Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Venant Daud Protas (17 total)

MHE. VENANT D. PROTAS Aliuliza:-

Jimbo la Igalula lina jumla ya vijiji 58, ambapo Vijiji 12 vimepata umeme na vijiji 46 bado havijapata umeme:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katika vijiji 46 ambavyo havijapata umeme?

(b) Je, gharama za kuunganisha umeme kwa kila mwananchi ni kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Igalula, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyobaki 46 katika Jimbo la Igalula vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa pili unaoanza katikati ya mwezi Februari 2021. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2022. Kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo, kutafanya vijiji vyote katika Jimbo la Igalula kupatiwa umeme.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua ya kuongeza kasi ya kutoa huduma ya umeme nchini mwaka 2019, Serikali kupitia TANESCO ilipunguza bei ya kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi wanaoishi vijijini na maeneo yanayofanana na hayo kutoka wastani wa shilingi 725,000/= kwa mita za njia tatu (three phase) hadi shilingi 139,000/= ikiwa ni punguzo la asilimia 80. Vilevile kwa mita za njia moja (single phase) kutoka wastani wa shilingi shilingi 177,000/= hadi shilingi 27,000/= sawa na punguzo la asilimia
84.75. Kwa ujumla, gharama hizo ni tozo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano ya simu kwenye Vijiji vya Igalula ambavyo havina mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini ambayo hayana mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa Mfuko wa Mawasiliano umeshatekeleza miradi 686 na bado kuna miradi katika kata 371 ikiwa inaendelea na utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Igalula lina kata 11 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi sita ya mawasiliano katika Jimbo la Igalula ambapo imejengwa minara sita ambayo imetolewa na watoa huduma katika Kata tano ambazo ni Kizengi, Loya ambayo ina Miradi miwili, Lutende, Miswaki pamoja na Tura.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata zenye watoa huduma wa mawasiliano katika Jimbo la Igalula ni 10 ambazo ni Igalula yenyewe, Kigwa, Loya, Lutende, Miswaki, Kizengi, Miyenze, Tura, Goweko pamoja na Nsololo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za Serikali, Kata ya Mmale na baadhi ya maeneo ya Jimbo la Igalula bado yana changamoto ya mawasiliano na kupitia Mfuko wetu wa Mawasiliano tunaendelea kufanya tathmini, ili tujiridhishe specifically kwamba kuna changamoto katika maeneo yapi ili yaingizwe katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za usoni kadri upatikanaji wa fedha utakapokuwa unaruhusu. (Makofi)
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Igunga – Miswaki – Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida yenye urefu wa kilometa 89?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daudi Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Igunga – Miswaki –Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida ni barabara inayouganisha Wilaya za Igunga na Uyui. Kwa upande wa Wilaya ya Igunga, barabara hii inajulikana kama barabara ya Igunga – Itumba – Buhekela – Simbo na ina urefu wa kilometa 107. Kwa upande wa Wilaya ya Uyui barabra hii inaunganisha barabara tatu ambazo ni Simbo - Miswaki - Loya – Migongwa – Magulyati yenye urefu wa kilometa 72.8, hivyo kufanya urefu wa barabara ya Igunga – Miswaki – Loya –Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida kuwa na urefu wa kilometa 179.8.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 361.99 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, kilometa 27, maeneo korofi kilometa 8.7 na matengenezo maalumu kilometa tano na ujenzi unaendelea. Aidha, katika mwaka 2021/2022 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 235 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa 35 na ujenzi wa daraja dogo (box culvert) mawili, makalvati mistari minne ili kuimarisha maeneo korofi ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kuzifanyia matengenezo barabara katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na upatikanaji wa fedha, nashukuru sana.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Igunga – Miswaki – Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida yenye urefu wa kilometa 89?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daudi Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Igunga – Miswaki –Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida ni barabara inayouganisha Wilaya za Igunga na Uyui. Kwa upande wa Wilaya ya Igunga, barabara hii inajulikana kama barabara ya Igunga – Itumba – Buhekela – Simbo na ina urefu wa kilometa 107. Kwa upande wa Wilaya ya Uyui barabra hii inaunganisha barabara tatu ambazo ni Simbo - Miswaki - Loya – Migongwa – Magulyati yenye urefu wa kilometa 72.8, hivyo kufanya urefu wa barabara ya Igunga – Miswaki – Loya –Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida kuwa na urefu wa kilometa 179.8.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 361.99 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, kilometa 27, maeneo korofi kilometa 8.7 na matengenezo maalumu kilometa tano na ujenzi unaendelea. Aidha, katika mwaka 2021/2022 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 235 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa 35 na ujenzi wa daraja dogo (box culvert) mawili, makalvati mistari minne ili kuimarisha maeneo korofi ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kuzifanyia matengenezo barabara katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na upatikanaji wa fedha, nashukuru sana.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Kata za Kigwa, Goweko, Igalula na Nsololo?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa uchimbaji wa mabwawa katika Kata za Mmale, Miswaki, Lutende na Kizengi ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igalula lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imepanga kuboresha huduma ya maji kwenye Kata za Kigwa, Goweko, Igalula na Nsololo kupitia bomba kuu linalotoa maji Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Nzega, Igunga na Tabora.

Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 1,000,000 na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 122. Mradi huu unatarajiwa kukamilika kabla mwezi Juni, 2022 na utanufaisha wananchi wapatao 123,764 kwa kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 kukamilisha usanifu wa ujenzi wa bwawa katika Kata ya Kizengi na wakandarasi watapatikana mwezi Machi, 2022 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo ambapo wananchi wa Kata za Kizenga, Mmale, Miswaki na Lutende zaidi ya 60,000 watanufaika.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo la Rais wa Awamu ya Tatu la kuitambua Kizengi kuwa Tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala hufanyika kwa mujibu wa mwongozo wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala wa mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo huu unaelekeza maombi ya kuanzisha maeneo hayo kujadiliwa na kupitishwa kwenye vikao vya kisheria ngazi za Vijiji, Kata (WDC), Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI haijapokea maombi ya Kizengi kuwa Tarafa. Hivyo, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kufuata mwongozo uliotolewa na kuwasilisha maombi hayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya tathmini na kufanya maamuzi kwa kadri ya taratibu. Ahsante.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumalizia maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa ajili ya elimu, afya na polisi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa maboma 1,715 ya zahanti na vituo vya afya yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ambayo yanahitaji jumla ya shilingi bilioni 98.7 kwa ajili ya ukamilishaji wake. Aidha, katika sekta ya elimu kuna jumla ya maboma 12,101 ambayo yanahitaji jumla ya shilingi bilioni 183.5 kwa ajili ya ukamilishaji wake.

Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 43.8 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati na vituo vya afya ambapo hadi kufikia Desemba, 2021 shilingi bilioni 29.5 zimepelekwa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma hayo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/22 Serikali imetenga shilingi bilioni 79 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya madarasa na maabara ambapo fedha hizo tayari zimekwishapelekwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya polisi 63 vilivyoanzishwa na wananchi kwa ajili ya kuimarisha huduma za usalama wa raia na mali zao katika maeneo yao ambapo hadi kufikia Desemba, 2021 shilingi bilioni 1.85 zimekwishatolewa sawa na asilimia 85. Mkakati wa Serikali ni kuendelea kutenga fedha kwa awamu. Ahsante.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA K.n.y. MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kurahisisha upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha watu wote wanaokidhi vigezo vya usajili na utambuzi wanasajiliwa kwa urahisi. Ili kufikia lengo hilo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatekeleza mikakati ifuatayo: -

(i) Kufungua ofisi za usajili na utambuzi katika Wilaya zote Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo jumla ya ofisi 152 zimefunguliwa katika Wilaya 150;

(ii) Kuendelea kufanya usajili na utambuzi wa wananchi kupitia ofisi za Mamlaka za Wilaya na kuendesha mazoezi ya usajili wa watu wengi (Mass registration); na

(iii) Ugawaji vitambulisho kwenye ngazi za msingi yaani Kata/Shehia na vijiji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati hiyo husaidia kupunguza usumbufu na gharama za usajili kwa wananchi. Nashukuru.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza maeneo kutoka kwenye hifadhi katika Jimbo la Igalula ili wananchi wa Igalula wapate maeneo ya kuchungia na makazi kwa kuwa idadi ya watu na mifugo imeongezeka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 Serikali ilifanya mapitio ya mipaka ya msitu wa Uyui Kigwa - Rubuga uliopo Igalula, Wilaya ya Uyui ambapo hekta 36,709 zilitolewa kwa ajili ya vijiji vya Matanda, Sawmill, Kalemela, Itobela, Ibelamilundi, Isenegezya na Isikizya.

Mheshimiwa Spika, Serikali haioni haja tena ya kumega eneo hilo kutoka kwenye hifadhi kwa ajili ya kuwagawia wananchi kutokana na umuhimu wa hifadhi hii kiikolojia. Aidha, vijiji vinaelekezwa kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migogoro mipya kujitokeza.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je lini Serikali itaigawa Halmashauri ya Wilaya Uyui, ili itoe Halmashauri nyingine ya Igalula kwa kuwa inakidhi vigezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, halmashauri huanzishwa kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 287 na 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014. Mwongozo huo umeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuanzisha halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria hii, hatua ya awali inahusisha kupata ridhaa ya vijiji, Kamati za Maendeleo za Kata, Baraza la Madiwani la Halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC). Baada ya hatua hii, maombi hayo yanawasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya uhakiki na tathmini na kuwasilishwa kwa Mamlaka husika ili itoe uamuzi.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI haijapokea maombi ya kuigawa Halmashauri ya Uyui. Hivyo, nashauri taratibu za uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala zifuatwe. Ahsante.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta watumishi wa afya na elimu katika Jimbo la Igalula ili kuondoa kero wanayoipata wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ajira ili kukabiliana na upungufu wa watumishi katika kada za afya na elimu unaotokana na kustaafu, kuacha kazi, kufukuzwa na kufariki. Tangu mwaka 2018/2019 hadi 2021/2022, Serikali imeajiri jumla ya walimu 26,598 wakiwemo 16,640 wa shule za msingi na 9,958 wa shule za sekondari.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022, watumishi wa kada za afya 7,736 waliajiriwa na kupelekwa kwenye maeneo mbalimbali nchini kulingana na uhitaji uliokuwepo. Mkoa wa Tabora ulipata walimu 565 wakiwemo wa shule za msingi 301 na shule za sekondari 264. Aidha, kwa upande wa kada za afya Serikali ilipeleka kwenye Mkoa wa Tabora jumla ya watumishi 265 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui ilipata watumishi wa kada ya afya 50.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari imetangaza nafasi za ajira za walimu na watumishi wa kada ya afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023. Jumla ya ajira 13,130 kada ya elimu na 8,070 kada ya afya zitatolewa hasa kwa kuzingatia maeneo yenye upungufu mkubwa.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia Vituo vya Afya Kizengi, Tura, Lutende na Goweko kwa kujenga OPD na kupeleka vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya katika kata za kimkakati ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali ilitenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Lutende katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya Lutende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini ikiwemo ukamilishaji wa Kituo cha Afya Lutende, na Tura, pamoja na ujenzi wa vituo vya afya katika Kata ya Goweke na Kizengi.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya ufundi stadi katika kuwasaidia wananchi kupata ujuzi utakao wasaidia kutekeleza kazi zao za kiuchumi. Kwa sasa Serikali inatekeleza azma ya kujenga chuo cha ufundi stadi katika kila mkoa na wilaya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Igalula lipo katika Wilaya ya Uyui na kwa sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa Chuo cha Wilaya ya Uyui. Ujenzi huo umefikia asilimia 97 na chuo hiki kimeshaanza kutoa mafunzo ya muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya zote nchini, Serikali itaangalia uwezekano wa kujenga vyuo vya VETA katika ngazi za majimbo na ngazi zingine za chini kadri ya upatikanaji wa fedha na uhitaji, nakushukuru.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Uyui - Tabora katika Kata ya Tura na Wilaya ya Ikungi – Singida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sekretarieti za Mikoa ya Tabora na Singida imeendelea kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui katika Kata za Tura na Wilaya ya Ikungi. Kamati za Ulinzi na Usalama za pande zote mbili zilikwisha kutana. Kila Mkoa ulipewa majukumu kwa ajili ya kutatua mgogoro huo kwa kufanya yafuatayo:

(i) Wataalam wa Wilaya zote mbili kufika uwandani ili kutafsiri ramani, kufuatilia historia ya eneo, kuandaa kikao cha Majadiliano ya Wataalam na kuandaa kikao cha Wakuu wa Mikoa kuelezea yaliyobainika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wataalam wa Ardhi wa Wilaya ya Ikungi na Wilaya ya Uyui, wanapitia nyaraka mbalimbali yakiwemo matangazo ya Serikali (GN) yaliyoainisha Mikoa hiyo, ramani na mihtasari mbalimbali iliyohusika kupima Vijiji.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA K.n.y. MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, nini mpango wa kuweka miundombinu ya kuhifadhi maji ya mvua badala ya kusababisha mafuriko Kata za Loya na Miswaki?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bwawa katika Kata ya Miswaki, lakini taarifa za kitaalam zilionesha eneo hilo kutokukidhi. Usanifu wa bwawa uliofanyika katika eneo la Kata ya Kizengi ulileta matokeo mazuri na Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa bwawa katika mwaka wa fedha 2023/2024. Kukamilika kwa bwawa hilo kutaboresha huduma ya maji kwenye vijiji kumi vya Kata za Loya, Miswaki na Kizengi. Aidha, wananchi wanaofanya shughuli za kilimo maeneo ya mabondeni wanashauriwa kuhama kipindi cha mvua kubwa.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja katika Mto Loya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga shilingi milioni 318.90 kwa ajili ya usanifu wa daraja la Mto Loya ambapo tayari kazi ya usanifu ilianza tarehe 22 Desemba, 2021 na inategemea kukamilika tarehe 21 Juni, 2022 ambapo gharama halisi za ujenzi zitakuwa zimejulikana. Kazi hiyo ya usanifu inafanywa na Mhandisi Mshauri Advanced Engineering Solutions ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kujulikana kwa gharama za ujenzi huo ambao unalenga kujenga daraja kubwa na daraja la watembea kwa Miguu ikiwa ni pamoja na kujenga barabara approach road yenye urefu wa kilometa 13, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Askari na kulipa fidia kwa Wananchi waliovamiwa na Tembo kwenye makazi na mashamba yao Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeweka askari sita wakiwemo askari wa uhifadhi wawili na askari wa vijiji (VGS) wanne katika kituo cha kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu cha Ndala kilichopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora. Aidha, askari hao wamepewa vitendea kazi ikiwemo pikipiki mbili na silaha ambavyo vinawawezesha kudhibiti wanyamapori hao popote wanapoonekana ikiwemo Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na Wanyama pori ambapo kwa upande wa Wilaya ya Uyui ambayo inajumuisha Jimbo la Igalula Wizara imepokea maombi ya wananchi 17 waliopata madhara ya wanyama pori wakali na waharibifu, maombi hayo kwa sasa yanaendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu niendelee kutoa rai kwa wakurugenzi wa Halmashauri wa wilaya hususan zenye changamoto za wanyama pori wakali na waharibifu kuharakisha kuwasilisha maombi yanayotokana na madhara ya Wanyama pori hao Wizarani ndani ya siku saba ili kuiwezesha Serikali kufanya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati.