Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (7 total)

MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza:-

Kasi ya ujenzi wa barabara ya Muheza – Amani sio ya kuridhisha na hadi sasa maeneo korofi bado hayajafikiwa:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na awamu ya pili katika ujenzi wa barabara hiyo kuanzia Amani kuelekea Muheza ili kutatua changamoto zilizopo wakati ujenzi wa barabara ukiendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara ya Muheza – Amani yenye urefu wa kilometa 40, Serikali iliamua kuijenga kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2015. Awamu ya kwanza ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sasa yenye urefu wa kilometa saba kuanzia Muheza kuelekea Bombani inaendelea na imefikia asilimia 70.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza ya mradi huu unaoendelea, ujenzi wa sehemu ya pili ya kuanzia Bombani hadi Amani utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kukamilisha ujenzi wa barabara yote kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za kukamilisha ujenzi wa sehemu ya barabara iliyobaki, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ikiwemo sehemu korofi ili kuhakikisha inapitika majira yote. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, barabara hii ilitengewa shilingi milioni 600 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali, ahsante.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha kuwa kunajengwa Kiwanda cha Kuchakata Viungo Wilayani Muheza?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa uchumi nchini, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa Sekta Binafsi ili iweze kuanzisha na kuendeleza shughuli za viwanda hapa nchini. Aidha, Wizara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) inaendelea kutoa huduma mbalimbali zinazohusiana na uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati ikiwa ni pamoja na mafunzo juu ya usindikaji wa mazao ya kilimo, uendelezaji teknolojia rahisi za uongezaji thamani mazao ya kilimo, utafutaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali na kutoa mikopo kwa masharti nafuu kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali Wananchi (NEDF).

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Muheza ina viwanda vidogo vitatu kwa ajili ya kuchakata viungo. Viwanda vinavyofanya kazi ni viwili ambavyo ni Trianon Investment Limited kilichopo eneo la Lusanga, Muheza Mjini, ambacho mwaka 2020 kimeuza nje jumla ya tani 120 za viungo ambavyo vimechakatwa katika kiwanda hicho. Kiwanda cha pili ni G.F.P Organic Limited kilichopo barabara ya kuelekea Pangani ambacho mwaka 2020 kiliuza nje jumla ya tani 80 za viungo.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivyo vinahudumiwa na Shirika letu la SIDO na vimetoa ajira za kudumu zipatazo 30 na vibarua zaidi ya 50. Viungo vinavyochakatwa ni pamoja na iliki, mdalasini, pilipili manga, karafuu, mchaichai, binzari, maganda ya machungwa na limao. Aidha, kiwanda cha Raza Agriculture Limited kilichopo katika Kijiji cha Muungano, Muheza, kinatarajia kuanza uzalishaji hivi karibuni.

Pamoja na viwanda hivyo wilayani Muheza kuna wajasiriamali wadogo wengi ambao husindika viungo katika ngazi za kaya (household level). Serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) inawasaida wajasiriamali hao kuwapatia mafunzo na ushauri ili waweze kuzalisha kwa ubora unaotakiwa na kuuza bidhaa zao katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha Sekta Binafsi kuwekeza zaidi katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata viungo nchini ikiwemo katika Jimbo la Mheshimiwa Hamis, Jimbo la Muheza.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaruhusu tena usafirishaji wa vipepeo nje ya nchi ili kuongeza vipato vya wananchi wa Muheza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwin’juma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 17/03/2016, Serikali ilisitisha biashara ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi. Tatizo kubwa lililosababisha maamuzi hayo lilikuwa ni ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za kufanya biashara hiyo, ikiwa ni pamoja na kutokea wimbi kubwa la utoroshaji wa wanyamapori hai. Vilevile Serikali iligundua matokeo hasi yanayoendelea kujitokeza kwa kuendelea kufanya biashara hiyo ikiwemo kuhamisha rasilimali ya wanyamapori nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali inafanya tathmini ya kina ili kubaini faida na hasara ya usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi kwa ajili ya kujiridhisha na biashara hiyo. Baada ya tathmini hiyo Serikali itatoa tamko kwa wadau wa biashara hiyo kuhusu uamuzi uliofikiwa.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawaruhusu wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Sakale, Kata ya Mbomele, Wilayani Muheza kuanza uchimbaji wa madini ya dhahabu yaliyothibitishwa kupatikana katika kijiji hicho?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za uchimbaji mdogo katika eneo la Sakale zilikuwepo kati ya mwaka 2004 na mwaka 2016. Baada ya ziara za viongozi wa Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Muheza, Wizara ya Madini pamoja na NEMC na pia Mheshimiwa Mbunge mwenyewe iligundulika kuwa uchimbaji huo unafanyika katika chanzo cha Mto Zigi ambacho ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa Muheza na Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya wataalam wa mazingira iliyofanyika mwaka 2018 Oktoba, ilionyesha kuwa athari za kimazingira ni kubwa endapo uchimbaji utaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo na kwa kuhifadhi chanzo cha maji katika bonde la Mto Zigi, uchimbaji mdogo wa dhahabu katika Kijiji cha Sakale, Kata ya Mbomele, Wilayani Muheza hauruhusiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha upatikanaji wa soko la machungwa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ya machungwa ambayo huzalishwa kwa wingi katika Mkoa wa Tanga hususan Wilaya ya Muheza, Wizara kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeendelea kutafuta masoko katika nchi mbalimbali, ambapo mwaka 2021/2022 liliweza kupatikana soko la machungwa katika nchi za falme za Kiarabu. Vile vile, Serikali inaendelea kutoa elimu ya ufungashaji na usindikaji wa matunda ya aina zote kwa wazalishaji ili kuyaongezea thamani na kuweza kunufaika na fursa hiyo ndani ya nchi ambayo itaongeza soko kwa matunda yakiwemo machungwa. Nakushukuru sana.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa maksudi wa kuwavutia Wawekezaji katika Kilimo cha zao la Muhogo Wilayani Muheza?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mkakati wa kuendeleza tasnia ya muhogo wa miaka kumi kati yam waka 2020 mpaka mwaka 2030 unaolenga kuimarisha utafiti na uzalishaji wa mbegu bora za zao la muhogo, kuongeza uzalishaji wa muhogo kutoka wastani wa tani 8.2 hadi tani 24 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Serikali inaendelea na jitihada za kuwavutia wawekezaji ambapo mwaka 2018 kampuni ya CMTL-Tanzania Limited ilipatikana na kupewa eneo la ekari 10 katika Kata ya Mbaramo kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata muhogo. Serikali inafuatilia ili mwekezaji awekeze kulingana na malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la MEDA inasambaza jumla ya pingili 700,000 za mbegu za mihogo aina ya Mkuranga 1 na Kiroba katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa ajili ya kupandwa katika eneo la ekari 175.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha matengenezo ya miundombinu ya usambazaji maji katika kata sita za Muheza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka 2021/2022 inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya maji katika kata sita za Muheza ambazo ni Mbaramo, Genge, Masuguru, Tanganyika, Majengo na Kwemkabala. Ukarabati huo unahusisha kazi ya kubadilisha bomba kuu lenye urefu wa kilomita Mbili na ukarabati wa bomba la usambazaji maji lenye urefu wa kilomita 14.5. Kazi hii itakamilika mwezi Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imepanga kuendelea na ukarabati wa miundombinu katika Kata Sita za Mji wa Muheza ikiwa ni pamoja na kusambaza maji katika maeneo ambapo mtandao wa usambazaji maji haujafika kwenye Kata hizo.