Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Michael Constantino Mwakamo (13 total)

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Makofia kupitia Mlandizi hadi Vikumbulu Kisarawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Makofia – Mlandizi – Vikumbulu yenye urefu wa kilometa 135.97 ni barabara ya mkoa inayounganisha Wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uhakiki wa mali zitakazoathiriwa na mradi sehemu ya Makofia – Mlandizi – Maneromango yenye urefu wa kilometa 100 umekamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza baada ya kupata fedha ambazo Serikali inaendelea kutafuta.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara yangu inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika Mwaka huu wa Fedha wa 2020/21 jumla ya shilingi 1,524.000.07 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA - K.n.y. MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusambaza Matangazo ya Serikali kwa maana ya Government Notices au GN yanayoonesha mipaka ya Wilaya na Mikoa kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini; kKuunda vikundi kazi na kuvipeleka kwenye maeneo yenye migogoro ya mipaka ili kutatua migogoro; kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi nchini kwa kuhakikisha Vijiji, Kata na Wilaya zinaandaa na kutekeleza Mipango ya matumizi ya ardhi, kutoa elimu kwa umma kuhusu Sera na Sheria za ardhi, kusimamia upimaji wa viwanja na mashamba katika Halmashauri, kurasimisha makazi na kumilikisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watumishi waliostaafu kupata mafao yao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulianzishwa rasmi tarehe 1/ 8/2018 kwa Sheria Namba 2 ya Mwaka 2018. Mfuko huu ni matokeo ya kuunganisha mifuko minne ya awali (LAPF, GEPF, PPF na PSPF) ambayo ilikuwa ikihudumia watumishi mbalimbali wa Umma na kuufanya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kubaki ukihudumia sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati, mipango na utekelezaji wa Serikali katika kuhakikisha watumishi waliostaafu wanapata mafao yao kwa wakati ni kama ifuatayo: -

(i) Kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuweza kuwatambua wanachama wake na kulipa mafao stahiki pale wanapodai mafao;

(ii) Kulipa malimbikizo mbalimbali ya mafao ya wanachama yaliyopaswa kulipwa na mifuko iliyounganishwa na yale yaliyopokelewa kipindi ambacho mchakato wa kuunganisha mifuko huo ulikuwa unaendelea; na

(iii) Kuandaa ofisi mbalimbali nchini kote na kuweka misingi bora itakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wanachama wake ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati, waajiri wanakumbushwa kufuata kikamilifu utaratibu ulioainishwa katika Sheria namba 2 ya Mwaka 2018 ambapo inaelekeza ipasavyo maandalizi ya taarifa za wastaafu kabla ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifuko imeendelea kuboresha mifumo yake ambapo matarajio ni kuwa waajiri nao wafuate vizuri utaratibu ulioainishwa kisheria ili kupunguza ucheleweshaji wa kulipa mafao kwa wastaafu.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, ni Ranchi ngapi nchini zimeshawapokea wafugaji na kuwapatia nafasi ya kufuga kwenye Ranchi hizo kama Serikali ilivyotoa maelekezo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo Mbunge wa Kibaha Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imetekeleza maelekezo ya Serikali kwa kutenga jumla ya vitalu vya muda mrefu 116 katika Ranchi 11 za NARCO na kuzikodisha kwa wafugaji wadogo 116. Ranchi hizo ni Kikulula (Kagera) vitalu 2, Mabale (Kagera) vitalu 7, Kagoma (Kagera) vitalu 18, Kitengule (Kagera) vitalu 10, Missenyi (Kagera) vitalu 11, Mkata (Morogoro) vitalu 7, Dakawa (Morogoro) vitalu 2, Mzeri Hill (Tanga) vitalu 9, Usangu (Mbeya) vitalu 16, Kalambo (Rukwa) vitalu 13 na Uvinza (Kigoma) vitalu 21. Jumla ya eneo la vitalu hivi ni hekta 322,525.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kutatua migogoro ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi nchini hasa baada ya wafugaji kuondolewa kwenye hifadhi za misitu na mapori ya akiba, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ilianzisha utaratibu wa kugawa vitalu vya muda mfupi ambapo jumla ya vitalu 128 vimekodishwa kwa wafugaji wadogo 128 kutoka katika Ranchi 10 za NARCO. Ahsante sana.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kutatua migogoro ya ardhi kati ya Wananchi na Wawekezaji wenye mashamba makubwa Kibaha Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendelo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 17 la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua jitihada za kutatua migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika maeneo mbalimbali hususan katika Jimbo la Kibaha Vijijini. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufanya ukaguzi wa ardhi iliyomikishwa kwa wawekezaji ili kubaini iwapo masharti ya umiliki yanazingatiwa.

Pili, kuchukua hatua za ubatilisho kwa wawekezaji waliobainika kukiuka masharti ya uwezekezaji; na Tatu, kupanga upya ardhi iliyobatilishwa kwa kushirikiana na Mamlaka za Upangaji kulingana na mahitaji halisi ya sasa hususan hazina ya ardhi, huduma za kijamii na makazi. Aidha, Wizara inaendelea kutoa elimu kwa jamii na wawekezaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na miongozo ya sekta ya ardhi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya mzunguko katika makutano ya Barabara ya Dar es Salaam, Morogoro na Bagamoyo kuelekea Mlandizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Makofia, Mlandisi hadi Mzenga kilomita 35, makutano ya barabara ya Dar es Salaam -Morogoro na Makofia- Mlandizi-Mzenga eneo la Mlandizi limesanifiwa kwa ajili ya kujenga barabara ya mzunguko yaani round about. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza ujenzi wa barabara ya Makofia – Mlandizi hadi Mzenga utakaohusisha na ujenzi wa round about katika eneo la Mlandizi. Ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kudhibiti kuhama kwa Mto Ruvu-Kibaha ili kuzuia uharibifu wa mashamba na miundombinu ya Reli ya SGR?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo Mbunge wa Kibaha Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Ruvu eneo la Kibaha hadi Bagamoyo umekuwa na kawaida ya kuhamahama kwa vipindi tofauti tofauti kutokana na kuwa katika uwanda wa chini karibu na Bahari ya Hindi. Hali hii hupunguza kasi na kufanya udongo kutuwama ndani ya mto na kusababisha mto kuhama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na kazi ya kunyoosha mto pamoja na kuimarisha kingo zilizoathiriwa kwa kuweka gabions na njia mbalimbali, ikiwemo upandaji wa miti pembezoni mwa mto na kwenye vyanzo vya maji, kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji, kuiwezesha jamii kutekeleza shughuli mbalimbali za kujipatia kipato ili kuondoka ndani ya vyanzo vya maji. Kuweka alama na mipaka na mabango ya makatazo ya kuzuia kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya vyanzo vya maji ili kurudisha uoto wa asili na kupunguza athari za mmomonyoko. Jitihada hizi zitaepusha mashamba katika eneo hilo kuathiriwa na maji ya mto Ruvu.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwawekea mazingira mazuri Wakulima wadogo wa kilimo cha Umwagiliaji katika Mto Ruvu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya kilimo kwa wakulima wadogo ndani ya Bonde la Mto Ruvu kwa kubaini maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa Skimu ya Kisere (Nyani), usanifu huu ukikamilika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji utaanza katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutoa mwongozo kwa wawekezaji kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo wanayowekeza?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wawekezaji wanachangia shughuli za maendeleo za jamii katika maeneo wanayowekeza, Serikali ina sheria za kisekta na miongozo inayosimamia wawekezaji katika sekta ya uziduaji ambayo ni mwongozo wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ndogo ya mafuta 2019, mwongozo wa kuwasilisha mpango wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini wa mwaka 2018 na mwongozo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu uwajibikaji kwa jamii wa makampuni wa mwaka 2022. Aidha, Serikali iliandaa mwongozo wa Taifa wa ushiriki wa Watanzania katika sekta mbalimbali wa mwaka 2019 kwa ajili ya kusimamia masuala ya ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji. Utaratibu huo unaruhusu wawekezaji kuchangia sehemu ya mapato yake kwa jamii ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii na kuchangia shughuli za maendeleo katika eneo la uwekezaji kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa. Nakushukuru.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, Serikali ina mipango gani ya kuliendeleza Bonde la Mto Ruvu kwa kushirikiana na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijiji kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Uhifadhi vidakio vya Maji wa mwaka 2021-2035 ambao unahusisha ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ikiwemo wananchi. Kupitia mpango huo, jamii inaelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji ambapo zimeundwa Jumuiya za Watumia Maji 11 na kupitia Jumuiya hizo, wananchi wanashiriki moja kwa moja kulinda na kutunza rasilimali za maji kwenye maeneo yao. Vilevile, kupitia mpango huo, Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu inaendelea kujenga miundombinu ya kunyweshea mifugo ili isiendelee kunywa maji kwenye vyanzo vya maji hasa mitoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kutafanyika uainishaji wa maeneo ya malisho na vivuko kwa ajili ya mifugo, na kuweka mipango ya pamoja ya matumizi bora ya ardhi hususani kwenye maeneo yanayohusisha vyanzo vya maji. Aidha, katika kuliendeleza Bonde la Wami Ruvu, kazi nyingine zinazotekelezwa kupitia mpango huo ni pamoja na kutambua maeneo ya uhifadhi wa vyanzo, kuyawekea mipaka na kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu ambapo hadi sasa maeneo 230 yametambuliwa, 13 yamewekewa mipaka na mawili yametangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, nini kauli ya Serikali juu ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Misitu Sura ya 323 na Kanuni zake za mwaka 2004 zimeelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuvuna, kusafirisha na kuuza mazao ya misitu kwa kuzingatia umiliki wa misitu au miti ambao ni ya watu binafsi, Serikali za vijiji, Serikali za mitaa au Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TFS haizuii kufanya biashara ya mazao ya misitu isipokuwa inasimamia sheria na kanuni ambazo zinahakikisha kunakuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu nchini. Natoa rai kwa wadau au wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya misitu wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda misitu yetu ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuwaendeleza vijana wanaomaliza kidato cha nne na kupata daraja la nne au sifuri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa fursa kwa vijana wote hata wale waliomaliza darasa la saba kujiunga na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyo karibu na maeneo wanayoishi kwa lengo la kujiendeleza katika ujuzi na stadi mbalimbali za maisha. Vile vile vijana hao wanaweza kurudia mitihani yao kama watahiniwa wa kujitegemea iwapo wanahitaji kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi kwa kuwapatia vijana mafunzo ya uanagenzi na utambuzi wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, lini Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Wazee?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM, alijibu:-

Mheshmiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinisia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, napenda kulithibitishia Bunge lako tukufu kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wazee nchini. Sera ya Wazee ya mwaka 2003 iko katika hatua za mwisho za mapitio ili kujumuisha masuala mapya yanayojitokeza tangu kupitishwa kwa Sera hiyo iliyopo.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mapitio ya Sera ya Wazee kutatoa fursa ya kutungwa Sheria ya Wazee na Serikali kuwakilisha Muswada huo wa Sheria ya Wazee Bungeni kwa hatua za sheria hiyo iliyotungwa, ahsante. (Makofi)