Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (12 total)

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali lakini nilikuwa nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itafanya tathmini ya tamaduni ambazo tunazo nchini ambazo haziendani na wakati huu na mila zetu na desturi ambazo zinakwenda kukwamisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili mna mkakati gani wa kuanzisha somo la maadili kwenye mtaala yetu ya elimu hapa nchini? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikibainisha mila na desturi zisizofaa nakuchukua hatua kadhaa, zikiwemo kutoa elimu kwa jamii pamoja na uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kutekeleza sera ya utamaduni ya mwaka 1997 Sura ya Nane na kifungu 1.3.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, it takes a village to raise a child, kwa hiyo pamoja na wajibu wa Serikali kulinda mila na desturi zetu haiondoi wajibu wa moja kwa moja wa wazazi walezi na jamii kujenga misingi imara ya makuzi ya vijana wetu katika ngazi ya familia na kaya zetu kwa kushirikiana na viongozi wetu wa kimila na viongozi wetu wa dini nchini kote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Bahati, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kutakuwa na somo la maadili kwenye mitaala mipya na itakuwa ni lazima kila mwanafunzi kulisoma. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa watu wengi ambao wameiona historia ya Tanzania na Zanzibar wameandika vitabu katika historia hii.

Je, ni lini vitabu vile vitatafsiriwa, Serikali itachukua maamuzi ya kutengeneza filamu ya vitabu vile ili kizazi kinachokuja kiweze kujivunia na kuona uhalisia wa historia ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa lengo la Serikali siyo tu kuhifadhi historia ya nchi na mashujaa wetu kwenye filamu, lakini ni kuhifadhi katika kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa. Kwa hivyo Serikali kwa sasa inafanya juhudi kubwa kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaongezwa kwenye tasnia ya filamu nchini kuhakikisha hilo linatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kudhibitisha hilo, ni juma lililopita tu Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, mama yangu, Mheshimiwa Balozi Pindi Hazara Chana, alihudhuria utiaji saini mkataba wa makubaliano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na Taasisi ya Mashirikiano ya Kimataifa ya Korea Kusini (BFIC), makubaliano ambayo pamoja na mambo mengine yanakwenda kuona uwekezaji mkubwa ukiongezeka kwenye tasnia ya filamu nchini ambapo filamu ambazo unazizungumzia Mheshimiwa zitakwenda kufanywa kwenye kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa, nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara hii inaangalia sana suala la maslahi ya wasanii na michezo kwa ujumla; ni lini Serikali itapitia upya makato inayokata katika mambo ya michezo? Kwa mfano juzi Simba wamepata milioni 180 katika 450; ni lini itapitia makato haya ambayo ni kandamizi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na swali la Mheshimiwa Mbunge Isack kuwa liko pembeni kabisa ya swali la msingi, lakini kimsingi tunaangalia utaratibu ambao utawezesha vilabu vyetu viweze kuendelea kufaidika zaidi. Lakini kuna gharama kubwa za uendeshaji wa michezo inayotajwa na taasisi zetu zinaingia gharama kubwa ambayo inatoka mifukoni kwao kuweza kuifanya michezo hii ifanikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo pamoja na lengo letu la kuhakikisha timu zetu zinafaidika, lakini kuna gharama kubwa ambazo taasisi zetu zitashindwa kujiendesha kama tutazizuia moja kwa moja kukata makato yale, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itawapa vitambulisho machifu wetu ili kuweza kuwatambua kwamba ni machifu wa nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha tunawekeza nguvu nyingi kuhakikisha utamaduni wetu haupotei. Na miongoni mwa mambo ambayo yanafanyika ni kutambua uwepo wa machifu wetu. Na hilo limefanywa hata na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukaa kikao na machifu mbalimbali – siyo mara moja – na kuwatambua kwenye masuala mbalimbali ya sherehe za Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, machifu bado wanatambulika na Serikali, lakini juhudi mbalimbali bado zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kutambulika kwao kunafahamika Kitaifa na kimataifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, katika dhana ileile ya kuendelea kutangaza utalii wa Taifa letu, je, Serikali haioni ni wakati sahihi wa kutengeneza filamu maalum ya kueleza historia ya Ukoo wa Simba wa Bob Junior na namna ambavyo ilisisimua Taifa na dunia kuhusu kifo cha Bob Junior?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazo zuri ambalo amelitoa, na sisi kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii tunaomba tulichukue na tutalifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa nusu ya Jimbo la Kawe kwa maana ya Msasani, Masaki, Oysterbay, Kunduchi, Mbweni, Kawe, Bunju, Sea Cliff na Coco yote iko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kuendeleza hii michezo ya Bahari kwa ajili ya afya, burudani na kipato cha watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, je, utakubali Jumapili hii tuandamane pamoja tukafungue Ligi ya Rede kwa michezo inofanyika katika Jimbo la Kawe? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuchukua nafasi hii ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Josephat Gwajima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kwa kuona fursa kubwa iliyopo katika mchezo wa soka la ufukweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, soka la ufukweni katika nchi hii limeanzishwa rasmi mwaka 2014 na ni kwa miaka tisa tu ambayo tumekuwa tukilifanya, lakini limeonyesha kuwa na mafanikio makubwa. Kwa sasa tuko Namba Tano kwa Bara la Afrika kwa soka la ufukweni na Namba 42 kwenye rank za FIFA za kidunia kwa soka la ufukweni, namba ambazo hili soka letu la kawaida hatujawahi kuzifikia na pengine itatuchukua muda mrefu kidogo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mafanikio haya yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na TFF kwa kushirikiana na Serikali, kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaweka mkazo kwenye michezo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TFF wanao mpango mkakati wa miaka mitano, ambao pamoja na mambo mengine unahakikisha kwamba soka la ufukweni linafundishwa mashuleni na vyuoni na kila Mkoa ambao una fukwe kuweza kuwa na ligi yake kwa ajili ya soka la ufukweni. Lengo ni katika kipindi cha miaka mitano hii inayofuata tuwe na wachezaji angalau 10,000 na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali imeanzisha mazungumzo na JKT na wadau wengine kadhaa ili kuhakikisha tunaongeza uwekezaji kwa ajili ya soka la ufukweni. Pia, kumekuwa na mashindano ya Copa Dar es Salaam ambayo yanazishirikisha nchi mbalimbali kama Burundi, Uganda, Comoro, Ushelisheli na Malawi, mwaka huu tuna mpango wa kuwaalika Kenya, Oman, Morocco na Senegal. Kwa hiyo, tutakuwa na Ligi ya Soka la Ufukweni yenye nchi Tisa, ambapo ni wazi kabisa itaongeza Pato la Taifa lakini wachezaji wetu wengi watashiriki na itatoa ajira za moja kwa moja na ajira nyingi nyingine zinazozunguka mchezo huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, najua Askofu utakuwa na maono, umengundua kama Jumapili ninao muda na tutaambatana mimi na wewe kwa ajili ya kwenda kuanzisha Ligi yako ya rede pale Jimboni Kawe. Ahsante. (Makofi/Kicheko)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninashukuru Serikali kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, kuna academies za mchezo wa mpira wa miguu kama vile Kilombero Soccernet Academy ambazo zimesajiliwa rasmi na ziko pale Wilaya ya Kilombero, lakini zina uhaba mkubwa wa vifaa.

Je, kwa dharura, Wizara haioni kwamba inaweza ikachukua hatua za kutafuta vifaa, hata kama ni mipira, jersey, ikazipelekea hizi academies ambazo zimesajiliwa rasmi na TFF?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilimwomba Mheshimiwa Naibu Wazri mipira 100 ya vijijini na aliniahidi atanipatia; je, lini tunakwenda kukabidhi mimi na yeye mipira hiyo Ifakara na kukiamsha pale Ifakara Mjini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kama nilivyosema kwa sasa Serikali inachoweza kufanya kutokana na upatikanaji wa fedha ni kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo kama vile nyasi bandia na viambata vyake. Haya mengine kwa kadri fedha zitakavyopatikana tutaendelea kuvi-support vituo hivi na kuhakikisha vinapata nguvu kupitia Serikalini vilevile, ahsante.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuirejesha Ligi ya Muungano?

Swali langu la pili, je, ushirikiano wa ZFF na TFF unasaidia Soka la Zanzibar la Wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha Ligi ya Muungano inaanzishwa upya na tunafahamu umuhimu wake kwenye kuimarisha ushirikiano hasa kwenye upande wa michezo. Kwa hivyo, kwa nyakati tofauti TFF na ZFF wamekuwa wakikaa kuangalia namna bora ya kuianzisha tena Ligi ya Muungano, japokuwa wanapata changamoto kwenye kupata udhamini wa kulifanya hili lakini nikuhakikishie dhamira ipo na tutahakikisha Ligi ya Muungano inaanza tena.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Ligi ya Wanawake, TFF na ZFF zimekuwa zikiendesha program mbalimbali za kiutawala na makocha wanawake kwa Soka la Zanzibar na unaweza kuona miongoni mwa mafanikio ambayo yameshapatikana ni kwa timu za wanawake za Zanzibar kufanya vizuri kwenye mashindano ya CECAFA. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki na mnafahamu kamati za kitaifa nyingi ni za wazi. Kwa mfano, ile Kamati ya Makinikia mnaikumbuka, kamati ya hamasa ya Taifa Stars inafahamika. Kwa nini, kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki? Je, Serikali wako tayari kuitangaza ili tuwafahamu?

Swali la pili, mchakato ni wa muda mrefu sana nadhani unafahamu. Serikali inahitaji muda gani wa ziada ili kuhitimisha jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Antipas Mgungusi kwamba, Kamati hii haikuwa ya siri. Kamati hii ilitangazwa tarehe 20 Julai, 2022 baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti, wake alikuwa Profesa Hermas Mwansoko na Katibu wake alikuwa Dkt. Emmanuel Temu, ikiwa na Wajumbe tisa, wakiwamo Masoud Ali Kipanya, Mrisho Mpoto, Ndugu Khadija Mwanamboka, Ndugu Mwanajuma Ali na wengineo. Kamati hii ilishakamilisha kazi yake kwa hiyo, hili jambo limerudi kwa Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ndiyo inafanya hatua za mwishoni za kukamilisha mchakato huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hamu yetu kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuona kwamba, mchakato huu unakamilika kama ambavyo ni hamu ya Mheshimiwa Mbunge Antipas. Kwa hivyo, mahali ilipofika sasa hivi ni mwishoni kabisa. Hivyo, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni inafanya michakato wa kumalizia kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwaka huu wa 2024 hautakwisha kabla hatujajipatia vazi la Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Kalenga limekuwa kinara wa kuendeleza mila na tamaduni; je, Serikali haioni haja sasa ya kutujengea hata kituo cha utamaduni katika Jimbo hilo la Kalenga ili tuweze kuendeleza utamaduni wetu wa Kihehe? (Makofi)

Swali namba mbili, kwa kuwa Makumbusho ya Mkwawa ambayo ndiyo sehemu ya kuenzi mila na tamaduni zetu yako katika eneo la makaburi ya familia ya Mkwawa na Uchifu wa Mkwawa upo hai. Je, Serikali haioni haja sasa katika vile viingilio wakawa wanatupa hata asilimia moja au mbili ili kuendelea kuimarisha ule utamaduni wetu na uchifu wetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kuhusuana na kujenga kituo cha utamaduni pele Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, inaendelea kufanya tathmini ya kutambua maeneo ya kiutamaduni ili kutoa maelekezo mahsusi kwa mamlaka husika za mikoa na wilaya, namna ya kuyaenzi na kuyahifadhi maeneo haya. Kwa hiyo, hili la kujenga kituo cha utamaduni pale Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge ninalichukua na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo italifanyia kazi na muda utakaporuhusu tutaweza kufanya hivyo. (Makofi)

Swali lake la pili kuhusuana na sehemu ya malipo ya maonesho ya kaburi la Chifu Mkwawa kwenda kwa familia, namuahidi Mheshimiwa Mbunge pia nalichukua na tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Makumbusho ya Taifa kuona namna ambavyo hili linaweza kufanyika na familia ya Chifu Mkwawa ikaweza kufaidika na sehemu ya kiingilio cha makumbusho yale, ahsante. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya utafiti gani ili kujua makabila yaliyoko nchini, kuweza kuyasaidia na kuyaendeleza kuwa kivutio ili kuweza kuiingiza Serikali Pato la Taifa na watalii zaidi ya Wamasai? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, mpaka sasa tafiti 286 zimeshafanyika, tunachofanya ni mwendelezo wa tafiti hizo na kuona namna ambavyo tunaweza kutumia ufahamu tulioupata kupitia tafiti hizo ili kuyaenzi na kuhifadhi tamaduni za makabila mbalimbali zaidi ya Wamasai hapa nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki na mnafahamu kamati za kitaifa nyingi ni za wazi. Kwa mfano, ile Kamati ya Makinikia mnaikumbuka, kamati ya hamasa ya Taifa Stars inafahamika. Kwa nini, kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki? Je, Serikali wako tayari kuitangaza ili tuwafahamu?

Swali la pili, mchakato ni wa muda mrefu sana nadhani unafahamu. Serikali inahitaji muda gani wa ziada ili kuhitimisha jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Antipas Mgungusi kwamba, Kamati hii haikuwa ya siri. Kamati hii ilitangazwa tarehe 20 Julai, 2022 baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti, wake alikuwa Profesa Hermas Mwansoko na Katibu wake alikuwa Dkt. Emmanuel Temu, ikiwa na Wajumbe tisa, wakiwamo Masoud Ali Kipanya, Mrisho Mpoto, Ndugu Khadija Mwanamboka, Ndugu Mwanajuma Ali na wengineo. Kamati hii ilishakamilisha kazi yake kwa hiyo, hili jambo limerudi kwa Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ndiyo inafanya hatua za mwishoni za kukamilisha mchakato huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hamu yetu kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuona kwamba, mchakato huu unakamilika kama ambavyo ni hamu ya Mheshimiwa Mbunge Antipas. Kwa hivyo, mahali ilipofika sasa hivi ni mwishoni kabisa. Hivyo, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni inafanya michakato wa kumalizia kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwaka huu wa 2024 hautakwisha kabla hatujajipatia vazi la Taifa, ahsante. (Makofi)