Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Vita Rashid Kawawa (24 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Mpango wetu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nia na lengo la Mpango wetu huu ni kuendelea kukuza uchumi, kupambana na umaskini na ku-maintain hali ya nchi kuendelea kuwa nchi ya kipato cha kati lakini kuelekea kwenye higher middle income. Hii ina maana Mpango una malengo ya kuleta ustawi wa watu wake na kuongeza kipato cha chini na uchumi wa jamii na kuleta ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi. Ili kuleta ustawi mimi nashauri Mpango uende sambamba na utekelezaji wa miradi ya utoaji huduma iliyokusudiwa katika Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika katika Mpango uliokwisha. Serikali imewekeza kwa wingi sana kwenye miradi mkakati au naweza nikasema product capacity project kubwa, reli, umeme, viwanja vya ndege, barabara na kadhalika. Katika eneo hili la umeme imewekeza sana, leo tunao umeme vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji yeyote anayewekeza anatakiwa lazima pia afahamu anatakiwa apate kile alichowekeza na Serikali imewekeza umeme ili kusaidia shughuli za kiuchumi kuanzia chini. Hapa nashauri Mpango uangalie uwezekano wa ku-trickle down economic activities katika maeneo ya vijijini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakulima tunalima lakini kazi yetu tukishalima mara moja tunauza basi, watu wanakaa wanasubiri mwaka unafika. Sasa umeme umefika vijijini, Mpango lazima uangalie kuhamasisha sekta binafsi kuona uwezekano wa kuleta viwanda vidogo kule vijijini lakini pia wale wawekezaji wengine waliokuwepo hapa kuona uwezekano wa kuanzisha viwanda vya kuwekeza kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namfahamu kijana ambaye anatambulika na SIDO, NYUMBU pia wanamtumia, amesoma Urusi na Uchina, yeye ana-assemble viwanda vidogo vya kutengeneza mafuta haya ya michikichi na pia anatengeneza viwanda vidogo vya kutengeneza sabuni. Ushauri wangu Serikali iwe na mpango wa kushawishi makampuni makubwa yanayoweza kuingiza viwanda vidogo kwenye vijiji vyetu ili wanaozalisha alizeti wakachakata alizeti, wanaozalisha mpunga wakakoboa mpungu. Hii itasaidia kuwa na activities za mwaka mzima pale, wa kuchakata mpunga, pumba za mpunga zitatumika kuchomea tofali; unga wa pumba za mpunga utaingia katika viwanda vya chakula cha mifugo na pia tutaendelea kuuza mali ambayo imeongezewa thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuuangalie jinsi gani ya kupata wawekezaji wakubwa wanaoweza kuingiza viwanda hivi vidogo. China kuna viwanda vidogo na vya kati ambavyo vinauzwa kuanzia Dola 3,500 mpaka China. Sasa tukiweza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa sekta binafsi wakaweza ku-import hizi tukapeleka huko vijijini, tukaondoa mentality ya sasa hivi ya kijijini mtu akistaafu, mtu akiwa mwalimu au mtumishi wa Serikali, akikopa ananunua pikipiki ndiyo anafanya biashara, kwa hiyo, biashara yake ni ya service. Sasa tutoe mentality zile wawekeze kwenye viwanda vidogo hivi vya uzalishaji ambavyo vitaajiri vijana wetu waliokuwepo kule vijijini na tutaongeza thamani ya mazao tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili naomba nizungumzie ustawi wa shughuli zetu za kiuchumi, kilimo na mifugo. Leo kuna mifugo 33,000,000 na inasambaa tu na inasumbuana na wakulima lakini sasa hivi imefikia mahali inasumbua pia Hifadhi za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alielekeza katika hotuba yake humu Bungeni kwamba watatenga hekta milioni 6 kwa ajili ya kuweka blocks za wafugaji ili waweze kufanya shughuli zao vizuri na wasiteswe, hili ni jambo zuri kabisa. Naomba sana hili lifanyike kwa sababu wafugaji wanaingiliana sana na wakulima. Leo hii sisi kwetu Namtumbo wafugaji waliondolewa Morogoro wameingia Namtumbo sasa hawana mahali maalum, wako ndani ya hifadhi na wako ndani na wakulima.

(Hapa kengele iligonga kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mpango utenge ardhi kwa ajili ya hawa wafugaji ili kuleta ustawi katika maeneo yetu. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 6) Bill, 2021
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika ahsante sana, kwa kunipa fursa hii kuchangia Muswada huu wa sheria wa dharura au special Bill Miscellaneous Amendment.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nikupongeze wewe mwenyewe, nataka kuzungumzia kuhusiana na kifungu hichi cha 83(b), ambacho kinaondosha ile sheria iliyopishwa ya withholding tax kwenye mazao ya kilimo. Nilipouliza swali hili kutaka kujua ukweli kwa wakulima kwa sababu wakulima walikuwa wanalalamika wanatozwa kodi ya asilimia 2 na Serikali ilitujibu kweli inatoza hizo asilimia 2 kwa ajili ya sheria.

Mheshimiwa Spika, ulilisimamia hili ukaliona kwamba si sahihi, tunakushukuru sana na ulitaka mpaka kuipangua Kamati ya Bajeti ambayo kumbe nayo ilishatoa mapendekezo sheria hii isiwekwe kwa ajili ya kuwakata wakulima asilimia 2 ya withholding tax. Kwa hiyo, nakupongeza kwanza wewe kwa kulisimamia hili vizuri sana na mpaka leo Serikali imerudisha kwa dharura mswada huu ili kutoa kifungu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nawapongeza pia kamati ya bajeti na wao kama ulivyowapongeza wamerudia na kuifanya kazi hii kwa haraka sana. Mchango wangu katika eneo hili mapendekezo yangu kwanza sisi kwenye tumbaku zao hili linajenga mjengeko wa bei mwezi wa pili, na tulipojenga mjengeko wa bei hii ambao unashirikisha wakulima, wadau lakini na wanunuzi, haikuweka kifungu ambacho au kipengele ambacho kitakuwa kinakatwa withholding tax.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ilipokuja hii iliwanchanganya sana kwa sababu mauzo ya tumbaku yalianza mwezi wa 6 na wa 7 na wa 8, kwa hiyo iliwachanganya sana wakulima na fedha zao mpaka sasa tunavyozungumza zimekuwa withhold na makampuni kwa mujibu wa sheria hii. Lakini isitoshe pia kwenye korosho mwezi wa kumi mnada uliopita nao pia wakulima wamekatwa hii withholding tax asilimia 2. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu nilikuwa nataka kuona na hata kwenye pamba vile vile yamefanyika hayo makampuni ya withholding asilimia mbili. Ushauri wangu Mwanasheria Mkuu kama anaweza kuiandika vizuri kisheria kwamba kuanzia sheria hii inapopitishwa basi iwe imefuta pia toka ilipopitiswa ili wakulima hawa makampuni yarudishe fedha zao kwao, kwa sababu kwenye korosho leo hii mwezi wa kumi wameshafanya mnada, aliyeuza mwezi wa 10 amekatwa hii asilimia mbili lakini atakeuza mwezi wa 11,12 na Januari hatokatwa tutakapopitisha sheria hii, kwa hiyo italeta mtafaruk hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba sheria kama Mwanasheria Mkuu akiiweka kwamba kuanzia ilipopitishwa mie naichukulia kama ilipitishwa kimakosa kwa sababu kamati ya bajeti ilishauri sheria hii isiwekwe kifungu hiki lakini Serikali ilileta tukapitisha, sasa kuanzia tarehe hii ilopitiswa basi ifutwe na wakulima wale makampuni walio- hold fedha za wakulima ambazo mpaka saivi hawajawasilisha TRA na TRA ina demand zile fedha basi irudishe fedha zile kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu ulikuwa ni huu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru nami kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha vyema hotuba yake iliyo-cover na kusheheni maeneo yote kwa ujumla na ufasaha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa majukumu ya Kikatiba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali, lakini pia kusimamia shughuli za Serikali Bungeni. Kazi hiyo imefanyika vizuri sana katika kipindi kilichopita; wameisimamia Serikali katika miradi ya kimkakati vizuri na mafanikio ya miradi yote tunayoiona ni kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nzuri iliyokuwa inafanyika Bungeni humu ni kazi ambayo imefanywa chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Waziri Mheshimiwa Dada Jenista Mhagama. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa kazi nzuri walioifanya. Kubwa ni ile kazi iliyotukuka na ikatufanya tukakaa kwa amani kabisa wakati wa kipindi cha msiba kwa aliyekuwa Rais wetu. Walifanya kazi ya uratibu mzuri wa maziko ya Rais wetu aliyetutoka na tukafanya kazi ile ya maziko kwa mafanikio makubwa sana na dunia imetupa heshima kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze katika kutoa ushauri wangu. Kazi kubwa ya miradi ya kimkakati imefanyika, sasa naiomba Serikali ijielekeze sana sasa hivi katika kuweka mazingira bora ya uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu inayojengwa au iliyokamilika. Kwa mfano, sekta mtambuka ziangalie ni jinsi gani zitaweza kutumia fursa ya SGR ambayo inajengwa, inaenda kukamilika sasa hivi.

Je, kwa mfano Wizara ya Ardhi na Wizara ya Viwanda na Biashara zimepitia na kutambua ardhi na kuweka mkakati wa viwanda katika maeneo ambayo itapita SGR ili tuweze kuvutia wawekezaji kwenda kuwekeza katika maeneo hayo tuweze kuitumia SGR effectively? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili pia Wizara ya Kilimo inaweka mpango gani kushawishi wawekezaji au wakulima wakubwa wakatambue maeneo inakopita SGR wakaweka kilimo kikubwa pale ili tuweze kutumia reli ile ya kati? Pia Wizara ya Maliasili nayo ina mpango gani wa kushawishi kuweka mashamba makubwa ya miti katika maeneo inapopita SGR? Hapa nina maana fedha nyingi zimewekezwa katika ujenzi wa reli hii, lakini inapopita reli kwa eneo kubwa ni kwenye mapori ambayo yalikuwa hayatumiki. Sasa ni fursa kwa sisi kama Serikali kushawishi sekta binafsi kuwekeza katika maeneo hayo ya kilimo, ya viwanda vitakavyo support kilimo, lakini pia kuwekeza katika mazao ya misitu ya mbao ambayo yana soko kubwa katika nchi zetu zinazotuzunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze jimboni. Naishukuru sana Serikali Waziri Mkuu ameeleza mafanikio yaliyofanyika katika kipindi hiki cha nyuma. Sisi wa Namtumbo tunawashukuru sana, Serikali imewekeza karibu billioi 27 katika usambazaji wa umeme, katika kuunganisha umeme wa grid katika Wilaya yetu na maeneo makubwa katika vijiji vyetu vimewekwa umeme na vingine vilivyobakia changamoto iliyopo ni katika vitongoji, lakini baadhi ya maeneo katika kuunganishwa umeme. Kwa hiyo tunaomba sana katika eneo hili mafanikio makubwa tumefanikiwa. Katika Sekta ya Afya Serikali ilituingizia bilioni moja na milioni mia nane na imetujengea hospitali ya wilaya. Haya ni mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio mengine, Serikali imetujengea Chuo cha Elimu cha VETA kilichogharimu bilioni sita na milioni mia tano na chuo sasa kinatumika. Tunachoiomba Serikali sasa iwekeze kwenye rasilimali watu katika maeneo haya ya elimu na afya ili waweze kuja kwa kutosha waweze kutoa huduma iliyokusudiwa kwa sababu tumeweka fedha nyingi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika maeneo ya kilimo sisi ni wakulima wakubwa sana wa mazao ya mahindi na tunategemea sana pembejeo, lakini katika wakati pembejeo za kilimo zinasambazwa bei inabadilika kila siku. Tunaomba Serikali kwa kuwa kwenye mpango Serikali imesema kutakuwa na tathminini ya ufuatiliaji wa miradi, lakini pia ifanyike tathmini ya masoko ya pembejeo. Tuangalie pia masoko ya mazao yetu mchanganyiko, tunaiomba sana Serikali ifungue masoko haya ya mazao mchanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara; katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ambao tulikabidhiwa na sisi ndio tulienda kuinadi katika uchaguzi, tuna barabara mbili kubwa za lami ambazo tunatakiwa tujengewe kutoka Mtwara Pachani kwenda mpaka Tunduru na kutoka Lumecha kwenda Kitanda hadi Malinyi Ifakara. Tunaomba sana Serikali katika mpango wake wa bajeti iziweke barabara hizo mbili katika utekelezaji kama ilani yetu inavyoelekeza. Tumeinadi ilani hiyo, tumeisema kwa wananchi kwa msingi mkubwa kwetu Wilaya ya Namtumbo Wizara ikianza kututekelezea ujenzi wa barabara hizi mbili; kwanza, barabara ya kutoka Lumecha kwenda mpaka Ifakara kupitia Malinyi inapunguza kilomita 350 kwa barabara tunayopita sasa hivi. Kwa hiyo tunaomba sana Serikali itutekelezee ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia na ninaunga mkono hoja zote tatu za Kamati. Vilevile nakushukuru wewe kwa kutuongoza vizuri Wabunge na kutuwezesha kufanya kazi zetu vizuri na kwa weledi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako lina mchanganyiko wa Wabunge wazuri wenye weledi mkubwa sana. Pia naomba nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifungua nchi kuitafutia fedha na pia kubwa, ku-control uchumi wa nchi yetu ambao umeweza kuhimili mfumuko (inflations rate) ambao upo duniani kwa sasa hivi. Nchi yetu imeweza ku-control, kwa mfano tu wa haraka haraka, duniani huko nchi iliyotutawala, Uingereza mpaka Septemba inflations rate yao, wao wali-target 2% ya infations rate, lakini mpaka Septemba, 2022 wamekuwa na inflations rate ya 10.1 percent kwa maana ya two digits.

Mheshimiwa Spika, kwa uwezo wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa ku-control uchumi wetu, sisi tumeendelea kuwa katika single digit ya uchumi wetu kwa maana ya kudhibiti kwa mfano mafuta, kupeleka ruzuku, pia lingine kubwa kuweka ruzuku ya mbolea kwa wakulima. Kwa hiyo, tunamshukuru sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, wetu.

Mheshimiwa Spika, pia kwenye hili la mbolea kabla sijaenda kwenye mada, tunaishukuru sana Serikali baada ya kuiomba kuweka kituo cha ununuzi wa mbolea Namtumbo ambacho kilikuwa Songea Mjini. Watu wa Namtumbo walikuwa wanatembea kilometa nyingi kwenda kufuata mbolea. Serikali ilisikia na imefungua kituo Namtumbo Mjini. Hata hivyo, bado haitoshi, tunaomba mbolea za ruzuku ziende vijijini kwa wakulima kama ilivyokuwa hapo nyuma. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itafakari ione jinsi gani inaweza ikasaidia kwenye hili.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein Bashe.

T A A R I F A

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Vita na Wabunge wote, siyo rahisi kwa Serikali kufungua vituo vya kuuzia mbolea katika kila kijiji katika nchi yetu. Vituo vya kuuzia mbolea ya ruzuku vitafunguliwa katika centers ambazo hapo awali biashara ya mbolea ilikuwa inafanyika na kwa Wakala ambaye atafikia vigezo tunavyoviweka vya udhibiti ili tusirudie matatizo yaliyotokea 2014, 2015, 2016 ambapo ruzuku haikumsaidia mkulima, bali iliwasaidia Mawakala na Wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge waelewe kwamba kama una concern ya eneo, wasiliana na Wizara, tutali-evaluate eneo hilo, kwa sababu unaweza ukapeleka kijijini gharama ya kusafirisha na ku-supply mbolea kule kijijini, mantiki yote ya ruzuku ikawa imekufa na wala isiwepo bila sababu yoyote. Kwa hiyo, tutafungua katika maeneo ambayo awali mbolea ilikuwa inauziwa na distribution tutendelea kuiongeza kadri ambavyo inawezekana.

SPIKA: Mheshimiwa, kabla sijamwuliza Mheshimiwa Vita Kawawa kama anaipokea taarifa hiyo, nadhani jambo la msingi ni kwamba mbolea isogezwe kwa wakulima. Hilo ndilo jambo la msingi. Sasa hoja ya kila Kijiji ni namna Mheshimiwa Mbunge anavyojenga hoja yake, lakini hoja ni kwamba maeneo ambayo wakulima ni wengi, mashamba ni makubwa, mbolea isogee kwao ili kuwapunguzia mzigo wa kusafiri umbali mrefu kwenda kufuata mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Vita Kawawa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, kuipokea ni ngumu kweli. Napokea maelekezo yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Sasa nirudi kwenye hoja. Taarifa ya CAG imetueleza kwamba baada ya kufanya tathmini, fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 185, kulikuwa na Shilingi bilioni 838 hazikupelekwa kwenye miradi ya maendeleo na pia matumizi ya kawaida. Pia imejitokeza taarifa ya CAG inasema, kuna Halmashauri 39 zilipokea fedha za makisio ya bajeti zilizohidhinishwa ziada Shilingi bilioni 74.38 kama 8% ya makisio yaliyoidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, hapa utakuta kwamba kuna halmashauri zimepata zaidi ya makisio yao ya bajeti ambayo yaliidhinishwa na Bunge lako Tukufu, lakini kuna halmashauri ambazo zimepata upungufu. Sasa ushauri wangu hapa ni kwamba, siyo vyema kwa Watumishi wa Serikali ambao wana disburse fedha hizi wakazigawa halmashauri. Halmashauri nyingine zinapendelewa, nyingine zinanyimwa fedha. Tutoe kulingana na tulivyoidhinisha kwenye Bunge letu Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa Kamati unasema katika ukurasa wa nane wa kwenye kishikwambi kwamba, Kamati imeona kuwa dosari hizo hazikutokea kwa bahati mbaya na ishara ya mkakati maalum unaoratibiwa na baadhi ya Watumishi wa Umma wasiokuwa na uadilifu kwa lengo la kuwa na upendeleo, udanganyifu na ubadhirifu. Katika hili, naomba Serikali na sisi Bunge katika maazimio yetu tusimamie ili Wizara ya Fedha ihakikishe inatoa fedha sawa kwa wote kama walivyoidhinishiwa na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Wizara ya Fedha itueleze katika eneo hili ambalo kuna baadhi ya halmashauri zimeongezewa fedha za ziada nje ya bajeti iliyoidhinishwa imelifuatitia kama kweli fedha hizo za ziada zilizotoka nje ya bajeti zilifanya kazi gani huko katika halmashauri zilikopelekwa? Suala la tatu, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe azimio lake kwamba, Bunge lifanye uchunguzi ili kubaini iwapo fedha zilizotolewa zaidi, au nje ya bajeti haikuwa na viashiria vyovyote vya upendeleo, udanganyifu au ubadhirifu.

Mheshimiwa Spika, vilevile Kamati iliendelea kusema halmashauri nyingi hufanya manunuzi kwa dharura bila kuzingatia mipango ya manunuzi kwa mradi wa mwaka. Wote tunafahamu kuna Sheria ya Manunuzi, lakini ukitazama shida iliyojitokeza hapa kubwa ni kwa sababu mfumo huu wa force account, ni mzuri lakini lazima tukubaliane kuwe na kiwango maalum cha fedha za miradi itakayofanyika kwa huu mfumo wa force account. Tukiacha mradi wa fedha, Shilingi milioni 800, Shilingi bilioni moja, Shilingi bilioni mbili, ukaendeshwa kwa mfumo huu wa force account peke yake, ndiyo shida hizi zitaendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini kinatokea? Kinachotokea ni kwa kwamba Watumishi wa Halmashauri ndio wanaonunua vifaa na wanatafuta fundi. Sasa hapa kwenye ununuzi wa vifaa mradi unaanza; wakati ukiwa kwenye msingi, Watumishi wa Halmashauri, Idara ya Manunuzi inanunua vifaa vyote vya mwanzo mpaka msumari wa bati, mpaka rangi inanunuliwa kwa mara moja. Ukitazama kiuhalisia kwenye tender au kwa Wakandarasi wanaofanya kazi hizi, huwa wanapewa fedha kulingana na kazi waliyoaifanya. Sasa pale wanaponunua vifaa vyote kwa mara moja, kwa maana nyingine wanaweza wakanunua vifaa vile kwa interest yao ya ten percent au wapate ziada, wana-inflate rate za bei na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaponunua vifaa vyote vile kwa pamoja, inapofika mradi umefikia mwishoni, fedha zimekwisha na kuna vitu vya msingi vinatakiwa, wanakosa fedha za kuzifanya. Kwa mfano, kwangu Namtumbo yaliyotokea Waziri Mkuu alipokuja kuangalia na kuona milango iliyokuwa chini ya kiwango, kwa sababu fedha zote zimekwisha, hawana fedha za milango, wanaenda kuchukua fundi wa Mwembeni kutengeneza mlango, ndiyo yaliyotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile siyo hayo tu, ukiondoa hiyo, baadaye wameingia tena kula hata mbegu yenyewe. Kwangu Namtumbo kule kuna mradi ulikuwa wa kutengeneza vyoo vya zahanati zetu tano. Wameenda kununua cement 1,200 lakini zilizoshushwa ni cement 600, na 600 nyingine zimeshuka huko njiani. Pia wameenda ku-order milunda 800 ya kutengenezea vyoo. Unatengeneza vyoo vya shimo ili uweke milunda ufunike! Milunda ya nini kwenye vyoo? Milunda haikuletwa, fedha zimelipwa toka mwaka 2021. Waziri Mkuu anakuja ndiyo wamestuka, wameenda kuleta milunda 800 wameilundika. Waziri Mkuu akastukia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala la force account nalo tunasema lazima tuliangalie. Hayo makosa yataendelea kuwepo, lazima tuwe na limit ya fedha kwa ajili ya Miradi ya force account. Miradi mikubwa ya fedha nyingi lazima itumike na Wakandarasi. Tukubali, tusikatae, mradi wa bilioni na zaidi hauwezi kutumiwa tu na fundi. Lazima tuangalie hilo pia. Vilevile kuepusha gharama. Kwa mfano, yaliyotokea kwangu Namtumbo kwenye hospitali ya Wilaya, fundi yule kashamaliza kazi yake, hakuna fedha za kuweza kurekebisha ile milango. Tunamlazimisha sasa technician aliyesimamia atengeneze kwa gharama yake. Ingelikuwa kazi ile inafanywa na Mkandarasi, kuna fedha zinabakizwa pale, hapewi miezi sita. Kama kuna dosari, anarekebisha.

Mheshimiwa Spika, sasa hili la force account ndiyo hasara yake hiyo. Pia force account fundi hela zote zile hazilipiwi kodi. Anapopewa Mkandarasi, analipa kodi;0 analipa service levy kwenye Halmashauri na pia analipa TRA. Hela nyingi kwa ajili ya force account kwa fundi tu hailipwi, Serikali hai-collect, inatoa tu, lakini ikimpa Mkandarasi, Serikali pale inatoa na inakusanya kodi.

Mheshimiwa Spika, leo hii mradi wa bilioni nne kwangu unajengwa na shule ya wasichana wanapewa mafundi wa kawaida. Pale Serikali haitakusanya na halmashauri haikusanyi, lakini on top of that wana-inflate rate ya vifaa vile.

SPIKA: Sekunde 30, malizia.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wana-inflate rate ya vifaa, gharama inakuwa kubwa, matokeo yake CAG anakuja kuona hayo, kwa hiyo, haya yataendelea kuonekana kutokana na watumishi wasiokuwa waadilifu. Nakubaliana kabisa watumshi wote ambao pia, hawakuwepo, shida wanayoipata Kamati zetu hizi wakiwaita, unakuta waliokuwepo sasa hivi wanakwambia mimi nina miezi miwili sikulifahamu hili. Kwa hiyo, tunaomba wale wote waliokuwepo mwaka huo 2021, waitwe watoe majibu kutokana na hoja za CAG na hatua zichukuliwe.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kunipa fursa hii. Kwanza naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake aliyoitoa iliyosheheni mambo mengi sana. Katika hotuba yake Mheshimiwa alizungumzia uchumi wa dunia umeendelea kuyumba kama alivyoainisha katika ukurasa wa 15 aya ya 20 mpaka aya ya 25 ukurasa wa 18. Hata hivyo Tanzania chini ya uongozi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua madhubuti kabisa na wote tunazijua zimefanya uchumi wetu usiendelee kuyumba. Ukuaji wa uchumi Duniani umeonesha umeshuka kutoka 6.2 asilimia mwaka 2021 mpaka 6.4 mwaka 2022. Lakini pamoja na kuteteleka kwa uchumi duniani, sisi Tanzania tumeweza kujiimarisha kutekeleza mambo ya msingi kwa ajili ya jamii yetu kama kutengeneza mazingira ya shule, infrastructure za shule, zahanati, vituo vya afya, miradi ya maji, barabara, miradi ya umeme na treni ya mwendokasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imeweza kutoa ruzuku katika maeneo ya makubwa ya mafuta na mbolea ili kuhimili mfumuko wa bei ambao tuliweza kufanikiwa kwani mwaka 2022 ilifikia wastani wa asilimia 4.3 kutoka kwenye asilimia 3.7 ya mfumuko wa bei kwa mwaka 2021. Kwa hiyo, hatua hizi zote zilizochukuliwa si kazi rahisi na watu wengine wanaweza kuwa hawayaoni haya au hawayafahamu, lakini wenzetu wa nje huko waliofanya tafiti kama hawa Numbeo Business Inside Africa imeripoti kuwa katika tafiti yao Tanzania kati ya nchi kumi Afrika ni nchi ya nane miongoni mwa nchi zenye gharama nafuu na ambayo imevutia wawekezaji kuja kuwekeza katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii si kazi ndogo, ni kazi ambayo Rais Samia ameifanya. Tunaposema anaupiga mwingi, ameifungua Tanzania ndio tunazungumzia mambo haya. Kwa hiyo, ili tuweze kuendelea kuimarisha uchumi wetu na kukuza uchumi wetu hatuna budi kuendelea kuhakikisha kwamba gharama za maisha tunaendelea kuzidhibiti, ndio kazi inayofanywa na Serikali yetu mpaka tumefikia hapo tulipofika. Wote tunafahamu wawekezaji wowote katika nchi zetu hizi wanakuja kuona nchi ambayo ina gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na taarifa mbalimbali pia za Business Insider inasema kwamba Tanzania is one of the first becoming the best investment destination in the world. Hii ndio ripoti ya wenzetu na hii ni kwa sababu ya hali inayofanywa na imejidhihirisha katika miradi iliyoandikishwa na TAC katika mwaka 2023 Februari, imeongezeka by hundred and twenty eight percent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha significant potential growth ya uchumi wetu nchini. Kwa hiyo, TIC imeorodhesha miradi hii gharama yake ni million dollars 339 sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni 780 na itaenda kuajiri watu 7,370. Kwa hiyo ni kazi kubwa sana hii ambayo inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi nyumbani Namtumbo. Kwanza tunaomba tuishukuru sana Serikali, katika kipindi hiki Serikali imeweza kutusaidia sisi zaidi ya shilingi 15,820,000,000 kutekeleza miradi mbalimbali. Katika afya tuliweza kupata shilingi 5,318,000,000 ambayo tumejenga majengo ya upasuaji katika hospitali ya Wilaya, wodi na tumejenga majengo ya Mama ngojea, katika kipindi hiki tumejenga mortuary na jengo la mama na mtoto zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano tulizozipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumejenga vituo vya afya katika Kata ya Magazini, Kata ya Ligela na miundombinu ya uboreshaji wa maji katika vituo vyetu vya afya. Vile vile tumeweza ukamilishaji wa zahanati na tumemaliza kuzijenga Ukiwayuyu, Misufini, Songambele, Naholo, Mhangazi, Luhangano na tunaendelea na zahanati zingine kama Namanguli, Nhamali, Ulamboni na Chengena katika kipindi hiki chote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki tumepata vifaa tiba vya thamani ya shilingi 758,848,000. Vilevile tumeweza kupata katika elimu, Serikali imetuletea shilingi 7,564,000,000 katika kuendeleza ujenzi. tumejenga shule ya sekondari ya wasichana kati ya shule kumi zilizojengwa nchini Tanzania, moja iko Namtumbo tumejenga kwa shilingi bilioni nne na shule hiyo iko mwishoni kukamilika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja kuitembelea na kuweka jiwe la msingi katika shule ambayo tumeiita Dr. Samia Suluhu Hassan Secondary School.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga pia Shule ya Sekondari katika Kata ya Mzizima, lakini vilevile tumejenga madarasa 86 yenye thamani ya zaidi ya shilingi 1,720,000,000. Vile vile tumeweza kujenga maabara katika shule zetu za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya maji; tumeweza kupata zaidi ya shilingi bilioni mbili na milioni mia tisa katika miradi mbalimbali ambayo tumeweza kukamilisha Mradi wa Maji Namtumbo Mjini, tumeweka line mpya na leo imepunguza adha waliyokuwa wanapata wananchi, walikuwa wanapata maji siku saba mara moja kwenye mgao, lakini leo angalau imepunguza adha hii. Kuna maji Litola-Kumbala tumeweza kufanikisha kupata maji lakini Luhimbalilo na Ikesi nayo kazi inaendelea. Vilevile maji Masugulu nayo shilingi milioni 578 kazi imekamilika na maji watu wanakunywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika barabara; tulipata zaidi ya shilingi bilioni mbili na milioni mia tano, tumeweza kujenga daraja kubwa Mto Luwegu. Mto Luwegu unatokea Namtumbo, kwa hiyo tumejenga pale daraja kubwa ambalo sasa hivi linawasaidia wananchi kuvuka. Vile vile tumejenga barabara za vijijini, fedha hizi tulizipata za TARURA ila tunaweza kuiomba Serikali tuna changamoto, tunaomba kwenye barabara, tuna barabara yetu ya Mtwara Pachani kupita Mkongo – Lusewa – Magazini mpaka Tunduru, hii barabara ni ya kiusalama, lakini vile vile ina eneo ambalo wanakaa watu wengi sana. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ifikirie kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi, ipo katika ukurasa wa 73, ahadi ya Ilani wa Uchaguzi wa 2020 - 2025. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ifanye ifanyavyo iweze kutekeleza ahadi yake ya kujenga kwa kiwango cha Lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru barabara ya kutoka Lumecha – Kitanda mpaka Malinyi iko katika hatua nzuri ambayo tuko katika hatua za manunuzi, tunaamini kabisa tutaweza kufanikiwa kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto tuliyonayo ni Kilimo. Kilimo tunashukuru sana mwaka 2022 tumepata mbolea za ruzuku, lakini mbolea hizi hazikufika katika maeneo ya vijiji vyetu. Tunaomba kama alivyosema leo Naibu Waziri asubuhi kwenye swali aliloliuliza Mama Anne Kilango, tunaomba utaratibu wa mwaka huu uende kama ulivyopangwa. Mbolea ziwafikie wakulima mapema. Tunashauri taratibu za manunuzi ya mbolea zianze mwezi huu Aprili ili mpaka mwezi wa Julai au Agosti mbolea ziwe zimeshafika nchini, ziwe zimesambazwa ili kama kuna changamoto tuweze kuzitatua changamoto hizo kabla ya wakati wa msimu kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba sana pia Serikali yetu isaidie, sisi tuna changamoto ya Kituo cha Mabasi katika Wilaya ya Namtumbo, tunaomba sana itufikirie. Hatuna kituo chenye hadhi ya Wilaya, vile vile hatuna soko. Sisi ni wakulima tuna mazao mengi lakini hatuna soko la mazao Namtumbo. Tunaomba Serikali itufikirie katika eneo hili. Hii ni changamoto mojawapo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna changamoto ya ukarabati wa Vituo vya Afya kongwe vitatu ambavyo vilijengwa miaka ya 1970; Mkongo, Lusewa na Mputa. Vituo hivi nasema ni kama zahanati, kwa hiyo vilijengwa miaka ile na vina upungufu wa majengo na vimechoka sana. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali iweze kutusaidia katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingiliano kati ya wakulima na wafugaji ni changamoto kubwa sana kwenye eneo letu. Sisi ni wakulima na nchi hii inategemea sana kilimo. Kwa hiyo tunaomba sana Serikali izingatie hili ije, haijawahi kuja toka nimeanza kuzungumza changamoto hizi hadi watu wamekufa hajawahi kuja Waziri wa Mifugo. Tunaomba Waziri wa Mifugo aje aone changamoto tuliyokuwa nayo. Mifugo inatusumbua sana sisi wakulima na sisi katika maeneo yetu nchini kuna maeneo sasa hivi yana uhaba wa mvua lakini kwetu sisi tuna mvua nzuri na sisi ndio ghala la chakula kule. Kwa hiyo, kukiwa na mwingiliano wa wakulima na wafugaji tutashindwa kulima na tutashindwa kuzalisha nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba kuishauri Serikali, ili kuendeleza uchumi wa nchi yetu na kuulinda lazima tu-focus zaidi kwenye export oriented industrialization ili tuweze ku-concetrate kuzalisha mazao tutakayokuwa tunauza nje ya nchi. Tukiwa na mazao na viwanda vinavyozalisha mazao ya kuuza nje ya nchi itatusaidia kuuza nje kwa sana na kutoa foreign exchange. Kutoa mifano ya nchi wenzetu walioendelea ambao tuliuwa nao katika miaka ya 1960 nchi za Asia pale Tiger ambao wao miaka ile walianza ku-concentrate kwenye hivi viwanda vya kuzalisha vitu vya kuuza nje, leo wanauza nje sana na uchumi wao wa Tiger kule umekuwa mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu huo ulikuwa ni huo. Naomba sana kukushukuru ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia mchango wangu. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuchaguliwa kuwa katika Wizara hii ya TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake, wanaofanya kazi vizuri. Sina wasiwasi na viongozi wetu hawa katika Ofisi hii ya Rais TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, moja ya majukumu yatokanayo na mgawanyiko wa majukumu yaani presidential instrument kwa Wizara hii ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni kuziwezesha Tawala za Mikoa kuendesha majukumu yake ya kisheria. Kwa kuwa moja ya majukumu hayo ya kisheria ya Serikali zetu za Mitaa yanatakiwa yaendeshwe kwa gharama zinazotolewa katika bajeti na Serikali.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Mkoa wetu wa Ruvuma Halmashauri zetu kwa ujumla wake nitatolea mfano mwaka 2019/2020 OC zilizoidhinishwa zilikuwa ni bilioni 20 milioni 255 lakini zilizopokelewa ni asilimia 47, bilioni tisa. OC ndiyo zinazofanya kazi ya kuendesha shughuli za Serikali za Mitaa Kisheria kwa maana ukiondoa mishahara, kwenda kuangalia shughuli za maendeleo, kusimamia n.k. sasa sisi mkoa wetu una square kilometers 67,372. Ukitoka kwa mfano mkoani kwenda mpaka Tunduru ni zaidi ya kilometa 260, kunahitajika magari ya kutosha, kunahitajika fedha za kwenda kugharamia mafuta n.k. ukifika Tunduru kwa mfano kwenda katika eneo la Kusini unatembea zaidi ya kilometa 100 na kidogo. Ukifika Namtumbo kwenda kufika katika Kata ya mwisho unatembea zaidi ya kilometa 200 na kidogo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, fedha za OC za miaka hiyo, 2019 zilikuja asilimia 47. Nasema haya kwa maana ya kwamba ukitazama katika mikoa mingine katika randama kuna wengine sekretarieti ya mkoa imepata zaidi ya asilimia 113. Kwa hiyo, ninachotaka kuiomba Serikali, wanaotoa fedha hizi, wanaofanya disbursement asilimia za ugawaji wa fedha uendane sawa na mikoa yote kuliko kufanya upendeleo mkoa fulani unapata asilimia 47, mkoa mwingine unapata zaidi ya asilimia 100. Kwa hiyo, naomba sana ili twende sambamba disbursement za fedha hizi zinatakiwa lazima zitoke sawasawa. Sitaki kutaja mkoa gani lakini tazameni kwenye randama mtaona tofauti zilizopo. Nimetolea mfano wa eneo langu la Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Spika, lakini fedha za maendeleo pia angalau tuliidhinishiwa bilioni 30 lakini tukapata bilioni 21 na milioni 600 sawa na asilimia 72. Lakini mpaka bajeti ya mwaka huu 2020/21 mpaka Februari, tumepata asilimia 31 za OC na development asilimia 26.9. Kwa hiyo, bado naamini kabisa sidhani kama tutafikia asilimia 100 mpaka tutakapofika Juni 2020.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kuomba kwanza Serikali ituongezee ukomo wa bajeti, ituongezee pia zile hela ambazo zinapitishwa kwenye bajeti basi tuzipate kwa asilimia 100 katika mikoa kama ya Kusini ambayo ina mipaka miwili ina kazi kubwa sana katika kuhakikisha kwamba wananchi wake wanasimamiwa na wanapata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Wilaya yetu ya Namtumbo ina kilometa za mraba 20,375 tuna watu 240,000 lakini jimbo hilo hilo lina jimbo moja na halmashauri moja lakini utakuta katika mkoa wetu nachukulia mfano, una halmashauri zingine zina square kilometer 6,000, watu ni wengi lakini kilometa za mraba ni ndogo ukilinganisha na eneo letu. Kwa hiyo, inakuwa ngumu sana katika wilaya na halmashauri yetu kusimamia au kwenda kuleta maendeleo ya wananchi kwasababu kilometa za mraba ni kubwa lakini fedha wanazozipata ni kidogo sana kulinganisha na shughuli zilizopo katika wilaya yetu. Lakini ukitazama malengo tunayowekewa na Serikali tunayatimizia kwa asilimia zaidi ya 100. Sisi tuliwekewa lengo la kukusanya bilioni 1.4, tulikusanya bilioni 1.6.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Kwanza kabisa naomba niwapongeze viongozi wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya katika nchi yetu ya kutengeneza barabara. Wizara hii toka tupate uhuru imefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Marehemu mama yangu aliniambia, hapo zamani wanatoka Songea walikuwa wanatembea kwa mguu wakati anakwenda kusoma Shule ya Sekondari ya Loleza, wanatembea kwa mguu kutoka Songea mpaka Njombe wiki nzima, ndiyo wanapata usafiri kwenda Mbeya kusoma Sekondari ya Loleza. Ukitazama katika miaka hii, kazi kubwa imefanyika. Kwa hiyo, hatuna budi kuwapa pongezi wataalam na viongozi wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika eneo ya barabara kuu zilizoingizwa katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 73, pamoja na barabara mbili za kimkakati Kitaifa zipo katika Mkoa wetu wa Ruvuma ambazo zipo katika Wilaya ya Namtumbo; Barabara kutoka Mtwara – Pachani - Ligela – Lusewa – Magazine - Lingusanguse hadi Narasi Wilaya ya Tunduru. Barabara ya pili ni kutoka Lumecha – Hanga – Mputa – Kitanda – Londo – Malinyi – Lupilo hadi Ifakara Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara katika barabara hii ya Mtwara – Pachani na Rasi – Tunduru ambayo ina wakazi wengi sana zaidi ya 140,000 na ina vijiji visivyopungua 39 na mitaa 10 iliyopo katika Tarafa ya Sasawala au Kata ya Lusewa. Eneo hili lina uzalishaji mkubwa sana wa mazao ya chakula na biashara na ndiyo njia ya kwenda mpakani Msumbiji pia. Kwa hiyo, strategically pia liko kiusalama ili ukihitaji kupeleka deployment kwa haraka katika maeneo ya mpakani katika eneo hilo barabara hii pia inahusika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, kwanza naishukuru Serikali, nimeona upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika. Nimeona katika hotuba ya Waziri ukurasa 41. Nawashukuru sana Serikali. Wisi wananchi wa Wilaya ya Namtumbo tunachoomba ni kufanyiwa ujenzi wa barabara hii haraka iwezekanavyo na tutashukuru sana ikianza kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara hii ya Lumecha – Londo – Malinyi – Lupilo – Ifakara Mkoani Morogoro nayo ni barabara ya kimkakati Kitaifa. Inafungua maeneo ya fursa zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro katika maeneo ya kilimo, utalii na usafiri. Barabara hii ukipitia njia ya kutoka Ruvuma kwenda Dar es Salaam kupitia Njombe mpaka Makambako na barabara hii ikikamilika inapunguza zaidi ya kilometa 350. Kwa hiyo, itaifungua na kupunguza gharama ya mafuta kwa maana ya kilometers lakini itasaidia sana kwenye maeneo ya kiutalii na pia itafungua pia mazao mbalimbali kusafirishwa na kulima katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mimi nilipata kuwa Mwenyekiti mwenza wa uratibu wa ujenzi wa ufunguzi wa barabara hii, wakati huo tunakata pori barabara hii na kujenga madaraja. Mwenyekiti mwenza mwenzangu alikuwa Mheshimiwa mzee wetu Dkt. Ngasongwa ambaye yeye alikuwa Mbunge wa Malinyi kipindi cha 2005 – 2010. Kwa hiyo, tulikuwa na Kamati ya uratibu wa barabara hii ambayo ilikuwa na Wajumbe Wakuu wa wilaya zote mbili; Ulanga na Namtumbo. Kulikuwa na Mameneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma na Morogoro, pia kulikuwa na ma-DED wa Halmashauri zinazopita barabara hii na Mkuu wa iliyokuwa Selous kwa sababu barabara hii inapita katikati ya Selous. Sasa tulikuwa tunakata miti ya Selous.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ile ilishauri na ilisimamia vizuri ujenzi wa madaraja kwa ukamilifu; Daraja la Mto Londo, Mto Mwatisi na Mto Fuluwa. Yalijengwa kwa ukamilifu na tumeifungua ile barabara, lakini Kamati ilishauri wakati ule na nilisahau Mjumbe mmoja alikuwa anatoka katika Wizara ya Ujenzi, Eng. Kilowoko. Kamati ya Uratibu wa Ufunguzi wa Barabara hii ilishauri pamoja na ufunguzi wa barabara hii, lakini TANROADS mikoa, Mameneja wa Mikoa wawe wanatenga fedha kwa ajili ya kuweka lami nyepesi katika maeneo korofi na ya miinuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, tulifanya hivyo katika eneo la Namtumbo. Tumekuwa tukiweka nusu kilometa au robo kilometa kwenye maeneo ya miinuko, yale korofi na maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki kabisa. Imesaidia sana na katika kipindi hiki naweza kutoa ushuhuda hapo nyuma katika eneo linaloitwa Kata ya Hanga kwenda mpaka Kata ya Kitanga kupitia Mputa na Naikesi, wakati wa mvua barabara ilikuwa haipitiki kabisa, lakini baada ya kufanya utaratibu huo wa kuweka lami nyepesi katika vipande vidogo tu korofi imekuwa inapitia miaka yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, unaweza ukakuta barabara ya kilometa 120 lakini sehemu korofi haziwezi kuzidi vipande vipande vya kilometa 20. Kwa hiyo, tunaweza tukaanza kutenga fedha za kuweza lami nyepesi sehemu za miinuko nusu kilometa, sehemu hii labda kilometa moja, utakuta kwamba tunaondoa kabisa malalamiko ya wananchi, lakini pia barabara hizo zinapotika throughout the year wakati Serikali inajipanga kutengeneza barabara hizo kwa kiwango kamili cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo ushauri wangu kwamba Serikali iwe inatenga sehemu kidogo kidogo ya kuweka lami nyepesi ili barabara ziweze kupitika moja kwa moja. Kama hii tuliyoifanya sisi ya kutoka Lumecha – Hanga – Mputa – Kitanda mpaka Londo kutokea Norogoro. CCM hoyee! Ah! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi kwenye barabara ya Mtwara – Pachani…

NAIBU SPIKA: Jamani, mwacheni Mheshimiwa Vita Kawawa anawaza Uchaguzi wa Kigoma. (Kicheko)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye barabara yetu hii ya Mtwara – Pachani ambayo inapita Ligela, inapita Lusewa - Magazine – Lingusanguse na mpaka Nalasi tuna mto unaoitwa Sasawala na katika kipindi hiki cha mvua mto huo daraja lake kubwa limekuwa washed away na mvua hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru TANROADS Mkoa wameenda kutuwekea kivuko tu kidogo cha kuweza watu kupita. Tunashukuru kazi ile wameifanya, lakini tunaiomba Serikali itutengee fedha ili kulikarabati lile daraja. Ndiyo daraja kubwa ambalo tunalitegemea katika Wilaya yetu ya Namtumbo na Tunduru. Naomba nikushukuru na naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara yetu hii ya Kilimo. Nawapongeza Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na watalaam wote wa kilimo wa Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nijielekeze katika malengo ya kimkakati ya Wizara ya Kilimo ambayo yapo tisa. Moja ya lengo la Wizara ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, masoko na miundombinu ya uhifadhi wa mazao. Naomba nianze kuzungumzia hili la ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, miradi ya umwagiliaji iliyofanyika ilikuwa ni kukusudia kuongeza uzalishaji kwa wananchi na kwa Taifa zima, lakini ilikuwa haijafanyika tathmini ya miradi hiyo ipoje kwa sasa na je, miradi hiyo ilikamilika? Je, iliyokamilika ina-perform vipi? Uzalishaji wake ukoje? Naona hii tathimini ilikuwa haijafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapopeleka fedha za maendeleo katika maeneo kama haya ya kilimo kwenye umwagiliaji tunaenda kujenga fixed asset na fixed asset yoyote lazima tupime wakati inajengwa na inapokamilika, utekelezaji wake baada ya kukamilika, je, kile tulichotarajia kinaleta tija au la?

Mheshimiwa Spika, leo tunawashukuru Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetuletea dodoso, Wabunge wote tumesambaziwa humu ndani, lakini dodoso hili tulilosambaziwa katika ukurasa wa pili, paragraph ya mwisho, mstari wa tatu kutoka mwanzo, paragraph ya mwisho, inasema:

“Aidha, Tume imeambatanisha orodha ya skimu za umwagiliaji zilizopo katika jimbo lako kutoka katika kanzidata kwa ajili ya rejea yako.”

Mheshimiwa Spika, ukimuuliza Mbunge yoyote humu hakuna list hiyo ya kanzidata humu. Sasa sisi tutajuaje hiyo miradi iliyopo katika kanzidata ambazo wamesema humu. Sasa hata tukijaza humu, tunajaza ile tunayoifahamu, kama mimi nimejaza ile ambayo haifanyi kazi na fedha nyingi zimeingia. Tuna Mradi wa Liyuni umeingia zaidi ya bilioni moja, lakini mradi haujakamilika mpaka leo. Nimekaa katika Ubunge miaka kumi, nikaenda likizo bila malipo miaka mitano ya ubunge, lakini ule mradi nimeukuta vilevile, haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Mradi wa Likonde, nao umeingia zaidi ya milioni 900, haujakamilika. Kuna Miradi ya Mwangaza, Mbecha na Mahoka, miradi hii haijakamilika, maana yake ilikuwa haijafanyika tathmini miradi ile imekamilika na inafanyaje, ina-perform au hai-perform. Kwa hiyo naomba sana tunapoelekeza fedha hizi lazima kweli tuwe tunaenda kufanya tathmini na ufuatiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nawashukuru sana Tume leo wametuletea, lakini tunaomba, naomba na mwongozo wako kwamba tupatiwe hiyo list ya miradi ya kanzidata za Serikali walizonazo ili tuweze ku-compare na tuone hiyo ni miradi ipi iliyokuwepo kule na sisi tuliyonayo ni ipi ambayo fedha nyingi za Serikali zimeingia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kuna jambo lingine sisi kwetu kule Namtumbo tuna kituo…

T A A R I F A

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, endelea.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu msemaji kwamba kiambatanisho hicho kipo katika hiyo bajeti iliyopo sasa hivi kipo, kinaonekana. Ahsante.

SPIKA: Ukurasa wa ngapi?

MBUNGE FULANI: Kipo Ukurasa wa ngapi?

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELE: Mheshimiwa Spika, kipo separate yaani kimekuwa kiko peke yake.

MBUNGE FULANI: Wapi?

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELE: Kwenye sehemu ya bajeti, kwenye kishikwambi pale..

SPIKA: Wanasema kwenye kishikwambi, hiyo orodha inapatikana.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELE: Ndiyo kwenye kishikwambi pale, zipo attachment tatu.

SPIKA: Ahsante sana. Endelea Mheshimiwa Vita.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa taarifa, nitaangalia kwenye kwishikwambi kwa sababu hotuba tumewekewa leo, ila humu hamna. Hili dodoso hili hatuwezi kulifanya leo tukalimaliza leo, kwa sababu kuna ekari humu zinatakiwa tuandike kuna ekari ngapi, maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, kijiji, kata na ekari za maeneo hayo. Kwa hiyo, lazima tupeleke kwa wataalam wetu wa kilimo katika halmashauri zetu, kwa hiyo lazima watupe muda na hili pia na hiyo tutaangalia kwenye vishikwambi vyetu hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea. Sisi kule Namtumbo tuna Kituo kilichokuwa kinaitwa Shirika la Kilimo Uyole, Suluti au SKU Suluti, Namtumbo. Kituo hicho kilikuwa ni kwa ajili ya uzalishaji na utafiti wa mbegu ambazo zinafaa kwa ajili ya mazingira ya Nyanda za Juu Kusini na hususani Mkoa wa Ruvuma. Kilifanya kazi yake vizuri sana kituo kile, kilikuwa kinazalisha na mbegu za mahindi na mazao mengine mchanganyiko, lakini kituo kile kimekufa. Toka nilipopumzika Ubunge miaka mitano na nimerudi sasa hivi kimekufa kabisa. Majengo yake ni magofu, sisi kwetu kule tunaita mang’oa au mang’oani. Mang’oani ni mahali ambapo waliishi mababu zetu halafu wakahamishwa kwenda kwenye vijiji au kwa jina lingine mahameni.

Mheshimiwa Spika, ukitaka kupajua hapa waliishi watu utakuta miembe mikubwa na yale magofu, mahameni. Sasa hicho kituo ni kama mahame tu, kule kwetu tunaita ling’oa na ni kituo cha Serikali kilichofanya kazi vizuri sana mpaka Mkoa wa Ruvuma ukawa unaonekana ni moja ya big five katika nchi hii kwa kuzalisha mazao ya mahindi, lakini kituo kile kimekufa…(Makofi)

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa, toa taarifa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Nataka nimpe taarifa Mbunge anayezungumza sasa kwamba na ni suala la mang’oa ni eneo ambalo walikuwa wanaishi watu na watu wale wameshaondoka, inakuwa kama ni eneo ambao ni zama zamadamu, zile kumbukumbu za kale ndivyo ilivyo, ndiyo tafsiri yake. Ahsante sana.

SPIKA: Wote mnaongea lugha moja wote.

MHE. VITA S. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, Ndiyo, tunaongea lugha moja na nashukuru.

SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Vita. Wote Wangoni hawa. (Kicheko)

MHE. VITA S. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, sasa kile kituo kimekuwa kama kumbukumbu tu ya watu wa kale na wakati kilikuwa kinatusaidia na kipo pale na ni ardhi ambayo imehodhiwa na Serikali, lakini ipo ndani ya Mji wa Namtumbo, Kijiji cha Suluti. Tunaiomba Serikali ituambie inapokuja kujibu, kituo kile watakifufua au waturudishie Suluti tuendelee kuifanyia shughuli zingine za kilimo au pale tujenge shule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, tuna shamba kubwa lililokuwa linaitwa NAFCO, nalo vilevile limekufa miaka mingi kabisa na hakuna chochote kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru wamenikatiza, lakini naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, na mimi nashukuru kwa kunipa fursa hii niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara yetu hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kufanya teuzi nzuri za mabalozi hawa wawili, Mheshimiwa Liberata Mulamula kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk kuwa Naibu wake.

Mheshimiwa Spika, mimi naimani sana na mabalozi hawa, kubwa, kwani nawafahamu. Na ninamfahamu Mama Mulamula kuwa yeye ni mbobezi katika eneo hili la diplomasia. Na kwa muda mfupi tu ametuonesha kwa ku-stimulate diplomasia ya uchumi kati yetu na nchi zetu za Afrika Mashariki kwa kumshauri vyema Mheshimiwa Rais na kutembelea nchi hizi na kufanya mikutano ya kibiashara na hasa Kenya na kufanya kufungua biashara ya mazao baina ya nchi yetu ya Tanzania na Kenya.

Mheshimiwa Spika, mimi napenda kuishauri Serikali tuendeleze na kukazania sana diplomasia hii ya uchumi kwani wote tunafahamu nchi ikiwa na mahusiano mema ya kiuchumi naamini kabisa tutaweza kuuza biashara na bidhaa zetu nje kwa wingi na tukiuza nje kwa wingi tutapata fedha za kigeni, lakini pia tuta-stabilize uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hivyo nilikuwa napenda sana kuishauri Wizara ya Fedha iangalie diplomasia ya uchumi nayo ina gharama yake, mahusiano yana gharama yake kwa hiyo, tuangalie sana kupeleka fedha kwa wakati; kama ni OC tusipeleke OC za mishahara tu, tupeleke OC pia za kugharamia mahusiano haya ya diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwani tunaweza tukalaumu wakati mwingine tunaweza tukafika mahali tukalaumu ma-diplomat wetu waliokuwepo nje kwamba, wanachelewa kutekeleza majukumu yao ya diplomasia ya uchumi, sababu tu wanaweza wakawa wanakosa hata gharama ya kugharamia ile round coffee table ya kuweza kuwaita na kuwashawishi potential investors kwa kukaa nao na kunywa nao kahawa na kuwaelezea hali halisi ya kwetu na kushawishi waweze kufika huku. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara ya Fedha kutenga na kusambaza fedha zile zinazotakiwa kwa ajili ya mabalozi wetu nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine napenda sana kuishukuru Wizara kwa kutekeleza ushauri wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya kuona kuna umuhimu wa kuongeza watumishi katika balozi zetu hasa wanaohusiana na wenye utaalam wa kufanya kazi hii ya diplomasia ya uchumi. Tunawapongeza sana kwanza wameshatekeleza jukumu hilo na sasa wako katika uratibu nadhani wa kupeleka hawa ma-diplomat wetu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia naipongeza Wizara kwa kutambua na kushirikiana nao mabalozi wetu wastaafu, tumewaona leo wamekuja hapa. Mabalozi wastaafu hawa ni encyclopedia ya Wizara hii ya Mambo ya Nje na Waziri umedhihirisha mahusiano mema ya diplomasia kuwakumbuka na kuwatambua mabalozi hawa na leo kuwaleta hapa na kushirikiana nao. Mabalozi hawa ndio walifanya kazi kubwa sana katika nchi hii kipindi cha nyuma wakati wakiwa kazini kwa hiyo, ni vema wana uzoefu mkubwa sana. Wizara iendelee kuwatumia mabalozi hawa ili kutoa ushauri wao na experience yao katika Wizara hii na mahusiano ya kimataifa, lakini pia katika dilpomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa na hayo tu machache, naomba nikushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nichangie katika Wizara yetu hii ya Fedha. Niungane na wenzangu kumpongeza Dkt. Mwigulu kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, yeye ni Mchumi mbobevu katika eneo hili, naamini Wizara hii ataitendea haki.

Nampongeza pia Engineer Masauni kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri. Wizara hii ndio Wizara yenye hazina ya nchi yetu na ndio inayofanya disbursement ya fedha katika Wizara zote na Mafungu yote katika sekta mbalimbali, baada ya kupitishwa na sisi Wabunge katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu kuishauri Wizara na Mawaziri, wajitahidi sana kugawa kwa uwiano fedha ambazo zimetengwa katika Wizara zetu. Wagawe kwa uwiano na kwa wakati ili kuweza kusukuma maendeleo ya nchi yetu yaweze kuendelea zaidi na zaidi.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii katika bajeti inayoishia sasa hivi mpaka mwezi Aprili yenyewe, Wizara, imeshajigawia asilimia 68.5. Kwa hiyo, naomba kuwaomba kama Wizara iangalie pia, ifanye tathmini Wizara zingine imezigawia nazo mpaka sasa Aprili, asilimia 68.5? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa mpaka mwisho wa mwaka wa bajeti, mwisho wa mwezi huu, Wizara hii itakuwa imeshajigawia asilimia 100 ya matumizi ya Wizara. Kwa hiyo, naomba sana nayo iangalie Wizara zingine nazo pia zipate hivyo hivyo, Mafungu hayo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nizungumzie kuhusu eneo la majukumu ya CAG. CAG kama controller General kazi yake ya kwanza ni kudhibiti mapato ya Serikali, matumizi ya Serikali na mali za Serikali. Kazi yake ya pili ni Auditor General ambayo ni kufanya ukaguzi wa masuala yote niliyoainisha hapo mbele. Kwanza, kuhakikisha kwamba mapato yote ya Serikali yanakusanywa na kuhifadhiwa kwa wakati kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizowekwa. La pili, matumizi ya Serikali yanafanywa kulingana na bajeti kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha. La tatu, mali za Serikali zinatunzwa kwa umakini mkubwa na kwa manufaa ya Watanzania tuliopo sasa hivi na kizazi kijacho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, CAG anapokwenda kwenye Taasisi au Wizara anakuwa kama External Auditor, lakini ndani ya Taasisi, Wizara au Halmashauri tuna wale Internal Auditors. Hawa wanakuwa accountable kwa Afisa Masuuli au returning officer wa taasisi husika. Sasa External Auditor kama CAG anapokwenda pale, anategemea sana taarifa za Internal Auditor. Hata hivyo, Internal Auditor kama kuna upungufu kwenye taasisi naye, yuko answerable kwenye Management ya Taasisi, kama atakubaliana na upungufu ule na taasisi au Afisa Masuuli, basi taarifa anazoweza kupata CAG zinaweza zikam-lead tofauti. Ndiyo matokeo haya tunayoyakuta baadaye kwamba kuna ubadhirifu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye hili, naiomba Serikali, eneo hili la Internal Auditor kama inawezekana wawe accountable moja kwa moja kwa Internal Auditor General Hazina ili kuweza kufanya kazi yao ipasavyo. Kwa sababu wengine unaweza ukakuta kwa mfano, bandari miaka ya nyuma, Internal Auditor pale waliweza kumhamisha, kwa sababu hakutaka kuendana nao wanavyotaka, wakampeleka Musoma huko wakati yeye alikuwa ni Internal Auditor wa Bandari, lakini ni kwa sababu hawakuwelewana tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri Internal Auditor angekuwa Accountable kwa Internal Auditor General kule ili taarifa zake zote awe anazipeleka kule. Pia CAG awe anazipata kule anapokwenda anaanza nazo taarifa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na utatuzi wa changamoto zinazojitokeza na kutoa ushauri kwa CAG, lakini fedha zimekuwa zikiibiwa kupotea ama kutumiwa vibaya bila kunufaisha Taifa na wananchi wake kwa ujumla. Taarifa za Mkaguzi Mkuu wa Serikali zenye Hati zenye mashaka ni dhahidi kuwa zinahitaji zaidi ukaguzi wa kina au kuzipeleka katika vyombo husika kufanyiwa uchunguzi zaidi. Hata hivyo, sheria inamtaka CAG atoe ushauri.

Mheshimiwa Spika, ningependa CAG kama anakabidhiwa Sheria ya kupeleka moja kwa moja TAKUKURU, ingekuwa bora zaidi. Kwani kutoa tu taarifa ya Hati zenye mashaka peke yake, hakuna tija. Naomba kama Sheria iliyoiunda Ofisi ya CAG bado ina upungufu au inahitaji mapitio, basi ingeletwa hapa Bungeni, tuyafanyie mapitio hayo ya kuwapa nguvu zaidi Ofisi ya CAG ya uchunguzi zaidi na kushirikiana na vyombo vingine ili kuwezesha Serikali yetu kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la Msajili wa Hazina, naomba nizungumzie kidogo mwishoni. Sisi kule Namtumbo kuna shamba lililokuwa la NAFCO na shamba hilo sasa hivi liko chini ya Msajili wa Hazina. Watu wakitaka kulima, lazima walipie Hazina, naamini ni kama shilingi 10,000/= hivi kwa eka. Kama Halmashauri tulishaiomba siku nyingi; liko ndani katikati au kwenye ramani ya Mji wa Namtumbo. Kwa hiyo, tunaomba sana, tufahamu hatima ya shamba lile ni nini; ili tuelewe mtaturudishia kama Halmashauri, na tungeomba hivyo au mtamweka mwekezaji kulima kama ilivyokuwa NAFCO zamani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba hilo, kwa sababu lipo shamba katikati ya ramani ya Mji wa Namtumbo. Tunaomba sana ama turudishiwe au mwone jinsi gani tunajua hatima yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Narudia kumpongeza sana Waziri wetu wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri Engineer Masauni. Naomba pia nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ndugu yangu Mheshimiwa Daniel Sillo, lakini na Makamu Mwenyekiti CPA Mheshimiwa Omari Kigua kwa kutuwakilisha vyema kama Bunge kwenye Kamati ya Bajeti na hasa katika vikao vya mwisho vya majumuisho ya bajeti hii. Tunawashukuru sana Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono bajeti hii na mapendekezo yake yote. Naiunga mkono bajeti hii kwa sababu inakwenda kuendelea na kukamilisha miradi ya maendeleo au miradi mkakati ambayo inafanyika sasa hivi Stigler’s Gorge, SGR na mingine mikubwa. Bajeti hii inaenda kuendeleza na kukamilisha miradi hiyo, lakini inaenda pia kuanzisha miradi mipya ambayo tumeainishiwa katika bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bajeti hii inaelekea kwenda ku-trickle down economic na ku-stimulate economic activities zilizopo kwa wananchi wake. Kwa nini nasema hayo bajeti hii pia leo tumeambiwa inakwenda kupandisha madaraja ya wafanyakazi. Naomba niseme hapa mpaka leo hii wafanyakazi karibu zaidi ya 86 wameshapandishwa madaraja na automatic wanaenda kupandisha mishahara yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ya upandishaji wa mishahara hii itaigharimu Serikali bilioni 300, lakini pia malimbikizo ya madeni ya wafanyakazi karibu bilioni 96 yanaenda kulipwa. Kwa hiyo ndiyo maana naipongeza Serikali na wafanyakazi maslahi yao yakitazamwa na yakipanda maana yake ni nini? Hawa ndiyo spender wakubwa na hawa waki-spend ndiyo Serikali inakusanya kodi yake. Hizi kodi zote tunazozisema hapa za simu sijui za nini tulizozipendekeza watumiaji wakubwa wakiwemo pia wafanyakazi, ndiyo wanafanya miamala mikubwa, ndiyo wanaotumia hela nyingi kupeleka sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake wanayoiongoza. Tangu Mheshimiwa Rais ameapishwa Samia Suluhu Hassan katika wilaya yetu ya Namtumbo katika kipindi hiki toka Aprili mpaka sasa hivi ametuletea bilioni mbili na milioni mia saba sabini na saba na milioni thelathini katika miradi ya elimu, afya, program endelevu ya maji safi na mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametuletea pia milioni 500 za barabara kwa ajili ya TARURA, lakini pia tunategemea kupata milioni 600 kwa ajili ya sekondari zetu za kata, naomba sana nimpongeze Rais wetu na Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye aya ya 110 katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, alizungumzia eneo la utamaduni wa kuheshimu mali na rasilimali hapa nchini; mali za Umma na binafsi. Naomba nimnukuu: “kwa upande wa Mali za Umma lazima tutangulize uzalendo na uadilifu tunapotekeleza majukumu yetu. Serikali inapoteza fedha nyingi kwenye kutekeleza Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kutojali thamani ya fedha kwa miradi. Watumishi wa Serikali wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kuongeza gharama za miradi ikilinganishwa na gharama halisi ingawa wanafuata taratibu zote za manunuzi. Taratibu za manunuzi zinapokamilika, watumishi na wafanyabishara hawa hugawana fedha na kiasi kidogo tu kilichosalia ndicho kinaelekezwa kwenye miradi husika na hatimaye miradi hiyo kuwa chini ya kiwango.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno alisema Waziri wa Fedha katika hotuba yake. Ni kweli, nakubaliana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuliona hili. Kuna haja ya kukazia eneo hili, kuheshimu kutunza Rasilimali za Umma, kwani ni kweli Serikali inapoteza fedha nyingi kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa, tumepata zaidi ya shilingi 2,700,000,000 zinakwenda katika Halmashauri zetu. Miradi hii inaongozwa na bajeti au inaongozwa na mwongozo wa kuhudumia miradi hiyo kwa Force Account. Mwongozo unasema, kuna Kamati ya Ujenzi, Kamati ya Manunuzi, Kamati ya Mapokezi na Kamati ya Ufuatiliaji. Kamati hizi ni za wale wananchi husika pale, lakini watumishi wa Halmashauri wanakuwa Wajumbe kama washauri na kusimamia ili shughuli iende sawa sawa kwa mujibu wa taratibu na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo inajitokeza baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu, wao sasa ndio wanachukua majukumu yale ya kufanya ununuzi na kufanya ujenzi. Sasa hii inasumbua sana na inaleta audit query kwenye Halmashauri zetu. Leo hii sisi tuna audit query pale zaidi ya milioni 120 kwa ajili ya mradi tu ambao haukufuata taratibu hizi. Kwa hiyo, naishauri Serikali, tunaomba mumpe nguvu Mkuu wa Mkoa wawe wanasimamia miradi hii ya maendeleo. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa isimamie kama taratibu zinafuatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni aya ya 75; Serikali katika eneo la kilimo, imependekeza katika miradi ya umwagiliaji kwamba itakuwa inatoza 5% ya mavuno katika miradi ile ya umwagiliaji. Nia ni njema, naiunga mkono kwa ajili ya kuendeleza kufanya service miradi yetu ya umwagiliaji. Hata hivyo, nina mapendekezo mawili. Kwanza, kuangalia hii miradi yote. Kuna miradi ambayo fedha nyingi za umwagiliaji zimeingia kule, lakini haijakamilika miaka nenda, miaka rudi. Naamini katika kanzidata ya Serikali inaonesha kwamba kuna fedha zimepelekwa katika miradi lakini miradi ile haikukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri hapa, kwamba kwa wale wasiokuwa waaminifu, hawakukamilisha miradi, sasa tozo hii lazima yatoke maelekezo kwamba kwanza tukakamilishe ile miradi ndipo tozo zianze kuchukuliwa. Maana yake tukitoa tu tozo, miradi isipokamilika na ile ambayo hai-perform vizuri, tozo zitaanza kuchukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima ifanyike tathmini ya miradi ambayo haijakamilika ili tuikamilishe ndiyo tozo hizi ziweze kuwapa wale wakulima wananchi kule, kuliko kupeleka tozo, wataenda kukamatwa hawajalipa tozo, wakachukuliwa tozo zao, miradi ile haikukamilika. Pili, tozo hizi tuelekeze wazi wazi zinakwenda wapi? Kama zinakwenda kwenye Tume ya Umwagiliaji, tujue; zisije kuwa tozo hizi zinakwenda kuchukuliwa tu kwenye Halmalshauri halafu zinaanza kupangiwa matumizi mengine baada ya matumizi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nami niungane na wenzangu, kwanza kabisa kwenye hili suala la Madiwani, Watendaji na Makatibu Tarafa kupewa na Serikali fedha zao na posho, naunga mkono kabisa. Naipongeza sana Serikali kwa kuamua kufanya jambo hili jema sana kwa ajili ya watumishi hawa. Ushauri wangu ni kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. VITA R. KAWAWA K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Spika, kwanza nami naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuja kuifunga hoja yetu hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi, Usalama. Katika eneo letu walichangia watu watatu na mmoja ni Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa sababu mijadala hii inaonekana eneo kubwa limechangiwa sana na Kamati ya Maliasili na Utalii. Kwa hiyo, waliochangia kwenye Kamati yangu ni Mheshimiwa Chumi, Mheshimiwa Christopher Ole- Sendeka na Mheshimiwa Mkenge.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Chumi alizungumzia sana ongezeko la biashara (balance of trade) katika Kanda zetu za Afrika Mashariki na Jumuiya ya SADC. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwanza kwa kuifungua nchi yetu. Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia alipoapishwa alifanya ziara katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za SADC. Hii imesaidia sana katika biashara yetu na tumeelezwa katika Kamati kwamba Itifaki ya Biashara ya mwaka 1996, nchi wanachama wa SADC zinatekeleza na zinaondoa vikwazo ambavyo vinasababisha biashara isifanyike vizuri.

Mheshiwa Spika, kwa hiyo, hii imesaidia baada ya Mheshimiwa Rais kwenda kuzungumza, sasa urari wa biashara umeongezeka kwa asilimia kubwa. Kwa mfano, nchi yetu katika kipindi hiki tumeweza kuuza na kupandisha biashara katika kipindi cha mwaka 2021 kutoka dola 1,235,000 mpaka dola 1,458,000 katika ukanda wa SADC. Takwimu zinaonesha kwamba balance of trade kwa mfano kati yetu na South Africa, sisi tunauza zaidi South Africa kuliko wao wanavyonunua kwetu sisi. Hii imetokana na juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais na Wizara ya Mambo ya Nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Chumi alizungumzia kidogo kuhusu Kamati ya Mawaziri Nane ambao walienda kutaka kutatua migogoro vijijini. Mwaka 2021 Kamati ililetewa tatizo lililokuwa limejitokeza Mbarali; kuna vijiji ambavyo vilikuwa vinaingiliana na eneo la maliasili na kulikuwa na mauaji ya watu watatu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kulishughulikia suala lile, tulilopewa na Spika tuliwaita pia Mawaziri wa Kisekta ambao mmojawapo walikuwa hawa wanane na tulishauriana nao tukawaambia waende wakakamilishe lile zoezi walilolifanya la kuzunguka nchi nzima na waliifanya kazi hiyo, wamezunguka na wakatoa kauli. Sasa Kamati inaishauri Serikali imalizie ile kazi nzuri waliyoifanya ya kuwapa vijiji vile maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, mwisho Mheshimiwa Mkenge naye alizungumzia mambo ya NIDA, pia amepongeza sana; amezungumzia mtangamano wa Jumuiya ambao nimeshauelezea. Vile vile amezungumzia kuhusu MSD kuteuliwa kuwa supplier wa dawa katika nchi za Kikanda za SADC. Sisi tunaipongeza sana juhudi ambazo zimefanywa na Wizara ya Mambo ya Nje kushawishi mpaka nchi yetu kuteuliwa kuwa eneo ambalo litakuwa supplier mkubwa wa dawa katika nchi za SADC. Kwa hiyo, hili tunaliunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaipongeza Nyumbu kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kamati inaishauri Serikali kwamba iendelee kuipa Nyumbu fedha za kutosha kuweza kufanya kazi yake nzuri kwa sababu sasa hivi inatengeneza magari ya fire ambapo tuna uhaba sana wa magari ya fire. Kwa hiyo, tunapenda sana iwe inapewa fedha za kuweza kufanya kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Spika, mwisho Mheshimiwa Chumi alizungumzia pia kuhusu Maafisa wa juu wa Magereza, ni kweli ili kuleta mageuzi katika Jeshi letu la Magereza, Kamati inashauri Serikali kuziba nafasi zile za Maafisa wa Juu kulingana na Muundo wa Jeshi la Magereza.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naliomba Bunge lako Tukufu kuunga mkono hoja Kamati yetu ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kutoa mchango wangu katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha vyema Hotuba yake lakini pia, nawapongeza Mawaziri wote walio katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge na Waziri wa Nchi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, nawapongeza sana. Nchi yetu imekuwa ikifanya vizuri katika hatua za maendeleo pamoja na changamoto zinazotukabili za ndani ya nchi na nje ya nchi. Lakini bajeti hii iliyowasilishwa leo naamini itatuvusha na kutufikisha mahali pazuri. Kuna maeneo ya huduma za jamii tumepiga hatua nzuri, lakini napenda kutoa ushauri pia kuna maeneo tunahitaji kuongeza juhudi za kutosha, ili kuweza kusaidia mahitaji ya kufanikisha kwa ufanisi maendeleo ya huduma za jamii kwa wananchi wetu kama tulivyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dunia imebadilika inakabiliana sasa hivi na changamoto kubwa ambazo na sisi zinatuathiri kiuchumi na kijamii. Hivyo, sisi kama nchi hatuna budi na sisi kukaza mkanda ili tuendelee kuwaendeleza wananchi wetu kiuchumi na kijamii. Katika kipindi hiki cha Serikali ya CCM Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tumeona Serikali ikifanya mambo makubwa ya kuendeleza hasa miradi ile mkakati iliyoanzishwa, lakini kuanzisha miradi mipya ya huduma za jamii. Shule zimeejengwa, vituo vya afya vimejengwa, hospitali za wilaya na mikoa zimejengwa na zinaendelea kujengwa. Miradi ya maji inaendelea kujengwa na kazi zingine zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii pia pamoja na miradi hiyo inayojengwa inahitaji watu wa kwenda kuifanya kazi. Kwa hiyo, naomba niishukuru Serikali kwa kauli yake leo iliyotoa hapa Bungeni kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama ya kuwa Serikali inategemea kutangaza ajira 32,000. Hii ni taarifa njema ni taarifa muhimu na yenye afya, kwani katika maeneo ya afya na elimu sasa hivi tunahitaji sana watumishi. Kama nilivyoeleza hapo awali tumejenga majengo ya afya, vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya tunahitaji watu wa kwenda kutoa huduma na hili likikamilika dhamira ya Serikali ya kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo haya ya elimu na afya itakuwa imetimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya afya ina unyeti wake inahitaji pia kufanyika uchambuzi wa kina ili kuangalia madaktari na madaktari bingwa, manesi na manesi bingwa wa maeneo yote, tunahitaji wangapi katika hospitali zetu na kwa sasa tunao wangapi? Ili kukidhi mahitaji hayo inatubidi tuchukue muda gani kuwapata hao wapya. Tukishajua hilo, tutaweza kupanga mkakati mahususi kabisa kwa ajili ya kuwatafuta na kuwapata hawa wataalam wetu. Wiki iliyopita nilisoma kwenye gazeti la Uhuru Mheshimiwa Waziri wa Afya alikuwa anaeleza kwamba tuna wataalam wa ubongo na wa mishipa ya fahamu 16 tu, lakini kwa population tuliyonayo sisi nchini takribani milioni 60 tunahitaji wataalam hao wawe kama 600. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna upungufu wa wataalam bingwa huo ni mfano tu. Kwa hiyo, hatuna budi tuweke mkakati mahususi wa kuona tunapataje wataalam bingwa kwa ajili ya kwenda kuhudumia wananchi wetu. Leo tumenunua vifaa vya kwenda katika hospitali za mikoa, hospitali za wilaya, tunahitaji watumishi ambao wataweza kuhudumia katika vifaa tiba hivyo. Pamoja na ajira mpya Serikali imetangaza leo, naomba iangalie pia na replacement za ajira za watu wanaokufa, wanaostaafu, wanaoacha kazi wenyewe, wanaofukuzwa kazi na replacement haiathiri wage bill. Kwa hiyo, Serikali iendelee kuangalia tunafanya replacement na eneo hili ndio tunalolipoteza sana la wataalam bingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali iangalie sana. Jana Profesa hapa wakati anauliza swali alitoa na pendekezo kwamba, wale wataalam/Madaktari Bingwa tuwaongezee muda na tuna pengo kubwa la wataalam bingwa kama nilivyoeleza awali. Kwa sababu, pia tulisahau hii replacement. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali iangalie kundi hili pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la uzalishaji. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali hatuna budi kuedelea kuliangalia kwa karibu sana na kuliwezesha na kulipa fursa zaidi eneo la uzalishaji. Eneo hili tukiliangalia kwa karibu wananchi/wawekezaji watapata fedha na Serikali itapata fedha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilitoa ushauri kwamba tunajenga SGR Standard Gauge Railway, lakini huko njiani kuna eneo kubwa sana ni porini. Nikasema sekta ya kilimo, sekta ya maliasili na sekta za viwanda zianze kufanya utafiti kuangalia maeneo gani inakopita hii reli kwenye mapori tunaweza tukapanda mazao ya miti. Pia, tunaweza tukaweka eneo la utafiti la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nichangie mchango wangu kwa kuanza kuipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pamoja na mambo mbalimbali ya msukosuko wa uchumi duniani, lakini inafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli takwimu hapa zinaonesha kwenye ukuaji wa uchumi wa mwaka 2020/2021, nchi yetu ilikua kwa asilimia 4.9, lakini mpaka Juni, 2022, takwimu zinaonesha kwamba, unakua kwa asilimia 5.2, lakini ugumu wa uchumi huu ukuaji wake ukiangalia uchumi wa dunia utauona unasinyaa. Uchumi wa dunia una-deteriorate na wote tunajua sababu kubwa ya msingi hapa ni Covid-19, lakini pia kabla hatuja-recover, dunia haija-recover kutoka kwenye hii pandemic effects hizi, tukaja tukaingia hii vita ya Ukraine. Kwa hiyo, sasa imekuja imechanganya economic destruction hii vita ya Ukraine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imejionesha pia huko duniani ambako kuna high inflation rate ambayo imefikia mpaka double digit, lakini sisi tumeweza ku-control bado tuna single digit mpaka sasa hivi. Mpaka sasa hivi tuko kwenye four point something, lakini wenzetu duniani huko labda tuchukulie mfano European Union, kwa nini nasema tunafanya vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, European Union, inflation rate yake kuna nchi pale zimefikia mpaka asilimia 25.5 na nchi ya chini kabisa ambayo inafanya vizuri, Ufaransa, iko 6.2 inflation yake. Data zilizokuwa revealed na Eurostat zinasema kwamba, kwa wale giants kwa mfano, Netherlands wana 13.7 ya inflation, Greece wana 11.2, Belgium 10.5, Spain 10.5, Denmark 9.0, Cyprus 9.0, Sweden 9.5. Kwa hiyo, hawa wote hawa ndio ambao wanatuchangia na sisi pia katika miradi mbalimbali, lakini wana high inflation rate, sisi tumeweza ku-control, bado tuko kwenye chini ya tano. Sasa ni lazima tujipongeze katika hili, tusikate tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza sana Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake katika eneo hili, lakini sisi sio kisiwa, duniani projections zinaonesha kwamba, ukuaji wa uchumi utashuka kutoka kwenye 6.1 mpaka 3.2. Kwa hiyo, sisi sio kisiwa, ni part ya dunia. Kama ilivyojionesha huko kwa wenzetu ulaya, European Union, inflation ilivyokuwa juu sasa bado sisi tuendelee kuhakikisha kwamba, Mpango wetu huu tujiwekeze sana katika kuhimili hali ya mtetereko wa uchumi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie; Mpango huu tujielekeze sana kwenye uhimili wa hali ya mtetereko wa uchumi duniani kwa sababu, tunapoelekea tumeambiwa pia, takwimu zinatwambia kwamba, tutakapofika half ya pili ya bajeti hii hali ya uchumi itashuka, ukuaji wa uchumi hapa kwetu nchini. Sasa tuwe na mpango wa kuhakikisha sekta za uzalishaji, kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, biashara zinakuwa na tunaziwezesha na kusimamia utekelezaji wake na masoko yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima tumalizie miradi yetu ya kimkakati, reli SGR tuimalizie, umeme vijijini tumalizie ili wananchi wetu waweze ku-add value mazao yao, lakini LNG, mradi ya gesi lazima tuhakikishe unajengwa na unakamilika, lakini miradi ya gesi ambayo ile ya kuzalisha umeme tuhakikishe kama ilivyopangwa katika bajeti hii nayo pia inakamilika, lakini Bwawa la Mwalimu Nyerere tulisimamie kwa karibu sana ili liweze kukamilika. Hii itasaidia uchumi wa jumla kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa nimeonesha mfano wa data hapa, wa Eurostat data, inaonesha European Union nchi ambayo uchumi wake, high inflation rate yake iko chini Ufaransa, wao waliwekeza sana kwenye energy. Waliwekeza kwenye energy kupitia hii nuclear, sasa hivi wao wameshindwa kubabaika, hawajababaika kabisa na hili tatizo lililokuwepo la Russia kukata au kupunguza umeme na gesi katika Nchi za Ulaya ambalo limesababisha high inflation rate. Hii ni kwa sababu, wao walikazana na wakawekeza kule. Sasa sisi tukazane tukamilishe hii miradi mikubwa ya kimkakati ili uchumi wetu usibabaike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, pia hali ya uchumi ya dunia inavyokwenda itatuathiri na sisi uchumi wetu katika nusu ya pili, naomba sana ili isituathiri sana tuwekeze kwenye kilimo. Leo kwenye kilimo Serikali iliwekeza bilioni 150 za ruzuku, lakini katika utekelezaji wake huu unasuasua practically kwa maana kwamba, Serikali imetuambia mpaka leo hii, leo asubuhi imetuambia itatufikishia mpaka kwenye makao makuu ya wilaya au tarafa, hautasambazwa vijijini. Kilichonishangaza ni kusikia kwamba, halmashauri ndio zisambaze Serikali itazipa mafuta. Halmashauri hizi zinatoa wapi magari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mkulima kwangu tarafa ya mwisho iko kilometa 220, kata ya mwisho iko kilometa 254. Mkulima kuifuata mbolea huko iliko kilometa 254 inabidi asafiri kwa gharama ya 40,000/= kwenda na kurudi, alale hapo, anunue mbolea, asafirishe na mbolea aipeleke kule, gharama inazidi. Kwa hiyo, ushauri wangu, lazima Serikali watafakari upya au watuachie kule wilayani, Mwenyekiti wa Kamati ya Pembejeo Mkuu wa Wilaya asimamie, basi wawaachie wafanyabiashara wa maeneo yale wasafirishe kwa gharama ambayo atailipia mkulima isizidi hata 5,000/=. Nawaomba sana wafanyabiashara tuwaachie kuliko sisi leo tuwaambie halmashauri tutawapa mafuta, magari watatoa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaachie wafanyabiashara waifanye kazi hii. Mkulima yuko tayari kuongeza hata shilingi 5,000 kwa ajili ya usafiri ili mbolea imfikie pale. Serikali tunafanya kazi nzuri sana, tumempunguzia nusu, mwaka jana tulikuwa tunanunua mbolea shilingi 130,000, leo tunanunua shilingi 60,000 mkulima sidhani kama atashindwa kulipia shilingi 5,000kwa ajili ya usafiri. Naomba Serikali walitafakari sana na msimu ndio huu hapa, wakati umeshafika wa maandalizi ya kilimo, watu wanababaika wanasafiri, wanapambana, wanalala siku tatu, siku nne, kutafuta mbolea, mnyonge wa kawaida anayeishi Magazini au anayeishi Lingusanguse, anayeishi Msisima kuja kufuata mbolea Namtumbo, kilometa 284, hawezi, kwa hiyo, ni lazima tusaidie hili. (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Taarifa Mheshimiwa Vita Kawawa. Jambo la Nkansi na arrangement ya Nkansi ni maamuzi na ushauri uliotoka kwenye Halmashauri ya Nkansi. Haina maana kwamba, modality tunayoifanya Nkansi ni uniform kwa nchi nzima, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimesema kwamba, Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa Wilaya, maeneo ambayo wanashauri kufunguliwe vituo sisi kama Wizara tuko tayari ku-facilitate kwa sababu, tunatumia taasisi zetu mbili maeneo ambayo wafanyabiashara hawaoni faida ya kwenda. Sisi kama Serikali tunatumia TFC na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kwa ajili ya kufikisha mbolea katika maeneo hayo, ili wakulima waweze kununua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, modal ya tatu ambayo tunaifanya kama Wilaya ya Rorya, Halmashauri inakusanya mahitaji yote ya vijiji vyake halafu tunachagua kampuni inayopeleka katika eneo lile kutokana na orodha ya wakulima. Kwa hiyo, kila eneo lina jiografia yake, lina tabia yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho. Hatuzuwii wakulima kuchangia gharama ya kusafirisha pale ambapo wao wenyewe wanaamua. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kawawa na muda wako umekwisha. (Makofi)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kawawa, muda wako umekwisha.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. VITA R. KAWAWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuhitimisha hoja niliyowasilisha asubuhi hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati ya NUU - Nje, Ulinzi na Usalama imechangiwa na wachangiaji Tisa, nikianza na Mchangiaji wa kwanza alikuwa Mheshimiwa Mbogo ambaye alizungumzia diplomasia ya uchumi, alieleza Mikoa ya pembezoni mipakani ipewe elimu ya diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati tulishatoa mapendekezo kwamba Bunge liazimie Serikali iandae mpango mkakati wa utekelezaji wa kidiplomasia ya uchumi nchini ikiwemo kuwapa elimu ngazi za Mikoa na Wilaya. Tunashukuru Wizara hapa imejibu na kuomba iruhusiwe ipate kuanza na mkakati mmoja, nasi kwa niaba ya Kamati tunakubali hilo. Pili, kupatiwa fedha Wizara ya Mambo ya Nje kukarabati Balozi zetu na kujenga, Kamati tulishatoa mapendekezo kushirikisha sekta binafsi, na sekta za umma katika ujenzi wa majengo ya Balozi na vitega uchumi kutarahisisha upatikanaji wa fedha na ujenzi wake kukamilika kwa haraka na hivyo kuwa na majengo ambayo yanastahili kwa hadhi ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wa pili, alikuwa Mheshimiwa Felister Njau, yeye amesisitiza upatiakanaji wa fedha zilizotengwa na kuidhinishwa na Bunge, kwamba mtiririko wake hauridhishi kwa Wizara zetu tunazo zisimamia, Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kwa hili mimi sina la kusema zaidi, ninaamini Serikali imekusikia na ninaamini italifanyia kazi. Kwa nyongeza tu Bunge linapotoa maazimio kuhusu mambo mahsusi linafanya kazi hiyo ili kuhakikisha kwamba tija iliyokusudiwa inafikiwa kwa ustawi wa wananchi. Hivyo ulinzi na usalama wa raia ni ustawi wa wananchi wake. Tukiwa na amani ndivyo hata tunaweza kufanya kazi nyingine. Hata hivyo, tuko hapa Bungeni kwa sababu ya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vyema sana Bunge linapotenga na kuidhinisha fedha kwa ajili ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, tunaiomba Serikali ivipe kipaumbele vyombo vya ulinzi na usalama ili waweze kufanya kazi yake inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Faharia pia alizungumzia PAROLE; Kamati ya NUU ilikwishatoa maelekezo kwa Wizara ya Mamabo ya Ndani ya Nchi kufanya tathmini ili kubaini changamoto ya utekelezaji wa Sheria ya PAROLE ili kuchukua hatua stahiki kuziboresha. Hata hivyo alizungumzia kuhusu Sera ya Mambo ya Nje; ni matumaini yetu Kamati na Bunge, Serikali itakamilisha maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje mapema kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Condester Sichalwe, naye alizungumzia kuhusu COMESA. Serikali imesikia na imetoa ufafanuzi hapa; ila ushauri wetu sisi kama Kamati, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ije kutupa elimu, kutueleza kwa kina ili tuwe na uelewa wa pamoja kuhusiana na hii COMESA. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri amepata muda mchache akalielezea kwa uchache; lakini kama akipata nafasi tunaomba uweze kuja na timu yako kulielezea Bunge kuhusiana na huu mtangamano na kujitoa kwetu COMESA na nini maana yake. Hata hivyo, tunafahamu kuna hii Tripartite, kuna EAC na SADC. Faida tunazozipata umezielezea hapa kwa ufupi. Hata hivyo, tungependa pia ungekuja kulielezea Bunge zima kama semina ili liweze kuelewa kwa makini kuhusiana na hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Neema Lugangira, yeye alizungumzia ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa diaspora kupata hadhi maalumu? Nadhani Waziri amelijibu vizuri suala hili, lakini sisi kama Kamati tunasisitiza Serikali ikamilishe mchakato huo ili hii kazi iweze kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Chumi naye alieleza kuhusu vijana waliopelekwa Israel kusomea kilimo cha kisasa, kwamba wanaporudi waunganishwe na vijana wa JKT na block farming zinazoanzishwa na vijana wengine. Mheshimiwa Chumi hili naamini Serikali imekusikia na naamini watalifanyia kazi. Serikali ina wajibu pia wa kuisaidia NIDA. Hoja yake ya pili, kuhakikisha inakamalisha utoaji wa vitambulish. Ni kweli, Kamati inaishauri Serikali kuendelea kuiwezesha NIDA kwa wakati ili kukamilisha zoezi hili; na tumesisistiza sana jambo hili liweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Mheshimiwa Getere pia aliongezea kwenye hili, alisema tuambiwe ni lini kazi ya kutoa vitambulisho inakamilika au inaisha lini kazi hii? Ushauri wa Kamati, Serikali iendelee kuipatia fedha kwa wakati NIDA kama zilivotengwa na kuidhinishwa na Bunge ili kuharakisha utambuzi, usajili na kuchapisha vitambulisho na kuvisambaza kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Londo naye alitoa ushauri kuhusu diplomasia ya uchumi. Kamati imepokea ushauri wake na tunaamini Serikali pia imemsikia ushauri wake, na kama haikumsikia vizuri, basi tunaomba iitishe Hansard ili iweze kumsikia na kuona jinsi gani ya kutekeleza ushauri wa Mheshimiwa Londo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Mheshimiwa Ally Kassinge naye alizungumzia mtiririko wa upatikanaji wa fedha katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Mimi ninaamini Serikali na Wizara ya Fedha, hususani Wizara ya Fedha imekusikia vizuri sana. Hata hivyo Kamati inapendekeza maazimio na haya yote ambayo yamo tunaomba Bunge liridhie ili yawe maazimio ya Bunge na Serikali iyafanyie kazi. Maazimio yetu yote tuliyoomba tunaomba Bunge liweze kuridhia ili yafanye kazi

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengine walikuwa Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Bashe Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Engineer Masauni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Stegomena Tax Waziri wa Mambo ya Nje, Mheshimiwa Innocent Bashungwa Waziri wa Ulinzi na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri wa Fedha. Tunawashukuru sana wote mliochangia mchango huu na ninaamini Serikali imewasikia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo baada ya kutoa ufafanuzi wangu naomba sasa kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likubali taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Pamoja na maoni na mapendekezo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuisimamia vizuri Wizara hii na kuhakikisha kwamba inapata fedha za kutosha ili kuendeleza uchumi wa nchi hii unaotokana na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Mheshimiwa Antony Mavunde; Katibu Mkuu, Gerard na Naibu Katibu Mkuu Hussein Mohamed kwa kazi nzuri na timu nzima ya Wizara wanayoifanya katika Wizara hii. Naomba ni-quote aya ya 29 ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri leo ambayo inasema, “Taifa lolote ambalo liko huru, lenye kulinda heshima na utu wa watu wake ni lile ambalo linajitosheleza kwa chakula na uchumi imara. Ili uwe na uhakika wa chakula ni lazima kuimarisha uzalishaji, tija na kuwa na umiliki wa mbegu zetu, kwani atakayetawala dunia hii, ni yule ambaye ana umiliki wa mbegu bora na utoshelevu wa chakula. Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwa hali ya mtetereko wa uchumi duniani ilivyo sasa hivi, uzalishaji wa chakula cha kutosha na mazao ya biashara ya kutosha ni nyenzo muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu na uchumi wake. Tumeshuhudia hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakimshukuru Waziri na Wizara kwa kuwapelekea chakula kwenye maeneo yao yale ambayo yalikuwa na upungufu wa chakula. Kama tusingekuwa tumejitosheleza kwa chakula, hasa mahindi, tungebabaika sana na uchumi wetu ungeyumba sana. Kwa hiyo, naipongeza sana Wizara hii, napongeza sana kwa utaratibu wenu mnaousimamia na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na chakula cha kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nirudi kwenye eneo la mazao. Nitaanza na zao la soya. Tanzania tunakadiria kwamba tuna mahitaji ya soya zaidi ya tani 250,000 kwa mwaka, kwani kuna mahitaji mengi ambayo yanahitajika kwa ajili ya chakula, lishe bora lakini pia kwa ajili ya kutengeneza chakula cha mifugo. Vile vile tuna upungufu mkubwa wa uzalishaji wa soya nchini. Kuna makampuni pia yanayotengeneza vyakula vya binadamu, yanahitaji soya hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi ya wenzetu ya Zambia, takwimu zinaonesha kwamba wanazalisjha kati ya tani laki tatu na nusu mpaka tani laki nne kwa mwaka na inaongoza kwa uzalishaji kusini mwa Bara la Afrika ikifuatiwa na Malawi ambao wanazalisha tani 250,000. Sisi tunakadiriwa, na haifiki tani 20,000 kwa mwaka, na asilimia 50 mpaka 70 ya Soya hii inazalishwa Jimbo la Namtumbo. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri, sisi tuna uhitaji wa hizo tani 250,000 ndani, lakini tuna trade agreement ya Soya na China ambayo inahitaji zaidi ya 500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, naiomba sana Wizara na timu ya Wizara ya Kilimo tushirikiane kuweka mkakati wa kulisimamia zao hili kwa karibu, uzalishaji wake, uzalishaji wa mbegu, utalaam katika kulima, uvunaji, uhifadhi, masoko yake pia yawe huru na ya ushindani ili kuwapa nguvu wakulima na kuongeza uzalishaji. Pia tuwe na viwanda ambavyo vitakuwa vinasafisha na ku-standardize quality kwa ajili ya kuuza nje hiyo soya. Tulisikia juzi Balozi wetu wa China alikuwa akilalamika kwa baadhi ya wanaopeleka soya China, walipeleka Soya chafu. Hii inaweza ikafanya tukaondolewa kwenye soko kama hatuangalii quality ya mazao yetu. Kwa hiyo, nilitaka kuanza na hilo la soya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni tumbaku. Msimu huu tumbaku tunakwenda vizuri. Nasi tunaishukuru sana Wizara kwa usimamizi mzuri chini ya Mheshimiwa Bashe. Pia tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alilisimamia sana zao hili na kujenga confidence kwa makampuni kurudi. Kwetu Namtumbo tulikuwa tunazalisha tani 500, lakini leo tuna mkataba wa tani 9,600 ambao ni mkataba mkubwa sana wa uzalishaji wa tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu kwenye hili, naungana na wenzangu, kwamba hawa Classifier, wateuzi wa tumbaku wawezeshwe waende wafike kwa wakati ili zao hili lisitumie muda mrefu kuuzwa sokoni, kwa sababu hawa ndio wateuzi wa tumbaku, sasa lazima wawezeshwe, wawe na usafiri wa kutosha, gharama zao; Wizara na Serikali ihakikishe inafanya zoezi la biashara hii au soko hili, likamilike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naungana na wenzangu, mbolea hii 101824NPK ambayo inatumika kwa wingi kwenye tumbaku ya mvuke na tumbaku ya hewa, tunaomba sana msimu wa mwakani 2024 basi iingizwe kwenye ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wengi wanolima tumbaku ya mvuke na tumbaku ya hewa wanatumia mbolea hii. Kwa hiyo, tunaomba sana hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuwa sisi nchi yetu Mungu ametujalia. Narudia kusema hili, kijiografia sisi kule Namtumbo kiasili ni wakulima na wahifadhi. Sisi haya mahindi ambayo yamechukuliwa na yakahifadhiwa na tumewagawia wenzetu, asilimia fulani yametoka Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, tunachoomba sisi, ili maeneo haya ya kilimo yasiingiliane na mifugo, narudia tena yasiingiliane na mifugo. Leo hii sisi mifugo imekuja bila hata taarifa, bila vibali, hii leo naomba nirudie pia ni-quote hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ambayo aya ya 30 ilisema; “Tathimini ya kina ya hali ya chakula na lishe imebaini kuwa upungufu wa uzalishaji katika baadhi ya maeneo kwa msimu wa 2021/2022, ulitokana na athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi.” Nasema sio tabia ya nchi tu na pia mabadiliko ya tabia ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nchi yetu ilikuwa ina maeneo ya watu wafugaji, maeneo ya kilimo, maeneo ya uvuvi, maeneo ya uzalishaji wa dhahau n.k. Sisi Kusini ni wazalishaji wa kilimo. Leo hii huku maeneo haya ya mifugo mvua zinachenga, leo ndio tunachukua chakula tunawapelekea lakini sasa leo hii wanatuletea mifugo sisi, leo hii mtu ana mifugo 1000, 2000, akiingia kwenye shamba la mtu lote limekwisha mara moja. Halafu, mbaya zaidi wamekuja kama wako vitani na sasa wanatuambia sisi kule sio watanzania. Wamefika wanasema kauli ninyi sio watanzania, sisi ndio Watanzania, kwenu Msumbiji, sisi tuna haki ya kuishi hapa, wanaingiza ng’ombe kwenye mashamba ya watu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Vita, malizia mchango wako muda umekwisha.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kero kubwa sana kwetu. Naunga mkono hoja lakini hili suala la mifugo na wakulima tunaomba Mheshimiwa Bashe, mshirikiane Serikalini muone jinsi gani ya kuacha aneo hili kilimo liweze kutumika kwa kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu kwetu kwa afya zetu na kwa wananchi wetu wa Tanzania. Naomba nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. Tumeshuhudia wakiwa mstari wa mbele katika mambo mbalimbali na magonjwa mbalimbali ya mlipuko yanapotokea na wanajitahidi chini ya uongozi wao kuzima magonjwa hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki cha mwaka 2022/2023, tumeweza kupata zaidi ya bilioni tano na milioni 318 katika kujenga miundombinu ya hospitali zetu katika Wilaya ya Namtumbo. Hospitali ya Wilaya tulipata bilioni mbili na milioni mia tatu, tumejenga majengo, wodi ya akinamama na akinababa, tumejenga Hospitali ya meno na macho, lakini tumejenga jengo la mama ngojea, tumejenga na mortuary pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mama ngojea ni muhimu sana sisi kwetu kwa sababu, jiografia ya Namtumbo, Kijiji cha mwisho kinafika kilometa 254, kwa hiyo, kuna akinamama wanaopata complications kutoka katika hospitali wanapata rufaa kuja pale wengine kwa ajili ya kungojea kusubiri kujifungua, basi Serikali imewajengea jengo la mama ngojea, wanasubiri wakiwa palepale. Kwa hiyo, hii ni kazi nzuri sana waliyoifanya na inawasaidia sana mama zetu wale ambao wakifika pale wanakuwa bado hawajawa-admitted, lakini wanakuwa katika jengo lile la mama ngojea. Kwa hiyo, dharura yoyote inapotokea wanatibiwa, kwa hiyo, tunashukuru sana Wizara na Serikali kwa eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili Serikali wametujengea vituo vya afya vilivyokamilika. Kilichokamilika kimoja cha Mtakanini, lakini tuna vituo vya afya viwili viko mwishoni tulipata bilioni moja, Kituo cha Afya cha Ligela milioni 500 na Kituo cha Afya cha Magazini milioni 500 ambayo tuko katika hatua za mwisho kabisa. Pia Serikali ilitugawia fedha za kukamilisha zahanati nane, tulipata milioni 400; kila zahanati milioni 50 na tumekamilisha Zahanati ya Namali, Uramboni nayo iko mbioni kukamilika, Nahimba pia iko mwishoni, Kilangalanga iko mwishoni kukamilika, Misufini iko tayari na inatoa huduma, lakini Kumbara iko mwishoni kukamilika, Nahoro nayo ipo mwishoni, Luhangano nayo iko mwishoni kukamilika na Muhangazi iko mwishoni kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo ila tuna mapungufu ambayo pia, naomba niiombe Wizara kwamba, Kituo chetu cha Afya cha Mtakanini kina upungufu bado wa wodi mbili, wodi ya akinamama na wodi ya akinababa ya kulaza wagonjwa, lakini pia tuna upungufu wa wataalam wa usingizi, hatuna mtaalamu wa usingizi pale, alkini pia hata Hospitali ya Wilaya pia ina upungufu wa mtaalam wa usingizi, lakini ikama ya watumishi katika Hospitali ya Wilaya haijatimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru Kituo cha Afya cha Mtakanini walitupatia watumishi 11 na walifika wameripoti na wanaendelea na kazi, lakini bado tuna upungufu wa mtumishi wa usingizi. Hospitali ya Wilaya nayo ina upungufu wa vitendeakazi vingine kama standby generator kwa ajili ya mtu akiwa anafanyiwa operation na dawa zile ambazo zinahitaji kuwekwa kwenye majokofu umeme unapokatika, hatuna standby generator katika Hospitali ya Wilaya na vituo vyetu pia havina standby generator.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya pia ina upungufu wa vitanda, baada ya majengo mengi kujengwa bado tuna upungufu wa vitanda. Kwa hiyo, tunaomba sana Wizara ituangalie kwenye hili, watumishi, lakini pia baadhi ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tunaambiwa hela zimepelekwa MSD, lakini kuna kuchelewa kufika kwa vifaa tiba na dawa pamoja na kwamba, tulipata vifaa tiba vya milioni 758, tunaishukuru sana Serikali, vifaa tiba vya milioni 758 tumeshavipokea, lakini kuchelewa kwa vifaa tiba vingine nayo inatuchosha, lakini tunawashukuru sana. Nawashukuru sana Waziri wakati wote na Naibu Waziri nikiwafikia, basi huwa wananisikiliza na wananitatulia tatizo langu, kwa hiyo, nawashukuru sana, waendelee hivyohivyo na kwa kusema kweli wameiweza Wizara yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu pia wa wataalam wa meno na vifaa vyake. Kwa sababu, tuna jengo jipya la huduma hii ya meno kwa hiyo, hatuna vifaa vyake, lakini tuna upungufu pia wa ultra sound katika Kituo cha Afya cha Mtakanini kwa hiyo, tunaomba sana. Hivi vituo vya afya vingine viwili vilivyobakia ambavyo viko mwishoni tunaamini kabisa wakati wowote vitakamilika na watatupatia vifaa tiba. Tunaomba sana ili majengo yasikae muda mrefu, tungeweza kuanza kupata vifaa tiba sasa hivi yanapokamilika kwa sababu, yameshaisha, wako kwenye final touches, kwa hiyo, vile vifaa tiba vingeanza kupelekwa sasa hivi, ili wakimaliza kabisa, basi huduma inapatikana. Tunawashukuru sana kwa yote ambayo wanatutendea sisi Namtumbo katika kipindi hiki, asanteni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Viongozi wote Wakuu wa Majeshi walio chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza Wabunge mbalimbali ambao wameweza kueleza maeneo mbalimbali katika majeshi yetu na kazi wanazozifanya, lakini naomba tu niwaambie majeshi yetu haya yanafanya kazi nzuri sana, sisi tunaosimamia Kamati tunajua umuhimu, Jeshi la Polisi wanafanya kazi saa 24 kwa siku saba na ndio maana leo tuna amani katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linalinda usalama wa raia na mali zake, lakini tuna Jeshi la Magereza linahifadhi wale ambao wanakuwa wakorofi na wanawahifadhi vizuri na wanarekebishwa. Tuna Jeshi la Uhamiaji ambalo linakaa, lipo mipakani mwetu, linafanya kazi masaa 24 siku saba au wiki, kuangalia kila mtu anayeingia nchini na linaruhusu watu wanaokuja waliokuwa wema, waliokuwa wabaya wanaondoka, ndio maana nchi yetu leo hii inaendelea kuwa na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna budi kuyapongeza majeshi yetu haya. Tuna Jeshi la Fire basi ikitokea moto, linakuja kuzima, kwa hiyo tunaomba sana Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge tutambue majeshi yetu haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati tulibahatika kutembelea na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani tulitembelea nchi moja sitaweza kuitaja, nchi hiyo hakuna amani. Tumefika nchi ile pale tumewekwa sehemu moja na tunatakiwa twende sehemu nyingine, umbali wa kutoka hapa mpaka Morogoro lakini kwa gari ni siku nne, umbali wa kutoka hapa mpaka Morogoro, siku nne na njiani humo kuna vikundi vitatu, kila kikundi kinafanya kazi yake ya uhalifu, kwa sababu hakuna amani. Kwa hiyo tulishindwa kwenda kwa chini na tukashindwa kwenda kwa kuruka kwa sababu hakuna amani. Kwa hiyo sisi hatuna budi kuyapongeza majeshi yetu na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri inazozifanya za kulinda amani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwanza kwa kukubali na kuridhia maombi ya Wizara chini ya Mheshimiwa Engineer Masauni, kuridhia kutoa shilingi bilioni 42.5 kwa NIDA, Taasisi yetu ya Vitambulisho vya Taifa kwa ajili ya kuchapisha vitambulisho milioni 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii NIDA imeshapokea fedha hizo na imesha-order vitambulisho, kwa hiyo tunachosubiri ni ujio wa vitambulisho ghafi na kuanza kuzalishwa milioni 13. Naamini kabisa maneno yote ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Taasisi ya NIDA ikikamilisha, kelele zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mategemeo yetu kwa Taasisi yetu hii ya NIDA ikisimamiwa vizuri chini ya Wizara na ikafanikisha zoezi hili la kuzalisha vitambulisho milioni 13, tutavuka hapa tulipo kwa sababu vitambulisho ni jambo muhimu sana kwa Taifa letu, lakini pia na kwa dunia yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haja ya kuboresha sheria ili kuona taasisi zetu muhimu zinazohusika na utambuzi kwa watu wetu na kwa ajili ya shughuli za kimsingi za kijamii na kiuchumi zisiachwe nyuma kutokana na vitambulisho hivi vya NIDA, kwanza ni vitambulisho janja kwa maana vina smart card, vina chip ndani yake ambayo inahifadhi taarifa zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunafanya kazi ya duplications katika taasisi mbalimbali ya utambuzi wa watu, lakini ushauri wangu ni kwamba lazima tuwe na uniform au tunakuwa na universal identity data bank kwa ajili ya vitambulisho vyetu vyote ili kupata taarifa zilizo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano leo tumesikia hapa kwa Mheshimiwa mkongwe Maida kwamba kuna mtu aliumwa, akapelekwa Zanzibar, alipofika Zanzibar akafariki na alipofariki baada ya mwaka akaletewa barua ya kuambiwa amestaafu na anatakiwa arudishe vifaa vyote vya Jeshi la Polisi. Hii yote ni kwa sababu ya kukosa mfumo unaounganika pamoja ulio sahihi. Kwa hiyo tuuboreshe mfumo huu wa NIDA, tukipewa vitambulisho vyote watu wote wakapata tujitahidi sana taasisi zetu zote ziunganishe mfumo uwe mmoja kwenye mfumo huu wa NIDA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami kwa utamaduni, naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yote ya Wizara yetu ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, pia nakuponggeza na kukuombea kwa Mwenyezi Mungu wewe binafsi ambaye unaomba nafasi ya Urais wa IPU, nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akusimamie na utashinda nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Namtumbo ni wahifadhi, na nimekuwa nikisema ni wahifadhi na wakulima. Kwa miaka yote tumekuwa ni watu wa aina hiyo. Ni sisi wenyewe pia tulifika mahali tuliamua kwamba tuanzishe maeneo ya uhifadhi kwenye maeneo yetu ya vijiji.

Mheshimiwa Spika, tulianzisha Wildlife Management Areas (WMAs) ambazo jumuiya hizi tulianzisha kwa kusini mwa Selous wakati ule mwaka 2007, ilikuwa inaitwa Mbalang’andu Kaskazini, na Kusini tuna Kisengue na Kimbande. Jumuiya hizi tulikubaliana hapo awali kwamba baada ya miaka 10 tutakuja kuwa na mapitio kwa ajili ya matumizi ya ardhi kwa sababu ile ilikuwa ni ardhi ya kijiji tuliiweka kwa ajili ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, miaka 10 ilishapita mwaka 2017 na wanavijiji wamekuwa wakiomba kufanyika mapitio ya ardhi kwa sababu wanahitaji ile ardhi kiasi, siyo yote kwa ajili ya kilimo. Lakini kumekuwa na danadana wasifanye yale mapitio na kuna sehemu wamefanya mapitio lakini majawabu hayaji. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali lazima tuishauri kwamba twendeni tukawaelewe wananchi mahitaji yao, ardhi yao ile waliitoa kwenye uhifadhi sasa wanahitaji kiasi kwa ajili ya kilimo. Lakini sasa hivi wanaonekana wananchi wale wa Namtumbo katika vijiji vile vyenye uhifadhi kana kwamba wao ndiyo wanataka kuvamia maeneo ya uhifadhi, kwa hiyo nguvu kubwa sana inatumika ili kuhakikisha kwamba wasiingie.

Mheshimiwa Spika, kama mtarudi mkazungumza nao kama mlivyowashawishi mwanzo, kuwapa elimu mwanzo na kukubali kufanya uhifadhi, tunaomba sana mrudi tena kuzungumza nao ili kuona ni kiasi gani na kufanya mapitio wapewe wananchi wale waweze kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda tufahamu Maafisa wa Hifadhi pia, tufahamu sisi sote ni binadamu, na binadamu hasa wa vijijini kule wanategemea mapato yao ni kilimo, ndicho kinachofanya wanakidhi maisha yao kuishi katika dunia yetu hii. Kwa hiyo, lazima tufikirie hilo pia, pamoja na uhifadhi. Kwa hiyo, ushauri wangu ulikuwa huo, naomba sana tunapokwenda kule tuwasikilize wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu utalii. Balozi zetu na consuls kuu zetu zinafanya kazi kubwa ya kutangaza utalii, lakini kwenye bajeti zao Balozi na consuls kuu hakuna vifungu maalum vya kutangaza utalii, wanatumia OC zao. Siyo vibaya, lakini kutumia OC zao zile za kawaida inawawia ugumu sana kufikia malengo ya kuutangaza utalii wa nchi yetu. Kuna Ubalozi una nchi saba, lakini unahitaji usafiri uende ukatangaze maeneo hayo, hawana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna uhitaji wa kutangaza, fedha zinakuwa hazitoshi. Kwa hiyo, tunashauri Wizara mtenge fedha kwa ajili ya balozi zetu kuchapisha matangazo, majarida kwa lugha za kule, lakini kufanya matagazo kwenye televisheni pia. Ni muhimu sana kwenye hili kuzisaidia Balozi zetu. Hakuna fedha mahsusi zinazotumika kwa ajili ya utalii. Mimi naamini hili litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuutangaza utalii wetu. Nilipata bahati alikuja Spika wa India, Lok Sabha Om Birla. Uliniteua niwe mmoja wa watakaompokea na kuwa naye, lakini ulinipa kazi ya ziada kwenda Serengeti. Tulipokwenda Serengeti kule walihitaji kuona wale Big Five, waliwaona kweli, walibahatika wote, faru, a pride of 18 Alliance waliwaona kwa mara moja. Na Spika yule alishangaa kabisa, alisema katika maisha yake mpaka utu uzima hajawahi kuona simba zaidi ya mmoja, alikuwa ameona simba wale 18 live.

Mheshimiwa Spika, pia waliona nyumbu wengi, toka asubuhi wanaona nyumbu mpaka wakati wanapovuka. Wakasema walikuwa wanajua hawa nyumbu wako upande wa nchi ya pili kule, wenzetu kule wanatangaza sana, wao wanafahamu upande ule wa pili, lakini kumbe eneo kubwa la nyumbu hawa liko huku Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Wahindi nao hawakuwa wanafahamu kama Serengeti ndiyo ina wanayama wengi na wale wanyama nyumbu wanakuwa wengi upande huu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, tukazane sana kwenye eneo hili na hili ni pekee kwa kuwezesha Balozi zetu wazitangaze vizuri kule. Kwa hiyo ile timu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaj)

SPIKA: Haya, ahsante sana. Maliazia sentensi.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ile timu ya Spika wa Lok Sabha ndiyo imekwenda kutusaidia kututangazia kule. Kwa hiyo, tuongeze nguvu ya fedha kwenye Balozi zetu kutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo. Nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii, kuna mtu mmoja ananiambia nisimame, nimesimama. Kama hawanioni nina mpango wa kununua vile viatu vinavyoitwa raizoni ili niwe navivaa wawe wananiona vizuri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayoifanya, pia kwa kuwasilisha hotuba yao hapa Bungeni. Nchi yetu kijiografia imejaliwa katika maeneo mbalimbali ya kuzalisha kiuchumi. Kuna maeneo ya uvuvi ambayo katika Maziwa yetu Makuu wananchi wetu wanategemea uvuvi. Kuna maeneo ya bahari wanaoishi katika Visiwa vya Bahari na pembezoni mwa bahari wanategemea uvuvi. Leo hii tuna maeneo pia ya Mikoa ambayo yanategemea mifugo, Mikoa ya Kaskazini na Katikati hapa. Kuna Mikoa pia inategemea kilimo, Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa na Mwenyezi Mungu kutupa jiografia ya namna hii ni kwamba ili tuweze kuzalisha chakula, tuweze kufuga, tuweze kuvua pia na Samaki, sasa katika eneo letu la Mkoa wetu wa Ruvuma na hususan Wilaya ya Namtumbo ni wakulima. Tunategemea sana kilimo ndiyo kipato chetu cha uchumi wa wananchi wetu, sasa katika miaka hii ya karibuni, miaka miwili ya karibuni hapa kumetokea na mfumuko wa mifugo kuja katika Wilaya yetu ya Namtumbo, pia kumekuwa na Mikoa ambayo inatoa vibali vya kusafirisha mifugo hiyo itoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanatoa vibali vinavyosema ameruhusiwa aende bila ya kushirikisha mamlaka za Mikoa ambayo mifugo hiyo inakwenda kama wana mipango gani ya ardhi katika eneo lao la Mikoa hiyo. Sasa Mikoa ile inayokwenda mifugo hii, Serikali au Mamlaka ya Mikoa ikiwakamata wanaonesha vile vibali na wanasema kwamba, Katiba inaturuhusu, binadamu yeyote raia wa Tanzania unaweza kuishi mahali popote pale, lakini wanashindwa kusema kwamba, bila kuvunja sheria, sasa wanapozuiliwa wanasema wanaonesha vile vibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, kuwe na utaratibu mzuri wa mawasiliano ya ng’ombe au mifugo inakotoka kule wanaoomba kibali na mamlaka ya Mkoa ule iwasiliane na mamlaka ambayo yule mfugaji anataka kuhamishia ng’ombe wake kule ili waweze kuelewana, nafasi ipo au hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika Wilaya yangu ya Namtumbo wamejaa ng’ombe wengi sana. Sisi ni wakulima, mwaka jana tu 2021, tumezalisha zaidi ya tani 157,000 ya mazao ya nafaka, ni mazao ambayo yanategemewa katika Taifa hili, lakini sasa kumekuwa na taharuki mwaka huu wa ng’ombe kulisha katika mazao hayo. Mkulima anaandaa shamba, analima anatafuta mbegu dukani, anapanda, anapalilia; anaenda kununua mbegu ambayo mwaka huu imezidi zaidi ya Shilingi 100,000/= anatia shambani, mahindi yanatoka ya kijani, mtu analeta ng’ombe analisha kwa dakika 20 au usiku mzima. Kwa hiyo, hii inaleta tafarani kati yetu sisi wakulima tusiozoea kuwa na mifugo, tuliozoea kuzalisha chakula kwa ajili ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, Serikali itambue kwamba sisi ni wakulima, lazima mje mtutambue kwa sababu hamjatambua kuna mifugo kiasi gani, kuna mifugo mingi sana kule Wizara haijafika kutambua shida hii ya mifugo kule. Kuna vuguvugu la magongano haya kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu mifugo ina thamani, lakini chakula pia kina thamani. Sasa unapohamisha mifugo kutoka eneo moja; kutoa tatizo mahali na kupeleka eneo lingine, ni sawasawa na kidonda, unakitoa mguuni, unakihamishia tumboni, kitakuua tu. Kidonda lazima ukitibie. Kwa hiyo, lazima tutafute utaratibu wa kutibu hili tatizo kuliko kukihamisha kidonda mguuni ukakiweka tumboni, kitakuua tu. Sasa Serikali au mamlaka ya mkoa fulani inapotuhamishia sisi tatizo, kama wao wana ugomvi kati ya wakulima na wafugaji, wanatuhamishia sisi ambao tulikuwa hatuyaelewi hayo, sasa wanatuhamishia tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Wizara ya TAMISEMI na Ardhi washirikiane waone jinsi gani ya kuwagawia maeneo wafugaji wasije wakaingiliana na wakulima ili sisi tuendelee kuzalisha chakula, tuendelee kupata maslahi yetu na kuendelea kuweka usalama wa chakula katika nchi yetu. Sisi sasa ndiyo watunga Sheria katika Bunge hili. Ni wakati sahihi sasa wa kuweka utaratibu na mkakati endelevu utakaowezesha wafugaji na wakulima kufanya shughuli zao bila migongano yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo letu pia wafugaji wanaingia katika hifadhi. Kule tuna Hifadhi za Jamii na Jifadhi ya Taifa. Hifadhi ya Jamii WMAs zile tuliziweka kwa ajili ya kuhifadhi, kwa maana nyingine sisi ni wakulima na wahifadhi. Katika maeneo yale ya uhifadhi wa WMA, wakulima tulikuwa tunawazuia kabisa wasiingie kule, wakiingia wanapata adhabu kali sana. Sasa wafugaji ndio wameingia huko. Wakulima wanauliza, sisi mlikuwa mnatuzuia, wafugaji mbona wamekaa kwenye hifadhi na wanatuharibia vyanzo vya maji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetengeneza miundombinu ya umwagiliaji, lakini wafugaji wanaenda kwenye vyanzo vya maji kutumia maji yale. Kwa hiyo, kazi yetu ya kilimo inakosa maji wakati wa kiangazi, tunashindwa kufanya kazi yetu. Kwa hiyo, ni jambo ambalo Serikali lazima ije Namtumbo, ije Mkoa wa Ruvuma kuangalia shida hii, ni kubwa. Tusingoje mpaka watu waanze kuuana kama Morogoro ndiyo Serikali ianze kuingia pale. Tunawaomba sana Serikali ije kuangalia tatizo hili tulionalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 13 Novemba, 2020 wakati anafungua Bunge hili la 12 Marehemu Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli alisema, Serikali itaongeza hekta kufikia milioni sita kutoka 2,788,000/= kwa ajili ya maeneo ya wafugaji, malisho na maji. Serikali mmefikia hatua gani katika hilo? Alisema mwaka 2020 tarehe 13 Novemba; Serikali ni ile ile Serikali ya Awamu na Sita, mama alipokuja alisema, “Kazi Iendelee.” Kwa hiyo, moja ya kazi inayoendelea ni hii. Nawaomba sana Wizara mhakikishe kwamba tunatenga maeneo ili wasiingiliane wakulima na wafugaji, tuishi salama. Sisi wote ni Watanzania, lakini lazima tuwa-guide hawa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara katika ukusasa wa 47 imesema, Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imetenga jumla ya hekta 128,000 kwa mwaka huu na Mkoa wa Ruvuma umetengewa hekta 1,696 basi, kati ya 128,000 na kuna ng’ombe hatari huko. Ng’ombe wote waliokuwa huko kama sehemu hizi ambazo migogoro imetulia, ndiyo ng’ombe wote wale wamekuja Namtumbo Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana mje mtuangalie. Mkoa wa Ruvuma umetengewa hekta 1,600 kwa ajili ya wakulima. Tunawaomba mwingiliano huu kati ya sekta ya maliasili, wana maeneo makubwa; ardhi, mifugo, TAMISEMI, mkae pamoja mtupangie ili hao wafugaji wapewe maeneo, wasiingiliane na wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu mdogo katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri Mbarouk Mbarouk, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya na wamefanya kazi nzuri katika kutekeleza majukumu yao katika Wizara hii, katika kusimamia na kuratibu masuala ya uhusiano wa kimataifa kati ya nchi yetu ya Tanzania na nchi nyingine duniani na kwa kumshauri vyema Rais wetu katika kazi anayofanya ya diplomasia ya uchumi na ya siasa duniani na kwa ushauri wao mzuri mpaka wamefanya Rais wetu katika kipindi cha miezi 13 na nusu ameweza kutangazwa na gazeti pia la Times kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri katika wale 100. Na inaelezwa katika vyombo vya habari kwamba kwa mara ya mwisho Gazeti la Times ambalo lina miaka 99 lilianzishwa mwaka 1923 lilimtangaza Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa kiongozi mashuhuri mwaka 1964 miaka 58 iliyopita, mwaka niliozaliwa mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika kipindi cha miezi 13 na nusu Rais wetu amefanya kazi nzuri sana na mpaka ameonekana duniani anafaa kupata nafasi hiyo. Ni jukumu letu sisi kuwa proud na Rais wetu na tuendelee kumpongeza sana Rais wetu katika eneo hilo.

Ushauri wangu naomba muendelee kama Wizara kusimamia kwa umakini pia jukumu lenu la kuratibu masuala ya mikataba na makubaliano ya kimataifa, lakini pia muendelee kuratibu biashara ya kimataifa na diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 ukurasa wa 184 imesisitiza kuhusu diplomasia ya siasa na ya uchumi. Tumeona Rais wetu amehudhuria mikutano mingi ya kimataifa na kikanda katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kuifungua nchi yetu diplomasia ya kiuchumi. Mimi ushauri wangu naomba wananchi wote tuendelee kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan, Chifu Hangaya kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuiunganisha nchi yetu na mataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu siyo kisiwa, nchi yetu inahitaji kujumuika pamoja na nchi za kimataifa na nchi za kimataifa pia zinahitaji nchi yetu. Hivyo ushauri wangu pia kwa kuwa Rais anatekeleza kwa vitendo kazi zilizoainishwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni muhimu kwa Wizara zingine pia katika majukumu yao yaangalie pia mambo ya diplomasia ya uchumi. Tunafahamu diplomasia ya uchumi tumeipa Wizara hii ndiyo jukumu lake, lakini kuna umuhimu wa sekta zinazoambatana na uzalishaji mali kwa mfano za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, utalii na huduma, nishati na madini, Wizara zake pamoja na Kamati zake zinazozishauri na kuzisimamia Wizara hizi kuwa na mpango mkakati wa pamoja wa kufanikisha mahitaji ya masoko haya ya nje ambayo Wizara hii inayafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii tumewapa Mabalozi na ni kweli wanaifanya kazi hii, lakini bila ushirikiano wa sekta zingine wakileta wateja kwa ajili ya masoko yao tunaweza kukawa kuna ugumu.

Mimi nitawapa mfano mmoja tu mfupi, katika Balozi yetu ya Misri mwaka jana ilitafuta soko la viungo vya ndani kama hiliki, mdalasini, pilipili mtama na kadhalika, angalau tani tano ziwe zinasafirishwa kwenda Misri kwa mwezi. Lakini soko lake lilikuwa taabu sana kupata bidhaa zile, maana yake ni kwamba wazalishaji walikuwa hawajaandaliwa, sekta husika ilikuwa bado haijajiandaa.

Sasa tunaomba sana huo ni mfano mmoja, sisi tumesema katika mifugo tuna ng’ombe milioni 36, sasa tuandae wafugaji wetu wasiwe wachungaji tu, wawe pia wanajiandaa kibiashara kwa ajili ya soko la nje. Lakini pia mazao yetu ya kilimo kama mfano niliyoutolea hapa tuwaandae kifikra, tuwape elimu ya soko hili la nje ili tuhakikishe kwamba wanapozalisha wazalishe kwa masoko ya nje, soko la ndani na soko la nje ili waweze kufahamu taratibu ya masoko ya kikanda na masoko ya kimataifa. Kwa hiyo ni muhimu sana sekta hizi zingine tusichoke kutoa elimu na kuwafunza wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye uvuvi pia tuna bahari kubwa, nakumbuka miaka ya nyuma kuna meli zilikamatwa zinazokuja kuvua katika eneo letu la bahari kuu. Hivyo hivyo maana yake ni kwamba tuna samaki wa kutosha katika soko la nje. Kwa hiyo, ni muhimu pia tuangalie eneo hili hapa la uvuvi wa bahari kuu yetu na kuweza kuzungumza vizuri na hao wanaohitaji samaki wetu ili tuweze kupata soko na kuweza kuuza katika soko la kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu ulikuwa mdogo huo wa diplomasia ya uchumi, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, naomba uzingatie ushauri uliotolewa na Wabunge katika maeneo mbalimbali ili muende kuyafanyia kazi na tunaomba mzingatie pia ushauri tulioutoa na Kamati. Tutaendelea kushirikiana na ninyi kuhakikisha tunaisogeza mbele nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa. Kwanza naungana mkono na wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wataalam wote wa Wizara na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, EWURA na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wizara kwa maana ya Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Waziri kwa dhamira ya dhati ya kuongeza nguvu ya umeme na usambazaji wa umeme na utayarishaji, kuanzisha umeme katika maeneo mbalimbali ambayo kwa ujumla wake watakaoweza kuzalisha katika mwaka huu bajeti 2022/2023 megawatts 1,466 lakini zilizopo mbioni kwenye kukamilika ni megawatts karibu 2,380 ambayo ni Nyerere Hydro power, Rusumo megawatts 80 na Kinyerezi 185. Jumla yake zikikamilika na kwa sasa tuna megawatts 1,694 tunazozalisha kwa maji na gesi na biomass megawatts 1,694, jumla yake tutakuwa na megawatts 4,075.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tulivyo megawatts 1,694 na matumizi ya juu kabisa ya umeme nchini ni megawatts 1,335. Kwa hiyo, hapa tukijumlisha na miradi hii iliyopo na ukaenda kukamilika nadhani mwishoni mwa mwaka huu na mwakani tutakuwa na megawatts 4,075, lakini tutakuwa na surplus ya umeme ya megawatts 2,740. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu, sasa hivi tukishakamilisha hii miradi tu-concentrate katika kazi ya kusambaza kwa maana ya kusafirisha na kusambaza umeme na ile kufanya ile kazi ya National Grid Stabilization Project. Tukishamaliza miradi hii ya kuzalisha umeme, tutakuwa na megawatts 4,755, fedha nyingi tuzielekeze huko kwenye kusafirisha, kusambaza na stabilization za grid kwa sababu tutakuwa na surplus ya 2,740. Kwa hiyo, nadhani sasa hivi tukiendelea na concentration ya eneo hili itatusaidia sana kuwafikia wananchi vijijini ili waweze kufikia vitongoji vile tu-concentrate kwenye kukopa kwenye umeme wa kusambaza kwa wananchi vijijini badala ya kuendelea ku-invest kwenye uzalishaji wa umeme kwa sababu tutakuwa na surplus kubwa ya umeme katika kipindi hiki mpaka hapo tukiona hitaji linazidi kuongezeka basi tuendelee pamoja na kwamba policy or electric supply industry reform ile strategic road map inatutaka mpaka 2025 tuwe tunazalisha megawatts 10,000, lakini kwa sasa hivi mimi nadhani tukishafika hapo tu-concentrate na usambazaji na stabilization ya umeme vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, namshukuru Waziri walivyoleta timu yao hapa na nikaenda kuzungumza nao na wakanielewa, tuna proposal ya additional villages ambavyo vilirukwa katika vijiji vyetu na maeneo, tuna maeneo ambayo niliyasema ya maji. Serikali ina-invest fedha nyingi sana kwenye vituo vya maji, kwa maana visima kwenye vyanzo vya maji, lakini hakuna umeme katika vile vyanzo vya maji, tunatumia nishati ya mafuta ambayo ni very expensive. Kwa sasa hivi katika vijiji vya kwangu kule kwa mfano Ligunga, Lusewa wanalalamika na wanagoma kulipia kwa sababu wanashindwa kumudu gharama ya mafuta ili kusukuma maji yaweze kusambazwa. Kwa hiyo, ni vyema Serikali waka-concentrate sasa hivi kupeleka umeme katika maeneo ya vyanzo vya maji, kwenye vitongoji vyenye shule, zahanati na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwangu na vijiji na maeneo ya Ligunga pale nilishaeleza nilikubaliwa kwamba utashushwa umeme, kuna Sasawala Sekondari ambako kuna water pump pia, kuna eneo la Kijiji Zanzibar, Mchanjira, Likuwi Water pump, Selous Camp, Selous Sekondari, Vitongoji vya Mfuate, Rukimwa na Semu Zahanati, Magazine Sekondari lakini pia tuna Kituo cha Jeshi pale hakina umeme na kuna sehemu wana pump nazo hakuna umeme. Kwa hiyo, tutashukuru sana maombi yangu yale yakienda kutekelezwa ili tuweze kufanya kazi yetu ikiwa njema ya kusambaza maji na wapate huduma iliyo bora ya umeme. Nina imani sana na Waziri na Naibu Waziri kwa ubunifu wao, usimamizi wa kazi zao, tunaamini tutafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, sisi katika East Afrika hapa kwenye suala la mafuta, Uganda mafuta wao kwa bei ya Tanzania ni Sh.3,468, Kenya baada ya ku-subsidize ikashuka mpaka Sh.3,001, sisi Tanzania Sh.3,148 na leo hii bei imeshuka naamini itakuwa imefika 3,000 kwa bei. Kwa hiyo, tupo vizuri na hii crisis iko dunia nzima, tuendelee kuwa wavumilivu, naamini kabisa Waziri na timu yake na EWURA wataendelea kuratibu vizuri suala hili la mafuta kwa nchi yetu. Hata hivyo, lazima tumshukuru Rais wetu kukubali kutoa bilioni 100 ambayo leo hii hapa kwetu bei imeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tuendelee kuwa wavumilivu na tukiamini kwamba Serikali yetu imara ipo na inawajali wananchi na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunasimamia vizuri bei hizi za mafuta. Kwa kushuka kwa bei ya leo naamini katika nchi za Afrika Mashariki tutakuwa chini zaidi. Kwa hiyo, nawaomba sana Wizara, Mheshimiwa Waziri waendelee kusimamia hivyo hivyo, waendelee kusimamia ule mfumo wa bulk procurement ambao unatuhakikishia kuwa na mafuta ya kutosha katika mwezi mzima na kidogo na tunaweza tukawauzia na wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ulikuwa huo, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, kwa kuwasilisha hotuba zao zote mbili hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba niseme, kiongozi mzuri hajitengenezei ubinafsi. Narudia, kiongozi mzuri yeyote duniani hajitengenezei ubinafsi, bali anatengeneza mambo ya kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo kwa watu anaowaongoza na kuleta legacy. Sasa hii imejidhihirisha kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutengeneza na kuwafikia wananchi wa kawaida vijijini. Kuwatengenezea huduma za kijamii, shule, afya, maji na barabara na anatengeneza legacy kwa kuwafikia wananchi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anatengeneza shule na tumeona wote katika kila jimbo madarasa yamejengwa vizuri, anajenga vituo vya afya na hospitali. Naamini kwamba ukitaka kumfikia mwananchi wa kawaida maskini kijijini, wape elimu watoto wake. Ukitaka kufikia familia maskini kijijini, wape mazingira bora ya afya katika maeneo yao. Haya ndiyo anayoyafanya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi kwenye hoja, kwenye suala la Mpango ulio mbele yetu. Uchumi duniani unapodorora unaathiri pia Taifa letu. Tunaambiwa sasa hivi utaathiri upatikanaji wa fedha za mikopo, kupanda kwa riba ya mikopo huko duniani na uwezekano wa kupungua au kukosa misaada kutoka katika nchi hizo. Nchi hizo marafiki zetu kihistoria, ambao wamekuwa wakitupa misaada na mikopo, Marekani, Japan, Uingereza, Canada, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Hispania na maeneo mengine ya Ulaya; kiwango cha ukuaji wa uchumi wao kinatarajia kushuka kutoka asilimia 2.6 mwaka 2022 mpaka asilimia 1.5 mwaka huu 2023, lakini ukuaji wa uchumi utaendelea kushuka tena mwaka 2024 mpaka asilimia 1.4. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo yote lazima tuyatafsiri kwa kukaza mkanda na kujiimarisha katika kazi zetu na kuona mpango wetu huu unajielekeza katika kukabiliana na hali hii ya mabadiliko ya kudorora kwa uchumi duniani hasa kwa nchi hizi nguli za magharibi. Kwa kuwa watu hawa tumekuwa na mahusiano nao mazuri, ya mikopo na misaada mbalimbali na sasa riba kwao zimepanda za mabenki yao, lakini pia hali ya ukuaji wa uchumi wao umeshuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie, je, ni nini itakuwa athari yake kwetu sisi kama Tanzania, lakini tukikopa pia kwa wakati huu athari yake itakuwa nini kwa riba kubwa kwa nchi zile? Mpango utuoneshe maeneo yale ya misaada kutoka kwao tutakayokosa katika kipindi hiki yatatuathiri kiasi gani na tumejipangaje kuziba pengo hilo la misaada ambayo tunaipata kutoka kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, tuongeze uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa kilimo, lakini bidhaa mbalimbali zitakazoongezwa thamani kuuza nje. Tuongeze thamani katika bidhaa mbalimbali, nitatolea mfano katika mazao haya ya biashara ya kilimo, lakini kutokana na muda nitalisemea moja la tumbaku. Zao la Tumbaku limekuwa ni zao ambalo linauzwa kwa dola. Kwanza ni zao la kimkataba, mkulima kabla hajaingia shambani, unafanika mkataba wa ununuzi na ununuzi ule ni kwa dola lakini zao hili pia lilishanunuliwa kwa mkulima kwa dola, linaenda kuwa processed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda hapa vya ku-process tumbaku, semi-product ambao wanafanya blending ya ile tumbaku. Ikishafanyiwa blending, asilimia kadhaa kubwa inauzwa nje ikiwa imekuwa processed kiasi kwa kufanyiwa blending. Inauzwa nje kwa dola lakini asilimia nyingine inauzwa ndani katika viwanda vya ndani, inatengeneza final product ambayo ni sigara. Pia, nayo hiyo sigara inauzwa nyingi asilimia kubwa nje kwa dola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi nchi yetu sasa hivi tuna uhaba wa dora na tunakazania sana tupate dora. Tulitazame sana zao hili. Zao hili ni zao la kimkataba na kwa mwaka huu tu limeuza zaidi ya dola milioni 400. Takwimu zaidi sina za uhakika, lakini Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, watafute takwimu vizuri. Mwaka huu tumeuza tumbaku kwa dola nyingi, lakini mwaka huu pia msimu unoakuja tumeingia mkataba wa uzalishaji wa tani nyingi zaidi za tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu hili zao tuliangalie kwa karibu sana, kwa sababu kama nilivyosema, linauzwa kwa dola kwa mkulima, linapokuwa processed linauzwa nje kwa dola, lakini pia linapokuwa processed hapa na kupata final product ya sigara nyingine kwa wingi, zinauzwa nje kwa dola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachoomba, tuliangalie hili zao katika uzalishaji wake. Leo hii zao hili, mbolea yake inalipiwa ruzuku. NPK hailipiwi ruzuku, inauzwa kwa bei ghali Sh.160,000 mpaka Sh.170,000, lakini mbolea nyingine zozote za mazao, zinapewa ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, Serikali itoe ruzuku katika zao la hili la tumbaku ili tuweze kupata dola nyingi zaidi. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, aliwahi kutuambia hapa Bungeni, ukitaka kula, lazima uliwe. Kwa hiyo, haya madola yote wanayoyasema haya ili Serikali iyapate mengi zaidi, ni lazima tuliwe. Lazima tutoe ruzuku ya NPK kwa zao la tumbaku. Pia, naomba mpango ujielekeze kwenye hilo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunashukuru sana mpango hapa umetueleza katika Aya ya 31, Ukurasa wa 14, mafanikio yale. Serikali imetoa ruzuku katika mazao ya kilimo. Pia, ongezeko la uzalishaji wa mazao, limeongezeka kutoka tani milioni 17 mpaka 20, lakini pia wameimarisha masoko. Wameyasema wazi NFRA wamenunua mazao. Tunashukuru sana imenunua kweli na mazao mchanganyiko wamenunua NFRA, lakini bado wakulima walikuwa wanawadai Serikali bilioni 40. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ni kipindi cha wakulima kwenda kulima na kilimo kinataka maandalizi na maandalizi ni fedha. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali, nashukuru mpaka Ijumaa Serikali imeshalipa bilioni 19 kwa wakulima waliouza mahindi kupitia NFRA. Sisi Mkoa wa Ruvuma tunadai bilioni 9.9 na tumeshalipwa bilioni 4.0, bado wakulima wanadai bilioni 5.9 (Bilioni tano na milioni mia tisa). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kupitia NFRA iwalipe wakulima hawa warudi tena shambani waweze kuzalisha, mazao yaweze kuongezeka. Kwa hiyo, tunaomba sana hili walichukue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine. Mipango yote hii tunayoifanya, yote inahitaji usalama. Ni lazima eneo la usalama tulizingatie sana katika mipango yetu ya Taifa. Tuhakikishe kwanza tunalinda mifumo yetu ya fedha. Eneo hili la usalama tuhakikishe tunalinda mifumo yetu ya fedha kwani sasa hivi kumekuwa na ushamirishaji mkubwa sana wa wizi kupitia mifumo yetu ya fedha za Serikali. Kwa hiyo, lazima kuwe na fedha za ziada ambazo zitakuwa zinalinda wakati wowote kubadilisha mifumo ili kukabiliana na wizi huu wa fedha za Serikali kupitia mifumo. Kwa hiyo, tunaomba sana uhalifu wa mifumo yetu ya Fedha za Serikali na mwingine umeongezeka sasa hivi ambao udhibiti wake… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa…

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, lakini naomba unipe nusu dakika. Mifumo ambayo udhibiti na ufuatiliaji wake wa mifumo hii, unahitaji teknolojia na teknolojia inahitaji fedha. Kwa hiyo, sasa katika mpango huu ni lazima tuweke fedha za kulinda mifumo yetu kwa ajili ya usalama wa fedha za Serikali na kuzuia hawa wahalifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
The Fire and Rescue Force (Amendment) Bill, 2021
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza naomba niungane mkono na Kamati kwa mapendekezo yote ambayo yametolewa naungana nayo mkono.

Pia ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake lakini pia kwa kukubali mapendekezo ya Kamati ya Muswada huu, naomba niende kwenye kifungu cha 6 cha Muswada ambao una-amend kifungu cha 13 katika ile principal act ambayo inataka kutoa adhabu kwa wale ambao watazichezea zile hydrant.

Mheshimiwa Spka, hii naungana nayo mkono kwasababu ni muhimu sana wananchi wafahamu umuhimu wa miundombinu hii ya maji ya kuzimia moto, hasa wakati inapotokea majanga kama yaliyotokea hivi karibuni Kariakoo, miundombinu mingi hizi fire hydrant zilikuwa hazionekani zilipo zimepotea.

Mheshimiwa Spika, pamoja na adhabu iliyowekwa ili kuwakumbusha wananchi umuhimu wa hii hydrant lakini ninaishukuru sana Serikali katika kile principle act haikuondoa kile kifungu cha 13 (1) ambacho kinaleta wajibu kwa jeshi letu la fire la kutunza pia hizi hydrant zilizopo, kuweka tunasema kwamba the force shall provide and maintain or course to be provided and maintain such fire Hydrants and other water installations, huo ni wajibu kwa fire na wajibu
huu nao unahitaji gharama pia kwa jeshi letu la Fire kwa hiyo hapa leo kwakuwa tupo na Serikali inatusikiliza ushauri wangu kwa Serikali pia.

Mheshimiwa Spika, katika mipango yetu ya bajeti tuiangalie sana pia Jeshi la Fire kuipa fedha za ku-maintain na ku-install hivi fire hydrants lakini pia suala hili pia ni mtambuka miundombinu hii ya fire hydrants inaharibiwa bia wakati tunatengeneza barabara wenzetu wa TARURA, TANROADS wanaifukia kwa hiyo ni wajibu nao pia kutambua hii miundombinu hii inakuwepo…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa!

SPIKA: Mheshimiwa Vita unapewa taarifa na Mheshimiwa Sophia.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba ni kweli anachozungumza kwamba jeshi hili linahitaji Serikali iwekeze zaidi ni jeshi ambalo katika bajeti wanapoomba bajeti ni jeshi ambalo linapata chini ya kiwango cha bajeti walichoomba, na hata ukiangalia mavazi yao tu hawezi kuwa na ujasiri wa kufanya kazi kama Jeshi

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninakuunga mkono kwamba Serikali ilitazame jeshi hili linapoitwa jeshi liwe kama majeshi mengine na hii Waziri husika nafikiri unahaja una watoto watatu hakikisha huyu mtoto wa tatu na yeye anakuwa kama wale watoto wengine wawili, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kamishna General yupo anasikia, Mheshimiwa Sophia anasema hata ile uniform yenu ebu tafuteni nyingine mkishaitwa jeshi sasa mbadilike na kikosi mje kivingine Mheshimiwa Vita Kawawa unapokea taarifa hiyo (Kicheko)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, naipokea vizuri kabisa asilimia 100 taarifa hiyo, kwa maana ya kwamba miundombinu pia inaharibika kwa wenzetu wanapotengeneza barabara kwa hiyo ushauri wangu ni kwamba wanapotengeneza barabara pia wawe wanawasiliana na Fire lakini pia na Mamlaka za kutengeneza maji.

Mheshimiwa Spika, leo hii zinapungua sana Fire Hydrants, kwa mfano Dar es Salaam pale, nitatoa mfano wa Dar es Salaam barabara kutoka Morocco mpaka Mwenge kuna Fire Hydrant mbili na pale kuna maghorofa yapo mengi na wameweka hizi wakati wanatengeneza barabara, lakini Fire hydrant mbili pale pana not less than 3 kilometers kutoka Morocco mpaka Mwenge. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Vita samahani endelea kusimama hivi Makatibu Bungeni hapa kuna Fire Hydrant tusije tukaungua hapa. Mheshimiwa Vita endelea na mchango wako. (Makofi/Kicheko)

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ziko mbili kwamba kwa mujibu wataratibu kwamba kila hatua au mita 100 kunatakiwa kuwe na Fire hydrants kwa hiyo angalu pale kwenye kilometa 3 zingekuwa kama 10 hivi angalau zingesaidia, kwa hiyo ni muhimu sana kuwepo ndio maana ninasisitiza wenzetu wa Jeshi la Zimamoto waongezewe fedha kwa ajili ya kuweza kuziweka hizi na kuzi- maintain hizi Fire Hydrants. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu kusema kweli lingine lilikuwa kwanini ninaelezea pia suala hili la Jeshi la Zimamoto kuongezewa fedha kwa sababu moja wana upungufu pia wa rasilimali watu, lakini pia vifaa na mafunzo, tunalifanya kuwa jeshi kwa hiyo hatuna budi pia waongezewe rasilimali watu, waongezewe vifaa, miundombinu kama vile magari ya Fire, magari ya Fire toka mwaka 2007 ndio walipewa magari mapya toka nje leo hii wana magari hapa Dodoma hapa nadhani tuna gari moja la Fire hapa lingine sijui tuliazimishwa kutoka Iringa. Kwa hiyo, yaani kuna haja kabisa mahsusi ya kuwekewa fedha za kununuliwa vifaa au miundombinu ya kuzima moto wenzetu hawa wa Fire.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kusomesha wataalam wa Fire zaidi ili waweze kujua kazi yao vizuri vijana hao wengine wapya wanaopelekwa kwa hiyo tunaomba sana kwa sababu hapa sasa hivi tuna chuo pia cha Fire kinafundisha basic hatuna kile cha advance courses ambazo wanaweza wakawa wanapata utaalam wa kutosha kwa hiyo tusaidie Serikali iangalie maeneo hayo yote ya kuwapa elimu, rasilimaliwatu, lakini pia vifaa kwa ajili ya kuweza kusaidia katika maeneo ya uzimaji moto.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha na ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)