Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maryprisca Winfred Mahundi (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kukushukuru wewe pamoja na Bunge lako Tukufu kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee napenda kumshukuru Waziri wangu wa Maji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, Mbunge kwa kuwasilisha kwa umahiri hoja ya Wizara yetu ya Maji kuhusu Mpango wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Maji imechangiwa na Wabunge wengi, tunashukuru sana Ni wazi kuwa muda niliopewa kikanuni hautanitosha kujibu hoja zote kwa ufasaha. Hivyo, katika muda huo mfupi, kwa kuzingatia wingi wa hoja, naomba nijikite kwenye baadhi ya hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mkoa wa Mtwara, napenda kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge wote maelezo yote waliyoyatoa kutokana na matatizo ya maji katika Mkoa wa Mtwara, kwa uchache nichukue matamshi ya Mheshimiwa Tunza Malapo na Mheshimiwa Hokororo; waliongea kwa hisia kali sana kuhusiana na akina mama wa Mtwara kuchota maji ambayo wanasema ni maji ya kuokota. Wamekuwa wakitamka hivyo kwa sababu ni maji ambayo walikuwa wakiyatega nyakati za mvua na kuingia kwenye mashimo ambayo wanakuwa wameyaandaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa kama mama, suala hili limeniingia na kujisikia vibaya. Nitawajibika kwa nafasi yangu kuhakikisha tunaenda kutekeleza mikakati ya Wizara ambayo tumejiwekea hasa kwa kutumia Mto Ruvuma. Chanzo hiki cha Mto Ruvuma naamini kitakuwa ni suluhu ya matatizo ya maji Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia mradi wa maji Ziwa Victoria kwa Mkoa wa Simiyu. Mkoa huu upo katika hatua za mwisho kupata huu mradi wa maji na tayari tuko kwenye hatua za kuweza kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya kazi ya usimamizi. Mara baada ya kupata Mhandisi Mshauri, kazi ya kumpata mkandarasi wa ujenzi pia itafanyika. Lengo ni kuona kwamba ujenzi wa mradi huu unakwenda kuanza mara moja. Tutafanya hivi kwa kuhakikisha tunasambaza maji maeneo yote ambayo bomba kuu litapita; kilomita 12 kulia na kilomita 12 kushoto kama sera inavyotutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mkoa wa Songwe, napenda kuwapongeza Wabunge wote; Mheshimiwa George Mwenisongole, Mheshimiwa Shonza, Mheshimiwa Hasunga, Mheshimiwa Condester na Mheshimiwa Neema. Wote wamechangia kwa uchungu, namna ambavyo maji yamekuwa ni tatizo. Kwa Mkoa wa Songwe tuna mradi mkubwa wa chanzo cha maji cha Ileje; na yenyewe tunakwenda kushughulikia mwaka ujao wa fedha. Baada ya kushughulika na chanzo hiki cha Ileje, tunaamini tunakwenda kutatua tatizo la maji Mkoa wa Songwe katika Majimbo karibia yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuhusiana na kufikisha maji katika taasisi zetu za Serikali kama vile mashule ama mahospitali na vituo vya afya, tayari Wizara ipo kwenye mchakato wa kuona tunafanya ushirikiano mzuri pamoja na Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya ili kuhakikisha shule zetu zinapata maji na watoto wanapata maji katika mazingira rafiki. Lengo ni kuona tunakwenda kuondoa changamoto ya mimba za utotoni na vile vile kuhakikisha watoto nao wanafikia ndoto zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tayari katika utekelezaji nimeshalifanya katika ziara zangu. Nilishakwenda Biharamulo na nikahakikisha nimeacha maagizo pale ya shule ya sekondari kupata maji; Singida vilevile na pia katika Mkoa wa Mbeya nimetoa maagizo katika Sekondari ya Lyoto na yenyewe iweze kupatiwa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikiongea mara nyingi, kwa sasa hivi Wizara ya Maji tuko katika mageuzi makubwa. Malalamiko haya ya Waheshimiwa Wabunge tunayasikia na sisi tukiwa kama sehemu ya jamii, tunayafahamu. Tukwenda kutekeleza miradi yote ambayo imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu na tutahakikisha inakwenda kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote ambayo imekuwa ikiwasumbua wananchi katika maeneo mbalimbali kwa kutokukamilika, sasa hivi RUWASA imechukua nafasi. RUWASA imekuwa ni changa, bado tu ina mwaka mmoja lakini wameshafanya ufumbuzi wa miradi mbalimbali. Kwa hiyo, tutaendelea kutumia pia wanafunzi wetu ambao tunawapata kwenye Chuo chetu cha Maji na vile vile watumishi ambao wapo ndani, tayari na wao wameendelea kuchukua kasi ya Waziri wetu Mheshimiwa Jumaa Aweso, kwa sababu yeye wakati wote anahitaji kuona matokeo ya haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi watendaji wameshabadilika, wameshaachana na kufanya kazi kwa mazoea na sasa hivi wanafanya kazi vizuri. Wakurugenzi, Mameneja wa Mikoa na Wilaya tunawashukuru sana kwa sababu maagizo tunayowaachia tukiwa katika ziara zetu, yamekuwa yakifanyiwa kazi kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mikakati ambayo tumejiwekea kama Wizara ya kuhakikisha maeneo ya vijijini ambako maji hayajawahi kutoka bombani, sasa ndiyo wakati wa maji kutoka bombani. Tunataka tuhakikishe akina mama wanaachana na kazi ngumu ya kubeba maji vichwani, tunakwenda kumtua ndoo mwanamama kichwani. Hapa nina kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake ya matumaini makubwa kwa Wizara ya Maji alipokuwa akihutubia Bunge lako Tukufu aliweza kutuhakikishia kwamba atakwenda kutuongezea fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukishapata fedha, ni usimamizi; sisi tuko tayari tutakesha, tutafanya kazi usiku na mchana. Lengo ni kuona kwamba tunahakikisha akina mama wanapata maji kwa umbali ambao ni rahisi kufikika na wanaachana na shughuli za kubeba ndoo vichwani na kupoteza muda mwingi. Tunafahamu kwamba ndoa nyingi zimekuwa zikivunjika kwa akina mama hawa kukesha huko kwenye visima, vilevile tunafahamu kuna akina mama waliopata hata ulemavu kwa sababu ya kupata vipigo vikali kutoka kwa waume zao. Sisi kama Wizara tumesema kwamba suluhu sasa ya akina mama kuondokana na dhoruba hizi zote inakwenda kupatikana mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mkoa wa Mbeya kuna mradi mkubwa wa kimkakati wa Kiwira. Huu utasambaza maji katika maeneo yote ya Jiji la Mbeya, maeneo ya Chunya kwa badaye, maeneo ya Rungwe Mbeya Vijijini na maeneo ya Ileje pia yatajikuta yananufaika na mradi huu mkubwa. Huu mradi tutausimamia kwa karibu na tutaona kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha tumeshautengea fedha ya kutosha na tutakuwa tunautengea mara kwa mara. Lengo ni kuona kwamba unakwenda kukamilika ndani ya muda ambao unahitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa Mkoa wa Mbeya kwa mji wa Tukuyu pale mjini, tayari tumeendelea kupeleka fedha. Hivi karibuni tumepeleka shilingi milioni 500. Lengo ni kuona kwamba tunaboresha maji katika Mji wa Tukuyu, lakini vilevile kusimamia fedha ambazo tunazipeleka kule wilayani na mikoani ili ziweze kufanya kazi na tutasimamia kuhakikisha thamani ya pesa inakwenda kuonekana katika utekelezaji wa miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mbeya pale mjini tumepeleka Ilunga Project ambayo itasaidia maeneo ya Iwambi mpaka Mbalizi. Kwa Chunya tutaangalia mradi wa Matwiga ambao sasa umekuwa ni wa muda mrefu sana toka mwaka 2012, lakini toka baada ya RUWASA kuundwa mradi ule sasa unaelekea mwishoni, unakwenda kukamilika na vijiji 16 vinakwenda kunufaika. Yote haya ni katika kuona kwamba mageuzi ndani ya Wizara ya Maji yanakwenda kutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuongea haya yote, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nampenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametufanikisha kujadili mjadala huu muhimu sana kwa mustakabali wa maisha yetu kwani maji ni uhai na ni haki ya msingi kwa mwanadamu yeyote yule.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo ameweza kutuheshimisha Wizara ya Maji. Kwa mara ya kwanza tayari tumeweza kufikia asilimia 95 za kupata fedha za mwaka wa fedha tunaoelekea kumaliza, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, na tunasema hatutaacha kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha dhamira yake njema ya kumtua mama ndoo kichwani inakwenda kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende kukushukuru wewe binafsi kwa namna ambavyo umeweza kutuongoza vyema na hata leo hii ndani ya Bunge lako tukufu bajeti hii imeweza kujadiliwa kwa mapana.

Mheshimiwa Spika, nipende kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa umoja wetu, mmeweza kutupongeza, tumepokea pongezi zote; mmeweza kutupa changamoto, yote tumeweza kuyapokea. Tunaahidi haya yote ambayo mmeweza kuyajadili kwa siku mbili ndani ya Bunge hili Tukufu ni deni kwetu.

Mheshimiwa Spika, mmetupongeza tumepokea kama deni. Kazi ambayo tumeweza kuifanya kwa mwaka mmoja ambao tunaelekea kuumaliza tunaahidi tutaongeza ushirikiano kwenu kuhakikisha majimbo yote tunayafikia na huduma ya maji inakwenda kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, michango ni mingi na tunashukuru sana kwa michango yote. Ninakwenda kuongea tu kwa uchache kwa sababu Mheshimiwa Waziri ataongea kwa marefu.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuongea kwenye Jimbo la Chemba; Mheshimiwa Monni ameongea mengi lakini nipende tu kusema kwamba Wizara inatambua changamoto zote ambazo Wilaya ya Chemba inaishi nazo.

Mheshimiwa Spika, lakini changamoto hizi kulingana na upendo wa Mheshimiwa Rais ambavyo ameweza kutupatia fedha za kutosha tutaendelea kuhakikisha changamoto iliyoko chemba tunakwenda kuifanyia kazi. Tayari tunakwenda kuchimba Bwawa la Farkwa ambalo maji yatakwenda mpaka Chemba, hiyo nayo itasaidia kwa sehemu kubwa sana kuwa na chanzo cha uhakika na mradi kuwa endelevu kwa sababu tunatamani mradi utakapokamilika basi mradi huo uwe na manufaa kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaongelea pia kidogo kwa Mheshimiwa Dunstan Kitandula, Mbunge wa Mkinga. Naye pia tumepata hoja yake kuhusiana na matumizi ya Mto Zigi. Tumezingatia, tumepokea, na tutakwenda kuhakikisha tunatumia Mto Zigi ili uweze kupeleka maji Mkinga katika maeneo yale ambayo imeshindikana kupatikana mabwawa yakiwa yanakauka, sasa Mto Zigi utakwenda kuwa suluhu.

Mheshimiwa Spika, pia nitaongelea kidogo Mbeya Mjini; hili ni jimbo lako wewe. Umetuongoza hapa Wabunge wote tunafanikiwa, ni kwa sababu ya umahiri wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Mbeya Mjini tunafahamu tatizo la maji suluhu yake ni Mto Kiwira. Tayari Mhandisi Mshauri ameshaleta andiko lake la awali sasa hivi tunamsubiria aweze kukamilisha andiko ambalo litatupatia gharama nzima ya mradi na tayari sisi kama Wizara tunaendelea kufanya shortlisting ya kupata wakandarasi ili tuweze kumpata mkandarasi sahihi ambaye ataweza kumudu mradi ule mkubwa, mradi ambao Mbeya Jiji unautegemea.

Mheshimiwa Spika, mradi ule hautakuwa kwa ajili ya Mbeya Jiji tu, ni mradi ambao maeneo ya pembezoni mwa Mbeya Vijijini pia yanakwenda kunufaika; maeneo ya Chunya tunarajia yaje yanufaike na mradi huu; maeneo ya Mbalizi yanakwenda kunufaika; maeneo ya Rungwe pia yatakwenda kunufaika. Ni mradi ambao una tija hivyo, kwa heshima kubwa sana tunaliyonayo juu yako tutakwenda kufanya hili na wananchi watakwenda kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Mbeya, nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Suma Fyandomo, jana amechaniga kisomi sana, naamini sote tumesikia. Mradi wa Tukuyu Mjini nao pia tutakwenda kuuzingatia; ushauri tumeupokea na tutaufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lengo la kuona kwamba force account huenda inachelewesha mradi, tutazingatia kuona namna tutaweza kushirikiana labda ya wakandari ili kuona mradi ule unakamilika. Na maeneo yote ambayo uliyataja kwa Tukuyu Mjini pamoja na kule alikotokea Mheshimiwa Spika wetu, basi yatakwenda kupata maji. Na haya tunayaongea siyo kama siasa, ila tunasema tunakwenda kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mungu katika hoja zote zilizotolewa zipo ndani ya uwezo wa Wizara na tunaweza kuongea haya yote kwa sababu Mheshimiwa Rais yupo tayari kuwa begabega na sisi. Tumejionea wenyewe kwa matendo, mliongoea hapa bajeti iliyopita lakini matendo na utekelezaji wa miradi sisi sote ni mashahidi. Hivyo, haya yote ambayo ninayaongea tutakwenda kuyafanyia kazi kadri Mungu atakavyotuongoza na namna ambavyo Mheshimiwa Rais ataendelea kutuwezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nihamie Jimbo la Magu kwa kaka yangu, Mheshimiwa Boniventura Kiswaga. Jana ameongelea hapa kuhusu maji katika eneo lake. Sisi kama Wizara tumesema miradi ambayo inaendelea na utekelezaji ndani ya jimbo lake tutaisimamia kuhakikisha inakamilika; lengo ni kuona maji yanatoka bombani.

Mheshimiwa Spika, tunaposema mradi ukamilike tunahitaji kuona akina mama wanapata maji bombani yakiwa safi na salama na yakutosha na katika umbali rafiki. Tunahitaji kuona kwamba dhamira njema ya Mheshimiwa Rais inakwenda kuokoa ndoa za akina mama wengi.

Mheshimiwa Spika, akina mama wamekuwa wakiamka usiku wa manane na hii sasa tunaelekea ukingoni. Akina mama watapumzika nyumbani mpaka kunapambazuka, shughuli za nyumbani zitakamilika na maji yatakwenda kupatikana karibu na makazi ya wananchi. Na hili tutalitekeleza kuendana na mradi wake wa Butimba na miradi yote ambayo ipo ndani ya jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia basi pia naomba niongelee kidogo kwenye Jimbo la Biharamulo, Mheshimiwa Engineer Ezra ameweza kutuelekeza hapa hitaji la matumizi ya maji ya Ziwa Victoria. Sisi kama Wizara tumesema Biharamulo inakwenda kupata maji kupitia Ziwa Victoria. Na hii tutaifanya, tutafika kuhakikisha tunaleta msukumo mkubwa ili maji yaweze kupatikana na ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, kwa ufupi nipende tena kuwashukuru Wabunge wote. Wabunge tunaomba mtusaidie kupitisha hii bajeti, lengo ni kwamba tuweze kukutana site, Sisi ombi letu kwenu ni kupitisha bajeti tuje tusimamie miradi, kama ambavyo tumefanya tuna uhakika tutafanya zaidi na zaidi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu. Ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)