Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nikipongeze Chama changu cha Mapinduzi kwa uwepo wangu hapa, kikiongozwa na Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli; lakini zaidi niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Handeni pamoja na familia yangu kwa kunifanya niwepo mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa mengi hapa kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais. Hotuba yenyewe ilijielekeza kutoa uelekeo wa nchi yetu kwa miaka mitano ijayo, pamoja na yote ambayo Mheshimiwa Rais anayafikiria ni ya muhimu na ambayo yatatuvusha kama taifa kuelekea miaka mitano na pamoja na hoja zote ambazo Wabunge wamezichangia. Kimsingi ukiangalia ni kwamba mambo haya mwisho wa siku yanahitaji fedha; ili tuweze kuyafanya yanahitaji fedha.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nataka nichangie ili kujaribu kuishauri Serikali ni namna gani kama nchi tutajidhatiti kuweza ku-raise hizi fedha ambazo zinahitajika kwa ajili ya kuyatekeleza mambo haya ya kutuvusha miaka mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika, la kwanza ambalo nataka nilishauri kwa Serikali yangu, tutakumbuka mwaka 2019 Bunge lako lilipitisha Finance Act yenye maboresho ya kikodi mengi sana, na moja kati ya maboresho hayo ilikuwa ni kupendekezwa kuanzishwa kwa Ofisi ya Tax Ombudsman, jambo ambalo mpaka leo halijafanyika.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali yangu sikivu ianzishe ofisi hii muhimu ili kuendana na hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 12 ambapo ameelekeza kwamba lazima tuwe tunafanya business disputes, njia pekee ya kufikia hapo ni kuanzisha ofisi hiyo muhimu ya Tax Ombudsman.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nataka nilishauri ni structure yetu ya chombo chetu muhimu cha TRA. Yote tunayotategemea yanategemea makusanyo ya ndani yanayofanywa na ofisi hii ya TRA. Ninachoishauri Serikali yangu ni kwamba TRA isiogope kuajiri vijana kwa sababu waajiriwa wa TRA siyo sawa na waajiriwa wengine wa pande nyingine za idara za Serikali, hawa unaajiri watu ambao wanakwenda kuzalisha moja kwa moja, wanatusaidia kukusanya kodi. Haiwezekani eneo la kimkakati kikodi kama ilivyo Ilala unakuwa bado una ofisi zenye watumishi wasiotosha, tunajichelewesha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nataka nilishauri ni habari ya informal sector. Informal sector inafanya biashara kubwa sana lakini haiwi captured kwenye mifumo ya kikodi. Hili ninapendekeza ufanyike utafiti mzuri na wa kutosha ili watu wetu wa TRA waweze kutoza kodi sehemu zote zinazozalisha ambazo ziko kwenye informal sector. Tusipojaribu kuli-balance hili litakuja kutuingiza matatizoni kwa sababu formal sector inayolipa kodi itakuja nayo kugeuka kuwa informal sector, ni lazima tufanye utafiti na tujaribu kuya- balance haya mawili.

Mheshimiwa Spika, pamoja na makusanyo mazuri yanayofanywa na TRA, ninashauri tusiwe tunapima ufanisi wa TRA kwa kuangalia increment ya makusanyo yao, kwamba mwaka jana walikusanya hapa, mwaka huu wameongeza kiwango hiki, hicho si kipimo peke yake cha kuonesha ufanisi wa taasisi hii muhimu kwetu.

Mheshimiwa Spika, naomba TRA na Serikali yetu kupitia Wizara ya Fedha wawe wanaangalia ratio kati ya taxes zinazokusanywa kwa uwiano na GDP ya kwetu. Tusipofanya hivyo hatari yake ni kwamba tutakuwa tuna- impose tax burden kwa walipakodi wachache kwa sababu increment hiyo unaweza ukakuta ni kwa sababu ya vertical raise kwa kuongeza tu makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara walewale waliopo badala ya kui-spread ile kodi kwa uchumi wote.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nilishauri ni habari ya mamlaka za Kiserikali. Mamlaka zetu za Serikali zinakuwa supplied na wafanyabiashara, sasa wafanyabiashara wanapokuwa wame-supply Serikalini ukichelewa kuwalipa maana yake unajichelewesha mwenyewe kuchukua kodi yako. Ni bora hata ukafanyika utaratibu kama fedha ya kuwalipa inakuwa haijapatikana, ile component ambayo ina kodi ndani ilipwe kwanza halafu ndiyo waendelee na procedures nyingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Reuben Kwagilwa.

MHE KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii. Moja kwa moja nijielekeze kwenye kuchangia lakini sababu dakika tano ni chache sitaingia ndani sana ila nataka nitoe ushauri mmoja kabla sijatoa maelezo yangu ya jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ambao nataka nitoe, kuna suala hapa limezungumzwa sana nalo ni la maji. Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 pamoja na Sheria ya Maji Na. 5 ya mwaka 2019, Sheria hii ya Maji ya mwaka 2019 ndiyo ilianzisha RUWASA lakini kana kwamba haitoshi ikaenda mbele ikaleta Mfuko wa Maji wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuwa anazunguka kufanya kampeni kwenye hotuba yake amekiri, namnukuu anasema: “Hata hivyo, napenda nikiri nilipokuwa kwenye kampeni moja ya changamoto kubwa niliyoelezwa na wananchi ilikuwa ni shida ya maji hususan maeneo ya vijijini”. Kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaliona hili, nashauri Serikali iirejeshe hapa ile Sheria ya Maji, Na. 5 iliyotungwa na Bunge letu ya mwaka 2019 ili tuirekebishe kidogo. Marekebisho yake yaweje? Tumeweka pale source ya fedha za huu Mfuko; tumesema tutatoza shilingi 50 kwenye petrol na shilingi 50 kwenye diesel. Nachoomba ili tuweze kuisaidia RUWASA lazima sheria ije hapa tuitengeneze iweze ku-state ni asilimia ngapi iende kwenye maji katika hiyo shilingi 100 inayotozwa kwenye petrol and diesel. Kwa sababu tukiiacha hivi miradi ya mjini inatumia fedha nyingi kuliko miradi iliyopo vijijini. Kwa hiyo, kuna haja ya kufanya hayo marekebisho ya hiyo sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la jumla sana mimi nataka tu niseme kwamba ndugu zangu unapopanga la kwanza unatumia takwimu na pili unatumia assumptions. Kwenye hili eneo la takwimu tusipojizatiti vizuri kuboresha namna ya upatikanaji wa takwimu kwenye nchi yetu kila tunapopanga tutakuwa tunajikuta tuko nje ya malengo. Kwa hiyo, ni vema tuboreshe sana eneo hili la takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye huu Mpango ambao ndiyo mpango wa mwisho kuelekea Vision yetu ya 2025 kama Taifa kukamilika wakati nimekuwa nikiusoma mara kwa mara na kuurejea sijaona mahali ambapo Mpango huu umeweka provision kwamba baada ya Vision 2025 kukamilika inayotekelezwa mwishoni kwenye huu Mpango ni kitu gani kitafuata? Vision nyingine itakapotengenezwa, sijaona provision kwenye Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine tunapopanga ni vema tukajua financing mode ya hii miradi tunayoipanga especially hii miradi ambayo tunaita flagship projects. Ukifanya tathmini vizuri kwenye Mpango uliopita utagundua tulikuwa na miradi karibia 20 na yote ni mikubwa. Miradi 20 yote hii hatuwezi kui-finance na kodi za wananchi za kwetu za ndani. Kwa hiyo, ni vema tujikite kama taifa na ni wakati muafaka sasa tukubali tu kwamba ili tuitengeneze hii miradi ni lazima tutafute sources nyingine, namna nyingine ya kuitekeleza ama kwa partnership au kwa kukopa lakini tuifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huohuo lazima twende na tahadhari, tumejaribu kufanya partnership pale Liganga na Mchuchuma na mradi huu umezungumzwa sana tokea tuko shule na bado mpaka leo haujatekelezeka. Naishauri Serikali yangu sikivu kama hili la Liganga na Mchuchuma limeshindikana kwa mwekezaji huyo tuliyenaye, ni vyema tukaenda mbele tukatafuta mtu mwingine kwa sababu dunia kwa sasa ni chuma na mafuta. Ni bidhaa mbili tu zinazotawala soko la dunia za mafuta na chuma. Kwa hiyo, tunapochukua muda mrefu miaka 7 toka 2014 tunafanya mazungumzo tunajichelewesha tu wenyewe. Tunahitaji tu- mobilize fedha kutokana na hii miradi ya kimkakati ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, mimi ya kwangu yalikuwa hayo machache. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii ili niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupanga ni taaluma, lakini kwa Taifa letu na kwa Serikali yetu kupanga si tatizo. Mpango huu tulionao ni mzuri sana kuliko mipango mingi sana ya nchi nyingi hapa Afrika, lakini shida tulionao sisi kwenye kupanga ni kutekeleza Mpango tuliouweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sitaongelea mengi isipokuwa nataka nijielekeze eneo moja tu, la Mradi Mkubwa tulionao wa Standard Gauge Railway, tunayoijenga. Standard Gauge Railway tunayoijenga ukijumlisha tu zile njia kilometa zinazojengwa tunatakiwa tujenge kilometa 4,886, hapo naongelea njia tu, siongelei mahala ambapo reli zinapishana. Mpaka sasa tumeshajenga kipande cha Dar es Salaam kuja Morogoro kilometa 300 na tunaendelea na kipande cha Morogoro – Makutupora kilometa 422, lakini vilevile tuko upande ule mwingine wa Isaka na Mwanza kilometa 249.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa aina ya financing ya mradi huu tunavyoindesha tukiendelea nayo tutaujenga Mradi huu wa Standard Gauge kwa nchi nzima kwa miaka 81, miaka 81. Ikiwa miaka mitano tumejenga kilometa 300 ndio ambazo ziko above 90 then kilometa 4,886 tutazijenga kwa miaka 81. Hii katika nchi ambayo inapambana kutafuta maendeleo ni kitu hakikubaliki, ni kitu hakikubaliki. Hivyo vipande nilivyo vitaja ambavyo vinajengwa vimetugharimu takriban trilioni 11. Trilioni 11 ni Idle Investment kwa sababu gani, kwa sababu hatutakamilisha leo ili tuanze kutumia mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokishauri Serikali yetu iondekane na habari ya Traditional Methods za ku-finance miradi hii mikubwa. Kwanza tunajipa pressure kama Serikali, ya ku-finance mradi huu halafu tunashindwa kupeleka huduma kwa wananchi ambazo ni za kila siku. Kwa hiyo ninachokishauri Wizara ya Fedha waangalie utaratibu wa ku- finance mradi huu Infrastructure Bond. Wamefanya hivyo nchi za wenzetu, ukienda Benin wamefanya, ukienda Tunisia wamefanya. Hii inatupa ahueni ya kutekeleza mradi huu na kuutekeleza kwa wakati. Tunapoendelea kutekeleza mradi huu hivi kidogo kidogo ni hasara kwa Taifa letu, ni vile tu hatui- merge hii hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa faida ya wasiofahamu na Watanzania kwa ujumla, tunatakiwa tuitoe reli itoke Dar es Salaam iende mpaka Tabora kwa kupitia Singida, ikifika Tabora iende Isaka Shinyanga mpaka Mwanza, ikitoka Tabora iende Keeza ili tukahudumie Kigali na Burundi, ikitoka hapo Tabora tuipeleke Kaliua kwa ndugu yangu hapa, iende Uvinza mpaka Kigoma tukaihudumie Kongo na tukitoka Kaliua tuje Mpanda mpaka Katema; hiyo ni Reli ya Kati tunayojenga. Bado kuna kipande cha Tanga, Musoma, Arusha kilometa takriban 1,233; na hapo hapo bado kuna kipande cha Mtwara – Mbambabei kilometa 10,092.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni kitu serious sana, hatuwezi tu kuendesha mradi huu kwa kutumia mapato ya ndani tutawaumiza Watanzania na tunajichelewesha wenyewe kupeleka maendeleo ambayo yanahusu huduma za moja kwa moja za wananchi za kila siku kama vile elimu na afya; na ndio maana kwa mwenendo huu wananchi wa Handeni mpaka sasa hatuja pata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa mradi huu kwa pamoja kutatusaidia sana kama Taifa kwanza kuifungua Bandari yetu ili iongeze mzigo unaopita pale. Kwa sasa hivi tunapitisha tani milioni 17 ukilinganisha na wenzetu wakenya wanapitisha pale Mombasa tani milioni 37. Kukamilika kwa pamoja na kwa wakati mmoja kutatusaidia sana kupata mapato kupitia mradi huu, kwa maana TRA wataweza kukusanya lakini vilevile wananchi wetu uchumi wao unataweza kuwa activated.

Mheshimiwa Naibu Spika, jinsi tunavyojenga kwa vipande vipande hivi na kuchukua muda mrefu kuna maeneo ya nchi yetu yatabaki kuwa-disadvantaged. Kwa mfano kipande hiki cha Mbambabei – Mtwara kitabaki kuwa ni historia tu ikiwa hatutatekeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma, viability ya hii reli hapa haipo. Vivyo hivyo kipande kile cha kutoka Tanga kwenda Arusha kwenda Musoma kama hatukuimarisha vile vipaumbele tulivyoweka ukanda ule ikiwemo soda ash pale Lake Natron hakuna viability ya mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lipo bomba linalotoka Uganda Hoima kuja Chongoleani Tanga. Kwa vyovyote vile mafuta yatakapofika Tanga yatahitaji reli hii hii kuyarudisha yakisha kuwa refind. Kwa hiyo Serikali ione umuhimu wa kwenda kukopa kwa kutumia Infrastructure Bond ili tutekeleze mradi huu kwa pamoja kwa mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo na baada ya kushauri hilo ni malizie kwa kusema; limezungumzwa hapa asubuhi kidogo lakini halikukaziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 ambayo inatu-guide kuanzia mwanzo tunapotengeneza bajeti mpaka tunapoitisha bajeti hapa Bungeni, lakini sheria tukishapitisha bajeti hapa wenzetu wa Serikali wanapokwenda kutekeleza bejeti hakuna Sheria ya Monitoring na Evaluation. Kwa maana hiyo tunamuomba hapa Waziri wa Sera Serikali yetu hapa walete Sera. Kwanza wao watunge Sera ya Monitoring na Evaluation ili wailete hapa tuitungie sheria. Ndiyo maana ripoti hii ya CAG ambayo tunakwenda kuijadili ni aibu ni aibu ni aibu ni aibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tusipofika mahala tukatunga sheria hiyo; huwezi; kwa mfano mradi wa bilioni 380 unaotekelezwa, wa maji kule Handeni, unaojengwa kutoa Maji Korogwe kuyaleta Handeni eti ukasimamiwe na Mtendaji wa Kata, usimamiwe na Diwani. Lazima tutunge sheria ikae vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mpango uliopo mezani, naomba kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi).