Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Mary Francis Masanja (111 total)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kunakuwepo na Mwongozo kwa Tour Operators wanaopandisha watalii Mlima Kilimanjaro wanaoajiri Wapagazi, Wapishi na Waongoza Misafara kwa kuwalipa ujira stahiki?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kusimama mbele ya Bunge hili. Vile vile namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na chama changu kwa kuniamini na leo hii nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2015 ilitoa Mwongozo kwa Mawakala wa Utalii wa Mlima Kilimanjaro Tour Operators wa kuwalipa ujira stahiki Wapagazi, Wapishi na Waongoza Watalii waliowaajiri kwa ajili ya kuwahudumia watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwongozo huo, Serikali iliagiza kuwa mwongoza watalii alipwe dola za Kimarekani 20 kwa siku, sawa na Sh.40,000 kwa siku, mpishi alipwe dola za Kimarekani 15 sawa na shilingi 30,000 na mpagazi alipwe dola za Kimarekani 10 sawa na Sh.20,000 kwa siku. Wastani wa siku za kupanda mlima hadi kileleni na kushuka ni kuanzia siku 5 hadi 7.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 12 Disemba, 2015, wadau wa utalii wa Mlima Kilimanjaro ambao ni mawakala wa utalii, viongozi wa wawakilishi wa vyama vya waongoza watalii, wapagazi na wapishi walikutana na kusaini mwongozo huo wa malipo ambapo pande zote ziliridhia viwango hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mwongozo huu na makubaliano hayo. Katika utekelezaji wa mwongozo, kulijitokeza changamoto ya baadhi ya mawakala wa utalii kutokulipa viwango hivyo na kwa hivyo Serikali iliweka mikakati kadhaa ya kuhakikisha kuwa viwango hivyo vinalipwa kama ilivyoagizwa. Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na: -

(i) Kushirikiana na Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kuandaa mikataba ya kisheria ambapo mawakala wa utalii husaini pamoja na waongoza watalii, wapagazi na wapishi wanaoajiriwa kabla ya kuanza kazi. Mkataba huo umeainisha kiwango cha malipo na idadi ya siku atakazofanya kazi na jumla ya malipo anakayostahili kulipwa. Nakala moja ya mkataba huu hukabidhiwa kwenye lango la kupandia mlima, nakala nyingine hupewa waajiriwa (waongoza watalii, wapishi na wapagazi) na nakala moja hubaki kwa wakala wa Utalii.

(ii) Idara ya Kazi imekuwa ikihimiza waajiriwa kutokuanza kazi bila ya kuwa na mikataba. Pia, Idara imekuwa ikifanya ukaguzi wa karibu na wa mara kwa mara katika malango ya hifadhi, ofisi za mawakala wa utalii ili kujiridhisha kuwa utaratibu huo unazingatiwa wakati wote; na

(iii) Changamoto zinazotokana na waajiriwa kutokulipwa kiwango stahiki, kuchelewa kulipwa au kutokulipwa kabisa zimekuwa zikishughulikiwa kwa karibu na Idara ya Kazi na vyama vya waongoza watalii na wapagazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutoa wito kwa waongoza watalii, wapishi na wapagazi kuendelea kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya Taifa. Pia, Serikali inaendelea kutoa wito kwa mawakala wote wa utalii kuhakikisha kuwa wanatoa ujira stahiki kwa wahusika ili waendelee kupata motisha ya utendaji kazi.
MHE. MARGARET S. SITTA Aliuliza: -

Serikali imeanzisha Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla Wilayani Urambo: -

(a) Je, ni lini Serikali itatoa elimu elekezi kwa wananchi wa maeneo hayo juu ya matumizi ya eneo husika baada ya mabadiliko yaliyotokea?

(b) Kutokana na ongezeko la watu, je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi maeneo kwa ajili ya ufugaji nyuki, mifugo na kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Urambo lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla ina ukubwa wa kilomita za mraba 3,865. Hifadhi hii ilianzishwa kwa Azimio la Bunge la tarehe 10 Septemba, 2019 na Tangazo la Serikali Na. 936 la tarehe 29 Novemba, 2019. Hifadhi ipo katika Wilaya ya Urambo na Kaliua Mkoani Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya kuanzishwa kwa hifadhi hii ni kuimarisha uhifadhi ili kuunganisha mfumo wa ikolojia wa Malagarasi - Muyowosi ambao ni ardhi oevu yenye umuhimu wa kitaifa na kimataifa pamoja na kuongeza pato la Taifa kutokana na ongezeko la idadi ya watalii, kuwezesha jamii kunufaika na fursa za utalii na kutunza vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na Mpango kutoa Elimu ya Uhifadhi ambao unalenga kujenga uwezo na uelewa kwa wananchi, viongozi na wadau wengine wa uhifadhi ambao wanapakana na Hifadhi za Taifa. Utekelezaji wa mpango huo, ulianzia kwenye Wilaya ya Kaliua, ambapo ulihusisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na vijiji 12. Hatua inayofuatia ni kuendelea na programu hiyo kwenye Wilaya ya Urambo, ambapo zoezi litaanzia kwenye Kata ya Nsendo ambako vijiji nane (8) vitahusishwa. Nia kubwa ya uhamasishaji huo ni kujenga uelewa kuhusu sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa Hifadhi za Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2021/2022, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kutekeleza mpango wa kutoa elimu ya uhifadhi na kuweka mkazo kwenye kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya husika, pamoja na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi; kuendelea kuhakiki mipaka ya maeneo ya hifadhi kwa kuweka alama za kudumu na mabango elekezi ili mipaka ionekane kwa urahisi; na kuendelea kutoa huduma za ugani kwa ushirikiano na wadau wa uhifadhi katika maeneo mbalimbali ili kutunza mazingira, vyanzo vya maji na misitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Hifadhi za Taifa Tanzania, Sura 282 iliyofanyiwa Mapitio mwaka, 2002 kinabainisha kuwa Mheshimiwa Rais akishatangaza eneo la ardhi yoyote kuwa Hifadhi ya Taifa, haki zote za awali zikiwemo hati miliki zilizokuwa juu ya eneo husika zinakoma. Wizara yangu itawasiliana na Mamlaka za Mikoa na Halmashauri ili kupata maeneo nje ya Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla kwa ajili ya shughuli za ufugaji nyuki, mifugo na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa wananchi wote wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuzuia na kupambana na ujangili na hatimaye kuboresha utalii kwa ajili ya maendeleo endelevu katika jamii husika na nchi kwa ujumla.
MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:-

Kumekuwa na ongezeko la wanyamapori katika Hifadhi ya Mbuga ya Selous na sasa tembo na nyati wanavamia mashamba pamoja na makazi ya wanavijiji na kuleta taharuki:-

Je, Serikali inaweza kuwarudisha wanyama hao porini mbali zaidi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mali asili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Aidha, Wizara inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuweka alama katika shoroba na mapito ya wanyamapori ili kuimarisha uhifadhi wake na kuendelea kufanya utafiti na kueneza matumizi ya mbinu mbadala za kujikinga na wanyamapori waharibifu hasa tembo. Baadhi ya mbinu hizo ni: Matumizi ya pilipili, mafuta machafu (oil) na mizinga ya nyuki; na kutoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji. Katika Wilaya ya Namtumbo, jumla ya askari wa wanyamapori wa vijiji 198 wamepewa mafunzo.

Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikiendelea kufanya doria za msako kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2020 zilifanyika doria za msako zenye jumla ya sikuwatu 133 katika vijiji vya Wilaya ya Namtumbo; kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo jumla ya wananchi 2,303 walipata elimu katika vijiji 42 vya Wilaya za Namtumbo na Tunduru; kuimarisha vituo maalum vya doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika Kanda za Kalulu na Likuyu- Sekamaganga.
MHE. FESTO R. SANGA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarudia zoezi la kuweka alama za mipaka kwa kuwashirikisha wananchi ili kumaliza mgogoro uliopo wa mipaka kati ya Hifadhi ya Kitulo na wananchi wa Vijiji vya Misiwa, Makwalanga, Igofi na Nkondo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2016, Serikali ilishaweka alama za mipaka za kati kwenye maeneo ya Hifadhi ya Taifa Kitulo inayopakana na vijiji vya Misiwa, Mwakalanga, Igofi na mwaka 2018 katika Kijiji cha Nkondo.

Mheshimiwa Spika, zoezi hili la uwekaji wa alama lilishirikisha Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Makete, Waheshimiwa Madiwani, Serikali za Vijiji, wananchi kwa ngazi ya vijiji, pamoja na wataalam wa ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Elimu ilitolewa kwa wananchi kuhusu zoezi la uwekaji alama za mipaka kwenye vijiji hivi kabla ya uwekaji wa alama za mipaka hiyo. Baada ya utoaji wa elimu, wananchi walichagua wawakilishi watano katika kila kijiji ili kujiunga na timu ya watumishi kutoka Hifadhini na wataalam wa ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Makete, ili kufanya utambuzi wa eneo la mipaka na kuweka mipaka hiyo kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na.279 la Mwaka 2005 la uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa Kitulo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa kwamba maeneo hayo tajwa yalikwishawekewa alama za mipaka na zoezi hilo liliwashirikisha wananchi kikamilifu. Lengo kuu la zoezi hilo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa mipaka inaonekana bayana na pia shughuli za kibinadamu hazifanyiki ndani ya eneo la hifadhi.

Mheshimiwa Spika, ni imani yetu kwamba mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Taifa Kitulo na vijiji vilivyotajwa ulishapatiwa suluhu kwa kuzingatia Tangazo la Serikali na tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano wao ili kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi.
MHE. SILLO D. BARAN Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya mipaka kati ya Hifadhi ya Tarangire na Vijiji vya Gijedabung, Ayamango, Gedamar na Mwada katika Jimbo la Babati Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilihakiki mpaka wa Hifadhi ya Taifa Tarangire mwaka 2004 kwa kutumia Tangazo la Serikali Na. 160 la tarehe 19 Juni, 1970 ambapo alama za mipaka ziliwekwa ardhini. Kazi hiyo ilifanywa na wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Spika, uhakiki huo ulibainisha kuwa: (i) hifadhi ilikuwa imechukua baadhi ya maeneo ya Vijiji vya Mwikantsi (Hekta 1,014) na Sangaiwe, Kata ya Mwada (Hekta 536), hivyo maeneo haya yalirejeshwa kwa wananchi. (ii) wananchi pia, walichukua maeneo ya hifadhi katika Vijiji vya Ayamango (Hekta 2,986.3), Gedamar ( Hekta 2,185.1), Gijedabung (Hekta 1,328.2), Quash (Hekta 1,587.9) na Orng’andida (Hekta 930.6) ambavyo vimerejeshwa.

Mheshimiwa Spika, katika Vijiji vya Quash na Orng’ndida maeneo yaliyoangukia ndani ya mpaka wa hifadhi hayakuwa na watu, hivyo ilikuwa rahisi kuyarejesha hifadhini. Upande wa maeneo ya Vijiji vya Ayamango, Gedamar na Gijedabung uthamini wa mali za wananchi ambao walikuwa ndani ya mpaka wa hifadhi ulifanyika. Jumla ya kiasi cha shilingi za Kitanzania 175,050,924 zililipwa kwa wananchi hao kama fidia ya mali, posho ya usumbufu, posho ya makazi na posho ya usafiri kwa wote waliotakiwa kuhama. Malipo hayo ya fidia yalifanyika kama ilivyokuwa imepangwa na wananchi waliondoka ndani ya hifadhi.
MHE. MRISHO M. GAMBO Aliuliza: -

Serikali imeongeza viwango vya tozo za utalii kwa Hifadhi zilizo chini ya TANAPA kuanzia mwezi Julai, 2021.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kusitisha tozo hizo ili kutoa fursa kwa Sekta ya Utalii nchini ambayo imeathirika sana na ugonjwa wa Corona?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ongezeko la tozo limelenga Hifadhi za Taifa nne ambazo ni Ziwa Manyara, Serengeti, Tarangire na Arusha. Kiwango cha tozo kilichoongezeka kwa hifadhi husika ikilinganishwa na viwango vya sasa ni kama ifuatavyo: -

HIFADHI ENTRYFEE SEASONAL ANDSPECIALCAMPING FEE CONCESSIONFEE
Tozoya sasa Tozokuanzia 1/7/2021 Tozoyasasa Tozo kuanzia 1/7/2021 Tozoya sasa Tozo kuanzia 1/7/2021
Serengeti 60USD 70USD 50USD 60USD 50USD 60USD
Manyara 45USD 50USD 50USD 60USD 40USD 40USD
Tarangire 45USD 50USD 50USD 60USD 40USD 40USD
Arusha 45USD 50USD 50USD 60USD 40USD 40USD

Mheshimiwa Spika, wakati wafanyabiashara ya utalii wakiishinikiza Serikali kuacha tozo zikiwa za chini sana, wenyewe wamekua wakiwatoza watalii tozo za juu ambazo hawataki kuziweka wazi kwa Serikali. Usiri wa tozo za makampuni binafsi unainyima Serikali taarifa za msingi za kuweza kuona uzito wa hoja yao.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwamba suala la COVID-19 lisitumike kuinyima Serikali mapato ambayo yanasaidia kukuza uchumi wa nchi. Pia, nisisitize kwamba pamoja na shinikizo la kupunguza tozo, sekta binafsi haijawasilisha takwimu zozote Serikalini za kuthibitisha ongezeko la idadi ya wageni waliofuta safari zao kuja nchini kutokana na ongezeko la tozo.

MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi uliopo katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Pori la Akiba la Uwanda?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba Uwanda lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5,000 lilianzishwa mwaka 1959 na kutangazwa upya kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na.12 ya mwaka 1974 kwa Tangazo la Serikali Na. 275 la tarehe 8/11/1974. Tangu mwaka 1974 hadi 2013 pori hilo lilikuwa likisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na lilikabidhiwa rasmi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii tarehe 20/01/2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, pori hilo linapakana na vijiji 11 kama ifuatavyo; kuna Kijiji cha Ilambo, Kilyamatundu, Mkusi, Kapenta, Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta; na vijiji saba ambavyo ni Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta, ndivyo vyenye mgogoro na Pori la Akiba Uwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia mgogoro huo, orodha ya vijiji husika iliwasilishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Migogoro iliyojumuisha Wizara nane. Utekelezaji wa ripoti ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya Mawaziri nane, chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, utaleta ufumbuzi wa mgogoro huu na migogoro mingine kama huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, tunaomba Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, pamoja na Watanzania wote tuwe na subira wakati utekelezaji wa ufumbuzi wa migogoro hii unaratibiwa. Naomba kuwasilisha.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka miundombinu mizuri ya barabara katika Mbuga ya Ibanda na Rumanyika ili kuvutia watalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu kwa kuendelea kuniamini kuhudumia Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hifadhi za Taifa Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe zilianzishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 509 na 510 la tarehe 05/07/2019. Hifadhi hizo zilitokana na kupandishwa hadhi kwa yaliyokuwa Mapori ya Akiba Ibanda na Rumanyika Orugundu.

Mheshimiwa Spika, katika kuwezesha kufikika kwa hifadhi hizo, Serikali kupitia Taasisi za TANROADS na TARURA imekuwa ikitengeneza barabara mbalimbali zinazorahisisha kufika kwa watalii katika hifadhi hizo. Barabara hizo ni pamoja na Mgakorongo (Karagwe) hadi Murongo (Kyerwa) yenye urefu wa kilometa 112, ambayo inafanyiwa matengezo na TANROADS kila mwaka na imewekwa katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami katika Mwaka wa Fedha 2020/2021. Vilevile barabara ya Omushaka – Kaisho – Murongo yenye urefu wa kilometa 120 imekuwa ikifanyiwa matengenezo kila mwaka na TANROADS.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha uwepo wa miundombinu mizuri ya barabara ndani ya hifadhi, Serikali imetenga shilingi milioni 311.9 kwa mwaka wa fedha 2020/ 2021 kwa ajili ya kuchonga barabara yenye urefu wa kilometa 20 katika Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe. Vilevile, kwa mwaka 2021/2022, Serikali ina mpango wa kutengeneza barabara yenye urefu wa kilometa 51 katika Hifadhi ya Taifa Ibanda-Kyerwa; na barabara ya kilometa 20 katika Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe.

Mheshimiwa Spika, ni imani yetu kwamba jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara katika Hifadhi za Taifa Ibanda- Kyerwa na Rumanyika-Karagwe na maeneo mengine yote ya hifadhi zitasaidia kuweka mazingira mazuri ambayo yataziwezesha hifadhi hizo kutembelewa na watalii wengi waliopo katika maeneo ya karibu pamoja na wageni kutoka nchi jirani. Naomba kuwasilisha.
MHE. DANIEL A. TLEMAI Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Kata ya Mbulumbulu katika Kijiji cha Lositete?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mgogoro wa mpaka kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Kata ya Mbulumbulu katika Kijiji cha Lositete ulidumu kwa muda mrefu. Mgogoro huu ulitatuliwa kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali zikiwemo:-

(i) Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Karatu, Monduli na Ngorongoro;

(ii) Wataalam kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha; na

(iii) Wataalam kutoka Ofisi ya Katibu Tawala ya Wilaya za Karatu, Monduli na Ngorongoro; na Wahifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka hizi zote zilishiriki kutafsiri GN iliyoanzisha mipaka ya maeneo hayo kisheria.

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Lositete kiko katika Wilaya ya Karatu na sio Wilaya ya Ngorongoro ambapo wananchi wa kutoka kijiji hicho walivamia eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na taratibu za kuwaondoa zilifanyika na kuwarudisha katika maeneo yao. Pamoja na kuwa Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro inaruhusu matumizi mseto, sheria hii iliwekwa kwa ajili ya wenyeji waliomo ndani ya hifadhi. Aidha, ndani ya hifadhi pia kuna maeneo ambayo yanasimamiwa Serikali ili kulinda uoto wa asili likiwemo eneo hili.

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa msisitizo kwa jamii zote zinazozunguka mipaka ya hifadhi kuheshimu maeneo yote yaliyohifadhiwa kwa faida ya jamii na maslahi ya Taifa kwa ujumla. Ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaondoa wanyama wakali hasa tembo katika Tarafa ya Mlali na kuwarudisha kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa kuwa wamekuwa kero kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pole kwa wananchi wote wanaokutana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo. Wizara imeendelea kudhibiti wanyamapori hawa katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kukabiliana na matukio haya, Wizara kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa iliweka mkakati wa pamoja ambapo kutakuwa na vikosi maalum vya kudhibiti tembo. Vikosi hivyo vimeendelea kutoa msaada wa haraka pale inapotokea tatizo katika Mkoa wa Morogoro na maeneo mengine ikiwemo Wilaya ya Mvomero. Vikosi hivyo vimewezeshwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu vinavyohitajika katika zoezi la kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Vifaa hivyo ni pamoja na magari, risasi za moto, risasi baridi na mabomu maalum ya kufukuzia wanyamapori hususan tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na jitihada hizo, Wizara imenunua na kusambaza simu zenye namba maalum katika maeneo 14 nchini kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanatoa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, kwa haraka bila malipo na kwa wakati ili ziweze kushughulikiwa mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa eneo la Hifadhi ya Bonde la Wembere kwa Wananchi wa Igunga kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo na ufugaji ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo kwa kuwa Bonde hilo limepoteza sifa ya kuwa Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Jimbo la Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Bonde la Wembere ni ardhi oevu inayofahamika Kitaifa na Kimataifa kwa kuhifadhi ndege wa aina mbalimbali ambao huishi na kuzaliana kwa wingi. Eneo hili ni dakio na chujio la maji ya Ziwa Kitangiri na Eyasi, pia ni mapito, mazalia na malisho ya wanyamapori linalounganisha mifumo ya ikolojia ya ukanda wa Kaskazini, Kati, Magharibi na Kusini mwa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na umuhimu wa eneo hilo, wananchi wameendelea kuvamia eneo la ardhi oevu la Wembere kwa ajili ya shughuli za kilimo, malisho na ukataji miti. Hali hiyo inasababisha mwingiliano wa shughuli hizo na kusababisha migogoro kati ya wakulima, wafugaji na wahifadhi. Pamoja na uvamizi huo, eneo hilo bado lina umuhimu katika shughuli za uhifadhi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa eneo hili la ardhi oevu la Bonde la Wembere na kwa kuzingatia kuwa ni chanzo muhimu cha maji kwa wananchi wa mikoa ya Tabora, Singida na Simiyu, Serikali itafanya tathmini na kutambua mipaka ya ardhi oevu kwa njia shirikishi ya wananchi na Serikali. Na lengo ni kupanga matumizi ya ardhi kwa vijiji vinavyopakana na eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kutoa ushirikiano kwa Serikali na wananchi katika kushughulikia suala hili ili kupata suluhisho la kudumu. Naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum Iringa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) tayari umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2017. Mradi huu unatekelezwa kwa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 150 kutoka Benki ya Dunia katika maeneo ya kipaumbele zikiwemo Hifadhi nne za Taifa ambazo ni Hifadhi ya Taifa Ruaha, Mikumi, Nyerere, Milima Udzungwa na maeneo yanayozunguka hifadhi hizo pamoja na eneo la chanzo cha maji cha Mto Great Ruaha. Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka 2017 - 2023.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2021, mradi huu umeendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa ambapo kazi zifuatazo zimetekelezwa: ununuzi wa vifaa vya doria vimeshanunuliwa, magari 44 yameshanunuliwa, mitambo mikubwa mitatu kati ya 18 inayotarajiwa kununuliwa, pia mradi umeajiri kampuni sita ambazo zinaendelea na usanifu wa majengo, barabara na viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali kama vile majadiliano ya utekelezaji wa mradi huu katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, mradi ulichelewa kuanza utekelezaji wake kwa takribani miezi 17.

Aidha, uwepo wa ugonjwa wa Covid – 19 umechangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuchelewesha utekelezaji wa mradi huu. Kutokana na kazi nyingi kusimama, mradi huu sasa umeshaanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto zote ambazo zilijitokeza, mradi umefanyiwa mapitio ya kati ambapo miongoni mwa mambo mengine ni kuongeza muda wa utekelezaji wa mradi huu hadi mwaka 2025 ili kufidia muda uliopotea.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mikakati gani wa kumaliza mgogoro kati ya Hifadhi ya Ruaha na Wakulima na Wafugaji wanaozunguka Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali iliunda Kamati iliyojumuisha Mawaziri kutoka Wizara nane kwa ajili ya kufuatilia na kutatua migogoro ya ardhi nchini. Migogoro hiyo iliyofanyiwa kazi na Kamati husika ni pamoja na migogoro kati ya wakulima na wafugaji wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Mheshimiwa Spika, Kamati hiyo imefanya tathmini ya migogoro hiyo na kutoa mapendekezo ambayo yameshatolewa maamuzi na Baraza la Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji utakaoanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine na wananchi ambao maeneo yao yana changamoto za migogoro hiyo kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:-

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ili ifahamike kwa Watalii wa ndani na nje?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ilianzishwa kwa GN Na. 279 ya mwaka 2005. Hifadhi hii ina sifa ya kipekee kwa kuwa na jamii mbalimbali za maua na kwa nyakati tofauti Serikali imeendelea kuitangaza hifadhi hii na nyingine ziilizopo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati iliyopo kwa sasa ni kuendelea kuzitangaza hifadhi zote za Taifa ndani na nje ya nchi ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Kitulo. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuzitangaza Hifadhi za Taifa kupitia tovuti na mitandao ya Kijamii (Instagram, Facebook na Twitter) pamoja na kuandaa video na filamu mbalimbali na vilevile kuna kuimarisha miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi ili kurahisisha kufikika kwa maeneo ya vivutio ndani ya hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati mwingine ni kuzitangaza hifadhi hizi kupitia chaneli maalum ya “Tanzania Safari Channel”; vile vile kuandaa safari za mafunzo kwa wanahabari, mawakala na wadau mbalimbali wa utalii kwa lengo la kuwapa fursa ya kuvielewa vivutio vya utalii na kuvitangaza ndani na nje ya nchi; kujenga sehemu ya malazi ya bei nafuu kwa ajili ya wageni wa ndani na nje ya nchi; na mkakati mwingine ni kuvutia wawekezaji kujenga kambi za watalii au lodge zenye hadhi za Kimataifa, ambapo maeneo manne ya uwekezaji yamebainishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kuona umuhimu wa maeneo ya uhifadhi, bajeti ya mwaka 2021/2022 pamoja na masuala mengine, imezingatia uimarishaji wa utangazaji wa utalii na kuboresha miundombinu ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na maeneo ya malazi ya wageni ili kuvutia watalii kutembelea maeneo hayo kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha Mifuko ya Kuendeleza Utalii na Wanyamapori na kufikia lengo la watalii milioni tano ifikapo 2025?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii (TDL) ulianzishwa kwa Sheria ya Utalii Na. 29 ya Mwaka 2008, Kifungu cha 59(2). Lengo la Tozo hiyo ni kuendeleza mazao ya utalii; kudhibiti ubora wa huduma za biashara za utalii; kukuza na kutangaza vivutio vya utalii; kujenga uwezo katika sekta ya utalii; na kuwezesha tafiti na shughuli nyingine yoyote kwa ajili ya maendeleo na kuboresha sekta ya utalii.
Kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020, vyanzo vya tozo hii kwa sasa vinakusanywa na Wizara kwa kushirikiana na TRA na makusanyo hayo huingizwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wanyamapori, upo Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania ambao ulianzishwa kwa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura 283, Kifungu cha 91(2). Mfuko huo unawezesha shughuli za kuhifadhi wanyamapori ndani na nje ya maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wanyamapori wanaendelea kulindwa na kusimamiwa kwa ajili ya kuendeleza utalii nchini, mifuko ya utalii na wanyamapori imekuwa ikiwezeshwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Pamoja na vyanzo vya mapato vya mifuko hii kukusanywa na kupelekwa kwenye Mfuko Mkuu (Hazina), Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga fedha kupitia bajeti kuu ya Serikali kwa ajili ya kutekeleza kazi za mifuko husika. Hivyo, kazi zilizokuwa zinafanywa na mifuko hii sasa zitatekelezwa kupitia bajeti kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italiangalia zao la asali na kulitafutia soko la uhakika ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, asali ni mojawapo ya mazao yanayozalishwa na nyuki, mazao mengine ni pamoja na nta, gundi ya nyuki, sumu ya nyuki, chavua na maziwa ya nyuki. Wizara imeendelea na jitihada za kutangaza mazao ya nyuki ya Tanzania kwa kushirikiana na TANTRADE kwenye mikutano mbalimbali ya kibiashara, maonyesho, warsha na makongamano yanayofanyika ndani na nje ya nchi pamoja na Balozi zetu zilizopo katika nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa uzalishaji wa asili nchini ni wastani wa tani 30,400; sehemu kubwa ya asali hiyo zaidi ya asilimia 95 huuzwa katika soko la hapa nchini na asilimia tano huuzwa kwenye soko la nje kwenye nchi za Rwanda, Kenya, Burundi, Umoja wa Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ukarabati pamoja na ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki katika Mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma na Geita ambavyo vitatumika kama soko la mazao ya nyuki. Serikali pia imeweka mfumo wa ufuatiliaji wa mazao ya nyuki katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao hayo kwa lengo la kuthibiti viwango vya ubora wa mazao ya nyuki pamoja na kufufua, kuendeleza na kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika wa ufugaji nyuki ili kuunganisha nguvu za uzalishaji pamoja na soko la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa soko la mazao ya nyuki kupitia mradi mpya wa kusaidia mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki utakaotekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022. Naomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-

Je, ni kwa nini Serikali haitumii risiti za kielektroniki inapotoza faini za kuingiza mifugo kwenye Hifadhi zilizopo Sikonge?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu ya Sheria ya Wanyamapori Na.5 ya Mwaka 2009, ni kosa kwa mtu yeyote akiwemo mfugaji kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa. Serikali iliweka sheria hii sio kwa ajili ya kujipatia mapato bali kudhibiti uharibifu ikiwemo uvamizi, ujangili na uingizaji wa mifugo ndani ya maeneo hayo kwa lengo la kuyatunza.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kudhibiti upotevu wa mapato, Serikali ilianzisha mfumo wa TEHAMA kwa ajili ya utoaji wa leseni au vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato ya vyanzo mbalimbali vya Sekta ya Maliasili na Utalii unaoitwa MNRT Portal ambao umefungamanishwa na Mfumo wa Government electronic Payment Gateway yaani GePG kwa ajili ya kutoa Control Number inayomwezesha mteja sasa yeyote yule kulipa. Aidha, baada ya kufanya malipo hayo mfumo wa MNRT Portal unatoa risiti ambazo zinatambulika na Mamlaka ya Mapato Tanzania yaani TRA.

Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa risiti zinazotolewa na mfumo huu ni halali kwa malipo ya Serikali sawa na zinazotolewa na mfumo wa Electronic Fiscal Devices yaani EFDs.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Sehemu kubwa iliyokuwa ikitumika kwa shughuli za uchumi katika Wilaya ya Malinyi imetwaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mwaka 2017 ambapo waliweka mipaka maarufu kama “TUTA LA 2017” bila kushirikisha wananchi.

Je, Serikali haioni haja ya kurejea na kufanya upya mapitio shirikishi ya mipaka ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo yanayozungumziwa na Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero lililoanzishwa mwaka 1952 na kuhuishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 269 la mwaka 1974 likiwa na ukubwa wa Kilomita za mraba 6,500. Eneo hilo vile vile ni sehemu ya ardhi oevu yenye umuhimu kitaifa na kimataifa kutokana na kuhifadhi bioanuai mbalimbali na zilizo adimu duniani kama vile mnyama aina ya Puku. Aidha, Bonde hilo huchangia takriban asilimia 62.5 ya maji yote ya Mto Rufiji na hivyo kuwa chanzo muhimu cha maji kwa mradi tarajali wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere.

Mheshimiwa Spika, aidha tuta linalozungumziwa liliwekwa mwaka 2012 hadi 2013 kwa lengo la kuokoa kiini cha Bonde la Mto Kilombero kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira uliokuwa unaendelea.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2017 ilifanya mapitio ya mipaka ikiwa ni hatua mojawapo ya kuangalia uwezekano wa kurekebisha mipaka (GN) ili iendane na hali halisi kwani kwa asilimia kubwa eneo la hifadhi lilikuwa limeathiriwa na shughuli za kilimo na ufugaji. Suala hili lilipelekwa kwenye Kamati ya Mawaziri Nane iliyoundwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano. Utekelezaji wa mapendekezo hayo umeshafanyika na muda si mrefu wananchi watajulishwa maamuzi ya Kamati hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Wilaya ya Malinyi waendelee kuwa na subira wakati utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri ukiendelea kufanyiwa kazi, naomba kuwasilisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-

Wananchi wanaoishi jirani na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Wilayani Karatu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata adha kubwa ya wanyama kuingia na kuvamia mashamba yao na wakati mwingine kujeruhi wananchi:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo na ufugaji kwenye shoroba za wanyama, maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na maeneo ya kinga ya Hifadhi ya Ngorongoro, kumekuwepo na changamoto ya wanyamapori kuingia kwenye mashamba yaliyopo pembezoni mwa hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto hii, Wizara inatoa rai kwa wananchi kutumia mbinu mbadala za kuepuka wanyamapori wakali na waharibifu kuingia kwenye maeneo yao. Mbinu hizo ni pamoja na kwanza, ni kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki kwenye mipaka ya Hifadhi zilizo karibu na maeneo ya vijiji ili kuhakikisha kuwa wanyamapori hawavuki kwenda kwenye mashamba hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbinu nyingine ni wananchi wanahamasishwa kulima zao la pilipili kandokando ya mashamba yao, kwani zao hili limeonekana kuwa ni tishio kwa wanyama wakali na waharibifu kama tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbinu nyingine ni wananchi wanashauriwa kutopanda mazao yanayovutia tembo kusogea katika mashamba yao kama vile mazao yanayohusiana na katani, miwa, ndizi na matikiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wananchi kuendelea kutumia oil chafu iliyochanganywa na pilipili na majivu ili kuzuia wanyama kama tembo kusogea kwenye maeneo ya mashamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni wananchi wanashauriwa sasa kutoa taarifa haraka pindi wanyama hao wanapoonekana kukaribia kwenye maeneo ya mashamba.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za kuongezeka kwa matukio mbalimbali ya wanyama wakali wakiwemo tembo, Wizara imeongeza idadi ya vituo vya muda na vya kudumu vya askari katika maeneo yaliyohifadhiwa likiwemo eneo la Ngorongoro (Wilaya ya Karatu) na kuendelea na doria za usiku kuhakikisha wanyamapori waharibifu wanarudishwa hifadhini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi pamoja na mali zao wanakuwa salama kwani wanyamapori wamekuwa wakiingia na kufanya uharibifu kwenye vijiji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba kutoa pole kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mikumi kwa kadhia hiyo ya kupambana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vinavyozunguka hifadhi za wanyamapori nchini vinakabiliwa na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kama vile tembo, simba, fisi, nyati, viboko na mamba. Pamoja na mambo mengine, hali hii hii inasababishwa na kuvamiwa kwa maeneo ya kinga (buffer zone) na mapito ya wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu, Serikali imeunda kikosi maalum ambacho kimekuwa kikishirikiana na wadau mbalimbali kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yanayozunguka hifadhi kwa kadri taarifa za matukio zinavyopatikana. Aidha, Serikali imeandaa mpango mkakati wa kitaifa wa kushughulikia wanyamapori wakali na waharibifu unaotoa mwongozo wa namna nzuri ya kuwawezesha wananchi kutumia maeneo yao bila kuathiriwa na uwepo wa wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa hifadhi kuhusu mbinu bora za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu. Mafunzo haya ni endelevu na yatafanyika katika maeneo yote yenye changamoto hapa nchini. Pili, kuimarisha vikosi vya doria za kudhibiti wanyamapori vikiwemo vitendea kazi ili viweze kufanya doria ipasavyo. Tatu, kushirikiana na Halmashauri za wilaya na vijiji, ili kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe rai kwa wananchi wa Mikumi na maeneo mengine yanayozunguka hifadhi waendelee kutoa ushirikiano na kuendelea kufuata maelekezo ya wataalam wa wanyamapori kwa kutekeleza mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori hao ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-

Je, ni upi mpaka sahihi wa Bonde la Kilombero kati ya mpaka uliowekwa mwaka 2012 na ule uliowekwa mwaka 2017?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Pori Tengefu la Kilombero (Kilombero Game Controlled Area) lilianzishwa kupitia Tangazo la Serikali (GN) Na. 107 chini ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori na Mimea (Fauna and Flora Ordinance) ya Mwaka 1951 iliyoanza kutumika mwaka 1952. Baada ya kurejea mwaka 1974, Pori Tengefu la Kilombero lilitambulika kwa GN. Na. 269 ya mwaka 1974 iliyohuishwa kwa GN. Na. 459 ya Mwaka 1997 chini ya Sheria ya Wanyamapori Na. 12 ya mwaka 1974 lilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 6,500. Pori hilo ni sehemu ya ardhioevu ya Bonde la Kilombero lenye ukubwa wa kilometa za mraba 7,950. Aidha, bonde hilo linachangia takriban asilimia 62.5 ya maji yote ya Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pori Tengefu Kilombero halijawahi kubadilishwa mipaka yake. Hata hivyo, mwaka 2012 na 2017 iliwekwa alama kwa ajili ya kuokoa kiini cha Mto Kilombero. Aidha, Serikali iliunda Kamati ya Mawaziri Nane (8) kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi ya maeneo yaliyohifadhiwa na watumiaji wengine wa ardhi likiwemo Bonde hilo la Mto Kilombero. Kamati hii ilitoa mapendekezo ambayo yalijadiliwa kwenye Baraza la Mawaziri na maamuzi yake yamekwishafanyika na utekelezaji wake utatolewa hivi karibuni.
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa Wananchi wa Bugeli na Hifadhi ya Manyara pamoja na mauaji ya Wananchi yanayotokea mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bugeli, hasa wafugaji wanapoingiza mifugo hifadhini na kukamatwa na Askari wa Hifadhi, wamekuwa na tabia ya kukataa kutii sheria bila shuruti na kupiga yowe maalum ijulikanayo kama “hayodaa” ikiwa ni kiashiria cha hatari kubwa kwa kabila la Kiiraki. Hivyo, baada ya yowe hiyo kupigwa, wananchi wengi hupata morali na kujitokeza wakiwa na silaha za jadi zikiwemo fimbo, mishale, mapanga na mikuki ili kupinga ukamataji huo wa mifugo na kuchukua mifugo yao kwa kutumia nguvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kumekuwepo na baadhi ya matukio ya Askari kunyang’anywa silaha au mifugo iliyokamatwa hifadhini na wananchi ambapo husababisha kutokuelewana kati ya Askari wa Hifadhi na wananchi. Pamoja na taharuki hizo, kumekuwepo pia na mauaji ya Askari wapatao wawili na majeruhi kwa Askari watatu katika eneo hilo. Aidha, matukio kama haya yamekuwa yakijitokeza katika maeneo mengine yanayozunguka hifadhi mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiunda Kamati mbalimbali kuchunguza matukio hayo ili kubaini chanzo cha changamoto hizo. Kwa ujumla, imebainika kuwa tatizo kubwa ni wananchi kutoheshimu makubaliano ambayo yamekuwa yakifanywa mara kwa mara kati ya Uongozi wa Wilaya, Hifadhi, Serikali ya Kijiji na wananchi kuhusu taratibu za kufuatwa na wananchi hao pindi wao wenyewe au mifugo yao inapokamatwa ndani ya hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kwa dhati kuleta mahusiano mazuri kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi kwa kuchukua hatua mbalimbali, zikiwemo kufanya vikao vya kutafuta suluhu pamoja na kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo husika. Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakiki mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na kuandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwa Kijiji cha Bugeli. Utekelezaji wake kwa sasa upo katika hatua za kukabidhi hati kwa wananchi wa kijiji husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa rai kwa wananchi wanaopakana na maeneo yaliyohifadhiwa kuepuka uvunjifu wa sheria za nchi na za uhifadhi na hivyo kudumisha amani kwa jamii husika na Taifa kwa ujumla.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Katavi ili iweze kupata watalii wengi na kuongeza mapato. Aidha, Hifadhi ya Taifa Katavi imekuwa ikitangazwa kupitia vyombo vya habari vilivyopo ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Katavi iliandaa Mpango Mkakati wa Kukuza Utalii kwa Mkoa wa Katavi mwaka 2019 ambao umesaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza Hifadhi ya hiyo na mikakati mingine inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na Kuvitangaza vivutio vilivyomo ndani ya hifadhi ikiwa ni pamoja na wingi wa Viboko, Simba na Twiga weupe. Vilevile Wizara ina mkakati wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa Katavi kupitia tovuti na mitandao ya Kijamii yaani Instagram, Facebook na Twitter lakini pia kuimarisha miundombinu ya barabara ndani ya Hifadhi husika ili kurahisisha kufikika kwa maeneo ya vivutio ndani ya Hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuitangaza Hifadhi hii kupitia chaneli maalum ya Tanzania Safari Channel, lakini pia kusimika mabango kwenye mikoa ya jirani kama vile Mbeya, Songwe, Tabora na Kigoma. Serikali pia inaandaa safari za mafunzo kwa wanahabari, mawakala na wadau mbalimbali wa utalii kwa lengo la kuwapa fursa ya kuvielewa vivutio vya utalii na kuvitangaza ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mwingine ni pamoja na kujenga sehemu ya malazi ya bei nafuu kwa ajili ya wageni wa ndani na nje ya nchi, na pia kuandaa video au filamu na machapisho mbalimbali na kuyasambaza kwa wananchi na mabasi ili kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Katavi;

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuzitangaza Hifadhi za Taifa kupitia maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ili kuwezesha kupata wawekezaji na watalii. Ni imani ya Serikali kwamba jitihada zinazoendelea kufanywa za kutangaza vivutio hivyo katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi zitaendelea kuzaa matunda na hivyo kuwapatia wananchi wa Katavi na Taifa kwa ujumla manufaa stahiki.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya Hifadhi ya Lwafi iliyopo Nkasi Kusini na wananchi wa Vijiji vya Mlambo, King’ombe, Tundu na Kata ya Wampembe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Lwafi liliwahi kuwa na mgogoro wa Kijiji cha King’ombe ambapo baadhi ya wananchi wake walivamia eneo la hifadhi kwa ajili ya shughuli za kilimo. Hata hivyo, mgogoro huo ulitatuliwa na Serikali baada ya kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo wananchi kupewa elimu na kuonyeshwa mipaka halisi.

Mheshimiwa Spika, aidha, mgogoro huo ulikwisha, lakini kuna mgogoro mwingine kwa sasa ambao ni kati ya Msitu wa Hifadhi ya Loasi yaani Loasi River Forest Reserve na Vijiji vya Mlambo, King’ombe na Tundu, ambapo wananchi walivamia msitu huo kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo. Serikali imefanyia kazi mgogoro huo kupitia mapendekezo ya Kamati ya Mawaziri Nane ambapo maamuzi ya mgogoro huo yameshatolewa na utekelezaji wake utafanyika katika bajeti ya mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wanaozunguka eneo hilo kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhimiza, kulinda na kutatua migogoro hiyo inayohatarisha uwepo wa maliasili zinazowazunguka.
MHE. JOSEPH A. TADAYO K.n.y. MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Idadi ya watu wa Same imekuwa ikiongezeka tangu tupate Uhuru na mpaka wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi upo kilometa tatu kutoka Same Mjini. Wanyamapori na hasa tembo wameonekana Same Mjini mara nyingi.

Je, ni lini Serikali itafikiria kuweka upya mipaka mipya ya hifadhi ili kutoa maeneo kwa ajili ya makazi ya watu na shughuli nyingine za kijamii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Makao Makuu ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi yapo eneo la Zange lililopo umbali wa kilometa sita kutoka Same Mjini. Wanyamapori hususan tembo wanaoonekana karibu na Mji wa Same mara nyingi ni wale wanaotoka katika maeneo ya Ruvu na Simanjiro kuelekea Hifadhi ya Taifa Mkomazi na wale wanaotoka katika Hifadhi ya Taifa Tsavo West nchini Kenya kupitia Ziwa Jipe na Kijiji cha Toloha katika Wilaya ya Same. Ikumbukwe pia kuwa maeneo mengi ambayo wananchi wanaishi kwa sasa yalikuwa yanatumiwa na wanyamapori kama mapito (shoroba) kuelekea maeneo ya Ruvu na Simanjiro.

Mheshimiwa Spika, kuendelea kumega eneo la hifadhi kwa kuweka mpaka mpya wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi siyo suluhu ya mgogoro huo kwa sababu eneo hilo litaendelea kuwa makazi na mapito ya wanyamapori. Hata hivyo, katika kudhibiti wanyamapori hao, Serikali itaendelea kuimarisha mikakati inayotumika ambayo ni pamoja na kuendelea kutoa mafunzo kwa wananchi ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo mafunzo hayo yanaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Pia kuimarisha, kuendeleza tafiti na kutumia mbinu mbalimbali za udhibiti na ufuatiliaji wa tembo. Mbinu hizo ni pamoja na mikanda ya elektroniki (collaring) kwa ajili ya kufuatilia makundi ya tembo ambayo ni korofi na kufundisha na kuviwezesha vikundi vya wananchi kwa ajili ya kufuatilia maeneo walipo tembo.

Mheshimiwa Spika, pia matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani, matumizi ya pilipili, matumizi ya mizinga ya nyuki na matumizi ya vilipuzi na vifaa vyenye mwanga mkali; lakini pia kutengeneza minara ya kuangalia mbali katika maeneo yanakabiliwa na changamoto ya tembo kuingia. La mwisho ni kuhamasisha wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanyamapori ikiwemo tembo wanapoonekana kwenye maeneo ya makazi au mashamba.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa wananchi wote wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Mkomazi waendelee kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa pamoja na kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto za wanyamapori wakiwemo tembo pindi zinapojitokeza katika maeneo ya makazi ya watu na shughuli nyingine za kijamii.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imekumbwa na wimbi kubwa la uvamizi wa wanyamapori kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba la Maswa na Hifadhi ya Wanyamapori Makao na kusababisha uharibifu wa mazao na kutishia usalama wa watu.

(a) Je, ni lini Serikali itashughulikia tatizo la uhaba wa watumishi wa Idara ya Wanyamapori?

(b) Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vikiwemo gari na silaha?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu Swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu lenye sehemu
(a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Maswa lililopo Mkoani Simiyu katika Wilaya za Bariadi, Meatu na Itilima limepakana na vijiji 32 ambapo vijiji 18 vipo katika Wilaya ya Meatu. Pori hilo lina ukubwa wa kilometa za mraba 274 na lilianzishwa mwaka 1974 kwa Tangazo la Serikali Na. 275. Mwaka 2016 usimamizi wa pori hilo ulihamishwa kutoka Idara ya Wanyamapori kwenda Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na wakati huo kulikuwa na watumishi 62.

Mheshimiwa Spika, kwa vipindi tofauti TAWA imechukua hatua za kuongeza watumishi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa eneo hilo. Hadi kufikia Januari, 2021 pori hilo lina watumishi 87 sawa na ongezeko la asilimia 40 kutoka watumishi waliokuwepo mwaka 2016. Serikali inaendelea kuziba mapengo ya idadi ya watumishi kwa kadri ya upatikanaji wa vibali vya kuajiri watumishi. Vilevile Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kujenga uwezo wa Halmashauri kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ukosefu wa vitendea kazi, Wizara itaendelea kutenga fedha za ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo magari na silaha ili kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba la Maswa.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza:-

Sehemu kubwa ya maeneo ya Kilimo cha Mpunga Malinyi imemegwa na Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) kwa Mipaka mipya iliyowekwa Mwaka 2017 bila maridhiano na Wananchi wa sehemu ya bonde la Kilombero. Je, Serikali haioni kuwa ni vema kufanya upya mapitio shirikishi kwenye mipaka ya eneo la Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la Bonde la Kilombero ni sehemu ya ardhioevu yenye umuhimu kitaifa na kimataifa kutokana na kuhifadhi bioanuai mbalimbali na zilizo adimu duniani kama vile mnyama aina ya sheshe. Aidha, Bonde hilo huchangia takriban asilimia 62.5 ya maji yote ya Mto Rufiji na hivyo kuwa chanzo muhimu cha maji kwa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere.

Mheshimiwa Spika, uwekaji wa mipaka wa Bonde la Kilombero ulizingatia mfumo halisi wa kiikolojia wa Bonde hilo, ili uweze kukidhi matarajio ya uhifadhi wa ardhioevu. Hivyo basi, Pori Tengefu Kilombero lilianzishwa mwaka 1952 kwa GN. Na. 107/1952 na halijawahi kubadilishwa mipaka yake. Naomba kuwasilisha.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa wananchi maeneo ya Hifadhi ya Kitulo ambayo hayatumiki ili wayatumie kulisha mifugo yao hususani eneo la Kwipanya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Kitulo ilianzishwa kwa GN. Na.279 ya mwaka 2005. Maeneo yote yaliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Kitulo likiwemo eneo la Kwipanya yamehifadhiwa kisheria kulingana na umuhimu wake kiikolojia, kijamii, kitamaduni na kiuchumi. Miongoni mwa sababu zilizopelekea Serikali kuanzisha Hifadhi hii ni pamoja na:-

(i) Kuhifadhi vyanzo vya maji ambavyo vinatoa maji yanayoenda kwenye Bonde la Ziwa Nyasa na Bonde la Mto Rufiji ambapo kwa sasa maji hayo yanachangia kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Maji uliopo katika Bwawa la Julius Nyerere pamoja na Bwawa la kufua umeme wa maji la Mtera;

(ii) Eneo hili linahifadhi uoto adimu wa asili wa misitu na maua uliopo katika eneo husika;

(iii) Kutunza makazi ya wanyama adimu duniani kama vile Kipunji na Minde; na

(iv) Pamoja na kuhifadhi mandhari ya asili ya milima kwa ajili ya shughuli za utalii.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhifadhi eneo hili la Taifa la Kitulo kutokana na umuhimu wake. Ahsante.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaruhusu tena usafirishaji wa vipepeo nje ya nchi ili kuongeza vipato vya wananchi wa Muheza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwin’juma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 17/03/2016, Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi. Tatizo kubwa lililosababisha maamuzi hayo lilikuwa ni ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za kufanya biashara hiyo, ikiwa ni pamoja na kutokea wimbi kubwa la utoroshaji wa wanyamapori hai. Vilevile Serikali iligundua matokeo hasi yanayoendelea kujitokeza kwa kuendelea kufanya biashara hiyo ikiwemo kuhamisha rasilimali ya wanyamapori nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali inafanya tathmini ya kina ili kubaini faida na hasara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi kwa ajili ya kujiridhisha na biashara hiyo. Baada ya tathmini hiyo Serikali itatoa tamko kwa wadau wa biashara hiyo kuhusu uamuzi uliofikiwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itazalisha mbegu za mti wa mninga ili wananchi waweze kupanda na kuzalisha miti hiyo kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umaarufu wa mti wa mninga katika matumizi ya shughuli za ujenzi na utengenezaji wa samani. Kutokana na umuhimu huo, Wizara kupitia TFS imeandaa mpango wa miaka mitano wa kuendeleza mti huo na miti mingine kibiashara kwa kuipanda kama ilivyo miti ya kigeni. Mpango huo unahusisha aina 56 za miti ya asili ikiwemo mninga ambapo kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Wizara imetenga shilingi 60,000,000 kwa ajili ya kuzalisha mbegu za miti hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Wizara ni kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu za miti ya asili ili wananchi waweze kuzipata kwa urahisi kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania zilizopo kwenye kanda mbalimbali hapa nchini. Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha elimu ya upandaji wa mti wa mninga ili kuleta hamasa ya kupanda na kutunza miti hiyo. Serikali itahakikisha elimu ya utunzaji na uendelezaji wa miti ya mninga iliyopo katika maeneo ya mashamba ya wananchi inatolewa ili miti hiyo itunzwe kwa ajili ya kuzalisha mbegu ili kuwezesha wananchi kupanda miti ya mninga kibiashara.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na baadhi ya askari wa TANAPA wanaolinda Hifadhi ya Msitu wa Marang inayopakana na Kata ya Buger Wilayani Karatu kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wananchi wanaoingia kwenye hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, baadhi ya wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Msitu wa Marang, hasa wafugaji wanapoingiza mifugo yao hifadhini na kukamatwa na askari wa hifadhi, hukataa kutii sheria bila shuruti na kupiga yowe maalum ijulikanayo kama HAYODAA ikiwa ni kiashiria cha hatari kwa kabila la Wairaki. Hivyo, wananchi wengi hujitokeza wakiwa na silaha za jadi zikiwemo fimbo, mishale, mapanga na mikuki ili kuwadhuru askari wa hifadhi na kupinga ukamataji huo wa mifugo na kuchukua mifugo yao kwa kutumia nguvu.

Mheshimiwa Spika, yamefanyika matukio mengi ya askari kunyang’anywa silaha au mifugo iliyokamatwa hifadhini na wananchi ambapo husababisha kutokuelewana kati ya askari wa hifadhi na wananchi. Kati ya mwaka 2013 hadi 2020 jumla ya matukio saba yalitokea ambayo yalihusisha wananchi kuwashambulia askari wa hifadhi, kuwajeruhi na wengine kupoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau pamoja na wananchi wa maeneo hayo imeandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ambapo kwa sasa hati zinaandaliwa na baada ya uhakiki wananchi watakabidhiwa hati hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakarabati boma la kihistoria la Mjerumani lililopo Wilayani Mkalama ili liendelee kuweka historia na kumbukumbu kwa vizazi vijavyo na kuzalisha mapato kwa Serikali?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008, watu binafsi, Taasisi za Umma na Taasisi za Kidini, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinaruhusiwa kuhifadhi, kuendeleza na kunufaika na urithi wa malikale.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mambo ya Kale Sura 333 kifungu cha 16 kinazipa mamlaka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutunga sheria ndogo ndogo za kutunza na kuhifadhi maeneo ya malikale katika maeneo yao. Boma la kihistoria lililopo Wilaya ya Mkalama linasimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. Hivyo, tunaishauri Halmashauri husika kulikarabati na kulihifadhi ili kiwe chanzo cha mapato na Halmashauri iweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, Wizara iko tayari kutoa ushirikiano na miongozo ya namna ya kulikarabati na kulihifadhi boma hilo la kihistoria lililopo Mkalama ili kulindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mambo ya Kale. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: -

Hifadhi ya Taifa Mkomazi imebana sana maeneo ya wananchi na kusababisha kazi za kijamii katika Kata za Lunguza, Mng’aro na Mnazi kushindwa kufanyika: -

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kupunguza sehemu ya Hifadhi ya Mkomazi na kugawa kwa Serikali za Vijiji?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetokana na kupandishwa hadhi kwa lililokuwa Pori la Akiba la Mkomazi kupitia Tangazo la Serikali Namba 27 la mwaka 2008.

Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi hii ni sehemu ya mfumo wa ikolojia wa Tsavo-Mkomazi wenye wanyamapori wengi. Vilevile, ni maeneo ya mtawanyiko na shoroba za wanyamapori na tayari kumekuwa na changamoto nyingi za shughuli za binadamu katika maeneo hayo ambazo zimesababisha kuwepo na migongano kati ya wanyamapori wakali na waharibifu yaani tembo na wananchi wanaozunguka maeneo hayo ya hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Serikali haina mpango wa kumega eneo hilo kwani kuendelea kumega eneo hilo ni kuendeleza migongano kati ya binadamu na wanyamapori waharibifu kama tembo. Ahsante.
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvuna mamba katika Mto Ruvu hasa katika Vijiji vya Kigamila, Bwila juu, Magogoni, Bwila chini, Kongwa, Tulo, Lukuhinge, Kata za Mvuha na Serembala katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mamba hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya mamba katika mito iliyopo katika Mikoa ya Katavi, Rukwa na Morogoro. Baada ya tathmini hiyo kukamilika na kubainika kuwa idadi ya mamba waliopo ni kubwa, mamba hao watavunwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, endapo itabainika kuwa idadi ya mamba katika maeneo husika ni ndogo, Serikali itabaini mamba wanaosababisha adha kwa wananchi na kuwavuna ili wasiendelee kuleta madhara makubwa kwa wananchi. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Utalii Nyanda za Juu Kusini katika eneo la Kihesa – Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iko kwenye hatua za awali za ujenzi wa jengo la kituo cha utalii katika eneo la Kihesa -Kilolo Mkoani Iringa, kupitia mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania - REGROW. Hadi kufikia mwezi Julai, 2021, Wizara imeajiri Mshauri Mwelekezi ambaye anaendelea na kazi ya kutengeneza Mpango wa Biashara na upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa awali wa kituo hicho. Aidha, Mshauri Mwelekezi ameshawasilisha taarifa ya awali.

Mheshimiwa Spika, lengo la kituo hicho ni kutoa huduma za utalii ikiwa ni pamoja na vibali vya kuendesha utalii, kutoa taarifa zinazohusiana na maeneo ya uwekezaji wa utalii na pia kuweka jukwaa kwa sekta binafsi kukaa pamoja na kujadiliana fursa na changamoto mbalimbali katika Sekta ya Utalii ikiwa ni pamoja na kupeana uzoefu kwenye kutoa huduma kwa watalii katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kuwajumuisha Wenyeviti wa Halmashauri na Wabunge kwenye Kamati za kujadili na kupitisha maombi ya wavunaji wa mali za misitu kwenye Wilaya zetu nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi, uwakilishi wa wananchi upo katika ngazi mbili. Ngazi ya kwanza ni ambapo Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji vinavyovuna hushiriki kwenye vikao vya Kamati, ngazi ya pili ni ambapo Waheshimiwa Madiwani na Wabunge katika vikao vya Baraza la Madiwani hupata wasaa wa kujadili na kutoa ushauri juu ya taarifa za Kamati zinazohusu maombi yote ya uvunaji wa miti na tathmini ya mwenendo wa uvunaji katika Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ugawaji wa malighafi ya miti ya kuvunwa katika misitu ya asili ya Serikali unasimamiwa na Kamati ya Usimamizi ya Uvunaji katika kila Wilaya. Jukumu la kwanza la Kamati hii ni kujadili na kutoa maamuzi ya maombi ya uvunaji wa miti Wilayani katika misitu ya asili inayovunwa kwa ajili ya magogo, mbao, nguzo, fito, kuni na mkaa. Mazao hayo ni yale tu yatakayovunwa kwa ajili ya biashara. Jukumu la pili ni kufuatilia utekelezaji wa mpango wa uvunaji katika msitu husika na kutoa ushauri katika ngazi za Wilaya na Wizara pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mpango wa upandaji miti katika eneo la msitu unaovunwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE.COSATO D. CHUMI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatoa GN kuwezesha Mradi wa Regrow kuanza rasmi katika eneo la Kihesa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa tangazo la awali la siku 90 la nia ya kubadilisha matumizi ya sehemu ya eneo la Msitu wa Kihesa Kilolo, tarehe 9 Julai, 2021. Siku 90 tayari zimekwisha, hivyo Serikali imepanga kutoa GN ya Msitu wa Kihesa, Kilolo mwezi Novemba, 2021. Naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaruhusu usafirishaji wa Viumbe Hai nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Malum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tarehe 17 Machi, 2016 Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi. Tatizo kubwa lililosababisha maamuzi hayo lilikuwa ni matokeo hasi yaliyokuwa yakiendelea kujitokeza kutokana na kufanya biashara hiyo ikiwemo kuhamisha rasilimali ya wanyamapori nje ya nchi. Aidha, Serikali ilirejesha jumla ya shilingi 173.2 ya ada na tozo zilizolipwa awali na wafanyabiashara kabla ya kusitishwa kwa biashara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya kina kuhusu biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi. Kufuatia tathmini hiyo, zuio la biashara litaondolewa ambapo biashara hiyo itafanyika kwa utaratibu ufuatao: -

(i) Wanyamapori hai wataruhusiwa kusafirishwa kwa shughuli za utafiti na kidiplomasia tu.

(ii) Wanyamapori watakaosafirishwa nje ya nchi watakuwa ni wale waliokaushwa au mazao yatokanayo na wanyamapori hao.

(iii) Biashara ya wanyamapori waliokaushwa pamoja na mazao yake itafanywa na wafanyabiashara wenye miradi ya ufugaji wanyamapori ili kuhamasisha uanzishwaji wa miradi ya ufugaji wa wanyamapori.

(iv) Serikali itatoa muda wa miezi mitatu ili kuruhusu wafanyabiashara kusafirisha wanyamapori waliosalia kwenye mazizi na mashamba kabla ya zuio ambao walikuwa wanafugwa kwa lengo la kuwasafirisha nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Burigi – Chato ili waache kuingiza Mifugo ndani ya Hifadhi na kumaliza mgogoro kati ya wananchi hao na Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Ezra John Chiwelesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia TANAPA imeendelea kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi 20,836,200 zilitumika kutoa elimu ya uhifadhi katika vijiji 37, ambapo katika Wilaya ya Biharamulo elimu hiyo ilitolewa kwa vijiji sita vya Kiruruma, Nyabugombe, Ngararambe, Kabukome, Katerela na vya Kitwechembogo.

Aidha, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Milioni 96.7 kwa ajili ya utoaji wa elimu ya uhifadhi katika maeneo ya vijiji 38 vinavyopakana na hifadhi hiyo vikiwemo vijiji 10 vya Wilaya ya Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na utoaji wa elimu kwa vijiji, Serikali imejipanga kutumia makundi maalum wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waweze kusaidia katika kuelimisha faida za uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha makongamano ya Kimataifa ili kukuza utalii wa Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kutuamini mimi na Mheshimiwa Waziri kuendelea kuhudumu Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kipekee nikupongeze wewe binafsi kwa kuteuliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikiendelea kuutangaza Mlima Kilimanjaro kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo: -

(a) Onesho la Utalii la Kimataifa la Kilifair linalofanyika Mjini Moshi Mwezi Juni kila mwaka;

(b) Mbio za Kilimanjaro (Kilimanjaro Marathon) zinazofanyika Mkoani Kilimanjaro mwezi Februari kila mwaka;

(c) Kushiriki makongamano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo WTM – London, ITB - Ujerumani, Fitur-Hispania na Expo - 2020 Dubai;

(d) Kushiriki makongamano ya kimataifa yanayolenga kuimarisha uhifadhi na kutangaza utalii wa Mlima Kilimanjaro likiwemo Kongamano la Milima Mirefu Duniani (International Mountains Alliance - ITA);

(e) Mlima Kilimanjaro ni moja ya eneo la urithi wa dunia ambapo kupitia mikutano mbalimbali ya UNESCO Mlima huo hutangazwa;

(f) Kuwatumia watalii wanaofika Tanzania kama mabalozi wa kuutangaza Mlima Kilimanjaro;

(g) Kuendelea kutumia matukio muhimu ya Kitaifa kama sherehe za Uhuru kuhamasisha jamii kupanda Mlima Kilimanjaro; na

(h) Kuandaa na kushiriki katika Onesho la Kwanza la Kimataifa la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki lilofanyika Jijini Arusha ili kutangaza vivutio vya utalii ikiwemo Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kubuni mikakati zaidi ya kuutangaza Mlima Kilimanjaro kwa maslahi mapana ya nchi. Ahsante.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa moja ya kitovu kikuu cha utalii duniani kwa kuwa ni Mkoa wenye vyanzo vingi vya utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii katika Mkoa wa Morogoro, Serikali ilipandisha hadhi sehemu ya Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Sambamba na jitihada hizo, Serikali kupitia Mradi wa Kukuza Maliasili na Kuendeleza Utalii (REGROW), barabara zenye urefu wa takribani kilometa 996, njia za watembea kwa miguu kilometa 132.5, viwanja vya ndege saba, malango ya kuingilia wageni nane, vituo vya askari nane na vituo vya kutolea taarifa kwa wageni vitatu vitajengwa katika Hifadhi za Taifa za Mikumi, Udzungwa na Nyerere Mkoani Morogoro. Juhudi hizi zitaendelea kuchochea hali ya utalii katika Mkoa huo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo katika hatua nyingine Serikali imeendelea kupandisha hadhi maeneo mbalimbali ikiwemo Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii ya Wami Mbiki kuwa Pori la Akiba. Vilevile kukamilika kwa reli ya mwendokasi (SGR) pamoja na kutumika kwa reli ya TAZARA kutaongeza wigo wa shughuli za utalii katika mikoa ya Morogoro na Pwani. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Uwanja wa Ndege wa Ipole pamoja na nyumba ya kupumzikia wageni wanaokuja kwa ajili ya utalii wa picha na kuangalia Wanyama kwenye WMA ya JUHIWAI, Mbuga za Ipembampazi na Isuvangala utajengwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa wageni wanaokwenda Ipole WMA kufanya shughuli za utalii wanatumia uwanja wa ndege wa Tabora, pamoja na kiwanja kidogo cha Koga kilichopo katika eneo la WMA. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuhamasisha wawekezaji wanaowekeza katika maeneo hayo kujenga uwanja wa ndege pamoja na nyumba ya kupumzikia wageni ili kuhakikisha wageni wanaokwenda kwenye WMA ya Ipole, Mbuga za Ipembampazi na Isuvangala kwa ajili ya utalii wanaofika katika eneo husika bila tatizo.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TFS/TANAPA na wananchi wa Kata za Inyala, Itewe na Ilungu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa Kitulo haina mgogoro na vijiji vya Kata za Inyala, Itewe na Ilungu. Changamoto iliyopo ni kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuchumi. Maeneo hayo yalikuwa yanatumiwa kinyume cha sheria kwani kwa eneo ambalo ni Hifadhi ya Taifa Kitulo lilikuwa ni shamba la Serikali la mifugo ambamo ndani yake kulikuwa na (ng’ombe na kondoo wa sufu) lililojulikana kama Kitulo Dairy Farm.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa ardhi zaidi, wananchi wamekuwa wakidai maeneo waliyo kuwa nayo wanatumia kabla ya Hifadhi ya Taifa Kitulo kuanzishwa mwaka 2005 yarudishwe kwao ili kukidhi mahitaji zaidi ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji. Kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi na hifadhi za mazingira kwa ujumla ili kutatua changamoto hiyo.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -

Fursa zimetolewa kwa watu binafsi kuanzisha ranchi, mashamba na bustani za wanyamapori?

Je, ni wanyama wa aina gani wanaruhusiwa kufugwa na utaratibu gani unaotumika kuwapata na Serikali ina mkakati gani kuhakikisha wanyama hao hawasafirishwi kwenda nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ufugaji wanyamapori katika ranchi, mashamba na bustani za wanyamapori unasimamiwa na Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na Kanuni za Usimamizi wa Maeneo ya Ufugaji Wanyamapori za mwaka 2020. Kwa yeyote anayehitaji kufuga atapaswa kuwa na leseni inayotolewa na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kufuata vigezo vilivyowekwa.

Mheshimiwa Spika, wanyamapori aina zote wanaruhusiwa kufugwa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa mfano, aina ya mnyamapori, ukubwa wa eneo, na upatikanaji wa chakula na bei zake zimeainishwa katika jedwali la sita la Kanuni za Usimamizi wa Maeneo ya Ufugaji Wanyamapori za mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, kutokana na Tamko la Serikali lililotolewa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 25 Mei, 2016 kuhusu zuio la biashara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi, leseni zote zinazohusu usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi zilizuiliwa.

Aidha, ulinzi katika malango ya kutokea ikiwa ni viwanja vya ndege, bandari, barabara na mipaka ya nchi umeimarishwa ili kuhakikisha hakuna wanyamapori au nyara inayosafirishwa bila kibali ama leseni. Ahsante. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -

Wananchi wa Kata za Mgori, Mughungu na Ngimu Jimbo la Singida Kaskazini wapo tayari kukabidhi Msitu wa Mgori kwa Serikali kuwa Hifadhi ya Taifa: -

Je, mchakato wa Serikali kukamilisha zoezi hilo umefikia wapi na faida gani wananchi watazipata kwa msitu huu kuwa hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kupongeza jitihada zote zilizochukuliwa na Serikali katika ngazi ya Vijiji, Wilaya na Mkoa pamoja na Mheshimiwa Mbunge katika kuhakikisha Msitu wa Mgori ambao ni makazi ya wanyamapori wadogo na wakubwa hususani tembo unahifadhiwa.

Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikia mpaka sasa ni mchakato wa kupata Tangazo la Serikali ili kuutambua msitu huo kama hifadhi. Rasimu ya kwanza ya Tangazo la Serikali imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 4 Februari, 2022. Tangazo hilo litadumu kwa siku 90 kabla ya kutolewa tangazo la mwisho ambalo litatoa idhini kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kusimamia msitu huo.

Mheshimiwa Spika, faida za kuhifadhi msitu huu wenye ukubwa wa hekta 49,000 ni pamoja na: -

(i) Kuweka hali ya hewa nzuri kwa Mkoa wa Singida wenye misitu michache sana ya hifadhi na kuwezesha upatikanaji wa mvua hivyo kusaidia kwenye ukuaji wa sekta nyingine kama kilimo, ufugaji na maji;

(ii) Lakini vilevile utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji;


(iii) Lakini pia uwepo wa baioanuai nyingi za mimea ya asili na makazi ya wanyamapori kama tembo na wengine hivyo, kuchochea shughuli za utalii;

(iv) Sambamba na hilo kuwepo kwa fursa za ufugaji nyuki kwa wenyeji ili kuwaongezea kipato.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni vivutio gani vya utalii vimetambuliwa Wilayani Ukerewe na hatua zipi zimechukuliwa kuendeleza na kuvitangaza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara katika kipindi cha mwaka 2020/2021 kwa kushirikiana na maafisa wa Mkoa wa Mwanza walitekeleza zoezi la kubaini na kuvitambua vivutio vya utalii vilivyopo katika Kisiwa cha Ukerewe. Vivutio hivyo ni pamoja na utalii wa ikolojia, utalii wa fukwe, utalii wa kiutamaduni na kihistoria.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati ya kuvitangaza na kuviendeleza vivutio hivyo vya utalii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii hapa nchini. Sambamba na hilo Serikali inaendelea kuimarisha Ofisi ya Kanda ya Utalii iliyopo Jiji la Mwanza na kuanzisha Chuo cha Utalii cha Taifa katika Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kusogeza huduma za Kanda ya Ziwa.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuboresha Hifadhi ya Taifa Kitulo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Kitulo ni hifadhi ya kipekee ambayo huwezi kuifanananisha na hifadhi nyingine hapa nchini. Hifadhi hii ina utalii wa maua, maporomoko ya maji, ndege wa aina mbalimbali na vivutio vingine. Wizara kwa kutambua hilo imeendelea kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi. Miundombinu hiyo ni pamoja na kuimarisha barabara zilizomo ndani ya hifadhi, kuanzisha huduma za malazi na chakula, kuongeza mazao mapya ya utalii ndani ya hifadhi kama vile utalii wa kutumia baiskeli, utalii wa kutembea kwa miguu na utalii wa kupanda vilima.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo maeneo ya malazi na shughuli za utalii kama vile utalii wa farasi, utalii wa kubembea na kamba na mazao mengine ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii na idadi ya siku za kukaa hifadhini na hivyo kuongeza mapato zaidi.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya askari wa misitu wanaopiga na kuwanyang’anya mkaa wananchi wa Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Askari wa Uhifadhi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya viongozi mbalimbali ikiwemo ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kuzingatia haki za binadamu. Endapo kuna uvunjaji wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo, Wizara haitosita kuwachukulia hatua watumishi wake wanaohusika na uvunjaji huo wa sheria.

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na wimbi la uvunaji wa mazao ya misitu, ukataji na uchomaji wa mkaa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara hii. Hali hii imesababisha kutoweka kwa kasi kwa maeneo ya misitu na hatimaye kujitokeza kwa athari za mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo, inapotokea mwananchi anasafirisha mazao ya misitu (mkaa) bila kufuata utaratibu, mazao hayo hutaifishwa na Serikali. Nitoe rai kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara hiyo kufuata sheria, kanuni na taratibu husika.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -

Je, ni lini vibali vya uwindaji vitatolewa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasli na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uwindaji wa wanyamapori umegawanyika katika makundi mawili ambayo ni uwindaji wa kitalii na uwindaji wa wenyeji/wageni wakazi. Uwindaji wa kitalii ambao unalenga kupata nyara kwa ajili ya watalii unasimamiwa kwa kuzingatia Kanuni za Uwindaji wa Kitalii. Aidha, uwindaji wa wenyeji na wageni wakazi hufanyika kwa ajili ya kitoweo na unasimamiwa kwa kuzingatia Kanuni za Uwindaji wa Wenyeji na Wageni Wakazi.

Mheshimiwa Spika, vibali vya uwindaji wa kitalii vinaendelea kutolewa kwa mujibu wa Kanuni husika ambapo hadi sasa jumla ya minada Saba imefanyika na wadau wamepewa vibali vyao. Kwa upande wa Uwindaji wa wenyeji na wageni wakazi, vibali hivyo vitaanza kutolewa mara baada ya mapitio ya Kanuni za Uwindaji wa Wenyeji na Wageni Wakazi kukamilika.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza: -

Je ni lini, Serikali itamaliza mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Vikonge na Nomalusambo dhidi ya TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa ardhi uliokuwepo kati ya Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East na Kijiji cha Vikonge ulitokana na kutotambulika mipaka. Wizara kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji, wananchi pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi walienda kutafsiri mipaka hiyo. Hivyo, Serikali inahimiza kuendelea kuheshimu makubaliano yaliyosainiwa kati ya Kijiji cha Vikonge na TFS juu ya mpaka na hivyo kumaliza mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kijiji cha Nomalusambo ambacho kina kitongoji kiitwacho Ijenje ambacho kiko ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East, mwaka 2017 kitongoji hiki kiliondolewa katika eneo la hifadhi kupitia zoezi la uondoaji wavamizi msituni ambapo wananchi wa kitongoji hicho walitii maekelezo na kuondoka ndani ya hifadhi. Hivyo, Serikali inashauri wananchi wa Kijiji cha Nomalusambo waendelee kushirikiana na Serikali katika kuhifadhi Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East kwa ajili ya manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaondoa wananchi waliovamia Msitu wa Bondo uliopo Kata ya Mswaki, Kijiji cha Mswaki?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nyakati tofauti Hifadhi hii imekuwa ikivamiwa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo, makazi na kuchungia mifugo. Hadi sasa, Serikali imeweka matangazo ya kuwataka wavamizi wote kuondoka ndani ya Hifadhi hiyo ya Bondo kwa hiari yao ifikapo tarehe 30 Desemba, 2022.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kupunguza eneo la Hifadhi ya Msitu wa Mbiwe ili litumike kwa matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache N. Kasaka, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzishwa hifadhi hiyo ni kulinda bayoanuai zilizomo ndani ya hifadhi ikiwemo vyanzo vya maji vinavyotumika kwa matumizi ya binadamu na wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, Serikali haioni haja ya kupunguza eneo la hifadhi ya Msitu wa Mbiwe. Aidha, Sheria ya Misitu inaruhusu uchimbaji wa madini ndani ya hifadhi kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizopo kwa njia endelevu.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, ni lini TFS itaanza kutoa vibali vya malisho kwa wafugaji kama inavyotoa vibali vya kuvuna mbao na mkaa ili Serikali ipate mapato?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Misitu, Sura ya 323, Kifungu cha 26(n) kinakataza kuingiza au kuchunga mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. Aidha, Kanuni za Misitu za mwaka 2004, Kifungu cha 14(4) kimeweka katazo la kutoa vibali vya kuchunga au kulisha mifugo au kufanya shughuli za kilimo kwenye hifadhi za misitu.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kuchunga, kulisha mifugo au kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ya hifadhi za misitu ni kuvunja sheria. Hivyo, sheria zimewekwa ili kulinda rasilimali zilizomo hifadhini kwa matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE K.n.y. MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza: -

Je, ni wananchi wangapi wameathirika na uvamizi wa wanyama wakali katika Wilaya ya Kyerwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitano, Wizara imepokea taarifa ya matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ambapo jumla ya wananchi 54 katika Vijiji vya Kibare, Businde na Nyakashenyi walipata madhara ya uharibifu wa mazao yao uliosababishwa na tembo.
MHE. MOHAMED JUMAH SOUD aliuliza: -

Je, Kampeni ya AFR 100 imetekelezwa kwa kiasi gani na maendeleo gani yamefikiwa hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara imefikia hatua zifuatazo katika utekelezaji wa Kampeni ya AFR 100: kuondoa wavamizi na kurejesha ardhi iliyoathiriwa; Kuimarisha usimamizi wa misitu ya mikoko; Kutoa elimu ya kudhibiti moto wa msituni ili kulinda uoto wa asili; na Kutekeleza Mpango wa Dodoma ya Kijani.

Mheshimiwa Spika, maendeleo yaliyofikiwa ni pamoja na kusainiwa kwa makubaliano ya Kurejesha Mandhari ya Kiafrika – (AFR 100) na Mbinu ya Tathmini ya Fursa ya Marejesho. Aidha, Tanzania imefanikiwa kuandaa na kukamilisha Mkakati wa Kitaifa wa Kurejesha Mandhari ya Misitu. Mkakati huu unatarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Nchi Wanachama wa kujadili masuala ya Mazingira (COP 27).
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Askari Wanyamapori katika Wilaya ya Itilima na maeneo yanayozunguka Pori la Akiba Maswa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Askari Wanyamapori katika Wilaya ya Itilima mwezi Oktoba, 2022. Kituo hicho kipo katika Kijiji cha Longalombogo ambapo kitakuwa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi na Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) na kitahudumia zaidi ya vijiji tisa vikiwemo Longalombogo, Nding’ho, Lung’wa, Nyantugutu, Mbogo, Shishani, Pijulu, Ng’walali na Mwamakili.
MHE. TABASAM H. MWAGAO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawavuna tumbili katika Kisiwa cha Juma Wilayani Sengerema ambao wanakula mazao ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Hamis Mwagao, Mbunge wa Jimbo la Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi ya kuyabaini na kuyadhibiti makundi (familia) ya tumbili yanayosumbua wananchi katika Kisiwa cha Juma, Wilayani Sengerema. Aidha, Serikali itaendelea kuhamisha makundi hayo na kuyapeleka katika hifadhi nyingine zenye mahitaji ya wanyamapori hao. Wizara itaendelea kuimarisha doria za kudhibiti wanyamapori waharibifu wakiwemo tumbili na nyani.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza maeneo kutoka kwenye hifadhi katika Jimbo la Igalula ili wananchi wa Igalula wapate maeneo ya kuchungia na makazi kwa kuwa idadi ya watu na mifugo imeongezeka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 Serikali ilifanya mapitio ya mipaka ya msitu wa Uyui Kigwa - Rubuga uliopo Igalula, Wilaya ya Uyui ambapo hekta 36,709 zilitolewa kwa ajili ya vijiji vya Matanda, Sawmill, Kalemela, Itobela, Ibelamilundi, Isenegezya na Isikizya.

Mheshimiwa Spika, Serikali haioni haja tena ya kumega eneo hilo kutoka kwenye hifadhi kwa ajili ya kuwagawia wananchi kutokana na umuhimu wa hifadhi hii kiikolojia. Aidha, vijiji vinaelekezwa kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro mipya kujitokeza.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fidia kwa Wananchi wa Simiyu wanaopakana na Hifadhi za Wanyamapori na kuathiriwa na wanyama hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020/2021 mpaka 2025 kwa kufanya yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nikufanya doria za mara kwa mara kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Aidha, Mheshimiwa Rais alielekeza vijengwe vituo vya askari katika maeneo ya Busega na Meatu. Mchakato wa ujenzi umeanza ambapo vituo viwili vitajengwa katika maeneo tajwa mwezi Aprili, 2022. Sambamba na hilo, maombi ya vibali vya kuajiri askari 600 yameshawasilishwa kwenye mamlaka husika.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ni kutoa mafunzo ya mbinu za kujilinda na kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu. Jumla ya Halmashauri 17 zimepatiwa mafunzo hayo. Aidha, Wizara ina namba maalum za simu kwenye kila kanda za kiutendaji ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za matukio ya wanyamapori bila malipo.

Mheshimiwa Spika, malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya Sh.790,721,500 imetolewa kwa wananchi 3,598. Aidha, Wizara imepokea maombi ya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kutoka wilaya mbalimbali zikiwemo Wilaya za Mkoa wa Simuyu. Kwa sasa Wizara inafanya uhakiki wa maombi kabla ya malipo kufanyika. Ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itarejesha kwa wafugaji mifugo iliyokamatwa na TAWA, TFS na WMA ambapo Mahakama ilitoa hukumu irejeshwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ni kosa kuingiza na kuchunga mifugo ndani ya Hifadhi. Serikali ina jukumu la kulinda Rasilimali na Maliasili za Taifa, ikiwa ni pamoja na kuzuia uharibifu unaosababishwa na uvamizi wa mifugo ndani ya maeneo ya Hifadhi.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wanapokamatwa na mifugo ndani ya hifadhi kesi zao hupelekwa Mahakamani ambapo hukumu hutegemea na maamuzi ya Mahakama. Hukumu inaweza kuwa kulipa faini na kurejeshewa mifugo au kutaifishwa. Endapo kuna wananchi ambao mifugo yao ilikamatwa na Mahakama kuamuru kurejeshewa mifugo yao na hawajarejeshewa, wawasilishe malalamiko yao Wizarani ili yashughulikiwe.

Mheshimiwa Spika, ili kuepukana na migogoro ya wafugaji, Serikali inawaomba wananchi hususani wafugaji kujiepusha kuingiza mifugo kwenye maeneo ya Hifadhi.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa mpaka kati ya wananchi wa Kata ya Itaka na Nambinzo na TFS kuhusiana na Pori la Hifadhi Isalalo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) haina mgogoro wowote wa mpaka kati ya msitu wa Isalalo-Lunga na wananchi wa Kata ya Itaka na Nambinzo. Hali iliyopo ni uvamizi unaofanywa na wananchi wachache wanaoingia kwenye hifadhi kinyume cha sheria kwa ajili ya kilimo cha mazao ya muda mfupi. Aidha, ndani ya msitu huu hakuna makazi na Wizara imeendelea kuimarisha mipaka ya msitu kwa kuweka vigingi vikubwa 20 na vinavyoonekana vizuri. Sambamba na hilo, mabango 15 yamewekwa ili kuwakumbusha wananchi kuzingatia sheria.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani kudhibiti tembo wanaovamia Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenyanga, Gurungu, Muhanga na Njirii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kunusuru maisha na mali za wananchi katika Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenyanga, Gurungu, Muhanga na Njirii-Manyoni. Aidha, Wizara imeanza kuimarisha Kituo cha Askari cha wanyamapori kilichopo Kijiji cha Doroto kwa kuongeza Askari, vitendea kazi na kutoa Elimu kwa wananchi juu ya mbinu rafiki za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji umeme vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Misitu Sura ya 323 haijazuia upitishaji wa nguzo za umeme katika Hifadhi za Misitu hapa nchini. Kupitia Kifungu cha 26 cha Sheria ya Misitu Na. 14 ya Mwaka 2002, utaratibu umewekwa kwa taasisi au mtu anayetaka kufanya shughuli mbalimbali ndani ya Hifadhi ya Msitu na utaratibu huo unamtaka mtu huyo au taasisi kuwa na kibali kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kinachomruhusu kufanya shughuli husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TFS kwa nyakati tofauti imekuwa inashirikisha Wizara za kisekta kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini bila kuchelewa.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini mgogoro wa mipaka kati ya Vijiji vya Utengule, Ovindembo, Ipinde, Tanganyika na Kampuni ya Kilombero North's utatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Uwindaji ya Kilombero North’s Limited imekodishwa Kitalu cha Uwindaji cha Mlimba North’s ambacho ni sehemu ya Bonde la Mto Kilombero. Maeneo ya kitalu hicho ni chanzo muhimu cha maji yanayoingia katika Mto Kilombero ambayo pia yanachangia katika Mradi wa Kitaifa wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Eneo la Kitalu cha Uwindaji cha Mlimba ni moja kati ya maeneo yanayoshughulikiwa na Kamati ya Mawaziri nane inayofanyia kazi migogoro hiyo iliyopo katika vijiji 975. Kufuatia Kamati hiyo, timu ya wataalamu ya Kitaifa inayohusika na utatuzi wa migogoro kwa kushirikiana na Mkoa wa Morogoro na Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga imeshakwenda kwenye eneo lenye mgogoro huo kwa lengo la kufanya tathmini na kubaini maeneo halisi yanayostahili kuhifadhiwa kwa maslahi mapana ya Taifa na maeneo mengine wataachiwa wananchi ili waendelee kufanya shughuli zao ikiwemo kilimo, makazi na ufugaji.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza: -

Je, ni Wananchi wangapi Kondoa Mjini walioharibiwa mazao yao na tembo wamehakikiwa na lini watalipwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya tarehe 25 na tarehe 28 Septemba, 2022, Wizara ilifanya uhakiki wa madai ya kifuta jasho ya wananchi 274 wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa walioharibiwa mazao yao na tembo. Baada ya uhakiki huo kukamilika, Wizara iliwalipa wananchi 198 wa Vijiji vya Chemchem, Tungufu, Tampori, Mulua na Iyoli mwezi Novemba, 2022. Jumla ya shilingi 40,013,750 ikiwa ni kifuta jasho kutokana na madhara yaliyosababishwa na wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imepokea madai mengine mapya ya wananchi 28 wa vijiji vya Unkuku, Kwapakacha, Serya, Damai, Chemchem na Mulua ambayo yamewasilishwa hivi karibuni. Madai hayo yanaendelea kufanyiwa kazi na malipo yatafanyika baada ya taratibu stahiki kukamilika.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapunguza ukubwa wa Msitu wa Mbiwe na kurudisha kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Msitu wa Hifadhi wa Mbiwe una ukubwa kilomita za mraba 491 na umeanzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 598 la mwaka 1995. Hifadhi ya Msitu wa Mbiwe ni muhimu kwa uhifadhi vyanzo vya maji, kuhifadhi mimea na wanyama, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kivutio cha utalii. Eneo hili pia ni ushoroba unaounganisha mapori ya akiba ya Rukwa - Lukwati, Lwafi na Hifadhi ya Taifa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu huo, Serikali haioni haja ya kupunguza eneo hilo.
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia Pori tengefu la Mabwepande kama chanzo cha mapato?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha Pori la Akiba Pande linaendelea kuwa kitovu cha utalii katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani kuwa chanzo cha mapato, Serikali imetumia kiasi cha shilingi 710,789,122 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya utalii zikiwemo public camp site Mbili katika eneo la Msakuzi na Jomeke na Picnic Site Mbili eneo la Bwawani na Crater pamoja na ujenzi wa uzio wa bustani ya wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hiyo imekamilika na imeanza kutumiwa na watalii ambapo kwa sasa shughuli mbalimbali zikiwemo mbio za Marathon, nyama choma festival, utalii wa kutembea kwa miguu na kuendesha baiskeli, upigaji picha na matamasha mbalimbali vimeanza kutumika.
MHE. VINCENT P. MBOGO K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwapatia Wananchi maeneo ya kulima kutoka kwenye mapori na Hifadhi ambazo hazina wanyama kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi ni mojawapo ya wilaya zitakazonufaika na uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kumega maeneo ya hifadhi kwa ajili ya shughuli za wananchi ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi. Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi unatakiwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya hekta 10,828 zimependekezwa kumegwa kutoka Msitu wa Hifadhi ya Lowasi unaopakana na Pori la Akiba la Lwafi kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, Serikali imechukua hatua gani ili kumaliza mgogoro uliopo kati ya Mbuga ya Rwanyabara na Kijiji cha Bushasha kata ya Kishanje Wilayani Bukoba ambao umedumu kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Bushasha kipo Kata ya Kishanje katika Wilaya ya Bukoba. Kijiji husika hakipakani na hifadhi yoyote ya wanyamapori katika Mkoa wa Kagera. Aidha, hakuna mgogoro wowote kati ya Kijiji cha Bushasha na hifadhi yoyote ya wanyamapori zilizopo katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, mgogoro uliokuwepo katika Wilaya ya Bukoba ulikuwa kati ya Kijiji cha Kangabusharo katika Vitongoji vya Nshisha, Kangabusharo na Kayaga na Hifadhi ya Msitu wa Ruasina ambao tayari umefanyiwa kazi na timu ya wataalam.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Wamembiki na Wananchi wa Vijiji vinavyopakana na Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba Wami-Mbiki linapakana na vijiji 24 ambapo vijiji Nane vipo upande wa Wilaya ya Mvomero na vijiji Vitatu vipo upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Aidha, vijiji 13 vipo upande wa Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa migogoro hii iliwahi kupitiwa na Kamati ya Mawaziri Nane, Serikali kupitia maamuzi ya Baraza la Mawaziri imeshaanza kutatua migogoro hiyo. Utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri ulianza tarehe 05 Oktoba, 2021 kwa Mawaziri wa Kisekta na wataalam kupita katika Mikoa yenye migogoro ikiwemo Mkoa wa Morogoro. Aidha, wataalam kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa na Wilaya husika wamepita katika vijiji vyote 24 vinavyopakana na Pori la Akiba la Wamembiki. Baadhi ya mipaka ya vijiji imeonekana kuwa na muingiliano na Mipaka ya Pori la Akiba la Wamembiki. Kwa kuwa watalaam wa Kamati ya Kitaifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi bado wako uwandani Mkoani Morogoro suala hilo litapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa na Wilaya husika.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa wananchi wa Wilaya ya Mvomero hususani katika vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba Wamembiki kuwa wavumilivu na kuheshimu mipaka iliyopo wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hiyo.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -

Je, Tanzania inapokea watalii wa aina ngapi kutoka nje na sekta hii inachangia kiasi gani katika Pato laTaifa kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa ikipokea watalii mbalimbali kutoka masoko ya Kimataifa ikiwemo nchi za Bara la Afrika, Amerika, Asia na Pasifiki, Ulaya, na Mashariki ya Kati. Watalii hao wamekuwa wakitembelea Tanzania kwa madhumuni tofauti, ikiwa ni pamoja na mapumziko, kutembelea ndugu na jamaa, biashara, mikutano, matukio, na sababu nyinginezo ikiwemo ziara za kujifunza na matibabu.

Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii kabla ya mlipuko wa janga la UVIKO - 19 ilikuwa ikichangia wastani wa asilimia 17.2 ya Pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni, asilimia 60 ya biashara za huduma na kuzalisha ajira takribani Milioni 1.5, ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, mlipuko wa janga la UVIKO-19 ulioikumba Dunia mwishoni mwa mwaka 2019 ulisababisha kupungua kwa idadi ya watalii kutoka 1,527,230 mwaka 2019 hadi watalii 620,867 mwaka 2020. Mapato kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.6 hadi Dola za Marekani Bilioni 0.7.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itazuia Mamba wanaoua watu na kujenga uzio wa nondo maeneo ambayo watu huchota maji Jimboni Buchosa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na matukio mbalimbali ya wanyama wakali kujeruhi au kusababisha vifo vya watu pembezoni mwa maeneo yenye maziwa, mito na mabwawa hususani mamba. Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Migongano baina ya Binadamu na Wanyama wakali na waharibifu. Aidha, kuanzia kipindi cha Julai, 2021 hadi Aprili, 2022 jumla ya mamba wawili wamevunwa katika Kata ya Maisome Wilayani Buchosa. Vilevile, katika kipindi tajwa watu 992 wamepewa elimu kuhusu namna ya kuepuka madhara ya wanyama wakali na waharibifu. Hadi sasa kikosi cha Askari wa Uhifadhi watatu wapo uwandani wanaendelea na doria za kudhibiti mamba katika Wilaya ya Buchosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazishauri Mamlaka ya Serikali za Mtaa (Halmashauri) kuandaa mpango madhubuti wa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vizimba na Wizara ya Maliasili na Utalii itatoa wataalam.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukuza utalii wa fukwe za bahari nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuendeleza Mazao mbalimbali ya Utalii, ikiwemo Utalii wa FUKWE. Katika kutekeleza mikakati hiyo, Idadi ya Watalii wanaotembelea fukwe zetu zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara imeendelea kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sambamba na hilo, Serikali imetekeleza yafuatayo: -

i. Kwanza ni kubaini maeneo mapya ya fukwe za Bahari ya Hindi yanayofaa kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za utalii katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara;

ii. Lakini pia kuweka utaratibu wa kusajili maeneo ya fukwe yanayofaa kwa shughuli za Utalii kama Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Shughuli za Utalii (Tourism Special Economic Zone); na

iii. Lakini la mwisho ni kuendelea kuwahamasisha wamiliki wa maeneo ya fukwe nchini ili kusajili maeneo ya fukwe wanayoyamiliki chini ya utaratibu wa Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Shughuli za Utalii kwa lengo la kuiwezesha Serikali kushirikiana na wamiliki hao kuhimiza uwekezaji wa utalii wa fukwe.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga na Hifadhi kwa kutoa CSR kwenye mapato ya utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kupitia utekelezaji wa Sera ya Uwajibikaji Kijamii (Community Social Responsibility - CSR), Serikali inatekeleza miradi ya ujirani mwema kwa jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa zikiwemo Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMAs). Katika kutekeleza Sera hiyo, Halmashauri za Wilaya pamoja na jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa, zinanufaika na mapato yanayotokana na utalii ikiwemo kupatiwa miradi mbalimbali ya kijamii inayoibuliwa na wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya, Sekta ya elimu, Sekta ya Maji na Sekta ya Ujenzi. Miradi hii hutekelezwa na Taasisi za Uhifadhi nchini ambazo ni TANAPA, TAWA na NCAA.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Uwindaji wa Kitalii, Serikali pia imekuwa ikitekeleza Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na.5 ya 2009 ambayo inaelekeza kuwa asilimia 25 ya fedha zinazotokana na ada za wanyamapori waliowindwa katika vitalu vya uwindaji wa kitalii zirudishwe kwenye halmashauri zinazopakana na maeneo ya uwindaji. Aidha, katika maeneo ya WMAs, Kanuni za WMAs za mwaka 2018 zinaelekeza kuwa asilimia 75 ya ada ya kitalu, asilimia 55 ya ada ya wanyamapori wanaowindwa na asilimia 45 ya gharama za uhifadhi zinazotokana na uwindaji wa kitalii zirudishwe kwa jamii inayomiliki maeneo husika. Wizara imekuwa ikitekeleza matakwa haya kupitia TAWA. Ahsante.
MHE.ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kurekebisha utaratibu wa kuwaachia makusanyo ya fedha Jeshi la Uhifadhi hasa TANAPA?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kupongeza Serikali ya Awamu ya Tano na Sita kwa kuendelea kutekeleza takwa la kisheria la kuhakikisha makusanyo yote yanaingia kwenye kapu moja (Mfuko Mkuu wa Serikali). Katika kuendelea kutekeleza takwa hilo, Serikali ilibadili Sheria ya Fedha ya mwaka 2020 ambapo jukumu la kukusanya mapato yasiyo ya kodi ikiwemo ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lilikasimiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019/2020, mapato ya Jeshi la Uhifadhi (TANAPA) yalishuka kutokana na kushuka kwa ukusanyaji wa mapato kulikosababishwa na kupungua kwa wageni kufuatia makatazo ya kusafiri na kufungiwa (lockdown) baada ya kuibuka kwa janga la UVIKO-19. Hii ilisababisha Jeshi la Uhifadhi (TANAPA) kushindwa kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizo za kimapato, Serikali iliamua kugharamia shughuli zote za uhifadhi ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi na kutoa ruzuku ya kugharamia matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Aidha, katika kuhakikisha Jeshi la Uhifadhi (TANAPA) halikwami katika utekelezaji wa majukumu yake kwa wakati, Serikali imekuwa ikitoa fedha za matumizi kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) miezi miwili kabla yaani advance disbursement. Hata hivyo, Serikali itaendelea kufanyia kazi hoja ya Mheshimiwa Mbunge wakati ikiendelea na utaratibu huu hadi hapo itakapoona kama kuna uhitaji wa kubadilisha Sheria.
MHE. JACQUELINE K. ANDREW aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga bajeti kwa Hifadhi changa za utalii ili kukuza utalii katika hifadhi hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrew, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia fedha za Mpango wa Maendeleo na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, tayari ilishaanza mchakato wa kuboresha hifadhi changa 17 za utalii ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara, huduma za malazi na chakula na maeneo ya uwekezaji ambapo tayari wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza. Hifadhi za Taifa changa zilizopo katika mkakati huo ni Burigi-Chato, Gombe, Ibanda-Kyerwa, Katavi, Kigosi, Kisiwa cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane, Kitulo, Milima ya Mahale, Milima ya Udzungwa, Mikumi, Mkomazi, Mto Ugalla, Nyerere, Ruaha, Rumanyika-Karagwe na Saadani.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha hifadhi hizo kwa lengo la kukuza utalii na kuongeza mapato. Maboresho hayo yanaenda sambamba na utekelezaji wa Programu ya Tanzania, the Royal Tour ambapo kwa sasa Serikali imejikita zaidi kwenye maeneo mapya ya utalii zikiwemo hifadhi hizo.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, kwa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 ni kiasi gani cha gawio kimetolewa na eneo la Utalii Kaole kwa Halmashauri ya Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Magofu ya Kaole kilianza kutambuliwa na kuhifadhiwa kisheria mwaka 1937 ilipoanzishwa Sheria ya Uhifadhi wa Majengo ya Kihistoria, kipindi cha utawala wa Mwingereza na kwa sasa yanalindwa kwa Sheria ya Mambo ya Kale, Sura 333. Hapo awali vituo vya mambo ya kale vilitumika zaidi katika masuala ya tafiti na elimu hivyo kutembelewa zaidi na wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo hakuna gawio lolote linalotolewa kwa Halmashauri kutokana na mapato ya vituo vya malikale. Aidha, Magofu ya Kaole yanatoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri ya Bagamoyo kunufaika kiutalii kwa kuuza bidhaa mbalimbali kwa watalii kama vile vitu vya kiutamaduni, vyakula na kutoa huduma ya malazi. Kwa kufanya hivyo, halmashauri hunufaika kupitia tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara hao.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha barabara zinazowapeleka Watalii Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka kipaumbele na jitihada katika ukarabati wa barabara zinazotumika kupeleka watalii katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau na mamlaka zinazohusika na utengenezaji na ukarabati wa barabara hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa jitihada hizo zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara za Machame, Mweka na Marangu kwa kiwango cha lami na ukarabati wa mara kwa mara wa barabara za changarawe zinazoelekea lango la Rongai, Lemosho, Kilema, Londorosi na Umbwe. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali itafanya
ukarabati kwa kiwango cha changarawe kwa barabara inayoelekea kwenye lango la Umbwe.
MHE AIDA J. KHENANI K.n.y. MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isitumie mbao za Mitiki zenye ubora sawa na Mninga/Mkongo kwani tenda za Serikali zinataka Mninga/Mkongo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, shughuli za ujenzi na utengenezaji wa samani ambazo kiuhalisia zimekuwa zikikua sambamba na ongezeko la watu, zinategemea sana rasilimali ya misitu kama chanzo cha malighafi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kukua kwa mahitaji na changamoto ya upatikanaji wa miti migumu kutoka katika misitu ya asili hasa jamii ya mninga na mkongo, Wizara imefanya utafiti kuhusu tabia na sifa za mbao za matumizi kutoka kwenye miti isiyofahamika sana. Utafiti huo uliolenga kutambua tabia na sifa za kimwonekano, kiufundi na kianatomiki za mbao za miti isiyojulikana sana, ulionesha kuwa mti wa mitiki, una sifa ama sawa au zinazokaribiana sana na miti ya mkongo na mninga.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia matokeo ya utafiti huo, Serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza miti mipya iliyofanyiwa utafiti katika orodha ya miti iliyoainishwa katika Sheria ya manunuzi inayosimamiwa na PPRA ili itumike katika kutengeneza samani za Serikali.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itabadili majina ya kigeni kuwa ya Kitanzania kwenye rasilimali za Taifa ikiwemo Mlima Livingstone na Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo baadhi ya Rasilimali za Taifa zenye majina na maeneo ambayo zilipewa tangu kipindi cha utawala wa ukoloni. Majina hayo yalitolewa kutokana na juhudi za waasisi katika ulinzi na uhifadhi wa rasilimali hizo. Majina na maeneo hayo yameendelea kufahamika kihistoria kutokana na kutangazwa na Taifa na kuandikwa kwenye nyaraka na vitabu mbalimbali na rasilimali hizo zimeendelea kuhifadhi historia ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa rasilimali hizo kwa historia ya nchi yetu na kuendelea kufahamika zaidi kitaifa na kimaitafa pasipokuwa na changamoto yoyote, Serikali haioni haja ya kubadili majina na maeneo hayo ambayo kwa sasa yana mchango mkubwa kiuchumi kwa Taifa letu. Aidha, Serikali kwa sasa inaendelea pia kuzingatia majina ya wazawa kwenye rasilimali mbalimbali za Taifa kadiri zinavyoanzishwa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupanda Hifadhini mazao yanayofuatwa na wanyama waharibifu kutoka Hifadhi za Rungwa, Muhesi na Kizigo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya ongezeko la matukio ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara kwa wananchi na mali zao. Changamoto hiyo imesababishwa na uanzishwaji wa shughuli za binadamu kwenye shoroba, maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na maeneo ya pembezoni mwa hifadhi. Maeneo hayo hutumiwa na wanyamapori wanaohama kutoka katika mfumo mmoja wa ikolojia kwenda mfumo mwingine kwa ajili ya kutafuta maeneo ya malisho, maji, mazalia, ulinzi na mapumziko kwa nyakati tofauti.

Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hiyo ya kiikolojia, upandaji wa mazao katika hifadhi za wanyamapori hauwezi kuzuia wanyamapori kuhama kutoka mfumo mmoja wa ikolojia kwenda mfumo mwingine.

Vilevile upandaji wa mazao hifadhini ni ukiukwaji wa sheria za uhifadhi kwa kuwa wanyamapori wanaishi katika mazingira asilia ambapo mimea mingine ambayo siyo ya asili hairuhusiwi ndani ya hifadhi.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, ni lini Wananchi wa Sikonge watapatiwa eneo la hekta 33,000 kwenye Mbuga ya Ipembampazi litumike kwa kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Msitu wa Ipembampazi ina umuhimu katika kuimarisha mfumo wa ikolojia wa Ugalla - Moyowosi unaojumuisha maeneo ya hifadhi yaliyopo katika Mikoa ya Tabora na Kigoma ambapo eneo la msitu huo linatumika kama mtawanyiko na mapito ya wanyamapori hususan tembo. Eneo hilo lina wanyamapori wa aina mbalimbali na limetengwa kuwa kitalu cha uwindaji wa wenyeji.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -

Je, lini mpaka wa Hifadhi ya Ugalla utarekebishwa ili kurejesha kwa wananchi eneo walilokuwa wanatumia kwa ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Ugalla ilianzishwa kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282 baada ya kupandisha hadhi Pori la Akiba Ugalla kwa Tangazo la Serikali, G.N. No. 936 la mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo hili ni muhimu kiuhifadhi na ndani yake kuna vyanzo vya maji, kabla ya kubadilishwa hadhi eneo hili lilihusisha shughuli za uvunaji zikiwemo ufugaji nyuki na uvuvi. Hali hii ilileta changamoto za kiuhifadhi ikiwemo uchomaji moto unaoathiri uoto wa asili na uchafuzi wa vyanzo vya maji. Hivyo, Serikali haioni haja ya kufanya marekebisho ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, ni wananchi wangapi wa Jimbo la Nanyumbu wamefidiwa kutokana na uharibifu uliofanywa na tembo katika mashamba yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2022/2023, Wizara ilipokea jumla ya maombi nane kutoka kwa wananchi wa Vijiji vya Mchenjeuka, Lukula, Masuguru, Marumba na Mpombe walioathiriwa na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu. Baada ya taratibu za malipo kukamilika, mnamo tarehe 21 Machi, 2023, Wizara ilifanya malipo ya kifuta jasho ya jumla ya shilingi 5,160,000 kwa wananchi saba wa Vijiji vya Michenjeuka, Lukula, Masuguru na Mpombe walioharibiwa mazao. Aidha, mwezi Machi mwaka huu, Wizara ilipokea maombi mapya 12 ya wananchi wa Vijiji vya Nanyumbu na Marumba ambayo yanaendelea kushughulikiwa kwa ajili ya kuandaa malipo.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha mifumo ya utoaji leseni katika Sekta ya Utalii ili kurahisisha upatikanaji wa leseni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeshaunganisha mfumo wa utoaji wa leseni katika sekta ya utalii kupitia mfumo wa kieletroniki wa MNRT – Portal. Hatua hiyo imeongeza tija katika utoaji huduma ikiwemo kurahisisha mchakato wa utoaji wa leseni za biashara za utalii na hivyo kupunguza gharama, muda na kuongeza wigo wa ushiriki wa wananchi na wawekezaji mbalimbali katika biashara hizo.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, lini Jeshi la Uhifadhi litapata Kamishna Jenerali na kuleta muunganiko katika divisheni za NCAA, TANAPA, TAWA na TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu (The Wildlife and Forest Conservation Service) lilianzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Sura ya 283.

Mheshimiwa Spika, utendaji wa taasisi zinazounda Jeshi hilo upo chini ya Kamishna wa Uhifadhi wa kila taasisi nao watakuwa ndio makamanda wa taasisi zao. Muundo wa Jeshi la Uhifadhi unaotumika kwa sasa unafanya kazi vizuri. Endapo kutabainika kuwa na changamoto katika kutekeleza mfumo huo, Serikali itafanya marejeo ya Sheria ya

Wanyamapori ili kuwezesha kuwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka miundombinu katika kivutio cha utalii cha Mount Uluguru Waterfall?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nora Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo ngazi kuelekea kwenye Maporomoko ya Hululu, ujenzi wa choo, kuweka miundombinu ya maji, mfumo wa umeme wa jua na mashine ya kusukumia maji na kujenga daraja la mbao kuvuka mto Mgeta. Aidha, Serikali kupitia mradi wa kupunguza athari za UVIKO -19 ilikarabati barabara ya kuelekea kwenye msitu huo wenye urefu wa Kilometa nane kutoka Kijiji cha Kibaoni hadi Bunduki kwenye kivutio cha Maporomoko ya Hululu. Ukarabati huo umewezesha kufikika kwa urahisi kwenye kivutio hicho kwa shughuli za utalii na uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza miundombinu ya utalii katika msitu huo. Miundombinu ya utalii inayoweza kuwekezwa na sekta binafsi ni pamoja na makambi (camp sites), lodge, hotel na maeneo ya burudani, nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaondoa Kijiji cha Ngaresero kwenye eneo la Pori Tengefu la Pololeti baada ya kujumuishwa kimakosa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshiwa Naibu Spika, Kijiji cha Ngaresero hakipo katika Pori la Akiba Pololeti ila kipo Kata ya Ngaresero, Tarafa ya Sale. Kijiji hicho ni mojawapo ya vijiji ambavyo vipo ndani ya Pori Tengefu Ziwa Natron. Kulingana na Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2019, ardhi ya Pori Tengefu Ziwa Natron ipo kwenye kundi la ardhi ya hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pori Tengefu Ziwa Natron ni moja kati ya maeneo yaliyotolewa maelekezo na Baraza la Mawaziri kuwa lipandishwe hadhi. Hivyo, wakati wa utekelezaji wa maelekezo hayo, wananchi wa kijiji cha Ngaresero watashirikishwa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua migogoro kati ya Wananchi na maeneo ya Hifadhi za Taifa ikiwemo Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa inachukua hatua mbalimbali kutatua migogoro baina ya hifadhi na wananchi. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kufanya tathmini ya aina, chimbuko na namna ya kutatua migogoro husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inasimamia misitu minne ya hifadhi katika wilaya ya Momba. Misitu hii ni Isalalolunga, Isalalo, Ivuna North na Ivuna South ambayo kimsingi haina mgogoro na wananchi. Katika kuimarisha ulinzi na usimamizi wa hifadhi hizi, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na uharibifu zikiwemo kuweka alama za kudumu za mipaka, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii, kuondoa wavamizi na kuchukua hatua za kisheria kwa wahalifu.
MHE. FESTO R. SANGA: Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Kitulo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuitangaza hifadhi ya Taifa Kitulo Kitaifa na Kimataifa kwenye maonyesho na matamasha mbalimbali kama vile Karibu Kusini, Kili-fair, Sabasaba, na Nanenane. Pia, tumeanza kuitangaza kwa njia ya kidigitali, mitandao ya kijamii, majarida na Safari Channel. Lengo ni kuvutia watalii na wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara imeanza kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi ikiwemo ujenzi wa nyumba tatu na tunatarajia kujenga nyumba mbili na kambi moja ya kuweka hema katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024, pamoja na kukarabati miundombinu ya barabara.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuvuna fisi wanaovamia makazi ya Wananchi, kujeruhi na kuua Watu katika Kata ya Endamarariek?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto ya fisi kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi hususan kwenye Kata ya Endamarariek Wilayani Karatu, Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imekuwa ikifanya msako wa fisi katika maeneo husika ambapo tangu mwaka 2019 hadi sasa jumla ya fisi saba wamevunwa. Aidha, mapango/makazi ya fisi 11 yameharibiwa katika maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fisi wanaishi katika makundi, Wizara inaendelea kufanya soroveya ili kuyabaini makundi ya fisi yaliyosalia na kuyavunja ikiwa ni pamoja na kuharibu makazi yao.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia wafugaji kuchunga mifugo katika Hifadhi ya Julius Nyerere?

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Sura Namba 283 iliyorejewa mwaka 2022, Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002, zimeweka zuio la kuingiza mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya uingizaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa Nyerere ni ya muda mrefu. Wizara inakabiliana na changamoto hii kwa kuimarisha doria katika maeneo ya hifadhi na kuwachukulia hatua wanaoingiza mifugo hifadhini kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo. Aidha, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukabiliana na changamoto hiyo.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza: -

Je, upi mpango wa kudhibiti wanyama wanaoharibu mazao na kugharimu maisha ya watu Kata za Naarami, Lokisale, Moita, Lepruko na Makuyuni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori umekuwepo kwa muda mrefu. Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni mwingiliano huo umeongezeka na kusababisha madhara kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuua mifugo na kuharibu mali za wananchi ikiwemo mazao na wakati mwingine kusababisha vifo au kujeruhi wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kuwepo kwa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, Wizara imeandaa mpango wa kongoa shoroba katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Kata za Naarami, Lokisale, Moita, Lepruko na Makuyuni. Aidha, Wizara imewaelekeza wananchi kuacha kuanzisha shughuli za kibinadamu kwenye mapito ya wanyamapori ili kuepuka madhara yanayotokana na wanyamapori hao.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itapitia upya mipaka na kuweka alama za Hifadhi katika Vijiji vya Ndongosi, Mtunduaro, Litumbandyosi na Kiwombi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Ndongosi, Mtunduaro, Litumbandyosi na Kiwombi vinapakana na Hifadhi ya Msitu wa Litumbandyosi katika Wilaya ya Mbinga. Kwa sasa Serikali inaendelea na utaratibu wa kuhakiki msitu huo wa Hifadhi wa Litumbandyosi kwa kuwashirikisha wananchi, baada ya kukamilika kwa uhakiki huo zitawekwa alama za mipaka zinazoonekana ili kuwezesha wananchi kutambua eneo la hifadhi na hivyo kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na kutokuwepo kwa mipaka inayoonekana wazi.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza: -

Je, watalii wangapi walitembelea Mbuga ya Ruaha kwa mwaka 2019/2020 na upi mkakati wa kuongeza watalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasilinna Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ilipokea jumla ya watalii 18,678 ambapo watalii 11,601 kutoka nje ya nchi na watalii 7,077 kutoka ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha idadi ya watalii inaongezeka, Serikali imeweka mikakati ifuatayo: -

(i) Kuanzisha na kuboresha miundombinu ya barabara za ndani ya hifadhi kwa kiwango cha changarawe na kuboresha barabara kuu kutoka Iringa Mjini hadi hifadhini.

(ii) Kuongeza na kuboresha viwanja vya ndege saba ndani ya hifadhi.

(iii) Kuongeza miundombinu ya malazi kwa kuongeza vitanda 263 na kutangaza maeneo ya uwekezaji.

(iv) Kuongeza na kuboresha mazao ya utalii kama utalii wa puto, boti, farasi, kuvua samaki, utalii wa kitamaduni na kihistoria, utalii wa mikutano na utalii wa michezo.

(v) Kuongeza utangazaji wa vivutio vya hifadhi katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, lini Serikali itatenga maeneo ya malisho ya mifugo katika Pori la Usumbwa Forest Reserve?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji ya Wananchi wa Ushetu na inaendelea kufanya tathmini ya eneo la Msitu wa Usumbwa Forest Reserve ili kujiridhisha kama unastahili kumegwa kwa ajili ya kutengwa eneo la kuchungia. Pindi tathmini itakapokamilika wananchi watajulishwa. Wakati Serikali inaendelea na tathmini hiyo wananchi wanashauriwa kuendelea kuheshimu maeneo hayo ili kuhifadhi msitu huo.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kubadilisha utaratibu wa utoaji vibali vya kuvuna miti ili kuhusisha Kamati za Maendeleo za Kata na Vijiji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, usimamizi na matumizi ya rasilimali za misitu hufanywa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Sura 323 na Kanuni zake za mwaka 2004. Aidha, katika kuhakikisha matumizi endelevu, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii huandaa mwongozo unaotoa namna ya kutoa vibali na usimamizi wa jumla wa matumizi ya misitu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia utaratibu huo Serikali ilitoa mwongozo mwaka 2017 unaofahamika kama ‘Mwongozo wa Uvunaji Endelevu wa Mazao ya Misitu.’ Mwongozo huo umebainisha wajumbe wanaounda kamati ya uvunaji ngazi ya wilaya chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -

Je, lini Kituo cha Utalii Kihesa Kilolo chini ya Mradi wa REGROW kitaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha taratibu zote za usanifu na makadirio ya ujenzi ikiwemo michoro ya usanifu (Detailed Design), kabrasha la zabuni (Tender Document), makadirio ya gharama za ujenzi na michoro (BOQ). Kwa sasa tunasubiri kibali cha Benki ya Dunia ili taratibu za manunuzi zianze. Tunatarajia ifikapo Julai, 2023 tuwe tumempata Mkandarasi.
MHE. ANTIPAS Z. MAGUNGUSI aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuwatumia vijana waliopata mafunzo ya JKT kutumikia Jeshi la Uhifadhi kwa mkataba wa muda mfupi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Magungusi, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu imekuwa ikiajiri Askari wenye taaluma kuu tatu ambazo ni Askari waliohitimu Astashahada ya Wanyamapori, Astashahada ya Misitu na Askari waliohitimu Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi hususan Askari, SUMA JKT wamekuwa wakiingia mikataba ambayo inawezesha vijana waliohitimu JKT kupata kazi za mikataba kwa shughuli mbalimbali za ulinzi wa maliasili (wanyamapori na misitu). Mfano, kwa sasa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wameingia mkataba na SUMA JKT kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ulinzi wa misitu kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa wa Askari.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, lini Seriikali itafanya ukarabati wa majengo ya magofu ya Bagamoyo ili yasianguke na kuleta madhara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umiliki wa majengo mengi katika eneo la Bagamoyo kuwa chini ya usimamizi na umiliki wa mamlaka mbalimbali ikiwemo watu na taasisi binafsi, Wizara imeendelea kuwahamasisha wadau wote kufanya ukarabati usioathiri mwonekano au kuharibu historia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa tayari wadau wanne wamepewa vibali vya kufanya ukarabati wa majengo yao ndani ya Mji Mkongwe wa Bagamoyo. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ipo katika mpango wa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Ngome Kongwe baada ya kufanyiwa uokoaji kwa kuliimarisha jengo hilo.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka wa Pori la Usumbwa Forest Reserve na Hifadhi ya Pori la Kigosi Moyowosi - Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Usumbwa Forest Reserve ambalo kwa sasa ni hifadhi ya Taifa Kigosi haina mgogoro wowote wa mpaka na wananchi wa Ushetu. Kwa sasa kilichopo ni wananchi wa Ushetu waliwasilisha maombi ya kumegewa eneo, ambapo Serikali inaendelea na tathmini na pindi litakapokamilika, wananchi watajulishwa. (Makofi)
MHE. AGNES M. MARWA aliuliza:-

Je, Serikali imewatafutia eneo mbadala wananchi wa Vijiji vya Kata ya Nyantwari – Bunda wanaofanyiwa uthamini kupitia uhifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali iliamua kutwaa eneo la ghuba ya Speke lenye ukubwa wa ekari 14,250 kwa manufaa ya umma ili kuimarisha uhifadhi endelevu wa mfumo ikolojia wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na usalama wa wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, zoezi la uthamini lipo katika hatua za mwisho na baada ya hapo wananchi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria. Fidia itakayolipwa kwa wananachi husika, itahusisha gharama za thamani ya ardhi, mazao, majengo, posho ya kujikimu, usafiri na posho ya usumbufu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda imetenga na kupima viwanja 350 katika Eneo la Virian, Kata ya Stoo ambapo wananchi watakaohama kutoka Kata ya Nyantwari watapewa kipaumbele wakati wa uuzaji wa viwanja hivyo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Halmashauri ya Mji wa Bunda imeandaa mpango wa kutwaa na kulipa fidia maeneo mbadala ya makazi yenye ukubwa wa ekari 1,625 katika maeneo ya Manyamanyama, Bitaraguru, Butakale na Guta. Maeneo yote hayo yatapimwa na kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaotoka Kata ya Nyantwari.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, nini kauli ya Serikali juu ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Misitu Sura ya 323 na Kanuni zake za mwaka 2004 zimeelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuvuna, kusafirisha na kuuza mazao ya misitu kwa kuzingatia umiliki wa misitu au miti ambao ni ya watu binafsi, Serikali za vijiji, Serikali za mitaa au Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TFS haizuii kufanya biashara ya mazao ya misitu isipokuwa inasimamia sheria na kanuni ambazo zinahakikisha kunakuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu nchini. Natoa rai kwa wadau au wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya misitu wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda misitu yetu ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa uvamizi wa tembo kwa wananchi na mashamba katika Wilaya za Liwale na Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kuwepo na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu wakiwemo tembo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020 – 2024. Wizara inaendelea kufanya yafuatayo; kutoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; kujenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; kuwafunga mikanda tembo na kuanzisha timu maalum (rapid response teams).

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa Askari wa Vijiji (VGS) ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: -

Je, Serikali ipo tayari kutenga sehemu kwa ajili ya shule ya sekondari katika Pori Tengefu Mabwepande lililopo Kibesa, Jimbo la Kibamba?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba Pande lenye ukubwa wa kilometa za mraba 15.39 limetengwa kwa sababu kuu zifuatazo; kufyonza hewa chafu (carbon sink) inayotokana na shughuli za kibinadamu ili isisababishe madhara kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, na kuhifadhi mimea na viumbe hai wengine kama wadudu na wanyamapori ambao ni muhimu katika kuhakikisha mifumo ikolojia ya maeneo husika inaimarika na kutoa huduma za kiikolojia. Aidha, eneo hilo pia linatumika kwa shughuli za utalii na kwa sasa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya pori hilo ili kuvutia watalii wengi na kuongeza mapato yatokanayo na utalii.

Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo na kuzingatia kwamba eneo hilo ni dogo, Wizara haioni busara kuendelea kumega eneo hilo kwa shughuli za kijamii.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha Maporomoko ya Kalambo yanatangazwa ili yawe na mchango wa kiuchumi kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege Mbunge wa Jimbo la Kalambo kama ifuatavyo:-

Katika kuhakikisha maporomoko ya Kalambo yanatangazwa kikamilifu, hatua zifuatazo zimeanza kuchukuliwa. Hatua ya kwanza ni kutumia vyombo vya habari kuandaa machapisho na majarida kushiriki katika maonyesho matamasha matukio na makongamano ya utalii na biashara yanayofanyika ndani na nje ya nchi. Aidha, jumla ya watalii 2,365 walitembelea maporomoko hayo mwaka 2021 ikilinganishwa na watalii 300 kwa mwaka 2016 na kuweka mabango katika viwanja vya ndege ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Songwe na maeneo mengine katika Mkoa wa Rukwa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, kuna mango gani wa kudhibiti Tembo wanaoharibu mazao na kujeruhi wananchi Kata za Mindu, Kahulu na Tinginya -Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vijiji vingi katika Wilaya ya Tunduru vinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na ushoroba wa wanyamapori wa Selous Niassa ambao ni mapito ya wanyamapori kati ya Tanzania na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, Wizara imechukua hatua zifuatazo: -

(i) Kuomba kibali cha kuajiri Askari wapya 600 ambao watasambazwa kwenye maeneo hatarishi ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Sambamba na hilo, Wizara ina mkakati wa kuanzisha vituo vya kikanda vya Askari katika maeneo yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu;

(ii) Kutoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji; na

(iii) Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kupunguza athari zinazotokana na wanyamapori wakali na waharibifu.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya wananchi na TAWA katika Bonde la Mto Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Jimbo la Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutekeleza maamuzi yaliyotolewa na Baraza la Mawaziri tangu Oktoba, 2021. Utekelezaji wa maamuzi hayo ulianza katika mikoa yenye migogoro ikiwemo Mkoa wa Morogoro hususan Pori Tengefu la Kilombero. Timu ya Wataalam ya Kitaifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi iko uwandani, inaendelea na zoezi la tathmini kwa kushirikisha mkoa, wilaya na wananchi wa maeneo hayo. Aidha, timu hiyo inafanya tathmini ya makazi na shughuli zenye athari kwenye uhifadhi wa vyanzo vya maji na rasilimali za wanyamapori ndani ya eneo la Pori Tengefu na Bonde la Mto Kilombero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utatuzi wa migogoro hiyo utaanza baada ya tathmini kukamilika.
MHE. JEREMIAH A. MRIMI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka alama za mipaka katika Hifadhi ya Serengeti na Pori la Akiba la Ikorongo ili kumaliza migogoro na vijiji jirani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kufanya tathmini ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji imekamilika kwenye vijiji sita ambavyo ni Mbilikili, Gwikongo, Bisarara, Machochwe, Nyamakendo na Mbalibali. Zoezi linalofuata ni kuweka alama za kudumu kwenye mipaka ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. Kazi hiyo itafanyika kwa njia shirikishi ili kuhakikisha kwamba kila upande unaridhika na zoezi hilo. Aidha, katika vijiji vya Robanda na Rwamchanga, Serikali iliweka mpaka wa Pori la Akiba Ikorongo kwa kuwashirikisha kikamilifu wananchi wa vijiji hivyo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupitia upya mipaka ya hifadhi na makazi ya wananchi Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutatua changamoto hiyo kwa kuweka vigingi ambapo hadi sasa jumla ya vigingi 111 vimewekwa kati ya vigingi 322 vinavyohitajika. Zoezi hili linaendelea hata kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo vigingi vilivyobaki vitawekwa. Serikali itaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutambua na kuheshimu mipaka ya hifadhi.
MHE. DANIEL B. SILLO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Vilima Vitatu, Mwada na Ngolee dhidi ya Hifadhi ya Tarangire?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Sillo Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa changamoto za migogoro katika Hifadhi ya Taifa Tarangire na baadhi ya vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tutatuma wataalam kwenda kufafanua au kutafsiri mipaka ili wananchi wajue maeneo ya vijiji na kuheshimu mipaka ya hifadhi.