Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Vincent Paul Mbogo (12 total)

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri. Ukanda wa Ziwa Tanganyika akina mama wengi wanakufa kwa kutokupata huduma za afya, hasa upande wa ambulance boat kwa sababu kule miundombinu ya barabara hakuna, usafiri wao ni ndani ya maji na vijiji vipo vingi sana ndani ya Ziwa Tanganyika ambavyo vinatumia usafiri wa boti. Ni lini Serikali itapeleka ambulance boat kwa ajili ya kuokoa akina mama wajawazito? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika mwambao ule wa Ziwa Tanganyika kuna changamoto ya usafiri pale ambapo tunapata dharura za wagonjwa na hususan akina mama wajawazito ambao wanahitaji kwenda kwenye vituo vya rufaa kwa ajili ya huduma za upasuaji. Serikali imeendelea kuweka mipango ya kuhakikisha kwamba maeneo hayo ambayo yana changamoto kubwa za usafiri, hasa ambulance kwa maana ya ambulance boats, tunaendelea kuangalia utaratibu mzuri zaidi wa kutenga fedha kadri zitakavyokuwa zinapatikana ili tuwezeshe ufanisi wa rufaa katika maeneo hayo ili tuendelee kuokoa maisha ya wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo kwamba suala hili kama Serikali tunalichukua, tutalifanyia kazi na kuona namna bora zaidi ya kupata ambulance boat ili iweze kusaidia wananchi katika Jimbo la Nkasi Kusini. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkasi ina kadiriwa na changamoto kubwa sana ya maji, ni lini Seikali itatoa maji Ziwa Tanganyika ambacho ndiko chanzo kikuu cha uhakika kuweza kutatua changamoto Wilayani Nkasi?

Swali la pili; Wilaya ya Nkasi katika Tarafa ya Nkate upo mradi wa maji ambao umekaa muda mrefu sana Tarafa ya Nkate ambao unahudumia vijiji vya Ntuchi, Ntemba, Siriofu na Ifundwa, mradi huu Mkandarasi hajalipwa ili aweze kumaliza mradi huu na ipo kesi ambayo anatuhumiwa mahakamani, naomba Wizara hii iweze kushughulikia kesi ya Mheshimiwa Felix Mkandarasi atoke ili aweze kumalizia mradi huu umekaa muda mrefu wananchi wanahangaika na maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, lini Serikali itatumia maji ya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya kulisha katika Mji wa Nkasi wote. Serikali ya Awamu ya Sita katika vipaumbele vyake cha kwanza ni kuhakikisha kumtua ndoo kichwani mwanamama, kwa hivyo nataka nimhakikishie kazi kubwa imefanyika katika maji eneo la Ziwa Victoria kuyatoa na kuyapeleka Mikoa mbalimbali ikiwemo Tabora na kwingineko, kwa sasa kwenye bajeti hii ya 2021/2022 Serikali inaendelea kutafuta fursa ya kuona namna ya kuweza kusaidia na kwa hivyo hili la Ziwa Victoria naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge linaweza kuwa ni moja ya sababu ya kuweza kulifanyia kazi ili kuondosha hii adha inayowapata wananchi wa Nkasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili juu ya mradi uliokwama wa Kata ya Nkate jambo hili naomba nilichukue na mara baada ya kikao hiki kuisha tuje tulizungumze tulielewe tatizo lake ni nini na baadaye tuweze kulitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Uchumi wa blue unafanana na mazingira mazuri kabisa sawa sawa na Ziwa Tanganyika. Je, Serikali ina mpango gani kama inavyofanya kwenye mazingira ya Bahari ya Hindi rasilimali zinavyopatikana baharini, vivyo hivyo na rasilimali zinapatikana Ziwa Tanganyika. Ni lini Serikali mnakuja na mkakati maalum swali namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali namba mbili dagaa Ziwa Tanganyika ni zao la kipekee ambalo ndio linasababisha uchumi wa Mikoa mitatu Kigoma, Rukwa na Tanganyika. Serikali ina mpango gani na zao hili na pia kwa sababu linavuliwa ndani ya Mikoa mitatu, libadilishwe jina sio dagaa wa Kigoma waitwe dagaa wa Ziwa Tanganyika ili kuweza kutangaza Ziwa Tanganyika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua kwanza fursa hii, kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza naomba kwa namna ya kipekee nimpongeze yeye na Wabunge wote wa Mkoa wa Kigoma, Katavi na Rukwa kwa kuona umuhimu wa Ziwa Tanganyika na mazao yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan, moja ya mkakati ni hili la uchumi wa blue na ni kipaumbele kama Taifa letu na ndio maana katika bajeti ya mwaka huu, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka jumla ya kiasi cha shilingi milioni 800. Kwa kusudio la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunafanya stock assessment. Ziwa Tanganyika halijawahi kufanyiwa stock assessment kwa mara ya kwanza sasa tunakwenda kufanya stock assessment, ya kujua ni kiasi gani cha Samaki migebuka na dagaa tulionao katika eneo lile. Hii itatusaidia sana kwenye mkakati wa uchumi wa blue, ili kuweza kuvutia uwekezaji na watu kuweza kujua kwamba akiweka fedha yake itakwenda kumlipa kwa kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hili la pili la ushauri la kwa nini dagaa hawa wasiitwe dagaa wa Ziwa Tanganyika? Nataka nimhakikishie yeye na Waheshimiwa Wabunge wote tumeuchukua ushauri huu. Isipokuwa kibiashara wewe unafahamu ya kwamba katika marketing strategy dagaa hili limetambulika kwa miaka mingi sana kama dagaa la Kigoma.

Kwa hiyo, ikiwapendeza sisi tutakaa nao tutashauriana nao badala ya kuwa dagaa la Kigoma, tutasema kwamba liitwe dagaa la Tanganyika. Kwa dhumuni jema lile la kwamba wanavuliwa kwenye Mikoa yote mitatu, Rukwa, Katavi na Kigoma kwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na dagaa hizi ni mali sana hazijawahi kushuka bei hivi sasa inauzwa mpaka shilingi 30,000 kwa kilo na haijawahi kushuka chini ya shilingi 20,000. Ahsante sana.
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina swali moja la nyongeza. Jimbo la Nkasi Kusini Tarara ya Kate, huduma za kimahakama wanatumia godown; upande mmoja magunia, upande mmoja Mahakama inaendelea.

Mheshimiwa Spika, nilimpigia simu Mheshimiwa Naibu Waziri, akafika, tukatembelea Tarafa ya Kate yeye mwenyewe akajionea mazingira magumu, jinsi gani huduma za haki za kimahakama zinatolewa katika mazingira ambayo siyo mazuri. Ni godown, wakiweka dawa kwenye mazao, Mahakama haikaliki, ni harufu tupu: Je, ni lini serikali inakuja kujenga jengo la kisasa Tarafa ya Kate? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa
Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Mbogo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana masuala haya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupata eneo sahihi la kupata huduma za haki. Ni kweli kabisa nilitembelea Kate, na nilikuta ni kweli wanatumia godown ambalo ndiyo linakuwa kama Mahakama.

Mheshimiwa Spika, vile vile nilimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili jambo tumelichukua na kwa sasa hivi katika ule mpango kazi ambao Mahakama imejiwekea, tunamwahidi Mheshimiwa Mbunge, katika kipindi hiki tunachoendelea nacho mpaka kufika 2025, Makao Makuu yote ya Tarafa nchini tunakwenda kujenga majengo ya Mahakama ya Mwanzo. Kwa hiyo, kwa sababu Kate ni Tarafa, inaenda kupata upendeleo wa pekee katika kipindi kijacho cha fedha. Ahsante. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Nina swali moja;

Kwa kuwa robo tatu ya Pori Tengefu la Lwafi la Wilayani Nkasi halina wanyama na wananchi wameshaingia wanafanya shughuli zao za kiuchumi; na mipaka hiyo tangu 1948 kipindi cha ukoloni iliwekwa, lakini baadaye ikaja ikabadilishwa ikasogezwa kwa wananchi.

Je, Mhesimiwa Waziri haoni kuwa ni kukwamisha juhudi za wananchi wa Wilaya ya Nkasi wanaojitafutia riziki zao?

Je, ni lini tutakuja kupitia upya ili mipaka irekebishwe, wananchi wameongezeka ili wapate maeneo ya kulima? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vicent Mbogo, Mbunge wa Nkasi, akiwakilishwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wilaya ya Nkasi haina uhaba wa maeneo, isipokuwa kuna changamoto ya mtawanyiko. Wananchi wanaishi pale ambapo wanahitaji kukaa, kitu ambacho tunaipa mzigo Serikali kupeleka huduma kwa wananchi tukiendelea kuwaruhusu waendelee kutokomea kwenye maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoelekeza Serikali ni kwamba wananchi wapangwe kwa kuangalia matumizi bora ya ardhi ili kuwepo na miundombinu inayowezesha huduma bora za wananchi ziweze kuwafikia wananchi. Hili swali analolisema kwamba robo tatu ya Lwafi haina wanyama. Ili eneo lihifadhiwe vizuri na ili liwe na madhari nzuri ni pale tu ambapo litaachana na shughuli za kibinadamu. Ndiyo maana yale maeneo ambayo tunayatunza vizuri wanyama huwa wanarudi taratibu na uhifadhi unakuwa ni endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka niwaambie tu wananchi wa Nkasi kwamba maeneo ambayo tunayahifadhi mengine tunayachukua yakiwa hayastahili kuwa hifadhi; lakini yanapotunzwa kwa muda mrefu uoto wa asili unarudi, madhari inarudi na wananyama wanaanza kurudi. Kwa maana nyingine wanyama wanatoweka baada ya shughuli za kibinadamu kuingilia maeneo ya hifadhi. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa sababu niliomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Kala Kijiji cha Mpasa ambapo kuna biashara kubwa sana ya Samaki inafanyika. Ukanda wa Ziwa Tanganyika kuna uhalifu wa mara kwa mara hasa Kata ya Kizumbi;

Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha polisi Kata ya Kizumbi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwamba Mheshimiwa Mbogo amekuwa akitoa ushirikiano kwa Wizara yetu na wakati mwingine kupitia halmashauri yake amekuwa akitenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki. Nimuahidi tu, baada ya kumaliza kituo hiki kadri hali ya fedha itakavyoruhusu maeneo tete kama ya Kizumbi tutaweza pia kuyajengea kituo cha polisi ngazi ya kata. Nashukuru.
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Nina swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Nkasi Kusini lina idadi kubwa sana ya mifugo na wananchi wa Kata ya Ntuchi pamoja na Chala wameshaandaa maeneo ya ujenzi wa majosho. Je, ni lini Serikali itakuja kujenga majosho hayo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, natambua kazi kubwa anayoifanya katika ufuatiliaji wa kuhakikisha maeneo yake yanapata majosho pamoja na malambo. Kwa bahati nzuri tulishakaa ofisini na kukubaliana jambo hili kwamba, katika mwaka wa fedha kwa sababu tunaendelea na mazungumzo na Wizara ya Fedha, fedha itakayotoka tutapeleka katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha, ahsante sana.
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kijiji cha Londokazi, Kalundi na Ntalamila wana changamoto kubwa sana ya maji.

Je, ni lini Serikali itakwenda kuchimba visima ili kuondoa adha hiyo ya maji?

Swali la pili, Jimbo la Nkasi Kusini vipo vijiji karibia 20 mwambao mwa Ziwa Tanganyika ambavyo hakuna barabara na hata hii miradi ya maji na vifaa vinashindwa kufika kule, kwa hiyo wananchi wanaendelea kuteseka wanakunywa maji ya kwenye visima pamoja na mifugo. Je, ni lini na ni mpango gani Serikali kwa kushirikiana na TARURA waweze kuchonga maeneo hayo ili vifaa vya miradi ya maji iweze kufika katika vijiji hivyo ambavyo ni Msamba, Kilambo cha Mkolechi, Izinga, Mbwiza, Lyela, Kasanga, Kasapa, Lupata, Lyapinda, Ninde, Kapumpuli na Kilabu cha Mkolechi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vincent Mbogo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uchimbaji wa visima sasa hivi tayari gari liko kwenye mkoa wako na tutakuja kuchimba visima kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha. Vifaa vyetu kupitika katika barabara ambayo ni mbovu tutafanya mawasiliano na Wizara husika tutahakikisha mitambo ile inafika kwenye vijiji hivi na vijiji hivi vinaweza kuchimbiwa visima ili waweze kupata maji safi na salama na kufaidi ile azma ya Mama kumtua ndoo Mama kichwani. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Vijiji vya Lusembwa, Ng’undwe, Mlambo, Minza na Ifinga vinashindwa kupata huduma ya maji, miradi ya maji, mawasiliano pamoja na minara ya simu.

Je, ni lini Serikali itajenga barabara katika hivi vijiji ambavyo viko Kata ya Wampembe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kata ya Wampembe na Kata ya Kala kuna vilima ambavyo ni korofi, vinasababisha magari ya abiria kutopita; je, ni lini Serikali itajenga kwa zege katika vilima hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo, la kwanza, hii barabara ya Ng’undwe – Mlambo – Lusembwa – Mvinza na Ifinga vilivyokuwepo kwenye Kata hii ya Wampembe, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, barabara hizi zilikuwa bado hazijafunguliwa na kuingizwa kwenye mtandao wa TARURA. Hivyo basi, muda siyo mrefu Meneja wa TARURA Wilaya ya Nkasi atapita kufanya tathmini ya barabara hizi na kuona ni kiasi gani kinatakiwa kutengwa ili barabara hizi ziweze kuchongwa na greda, na kadiri miaka inavyoenda na fedha kuruhusu basi nazo ziweze kuanza kuwekewa changarawe ili wananchi waweze kupita wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu barabara inayounganisha Kala na Wampembe, kwamba ina vilima vingi, nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Meneja wa TARURA Nkasi, kuweza kufika katika barabara hii ya Kala na Wampembe na kuanza tathmini, na kuona ni kiasi gani kinahitajika kwa ajili ya kuweka zege katika vilima hivi ili barabara hizi ziweze kuwa zinapitika wakati wote wa mvua na hata kipindi ambacho hakuna mvua.
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, katika swali langu la msingi naomba kuongeza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Wampembe ina Kata Nne ambazo kuna biashara kubwa sana ya samaki ambayo inafanyika na nchi jirani hakuna soko. Je, ni lini Serikali itawajengea soko kwa ajili ya biashara zao za samaki Kata ya Wampembe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mimi ningemuomba Mheshimiwa Mbunge, kwanza tumalize soko la Chala halafu baada ya hapo kama vipaumbele vinavyofuatia, maana yake linalofuatia ni hilo eneo ambalo amelifikisha hapa Mheshimiwa Mbunge. Ahsante sana.

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuweza kuuliza swali nyonyeza, nina maswali mawili.

Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi yana changamoto kubwa sana ya maji, ni nini mpango wa kutoa maji Ziwa Tanganyika ambao unaanzia Kata ya Wampembe kupeleka maji Wilayani Nkasi ?

Swali la Pili, Vijiji vya Mwinza, Diela, Katenge, Lupata, Lyapinda, Kasanga Ndogo, Katenge, Msamba, wananchi wanaliwa na Mamba wanapofuata huduma ya maji. Je, ni lini kama Wizara mtakaa na Wizara ya Maliasili ili muainishe maeneno yale ambayo wananchi wanapata huduma ya maji muwawekee wavu ili wananchi wasiliendelee kuliwa na mamba? Kwani ndani ya mwaka mmoja wameliwa watu Kumi. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya Ziwa Tanganyika kupeleka maji Makao Makuu ya Wilaya. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, umefuatilia sana na tayari Wizara tunaendelea na taratibu za kuona kwamba Ziwa Tanganyika tunaweza kuleta maji pale na maji yawe ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wananchi kuliwa na mamba. Mheshimiwa Mbunge nakupa pole sana kwa wananchi kupata hii kadhia, tutalichukulia kwa umakini mkubwa kuhakikisha kwamba tunakutana na wenzetu wa Maliasili basi tuje tuweke hiyo mipaka ya kuhakikisha wananchi wanachota maji maeneo yenye usalama. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Nina maswali mawili ya nyongeza. Ziwa Tanganyika, Wilaya Nkasi hakuna vizimba hata kimoja . Ni lini Serikali mtapeleka vizimba Wilaya ya Nkasi hasa Jimbo la Nkasi Kusini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la namba mbili, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Bwawa la Kacheche la kunyweshea mifugo pamoja na ujenzi wa majosho mawili Chala B, Kata ya Chala pamoja na Kijiji cha Kitosi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza na hili la vizimba, tumeshatoa maelekeza kwamba mvuvi yeyote ama mwananchi yeyote ambaye ana shida na vizimba ama boti au nyenzo zozote zinazohusiana na uvuvi, aombe haraka iwezekanavyo milango ipo wazi kwa Watanzania wote. Kwa kweli Mheshimiwa Rais, ametufungulia njia kama mnavyokumbuka Tarehe 30, aligawa kule Mwanza vizimba na boti za kutosha na Wizara ipo katika mchakato wakutafuta vizimba vingine ili kuwagawia wananchi watakaohitaji kwa awamu ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuhamasisha Wananchi wake wenye uhitaji. Tupo tayari kupeleka Ziwa Tanganyika na tayari tumeshaanza Ziwa Victoria na kwa kweli vijana wote na wavuvi wote wenye shida na wenye uhitaji wa nyenzo za uvuvi Serikali ipo tayari kuwagawia. Ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili, kuhusiana na lini bwawa litakamilika na majosho. Hapa katikati tulisimama kidogo kwa sababu ya upatikanaji wa fedha. Mara tu Serikali itakapopata fedha tutakwenda kukamilisha ujenzi wa majosho hayo. Mheshimiwa Mbunge atakumbuka katika Wilaya yake tumemtengea jumla ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki katika eneo hilo. Tukapopata fedha nyingine tutakwenda kukamilisha ujenzi wa majosho hayo na mabwawa ambayo yapo katika Wilaya yake, ahsante. (Makofi)