Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Deodatus Philip Mwanyika (3 total)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa mradi huu kama alivyosema yeye mwenyewe utachukua miezi 24, miaka miwili na wananchi wa Njombe wakati huo wataendelea kupata tabu na kuteseka hasa wakati wa kiangazi maji yanapopotea kabisa. Je, Serikali itakuwa tayari kutekeleza miradi mingine midogo midogo ambayo baadhi imekwishabuniwa na inafahamika na mingine inaweza kubuniwa, kwa vile Njombe tumezungukwa na mito kila upande?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali ilishatekeleza mradi mdogo katika Mji wa Kibena pale Njombe, kwa kupeleka maji mpaka Hospitali ya Wilaya ya Njombe na kuna tanki kubwa sana wamelijenga pale na tanki hilo lina maji mengi na saa nyingine yanabubujika na kumwagika. Kwa bahati mbaya wananchi wa eneo la Kibena ambao wanaishi maeneo yale bado hawana. Je, Serikali haioni kama itakuwa ni busara na jambo jema badala ya maji yale kuwa yanabubujika na kumwagika sasa wakatoa pesa na kuweka mradi mdogo wa kutawanya maji ili wananchi wa Kibena wapate kuwa na maji ya uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanyika kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la hofu kwa sababu mradi utaanza mwezi Aprili na yeye anapenda visima ama miradi midogo midogo, nipende tu kumwambia kwamba tayari Wizara inafanya mchakato huo na hili linashughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mradi ambao unapeleka maji kwenye hospitali ya Kibena pale kwa kuhitaji distribution tayari Wizara imetoa maelekezo kwa mameneja walioko pale wanafanyia upembuzi yakinifu ili kuona namna gani kama distribution itawezekana. Naomba kukupa amani Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huu ambao tunauanza mwezi Aprili, tutaenda kuufanya kwa kasi nzuri na tutaweza kutawanya maji kadri mradi unavyokamilika hatutasubiri mradi ukamilike mpaka mwisho, ukifika hata asilimia 40 wale ambao wanapitiwa na lile eneo ambalo miundombinu imekamilika maji yataweza kutoka. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo inaongelewa ya kwenda Kishapu ni sawasawa kabisa na barabara ya kilometa 60 ndani ya Mji wa Njombe yaani Ntoni na kwenda mpaka Lusitu. Barabara hii tunaambiwa ilishafanyiwa upembuzi yakinifu, imeshafanyiwa usanifu wa kina lakini sio tu hivyo, barabara hii vilevile imekuwa kwenye ahadi za Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 - 2020 na mwaka 2020 – 2025.

Swali, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii ambayo ni muhimu sana kiuchumi na inapita katika maeneo ya Njombe Mji, Uwemba, Luponde na Matola? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Njombe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema atakubaliana na mimi kwamba iko sehemu ambayo ndiyo inakwenda mpaka huko Ludewa tayari imeshaanza kufanyiwa kazi na mimi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kipindi hiki ni cha bajeti tunatambua umuhimu wa hii barabara na nadhani baada ya bajeti ataamini kwamba Serikali kweli ina mpango wa kuhakikisha kwamba barabara hii ya Njombe – Itoni – Lusitu inajengwa. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii iko kwenye mipango ya Wizara kwa maana ya Serikali kwamba itaendelea kujengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi lakini niulize swali la kwanza. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa maamuzi aliyoyatoa siku ya Jumatatu ya kuruhusu kuajiriwa kwa walimu 6,000 kwa haraka, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni ukweli kwamba walimu 6,000 wanaokwenda kuajiriwa bado wanakwenda kufanya replacement; mahitaji ya walimu katika shule bado ni makubwa sana. Maamuzi ya Serikali ya kutoa elimu bure kwa nia njema yamefanya kuwe na uhaba mkubwa sana wa walimu katika maeneo hasa ya vijijini. Kwa hiyo, pamoja na mipango ambayo imeelezewa lakini bado kuna tatizo kubwa na ninapenda kujua, je, Serikali inaweza bado ikatoa commitment kwamba itaajiri walimu wa kutosha? Kwasababu hii namba iliyotajwa hapa bado haitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; naelewa kuna vigezo ambavyo vinatumika kwenye ugawaji wa walimu kwenye maeneo mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa yale maeneo ambayo ni miji ambayo iko ndani ya halmashauri vigezo ambavyo vinatumika kwa kweli havina uhalisia kwasababu maeneo hayo unakuta yanaangaliwa sana kwasababu yana miji lakini vilevile yana maeneo mengi sana yenye shule nyingi sana ambayo wananchi wamejitoa wakajenga shule ambazo zipo katika maeneo ya vijijini. Wanapoangalia vigezo vya reallocation unakuta kwamba hawaangalii hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali; je, Wizara itakuwa tayari kupitia upya vigezo vya ku-allocate walimu ili maeneo ya halmashauri za miji ambayo yana maeneo makubwa ya zaidi ya kilometa 25 yaweze kupata walimu ili elimu yetu iwe na tija? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri wazi kabisa kwamba alichozungumza Mheshimiwa Mbunge ya uhaba wa walimu nchini pamoja na replacement ya walimu 6,000 ambayo tunakwenda kuifanya hivi karibuni bado upo. Na Serikali imeji-commit hapa katika statement yangu ya awali kwamba tutaendelea kuajiri kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Na mpango huo upo na ni endelevu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ondoa wasiwasi kwenye hilo kwa sababu Serikali iko makini, na Serikali ya Rais wa Sita, mama Samia Hassan Suluhu, imejipanga kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumzia kuhusu Wizara kama tutakuwa tayari kupitia vigezo vya ugawaji wa walimu upya. Nikubali kabisa hilo tumelipokea, moja, ni kama ushauri, lakini pili, tutaendelea kulizingatia kuhakikisha kabisa ugawanyaji wa walimu wote nchini unafuata usawa na haki katika maeneo yote. Ahsante sana.