Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nicholaus George Ngassa (25 total)

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la vituo vya afya vilivyopo kwenye Jimbo la Tabora Kaskazini ni sawa na lililopo kwenye Jimbo la Igunga, Kata za Isakamaliwa, Kining’inila na Mtungulu. Ni kata ambazo hazina vituo vya afya vya kata na sisi kama wananchi tumeanza kutoa nguvu yetu kusaidia wananchi kujenga vituo vya kata. Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi kukamilisha vituo vya hizo kata husika ili tuweze kuwapatia wananchi huduma ya afya? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuunga mkono nguvu za wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya katika kata. Katika bajeti ambayo imetengwa lengo ni kuhakikisha kwamba kadri ya upatikanaji wa fedha nguvu za wananchi zitaendelea kuungwa mkono kwa Serikali kupeleka fedha ili kukamilisha vituo vya afya na zahanati zinazojengwa katika maeneo hayo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Igunga kwamba Igunga ni sehemu ya halmashauri na kata zake ni sehemu ya kata nchini kote ambazo zitanufaika na mpango huu wa umaliziaji na ujenzi wa vituo vya afya ili viweze kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru majibu ya Serikali, lakini kwa kuwa, mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu na umechukua eneo kubwa la Jimbo la Igunga, takribani kilometa za mraba 450. Sasa nilikuwa namuomba Naibu Waziri kwasababu, kumekuwa pia kuna mvutano kati ya wananchi na Serikali na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya yetu, nilikuwa namuomba Naibu Waziri kama atakuwa tayari baada ya Bunge hili la Bajeti niambatane naye tuende Igunga tukakutane na wananchi na Kamati ya Ulinzi na Usalama tuweze kulimaliza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UTALII NA MALIASILI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba tushirikiane Waheshimiwa wote Wabunge ambao tunawakilisha wananchi kutoka katika maeneo yetu husika. Suala muhimu la uhifadhi ni wajibu wa kila mmoja wetu kutambua kwamba, Serikali inapohifadhi maeneo husika ni kwa ajili ya faida ya wananchi wa eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia jibu langu la msingi ambalo nimelijibu mwanzo, nimeelezea kwamba, eneo hili ni moja ya vyanzo vya maji ambavyo vinategemewa katika Mikoa ya Tabora, Simiyu na Singida.

Kwa hiyo, ninakubaliana na wazo la Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaambatana naye, lakini ni wajibu wa kila Mheshimiwa kuelimisha wananchi wanaomzunguka kwamba, uhifadhi ni wajibu wa kila mtu na faida na hasara za uhifadhi tunaziona, lakini pia tunapohifadhi vyanzo hivi vya maji ni kwa ajili ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo husika. Lakini pia tunaepuka mambo mengi ikiwemo kuanzisha majangwa ambayo yanaweza yakasababisha ukame katika nchi yetu. Naomba kuwasilisha.
MHE. NICHOLAS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sasa naomba kuuliza swali la nyongeza kwa Serikali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Sera ya Afya ya Mwaka 2007, Sura ya 7 imeweka vigezo kwa Hospitali za Kata na Wilaya na moja ya kigezo ni lazima kuwe na gari la wagonjwa. Sasa Serikali imechukua gari la Kituo cha Afya cha Choma imepeleka Igunga na Kituo cha Afya cha Choma tena kimekosa gari. Je, Serikali haioni tunaendelea kukanyanga Sera ambayo tumejitungia sisi wenyewe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholas Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, gari la Kituo cha Afya cha Choma limepelekwa katika Hospitali ya Halmashauri ili kuweza kuboresha zaidi huduma za Halmashauri kwa kuwa Hospitali ya Halmashauri ina wagonjwa wengi zaidi kuliko Kituo cha Afya. Hata hivyo, gari hilo linafanya kazi katika vituo vyote viwili kwa maana Kituo cha Afya na Hospitali ya Halmashauri.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwanza niipongeze Wizara, Waziri na Naibu wake wanafanya vizuri. Mwezi Januari Naibu Waziri alipita pale alifanya ziara na akatoa maelekezo mwezi wa tatu chuo kikamilike lakini nimefanya ziara Jumamosi tarehe 12 changamoto imekuwa ni kwamba fedha zinakwenda kidogo katika kukamilisha huu mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba commitment ya Serikali katika kukamilisha fedha ambazo zitaenda kukamilisha huu mradi na kuanza udahili. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na kusuasua kidogo katika kupeleka fedha zile za awamu ya mwisho kuhakikisha kwamba tunakwenda kukamilisha ujenzi katika maeneo haya. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, fedha awamu ya mwisho zaidi ya Shilingi milioni 560 tayari zimeshapelekwa katika chuo hiki kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi huo na tutahakikisha kwamba tunasimamia vyema kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo Julai ili vijana wetu waweze kuanza mafunzo katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumwambia Naibu Waziri kwamba tulishapeleka maombi na Serikali ilituma wataalam wakafanya survey mwaka 2013/2014, lakini pia na mwaka 2016 walikuja wakafanya survey wakawa wamewasilisha Wizarani.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia barabara hii ndiyo kiunganishi cha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Simiyu ambao kimamlaka ulitengenezwa mwaka 2012.

Kwa hiyo, namwomba Waziri aweze kulipa kipaumbele, walifikirie ombi letu na waweze kuipandishwa hadhi ijengwe kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kupokea ushauri wa Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, kama alivyoomba.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie kwamba kama limeshafika Wizarani, basi tutaliangalia tuone kama limekwama; na kama kuna vigezo ambavyo vinashindikana, basi nitaomba tuwasiliane naye ili kama kuna shida tuone. Kama inakidhi vigezo vyote, nadhani barabara hii itapandishwa hadhi. Ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nyumba hizi tunazoziongelea kama alivyosema Naibu Waziri zipo nne na zinakaa familia 20 zilijengwa mwaka 1993 nakumbuka mimi nilikuwa darasa la kwanza; sasa zimechakaa sana na zinahatarisha usalama wa askari wetu. Mimi ninachoomba ni commitment ya Serikali na mwaka jana kwenye bajeti niliongelea. (Makofi)

Ni lini watatuweka katika kipaumbele cha kuzijenga nyumba hizi ili tusihatarishe maisha ya askari wetu? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili Naibu Waziri je, atakuwa tayari baada ya hili Bunge kuahirishwa apite Igunga, tuweze kwenda kuona hali halisi ambayo naiongelea hapa kabla maafa hayajatokea kuathirisha maisha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawii ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngassa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu commitment tunayo kama nilivyokwisha eleza tumefanya tathmini gharama zinajulikana, tutaanza awamu kwa awamu kukarabati nyumba ambazo zina hali mbaya sana. Kwa maana hiyo tutakapokuwa tunamaliza shughuli za Bunge katika ziara yangu niliyokwisha ahidi kutembelea Sumve - Mwanza, tutapita Igunga kuona kiwango cha uchakavu ili kuipa kipaumbele katika ukarabati wa nyumba hizo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Wizara ya Nishati kwa kituo hiki cha kupoza umeme ambacho kinatarajiwa kujengwa kwenye Kata ya Mbutu iliyopo Jimbo la Igunga ilikuwa ifanyike kwa mwaka huu wa fedha, lakini naona Serikali wameamua kuisogeza tena mwakani; ukiangalia imekuwa na changamoto kubwa kwa sababu tunapata umeme kutoka Lusu, Nzega ambayo ni kilometa 100. Sasa je, Serikali haioni kuchelewa kujenga kituo hiki ni kudumaza uchumi wa wananchi wa Jimbo la Igunga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Ngassa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatilaji wake wa mara kwa mara. Ni kweli Serikali ilikuwa imetoa ahadi ya kukijenga kituo hiki, lakini mwaka 2021 na mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TANESCO imefanya upembuzi yakinifu katika maeneo yote Tanzania Bara kuona uhitaji halisi wa ujenzi wa vituo vya kupooza umeme.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu niseme kwamba upembuzi yakinifu ulipokamilika, tukabaini mahitaji kutoka maeneo mbalimbali na uhitaji wa haraka zaidi kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Kwa hiyo, Kituo cha Igunga hakijachelewa ila imeonekana kijengwe mwakani kwa sababu kuna wenye uhitaji mkubwa zaidi kwa mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nivitaje vile vituo ambavyo vitajengwa mwaka huu ambavyo tayari vimepatiwa fedha katika ule mradi wetu wa grid stabilization project.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya nyumba za walimu ambayo iko kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ni sawa na changamoto iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ambapo angalau tumeanza hatua ya kwanza tumejenga maboma.

Je, ni nini mkakati wa Serikali kukamilisha maboma haya ambayo ni nyumba za walimu kwa ajili ya kuwapatia malazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya mkakati wa Serikali ni kuendelea kutoa fedha na tumekuwa tukifanya katika maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakijenga maboma, ikiwemo nyumba za walimu vituo vya afya pamoja na madarasa, kwa hiyo tumekuwa tukifanya hivyo. Hata hili analolisema ni kwamba Serikali tutaendelea kutekeleza na ndiyo maana moja ya kazi yetu kubwa sasa hivi ni kutafuta fedha kuhakikisha maboma mengi tunayafikia kwa kadri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo kwenye shule ya msingi Ng’ambo Tabora ni sawa na changamoto iliyopo kwenye shule ya msingi Igurubi ambayo ni Makao Makuu ya Tarafa ya Igurubi Jimbo la Igunga. Tunayo shule ya msingi ambayo kwa sasa ina wanafunzi wengi mpaka imezidiwa, kwa hiyo tunaomba pia Serikali katika utatuzi wa changamoto hizi iweze kuangalia pia shule ya msingi Igurubi ili iweze kulipatia ufumbuzi wa tatizo hili na changamoto hii ili wanafunzi wetu wasome kwa uhuru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus Ngassa Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nae ameeleza tu kwamba katika Jimbo lake la Igunga Tarafa ya Igurubi kuna Shule ya Msingi Igurubi ambayo na yenyewe ina wanafunzi wengi. Nimhakikishie tu kwamba moja ya mpango wa Serikali sasa hivi ni kutapisha shule zote zenye wanafunzi zaidi ya 2000 na ndio maana tuko katika mkakati wa kutafuta fedha na tumezitambua shule zote ambazo zina changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo mpango huu utakapokamilika maana yake tutawafikia na wao. ahsante. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Awali matarajio ya Serikali ilikuwa ni kuhakikisha maeneo haya ya vijiji vinawaka umeme ilipofika mwezi wa 12 mwaka jana, mwaka 2022, na ambapo ndio muda wa mkandarasi kukaa site ulikuwa unakamilika. Hata hivyo, mpaka ninapoongea hivi sasa, hivi vijiji maeneo mengi mashimo yamechimbwa na nguzo zimelazwa chini bado hazijasimamishwa.

Je, naomba kujua kauli ya Serikali; ni lini, hivi vijiji vitawashwa umeme kwa kuwa na muda wa mkataba wa mkandarasi umeshakwisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus Ngassa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mikataba iliyotakiwa kuisha Disemba mwaka jana. Hata hivyo, kama tunavyofahamu, tulipata changamoto ya kuongezeka kwa gharama za vifaa kipindi ambacho kulikuwa na magonjwa ya UVIKO. Pamoja na hayo tumepata faida nyingine ya kupata ongezeko la kilometa mbili kwa kila kijiji ambacho kilitakiwa kupelekewa umeme. Kwa hiyo vijiji vilivyo vingi upelekaji wa umeme utakamilika kufikia mwezi Disemba mwaka huu 2023. Kama nilivyosema kwenye majibu ya msingi kwenye baadhi ya maeneo kwa Mheshimiwa Ngassa, mwezi Aprili mwaka huu kuna maeneo ambayo tayari yatakuwa yamefikiwa na umeme kwa kadri alivyoiliza.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Serikali imekamilisha ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi - VETA kwenye Jimbo la Igunga.

Swali langu kwa Serikali; je, ni lini Serikali itafanya udahili na kuanza kwa wanafanzi kusajiliwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tulikuwa hatujakamilisha ujenzi kwa asilimia 100, Mheshimiwa Rais mwezi wa kumi na mbili alitoa fedha saidi ya shilingi bilioni 10.3 kwa ajili ya umaliziaji wa vile vyuo 25, fedha hizo tayari tumeshazipeleka kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo na pale Igunga. Kwa hiyo, ujenzi sasa tunaenda kukamilisha na tunatarajia kuanzia mwezi wa nne tuanza kudahili zile kozi za muda mfupi, nashukuru sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto ya majosho iliyopo kwenye Singida Magharibi ni sawa na changamoto iliyopo kwenye Jimbo la Igunga, kwenye Kata ya Kinikinila, Isakamaliwa, Mamashimba, Kilungu pamoja na Igulubi: -

Je, ni lini Wizara itatatua changamoto hii, ukizingatia Jimbo la Igunga ni miongoni mwa majimbo yenye mifugo mingi nchini?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus Ngassa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Igunga na Wilaya ya Igunga kwa ujumla tulipangia mwaka huu wa fedha kwamba tungeweza kujenga majosho zaidi ya matano, lakini majosho matatu hatukuweza kuyajenga kwa sababu hatukupata ushirikiano mzuri na Ofisi ya Mkurugenzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaamini kwenye bajeti ijayo, kwa sababu pia tumetenga majosho kwa Wilaya ya Igunga, tutapata ushirikiano wa kutosha na kwa hivyo maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tutayapangia kujenga majosho. Tupate ushirikiano wa kutosha ili kwamba majosho yatakayopangwa kwa wilaya hiyo basi yaweze kukamilishwa.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru sana Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Nape Nawuye na Naibu wake Mheshimiwa Kundo, kwa ushirikiano mkubwa walionipatia kuhusu hili suala la mawasiliano ya mitandao na kwa majibu mazuri haya ya Serikali sina swali la nyongeza ila niwaambie wana Igunga subiri neema ya mitandao ya simu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kupokea shukrani na pongezi kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wangu kwa ushirikiano ambao tunawapatia Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu kazi yao ni kuwawakilisha wananchi wao, ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Kata ya Isakamariwa, Kilinginira, Kilungu, Mwamwashiga na Mtungulu mkandarasi kaweka nguzo, je, ni lini atakamilisha kuweka waya wawashe umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali mawili la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa, kwamba kabla ya Disemba hii kuisha vijiji vyote na kata zote na maeneo ambayo yapo katika Mradi wa REA III Round Two yatakuwa yamewashiwa umeme.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Igunga ni moja ya miji inayokua kwa kasi kubwa sana kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu.

a) Je, Serikali, kwa kutowapatia mpaka sasa gari la zimamoto haioni ni kuhatarisha maisha ya raia na mali zao endapo itatokea janga la moto?

Mheshimiwa Naibu Spika, mafuta ni moja ya kimiminika hatarishi sana duniani, na sisi Igunga tunashughuli za bomba la mafuta zinaendelea pale na kuna camp kubwa sana ambapo tunaona itakuwa hatari sana endapo shughuli hizi zitaendelea na hatutakuwa na gari la Zimamoto endapo kutatokea na changamoto yoyote ya mlipuko au maafa.

b) Je, Serikali inachukua hatua gani au mkakati gani kwa ajili ya kukabiliana na jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika,napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika,kwanza tunatambua kwamba kuna uhaba wa magari ya zimamoto, tumekiri hapa ; na kwamba tumeanza utekelezaji wa bajeti kwa kupunguza tatizo hili kwenye maeneo ambayo hayana, lakini yote yanategemea upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, tumesema kwenye jibu la Msingi. Igunga kutokana na hizo shughuli nyingi za kiuchumi pamoja na hilo bomba la mafuta linalopita kwenye eneo lake, tunalipatia kipaumbele kwa mwaka ujao ili wapate gari la kuzimia moto, nashukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwanza nimpongese Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Igunga kwa hatua kadhaa ambazo ameendelea kutupa ushirikiano katika kutatua tatizo hili kwa niaba ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; pamoja na changamoto hii ya malipo ilijitokeza, lakini pia kumekuwa na changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara pake katika Mji wa Igunga hususan mjini kati pale, maeneo ya Mwamashimba, Igulubi, Nanga, Bukoko, Ikumba na Ikunungu. Je, nini kauli ya Serikali au Serikali ina mpango gani wa kutatua hii changamoto ya dharura ambayo inaathiri shughuli za kiuchumi za wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ukiangalia katika utekelezaji wa mipango hii ya Serikali pale katika jimbo letu. Kulikuwa na mpango pia wa Serikali kuongeza nguvu kwa kujenga kituo cha kuzalisha umeme. Je, Serikali ina mpango gani katika hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mbunge Ngassa kwa sababu ni mfuatiliaji mzuri sana wa miradi ya maendeleo katika jimbo lake. Kuna wakati hata mimi alinichukua kutoka Wizara ya Madini kwenda kumsaidia changamoto za wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala lake la kwanza, napenda kumjulisha kwamba Serikali imeanza kutekeleza Mradi wa Gridi Imara wenye thamani ya shilini bilioni 500 ambao utakwenda kujenga kwanza vituo vya kupooza umeme katika kila wilaya; pili kujenga njia ya kusafirishia umeme; na tatu kufanya marekebisho makubwa kwenye njia ya umeme ili umeme nchini uwe wa uhakika, lakini pia Bwawa la Nyeyere litakapokamilika nadhani hiyo adha ya kukatika kwa umeme itakuwa ni historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, kuhusu hawa wananchi ambao anasema waliahidiwa kuunganishiwa umeme, ni kwamba Wizara ya Nishati inaendelea na mchakato na mchakato huo utakapokamilika watafahamishwa, ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Wananchi wa Vijiji wa Mganzi, Chagana, Nguvumoja, Ilogelo na Mwagala, Jimbo la Igunga wamekamilisha ujenzi wa maboma ya zahanati; je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi kuunga nguvu za wananchi mkono? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus Ngassa, Mbunge wa Jimbo la Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ukamilishaji wa maboma ya zahanati yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi lakini ukamilishaji unaenda kwa awamu. Tumeshafanya katika miaka miwili, mitatu yote ya fedha na tutaendelea kufanya hivyo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani lakini pia kutumia fedha za Serikali Kuu, ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wakati wa usanifu wa maji kutoka Igunga kwenda Shelui wataalam wa Wizara waliwaaminisha wananchi kwamba yangetengenezwa matoleo kwa ajili ya kusambaza maji kwenye hizi kata ya Nguvumoja, Lugubu na Itumba lakini mradi umekamilika na matoleo ya maji hayajawekwa na wananchi hawajapata maji.

Je, Wizara hamuoni kutokutekeleza kwa kipengele hichi ni kuwachonganisha wananchi na Serikali yao sikivu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Wizara mmekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwa matokeo (P4R) na Mkoa wa Tabora tunafanya vizuri sana.

Je, hamuoni ni wakati sasa mtoe fedha ili kwenda kukamilisha huu mradi ili wananchi waendelee kuwa wanafurahia Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote ninapenda kukupongeza Mheshimiwa Ngassa kwa ufuatiliaji, lakini Mheshimiwa Ngassa Wizara hata siku moja haitaweza kuwa chonganishi kati ya Serikali na wananchi, tutaweza kufanya kwa bidii kubwa sana kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama mwenye uchungu wa wanawake wanaobeba ndoo kichwani inatekeleza miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutotoa matoleo ni sababu za kiufundi Mheshimiwa Mbunge, wakati fulani wakati usanifu unafanyika tulitarajia ingewezekana lakini population ya watu Tanzania sasa hivi inakua kila leo, kwa hiyo usanifu huu mpya utaleta maji ya kutosha na yatakuwa endelevu kwa eneo zima hili la Igunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu P4R tuna kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza sana Dkt. Samia, tulikuwa na Mikoa 17 pekee yenye kupata fedha za P4R lakini sasa hivi ni Mikoa yote 25 Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amepambana fedha zimepatikana kwa Mikoa yote, na eneo la Tabora kama ulivyosema linafanya vizuri tayari fedha pia zimeanza kupelekwa na fedha zimeongezeka. Kwa hiyo, ninakutoa hofu, hili mimi na wewe naomba tuonane ili tuweze kuweka sawa. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Jimbo la Igunga tuna skimu kubwa ya umwagailiaji ya Mamapuli iliyopo pale Mwanzugi na kwenye bajeti inayotembea, Serikali iliahidi kutupatia fedha. Je, ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ili kuboresha miundombinu kwa ajili ya kuwahudumia wakulima waliopo ndani na nje ya skimu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu hii ni kati ya skimu 42 ambazo tumezitengea fedha na nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tutakamilisha yale ambayo tuliahidi ndani ya Bunge hili kuhakikisha kwamba skimu ile inafanya kazi na inarekebishwa ili wananchi waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji kupitia skimu hiyo.

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Anachokieleza Naibu Waziri uhalisia kule si kweli kwa sababu mabasi yanayotoka masafa marefu unakuta yana abiria lakini yanasingizia hayana abiria matokeo yake yanawaacha wananchi juu kwa juu. Kwa mfano, pale Igunga maeneo ya mnadani wananchi wanafika wanashushwa tu wanaachwa wanaanza kuhangaika kutafuta bajaji na bodaboda kurudi Mjini.

Je, ipi ni kauli ya Serikali katika hili ili kuepusha adha kwa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, moja ya mwongozo wa Serikali ni kuhakikisha Halmashauri zetu zinakusanya mapato na Halmashauri nyingi vyanzo vyetu vya mapato ni pamoja na hizi stendi za mabasi lakini mabasi yanatumia kigezo cha kusema hawana abiria lengo wasiingie Halmashauri ili tusipate mapato. Pia naomba kauli ya Serikali katika hili, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nicholaus Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha kujibu kwenye jibu langu la msingi kwamba Sheria ya Usalama Barabarani, lakini pamoja na wadau, tulikaa na wadau mwaka jana tarehe 24, Mwezi wa Nne 2022, wadau wote wa usafirishaji, tulikubaliana kwamba ili kupunguza gharama kwa abiria ni pamoja na mabasi haya ambayo hayana abiria wa kushusha ndani wala hakuna anayepakia yasiingie ili kupunguza muda wa mabasi hayo kwenda kwa sababu wanasafiri umbali mrefu.

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kama kuna basi lolote ambalo limeshusha abiria njiani na wakati eneo hilo kuna kituo cha mabasi kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Kifungu cha 50 (1) na Sura ya 168 kimeelekeza wazi kwamba dereva huo lazima achukuliwe hatua za kisheria. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na jeshi la polisi tutaendelea kusimamia jambo hili ili mabasi haya yafuate utaratibu huu kama ambavyo tulikubaliana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu suala la mapato katika Halmashauri zetu hususan katika vituo hivyi vya mabasi, ni kwamba siyo kila basi kama nilivyokwisha kusema litaingia kwenye kituo, lakini kwa mabasi yale ambayo yataingia kwa masafa mafupi yana wajibu wa kulipa ushuru katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwanza niishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Igalula kwa kuanza kujenga bwawa kwa ajili ya kutatua changamoto, lakini tatizo hili pia lipo Igunga kwenye Kata za Itumba, Lugubu na Nguvumoja. Maji yamekuwa yakijaa kwa sababu ule ni ukanda wa Bonde la Mbeya ambalo linakwenda mpaka Igalula.

Je, ni lini Serikali itafanya kwa wananchi wa Jimbo la Igunga katika kutatua changamoto hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Jimbo la Igunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nipende kupokea shukrani kwa Serikali kutekeleza wajibu wake, na kwa maeneo ya kata ulizozitaja kwenye Jimbo la Igunga Mheshimiwa Mbunge na yenyewe pia tutaendelea kuwaletea wataalam waweze kufanya usanifu na tuweze kuchimba mabwawa maeneo yote ambayo yatasaidia kuondosha na kupunguza mafuriko.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; cha kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Naibu Waziri anavyosema kwamba mabweni mawili yamekamilika si kweli kwa sababu yale mabweni hayajakamilika. Mpaka sasa wameziba kwa mabanzi na mbao chakavu kwa ajili ya kuwa-accommodate wale wafungwa, jambo ambalo ni kinyume cha haki za binadamu na utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake walifanyie kazi waweze kulikamilisha gereza hili ili liweze kutoa huduma vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili,, kwa sasa Serikali inapata hasara kwa kuwa mabweni ya wanawake hayapo, inasababisha kama kuna mfungwa ambaye ana kesi mbili au kesi inaendelea anachukuliwa anatolewa Igunga anapelekwa Nzega na inapoitwa kesi mahakamani inabidi arudishwe. Jambo ambalo linaingiza Serikari hasara.

Je, haoni kuendelea kuingiza Serikali hasara wasipomaliza ujenzi wa hili gereza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ngassa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hili ambalo ameniambia kwamba majengo hayajakamilika na ni machakavu kwangu pia ni jipya. Nachukua dhima ya kuongozana na wataalam wetu baada ya Bunge hili kwenda Igunga kujiridhisha, kuona ukweli wa hiki ambacho kinasemwa na kwa kweli kama tutakuwa iko tofauti tutachukua hatua stahiki kwa hawa waliotupa majibu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la mabweni ya wanawake kutokuwepo Igunga tunatambua, lakini kama nilivyokwishasema tunajenga kulingana na upatikanaji wa bajeti. Kwa vile hatujapata fedha akubali tu Mheshimiwa hawa wafungwa wa kike waendelee kupelekwa katika gereza la jirani. Lakini mipango ya Wizara ni kuendelea kujenga mabweni hitajika, na kwa sababu angalau mwaka huu tuna bajeti tuweze kuona jinsi ambavyo tutaweza kuwa-accommodate akinamama ambao wanakuwa wanasafirishwa kwenda gereza la mbali. Nashukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kituo cha Afya Igulubi kilichopo kwenye Jimbo la Igunga kimejengwa kwa milioni 500 na Serikali ya Chama cha Mapinduzi na kituo kipya hakina gari la wagonjwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Nicholaus Ngassa, Mbunge wa Jimbo la Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kituo hiki cha afya ambacho kimekamilika ni sehemu ya vituo ambavyo vinahitaji magari ya wagonjwa, lakini safari ni hatua tutafanya tathimini kuona vigezo hivyo na kama itatimiza vigezo basi itapata gari la wagonjwa.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwenye Jimbo la Igunga, kuna changamoto kubwa sana kwenye Shule ya Msingi Butamisuzi Kata ya Mbutu na Mwajinjama. Tunaishukuru Serikali, Shule ya Msingi ya Buta wametupatia fedha kuboresha madarasa chakavu. Imebaki changamoto kwenye Shule ya Msingi Mwajinjama iliyopo Kata ya Mtungulu: Je, ni lini Serikali mtapeleka fedha kwa ajili ya kutusaidia kuboresha madarasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa, kwa sasa kuna tathmini ambayo ilikuwa inafanyika na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia kwa Maafisa Elimu wetu wa Msingi katika Halmashauri zote hapa nchini ili kuweza kupata taarifa sahihi ya idadi ya madarasa yanayohitajika ili fedha iweze kutafutwa na kupelekwa. Vilevile kule kwa Mheshimiwa Ngassa, itafanyika hivyo.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru na kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu. Wiki iliyopita walitupatia shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, Shule ya Sekondari ya Igurubi ilianzishwa mwaka 2000 na sasa ina miaka zaidi ya 20. Ina madarasa 19 lakini yanayotumika ni tisa tu, madarasa kumi yamebaki, ambayo inaongeza idadi ya miundombinu ya majengo ambayo tunaweza tukaibadilisha ikawa mabweni na mabwalo. Je, nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha tunapata kidato cha tano na sita kwenye Shule ya Sekondari ya Igurubi? Aahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngassa, kwanza naanza kwa kumpongeza yeye Mheshimiwa Ngassa kwa kuweza kufuatilia sana suala hili ya Shule ya Igurubi. Amekuja ofisini mara kadhaa kwa ajili ya kufuatilia iweze kupandishwa hadhi na kuwa shule ya A level.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule hii kama nilivyokwishasema kwenye majibu yangu ya msingi, tayari Serikali imeshapeleka fedha nyingi kwa ajili ya miundombinu mingine ya madarasa. Tutaendelea kutafuta fedha kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya kujenga miundombinu inayohitajika kwa ajili ya kusajiliwa. Baada ya miundombinu hiyo kuweza kujengwa tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Elimu kwa ajili ya kuweza kuipandisha hadhi shule hii na kuwa ya kidato cha tano na sita. (Makofi)