Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hassan Zidadu Kungu (25 total)

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali iko katika mpango wa kutafuta pesa ya kujenga barabara hiyo ya Mtwara Pachani – Tunduru Mjini.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga angalau kilometa tano tu za lami ambapo barabara hiyo inapita Tunduru Mjini Na ofisi zote za Serikali pamoja na taasisi za Kiserikali ziko kwenye barabara hiyo ambapo hakuna lami kabisa na zipo mjini kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara nyingi zinazopita katika ofisi zipo ambazo tunazihudumia sisi, lakini pia na TAMISEMI. Tumelichukua hili, tutakutana na wenzetu wa TAMISEMI tuone namna ya kutafuta fedha ili miji hii iweze kupata lami angalau kwa uchache kama miji mingine. Ahsante. (Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante nimeridhishwa na majibu mazuri ya Serikali, lakini je, Naibu Waziri yuko tayari kuja Jimboni kwangu ili kuweza kutembelea miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Zidadu kwa umahiri wake wa ufuatiliaji wa miradi ya maji. Suala la kuja Jimboni manta hofu, nitafika. (Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, cyanide na mercury ni kemikali ambazo zote zina athari kubwa kwa maisha ya watumiaji. Lakini pia cyanide ndiyo ina gesi ambayo inatoa sumu kali ambayo inaweza kusababisha vifo kwa watumiaji ukilinganisha na zebaki.

Je, Serikali imetoa elimu kiasi gani kwa watumiaji wale ili kuepukana na madhara ambayo yanaweza kupelekea vifo kwa wachimbaji wadogo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa upatikanaji wa cyanide ni mchakato mkubwa na unahitaji mtaji mkubwa lakini pia unahitaji kuwa kibali ili uweze kununua cyanide jambo ambalo linapelekea wachimbaji wadogo wakashindwa kuipata hiyo kemikali ya cyanide.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kuipata kwa gharama nafuu ambapo sasa waweze kufanya shughuli zao za kila siku kama walivyokuwa wanaitumia mercury ambayo ilikuwa inaweza kukamata kwa 0.1 ambapo kwa kila siku wanakuwa wanazalisha na kuweza kupata chakula chao cha kila siku kulinganisha na cyanide? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu kwa maswali yake mawili mazuri hususan katika kuhakikisha tunawalinda wachimbaji wadogo wa madini na madhara ya matumizi ya kemikali hatarishi.

Mheshimiwa Spika, ni kweli wachimbaji wadogo huko nyuma na wengine hadi sasa wanatumia madini au mercury kwa Kiswahili zebaki ili waweze kuchenjua dhahabu ambayo wanatenganisha dhahabu, udogo na madini mengine. Lakini kimataifa nchi yetu inawajibika kusitisha matumizi ya zebaki kwa mujibu wa Mkataba wa Minamata. Kwa hiyo, ndomana saizi tunasisitiza matumizi ya cyanide.

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba cyanide ni ghali ukilinganisha na zebaki, kwa hiyo wachimbaji wengi wadogo hawana uwezo wa kumudu. Tunaendelea kushirikiana na Wizara ya Madini kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ya matumizi ya cyanide na namna ya kujikinga na madhara na watu wa madini wako hapa.

Mheshimiwa Spika, pia tumeshajenga vituo vya mfano kwa ajili ya wachimbaji wadogo kujifunza jinsi gani ya kutumia madini haya ya cyanide kwa wachimbaji wadogo, kwa mfano pale Rwamgasa, Mkoani Geita tumeweka kituo hicho, Katente pia Mkoani Geita na Itumbi, Mkoani Mbeya.

Mheshimiwa Spika, lakini nataka nikiri bado tunayo kazi kubwa ya kufanya kwa sababu bado wachimbaji wetu wadogo hawana elimu, lakini pia vifaa kinga vya kujikinga na madhara yatokanayo na madini haya hatari ya cyanide.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kwa kutumia mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini pamoja na wenzetu wa OSHA kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata elimu pamoja na kujikinga na madhara ya madini haya.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuwa na azma nzuri ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya zote 63. Swali dogo tu la nyongeza, je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa vyuo hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoanza kueleza katika swali la mwanzo kwamba vyuo hivi tutajenga vyote kwa pamoja na tunachosubiri sasa ni upatikanaji wa fedha ambazo ndizo tumeshafanya maombi kwa Wizara ya Fedha na Mipango; na mara tu tutakapopata fedha hizi ujenzi huu utaanza kwenye vyuo vyote 63 katika Wilaya zote 63 kwa pamoja. Nakushukuru sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Tunduru ni Wilaya ambayo ipo mpakani na jiografia yake ni mbaya lakini pia kituo cha polisi kuna gari moja tu na tuna kilomita za mraba 18,778.

Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kunihakikishia kwamba katika magari hayo 78 nasi tutapata gari moja? (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nirejee tena majibu yangu kama ambavyo nimejibu mwanzo kwamba tunatambua kwamba Jimbo la Tunduru lina uhitaji wa gari basi na lenyewe vilevile tumepokea.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Wilaya ya Tunduru ni kati ya Wilaya ambazo hazina vyuo vya VETA, na eneo la ujenzi wa Chuo tayari tumeshaliandaa na lipo: Je, ni lini Serikali itatujengea Chuo cha VETA katika Wilaya ya Tunduru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Hassan, Mbunge wa Tunduru, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi kwa wilaya zote 63, ujenzi utaanza mara moja mara tu tutakapopata fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango. Ujenzi huo tunatarajia kuanza kwenye Wilaya zote kwa pamoja ikiwemo na Wilaya ya Tunduru. Nakushukuru sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itafanikisha kampasi ya Tunduru kuanza rasmi masomo ya muda mrefu badala ya ilivyo sasa kwa masomo ya vitendo ambayo ni ya muda mfupi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kungu Mbunge wa Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi kwamba kampasi ile tayari ilishaanza kazi toka mwaka 2018/2019, lakini kozi ambazo zinatolewa pale ni zile za muda mfupi wanafunzi wetu wanapokwenda kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 tumetenga zaidi ya Shilingi Milioni 250 kwa ajili ya kuongeza miundombinu kwenye eneo lile. Katika mwaka ujao wa fedha tutatenga tena fedha zaidi ya Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kuongeza miundombinu ambayo itasaidia sasa chuo kile kiweze ku-operate katika masaa 24 kwa muda wote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya michakato hii kukamilika tunatarajia baada ya miaka hii Miwili hadi Mitatu tutaweza kuanza kozi pale za muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Nakapanya, jengo la upasuaji limekamilika na baadhi ya vifaa vya upasuaji vipo na ambulance ipo.

Je, ni lini Serikali itakamilisha baadhi ya vifaa vya upasuaji ili kituo kile kianze kutoa huduma ya upasuaji na kumsaidia mama na mtoto katika kituo kile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya hiki cha Nakapanya ni kweli kwamba kuna baadhi ya vifaa tiba vimeshafika, lakini tayari tumepanga watumishi kwa ajili ya kuanza kutoa huduma na tunafahamu kwamba kuna baadhi ya vifaa tiba hasa kwenye jengo la upasuaji bado havijafika.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye bajeti ya mwaka huu, vituo vyote hivi vya afya vilivyokamilika ikiwemo hiki cha Nakapanya kimetengewa fedha kati ya ile shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya kupeleka vifaa tiba ili vianze kutoa huduma za upasuaji kwa wananchi, ahsante.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itatujengea barabara ya bypass Tunduru Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara husika itajengwa kwa bypass baada ya kufanyika usanifu wa kina. (Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hospitali ya Wilaya ya Tunduru majengo yake ni machakavu kweli kweli; na mingoni mwa hospitali kongwe ile naweza kusema ni namba moja.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutujengea hospitali mpya kama sio kukarabati hospitali ile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Tunduru kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ameendelea kuwasemea kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Tunduru, na amekuja Ofisi ya Rais - TAMISEMI mara kadhaa kwa ajili ya kuomba ukarabati au ujenzi wa hospitali hii. Na mimi na yeye tumeongea mara kadhaa. Nimhakikishie kwamba kwenye bajeti hii ya 2022/2023 tutaona uwezekano wa kuingiza hospitali hiyo. Na kama tutashindwa kufanya hivyo basi tutafanya kwenye mwaka ujao wa fedha. Ahsante sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, niishukuru na kuipongeze Serikali kwamba imeongeza kilometa mbili za usambazaji wa umeme katika kila kijiji na kuifanya kilometa tatu badala ya kilometa moja; je, ni lini sasa Serikali itaanza utekelezaji huo wa kujazilizia kilometa mbili ili kila kijiji kipate kilometa tatu za usambazaji wa umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Spika,swali la pili, kwa kuwa mradi huu wa REA vijijini ni mradi wa umeme vijijini; je, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme vitongojini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza ni kweli Serikali ya Awamu ya Sita iliongeza kilometa mbili kwa kila kijiji ambacho kipo katika Mradi wa REA III Round Two ambao unaoendelea kutekelezwa. Kazi iliyofanyika ni kupitia maeneo yale ya vitongoji na kuyabaini ili hizo kilometa mbili zionekane wapi zipelekwe.

Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza majadiliano na wakandarasi yanaendelea na tunaamini kuanzia mwanzoni mwa wiki inayokuja hiyo mikataba ya adendum mikataba ya nyongeza ya kupeleka umeme kwenye hizo kilometa mbili itasainiwa na hivyo tunatarajia mwanzoni mwa mwezi wa tano wakandarasi wataingia site kuendelea sasa na hiyo kazi ya kupeleka umeme katika hizo kilometa mbili za nyongeza ambazo zinatakiwa ziongezwe.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili kwamba ni lini umeme utapelekwa vitongojini. Nipende kusema hata sasa umeme unapelekwa kwenye vitongoji, Miradi ya rea inapeleka umeme vijijini ambapo vijiji vinaenda kwenye vitongoji, lakini upo mradi maalum wa densification 2B ambao unaendelea katika vijiji karibu 1,600 na wakandarasi tayari wameripoti site na wanapeleka umeme katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi Serikali ipo katika taratibu za mwisho za kutafuta fedha kupeleka umeme kwenye vitongoji karibu 6101 ambavyo bado havijapata umeme na inahitajika takribani shililingi trilioni 6.5 ambayo tunaamini tutaipata kwa mbinu ambazo tayari tumepeleka maombi yetu Serikalini na mchakato wa kutafuta pesa hiyo unaendelea. Hivyo katika miaka minne mitano tunatarijia kuwa tumemaliza vitongoji vyote ambavyo havina umeme na huo ndio mpango wa Awamu ya Sita.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Tunduru ambapo taasisi zote za Serikali zipo katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kungu Mbunge wa Tunduru Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ni barabara za TANROADS zinapita tuna mpango wa kuhakikisha katika kila Miji hasa ya Makao Makuu ya Wilaya, ambapo barabara zetu zinapita basi zijengwe kwa kiwango cha lami. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge mara baada ya hapa tuweze kuonana kama barabara zetu zipo zinapita katikati ya taasisi hizo ambazo amezisema ili tuweze kuona utaratibu wa namna ya kuzijenga kwa kiwango cha lami katika hayo maeneo aliyoyataja, ahsante.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushuru. Kutokana na mpango wa umeme vitongojini kwa Wilaya ya Tunduru bado haujaanza na kuna taasisi mbili za kidini ambazo hazina umeme na ziko vitongojini. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya umeme kwenye taasisi hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, tayari Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetoa fedha za nyongeza za kupeleka umeme katika kilometa mbili za ziada ukiachana na ile moja ambayo tulikuwa nayo katika Mradi wa REA III Round II. Kwa hiyo, naamini katika nyongeza hiyo ya kilomita mbili itazidi kuingia kwenye maeneo ya vitongoji na taasisi hizo zikiwekwa ni za kipaumbele, basi Mkandarasi atafikisha umeme kwenye maeneo hayo kwa kipindi hiki ambacho tumepata nyongeza ya pesa ya kupeleka umeme katika kilomita mbili za ziada ukijumlisha na ile moja ambayo itagusa vitongoji vingi zaidi.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; lakini pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali dogo moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru na kupongeza mpango wa TARURA kwamba taa hizo zilizozungumzwa zimefungwa kwenye barabara ya mtandao wa TARURA ambayo ziko pembezoni mwa mji. Lakini kuna barabara ya TANROADS ambayo inapita katikati ya mji ambapo ndipo sura ya Tunduru Mjini. Je, ni lini Serikali itatufungia taa za barabarani kwenye barabara ile ya TANROADS? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhususiana na barabara hii ya TANROADS ambayo inapita katikati ya Mji wa Tunduru, nafahamu wenzetu wa TANROADS wana mkakati wa kufunga taa katika barabara zote zinazopita katika makao makuu ya wilaya nchi nzima si kwa Tunduru peke yake kwa sababu tayari za TARURA kuanzia sasa barabara yote ya lami inayojengwa na TARURA lazima ifungwe taa; hivyo hivyo na wenzetu wa TANROADS nao wameweka mkakati huo wa kuhakikisha barabara zote kubwa zinawekewa taa.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mwili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza: Je, ni lini ujenzi huo wa mita 500 utaanza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Barabara hii ya lami inapita katikati ya Mji na ndiyo kwenye sura ya Wilaya ya Tunduru: Je, ni lini Serikali itatufungia taa za barabara ili kusaidia ulinzi na usalama nyakati za usiku? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mita 500, tunavyoongea mkandarasi ameshapatikana na sasa hivi anajiandaa, yuko kwenye mobilization kuanza kujenga hizo mita 500 kwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, habari njema kwamba mwaka ujao katika huo mji ambao taasisi zote zinapita katika barabara ya TANROADS, tutajenga kilometa 2.1 na kuweka taa eneo lote katika mji huo wa Tunduru, ahsante. (Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza naomba kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa majibu mazuri yanayoonyesha nia na mkakati wa kuanza mradi ule, lakini bado nina swali dogo la nyongeza. Je, Naibu Waziri yuko tayari kutembelea eneo la mradi ili kujionea umuhimu au ukubwa wa uhitaji wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nipokee pongezi zake kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa iliyoifanya katika ujenzi wa vituo vya mabasi nchini kote. Nimhakikishie tu Mheshimiwa kwamba niko tayari baada ya kumaliza shughuli za Bunge, tutakubaliana baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tupange ratiba ya kwenda Tunduru tukapitie pale.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya Kuuliza swali la nyongeza. Rais wa Awamu ya Tano wakati wa uhai wake alipokuwa katika ziara Wilaya ya Tunduru aliahidi ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Namihungo. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais ya ujenzi wa kituo cha afya katika kituo cha Namihungo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ahadi za Viongozi wetu wakuu wa kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji wa miradi hiyo kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nachukua hoja hii, tayari najua tumeshaanza kuiratibu na tunatafuta fedha na mara fedha zikipatikana tutaleta shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo hiki cha afya, ahsante.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona; barabara ya Pachayamindu – Ngapa kuelekea Nachingwea, ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge, Serikali inatafuta fedha ili kwanza iweze kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, baada ya hapo gharama itajulikana na Serikali itafuta fedha kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa kutokana na Waraka huo wa Serikali sina uhakika sana kama unazingatiwa kwa Wilaya ya Tunduru, kutokana na mwaka jana tulipata Walimu wa Shule za Msingi 56 na waliohama ni 57. Je, Serikali ina mpango gani wa kutufidia wale waliohama?

Swali la pili, je, Serikali haioni haja ya kutoa Waraka maalum kwa ajili ya Tunduru pekee kwa kuwa wale wote wanaohama labda inawezekana kutokana na mazingira waliotokea na wanayokwenda kuyakuta hawakubaliani nayo.

Je, Serikali haioni haja ya kutuletea ama kuajiri waajiriwa ambao wanaotokana na maeneo yale ili waendelee kubaki pale na kupunguza kero hiyo ya kuomba kuhama? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu kilio cha wananchi wa Tunduru kilishafikishwa katika Ofisi zetu mbili zote ikiwemo Ofisi ya Rais, Utumishi ili kuweza kuyashughulikia na hizo taratibu kufuatwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali, kwa maana ya kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi hilo jambo tumeshalichukua na tutakwenda kulifanyia kazi na Mheshimiwa Mbunge tutakapokuwa tayari tutakujulisha ili upate kujua hatua ambayo zimefikiwa katika jambo la kufidia hili gap lililopo katika upande wa walimu wako.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili nataka kumhakikishia Mbunge kwamba siyo taratibu za Serikali kutengeneza Waraka kwa ajili ya Halmashauri moja au Wilaya Moja. Waraka ni kwa ajili ya Tanzania nzima ili kuweza kukabiliana na changamoto iliyopo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imechukua kilio hicho na inakwenda kukifanyia kazi na itakapokuwa tayari tutakuja kumjulisha yeye pamoja na Bunge lako.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri naona umesimama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru juu ya eneo linalohusu watumishi kuwa wako kwenye harakati za kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine muda mwingi kuliko hata kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, wewe ni Mbunge unajua kinachotokea, jambo hili linapaswa kupatiwa majibu ya uhakika kwa sababu ni kweli kabisa kwamba watumishi wengi wanapangiwa mahala na wanakwenda kule kwa mipango ya harakati za kuanza kuondoka toka siku waliyofika. Ni ukweli kwamba huwezi ukazuia mobility ya watumishi wa umma kwa sababu wao ni binadamu kuna changamoto na mambo mbalimbali yanayowasibu pia.

Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya watumishi ambao wao ni wanandoa wanachangamoto kubwa unamkuta mume yupo Kigoma, mke yuko Mbeya familia hii inapata changamoto ya kutokuwa Pamoja, pia watumishi hawa hawatafanya kazi kwa ufanisi kwa sababu muda mwingi wanafikiria juu ya mwenza wake yuko mbali.

Mheshimiwa Spika, jambo hili wacha tulichukue tusijibu kwa haraka tukae na mamlaka za ajira na hasa TAMISEMI ili tuweze kutengeneza mfumo mzuri, tuangalie pengine inawezekana huko Tunduma ambako wanahama walipelekwa ambao hawapendi Tunduma lakini wako wengi wanaopenda kwenda Tunduma kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, tutajaribu kutengeneza utaratibu tuone tunaweza tukafanyeje bila kuvunja umoja na mshikamano wa Taifa letu kwa sababu pia kuwapangia watu kutoka sehemu aliyotoka huko huko itakuwa ni jambo, lakini wapo wanaoweza kuwa wanapenda kwa kiasi fulani, tunaweza tukafanya maamuzi hayo kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itapeleka Mradi wa Maji katika Kata ya Kalulu na Kata ya Jakika? Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata hizi alizozitaja mwaka ujao wa fedha tunatarajia kupeleka maji safi na salama kwa kupitia visima vilevile maeneo mengine tutatumia vyanzo vile vilivyo vya uhakika.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Wilaya ya Tunduru imezungukwa na hifadhi ya wanyamapori na wananchi wa Tunduru wanategemea kilimo. Kutokana na uvamizi wa tembo uharibifu ni mkubwa pamoja na watu kupoteza Maisha, na Serikali inatumia kiwango kikubwa sana kulipa fidia kwa wananchi.

Je, Serikali sasa haioni haja ya kuwaajiri wale askari wa VGS ambao wako vijiji vyote na kuwatengea posho, ili kupunguza hizi athari na kutokana kwamba watumishi hawa wa wanyamapori wako saba tu Wilaya nzima? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea maswali tisa ya nyongeza kwa Waheshimiwa mbalimbali na naomba niyajibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Londo; ameuliza ni nini kauli ya Serikali? Kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi. Ni kwamba sasa hivi tunaangalia njia mbadala wakati huo huo tunaendelea kutatua migogoro hii ya wanyama wakali na waharibifu. Tunajenga vituo, tunaajiri VGS, lakini wakati huo huo tumeshaweka sasa mipango kwenye baadhi ya maeneo tuanze kuweka fence ya umeme ili kupunguza hii athari ya wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la Mheshimiwa Anne Malecela, naomba niahidi mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba baada ya Bunge hili tutaongozana naye katika maeneo yale. Lakini pia tumeshaanza kuongeza nguvu kwake, tumepeleka askari na tutaendelea kuajiri VGS katika maeneo hayo ili tuweze kushirikiana pamoja. Kwa hiyo, wananchi wa Same kilio chenu kimeshasikika Bungeni na tutaongozana na Mheshimiwa Mbunge (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la Mheshimiwa Vita Kawawa, ni kweli Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya ujenzi wa madarasa katika jimbo lake, na huu ulikuwa ni mpango wa CSR si kwa ajili ya fidia ya wanyama wakali na waharibifu. Ni kwamba Mheshimiwa Waziri alifanya ziara katika jimbo hilo na akatoa ahadi ya ujenzi wa madarasa ili kuwafanya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo tushirikiane pamoja katika uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee tu kuahidi kwamba ahadi ni deni, Wizara itatekeleza. Na kwa kuwa ilikuwa ni kauli ya Mheshimiwa Waziri basi tutafuatilia ili ahadi hii iweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dunstan, Mbunge wa Mkinga, yeye ameongelea kuhusu kituo; niahidi tu kwamba katika mpango wa fedha wa 2023/2024 uliopitishwa katika Bunge lako hili, tutapeleka kituo katika Jimbo la Mkinga ili tuongeze nguvu ya kudhibiti wanyama wakati na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Justin Nyamoga, madhara makubwa; naomba niahidi tu kwamba tutaendelea kufuatilia katika maeneo haya ili wananchi waweze kulipwa fidia inayotokana na wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Grace Tendega; naomba tu nilitaarifu Bunge lako, na kwa ridhaa yako, nipe tu nafasi kidogo nitoe ufafanuzi. Tumekuwa na changamoto nyingine imejitokeza katika Mkoa wa Iringa; kuna uvamizi wa simba kwenye baadhi ya maeneo, lakini naomba niwataarifu wananchi, nadhani wameona juhudi za Serikali toka uvamizi huu umejitikeza tumekuwa karibu na wananchi, tunatoa elimu.

Mheshimiwa Spika, naniendelee kutoa elimu kupitia Bunge lako hili, kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa simba, wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku. Lakini pia wenye mifugo wawashe moto kuzunguka maeneo yale ya mifugo ili kuepusha simba wasisogee katika maeneo hayo tunajitahidi sana kulinda maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Wanairinga, Serikali iko kazini na tumeshapeleka helikopta inazunguka usiku na mchana kuhakikisha tunawasaka hawa simba. Tuendelee kushirikiana pamoja ili kuhakikisha zoezi hili tunalikamilisha na simba hawa tunawachukua na kuwarudisha katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mheshimiwa Charles, Mbunge wa Mwibara; kumekuwa na changamoto ya viboko na tembo. Naomba niendelee tu kuahidi, nakumbuka tuliwasiliana na Mheshimiwa Mbunge na tukaongeza nguvu ya askari katika maeneo hayo. Tuendelee tu kuwasiliana, nguvu tutaongeza lakini pia tutaendelea kuajiri VGS ili waweze kusaidia pale inapotokea dharura katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ombi la Mheshimiwa Jimbo la Tunduru kwamba tuongeze VGS (askari wa vijiji). Tunaomba tulipokee hili na tutaweka priority katika eneo hili, tunajua hii changamoto ya wanyama wakali.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna shida moja ya mratibu ambaye alihamishwa. Nadhani maelekezo yameshatoka, atarudishwa katika eneo hilo ili aweze kushirikiana na wananchi kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Matiko tayari nimeshalijibu, kwamba tuko kwenye process ya ku-review hizi sheria na kanuni kuangalia sasa angalau tusogeze kiwango fulani ili wananchi nao waweze kuona umuhimu wa namna ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Kituo cha Afya cha Namiungo, ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni Hayati, alitoa ahadi Milioni 500 ili kuweze kukamilisha Kituo cha Afya cha Namiungo. Sasa je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kituo cha Afya cha Nakapanya, kilitengewa fedha kiasi cha shilingi milioni 400 mwaka wa fedha 2021 na kilipokea shilingi milioni 200 na kujenga majengo ya upasuaji pamoja na maabara.
Je, ni lini Serikali itatupatia kiasi kilichobaki ili kuweza kujenga majengo mengine muhimu kama vile mortuary na mionzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeza sana Mheshimiwa Kungu kwa namna ambavyo anawakilisha kwa dhati wananchi wa Tunduru Kaskazini, na nimhakikishie kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kipaumbele cha Serikali. Tunafahmu kwamba Namiungo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, nasi tayari tumeshaweka mpango wa kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Namiungo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Nakapanya, hiki ni kituo kati ya vituo 52 ambavyo katika mwaka wa fedha huu tumetenga Bilioni 15.6 kwa ajili ya umaliziaji wa vituo hivi kikiwemo kituo hiki cha afya cha Nakapanya. Ahsante.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, kituo cha afya cha Matembanga kiko kilometa 80 kutoka hospitali ya Wilaya ya Tunduru Mjini na tayari tunaishukuru Serikali majengo ya upasuaji yamekamilika na vifaa vyote vimekamilika na tumeanza upasuaji hapa majizi na kituo kile hakina gari la wagonjwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupatia gari la wagonjwa kituo kile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba tunafanya tathimini ya vituo vya afya ambavyo vimekamilika na vinatoa huduma za upasuaji kikiwemo kituo hiki na kuona uwezekano wa kupata gari la wagonjwa, lakini itategemea idadi ya magari ambayo tunayo na kipaumbele cha halmashauri kulingana na vigezo vya kitaalamu vya uhitaji wa magari ya wagonjwa.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujua ni njia gani nzuri Serikali inatumia kwenye matumizi ya cyanide, kwa sababu madhara ya zebaki ni bora zaidi kuliko madhara ya cyanide ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende tu kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba handlings kwa Kiswahili tunasema jinsi unavyo itumia cyanide kwa usahihi kwa kutengeneza yale malambo na kuweka tiling zile za kuzuia ili isivuje chini ya ardhi, ni njia ya uhakika kabisa kwamba ukishaitumia na ukaiacha ika-evaporate ndani ya anga/hewani haiachi madhara yoyote na ni salama zaidi kuliko zink ambayo upoteaji wake au biodegradability yake ni ngumu zaidi ya kuhifadhi katika maeneo ambayo hakutakaa kuwe na leakage.

Kwa hiyo, utaalam wa cyanide siyo mgumu kama ambavyo yeye anadhani na ni wa uhakika zaidi na ni salama zaidi kuliko zebaki.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kutoa ajira kwa mkataba wa muda mfupi kwa askari wa VGS ilikuweza kupunguza tatizo kubwa ama uhaba wa askari wa wanyama pori nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inao mkakati wa kuhakikisha kwamba pale ambapo mafunzo ya askari wa vijiji yamefanyika na kumekuwa na uhitaji wa askari hawa kupatiwa ajira, tunashirikiana na halmashauri kuona jinsi ambavyo kupitia miradi mbalimbali tulioyonayo akari hawa badala ya kupewa ajira wanaanzishiwa miradi itakayowaingizia kipato ili wakati wakifanya shughuli hii ya uhifadhi lakini vilevile waweze kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Spika, tumeanza zoezi hilo kwa mradi wa REGROW ambao unajielekeza kwenye kufungua fursa za utalii katika mikoa ya Kusini tunaamini mafunzo tutakayoyapata kutokana na mradi huu yatatuonesha ni jinsi gani tunaweza kuendeleza katika maeneo mengine.