijini. Serikali yetu imefanya mambo mengi sana hasa kutekeleza miradi mikubwa ya maji ikiwemo mradi wa shilingi bilioni 520 ulioko Mkoani Arusha. Naomba niishauri Serikali isiwekeze tu kwenye miradi mikubwa kama hii vilevile iangalie vyanzo vingine vya maji ikiwemo uchimbaji wa visima virefu. Nitatolea mfano tu, mradi huu wa shilingi bilioni 520 unapita Wilaya ya Arumeru lakini kuna kata katika Wilaya ya Arumeru kama Kata ya Nduruma haina maji. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie pia vyanzo vingine vya maji ukiachia mbali miradi hii mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara hii na Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuongelea maendeleo ya Wizara hii bila kutaja Kanda ya Kaskazini hususani Mkoa wa Arusha. Wameongea vizuri sana Wabunge wa Majimbo wa Mkoa wa Arusha, jana ameongea kaka yangu Mrisho Mashaka Gambo, ameongea vizuri kuhusiana na Wizara hii, umuhimu wa Wizara hii katika mkoa wetu. Vilevile baba yangu Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido ameongea vizuri sana kuhusiana na umuhimu wa Wizara hii na mimi kama mwakilishi wa Mkoa wa Arusha, naomba nisisitize umuhimu wa Wizara hii katika Mkoa wetu wa Arusha (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba pia niwashauri Wizara hii ya Maliasili na Utalii waendelee kuwashirikisha wadau wakuu wa maendeleo wa Mkoa wa Arusha katika maendeleo ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba niongelee suala moja tu la sintofahamu iliyoko katika Wilaya ya Longido kuhusiana na maamuzi ya Serikali kutenga maeneo yao kuwa Mapori ya Akiba. Naomba niikumbushe Wizara kwamba asilimia 95 ya wakazi wa Longido wanajihusisha na ufugaji na wanategemea sana mapori haya kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Maamuzi haya ya Wizara yataathiri Zaidi ya vijiji 19, vya Tarafa ya Ketumbeine na vijiji 11 vya Tarafa ya Engarenaibor na kijiji kimoja cha Tarafa ya Longido. Tukumbuke kwamba pia katika maeneo haya kuna wakazi zaidi ya 90,000 ambao wanategemea pori hili katika masuala yao mbalimbali ya kuishi na katika kuinua kipato cha uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa pia kwa juhudi zao binafsi wameendeleza miundombinu ya masuala ya kijamii kama afya, elimu na kadhalika. Kwa hiyo sidhani kwamba ni suala la busara kuwaondoa katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu wa Awamu ya Tano yake alifanya jitihada kubwa sana kurudisha zaidi ya vijiji 900 kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kuishi na kufanya shughuli zao mbalimbali za kiuchumi. Vile vile katika hotuba ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, aliyoisoma tarehe 22 Aprili, hapa Bungeni alionyesha dhamira kubwa ya Serikali katika kuongeza maeneo ya wafugaji hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizi za Wizara hii ya Maliasili na Utalii, naona dhahiri zinakinzana na dhamira njema ya Serikali kwa wananchi wetu. Naiomba sana Serikali yangu sikivu kupitia Wizara hii, itumie busara katika jambo hili ili basi lisiweze kuleta madhara kwa wananchi wetu. Naomba pia wizara hii kabla ya kufanya maamuzi kama haya iweze kuwashirikisha wadau mbalimbali hususani wa maeneo yale ili waweze kutoa maoni yao juu ya mambo haya. Vile vile naomba sana Wizara kabla ya kufanya maamuzi haya iweze kutembelea maeneo haya ili ijue basi, kama kweli maeneo haya ni mapori ama ni makazi ya wanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Waziri wa Fedha kwa uwasilishaji uliotukuka wa rasimu ya mpango. Mimi binafsi kama Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti pamoja na wenzangu tulipokea mapendekezo yale na tuliyafanyia uchambuzi wa kina. Nashukuru na pia, naipongeza Serikali kwa kuchukua mawazo yet una kuyajumuisha katika rasimu ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wowote ule unahitaji rasilimali fedha na Waheshimiwa Wabunge hapa wameongea mambo mengi sana ya kimkakati, jinsi gani tutapata fedha kwa ajili ya kuwezesha Mpango wetu utekelezeke kwa kiwango cha juu. Naomba nijikite kwenye suala la udhibiti wa mapato. Mambo yote haya yaliyoongelewa na Wabunge mambo mazuri yatakuwa hayana maana sana kama tutashindwa kudhibiti mapato yetu tutakayoyapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la GePG, yaani Government Electronic Payment Gateway. GePG ni mfumo wa Serikali wa kukusanya mapato kielektroniki. Naweza kusema kwamba, Serikali imeshindwa kudhibiti mapato yetu kupitia mfumo huu kwa kiasi kikubwa. Ni kweli, mfumo huu umeisaidia Serikali kuongeza mapato yake, lakini vilevile inabidi tuufanyie kazi zaidi kuhakikisha tunadhibiti mapato yetu mpaka mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu tumewaamini na tumewaachia sekta binafsi watusaidie kukusanya mapato haya, hususan sekta ya simu, makampuni ya simu na mabenki mbalimbali, lakini inavyoonekana makampuni haya binafsi yamewekeza sana kwenye rasilimali watu pamoja na teknolojia ukilinganisha na wafanyakazi wa Serikali wanaohusika moja kwa moja na mifumo hii. Kwa hiyo, kuna mwanya mkubwa sana hapo wa kupoteza mapato kwa sababu ya tofauti ya kiufahamu wa mifumo hii. Naishauri Serikali iweze kuwekeza kwa rasilimali watu na teknolojia kwenye mifumo hii ili basi tuweze kuitumia mifumo hii kwa ufasaha na ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee suala la mawasiliano. Naweza kusema kwamba, sekta hii ya mawasiliano ni moja ya sekta ambazo zinachangia kodi kubwa na uchumi wa nchi hii, lakini Serikali yetu sijaona jitihada zake za dhati kuisaidia sekta hii ili iweze kukua zaidi na Serikali iweze kukusanya mapato zaidi kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kodi kubwa, tozo mbalimbali na masharti mengi yanayowekewa sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kutolea mfano tu, kuna maeneo mengi ya vijijini, kwa mfano kule Longido kuna Kata ya Nondoto Matale, hata Wilaya ya Meru kuna Kata ya Ngabobo, hakuna mawasiliano ya simu, lakini sekta hii mdhibiti, ndio kazi yake kubwa kuhakikisha kwamba, sehemu mbalimbali zinapata mawasiliano, hususan sehemu za vijijini. Kampuni hizi za simu zinakatwa tozo ya asilimia tatu katika mapato yake inaenda kwenye mfuko unaitwa USCAF (Universal Fund) na lengo kubwa la Mfuko huu ni kuendeleza mawasiliano sehemu za vijijini na mijini. Sasa napenda kujua kwamba, Mfuko huu unafanya kazi gani hasa kama kuna sehemu nyingi tu za nchi hii ambazo hazina mawasiliano ya kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya Elimu. Mchango wangu utajikita hasa kwenye kuishauri Serikali katika mambo kadhaa ambayo yanaweza kuinua ubora wa elimu yetu ili kutoa wahitimu wenye weledi na wenye ujuzi sahihi ambao unahitajika katika soko letu la ajira. Naomba vile vile, niwapongeze Kamati ya Huduma za Jamii kwa maoni yao ambayo yanaonesha dira ya kuinua kiwango cha elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kuongelea suala la mikopo ya elimu ya juu. Naomba kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuweza kufuta ile retention fees ya 6% iliyokuwepo katika mikopo ya elimu ya juu. Tunamshukuru sana mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Elimu, nimesikiliza hotuba yake leo na ameweza kufuata maoni ya Wabunge wengi na kuifuta ile asilimia 10 ya penalty, tunashukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la mikopo bado kama Serikali, inabidi tufanye kazi sana, tuendelee kuondoa vikwazo na changamoto mbalimbali ikiwemo masharti magumu kwa wahitimu wetu wenye kupata mikopo hii ya elimu ya juu. Asilimia 15 ya marejesho ya mikopo hii bado ni kubwa kwa wahitimu wetu. Wahitimu wetu wengi wakiajiriwa wanapata mishahara ya kima cha chini na walio wengi hawazidi shilingi laki tano. Kuwatoza asilimia 15 ya marejesho ya mikopo ya elimu ya juu, bado kuna kodi na pensheni pamoja na tozo nyingine kwa kweli hatuwatendei haki wahitimu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kupitia Bodi ya Mikopo iweze kupunguza asilimia hii hadi kufikia basi angalau asilimia 10 ili tuweze kuwawezesha wahitimu wetu waishi maisha mazuri. Vilevile, tuwape nafasi wale ambao wanaweza kuchangia zaidi ya asilimia 10, basi wapeleke marejesho yao katika Bodi ya Mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo la ajira kwa wahitimu wetu bado ni changamoto. Naishauri Serikali, ili kukabiliana na tatizo hili, basi Serikali ianzishe scheme maalum ya mikopo kwa wahitimu wetu ili basi, wakimaliza pale vyuo vikuu kama hawajapata ajira, waweze kujiajiri wenyewe katika sekta ambazo siyo rasmi. Vile vile, nashauri mikopo hii tuishushe kwenye vyuo vyetu vya kati ikiwemo VETA ili basi wahitimu wetu wa-apply ujuzi wao na kwa kutumia mikopo hii waweze kujiajiri na kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la TEHAMA. Sasa hivi dunia yote inaelekea kwenye digital economy. Naomba Serikali kupitia Wizara ya Elimu iweze kuwekeza katika masomo ya TEHAMA hususan katika shule za sekondari ili basi, tuweze kuwawezesha vijana wetu kupambana na huu uchumi wa kidijitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii ukitaka kuongeza ukusanyaji wa mapato kidijitali, unahitaji wataalam wazuri wa TEHAMA; ukitaka kupata wataalam wa masoko ya mazao yetu na bidhaa nyingine, tunahitaji wataalam wazuri wa TEHAMA. Kwa hiyo, basi naweka msisitizo katika Wizara hii ya Elimu tuweze kuwekeza kwenye masomo ya TEHAMA ili tuwasaidie vijana wetu wapambane na changamoto za uchumi wa kidijitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, ili kuinua elimu yetu ya msingi na sekondari, nashauri, tuweze kuboresha mazingira mbalimbali ya utoaji wa elimu ikiwemo kuweka miundombinu ambayo ni bora zaidi, ikiwemo nyumba za walimu, madarasa na maabara hususan kwenye shule zile za sayansi. Tukiweka mazingira bora ya kufundishia na vile vile, tukiwapa motisha walimu wetu hususan wale wenye kufundisha vizuri na kufaulusha na wale wenye kufundisha kwenye mazingira magumu labda shule za pembezoni, sasi tutaweza kuinua elimu yetu kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kule Loliondo Ngorongoro, Karatu, Mang’ola, Lokisale, Monduli walimu wetu watapenda kwenda kufundisha wanafunzi wetu na kwa ujumla tutaweza kuinua kiwango chetu cha elimu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu katika mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Arusha vilevile naomba niendelee kumpongeza Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuongoza kwa weledi mkubwa na vilevile kwa kuendeleza diplomasia ya kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuchangia kwenye sekta muhimu ya afya. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma hizi za afya pamoja na maboresho yote yaliyofanyika bado kuna changamoto nyingi sana kwa wananchi wetu kupata huduma bora za afya. Changamoto hizi ni pamoja na gharama kubwa za afya kwa wananchi wetu, ubora wa afya wanaopata wananchi wetu na vilevile kupata kwa huduma za afya kwa wakati. Changamoto zote hizi suluhisho lake ni moja tu ni kuwapatia wananchi wetu bima ya afya kwa wote. Taarifa za kutoka Wizara ya Afya mpaka leo hii ni asilimia 12 tu ya Watanzania ambao wananufaika na huduma hizi za bima ya afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati ilivyoshauri kwenye mapendekezo yake na mimi naomba niweke msisitizo kwa Serikali kutuletea Muswada wa Sheria wa Bima ya Afya kwa wote ili basi sheria hii iweze kwenda sambamba na Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa na vilevile wananchi wetu waweze kunufaika na huduma bora za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niweze kuchangia katika mwenendo wa riba za mabenki. Jana tulimsikia Mheshimiwa Waziri hapa akisema moja ya mafanikio ya sekta hii ya mabenki ni kushuka kwa riba kutoka asilimia 16.8 hadi asilimia 16.6, punguzo la asilimia 0.2 tu. Sisi kama wawakilishi wa wananchi hatuwezi kwenda kusema kwamba punguzo la asilimia 0.2 tu ni mafanikio ya sekta hii ya kibenki. Wananchi wetu bado wanateseka na riba kubwa za mikopo ya kwenye mabenki nasi Wawakilishi wao inabidi tufanye jitihada za makusudi kuhakikisha riba hizi za mabenki zinashuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumemsikia Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwenye hotuba zake nyakati tofauti akiagiza Benki Kuu ya Tanzania iweze kushusha riba hizi za mabenki hadi kufikia asilimia 10 au chini ya hapo. Asilimia 16.6 inayosemwa hapa hii ni wastani tu, bado kuna wananchi wengi wanakopa kwa riba ya zaidi asilimia 18. Natambua sana jitihada zinazofanywa na Serikali yetu kuhakikisha riba hizi za mabenki zinashuka, wamesema wenzangu hapo ikiwemo mojawapo ni kupunguza kiwango cha chini cha akiba ambazo mabenki haya yanawekeza BOT yaani Statutory Minimum Reserve hadi kufikia asilimia Nane, lakini bado tumeona hili siyo suluhisho la kushusha riba za mabenki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali yetu imetoa Shilingi Trilioni Moja imewapa Benki Kuu ya Tanzania ili kuweza kushusha hizi riba za mabenki, lakini bado tumeona siyo suluhisho pia ya kushusha riba hizi. Pamoja na hayo jitihada zote zilizofanywa bado tunaona ni punguzo la asilimia 0.2 tu ambayo bado sidhani kama tunaweza tukajisifia kuwa ni mafanikio ya sekta hii ya kibenki. Naamini Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Wizara yetu ya Fedha inao wachumi wabobezi wengi na kwa pamoja wanaweza kushirikiana kuhakikisha riba hizi za mabenki zinashuka kwa asilimia kubwa. Ili uchumi wetu uweze kuwa uchumi shirikishi na jumuishi lazima wananchi wetu waweze kwenda kwenye mabenki mbalimbali na kuwa na uwezo wa kukopa kwa riba nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti tuliweza kukutana na Umoja wa Mabenki ya Tanzania (TBA) na walitupa changamoto zao nyingi ambazo zinachangia gharama kubwa za uendeshaji wa mabenki na hivyo wao wanalazimika kuongeza riba katika mabenki yetu. Sababu nyingi walizotupa kati ya hizo kuna sababu mbili ambazo zipo ndani ya Wizara ya Fedha ambao wao wanaweza kuzitatua ili basi kuhakikisha riba hizi zinaweza kushuka kwa wanachi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu walizozitaja moja wanasema kupishana kwa sera kati ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania na Benki Kuu ya Tanzania, zote hizi ni Taasisi za Serikali naamini Waziri wetu hapa anaweza kukaa na taasisi hizi na kusuluhisha na kufanya riba za mabenki ziweze kushuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine waliyoitaja Umoja wa Mabenki, walisema vilevile ni kutokuwa na ushirikiano kati ya Mamlaka ya Serikali na mabenki ya biashara. Naamini pia hii sababu iko ndani ya Wizara ya Fedha, wanaweza kwa pamoja wakashirikiana na umoja wa mabenki haya ili basi watafute suluhisho la kushusha riba hizi za mabenki kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia namuomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hotuba yake aweze kutueleza hapa mikakati Serikali iliyonayo itakayofanya kwa ajili ya kushusha riba za mikopo kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)