Primary Questions from Hon. Muharami Shabani Mkenge (10 total)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Maeneo ya wananchi wa Kata ya Zinga, Kitongoji cha Mlingotini na Pande, yalichukuliwa na Serikali ili kupisha Mradi wa EPZ lakini hawajalipwa fidia:-
Je, ni lini wananchi hao watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone ni moja ya miradi wa kielelezo na kimkakati ambao umepewa kipaumbele nchini na umeainishwa katika Mpango wa Miaka Mitano wa Kwanza, wa Pili na wa Tatu na katika Ilani ya CCM.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za uendelezaji ikiwemo kulipa fidia kwa baadhi ya watu waliopisha mradi kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, eneo ambalo lilifanyiwa tathmini ni hekta 5,743 ambazo fidia ilikuwa ilipwe jumla ya bilioni 58.5 na katika hekta hizo zilizolipwa fidia ni hekta 2,339.6 ambazo jumla ya fidia iliyolipwa ni takriban bilioni 26.6. Serikali inatambua uwepo wa maeneo yanayodaiwa fidia katika eneo maalum la kiuchumi la Bagamoyo yakiwemo maeneo yaliyoko katika Vitongoji vya Mlingotini na Pande katika Kata ya Zinga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza azma ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, Serikali inaendelea kuangalia namna bora zaidi ya utwaaji wa maeneo ya namna hii na kuweka utaratibu wa fidia wenye kuleta tija ya uwekezaji kwa Taifa kwa ujumla. Taratibu hizo zitahusisha ulipaji wa fidia kwa maeneo yaliyotathminiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali na fidia hufanywa kwa mujibu wa Sheria. Pia utaratibu huo unalenga kuyamiliki na kuyaendeleza maeneo hayo ili yawe na tija kwa Taifa letu. Hivyo, fidia kwa wananchi ambao bado wanadai katika eneo hilo la Mlingotini na Pande itafanyika kwa kuzingatia utaratibu hu una Serikali italipa wadai hao haraka iwezekanavyo.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaandaa wakulima wadogo wa miwa (outgrowers) wa Bagamoyo ili kuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo kimejiwekea mipango inayotekelezwa kwa awamu. Awamu ya Kwanza, kiwanda kinatarajia kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika hekta 2,050 za mashamba yake. Hadi kufika mwezi Desemba, 2020 jumla ya hekta 1,700 zimelimwa, kati ya hizo hekta 750 zimewekewa mfumo wa umwagiliaji wa matone.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wadogo wa miwa (outgrowers scheme) watahusishwa katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ambayo inatarajia kuanza mwaka 2022/ 2023. Katika awamu hiyo, Serikali kwa kushirikiana na mwekezaji imetenga eneo lenye hekta 3,600 kwa ajili ya wakulima wa miwa (outgrowers) ambao watazalisha na kuuza miwa yao katika Kiwanda cha Miwa cha Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda unategemewa kukamilika ifikapo Juni, 2022 kwa hiyo miwa ya wakulima itakomaa wakati kiwanda kimeanza kufanya kazi. Hivyo, wakulima hao watakuwa na uhakika wa soko la miwa watakayozalisha.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapima eneo la mifugo la Ruvu na kulikabidhi kwa Halmashauri ya Chalinze?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshapima na kutoa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 2,208 kutoka Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ilikatiwa hekta 1,488 kwa ajili ya vijiji sita ambavyo ni Kijiji cha Ruvu Darajani hekta 200; Kijiji cha Kidogozero hekta 200; Kijiji cha Kitonga hekta 480; Kijiji cha Magulumatali hekta 200; Kijiji cha Vigwaza hekta nane; na Kijiji cha Milo-Kitongoji cha Kengeni hekta 400.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imepima na kutoa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 120 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya vijiji vitatu vya Kidomole hekta 40; Fukayosi hekta 40 na Mkenge hekta 40. Pia, Serikali imepima na kutoa ardhi yenye ukubwa wa hekta 600 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini kwa ajili ya Kijiji cha Mperamumbi Kitongoji cha Waya.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-
Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa Kilomita tano ndani ya Mji wa Bagamoyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza ahadi ya Rais ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 5 iliyotolewa katika mwaka wa fedha 2015 ambapo hadi mwaka 2019/2020 barabara zenye urefu wa kilomita 2.36 zimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.37. Barabara hizo zinajumuisha Barabara ya Stendi ya Kongowe – Kwa Chambo kilomita 0.6, Mgonera – Forodhani kilomita 0.63, Rubeya kilomita 0.7 na Soko la Uhindini kilomita 0.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 375 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Bomani kipande chenye urefu wa kilomita 0.4 kwa kiwango cha lami. Tayari Mkandarasi ameshapatikana na yupo kwenye maandalizi ya kuanza kazi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 375 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Kapala kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 0.45.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya BMU ili kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe kuanzia Pwani ya Bagamoyo, Pangani hadi Tanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari ina mipango ya kuvijengea uwezo wa uelewa ili kujisimamia vikundi vyote vya BMUs katika kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe za bahari yetu. Jumla ya vikundi 18 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti vimepatiwa mafunzo ya kupanda, kuhifadhi na kusimamia mikoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vikundi vya BMUs vya Mlingotini Bagamoyo vimewezeshwa kupanda miche 7,000 ya mikoko. Vilevile, vikundi vya BMUs vya vijiji vya Moa, Ndumbani na Mahandakini Wilayani Mkinga vimepatiwa mafunzo ya usimamizi wa mazingira ikiwemo upandaji wa mikoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia mradi wa South West Indian Ocean Fisheries (SWIOfish) unaoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Vikundi vya BMUs vya Bagamoyo na Pangani wamepata uelewa wa kukusanya maduhuli ambapo kiasi cha fedha kinachokusanywa kitatumika katika kuendeleza shughuli za upandaji wa mikoko na usafi wa mazingira. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je ni lini Serikali itakabidhi majengo yaliyokuwa ya Hospitali ya Muhimbili kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili kupunguza uhaba wa majengo katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shaban Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba majengo hayo yanayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Muhimbili (MUHAS) na chuo kimekuwa kikiyatumia majengo hayo kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wake.
Mheshimiwa Spika, aidha, Chuo kikuu MUHAS bado kina mipango ya uendelezaji na upanuzi wa eneo hilo ili kutimiza majukumu yake, katika kuzalisha wataalam wa afya nchini.
Mheshimiwa Spika: Serikali tayari imepeleka fedha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za dharura kwenye Hospitali ya Bagamoyo na hivyo naomba majengo ya Chuo Kikuu MUHAS yaendelee kutumika kwa shughuli za ufundishaji na utafiti kwa wanafunzi wa Chuo cha MUHAS. Hata hivyo uwepo wa Chuo cha MUHAS ni fursa kwa ukuaji wa Hospitali ya Bagamoyo na ni fursa kwa watu wa bagamoyo kitiba na kiuchumi. Ahsante sana.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, ni lini wananchi wa Kata ya Makurunge watapatiwa eneo la makazi la Razaba baada ya maeneo yao kuchukuliwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 147 la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, wakati eneo hili linachukuliwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji wananchi waliokuwa wakazi wa eneo hilo walilipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria. Aidha, tunatambua uwepo wa wananchi 16 ambao wamekuwa wakidai kulipwa fidia zao, Serikali inaendelea kushughulikia madai hayo na yatakapokuwa tayari tutawapa taarifa.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuboresha minara ya mawasiliano ya simu katika Kata za Makurunge na Fukayosi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imezijumuisha Kata za Makurunge na Fukayosi katika Mradi wa Tanzania ya Kidigitali unaotekelezwa kwa fedha kutoka Benki ya Dunia ambapo zabuni ya mradi huo imeshatangazwa tarehe 24 Oktoba, 2022.
Mheshimiwa Spika, kata hizo zitapata huduma za mawasiliano kwa teknolojia za 2G, 3G na 4G. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga gati ya kuegesha boti na vyombo vya usafiri Bagamoyo ili kuvutia watalii kutembelea Mbuga ya Saadan?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya kisasa ya kuegesha vyombo vya usafiri katika pwani ya Wilaya ya Bagamoyo ili kuvutia watalii kutumia miundombinu hiyo kwenda kutembelea vivutio vya utalii katika mbuga ya Saadan pamoja na Visiwa vya jirani.
Mheshimiwa Spika, katika kutimiza azma hii, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchi kwa maana ya TPA iko katika hatua za mwisho za kuhuisha mpango kabambe wa kuendeleza miundombinu ya bandari nchini ambao utaainisha mahitaji sahihi ya miundombinu ya gati zinazotakiwa kujengwa kwa ajili ya kuegesha boti na vyombo mbalimbali vya usafiri katika Bandari ya Bagamoyo. Maandalizi ya Mpango Kabambe yanatarajiwa kukamilika Juni, 2022 na kufuatiwa na usanifu wa kina ili kupata taarifa za msingi ikiwa ni pamoja na gharama za utekelezaji wa mradi huo. Kazi hii itafanyika katika Mwaka wa Fedha 2022/2023. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, kwa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 ni kiasi gani cha gawio kimetolewa na eneo la Utalii Kaole kwa Halmashauri ya Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Magofu ya Kaole kilianza kutambuliwa na kuhifadhiwa kisheria mwaka 1937 ilipoanzishwa Sheria ya Uhifadhi wa Majengo ya Kihistoria, kipindi cha utawala wa Mwingereza na kwa sasa yanalindwa kwa Sheria ya Mambo ya Kale, Sura 333. Hapo awali vituo vya mambo ya kale vilitumika zaidi katika masuala ya tafiti na elimu hivyo kutembelewa zaidi na wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo hakuna gawio lolote linalotolewa kwa Halmashauri kutokana na mapato ya vituo vya malikale. Aidha, Magofu ya Kaole yanatoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri ya Bagamoyo kunufaika kiutalii kwa kuuza bidhaa mbalimbali kwa watalii kama vile vitu vya kiutamaduni, vyakula na kutoa huduma ya malazi. Kwa kufanya hivyo, halmashauri hunufaika kupitia tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara hao.