Contributions by Hon. Jonas William Mbunda (10 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya uhai. Vilevile naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua kuwa mgombea na pia niwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Mbinga Mjini kwa kunichagua kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye Mpango wa Awamu ya Tatu wa Maendeleo. Dhima ya Mpango wa Awamu ya Tatu wa Maendeleo ya Taifa ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Hata hivyo tutajengaje uchumi huu? Ni lazima tuhakikishe kwamba nyanja zote zinazotakiwa zilete maendeleo zimesimamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa kwenye suala la kilimo. Ukiangalia Mpango uliopita tulikuwa na malengo ya kukua kwa uchumi kupitia kwenye upande wa kilimo kwa asilimia 7.6 lakini uchumi huo ulikua kwa asilimia 4.4. Ukija kwenye uchangiaji wa pato la Taifa napo tumeshuka. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba kwenye suala la kilimo tumerudi nyuma lakini ukiangalia sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania wanashughulika na kilimo na wako vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya mwisho tunategemea kwamba tutakuja kupata maendeleo ya watu na kuondoa umaskini kwa kupitia kilimo. Tutakapokuja kugawa na kuona kila mwananchi anapata kiasi gani ili aweze kuonekana kwamba ameendelea kimaisha tutaangalia pamoja na idadi hiyo kubwa ya wakulima ambao wako vijijini na bado wanaishi katika maisha ya shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoishauri Serikali kwanza kabisa, kama walivyochangia wenzangu kwenye suala la mbegu tuhakikishe kwamba wakulima wanasaidiwa namna ya kupata mbegu bora. Pia Wizara ya Kilimo isimamie kuhakikisha kwamba wananchi wanapata pembejeo zenye ruzuku. Zaidi ya hapo wananchi hao wasaidiwe kupata masoko ya uhakika hasa wale ndugu zangu wakulima wa kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili sasa tuweze kufika kwenye maendeleo, hasa kwenye suala la viwanda, kwenye suala la elimu naipongeza Serikali imefanya vizuri lakini hatujawekeza sana kwenye suala la elimu ya ufundi. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwenye suala la elimu ya ufundi ijitahidi kujenga vyuo vya VETA kwenye wilaya zetu ili suala la ufundi lifike kwa wananchi wetu na waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili viweze kusaidia kwenye suala la maendeleo ili tuweze kufikia uchumi wa viwanda na wananchi hawa waweze kupata unafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kupata maendeleo lazima pawe na umeme wa uhakika. Naomba niipongeze Serikali kwa kujenga miundombinu mingi ya umeme na kugawa kwenye maeneo mbalimbali lakini tatizo kubwa lipo katika upatikanaji wa umeme wa uhakika. Katika Jimbo langu la Mbinga Mjini, kila mara natumiwa meseji za kunijulisha kwamba umeme umekatika. Kwa hiyo, tutashindwa kabisa kufanya kazi za maendeleo kama tutakuwa hatuna umeme wa uhakika katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa wanajeshi kama kujenga nyumba za kuishi pamoja na kununua vitendea kazi kama magari na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ihakikishe JKT inawezeshwa ili kuzalisha chakula cha kutosha kwa matumizi na biashara. Pia Serikali kuendelea kulisimamia Shirika la SUMA JKT kuendeleza viwanda na ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali kuongeza mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kusimamia na kuondoa migogoro ya ardhi na mipaka baina ya Jeshi letu la wananchi pamoja na wananchi wanaoishi jirani na kambi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Waziri na Naibu Waziri na Makatibu Wakuu pamoja na Mkuu wa Majeshi kwa utendaji kazi wenye weledi kwa kuimarisha ulinzi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kusimamia na kutatua migogoro mingi ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza pia Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kuandaa mpango mzuri wa mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi kwa mwaka 2021/2022.
Katika kuzingatia utekelezaji wa mipango hiyo napendekeza kama ifuatavyo; kwanza kusimamia na kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya ardhi ipimwe kwa kuwa kasi ya ukuaji wa miji ni kubwa.
Pili, kuhakikisha ankara za malipo ya kodi za ardhi zinatolewa kupitia simu za wateja n atatu, kuhakikisha hati za kumiliki ardhi zinatolewa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Serikali kuendelea kutatua na kumaliza migogoro ya ardhi; tano, Serikali kuongeza wafanyakazi hasa katika kitengo cha mipango miji na Upimaji wa ardhi; sita, Serikali kuhakikisha vitendea kazi kama vifaa vya kupimia, magari na pikipiki vinanunuliwa na saba, Serikali ihakikishe Mabaraza ya Ardhi yanakuwepo katika kila Wilaya na kuhakikisha haki inatendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nane, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kuhakikisha miundombinu ya barabara, umeme na maji inafikishwa katika maeneo yaliyopimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Kwanza kabisa, naomba nimpongeze Waziri wa Wizara ya Kilimo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa jinsi walivyoanza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili naomba niwapongeze kwa sababu wameleta mikakati mizuri ambayo itatusaidia kutukwamua kwenye suala hili la kilimo. Pamoja na mikakati mizuri ambayo imetolewa na Wizara, lakini bado kuna changamoto ambazo zinatakiwa zitatuliwe ili tuweze kufikia malengo na kilimo chetu kiweze kuchangia kwenye Pato la Taifa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza sana kwenye upande wa utafiti. Changamoto kubwa ambayo nimeiona upande wa kilimo ni suala la utafiti. Changamoto nyingi ambazo zimetokana na suala la kilimo zinatokana na kukosa utafiti.
Mheshimiwa Spika, suala la kwanza, mimi natoka Mbinga kule Milimani ni wakulima wa kahawa na takriban sasa miaka 80 kilimo cha kahawa kinaendeshwa katika milima ile ya Umatengo. Changamoto iliyopo ni kwamba udongo ule umechoka. Kwa hiyo, tunaomba tafiti ya kupima udongo ili wakulima wale sasa waweze kupata ushauri mzuri utakaowasaidia kuongeza uzalishaji katika mashamba yale yale ambayo wanatakiwa waendelee kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utafiti unahitajika pia kwenye suala la pembejeo. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo kwamba udongo ule umechoka na uzalishaji katika udongo ule bado ni tatizo na wakulima wale hawawezi kuhama katika maeneo yao ya asili. Kwa hiyo, leo usipopima udongo na ukajua wakulima wale wanatakiwa watumie pembejeo za aina gani ina maana wakulima watanunua pembejeo kwa kubahatisha, kitu ambacho hakitaleta tija kwenye uzalishaji wa kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la miche na mbegu upande wa mahindi. Unakuta kwamba kuna vituo vya utafiti havipewi nguvu za kuzalisha miche ya kutosha lakini kwenye suala la mbegu kuna kampuni nyingi sana zinazalisha mbegu lakini mkulima huyu hapewi maelekezo kwamba ni mbegu zipi sasa anatakiwa atumie ili aweze kupata mavuno mengi katika mazao yake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iongeze nguvu kwenye utafiti na kama utafiti huo unafanyika, unafanyika kwa manufaa ya nani? Kama huyu mkulima hajapata matokeo na ushauri kutoka kwenye utafiti huo, huo utafiti ambao unaendelea unafanyika kwa manufaa ya nani? Kwa hiyo, niiombe Serikali ihakikishe kwamba matokeo ya utafiti na ushauri yawafikie wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaongelea suala la wakulima ambao wako kule vijijini lakini wanahitaji msaada wa wataalam. Kama nilivyosema mwanzo kwamba utafiti kama umekamilika wale wataalam wanatakiwa wapeleke matokeo ya utafiti kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa waziri ametuambia kwamba wataalam waliopo ni takriban 7,000 lakini ukiangalia upande wa pili unakuta wataalam wale hawana vitendea kazi, sasa watafikaje kwa wakulima na kuwapa maelekezo kwenye masuala yanayohusu kilimo? Utakuta wataalam hawa hawana pikipiki, magari na hawawezeshwi mafuta ya kufika vijijini. Ni namna gani sasa hawa wakulima wetu ambao wako vijijini watapata utaalam ili waweze kuzalisha na waweze kuleta tija katika uzalishaji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo nilitaka nilielekeze kwenye suala la kilimo kama walivyosema wenzangu ni miundombinu. Miundombinu yetu ni shida kwenye suala la barabara, hata kama utafiti na mambo mengine yatafanyika, lakini bado tutapata kikwazo kwenye suala la namna gani wataalam wanafika kule vijijini kwa wakulima na ni namna gani wakulima wanatoa mazao kutoka vijijini kwenye zile feeder roads ambazo ziko katika hali mbaya kupeleka sokoni. Kwa hiyo, hilo bado ni tatizo kwenye upande wa kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine naomba niishauri Wizara iache utaratibu wa kubadilisha sera mara kwa mara. Sera zinavyobadilika Bodi za Mazao pamoja na vyama vya ushirika vinashindwa kusimamia mazao kwa sababu hakuna sera endelevu. Kunakuwa na tatizo kwamba sera imetolewa leo baada ya miezi sita maelekezo mengine yanatolewa. Kwa hiyo, kwenye mpango mkakati wa muda mrefu ni vigumu kuutekeleza kwa sababu kunakuwa na mabadiliko ya maelekezo ya kiutendaji mara kwa mara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni masoko. Suala la soko ni tatizo kwenye mazao, kwetu ni zao la kahawa na mahindi. Kwenye zao la kahawa niipongeze Serikali imeanzisha ile minada ya kanda, lakini mpaka mkulima anapeleka mazao yake sokoni hajui gharama za uzalishaji wala hajui atauza kwa bei gani na hajui kama akiuza kwa bei ile italipa gharama zile za uendeshaji. Kwa hiyo, unaona kabisa kwamba zile tafiti kama zingekuwa zinafanyika zingekuwa zina uwezo wa kumuelekeza mkulima ili ajue zile gharama anazotumia baada ya kuuza mazao yake fedha zake zilizotumika zinarudi na mkulima huyu anakuwa amezalisha mazao haya kwa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa mahindi kuna tatizo kubwa sana nalo linalotokana na soko kwamba wakulima wale wanalima kwa gharama kubwa na ni wakulima wadogo wadogo wanalima kwa jembe la mkono, lakini bado wanapata tatizo la soko kwenye upande wa mahindi.
Mheshimiwa Spika, kama mwaka 2020 wakulima wetu wa Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Mbinga na Songea Vijijini, kwa dada yangu Mheshimiwa Jenista wametapeliwa mahindi yao ambayo ni ya thamani kubwa na mpaka sasa hivi hawajui hizo fedha zitalipwa kwa namna gani? Hawajalipwa, Serikali ipo, inaona, lakini mpaka leo wakulima wamekopa kwenye benki na…
SPIKA: Wametapeliwa na nani?
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, wametapeliwa na mfanyabiashara mmoja anaitwa Njau na mpaka leo hawajui ni namna gani hela zao zitapatikana. Kwa hiyo, naomba wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha hapa atamke Kauli ya Serikali kwamba inasema nini kuhusiana na hawa wakulima ambao wamepoteza mazao yao.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/2022. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi leo kuwepo hapa kwenye Bunge lako Tukufu. Vile vile naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa utendaji wake mzuri uliotukuka ambao anasimamia na kuhakikisha kwamba kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile nichukue nafasi hii nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutupa shilingi milioni 500 kila jimbo kwa ajili ya kuondoa changamoto au kupunguza changamoto kwenye barabara zetu kupitia TARURA. Kwa kweli naomba nimpongeze sana.
Naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wake Engineer Masauni, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kuandaa taarifa ya bajeti ya mwaka 2021/2022 ambayo imetuonesha kwamba inajibu changamoto zinazotukabili katika maeneo mbalimbali hasa kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Daniel Sillo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Makamu wa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kigua pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti kwa maandalizi mazuri ya taarifa na kwa kushirikiana bega kwa bega na Wizara ya Fedha kuandaa na kukamilisha bajeti ya mwaka 2021/2022. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze Mawaziri kupitia Wizara zote na Manaibu pamoja na Makatibu Wakuu kwa sababu bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2021/2022 inajumuisha Wizara zote ili kuhakikisha kwamba sasa tunasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie kusema kwamba kwa ujumla bajeti ya mwaka 2021/2022 imejibu changamoto nyingi na sehemu kubwa ya changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tunachangia katika Wizara mbalimbali itatusaidia sana sisi kuonekana kwamba mwaka huu tumefanya kazi ya maana na tumejitahidi kushirikiana na Serikali; na kama Serikali itatekeleza bajeti hiyo kama ilivyoandaliwa, nina uhakika kwamba tutakuwa tumefanya jambo la maana sana kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Wizara ya Fedha kwa maono ya kuhakikisha kwamba tunakusanya kodi za kutosha ili kuweza kukidhi bajeti ambayo ipo mbele yetu. Binafsi naunga mkono mapendekezo yote ya makusanyo ya kodi yaliyopendekezwa, nina uhakika kwamba hatutaweza kufanya masuala ya maendeleo bila ya kuwa na fedha za kutosha. Kwa hiyo, lazima tupate maumivu lakini tutakuja kufurahia baada ya changamoto nyingi kuondolewa kwenye maeneo yetu ya majimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya utaratibu wetu wote tulioupanga, lengo kubwa ni kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu na kuondoa umasikini. Suala hilo haliwezi kutekelezwa kama mambo yale yanayohusu jamii na shughuli zote zinaohusu maendeleo yetu hazitasimamiwa na kutekelezwa kwa wakati. Tunaweza tukafanikisha tu kukamilisha dhima hiyo na siku ya mwisho lengo letu, tunachohitaji ni kuona kwamba wananchi wote tumeondokana na umaskini ambao umeenea kwenye maeneo mengi ya vijijini. Siku ya mwisho tutakapopima sasa kama malengo yetu tumefikia ni kuhakikisha kwamba huyu mwananchi sasa ameondokana na umasikini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuimarisha viwanda vyetu, naipongeza sana Serikali kwa kuondoa tozo kwenye maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanda vyetu sasa vinaimarika. Vile vile naomba niipongeze Serikali kwa sababu imeweka tozo kwenye bidhaa mbalimbali zinazoingia ndani ya nchi zikiwa na lengo kubwa la kuhakikisha tunalinda viwanda vya ndani. Tusipolinda viwanda vya ndani ina maana hatutaweza kufikia lile lengo ambalo tumelipanga la kuondoa umasikini na kuleta maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande huo wa viwanda naomba sana Serikali kuweka mazingira bora ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafanya biashara katika mazingira yanayokubalika. Kwa mfano kuna vikwazo vidogo vidogo, unaweza kukuta mwananchi wa kawaida anataka kuanzisha biashara ndogo, lakini mchakato anaotakiwa apitie mpaka aanzishe hiyo biashara, unamkatisha tamaa. Kwa mfano mtu leo ana mtaji wake mdogo, anataka aanze biashara, masharti anayopewa kama anahitaji leseni, lazima aende TRA akafanyiwe assessment. Kwa hiyo, ina maana mwananchi huyu anaanza kulipa kodi kabla hata hajaanza kufanya biashara yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe Serikali ingeweza kutengeneza mazingira ya kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanaweza kufanya biashara na baada ya kuanza kufanya biashara ndipo waanze kufikiriwa kwamba wanatakiwa wachangie kwenye pato la Taifa. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali yangu, kwa sababu ni Serikali Sikivu, imetusikiliza kwa mambo mengi, nina uhakika kwamba hilo mtalifanyia kazi ili kutengeneza mazingira mazuri kwa wananchi wetu waweze kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika maeneo hayo ya viwanda naishauri Serikali isimamie miundombinu ambayo ipo katika maeneo haya yaliyotengwa ya viwanda yawe katika hali nzuri. Kwa mfano barabara, umeme, maji kwenye maeneo haya yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda naiomba Serikali iweke mazingira mazuri ili tuhakikishe kwamba shughuli zetu zinaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo yote hayawezi kufanyika kama kuna nyanja nyingine za kiuchumi pamoja na kijamii hazitatendewa kazi. Kwa mfano, ukiangalia kwenye suala la afya, ili hawa wananchi baadaye tuweze kuwapima maisha yao kwamba yako bora au yanaenda vizuri lazima kwenye afya wawe kwenye hali nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa kuhakikisha kwamba inaendelea kujenga hospitali, vituo vya afya pamoja na zahanati na kupeleka dawa na vifaa tiba kwenye hospitali hizo. Yote hiyo lengo lake ni kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanakuwa kwenye hali nzuri kiafya. Kwa hiyo, naipongeza Serikali na ninaomba sasa tuendelee na juhudi hizo kwa sababu bajeti tayari imetengwa na itekelezwe ili tuhakikishe kwamba wananchi hawa wanaishi katika maisha mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni elimu. Naipongeza Serikali kwa kusimamia sana kutengeneza miundombinu kwenye suala la elimu, kujenga madarasa na sasa hivi tunategemea kupata fedha nyingine kwa ajili ya kujenga Shule za Sekondari kwenye kila Jimbo. Hiyo itatusaidia kwanza ku- rescue situation ya wanafunzi wengi ambao walianza kuingia kupitia mfumo wa Elimu Bila Malipo ambao wanaanza kutoka mwakani, kwa hiyo, hii itatusaidia kupunguza changamoto kwenye suala hili la elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze mama yetu Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa kutusikiliza sisi Wabunge, tulikuwa tunapiga kelele na kusema kwamba mitaala yetu irekebishwe. Tayari nimeona tangazo tarehe 18 wadau wameitwa kwa ajili ya kuanza kuchangia mawazo kwenye masuala ya mitaala ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali, naomba tuendelee ili tuhakikishe kwamba tunafikia malengo. Kuna suala lingine la umeme. Unakuta kwenye Majimbo yetu, kwa mfano mimi kwenye Jimbo langu kuna vijiji 27 havijapata umeme, lakini katika hivi vijiji 27 kuna kata mbili hazijapata kabisa umeme. Kwa hiyo, naomba sana baada ya bajeti hii Serikali isimamie wananchi wale wapate umeme na vijiji vile vyote vipate umeme ili tuweze kuhakikisha kwamba tunafikia maendeleo ya kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni maji. Naiomba sana Serikali, kwa sababu tutapitisha hapa bajeti; na ninaomba Wabunge wenzangu tushirikiane kuipitisha hii bajeti, ili sasa ile miundombinu ya maji na mambo mengine yasaidie tuweze kumtua mama ndoo kichwani. Kwa hiyo, naomba niishukuru sana Serikali kwa jitihada hizi, lakini naiomba sasa kutekeleza haya kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kilimo. Naiomba sana Serikali izingatie kilimo ambacho kinaleta tija. Tuangalie kwanza kwenye uzalishaji ambao unaleta tija. Vile vile naomba Wizara ya Kilimo watumie vituo vya utafiti ili sasa tuweze kufanya kilimo ambacho kitaleta tija kwenye wananchi watu. Kwa mfano, kuna mashirika ya utafiti kama TARI, TIRDO, TEMDO, CAMARTEC, Serikali ihakikishwe kwamba mashirika hayo yanapata bajeti ya kutosha ili sasa utafiti utakaofanyika na majibu yale ya utafiti yaweze kuwafikia wananchi kwa ajili ya kuendeleza kilimo chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la UVIKO 19. Kwenye suala la UVIKO 19 tumeathirika sana kwenye upande wa utalii na usafiri hasa kwa upande wa ndege, lakini kwenye taarifa ya bajeti ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sijaona kama Serikali imeweka mikakati ya dhati na kutenga fedha za kutosha kuhakikisha kwamba inatibu majeraha hayo yaliyotokana na UVIKO 19. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Serikali ifikirie kwa upande wa ndani tunafanya nini? Badala ya kutegemea mikopo kutoka nje au na misaada, sisi wenyewe tumejidhatiti namna gani kuhakikisha kwamba tunasimamia na kudhibiti suala hili la UVIKO 19? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye suala la sensa, kwa sababu sensa ni suala la msingi sana kwenye maendeleo ya jamii na ili baadaye tuweze kupata taarifa sahihi za idadi ya watu na makazi, ningeomba sana Serikali iweke nguvu za kutosha katika kusimamia na kuhakikisha kwamba tunapata sensa ya idadi inayokubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango ulioletwa mbele yetu. Vilevile naomba nichukue nafasi hii kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa kutoa bilioni 50 kwa ajili ya kunusuru soko la mahindi kwa wakulima wetu, limesaidia sana ingawa wakulima wale bado wanahitaji soko la kuuzia mahindi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza kwa kutoa shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo itasaidia kuongeza sana uhitaji na kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo yetu. Naomba naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Daniel Sillo kwa kuwasilisha taarifa nzuri pia niwapongeze wanakamati wenzangu kwa kuchambua hii taarifa na kuileta mbele ya Kamati yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuandaa taarifa pamoja na timu yake yote ya Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama hapa kuchangia draft ya mpango ulioletwa mbele yetu kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni, kabla sijaanza kuchangia naomba nitoe masikitiko niliyonayo kwamba tunajadili mambo mengi, tumekaa karibu miezi minne kujadii bajeti ambayo iliisha tarehe 30 mwezi wa Sita lakini kulikuwana mipango mingi sana ambayo tuliipanga na kuijadili ukifanya tathmini ya utekelezaji wa kipindi cha robo mwaka katika taarifa ambayo tumeletewa sasa hivi ukurasa wa 16 kwenye utekelezaji wa robo mwaka ya bajeti inaonesha kwamba kwenye utekelezaji, bajeti ya maendeleo ya mwaka 2021/22 hakuna fedha zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenye upande wa kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, slogan yetu tunasema kwamba kilimo ni uti wa mgongo kwa Watanzania. Sasa unajiuliza kilimo cha Tanzania sehemu kubwa tunalima kwa kipindi kwamba tunategema mvua na ni sehemu chache sana ambazo anafanya umwagiliaji. Sasa unajiuliza sasa hivi ni mwezi wa 11 na wananchi wanajiandaa kuingia kwenye kilimo hawana mbolea ya kupandia, hawana mipango yoyote wakati huo tunategemea kwamba ni kilimo ni uti wa mgongo katika uchumi wetu. Sasa najiuliza huu uti wa mgongo utakuwa ni uti wa mgongo salama au hauna msaada katika maisha yetu Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo vilevile tumepata changamoto kubwa sana huko nyuma sasa nilitaka nione, kwa mfano nimepitia mpango ukiangalia kuna changamoto ambayo ilijitokeza inayohusiana na sumukuvu. Mpango wa Serikali na mikakati ni kujenga maghala na kuhakikisha kwamba tunaondoa hili tatizo la sumukuvu lakini kumbe sumukuvu inatakiwa katika mpango wetu tuangalie uwezekano wa kusaidia kuanzia kwa wazalishaji ili ku-trace ile sumukuvu ni sehemu gani ambayo unatakiwa uisimamie. Kwa sababu ninachofahamu kwa uzoefu wangu sumukuvu wakati mwingine inatokana na ubichi au wakulima wanavuna mazao mabichi na kuyaweka kwenye maghala matokeo yake yanasababisha sumukuvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mpango wetu naomba uboreshwe, uwekwe mkakati ambao utasaidia kuondoa sumukuvu kuanzia kwa wakulima.
Vilevile nilipopitia mpango sijaona mkakati ambao umewekwa wa dharura kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanasaidiwa kwenye suala la pembejeo. Suala la pembejeo ni kizungumkuti. Sasa hivi hatuna taarifa yoyote ile ya mbolea na hatuna taarifa ya kwamba mbolea hizi hata kama zitapatikana zitauzwa bei gani kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba mpango utakapokuja uboreshwe, uoneshe kwamba bei za mbolea pamoja na pembejeo zingine ziwe zimeshuka kwa kiwango kikubwa ikiwezekana iwe sawa na bei ambayo wakulima wetu walinunua mwaka jana ili iweze kuwasaidia katika uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa kilimo utakuta mpango wetu haujaonesha muunganiko uliopo kuanzia kwenye uzalishaji, kwenye masoko na viwanda. Kwa mfano, sasa hivi tunaweka mikakati mingi sana ya kuhamasisha uzalishaji wa michikichi lakini mpango haujaonesha kwamba sasa hii flow ya uzalishaji, masoko pamoja na suala la viwanda kwa ajili ya kuchakata hiyo michikichi ambayoo tunaiandaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize sana kwenye upande wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawekeza kwa kiasi kikubwa sana kwenye upande wa kilimo ili kuwasaidia wakulima wetu kuondokana na mazingira magumu ambayo yapo ili kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji. Kwa hiyo, kwenye hilo nategemea kwamba mpango utakapokuja kama walivyoshauri wenzangu tuhakikishe kwamba Serikali inaweka subsidies kwenye pembejeo pamoja na mbolea za aina mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mikakati yetu tuliweka hoja ya kuhakikisha kwamba Serikali inapima udongo. Kwenye upimaji wa udongo nilikuwa nashauri mpango uangalie uwezekano wa kuweka maabara za upimaji wa udongo kwenye kila Mkoa ili tuweze kuwasaidia hawa wananchi kuweza kupima udongo na kupata mbolea ambazo zitakwenda sambamba na udongo uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumeweka mikakati mingi sana na mipango mingi ya maendeleo lakini tumeangalia kwenye masuala ya maji, masuala ya kilimo, ufugaji na miundombinu mbalimbali lakini nilikuwa naomba mpango unapokuja baada ya kuboresha uangalie ni namna gani tunaweka mikakati ya kusimamia kwenye suala la mazizngira ili kuhakikisha kwamba hii miradi yetu ambayo tunaitekeleza kwa kutumia fedha nyingi za Serikali iweze kuwa himilivu kwa kipindi kirefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitoe mchango wangu kwenye suala la madeni. Kwenye mpango tumeonesha kwamba kuna madeni mbalimbali ambayo Serikali inadaiwa lakini nataka nijikite kwenye suala la madeni ya ndani. Madeni ya ndani kuna madeni ya wafanyabiashara na kuna madeni ya wakandarasi, kuna kipindi Serikali ilikuwa inafanya uhakiki wa madeni ya wafanyabiashara ambao walisambaza mbolea na pembejeo mbalimbali kwa wakulima wetu. Takribani sasa ni zaidi ya miaka mitano wafanyabiashara wale hawajalipwa chochote, kila siku wakiuliza wanaambiwa kwamba uhakiki bado unaendelea na ninaona kwamba wale wafanyabiashara wameingia kwenye matatizo magumu na wana hali ngumu kwa sababu wana madeni mengi ya kwenye benki mbalimbali na wanashindwa kulipa yale madeni kwa sababu madeni yao bado hayajahakikiwa.
Kwa hiyo, naomba sana kwenye mpango utakaokuja uhakikishe kwamba unasimamia na unaweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunawalipa wale wadau mbalimbali ili kuondoa adha ambayo inawakabili. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuhudhuria katika Bunge hili la Bajeti. Pia, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jinsi anavyosimamia shughuli za maendeleo ya nchi hii hususani Wizara hii ya TAMISEMI kwa sababu iko katika Ofisi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri Innocent Bashungwa na wasaidizi wake Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dugange, Katibu Mkuu Profesa Shemdoe na Manaibu wake wawili; kwa jinsi wanavyochapa kazi kuhakikisha kwamba shughuli za maendeleo katika nchi hii zinaendelea. Vile vile niwapongeze sana kwa kuandaa taarifa ya bajeti ya mwaka 2022/2023. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, jinsi ilivyotoa fedha nyingi kwa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Majimbo yetu na katika nchi yetu kwa ujumla. Naomba nianze kuchangia upande wa TARURA. Kwa upande wa TARURA kwanza niishukuru Serikali kwa kutoa fedha za nyongeza shilingi bilioni moja kwa miradi ya utengenezaji wa barabara katika Jimbo langu la Mbinga Mjini. Pia nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kupitia Mkurugenzi Mkuu wa TARURA kwa kutoa gari aina ya Landcruiser mpya hivi karibuni, ambayo imesaidia sana wahandasi kuzunguka katika maeneo ya Jimbo la Mbinga Mjini na kufuatilia maeneo mbalimbali ambayo barabara zina shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hotuba ya Waziri imeeleza kwamba TARURA inasimamia mtandao wa barabara wenye kilomita 144,229. Katika kilomita hizo kilomita 2,473 ni kiwango cha lami, kilomita 30,756 ni kiwango cha changarawe, lakini kilomita 111,199 ni udongo. Mimi binafsi nataka nichangie hasa kwenye barabara zinazotengenezwa kwa kutumia udongo. Katika Jimbo langu kuna Barabara ya Mbinga – Kitanda – Masimeli – Miembeni, lakini kuna Barabara nyingine ya Mbinga – Kikolo – Kiungu na Barabara nyingine ya Mbinga – Magamao – Mpepai – Mto Lumeme. Barabara hizi zote zinatengenezwa kwa kutumia udongo. Maeneo ya Jimbo la Mbinga haya maeneo niliyoyatamka ni maeneo ambayo yapo kwenye miteremko, kiasi kwamba kama barabara inatengenezwa kwa kutumia udongo ina maana kwamba kipindi cha mvua barabara ile yote inaharibika; na wananchi hawawezi kupita katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua kwamba Serikali inapeleka miradi mbalimbali katika maeneo ya Kata hizo ni kwamba hasa kipindi kile cha mvua ujenzi wa miradi mbalimbali pamoja na kutengeneza barabara hizo, inakuwa ni ngumu kwa sababu tayari mvua zinakuwa zimeharibu miundombinu, kwa hiyo inakuwa ni shida. Ushauri wangu hapa naiomba Serikali kwa maeneo hayo ambayo yana hali ya kijiografia tofauti, barabara zake zingekuwa zinatengenezwa angalau kwa kutumia changarawe na kwa barabara hizo zinazotengenezwa, Serikali izingatie kujenga mifereji katika maeneo hayo ili kulinda uharibifu wa barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ni kwenye suala la afya. Kwenye upande wa afya naipongeza Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga zahanati kwenye vijiji mbalimbali pamoja na vituo vya afya. Lakini changamoto iliyopo katika Jimbo la Mbinga kuna changamoto ya uchakavu wa majengo ya hospitali ya wilaya. Hospitali ya Wilaya ya Jimbo la Mbinga Mjini inahudumia takribani Kata 13 mpaka Kata 14, lakini hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1970 mpaka sasa hivi majengo yale yamechakaa na ipo katika hali mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa Waziri atakapohitimisha aniambie kwamba ni lini atasimamia kuhakikisha kwamba majengo ya hospitali ile yanajengwa upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Wizara kwa kuandaa vizuri taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kuimarisha utafiti katika maeneo ya uvuvi ili kupata fursa ya kutumia vyema eneo la uvuvi wa bahari na maziwa makuu.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali kuimarisha miundombinu ya uvuvi; tatu, kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa viwanda vya minofu ya samaki na kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa zinazotokana na samaki; nne, Serikali iendelee kutoa huduma bora kwa wadau wa sekta ya uvuvi ili kuwa na maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii; tano, Serikali iendelee kuwekeza katika maziwa makuu kwa kununua meli za uvuvi kama Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa na sita, Serikali kuweka mazingira mizuri, sera na kanuni ili kuendeleza ufugaji wenye tija.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali kuweka misingi rafiki ya wafugaji ili kuondoa migogoro iliyopo baina ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zinazoendelea kufanyika za kusambaza umeme kwa nchi nzima. Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati umeandaliwa vizuri. Pia nampongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa utendaji mzuri.
Mheshimiwa Spika, nashauri mambo yafuatayo. Naishauri Serikali kuendelea kusimamia na kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara. Pia nashauri Serikali iedelee kusambaza umeme katika Vijiji na Vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na umeme.
Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iendelee kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Umeme wa Mwalimu Nyerere ili kupata umeme wa uhakika. Pia napendekeza Serikali kuendelea kufanya utafiti wa mafuta, gesi na vyanzo vingine vya kuzalisha nishati ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa Nishati.
Mheshimiwa Spika, nashauri pia Serikali iendelee kuanzisha vituo vya usimamizi katika ngazi ya Tarafa ili kusaidia kutatua changamoto za kiufundi zitakazojitokeza. Vile vile iendelee kusambaza umeme. Kuna changamoto ya uhaba wa upatikanaji wa Transfoma hivyo kuchelewesha usambazaji wa umeme. Hivyo, Serikali isimamie uzalishaji wa Transfoma za kutosha.
Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iendelee kusimamia usambazaji wa nishati ya gesi kwa matumizi ya majumbani.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Marekebisho ya Sheria Mbalimbali. Kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri wa Fedha pamoja na jopo lake kwa kuleta mabadiliko ya sheria hizi ambazo moja kwa moja sehemu kubwa zinalenga kuwasaidia wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutenga kiasi cha Shilingi Bilioni 150 kwa ajili ya kutoa ruzuku ya mbolea, hilo ni suala la muhimu sana na limeleta faraja kubwa sana kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitachangia Miswada hii hasa kwenye maeneo ambayo yanagusa wakulima. Eneo la kwanza Serikali imeleta mapendekezo ya kubadilisha Muswada wa Sheria Sura Na. 123 Kipengele cha 87(1) ambacho kimependekeza kupunguza mirahaba ya ushuru kwenye malighafi mbalimbali ambazo zinatumika kwa ajili ya kutengeneza mbolea. Suala hilo ni la muhimu sana, jambo la kwanza ni lilelile eneo sikivu la Serikali la kuhakikisha kwamba wakulima wetu wananufaika na kilimo katika nchi yetu. Suala la pili ni jambo la msingi ambalo litavutia wawekezaji wa viwanda mbalimbali vya mbolea katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la kupunguza mirabaha kutoka asilimia Tatu mpaka Moja ni suala la msingi sana, kwa sababu litasaidia kupunguza gharama mbalimbali za uzalishaji wa mbolea, kama mlivyoona kwamba kwa mwaka huo uliopita ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwa wakulima, kwa hiyo tunaona kabisa wazo hili la Serikali litasaidia kuleta manufaa makubwa sana kwa wananchi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuunga mkono hoja hii ya Serikali naomba nitoe ushauri ufuatao: Ushauri wa kwanza, naiomba Serikali sasa kama Wabunge wenzangu wataunga mkono na tukapitisha sheria hii, Serikali iweze kusimamia kwa karibu sana ili tuweze kupata matokeo chanya na tuone kabisa punguzo hili limewasaidia wakulima. Ushauri mwingine kama patakuwa na uwezekano Serikali iangalie uwezekano wa kutoa bei elekezi za mbolea kwa wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mabadiliko hayo tungeomba yahusishe madini yote ambayo yatatumika kwa ajili ya kutengeneza mbolea. Kwa maelekezo ambayo yametolewa kupitia Muswada huu kwenye upande wa phosphate vilevile chokaa ambayo itasaidia sana kurekebisha hali ya udongo katika maeneo mbalimbali ili wakulima waweze kutumia kiasi cha mbolea kidogo sana baada ya udongo kurekebishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali hoja yangu italenga hasa hasa kwa maeneo ambayo yanamnufaisha mkulima.
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ni kwenye suala la ushuru wa ongezeko la thamani. Wakulima wa mazao mbalimbali ukichukulia mfano wa zao la kahawa, korosho na mazao mengine kwa muda mrefu walikuwa wakilipa gharama kubwa sana ya magunia katika kuhifadhia hayo mazao mbalimbali na gharama hizo zinatokana na gharama kubwa ya uzalishaji wa hayo magunia ya katani.
Mheshimiwa Spika, tunavyo viwanda zaidi ya kimoja ambavyo vinazalisha magunia ya katani lakini wakulima walikuwa wanalipa bei kubwa sana kwa gunia moja la kuwekea kahawa au korosho kutokana na gharama kubwa ya uzalishaji. Kwa hiyo, hii Sheria Sura Na. 148, ambayo Serikali itatoa unafuu itatoa exemption kwenye uzalishaji wa haya magunia itasaidia sana kupunguza bei kubwa ya magunia na itapelekea kuwapa unafuu wakulima wetu kuweza kupata kipato kikubwa kwa sababu bei ya gunia moja ambalo watakuwa wanatumia kuwekea mazao haya itakuwa imepungua. Hiyo nayo itaendelea kuleta faraja kwa wakulima na itaendelea kuleta hamasa kubwa sana ya wakulima kuona kwamba mazao ambayo wanalima yanawasaidia kwenye masuala ya maisha.
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho naomba nichangie kwenye jedwali la Nne linalohusu mapendekezo ya Serikali ya kuongeza ushuru wa mvinyo kutoka Shilingi 2,466.45 kwa lita hadi Shilingi 5,600 kwa lita. Hiyo itasaidia sana kupunguza bidhaa zinazotokana na mvinyo kuingia nchini na itasaidia sana kulinda soko la wakulima wa zao hili la zabibu ili kuweza kuwapa hamasa kubwa zaidi ya kuendelea kujali kilimo chao na kuwafanya waridhike na hali halisi ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo naomba niishauri Serikali kuzingatia mambo yafuatayo: -
Kwanza; Serikali isimamie sasa ubora wa uzalishaji wa mvinyo ambao tunazalisha ndani ya nchi ili kuhakikisha kwamba tunaingia kwenye ushindani kwenye soko la mvinyo;
Pili; Baada ya kupitisha sheria hii Serikali iangalie kama mvinyo unaozalishwa nchini utaweza kutosheleza mahitaji ya viwanda vyetu vinavyozalisha bidhaa za mvinyo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi naomba niunge hoja kwa Miswada hii. Ahsante sana. (Makofi)