Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Zacharius Kamonga (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa neema na rehema zote, niwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Ludewa na chama changu Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nimshukuru pia Mheshimiwa Rais na Serikali yake yote kwa kazi nzuri ambazo zimekuwa zikifanyika na sisi kule Ludewa tumekuwa tukiziona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ludewa kwa kuniamini na kunituma nije niseme hapa Bungeni kwa niaba yao na vilevile sisi Wanaludewa tumezisoma vizuri hotuba zote za Mheshimiwa Rais na tukajitahidi kuzitafsiri ziendane na mazingira yetu ya Jimbo la Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na eneo la uwekezaji kwenye miradi mikubwa ambayo inaweza ikaongeza mapato ya Taifa letu. Mwaka 1996 Baraza la Mawaziri kupitia Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 06/96 wa mwaka 1996 waliridhia miradi ya Mchuchuma na Liganga iweze kuanzishwa na viwanda vikubwa vijengwe kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, NDC kwa maelekezo ya Serikali na Baraza la Mawaziri waliunda Kampuni ya ubia Tanzania-China International Mineral Resources Limited. Kampuni hii ilikwenda Ludewa na kufanya uthamini kwa nia ya kuwekeza kwenye huu mradi wa Mchuchuma na Liganga, baada ya kufanya upembuzi yakinifu na kujiridhisha eneo lile lina mali za kutosha.

Upande wa Liganga kuna chuma ambapo kampuni hii ingeweza kuzalisha zaidi ya tani milioni 2.9 kwa mwaka na kwa makaa ya mawe wangeweza kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na ajira za moja kwa moja milioni sita na laki nne na ajira zisizo za moja kwa moja milioni 33. Lakini cha kushangaza ni kwamba mradi huu umekwama.

Mheshimiwa Spika, Wabunge watangulizi wangu wamejitahidi kupambana miradi ianze, lakini hatujaweza kufanikiwa. Wananchi wa Ludewa wana imani na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na wanamwalika sana aweze kwenda kutembelea miradi hii mapema iwezekanavyo kwani Wabunge wengi hapa wamekuwa wakilalamika fedha TARURA. Mimi nikuhakikishie Serikali ikiamua kuwekeza kwenye miradi ile tutapata fedha nyingi ambayo itatatua changamoto ya fedha na changamoto ya ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile upo mradi wa Chuo cha VETA ambao ulianzishwa pale Shaurimoyo ambao nao umekwama kwa muda mrefu sana. Tulikwenda kufanya ziara Desemba na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na ninamshukuru Rais kwa kutuletea Mkuu wa Mkoa mahiri, Engioneer Marwa Rubirya, tulikwenda naye, watu wa VETA waliahidi Januari wangeweza kuanza kujenga chuo kile, lakini cha kushangaza bado hakijafanikiwa. Kwa hiyo, tunaomba chuo kile kijengwe ili miradi hii inavyoanza na sisi wananchi wa Ludewa na Wananjombe tuweze kupata ajira kwenye miradi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye Sekta ya Maji; namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji, nilipata nafasi nikateta naye, akanihakikishia kwamba mambo yatakwenda vizuri. Pale Ludewa kuna mradi ulitengewa shilingi bilioni saba, lakini kwa miaka mitatu zimeletwa milioni 180 tu, kwa hiyo pana mkwamo mkubwa. Tarafa ya Masasi ina changamoto kubwa ya maji, pale Lupingu walitengeneza mradi wa maji ila umesombwa na maji kwa hiyo kuna changamoto.

Na vilevile pale Kiogo kuna wanafunzi huwa wanakwenda kuchota maji kwenye Mto Ruhuhu kwa hiyo wanaliwa sana na mamba. Manda Sekondari kuna changamoto kubwa ya maji na wataalam wamejitahidi kufanya upembuzi yakinifu Kata ya Mawengi na maeneo mengine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kamonga.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mipango hii ya maendeleo ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu. Niwashukuru pia wale wote ambao wameweza kutambua juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kueleza kwamba asilimia 75 mpaka 80 ya Watanzania wanaishi kijijini na ni maskini. Tushukuru Serikali kwa kutuingiza kwenye uchumi wa kati ila pia tuiombe iongeze fursa, kazi ya Serikali ni kuandaa mazingira mazuri ya biashara ili watu waweze kupata kipato na pato la Taifa liweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pia nimshukuru dada yangu, Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, amezungumzia changamoto ya bei ya mbolea. Ni kweli; kwa mfano kule kwetu Ludewa mfuko mmoja wastani unauzwa kati ya 56,000 mpaka 65,000 na kwa ekari moja mkulima anatumia mifuko siyo chini ya minne ambapo mavuno yake anapata sanasana roba kumi. Sasa akija kuuza hizi roba kumi, roba moja shilingi 40,000, kwa hiyo anapata mapato ya shilingi 400,000 wakati amewekeza gharama zaidi ya shilingi 400,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie namna sasa, nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amekaa na wataalam wa kilimo na kuweka mikakati. Hii ni ishara njema na nimwombe yale ambayo ameahidi aweze kuyatekeleza kwa sababu Wabunge wengi humu tunatokea maeneo ambapo wananchi wetu ni wakulima na wanategemea hasa jembe la mkono. Kwa hiyo naamini atawatoa jembe la mkono wakulima wale ambao asilimia kubwa wako vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na vituo vya utafiti, lakini vituo hivi vijengewe uwezo zaidi ili viweze kutoa taarifa nzuri na taarifa hizi zisibaki kwenye makabrasha, wawashirikishe wataalam wa kilimo kwenye halmashauri zetu, zinaweza kusaidia katika kuongeza tija. Vile vile kwenye ile mikoa yetu ambayo inajishughulisha na kilimo kungekuwa na vituo ambavyo vinafanya uchunguzi wa udongo, zile maabara. Kwa sababu mwananchi anaweza akawa anatumia mbolea ambayo saa nyingine haihitajiki kwenye udongo wa eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyokuwa kwenye Mkutano wa RCC Njombe, watu wa madini waliwasilisha taarifa kwamba Wilaya ya Ludewa ina leseni 104 za madini ambazo hazitumiki zimekuwa zikihuishwa tu. Kwa hiyo waliomba kwamba kwa kuwa eneo hili linaweza kutoa ajira nyingi kwa Watanzania na Wanamkoa wa Njombe na kanda nzima ile ya nyanda za juu; leseni hizi ziweze kufutwa, maeneo haya yagawiwe kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuongeza kipato chao na kipato cha Taifa kiongezeke. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, aliahidi kwamba atalishughulikia na atafanya ziara Ludewa; nimshukuru sana. Wananchi wa Ludewa wanamsubiri kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wanaomba kwenye eneo la makaa ya mawe pale kuna leseni kubwa mbili ambazo zote zimeshikiliwa na Serikali. Sasa si halmashauri mapato pale ni hafifu sana, milioni 800 na sisi tulitamani Mheshimiwa Waziri wa Madini angetumegea kidogo halmashauri pale tuweze kuwekeza kwenye uchimbaji ili pato letu la halmashauri liinuke, tuweze kuhudumia wananchi. Tukihudumia vizuri wananchi maana yake watakuwa na kipato kizuri watafungua biashara na Serikali itapata mapato kupitia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Sheria ya Kodi ya Mapato, TRA. Kuna kodi moja inaitwa Capital Gain Tax; mwananchi anavyonunua au kuuza ardhi hii kodi inatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mapato ya Mwaka 2004. Kodi hii siyo rafiki, wananchi wengi ambao wananunua ardhi wanashindwa kuhamisha umiliki wa viwanja vyao. Kwa hiyo naomba iangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)