Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (8 total)

MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha jamii inarudi katika maadili mema kutokana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kujibu swali kama Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba dakika moja niweze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kwa uhai na kila kinachotokea kwenye maisha yangu likiwemo na hili. (Makofi)

Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yangu Daktari Samia Suluhu Hassan kwa imani hii kubwa aliyonipa na nimuahidi ya kwamba nitatekeleza majukumu yangu kwa weledi tuwatendee haki wananchi tunao wahudumia. (Makofi)

Niwashukuru sana wananchi wa Muheza kwa kuendelea kuniunga mkono na ushirikiano mkubwa wanaonipa na niwahakikishie Muheza bado Mbunge mnaye na nitahakikisha nawaheshimisha. (Makofi)

Nikushukuru wewe Spika na Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania kwa miongozo na maelekezo ya kila mara, hili ni darasa kubwa na ninaendela kujifunza. Mwisho niishukuru familia yangu mke na watoto wangu kwa mapenzi mengi yanayofanya kichwa changu kiendelee kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, nijibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inachukua hatua zifuatazo ili kukabiliana na hali hiyo: -

(i) Wizara imeaandaa mwongozo wa maadili na utamaduni wa Mtanzania uliozinduliwa Tarehe 02 Julai, 2022 ambao unaendelea kusambazwa;

(ii) Kutoa elimu ya maadili na kufanya uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kwa jamii kupitia Vyombo vya Habari. Mathalani, katika kipindi cha Januari – Aprili, 2023 Wizara imefanya vipindi 11. Pia Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri 16 kati ya Halmashauri 184 nchini wamefanya vipindi 21 kupitia vyombo vya Habari;

(iii) Kutoa elimu ya maadili kwa wadau wa malezi na makuzi ikiwemo Viongozi wa Dini, wamiliki wa vituo vya malezi na shule za awali na Wasanii. Aidha Wizara inameandaa mdahalo na semina maalum kwa Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakati wa Tamasha la Pili la Kitaifa la Utamaduni litakalofanyika Mkoani Njombe tarehe 19-21 Mei, 2023;

(iv) Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Viongozi wa Dini, Machifu na Viongozi wa Kimila pamoja na Wizara zenye dhamana ya malezi na makuzi ya watoto na vijana pamoja na usimamizi wa maadili nchini katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya pamoja, ahsante.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI K.n.y. MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuandaa Filamu zenye kueleza Historia ya Nchi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na wadau imewezesha uzalishaji wa filamu zinazohifadhi na kuelezea historia ya nchi yetu.

Mfano Makala ya Uzalendo iliyoandaliwa na Bodi ya Filamu mwaka 2021 kupitia muandaaji filamu Bwana Adam Juma inaelezea historia ya viongozi wetu na ushujaa wao katika kuipambania nchi. Pia, mwaka 2022 Bodi kupitia Studio za Wanene iliandaa makala inayotangaza mandhari ya kupiga picha za filamu na kuelezea maeneo ya kihistoria yaliyopo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Bodi ya Filamu inaendelea na maandalizi ya filamu inayohusu maisha ya Chifu Mkwawa iitwayo Mkwavinyika. Pia kwa kushirikiana na wadau wa filamu, Bodi inaratibu mpango mahsusi wa uandaaji wa filamu zinazohusu maisha ya viongozi wetu, ambapo itaanza na filamu ya Bibi Titi Mohammed, ikifuatiwa na ya Chifu Kingalu, Mtemi Mirambo pamoja na Mwalimu Nyerere.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa kuitumia Bahari kwa michezo mbalimbali ya majini ili kuongeza kipato cha wananchi wa Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995, Ibara ya 7(i) hadi (vi), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo taasisi, mashirika na watu binafsi. Hata hivyo, Wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wako katika mkakati wa kuziendeleza fukwe za Kunduchi na Kigamboni katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kukuza mchezo wa Soka la Ufukweni ambao tayari TFF wameshaanzisha Ligi yake ambayo ilianza tangu Tarehe 19/08/2023 na inafanyika kwa siku za Jumamosi na Jumapili katika fukwe za Koko, na jumla ya Timu 16 zinashiriki Ligi hiyo. Aidha, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kuwa mwezi Julai, 2023, Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ilishiriki mashindano ya mchezo huo Barani Afrika yaliyofanyika Nchini Tunisia na kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Morocco na Senegal.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa rai kwa wadau wa michezo mingine kama Mitumbwi na Ngalawa, Kuogelea, Mpira wa Kikapu na Wavu kuwekeza katika michezo hii ya ufukweni na kuziendeleza fukwe tulizonazo ili kukidhi matakwa ya michezo yao, kwani pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi, michezo hii pia inasaidia kuimarisha afya na kutoa burudani kwa wananchi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuwawezesha wadau wa michezo kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo hasa mpira wa miguu?

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na kwa ridhaa yako, naomba nitumie sekunde chache kuwapongeza vijana wetu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa ushindi wa goli moja kwa bila walioupata dhidi ya Niger jana, ushindi ambao unatuweka katika nafasi nzuri na uwezekano mkubwa wa kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazochezwa mwakani kule Senegal. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo niliwaahidi jana ile milioni 10 yao ya goli la mama kutoka kwa shabiki na mwezeshaji namba moja wa timu ya Taifa itawafikia leo kwa sababu mama hana kona kona, akishaahidi lazima litekelezwe, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Abubakari Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuwezesha wadau kuwekeza kwenye uzalishaji wa vipaji vya michezo hasa mpira wa miguu imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuweka miongozo mahususi ya uanzishwaji na uendeleshaji wa shule maalum za kuibua; kukuza na kuendeleza vipaji (sports academies); kuweka mfumo madhubuti wa usajili wa academia na vituo vya michezo; kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo kama vile nyasi bandia na viambata vyake; kutoa utaalamu na ushauri katika ujenzi wa miundombinu ya michezo; na kuandaa mashindano ya UMISETA kwa shule za sekondari na UMITASHUMITA kwa shule za msingi ili kuwashindanisha, kuibua na kuendeleza vipaji vyao, ahsante.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-

Je, TFF inashirikianaje na ZFF kupandisha hadhi Ligi ya Zanzibar na kuendeleza vipaji vya wachezaji wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Jimbo la Magomeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imekuwa ikishirikiana na ZFF katika mipango mbalimbali kwa lengo la kuendeleza Soka la Tanzania. Kwa sasa Bodi ya Ligi ipo katika mchakato wa kuandaa mafunzo ya uendeshaji wa Bodi ya Ligi ya Zanzibar ambayo kimsingi yatalenga namna ya uendeshaji wa Bodi ya Ligi katika masuala ya menejimenti, ligi na masuala ya uwekezaji, udhamini na masoko.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kuibua vipaji, TFF imekua ikishirikiana na ZFF katika uteuzi wa wachezaji katika timu za Taifa za Vijana, ambapo vijana kutoka Zanzibar wamekuwa wakiitwa katika vikosi vya timu ya Taifa ya vijana na hatimaye kucheza katika timu ya Taifa ya wakubwa (Taifa Stars), ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, mchakato wa kuwa na Vazi la Taifa umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliunda Kamati ya Kitaifa ya kuratibu upatikanaji wa Vazi la Taifa. Kamati hiyo imefanikiwa kukusanya maoni kutoka kwa wadau na wananchi 2,452 kutoka Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuwa, Kamati itakutana ili kuwashindanisha wabunifu wa mavazi (designers), kutoka pande zote mbili za Muungano ili wale watakaokuwa washindi kwa upande wa wanaume na wanawake mavazi yao ndiyo yatakayopendekezwa kuwa vazi la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wabunifu hao watafanya kazi kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau pamoja na wananchi ili kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa vazi la Taifa kwa ufanisi na haraka zaidi. Aidha, tumeamua kutumia njia hii ili kuharakisha mchakato na kupunguza uhitaji wa matumizi ya fedha nyingi za uratibu wa upatikanaji wa vazi la Taifa. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaenzi Tamaduni za Makabila ili kulinda maadili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha tunaenzi tamaduni za makabila kwa lengo la kulinda maadili ya Mtanzania Serikali inafanya yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamza ni kuendesha Tamasha la Kitaifa la Utamaduni ambalo hufanyika kila mwaka. Tamsha hilo linashirikisha vikundi vya utamaduni kutoka Mikoa yote ya Tanzania bara na Visiwani, ambalo linahusisha shughuli mbalimbali za kiutamaduni, kama vile maonesho ya vyakula vya asili, urembo na utanashati, michezo ya jadi, teknolojia na sayansi jadia. Pia, Tamasha hilo linahusisha mashindano ya ngoma za asili, upishi na uandaaji wa vyakula vya asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sambamba na hayo, Tamasha hilo huambatana na mdahalo wa namna ya kupambana na mmomonyoko wa maadili. Hivyo kupitia tamasha hilo, wananchi wanasherehekea, wanaenzi, wanatunza na kuendeleza tamaduni zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili Serikali inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kama vile makongamano, semina, mikutano na warsha kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuthamini utamaduni na maadili ya Mtanzania

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, inaendelea kufanya Tafiti mbalimbali ili kubaini mila na desturi zinazo kubalika katika jamii ili ziendelezwe na zisizofaa waachane nazo, ambapo hadi sasa jumla ya tafiti 286 kuhusu mila na desturi za maeneo ya Kihistoria zimefanyika;

Mheshimiwa Mwenyekiti na mwisho inaendelea kushirikiana na wadau na kuwahimiza kufanya matamasha mbalimbali ya utamaduni nchini kote, ili kuhakikisha mila, desturi na tamaduni zetu zinalindwa na kuendelezwa.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, mchakato wa kuwa na Vazi la Taifa umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliunda Kamati ya Kitaifa ya kuratibu upatikanaji wa Vazi la Taifa. Kamati hiyo imefanikiwa kukusanya maoni kutoka kwa wadau na wananchi 2,452 kutoka Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuwa, Kamati itakutana ili kuwashindanisha wabunifu wa mavazi (designers), kutoka pande zote mbili za Muungano ili wale watakaokuwa washindi kwa upande wa wanaume na wanawake mavazi yao ndiyo yatakayopendekezwa kuwa vazi la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wabunifu hao watafanya kazi kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau pamoja na wananchi ili kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa vazi la Taifa kwa ufanisi na haraka zaidi. Aidha, tumeamua kutumia njia hii ili kuharakisha mchakato na kupunguza uhitaji wa matumizi ya fedha nyingi za uratibu wa upatikanaji wa vazi la Taifa. Ahsante.