Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo (2 total)

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa miaka mingi wananchi wa Jimbo la Handeni Mjini wamekuwa wakiishi katika dhiki kubwa ya maji. Ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji wa Handeni Trunk Main kutoka Mto Ruvu kwenda Handeni?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Napenda kumpongeza Naibu Waziri wangu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo ya mgonjwa. Mimi naishi Tanga, najua moja ya changamoto kubwa ni eneo la Handeni. Serikali imeainisha miji 28 na tumeshapata Dola milioni 500 kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tuko katika hatua ya manunuzi. Ndani ya mwezi Aprili, Wakandarasi wote watakuwa site kuhakikisha tunajenga miradi mikubwa ya maji. Hii ni katika kutimiza azma ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtua mwanamama ndoo kichwani. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. REUBEN N. KWAGILWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza ili yaweze kupata majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Wilaya ya Handeni ina majimbo mawili ya uchaguzi na mimi ni muwakilishi wa Jimbo la Handeni Mjini, je, Serikali haioni haja ya kuongeza wigo wa idadi ya viijiji ambavyo havijapata umeme upande wa Handeni Mjini hasa katika Kata ya Mlimani Konje, Kideleko kwa Magome, Kwenjugo, Kwadyamba, Malezi na Mabada?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kumekuwa na hali ya kukatika katika kwa umeme kila mara hali inayopelekea kuwapatia hasara wananchi kwa vyombo vyao vya umeme lakini vilevile kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi za uzalishaji. Ni lini Serikali itakomesha tatizo hili wananchi wa Handeni Mjini washiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa REA unapeleka umeme katiika vijiji vyote Tanzania Bara ambavyo havikuwa na umeme ambavyo mpaka sasa havizidi 1974. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyake vyote ambavyo havikuwa na umeme vitapata umeme katika awamu hii ya tatu, mzunguko wa pili ambayo imeanza tayari mwezi wa nne huu na itakamilika kufikia Desemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo linaenda pia kwa Waheshimiwa Wabunge wengine wote wa Tanzania Bara, kwamba vijiji vyote ambavyo havikuwa vimepata umeme vimeingizwa katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili na tutahakikisha tunapeleka umeme katika maeneo yote hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, ni kweli, Tanga kama Mkoa na Handeni ikiwemo imekuwa na matatizo ya kukatika kwa umeme ikiwemo Mikoa wa Mbeya Pamoja na Mkoa wa Kagera. Hata hivyo Wizara kwa kushirikiana na TANESCO imechukua juhudi mbalimbali kuhakikisha inamaliza tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa Mkoa wa Tanga na hasa Handeni tatizo kubwa lilikuwa ni miundombinu chakavu ambayo ilikuwa inapelekea umeme katika maeneo hayo; na hivyo yamefanyika mambo mawili moja ni la sasa na lingine ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme unaokwenda Handeni unatokea katika kituo chetu cha Chalinze unakwenda kwenye substation ya Kasija, unatoka Kasija unakwenda Korogwe – Handeni – Kilindi, na njia ndefu sana ina km. zaidi ya 500. Kwa hiyo, tumebaini kuna nguzo zaidi ya 1300 ambazo zilikuwa zimeoza zimeanza kufanyiwa marekebisho na kuondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka tunavyoongea sasa tayari nguzo zaidi ya 500 zimerekebishwa, na tumehakikisha kwamba kufikia mwishoni mwa mwezi wa nne, nguzo zote 1300 zitakuwa zimerekebishwa na kuhakikisha kwamba basi umeme haukatiki hovyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hatua ya pili ambayo ni ya kudumu na ya muda mrefu tumeshauriana na kukubaliana na wataalam, tumekubaliana tujenge kituo kidogo cha kupoza umeme pale Handeni. Kwa hiyo tutatoa umeme Kasija kwenye kituo cha kupoza umeme cha sasa tutapeleka Handeni, km. 81 kwa gharama ya shilingi bilioni 4nne. Tukishajenga kituo hicho cha kupoza umeme pale Handeni basi tutatoa line moja ya kuhudumia Handeni, tunatoa line moja kwenda Kilindi na line nyingine moja itaenda kwenye machimbo ambayo tumeambiwa itaanzishwa siku si nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo tunahakikisha kwamba basi tatizo la kukatika umeme Wilaya yetu ya Handeni na majimbo yote mawili litakuwa limefikia ukomo na tutakuwa tuna uhakika wa umeme.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri hapo umetoa maelezo marefu na mimi ninakupongeza sana. Sasa hapo umeitaja Mbeya halafu kule hujaeleza tatizo ni nini, maana huko kwingine umesema ni nguzo haya Mbeya unakatika katika kwa nini?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoitaja Mbeya nikaitaja Kagera kwasababu na mimi natokea Kagera ili utakaponipa nafasi ya kuzungumzia Mbeya basi na Kagera nipitie humo humo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbeya tunayo matatizo makubwa mawili, tatizo moja kubwa ni radi ambazo zimekuwa zikisumbua mifumo yetu ya umeme kwenye transfoma. Tatizo hilo pia liko Mkoa wa Kagera. Tulichokifanya katika mikoa hii miwili tumeanza kufunga vifaa vinaitwa auto recloser circuit breaker ambayo vinazuia radi isirudi kwenye maeneo mengine ambayo hayajaathirika hilo ni tatizo moja kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tatizo la pili lilikuwa ni uchakavu wa miundombinu kwenye maeneo hayo. Tumeunda vikosi kazi maalum katika mikoa hiyo mitatu, Mbeya, Tanga na Kagera ya kuhakikisha kwamba kinapitia kila eneo na kubaini tatizo kubwa ni nini ili iiweze kurekebisha. Vikosi kazi hivyo viko kazini, vinafanya kazi; na tunahakikisha kufikia mwezi wa sita, maeneo yote ambayo yalikuwa yana matatizo sugu yatakuwa yamefanyiwa kazi na kurekebishwa.