MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge kutoka Kibaha Vijijini. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, najua TASAF ilianza awamu ya kwanza kwa kuwapatia walengwa miradi ya uwekezaji kama majengo mbalimbali zikiwemo kumbi za maonyesho. Katika Jimbo la Kibaha Vijijini, wazee walipewa mradi huu awamu ya kwanza; je, TASAF wana mkakati gani juu ya kuwafanyia ukarabati jengo ambalo walipewa katika awamu ya kwanza ambalo sasa limechakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia nafasi hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge, awamu ya kwanza ilijikita zaidi katika ujenzi wa miundombinu na si Kibaha Vijijini tu bali katika halmashauri nyingi sana katika nchi yetu ambazo majengo haya au miradi hii ilifanyika. Sasa baada ya awamu ya kwanza kuisha na kwenda awamu ya pili na sasa tuko awamu ya tatu phase II, ni kwamba majengo haya na miradi hii yote ilikabidhiwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri husika. Na ni wajibu wa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba wanatunza majengo haya na wasiwaachie tu wale walengwa peke yao; ni wajibu wa Wakurugenzi kuhakikisha sustainability ya miradi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kuelekea katika halmashauri yake na kuhakikisha tunakwenda kuangalia miradi hiyo na kuwaagiza Wakurugenzi ili kuhakikisha kunakuwa na sustainability.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)