Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. George Ranwell Mwenisongole (3 total)

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Mbozi napenda kuuliza swali kuhusu Barabara la Mloo – Kamsamba mpaka Kilimamatundu na kutoka Utambalila mpaka Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, Chitete, kilometa 145. Kwa kuwa, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika; na kwa kuwa nyaraka za tenda ziko tayari.

Je, ni lini barabara hii itatengewa fedha na kutangazwa ili ijengwe kwa kiwango cha lami kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi na kama Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inavyoelekeza kwa mwaka 2020 - 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema ya Mbozi – Mtambalila mpaka Kamsamba ni barabara ambayo, kama alivyosema imeshafanyiwa usanifu na ni kati ya barabara ambazo zimeahidiwa kwanza kwa bajeti zinazokuja zitajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mwenisongole kwamba, barabara yake iko kwenye mpango na zitaendelea kujengwa barabara kadiri ya fedha itakavyopatikana katika kipindi hiki cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2021/2022 mpaka 2025/2026, asante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo yaliyoko Kasulu Vijijini yanafanana na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo langu la Mbozi katika Kijiji cha Sasenga na Itewe, kuna mgogoro kati ya wananchi na Kambi ya Jeshi. Napenda kumuuliza Waziri wa Ulinzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua huo mgogoro ambao umekuwa ni wa muda mrefu kati ya hivyo vijiji na Kambi ya Jeshi 845KJ. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba katika Kambi ya Itaka kuna shida hiyo ya mgogoro. Niseme kwamba migogoro hii imesababishwa na mambo mengi ikiwemo lile suala tu la uzalendo, majeshi yetu, pale ambapo tulikuwa tunawaruhusu wananchi kufanya shughuli zao; na walipozoea kufanya shughuli zao wakaamua kuhamia katika maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kwamba tunafanya utaratibu maeneo yote na tumeshatambua maeneo yote yenye mgogoro na kwa hiyo, tumejipanga kwa ajili ya kuitatua. Tumeanzisha kitengo maalum cha miliki kuhakikisha kwamba migogoro yote tunaimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mwenisongole kwamba tunafahamu shida ya Itaka na kuna hatua zinachukuliwa, tunakwenda kutatua shida ambayo iko kwa wananchi. Vilevile nawasihi sana wanasiasa na viongozi mbalimbali, kwamba kuna wakati mwingine tumetafuta kura Waheshimiwa Wabunge tukiahidi kwamba tutawasaidia wananchi kupata maeneo ambayo ni ya Jeshi. Niwahakikishie tu kwamba tutafuata taratibu kuhakikisha kwamba haki inatendeka, wananchi wanapata haki zao na Jeshi linaendelea kufanya shughuli zake bila kikwazo chochote. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Mimi ningependa kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwa nini Serikali isipunguze riba kwa hao wanaolipa deni lote kwa mkupuo kwa wakati mmoja ikatoka asilimia kumi au asilimia mbili au tatu au na vile vile kupunguza- retention fee ambayo ni kubwa na haipo kwenye mkataba wanaojaza wakati wa kukopa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu yaliyopita, kwamba tunaenda kufanya review ya tozo hizi pamoja na riba na kuweza kuangalia namna gani tunaweza tukazipunguza au kuziondoa kulingana na uhitaji kutokana na malalamiko yaliyopo.