Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo (3 total)

MHE. REUBEN N. KWAGILWA Aliuliza:-

Je, ni lini wananchi katika mitaa 30 isiyo na umeme Wilayani Handenni watapatiwa umeme kulipia mradi wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reubne Nhamanilo Kwagilwa Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vijiji, mitaa na vitongoji visivyokuwa na umeme kupiitia miradi mbalimbali. Kwa sasa mkandarasi Kampuni ya M/S Sengerema Engineering Ltd. amepewa kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 15 na mitaa vitongoji zaidi ya 30 katika Wilaya ya Handeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hizo zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa KV 0.4 umbali wa km. 27.5, ufungaji wa transfoma 11 za 50 kVA na 100 kVA; pamoja na kuwaunganisha wateja wa awali 669. Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 3.36. Utekelezaji wa mradi umeanza mwezi Februari, 2020 na utakamilika ifikapo Disemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TANESCO inaendelea kuunganisha umeme kwa wateja ambao hawajaunganishiwa umeme katika mitaa na vitongoji vya Tanzania Bara ikiwemo Wilaya ya Handeni kupitia majukumu yake ya kila siku.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji Handeni Trunk Main (HTM)?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim, jumla ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 nchini ukiwemo Mradi wa Maji wa Kitaifa Handeni (Handeni Trunk Main) utakaohudumia vijiji 84 katika Wilaya ya Handeni pamoja na Miji Midogo ya Mkata, Komkonga, Kabuku, Michungwani,Segera pamoja na Mji wa Handeni.

Mheshimiwa Spika, taratibu za kupatikana kwa wakandarasi watakaotekeleza mradi huu zimekamilika na unatarajiwa kuanza wakati wowote katika mwaka wa fedha 2020/2021 na ujenzi wa mradi umepangwa kutekelezwa miezi 24.
MHE. REUBEN N. KWAGILWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Handeni, Mziha hadi Turiani, Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Handeni – Mziha – Turiani yenye urefu wa kilometa 109.36, inahudumiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Handeni – Mziha – Turiani umekamilika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kulipa sehemu ya madai ya mkandarasi wa barabara ya Magole – Turiani yenye urefu wa kilometa 45.2 na kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Turiani – Mziha – Handeni yenye urefu wa kilometa 104.0 kwa kiwango cha lami. Ahsante.