Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Deodatus Philip Mwanyika (12 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kwanza nitoe shukrani kwa chama changu na Mwenyekiti wa Chama kunipa nafasi ya kuwa mgombea na mwisho wa siku kuwa Mbunge katika Bunge hili, lakini la pili vilevile nawashukuru sana wananchi wa Njombe Mjini kwa kuniamini na kunipa nafasi ya Ubunge nasema sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa ni hotuba ambayo imetoa matumaini makubwa sana. Ni matumaini yaliyojengwa katika msingi wa mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita, yameongelewa hapa kwa wingi hatuna sababu ya kuyataja yote, lakini mimi niongelee moja ambalo limenigusa na litaendelea kunigusa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais tumeshuhudia akifanya mabadiliko makubwa sana katika sekta ya madini. Mimi nasema yalikuwa ni maamuzi sahihi katika wakati sahihi. Tumeshuhudia sasa sekta hii ya madini kuwa ni sekta ambayo inaongoza kwa kuongezea nchi fedha za kigeni, lakini ni sekta inayokua kwa haraka sana. Naomba sasa Serikali iendelee kujikita na kuangalia madini mengine na hasa kwa vile utafiti katika sekta ya madini ni jambo la muhimu sana. Tunaelewa hatuwezi kutegemea wawekezaji kutoka nje kufanya utafiti, kwa hiyo, wazo langu au ushauri wangu kwamba Serikali ijikite kuiongezea STAMICO hela za kutosha ifanye utafiti. Na sisi tunawakaribisha kule Njombe kuna madini ya kila aina waweze kuja kufanya utafiti.

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo nilitaka niongelee ni suala zima la viwanda na uwekezaji. Ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais imejikita sana kuongelea sekta binafsi na viwanda. Ni jambo muhimu na ni jambo ambalo litatufanya sisi tuweze kufikia lengo la zile ajira milioni nane. Kule Njombe tumejikita katika uwekezaji na ukulima, lakini kwetu sisi suala la viwanda ni suala la muhimu sana na Mheshimiwa Rais anaongelea kutengeneza mazingira mazuri ya kuwavutia wawekezaji katika viwanda.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme moja kwamba wakati tunawavutia wawekezaji katika viwanda tuangalie wawekezaji waliopo katika maeneo yetu. Kule Njombe tuna zao moja la kimkakati la chai, ni zao ambalo linatakiwa lipewe umuhimu mkubwa sana. Kwa sasa zao hili linalegalega na kuna uwezekano kama hatua za haraka hazitachukuliwa litafikia mahali pabaya.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito, naelewa katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ameongelea kuweka mazingira wezeshi ambayo yatasaidia uwekezaji uweze kufufuka katika maeneo mbalimbali. Nipende kusema kwamba bado pamoja na kwamba kuna blue print na tunaelewa inakuja, tumeshuhudia kwamba bado kuna tozo za kila aina ambazo zimekuwa ni kero kwa wawekezaji na kero hizo kwa vile ni suala la viwanda na kwa vile tunaongelea chai, tunaongelea mkulima wa kawaida ambaye mwisho wa siku ndiye kipato chake kitashuka.

Mheshimiwa Spika, ukilinganisha ukulima viwanda vya chai ambavyo viko katika maeneo sio tu ya Njombe, lakini na maeneo mengine ya jirani tozo zake ukilinganisha na viwanda vingine vya Kenya vya chai na viwanda vingine vya nchi kama Malawi unakuta wenzetu tozo ni chache sana. Kuna study imefanyika inaonesha tozo za viwanda vya chai peke yake zinafika karibu 19 wakati wenzetu hawana tozo, kwa hiyo, ningeomba Serikali ilitupie macho jambo hilo kwa ukaribu sana.

Mheshimiwa Spika, lakini niongelee vilevile kero nyingine ambazo zinajitokeza katika kushughulikia masuala ya wafanyabiashara, hasa wa mazao ya miti katika Jimbo la Njombe na Jimbo la Njombe ni Jimbo la Njombe Mjini, lakini lina vijiji vingi sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, naomba niunge hoja mkono, lakini nipende kusisitiza iko haja ya kutatua kero za wakulima wa miti na mashamba ya mbao kule Njombe kama vile Rais alivyoahidi wakati wa kampeni. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza ningependa kutoa mchango wangu kwenye eneo la kilimo na biashara. Mpango huu ni mzuri, lakini unachangamoto hasa kwenye eneo hilo la kilimo na biashara ambalo ni eneo muhimu sana kwa uchumi wa nchi. Nianze kwanza ku-declare interest hata mimi ni mkulima wa chai kwa sababu nitachangia kwenye eneo la chai. Mpango huu kwa eneo la kilimo kwa maelezo ya Waziri mwenyewe haujaonyesha mafanikio makubwa kwa eneo la kilimo, ukuaji wa uchumi eneo la kilimo umekuwa mdogo na tunasema mchango wa kilimo kwenye pato la Taifa umekuwa mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo naliona kwamba linaweza likaleta mabadiliko makubwa ni eneo la chai. Zao la chai kwa ujumla wake na sekta ya kilimo kwa ujumla wake imekuwa chini kwa sababu moja kubwa, uwekezaji katika eneo la chai umekuwa mdogo, uwekezaji upande wa Serikali lakini hata uwekezaji kwa upande wa watu binafsi. Kwa hiyo ipo haja ya kuongeza kwa kiasi kikubwa sana uwekezaji kwa namna nyingi na nitazitaja hata chache tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo kubwa ni kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wakulima wa maeneo ya chai. Ukiangalia kwa undani kabisa utaona wazi kabisa utaona wazi kabisa wakulima wetu wa chai hasa wadogo wadogo bado wana-struggle sana kuzalisha chai yao. Kule kwenye maeneo ya Njombe kuna viwanda vikubwa vya chai kama kumi na tisa. Viwanda hivyo vyote vinakuwa own na watu wa nje, wakulima wetu bado wanafanya njia za kizamani za kulima na hawawezi kutoa mchango mkubwa. Ni vizuri sasa Serikali ikajikita zaidi huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia eneo ambalo unaliona lazima tuongeze uwekezaji, ni eneo la ugani. Katika global average wakulima 400 wanatakiwa wahudumiwe na Mgani mmoja, lakini kwetu sisi hapa ni wakulima 1,100. Ukienda kwenye upande wa miundombinu ya umwagiliaji bado tuko nyuma sana, hatuwezi kwenda na kilimo ambacho tunategemea mvua hasa kwenye mazao ya chai na mazao ya avocado. Kwa hiyo tuna kila sababu, Tanzania mpaka leo kwa eneo lililolimwa kwa mwaka 2019, karibu hekta 13,000,000 ni asilimia 20 tu ambayo ina umwagiliaji kama hekta laki nane. Tunatakiwa twende juu zaidi na zaidi ili tuweze kuona tija kwenye eneo la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tu fungamanishe hii sekta ya kilimo ya process na eneo la Nyanda za Juu Kusini Njombe ikiwemo, ni eneo lenye potential kubwa sana ya kuwa game changer kwenye kilimo kama tutafanya uwekezaji mkubwa na tutaita uwekezaji. Hata hivyo, tukumbuke tuna wawekezaji kule wana-struggle kwa sababu ya tozo nyingi sana ambazo kwa kweli pamoja na jitihada za Serikali na tumeona kwenye kitabu hapa, lakini tozo bado ni nyingi sana. Kwenye chai peke yake kuna tozo zaidi 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu na kwenye hotuba ya Rais na kwenye Mpango tunakwenda kwenye kilimo cha biashara maana yake kilimo cha biashara unakuwa competitive ukilinganisha na wenzako. Tuwaangalie Kenya kilimo chao chai, tozo ziko mbili tu; Uganda wana tozo moja; sisi tuna 13. Twende kwenye avocado na matunda matunda tuna tozo karibu 45; pamoja na kazi nzuri ya serikali bado jitihada zinatakiwa zifanyike. Nafahamu kuna blue print inaendelea, lakini kwa kweli impact kwa wakulima bado ni kubwa na negative.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee eneo la wakulima ambalo ni la viwanda sasa hivi vya chai vilivyopo. Nipende kusema wana mchango wao mkubwa, lakini wanaweza wakachanga Zaidi. Kuna mmiliki mwenye viwanda vya chai ametoka Kenya anaitwa DL, sasa hivi anashindwa hata kulipa mishahara, anashindwa kulipa pension, ni miezi 12 wafanyakazi hata pensions zao hazijalipwa, wafanyakazi wana maisha magumu, wakulima wana maisha magumu, wana mwaga chai. mahindi ukikosa mwekezaji au ukikosa mnunuzi utaweka ghalani, utauza mwaka unaofuata, lakini chai ukikosa mnunuzi unamwaga. Kwa watu ambao wanaisha maisha magumu wanatafuta mitaji kwa shida, wanalima chai, wana kila haki ya kuhakikisha kwamba wanasaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la mwekezaji huyu ni moja, amenunua viwanda vya chai lakini hajakamilisha process nzima ya ku-transfer viwanda vya chai na sababu kubwa tunaambiwa ni TRA kwamba wanasema kuna capital gain tax haijalipwa, lakini anayelipa capital gain tax ni yule aliyeuza. Kwa hiyo huyu anashindwa kwenda kukopa, anashindwa kwendelea, anashindwa kuchukua chai, watu wanamwaga chai yao, lakini kosa siyo lake. Sasa kama tunataka mpango huu na tunataka chai iweze kwenda kuzalishwa zaidi na malengo ya Serikali ni kufanya chai kama zao la mkakati liweze kuingia na pesa za kigeni; tuwaangalie wawekezaji hawa, hata huyu mmoja ambaye ana viwanda karibu zaidi ya vinne na anaajiri zaidi ya watu 2,000 na anasaidia kwa kutoa mbolea, kwa kutoa madawa kwa kulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye moja lingine la avocado, avocado it is not be a big business, avocado can be a big changer, tunaita green gold, kwa kweli tunatakiwa tujipange vizuri na naomba sana Serikali tunapozungumzia miundombinu wenzeshi, lazima tuangalie zao hili. Kwenye mazao ya mbao naomba niseme na nimalizie kwa kusema, wakulima na wafanyabiashara wa Njombe wana hali mbaya sana, kwa sababu tunahitaji mahusiano mazuri kati yao na TRA, tunapokwenda siyo kuzuri kwa maana watu wanaona hakuna faida ya kulima misitu, wamelima misitu hawawezi kuiuza, hawawezi kupata faida, ni jambo tunatakiwa tulitiliee maanani na Waziri wa Fedha ameshaandikiwa ili atoe nafasi kwa hawa Watanzania, wafanyabiashara wa Njombe waweze kukaa na TRA kuona namna gani wata-improve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii, ambayo ni bajeti ya kwanza ya awamu ya sita na vilevile ni bajeti ya kwanza katika mpango wa miaka mitano, wa 2021/2022 kwenda mpaka 2025/2026 ambayo dhima yake ni uchumi wa viwanda shindani na shirikishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linanigusa sana na nimeliongelea sana hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake pamoja na Naibu Waziri na timu yake kwa kutupa bajeti hii ambayo kwa kweli imegusa mioyo ya Watanzania. Sisi Wabunge ni mashahidi, mengi yaliyosemwa katika bajeti hii ni yale ambayo sisi kama Wabunge tuliomba Serikali iyashughulikie. Kwa hiyo tunamshukuru sana, na kwa vile hii ni Bajeti ya Taifa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais jemedari wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ndiye chachu kubwa ya bajeti hii, tunamshukuru sana. Mimi kibinafsi namshukuru kwanza kwa sababu ndani ya bajeti hii tunaona dhamira ya dhati ya kuishirikisha sekta binafsi katika kuendesha uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tupende tusipende sekta binafsi ndiyo sekta ambayo tunaitegemea kwa kupata mapato makubwa ya nchi. Lakini si hilo tu, ndani ya bajeti hii tunaona wazi kabisa kwamba Mheshimiwa Rais anatoa maono ya wazi na miongozo ya kuonesha kwamba miradi mbalimbali ambayo ilikuwa ni ya sekta binafsi ambayo imekwamba sasa ipate ufumbuzi na iweze kuendelea mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kwa kifupi kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais kiukweli kabisa kwa kutoa muongozo kuhusiana na mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu umeongelewa kwa muda mrefu sana, na ulifikia mahali ukawa kama ni wimbo tu; unaimbwa unaisha. Lakini sasa tunaona dhamira ya dhati kabisa ya Mheshimiwa Rais, kwamba majadiliano yale ambayo yalikuwa yamekwama yaweze kuendelea na kukamilishwa; na kama hayawezekani basi tutafute alternative nyingine. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maamuzi hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee sekta ya kilimo. Sekta hii ya kilimo wote tunafahamu kuwa ni sekta ambayo imetoa mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi; asilimia 26 ya Pato Ghafi la Taifa linatokana na sekta hii ya kilimo. Asilimia 65 ya waajiriwa ambao wanatoka katika maeneo ya vijijini Watanzania wanatoka katika sekta hii ya kilimo. Lakini siyo hilo tu mchango wa sekta hii kwa upande wa kuleta pesa ya kigeni ni takriban asilimia 24.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza ni kwamba sekta hii inatia huruma. Kwa sababu pamoja na hizo namba tunazoziongea hapa uwekezaji kwenye sekta hii bado ni mdogo sana, na wengi wameliongea hilo. Tunaongelea chini ya asilimia 0.8 wengine wanasema asilimia 1.9 lakini ukweli ni kwamba ni mdogo mno; na udogo wa uwekezaji huo si kwa Serikali peke yake kupitia bajeti bali hata kwa sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, benki zetu bado hazijachangamkia fursa kubwa ambazo zipo katika sekta hii kubwa ya kilimo. Ukiangalia mgawanyo wa fedha ambazo zimekwenda kwenye sekta binafsi kwa ajili ya kilimo inasikitisha kuona kwamba takriban asilimia 35.8 ya mikopo ya benki imekwenda kwenye mambo binafsi tu ya watu. Asilimia 15.7 imekwenda kwenye biashara za kawaida, asilimia 10 kwenye viwanda, lakini kilimo ni asilimia nane tu. Kwa hiyo tuna tatizo kubwa la uwekezaji kwenye sekta hii upande wa Serikali kupitia bajeti lakini vile vile kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani sasa wote tuna kazi ya kufanya hapa, lakini la kwanza kabisa tuanze na maamuzi ya kibajeti. Naelewa hakuna kitu tunachoweza tukakifanya katika bajeti hii kwa sasa, lakini tunaiomba sana Serikali na tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri, wote tutambue kwamba lazima tuitendee haki Tanzania; na huwezi kuitendea haki Tanzania kama hautatoa pesa za kutosha kwenye sekta hiii ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka mitatu minne iliyopita sekta hii uwekezaji wake umeteremka. lakini huko nyuma angalau tulifikia asilimia tano ya total collection. Lakini tukiweza angalau tukafika angalau tufikie hata asilimia sita, tukiweza kufikia asilimia saba ambayo ndiyo declaration ya Maputo nadhani tutakuwa tayari tunaenda katika mlolongo mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nitoe ushauri; tunahitaji kuvutia uwekezaji kwa namna ya pekee kwenye sekta hii ya kilimo, na ninavyoona tunahitaji kuwa na special scheme za sekta ya kilimo pamoja na vivutio katika sekta hii. Tunajua sekta hii iko katika maeneo ya vijijini huko mikoani. Wengine walisema na mimi nalisisitiza, kwamba iko haja ya kuwa na vivutio vya kikodi na vya kisera ambavyo vita-focus kwenye sekta ya kilimo na kwenye viwanda ambavyo vitakua na vitajengwa katika maeneo ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaloliona sasa hivi kiwanda kinachojengwa eneo la kilimo mikoani na kinachojengwa mikoa ambayo haina kilimo vinakuwa treated sawa; hatuwezi kufika katika utaratibu huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejitahidi kuweka vivutio vya aina fulani katika bajeti hii kwa upande wa cold rooms na vifungashio. Lakini mimi nasema kwamba, pamoja na hilo tunawashukuru lakini bado tutatakiwa tuangalie wapi hasa panahitaji kuwekewa hivyo vivutio. Tuangalie mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo. Mimi nasema, vifungashio sawa, cold rooms sawa, lakini twende tukaangalie pale ambapo kunafanyika uzalishaji wa mazao yetu ya kilimo ndipo hasa tuweke hivyo vivutio. Tuangalie maeneo ambayo kama kuna viwanda vya madawa, tuangalie viwanda vya mbolea, tuangalie vilevile pale ambapo tunahitaji utaalam na utaalamu hatuwezi kuupata hapa basi tulegeze masharti ya vibali kwa watu ambao watakwenda kufanya kazi kama wataalamu kwenye sekta ya kilimo. Tunahitaji kufanya kazi kimkakati ili tuweze kuifunua hii sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu zao la avocado, kwa kifupi tu. Nchi hii ina uwezo mkubwa sana wa kuongeza mapato makubwa sana kama tukiweza ku-focus kwenye zao la avocado. Zao hili linaweza kui-transform Tanzania. Ukichukua nchi kama ya Mexico ambayo eneo lake ni dogo, hata ukubwa wa mkoa wa Njombe Mexico ni ndogo lakini kwa mwaka 2018/2019 Mexico kwa avocado peke yake wameingiza 2.7 billion dollars. Hayo ni mapato yanayofikia mapato yetu yote ya dhahabu. Kwa hiyo iko haja ya kuliangalia hili jambo kwa umakini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa sasa watafiti wanasema katika miaka mitano ijayo Tanzania inaweza ikawa nchi ya uzalishaji mkubwa wa avocado kuliko hata Kenya. Lakini tuna kilio hapa ndani, kwamba avocado zetu sisi tunazi-register kama zinatoka Kenya, na kwa hiyo kuna upotevu wa mapato, lakini vilevile nchi yetu inakosa fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba tatizo hili litaendelea kama tusipoweka mikakati mahiri sasa hivi. Ukiangalia kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam ambayo ndiyo port of exit kubwa tunayoitegemea uwekezaji unaoendelea ni mkubwa lakini bado hauja focus kwenye perishables. Nchi hii inategemewa kuwa projected kuzalisha takriban laki sita za avocado.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda ukilinganisha na Mombasa watu wanakwenda Mombasa kwa sababu slot za cold rooms Mombasa ziko 1800, unakwenda na container una slot unangojea meli Tanzania TICTS Pamoja na TPA slot zipo 120. Kwa hiyo hakuna uwezo wowote utakaotufanya sisi tuende kwenye huo ushindani na tukashinda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuongea kidogo sekta ya Madini, ukiangalia utakuta kwamba tumelegalega na nchi yetu kwa kiasi kikubwa sana sekta ya utalii ime-collapse, lakini sekta ya Madini imeweza ku-balance na imenyanyua kwa kufanya shilingi yetu i-stabilize kwa sababu ya dhahabu. Tunamshukuru Mungu kwamba tunaiyo dhahabu, lakini kwa kiasi kikubwa dhahabu yote hiyo imetoka kwenye migodi kama miwili pamoja na wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kwamba, tunatakiwa tuendelee kuvuta wawekezaji kwenye Sekta hii ya Madini ili tuweze kupata mapato makubwa. Pia tunatakiwa tu-identify, twende kwenye sekta nyingine au sub- sector nyingine ambazo ndiyo sasa hivi dunia inakwenda na huko tuna wawekezaji kuna maeneo kama ya helium gas, kuna maeneo kama ya rare earth. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo haya tayari tuna wawekezaji, lakini wawekezaji hawa wanagombea mitaji na nchi nyingine na kama hatutafanya maamuzi haraka ina maana hiyo opportunity haitakuwepo na hatutaweza kukua na kupata mapato makubwa ambayo kama tungekuwa na migodi kila mahali inafanya kazi, kila mahali inazalisha, tungekuwa na uchumi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba, mambo mengi yamefanyika ya kikodi hapa ambayo yanataka kusisimua uchumi, lakini tukiwa na utendaji na uzalishaji na migodi na huku wewe unalima uchumi huu siyo kwamba utasisimuka lakini utazimuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Mpango huu wa Tatu wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie maeneo machache; eneo la kwanza ni sekta binafsi kwa ujumla. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa kweli kama tunataka kufanya uchumi ukue sekta binafsi haikwepeki. Sekta binafsi ni muhimu, kwa hiyo, tuiwezeshe ili iweze kusaidia kwenye kukuza uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachojitokeza kwa kiasi kikubwa sana kwa miaka hii ya karibuni, nachelea kusema kwamba sekta binafsi imeingia katika challenge kubwa sana na kwa kiasi kikubwa tumesikia kwamba baadhi ya wawekezaji katika sekta binafsi na hapa tunaongelea ngazi mbalimbali hatuongelei wakubwa peke yao, tunaongelea wakubwa wa kati na wadogo wamefika mahali wamekatishwa tamaa na baadhi yao wamefunga biashara au wamekaa pembeni wakiangalia kitachoendelea kama watazamaji. Hii haina afya kwa uchumi wetu na haina afya kwa mpango wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri jambo hili limeshapewa mwelekeo na Serikali. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutoa kauli ambayo imetoa mwanga mpya kwa nchi yetu. Mkubwa akishasema watendaji tunatakiwa tuwe tumeshaelewa, this is the tone from the top. Kwa hiyo, tunatakiwa sasa watendaji wajipange wakijua mwelekeo wa nchi yetu inavyoiangalia sekta binafsi ni tofauti na ilivyokuwa miaka ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uhusishwaji wa sekta binafsi uko katika maeneo mengi, uko katika ngazi ya sera lakini uko katika ngazi ya mambo ya kikodi. Sekta binafsi ina vyombo ambavyo ndivyo maalum kwa ajili ya kufanya dialog na Serikali. Vyombo hivyo vipo, kazi imekuwa ikifanyika lakini wote tunafahamu mwisho wa siku challenges ambazo sekta binafsi inazipata wengi tunaambiwa hapa zimefikia mahali ambapo wote tunangoja kitu kinaitwa blue print mkakati ambao ndiyo unaenda kujaribu kushughulikia masuala mengi ambayo dada yangu pale Jesca amezungumzia, ametamka neno pale nisingependa kulirudia lakini urasimu ambao ndiyo upo umeonyesha kwa kiasi kikubwa unaua sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe tu angalizo hii blue print inayoongelewa ni karatasi tu tunahitaji kuwa na mindset change kwa viongozi wa Serikali. Tunahitaji kuwa na mindset change katika taasisi mbalimbali zinazosimamia mambo yote ya kiuchumi kuanzia Benki Kuu, TRA na vyombo vyote vya udhibiti kwa maana ya regulators. Hawa watu wasipobadilisha mindset ya kuiona sekta binafsi kama engine ya kusaidia kukuza uchumi tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu, hatutapata matokeo tunayoyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikishwaji wa sekta binafsi ni pamoja na kuifanya sekta binafsi ishiriki kwenye uchumi. Serikali ndiyo mtumiaji mkubwa wa rasilimali fedha ambazo mwisho wa siku zinaishia kwenye mikono ya Watanzania kwa kupitia shughuli zao mbalimbali. Tulichokiona ambacho mimi naamini kinadumisha uchumi wetu ni Serikali kuona kwamba inaweza ikafanya mambo mengine mengi yenyewe ya kibiashara. Tumeona Serikali wakati mwingine inajenga yenyewe, tumeona maeneo ambayo hata kazi za kawaida ndogo ndogo taasisi za kibiashara za umma ndiyo zinapewa zifanye kazi hizo, hii haisaidii kuinua uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetunga sheria hapa za local content ambazo zinatakiwa zisaidie Watanzania ili waweze kushiriki kwenye uchumi. Napenda kusema sheria hizi zitabakia kuwa makaratasi tu kama Serikali yenyewe haitakuwa na initiative ya kuhakikisha mambo haya yanatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee eneo lingine la kilimo. Ndugu yangu pale ameshaongelea eneo la kilimo na maeneo ambayo ameyaongea mimi sitaongelea lakini ni ukweli usiopingika kwamba bado sekta ya kilimo itabakia kuwa ndiyo sekta kiongozi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupeleka mbele uchumi wa nchi yetu. Sekta hii tunafahamu ina matatizo mengi na makubwa, inahitaji vichocheo vya kila aina na kikubwa kuliko vyote ni miundombinu wezeshi. Tumeshaongea kwa kiasi kikubwa hapa sitapenda kulirudia lakini kwa kweli tukubaliane kwa wakulima hasa wa mazao fulani fulani mkakati kama tutaendelea kutokuwa na utaratibu wa kuwa na umwagiliaji wa mazao yetu, nina uhakika sekta ya kilimo bado itaendelea kubakia nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuangalia Mpango ulivyoandikwa unaona bado umwagiliaji ni chini ya 20%. Mazao kama chai ambalo ni zao kubwa sana maeneo ya Nyanda za Juu Kusini, ili uweze kupata mavuno hasa unahitaji kuwa na miundombinu ya umwagiliaji. Kuna makampuni makubwa yanafanya uzalishaji wa chai lakini makampuni hayo sisi tunasema yana mchango wake tunahitaji kwenda sasa kuwa na wakulima wadogo wadogo wa chai walio wengi ambao watatoa mchango wa moja kwa moja katika sekta ya chai.

Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze kwa waliofanikiwa ukienda Bangladesh, sisi tuna viwanda 21 vya chai lakini Bangaladesh wana viwanda vidogo vidogo vya chai 700. Wao Serikali imechukua jukumu kubwa la kuhakikisha hili linatokea kwa sababu chai inaajiri watu wengi sana katika uchumi hivyo una uhakika wa kupata kodi nyingi katika uchumi wako. Siyo hilo tu unasaidia kuinua maisha ya watu na hii inaendana na dhana nzima ya uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme moja ambalo limekuwa ni kikwazo kwa sekta ya chai. Chai ni zao la mkakati na la export lakini ukiangalia kuna tatizo kubwa sana la VAT. Kinachojionyesha ni wazi kabisa kwamba urejeshaji wa VAT katika maeneo mengi ya mazao ambayo yanapelekwa nje ya nchi umekuwa ni hafifu sana. Hii inawaondolea wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali uwezo wa kuweza kuwa na mtaji wa kuendeleza biashara zao na hiyo inaondoa na inapunguza ulipaji wao wa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kwa kifupi madini. Eneo la madini tumeona na tumeshuhudia mafanikio makubwa lakini naomba niseme wazi kwamba kama ambavyo Prof. Muhongo alituambia asubuhi na mimi nikazie tusijidanganye, tusipime success ya sekta hii kwa kuangalia mapato ambayo tumeyapata mpaka leo kwani hayatokani na kuongezeka kwa uzalishaji. Inawezekana kuna ongezeko la uzalishaji lakini sehemu kubwa ya ongezeko hilo limetokana na kazi nzuri ya Serikali ya kuzuia utoroshaji hasa uliokuwa unafanyika kwa kutumia njia za panya. Kwa hiyo, inaonekana kama kuna ongezeko lakini kwa kweli uzalishaji haujaongezeka, hakuna migodi mipya mikubwa iliyojitokeza au iliyojengwa katika miaka mitano mpaka sita toka tumebadili sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, inabidi tuwe makini kwa sababu tunapoangalia Mpango tuangalie na threats za wapi tunaweza tukashindwa kuendelea. Mimi naliona hili bei ya dhahabu siku zote huwa inakwenda juu na chini, wakubwa wameshaanza kukaa na tunaweza tukaona hali ya stability katika ulimwengu ambayo itasababisha bei ya dhahabu pengine, hatuombei, ianze kwenda chini na mara moja tutapata impact kubwa negative kwenye Mpango wetu, hili tulielewe na tulitilie maanani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tufanyeje sasa? Tufanye yale ambayo tumeshayasikia, twende kwenye maeneo ya madini mengine ambayo ni muhimu na tusichelee kuona kwamba Liganga na Mchuchuma ni eneo ambalo hatuna sababu kwa nini mpaka leo hatujaweza kuanza kuzalisha pale mawe pamoja na chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kama hiyo ni kengele ya pili. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Madini. Baada ya mageuzi makubwa katika sekta hii ya madini, tumeshuhudia sasa mabadiliko makubwa. Mchango wa sekta umeongezeka, kukua kwa sekta kumeongezeka kwa kiasi kikubwa. Mchango wake sasa hivi ni asilimia 5.2 ya pato la Taifa na bado unaendelea kwenda, imekuwa projected kwamba, utaongezeka zaidi. Kwa hiyo, niwashukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote ambao wameweza kutufikisha hapa na hasa kwa kuweza kutupa matokeo ya haraka kwenye maeneo mbalimbali ya sekta hii na hasa kwenye utoroshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kama nitakavyoeleza hapo baadaye tumeshuhudia sekta hii kukua lakini, hatujashuhudia sekta hii kuongeza uzalishaji kwa maana ya migodi mipya. Nianze kwa kusema Bajeti ya Wizara hii ni bilioni 66.8; kati ya hizo, bilioni 15.0 ni miradi ya mkakati na katika miradi ya mkakati tunaona kuna bilioni kama tatu zinakwenda STAMICO na bilioni 3.5 zinakwenda GST. Ni jambo jema kwa sababu, wengi wameongea hapa kwamba utafiti ni jambo la muhimu. Nipende kukazia maisha ya sekta ya madini yanategemea sana utafiti na utafiti wa uhakika. Wengi wamelia na kusema maneno mengi hapa hata kwa wachimbaji wadogo kuhusiana na suala la utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende kusema kukua kwa sekta hii na kuongezeka kwa mchango wa sekta hii, kwa kiasi kikubwa bado naweza nikasema sio himilivu, inatakiwa tufanye kazi za ziada na sababu kubwa ni kwamba, bado sekta hii kwa kiasi kikubwa inategemea dhahabu kama zao ambalo ndio hasa linaifanya hii sekta ionekane na itoe mchango mkubwa. Kwa maana hiyo basi, kama nia ni kufanya by 2025 tufikie asilimia 10 ya pato la Taifa, bado tuna kazi kubwa kwa sababu, napenda kuliambia Bunge lako kwamba, dhahabu ina tabia ya kupanda bei na kushuka bei.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba bei imekuwa ikipanda na nilishawahi kusema humu ndani kuna majira yanakuwa mabaya. Kwenye sekta ya madini tunasema kuna bust na kuna boom, tupo kwenye boom la madini lakini bust na yenyewe iko mahali fulani. Kwa hiyo, tujiandae na cha kufanya kama nilivyosema mara ya mwisho tuanze kuangalia madini mengine na madini haya, tunasema ni madini ya viwanda (industrial minerals). Tuna madini ya kila aina katika nchi hii, tuna utajiri mkubwa cobalt, graphite, helium gas, rare earth, mwenzetu mmoja ameongea kuhusu niobium hapa asubuhi, kwa hiyo, tuangalie haya.

Mheshimiwa Spika, vile vile, tujitendee haki kwa kuangalia ukuaji wa sekta hii, kwa kuangalia jambo la exploration. Ni ukweli usiopingika kwamba, sekta ya utafiti kwa maana ya pesa ambayo inaingia ndani ya nchi yetu kufanya utafiti imepungua sana kama haipo kabisa. Hata kwenye Bajeti ya Mheshimiwa Waziri sijaona akiongelea pesa ya utafiti na utafiti unaoendelea ndani ya nchi kwa pesa inayotoka nje kuja kufanya utafiti hapa ndani, ni ya muhimu. Lingekuwa ni jambo jema tukafanya utafiti kwa pesa zetu, tunalipenda lifanyike hilo, maana litatupa nguvu ya kuweza kujua nini kiko wapi kwa ukubwa gani na kwa miaka mingapi? Hiyo itatusaidia kuweza kuongea na watu wote ambao wanataka kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali halisi tuliyonayo, inabidi tukubali kwamba uwezo huo hatuna. Tukitaka tufanye ili tujue kila kitu kiko wapi katika nchi hii, hiyo bajeti tunayoongelea ya bilioni 400 au 500 ya Wizara ya Madini itabidi tuzidishe mara tatu au mara tano tuizike yote kwenye exploration. Sidhani kama litakuwa ni jambo la busara wakati tuna mahitaji mengi makubwa. Hata hivyo, sekta binafsi inaweza kuifanya hilo, tena kwa vizuri kabisa. Tukubaliane kabisa kwamba, katika utafiti kuna utafiti wa aina mbili; kuna utafiti ambao unafanywa na migodi ambayo ipo tayari sisi tunaita, brown exploration na utafiti huu unaendelea bado kwa migodi ile kwa sababu, wanataka wao waendelee kuongeza mashapo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utafiti tunaouongelea ambao ni mkubwa wa kuongeza na kukuza hii sekta, ni utafiti unakwenda kwenye maeneo mapya ambayo bado hayajaonekana tunaita green field exploration. Tunahitaji kuwa na uwekezaji kwenye eneo la green field exploration, ni muhimu kwa uhimilivu wa sekta ya madini.

Mheshimiwa Spika, nNipende kusema vile vile pesa nyingi za uwekezaji katika sekta hii ya madini kwa upande wa exploration, mara nyingi ni pesa za watu mbalimbali wanakusanya na kuziweka na kuzifanya ziwe available kwa nchi au kwa wawekezaji. Nadhani baada ya miaka mitano ya kuwa na mafanikio mazuri baada ya mageuzi makubwa kwenye sekta hii, lazima tuanze kujiuliza maswali magumu. Hatuna budi kujiuliza ni kwa nini kwanza, hatupati hizi pesa kutoka nje za uwekezaji kwa maana ya exploration?

Mheshimiwa Spika, vile vile ni miaka 10 sasa, hatujaona migodi mipya ikifunguliwa katika nchi yetu. Tunasikia michakato ya kutaka kufungua migodi, lakini ni wazi tunatakiwa kuwa makini sana ili tuweze kuhakikisha kwamba nchi yetu inanufaika, ni jambo jema. Pia ni wazi kwamba, bado tunaweza tukanufaika kwa kufanya fine-tuning tu katika sheria zetu. Hatuna sababu, tumefanya makubwa kwa kufanya mengi ya kubadilisha sheria, lakini kuna mambo madogo tunaweza tukayafanya ambayo yanaweza yakatupa faida zaidi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Deo Mwanyika, dakika tano zimeisha.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, tuliambiwa dakika saba.

SPIKA: No, ni tano! Ili orodha niliyonayo iweze kutimia, tunashukuru sana. (Makofi)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, basi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu ya Wizara ya Maji. Nianze kwa kumpongeza Waziri na watendaji wote ndani ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha Watanzania wanapata maji. Naelewa kwamba ni kazi ngumu na tunaelewa kwamba ina changamoto nyingi lakini niseme tu kwamba kazi hii wamepewa ni lazima wafanye kwasababu iko ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwamba wananchi wa Tanzania wa vijijini kwa asilimia 82 watapata maji na asilimia 95 watapata maji ifikapo mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo maneno ndani ya Ilani watu wa Njombe bado yanatutatiza Mji ya Njombe Wabunge wengi hapa wamelalamika na wanalalamika kwamba hawana maji ni tatizo kubwa lakini wengi wanalalamika kwa vile wana uhaba wa maji, lakini Njombe ni tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna maji ya kutosha, tuna maji mengi, tuna mito inapita kati kati ya mji wetu wa Njombe upande wa huku kula Agafilo upande huku kuna mto mwingine wa Ruhuji lakini tuna visima ukichimba tu unapata maj. Pia tuna maji ya chemichemi lakini cha kushangaza ni kwamba bado mji wa Njombe tatizo kubwa kero kubwa kuliko zote ni maji, hatuna maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Njombe wanapata maji kwa kiwango cha asilimia kama 60 tu na wakati wa kiangazi inakuwa mbaya zaidi, sasa niseme ni aibu lakini ni aibu ambayo lazima tuishughulikie. Kumekuwa na miradi midogo midogo ambayo Serikali imekuwa ikiitekeleza kwa ajili ya kutoa tatizo hili na Rais alipotembelea Njombe Marehemu Mungu Amrehemu mara mbili alipouliza shida yenu hapa ni nini wananchi wa Njombe walisema ni maji mwaka 2015 akigomea alisema shida yenu nini watu wakasema ni maji alipokuja tena kuomba kura akawauliza watu wakamwambia hatujapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa alikuwa pale aliitwa na akasema kwamba atahakikisha ndani ya miaka miwili maji yanapatikana ni miaka mitano sasa wananchi wa Njombe mjini hawana maji tunaongelea mjini. Jimbo la Njombe Mjini lina kata 13 kata 10 ni za vijijini na Kata tatu ni za mjini naongelea kata za mjini hazina maji sijaenda hata vijijini bado, tatizo ni kubwa tunafahamu kabisa kuna mradi mkubwa ambao umekuwa ukiongelewa lakini sisi wana Njombe tunapata wasiwasi bado hata na mradi huu mkubwa ambao tunasema wa miji 28.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sababu kubwa ni kwa vile tulikuwa ndani ya miji 16 au 17 scope yake ilikuwa inaeleweka sasa tunaongelea miji 28. Kwa hiyo, fedha zilizotengwa ni hizo hizo miji imeongezeka shida kubwa ya Njombe kwa miradi ya nyuma ilikuwa ni kwamba bado ilikuwa ni miradi ambayo haiwezi kutatua tatizo kwa kiasi kikubwa tukaambiwa huu mradi mkubwa unakuja kumaliza tatizo tunapata wasiwasi kama kweli mradi huu utamaliza tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Waziri atuhakikishie wana Njombe kwamba maeneo yote yaliyokuwa kwenye scope yatapata maji, maeneo ya Magoda yatapata maji, maeneo ya Lunyanyu yatapata maji Chuo Kikuu cha Lutheran kitapata maji, maeneo ya Ngalange yatapata maji na maeneo ya Msete yatapata maji, mji wa Njombe ni katika miji inayokuwa haraka sana katika Tanzania ukuaji wake ni karibu asilimia 3.5 ni kidogo juu ya average kwakweli na kuna eneo la Nundu linakuwa kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri hata kama scope imebadilika watu wa Njombe wawaangalie kwa tofauti kwasababu ni mji mpya ni Mkoa mpya, Mikoa mingi iliyoongezwa ina miradi mingi ya maji, hapa Njombe hatujawahi kupata mradi mkubwa hata mmoja wa Serikali, na ndio maana Rais alisema wazi Njombe tutahakikisha maji yanapatikana na Mheshimiwa Prof. Mbarawa ni shahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo jingine tuna mradi mwingine mkubwa ambao umekuwa ukiendeshwa kwa takribani miaka mitano sasa miaka sita unaitwa EGOGWI ninashukuru kwamba mradi huo umeonekana katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri lakini bado ni kwa kiwango kidogo sana cha fedha, mradi huo ni kama wa bilioni nne wakati Mheshimiwa Rais Mama Samia anapita katika maeneo ya Njombe kuomba kura alisimamishwa eneo ambalo mradi unapita na akaahidi kwamba maji yatapatikana katika eneo hili. Nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba kwakweli ahadi ya Mheshimiwa Rais ambaye wakati huo alikuwa ni mgombea ilikuwa ni kwamba maji lazima yatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nipende kusisitiza mradi ule ni moja ya miradi ambayo hadi leo haijakamilika kwasababu ninaamini ni uzembe wa watendaji waliopita ndani ya Mamlaka ya maji wakati ule ilikuwa chini ya halmashauri kwakweli tunauhakika kabisa na tunaomba tunapokwenda mbele wataalam wafanye stadi za kutosha za maeneo kujua kama kuna maji ya kutosha na wahakikishe wanatumia hata wananchi wa kawaida kuwaeleza kwamba jamani pamoja na stadi zetu eneo hili lina maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam kwenye Mradi wa EGOGWI waliambiwa kwamba chanzo hicho mnachotaka kuweka vijiji zaidi ya nane hakitoshi lakini walibisha matokeo yake pipe zimewekwa maji hayatoshi scope imebidi ianze kuandaliwa upya, ninadhani ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Kwakweli Mheshimiwa Waziri tunawashukuru sana Watendaji ambao wako RUWASA kwa sasa maana yake wameweza kuja na mradi mpya ku-scope upya hilo eneo na kuja na mradi mpya ambao unatupa moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini watendaji waliopita nadhani ni vizuri kauli ya Rais ianzie hapo kuhakikisha mnashughulika nao maana yake wapo na wapo kwingine na huko watafanya hivyo watafanya hivyo watatengeneza miradi isiyotoa maji na fedha za Serikali zinatumika, ni vizuri tukachukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuongelea mradi mwingine mdogo wa mji wa Njombe eneo la Kibena, tunaishukuru Serikali ilitumia fedha za kutosha kwa kiasi fulani kuleta maji katika mji wa Kibena Kata ya Ramadhani. Lakini kilichotokea ni kwamba ndani ya mradi huo mdogo maji yameweza kuja kwa maana Serikali imeweza kuongeza Capacity ya pumps imejenga Intech mpya imeongeza mabomba ukubwa wake kutoka inchi tatu mpaka inchi tisa, sasa kuna maji ya kutosha na hospitali yetu ya Wilaya ya Njombe ya Wilaya inapata maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza na cha kusikitisha ni kwamba eneo lile lina wananchi wengi waliounganishwa ni wananchi kama 3,000 bado kuna uhitaji wa watu wengine 3,500. Hapa niliuliza swali la msingi nikaomba kwenye swali la nyongeza kwamba tunaomba eneo la Kibena ile project ambayo maji ni mengi yanaonekana yanamwagika iongezewe fedha kidogo basi ili distribution line iweze kuenea na watu wapate maji kuliko wao wapo mjini wanaangalia maji kwa macho na maji yanamwagika kwenye matenki sababu tu project ya kwanza ilikuwa ni ndogo haikukamilika, nakuomba Mheshimiwa Waziri uliangalie hilo kwa jicho la huruma kwa wananchi wa Njombe eneo la Kibena ili angalau tupate fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijaona fedha zimetengwa katika bajeti hii labda kama nimeshindwa kusoma maeneo yote, lakini sijaona eneo lolote ambalo Kibena Project ya kuongezea ili wananchi waweze kupata maji ya kutosha, wananchi 3,500.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa hii nafsi na niombe kwa kumalizia kwa kusema tuna matumaini makubwa sana na Mheshimiwa Waziri na wana Njombe wanamatumaini makubwa sana na Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hii wanachapa kazi lakini tutawapima kwa matokeo wana Njombe watawapima kwa matokeo niwatie moyo kwamba bado tunategemea kwamba mtafanya kazi nzuri na mtakamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyopo Mezani. Nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja, lakini niseme sekta hii ya kilimo ndiyo inabeba maisha ya Watanzania walio wengi. Kwa hiyo, ningetegemea labda wangekuwa na bajeti kubwa ya kutosha, lakini matarajio hayo na bajeti iliyopangwa ni sidhani kama itakidhi matarajio ya wengi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nianze kwa kusema bado nampongeza Waziri na Naibu Waziri na Watendaji kwa juhudi zao mpaka muda huu. Kwenye bajeti hii nilichokiona pamoja na kwamba hakuna pesa za kutosha, lakini wamejaribu kuweka maeneo ya mikakati ambayo yanakwenda kushughulikia baadhi ya matatizo.

Mheshimiwa Spika, napenda kusema, itategemeana sana kama hata hiyo pesa ndogo iliyotengwa kama itapatikana. Kama isipopatikana tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu na sidhani kama kuna mafanikio yoyote ambayo yatapatikana kulinganisha na matarajio.

Mheshimiwa Spika, napenda niongelee mazao mawili ambayo ndiyo yapo katika Jimbo letu la Njombe Mjini, lakini yapo katika Ukanda mzima wa Nyanda za Juu Kusini. Tukianza na chai, wachache wameliongelea humu ndani, lakini ni zao ambalo tuna uhakika na tunaelewa kwamba kwa sasa hivi ni zao ambalo katika soko la dunia bei imetikisika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, nchi yetu uzalishaji wa chai umeshuka chini kwa maana ya majani mabichi ya chai, lakini napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Waziri, walikuja Njombe tarehe 10 mwezi wa Tatu, wakakaa na wadau wa chai, tukawaeleza matatizo yote ya chai, kwa hiyo, tukayajenga tukaweka mikakati.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo wanalielewa ni kuhusiana na umwagiliaji. Tunahitaji tija kwenye zao la chai, tunahitaji kuwa na bajeti ya kutosha ya umwagiliaji. Nimeona katika bajeti ya leo kwamba umwagiliaji umepewa pesa kidogo. Nina matumaini makubwa kwa sababu Mheshimiwa Waziri alikuja Njombe, akayasikia mwenyewe. Katika pesa hizo atahakikisha kwamba wakulima wa chai wa eneo hilo wanaangaliwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ni la muhimu…

T A A R I F A

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa.

MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nataka nimtaarifu msemaji kwamba, wakati wanahangaika na umwagiliaji pale Kilolo kuna eka zaidi ya 300 za chai. kwa miaka 30 ile michai sasa inachomwa mkaa; na hata hiyo ambayo mvua inanyesha yenyewe, bado haijafanywa kitu chochote na hakuna kiwanda na majani hayachumwi.

Mheshimiwa Spika, nampa taarifa hiyo ili aweze kujenga hoja vizuri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Deo.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yake, nami nilikuwa naenda huko. Najua wanakwenda kuongeza uzalishaji wa chai, lakini nilisema kwamba waanze na maeneo ambayo tayari chai ilishalimwa na imeachwa porini na mojawapo ni hilo la Kilolo. Ndiyo maana naongelea Nyanda za Juu Kusini na chai.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kubwa ni miundombinu wezeshi katika zao la chai. Ni ukweli usiopingika kwamba kama hatuta-address tatizo la miundombinu wezeshi kwenye zao la chai hatutapata mafanikio wala hatutapata yale malengo yetu ya kuongeza uzalishaji wa chai kutoka tani 37,000 kwenda kule ambako wanataka, hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ambalo limeongelewa sana hapa, la ugani, ni jambo la muhimu sana. Naelewa kwenye chai kwenye eneo la Njombe kuna Kampuni ya NOSC ambayo imeleta ushirikiano mkubwa na imesaidia, lakini kuna maeneo mengi bado tunahitaji Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Spika, naelewa umeliongelea hapa ukielezea kwamba Serikali haiwezi kuajiri. Ni kweli haiwezi kuajiri Maafisa Ugani wa kutosha, lakini kuna wakulima wadogo wadogo wa chai ambao wanahitaji msaada mkubwa wa Maafisa Ugani. Kwa hiyo niombe waendelee kuliangalia na nimeona kwamba bajeti yao imeongezwa.

Mheshimiwa Spika, soko ni tatizo kubwa sana, Njombe na zao la chai soko letu sisi ni viwanda, kiwanda kikifanya kazi maana yake tuna soko. Kinachojitokeza, Njombe tuna viwanda vinne vya chai, tuna uhakika wa hilo soko, lakini kwa bahati mbaya, katika waendeshaji wa viwanda vya chai katika Mkoa wa Njombe na maeneo yote ya Njombe ni mwekezaji mmoja tu ya Unilever ambaye yeye anaendesha kwa ufanisi na anaweza kulipa wakulima. Waendeshaji wengine wa viwanda vya chai ni jambo la kusikitisha sana kwamba wameshindwa kabisa kuwalipa wakulima wa chai. Naelewa jambo hili Waziri Mkuu aliliingilia, Mkuu wa Mkoa ameliingilia, Waziri amelisikia, lakini bado tatizo bado linaendelea. Tunaomba sana Serikali ioneshe kwamba ni Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kiwanda kilichobaki kimoja ambacho kinafanya kazi kina tatizo bado la kupata majani ya chai ya kutosha. Kuna uwezekano kama tatizo hili halitakuwa-addressed, kwa sababu mfumo wa kile kiwanda ilikuwa ni kupata majani ya chai kutoka kwa wakulima wadogo wadogo, majani ya chai hayatoshi. Ni kweli kwamba maeneo mengine yanayozalisha majani ya chai yanaweza yaka-supply kiwanda kile, lakini kwa sababu ya mikataba ambayo imeingiwa, wakulima wale wanatakiwa wapeleke chai kwenye kiwanda au viwanda vya yule mtu ambaye hawezi kulipa ambaye ni Mkenya wa Kampuni inaitwa DL Group.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo Wananjombe hatulikubali kwa sababu kama wananchi wanaweza wakapeleka majani kwenye Kiwanda cha Unilever ambacho kinalipa kwa nini wazuiwe. Kwa hiyo, naiomba Bodi ya Chai ifanye kazi yake, lakini namwomba vile vile Mheshimiwa Waziri naye aingilie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Deodatus Mwanyika.

DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akifanya.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri tunaambiwa sasa ni vijiji karibu 1,952 ndiyo bado havijapata umeme na katika REA III round II ndiyo vitapata umeme. Kwa Jimbo letu la Njombe tuna tatizo na nilishaonana na Mheshimiwa Waziri kumueleza matatizo ambayo tunayo. Njombe ni vijiji vinne tu ndiyo ambavyo vimeingia katika mradi wa REA III round II. Mheshimiwa Waziri alinihakikishia kwamba kulikuwa na makosa na kwamba vitajumuishwa.

Mheshimiwa Spika, Waziri ametushauri hapa kwamba tuwasiliane na wakandarasi ili tuweze kujua scope ya kazi yao na wanafanya nini. Nimewasiliana na wakandarasi kama Waziri alivyosema lakini cha kusikitisha ni kwamba wakandarasi mpaka sasa scope yao ya kazi inafahamu hivyo vijiji vinne tu.

Mheshimiwa Spika, naelewa pengine kuna mchakato wa kubadilisha hiyo scope lakini nimuombe Waziri kwa niaba ya wananchi wa Njombe awahakikishie kwamba vijiji vile 20 vyote vitaingizwa katika mpango huu.

Tunaomba sana asitupeleke kwenye Peri-Urban Project maana vijiji hivi ni vijijini kabisa siyo maeneo ya mjini kwa vile Jimbo la Njombe linaitwa Njombe Mjini. Vijiji hivyo ni kama vifuatavyo; Makoo, Ngelamo, Mamongolo, Lugenge, Kisilo, Kiyaula, Idihani, Utengule, Ngalanga, Uliwa, Igoma na kijiji ninachokaa mimi vilevile kina matatizo cha Makanjaula nacho hakina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimuombe sana Waziri atuangalie kwa jicho la huruma. Njombe program nzima ya REA I, II, III zote hizi kwa kiasi kikubwa sana zimekuwa propelled na Mkoa wa Njombe kwa sababu sisi ndiyo supplier wakubwa wa nguzo karibu zote ambazo zinakwenda katika project hizi zote. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuona Mheshimiwa Waziri na sisi anatuangalia.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna ya pekee nimuombe Waziri, tuna Shule ya Sekondari Yakobi, REA III round I uli-target taasisi mbalimbali za afya na za elimu lakini kwa bahati mbaya sana shule hii ambayo ina watoto karibu 600 mpaka leo wako gizani. Tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kuiingiza shule hii nayo ili iweze kupata umeme katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala la nishati jadidifu. Sekta madhubuti ya nishati ni ile ambayo ina mchanganyiko wa vyanzo mbalimbali vya umeme. Kwetu hapa tunaona kabisa kwamba kwa kiasi kikubwa umeme wa maji na umeme wa gesi ndiyo unachukua sehemu kubwa lakini tuna potential kubwa ya kuwa na umeme tofauti na huo au wa kuongezea kama umeme wa upepo au solar. Wawekezaji siyo kama hawapo lakini majadiliano na wawekezaji hawa yanachukua muda mrefu sana. Njombe tuna potential ya kuzalisha mpaka megawatt 150 kwa umeme wa upepo kama vile wenzetu wa Singida. Mheshimiwa Waziri ametuambia wanakwenda kufanya majadiliano na ni kweli wawekezaji tunajua wameshaitwa kwa majadiliano lakini majadiliano haya yafike mwisho basi ili na umeme wa upepo nao uingie katika mpango wetu wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama muda utaniruhusu niongelee kidogo kuhusu mradi wa kusindika umeme wa gesi. Kwenye vitalu Na.1, 2 na 4 ndipo ambapo tunategemea kwamba mradi huu mkubwa wa LNG utajengwa au utapata resource yake ya umeme. Tuseme wazi Tanzania ina bahati kuwa na endowment kubwa sana ya gesi 57 tcf ni umeme mkubwa, ukiu-put kwenye context ni umeme ambao unaweza uka-power nchi ya UK kwa miaka 20 bila wasiwasi, kwa hiyo, ni umeme mwingi mno. Hata hivyo, suala siyo kuwa na resource ni namna gani resource hii sasa tunakwenda kuifanya ifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niseme kimoja katika global scale bado Tanzania hatupo hata katika top twenty wenye resource kubwa ya gesi. Kwa hiyo, wawekezaji ambao tunao kwenye sekta hii ni vizuri tukakamilisha mazungumzo hayo. Tunafahamu siyo kitu cha kukimbilia au cha kufanya haraka lakini tuseme kama alivyosema Mbunge mmoja hapa kwamba kwa kweli hatuna muda mwingi wa kupoteza.

Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu ya Kuridhia Mkataba wa Eneo Huru la Afrika. Napenda kuanza kwa kusema kwamba Mkataba huu tunaelewa kabisa umeridhiwa na baadhi ya nchi na nchi hizo ziko katika eneo letu la Afrika Mashariki. Hata hivyo kuchelewa kwa Tanzania kuridhia mkataba huu kumeleta hisia kwamba pengine wafanyabiashara wa Tanzania wanaogopa au wana uoga. Napenda kukudhihirishia, wafanyabiashara wa Tanzania hawana uoga wa kuingia kwenye ushindani, wafanyabiashara wa Tanzania wanaamini ushindani ndiyo utakaoboresha biashara zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na nafasi ya kuwa Mjumbe wa Baraza la Biashara la Tanzania nikiwakilisha sekta binafsi katika nafasi yangu ya huko nyuma. Tatizo kubwa la wafanyabiashara wa Tanzania ni kuhakikishiwa kwamba kutakuwa na ushindani ambao upo level au uko sawa au una usawa, Waingereza wanaita level playing ground.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo naomba niwashauri Wabunge kwamba wafanyabiashara wetu wanaiona hii ni fursa, nao ndio watakaokwenda kwenye soko hili. Wafanyabiashara/sekta binafsi ndio watakaokwenda kwenye soko hili na tuna kila sababu ya kuwasaidia na kuwa-support. Nao wanachotaka siyo Serikali iwape fedha, Serikali iendelee kuboresha mazingira ya biashara. Tumeisema kwenye Kamati kwamba Serikali iendelee kuboresha mazingira ya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami napenda kusema kwenye hili, Serikali ina forum ya kuongea na wafanyabiashara on almost quarterly basis. Tunaomba sana forum hii itumike vizuri ili kuweza kujua matatizo ya wafanyabiashara wa Tanzania kila wakati ambapo yanajitokeza, isiwe inangojewa mpaka malalamiko yanafika mbali au yanakuwa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hapa kwa juhudi zake kubwa sana za kuliweka hili jambo wazi na kuwaambia Watendaji ndani ya Serikali na kuonyesha mwelekeo wa nchi yetu kwenye masuala yote ya uwekezaji pamoja na kutoa kauli ambazo sasa zinatabirika katika Jumuiya ya Wafanyabiashara. Jambo hili ni zuri kwa nchi yetu, jambo hili ni zuri kwa wafanyabiashara wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni la muhimu sana ili tuweze kufanikiwa kwenye suala hili ni kuhakikisha tunakwenda kwenye ushindani. Ushindani ni suala la bei na ubora. Sasa kwenye ubora, kwa kiasi kikubwa ni suala la mwekezaji mwenyewe au mfanyabiashara. Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba standards zinakuwa met. Kuna suala la bei. Kwenye bei wafanyabiashara wetu lazima tuwasaidie. Nasi msaada wetu kama nchi au kama Serikali ni kuhakikisha kwamba tunawapunguzia gharama ambazo siyo za lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wameliongea, kuna gharama nyingi ambazo siyo za lazima; nyingi tunasema ni kama tozo, lakini kuna gharama nyingine. Kwa mfano, ukichukua mkataba unaohusiana na masuala ya electronic stamp, tumeliongea sana hili hapa Bungeni. Gharama ya mkataba ule ni kubwa mno. Wenzetu watakaokuwa wanazalisha vitu hivyo na kuvileta katika soko letu, pengine hawana hiyo gharama au kama wanayo ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasi tuliangalie. Kwa mfano, TBL wanatumia dola milioni tisa kwa mwaka kwa kuweka hizo stamp tu. Hiyo gharama ni kubwa sana, nayo inakwenda kwenye masuala mengine vilevile. Tuangalie pia utaratibu mzima wa wafanyabiashara kuhakikisha kwamba tunaweza kuwarudishia kile ambacho wanadai kama VAT. Ni jambo la muhimu sana. Wengi tunashindwa kuelewa kwamba mtaji wa mfanyabiashara siku zote unahesabiwa kwa shilingi. Anapokuwa anadai Serikali marejesho na yanachukua muda mrefu, inampunguzia mtaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda niliseme, naomba sana Serikali ifanye uchambuzi vizuri. Najua ndani ya mkataba huu unatoa nafasi ya kuhakikisha kuna maeneo ambayo tunadhani kwamba bado hatujafikia uwezo wa ku-compete au pengine tuna-comparative advantage. Serikali iyachambue vizuri. Nitatoa mfano, kuna maeneo ya nguo tumeambiwa kwamba haya yatabakia kuwa yetu, lakini kuna maeneo mengine uchambuzi ufanyike na hasa maeneo yale ambayo SMEs zetu zitashiriki. Iko haja ya kuona namna gani tutawasaidia ili waweze kuingia kwenye soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hii hoja na naomba sana Wabunge wenzangu tuipitishe kwa nguvu zote. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DEO P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango na Mapendekezo ya Mpango ulio mbele yetu wa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nijikite kwenye maeneo mawili; eneo moja ni eneo la uwekezaji kwa maana ya Mradi wa Liganga na Mchuchuma na muda ukiruhusu niweze kuangalia Sekta ya Kilimo kama wenzangu ambavyo wameangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu unajaribu kujikita kutoa msingi wa maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa 2022/2023 na umeainisha maeneo muhimu ya vipaumbele. Katika maeneo haya kuna maeneo ya miradi ya kielelezo. Kwenye maeneo haya kuna eneo la Liganga na Mchuchuma; nipende kusema na mwenzangu Mbunge wa Ludewa ameliongelea, lakini mimi nitaliongelea kwenye angle tofauti kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuelewa kinachoelezwa katika Mpango, kuhusiana na mradi huu ni kwamba, majadiliano yanaendelea na tunakubali, lakini tuishauri Serikali kwamba mradi huu ni mradi mkubwa, ni mradi ambao unaweza ukawa game changer. Leo nataka nitoe takwimu kidogo tu hapo baadaye za kwa nini Mpango unaokuja ni lazima uzingatie kuona matayarisho ya Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma kwa maana ya makaa pamoja na chuma uweze kuanza kuonyeshwa na kuandaliwa wakati majadiliano yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majadiliano hayo ambayo hayaishi hatuelewi ni majadiliano gani. Tunaelewa kwamba pengine kuna ugumu kwenye kujadiliana, lakini tufike mahali maamuzi yafanyike na option za uwekezaji katika sekta hizi za madini kama chuma ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachumi wanasema kuna gharama au kuna hasara ya kutofanya jambo fulani kwa wakati fulani, wao kitaalamu wanaita opportunity cost. Sasa tukiangalia sasa hivi bei ya chuma ndani ya miezi 24 imefika dola za Kimarekani kwa tani 400 ni ongezeko kubwa la asilimia 200. Wachina peke yao ndiyo wanao-dominate soko hili la chuma kwa sasa. Wanazalisha karibu asilimia 56.5 ya chuma chote duniani. Afrika peke yetu tunazalisha kama asilimia 17, Tanzania ni sifuri, lakini tuna chuma hapa na tuna resource hapa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema kuna research imefanyika na Institute ya Global for Development Studies ya Boston University ambayo inaonesha katika kipindi cha 2008 mpaka 2019 Wachina peke yao wametoa mikopo ya financing ya maendeleo duniani ya karibu dola za Kimarekani bilioni 462. Ndani ya hizo dola bilioni 462 asilimia 80 imeenda kwenye miradi ya infrastructure, maana yake unaongelea bandari, reli, madaraja na kadhalika. Afrika peke yetu tumepata dola bilioni 106 katika hizo dola bilioni 462.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachotaka kusema ni nini? Hizo dola bilioni 106 ni karibu trilioni 230 za Kitanzania. Hoja hapa ambayo Mpango lazima uangalie ni kwamba tuna kila sababu ya ku-take advantage ya uchumi wa makaa ya mawe na chuma sasa hivi ili tuweze ku-benefit huko tunakokwenda. Kama Tanzania peke yetu tungeweza kupata, maana yake katika hii 80 percent infrastructure na Afrika ni dola bilioni 106, sisi tuna chuma, kama tungekuwa tumeanza uzalishaji hata tukapata asilimia 50 tu ya hiyo biashara ya ujenzi wa infrastructure katika maeneo ambayo yanahitaji chuma sana madaraja, SGR, barabara, ports, zote zinataka chuma, tungepata asilimia 20 tu ya hiyo biashara ya kuzalisha hiyo chuma, bajeti yetu nzima yote trilioni 39 ingeweza kutoka katika biashara ya chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ipo haja tuone kwamba tuna haja na tuna kila sababu ya kuhakikisha haya majadiliano yanafika mwisho ili tufanye huu uwekezaji katika hili eneo la chuma pamoja na makaa ya mawe. Tuliangalie vile vile pengine nje ya box, kama tunaona maana yake hapa hatuhitaji pesa ya Serikali, pesa ya uwekezaji kwenye maeneo haya ipo duniani na wawekezaji wapo duniani. Kama tuna mwekezaji ambaye hatuwezi kwenda naye anatuchelewesha, tujue kwamba hiyo opportunity cost inakula kwetu.

Mheshmiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningependa niombe sana sana Mpango huu, ukiangalia kwa mfano katika Mpango, matumizi ya mwaka jana katika robo ya kwanza hata wachukue robo mbili, matumizi ya Serikali kwenye maandalizi ya mradi huu huwezi kuamini wametumia shilingi za Kitanzania milioni 3.7, nadhani ni kuwalipa walinzi wanaolinda yale maeneo. Kwa hiyo ni kwamba hakuna uwekezaji wa aina yoyote kwenye eneo hilo na kwamba ni kama hatuoni umuhimu kwenye hii mradi huu wa kielelezo, ambao ni muhimu. Nchi yoyote ambayo ina chuma leo na ikaanza kuchimba itakuwa na bajeti nzuri, itakuwa na chanzo kikubwa sana cha mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuliongolea hilo, kwa hiyo nisema maandalizi ni pamoja na kuhakikisha kwamba hizo fidia zinalipwa kutengeneza hilo eneo ili mambo yakikamilika haya ya majadiliano, uwekezaji uanze, siyo tena tuanze kuhangaika kwamba kwenye bajeti hakuna compensation, hakuna hela za kulipa. Kwa hiyo Mpango ujaribu kuliangalia hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala pia ya miundombinu, project hii ita entail vilevile kuendeleza SGR kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay mpaka kwenye Mchuchuma. Kwa kweli kwenye Mpango inaonyesha kwamba bado wanaendelea kufanya tathmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba haya mambo yaharakishwe kwa sababu si lazima Serikali itumie pesa kujenga SGR, tufanye hii kitu tofauti na tulivyofanya kwenye central line, kuna watu wanaweza wakajenga kwa pesa zao tu-negotiate nao ili tuweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee haraka haraka kilimo, wengi wameongelea, suala zima la tija katika kilimo tuliliongelea hapa na tumeliongelea muda mwingi kwamba tunahitaji kupata mbolea kwa wakati na mbolea ambayo ni affordable. Hali si nzuri wote tunaelewa, tunajua kwamba Serikali itakuja na maelezo hapa kabla Bunge halijaisha kutuambia kuhusu suala la mbolea. Hata hivyo, nipende kusema, tunashukuru Serikali imefanya jitihada za kuona namna gani itashusha bei ya mbolea au itawapa nafuu wakulima. Ukweli wa mambo ni kwamba bado hakuna nafuu, tuiombe Serikali na Kamati imejaribu kuongea na imesema ni vizuri Serikali ikaangalia uwezekano wa kutoa ruzuku katika suala hili la mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuongelea zao la parachichi, kwa sababu nalo ni chanzo kingine kizuri sana cha mapato. Zao la parachichi ukiangalia kidunia Watanzania tumezalisha kama asilimia 0.2 ya mazao yote ya parachichi duniani. Ukweli ni kwamba, Tanzania ndiyo nchi pekee yenye potential kubwa sana ya kuendelea kukamata soko la parachichi katika dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaweza tu kufanya hiyo iwapo tutahakikisha kwamba sasa hivi Serikali ina-invest katika kilimo kwa maana ya kuhakikisha kwamba wakulima wote kwenye masuala ya mbegu, ubora wa mbegu, yanaangaliwa kwa umakini sana, kwa nini? Kwa sababu unalima parachichi leo, unaanza kuzalisha baada ya miaka mitatu, lakini full production inaanza baada ya miaka saba. Kama mbegu tunazotumia hazina uhakika, hazina ubora tutafika kule mwisho hatuta-realize hayo tunayotaka kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana tulikuwa na promise ya Serikali ya kuweka mamlaka ya kusaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie suala la Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni la muda mrefu na kama ripoti ya Kamati ilivyooneshwa hatujaridhishwa kabisa Wanakamati na taarifa tunazozipata kuhusu mwelekeo na muendelezo wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu tunachoambiwa ni kwamba uko kwenye majadiliano. Majadiliano haya ambayo hayaishi tunashindwa kuelewa ni majadiliano gani. Tuna uhakika kabisa wataalam wetu wana uwezo wa kufanya majadiliano na tumewaamini na tuna hakika pengine wanapigania maslahi makubwa ya nchi yetu ili tupate mkataba mzuri, lakini miaka 11 toka mkataba umesainiwa mpaka leo hatujaweza kukamilisha jambo hili? Hivi hatujui na hatuoni umuhimu wa chuma katika maendeleo ya nchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kusema wote tunafahamu majadiliano siku zote sio lazima ushinde kila kitu, lakini majadiliano yanataka compromise, ufike mahali ukubaliane na hasa kama unajua lengo lako ni nini. Sasa sisi tunaelewa chuma tunahitaji, tunaelewa mradi huu ni mkubwa, mradi huu utabadili maisha ya watu, mradi huu tunaouita mradi wa kielelezo, mradi huu tunauita upo katika mpango wa kwanza ulioishia 2021, upo kwenye mpango wa pili unaoishia 2026, upo kwenye kila bajeti ya kila mwaka, upo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Ndugu zangu, hivi tunataka nini? Tunafahamu kabisa kwamba tunapoteza kwa kutoendelea na uwekezaji kwenye mradi huu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda kupendeza; nafahamu Waheshimiwa Wabunge kwamba Kamati yetu inajaribu ku-negotiate ili tupate better terms, lakini nitoe ushauri hebu wajaribu kuangalia maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua approach ikiwa ni kuangalia negotiations kama kama kihasibu, unaangalia tu faida kwamba, tutapata faida, hatupati mpaka mwisho unapiga hesabu unasema hapa hatupati faida, nadhani hiyo approach sio nzuri. Waende na approach ya kiuchumi ya kuangalia multiplier effect kwenye mradi huu; mradi huu ajira 5,000 za moja kwa moja, mradi huu ajira 33,000 ambazo hazitakuwa moja kwa moja. Ndani ya mradi huu…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge, Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, sio tu kwamba utasaidia kuzalisha chuma ambacho tungeweza kutumia katika maendeleo mengine, lakini ni mradi ambao ni unganishi kwa kuendeleza pia Makaa ya Mchuchuma na chuma cha Liganga,

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa maana hiyo, kulikuwa na mpango sahihi kabisa wa kuzalisha megawati 600 ambazo nyingine zingetumika kuchenjua chuma na megawati nyingine 400 zingeingizwa katika njia ya msongo wa kilovoti 400 pale Makambako ili uweze kuingia kwenye Gridi ya Taifa kwa hiyo, ni mradi muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi.

NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Mwanyika, Taarifa hiyo.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana kaka yangu kwa kuendelea kunifilisi nilichotaka kuongea, lakini niseme mradi huu ni special. Mradi huu ukiuangalia kwa haraka upande mmoja ni mradi wa kiuchumi, lakini ni mradi wa kiundombinu; tunaongelea ujenzi mkubwa wa reli katika mradi huu ambao utaiunganisha Bandari ya Mtwara, inakuja mpaka Manda inapata mchepuko inakuja kwenye huu mradi. Kwa hiyo, ajira ngapi zitazalishwa katika hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuangalie kitu kingine, tunatumia fedha nyingi sana nnchi hii katika masuala ya chuma; ujenzi wa maghorofa, ujenzi wa madaraja, ujenzi wa SGR, ujenzi wa towers. Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ameongea kwamba hatuna towers, nchi hii ina towers za simu zaidi ya 10,000; hivi hiyo miradi yote hiyo ya towers ni chuma na sisi chuma tunacho hapa na tunalialia kwamba, hakuna towers za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia ni mengi, miradi hii itapunguza gharama nyingi sana ya vitu vingi. Kwa mfano, tunaongelea uzalishaji wa gesi, nani anafahamu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungashio cha gesi unachokiona, unakiita cylinder, asilimia karibu 50 ya ile gesi, gharama…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumpa Taarifa kaka yangu Mheshimiwa Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kuhusu suala la Liganga- Mchuchuma sio tu itasaidia hayo anayoyasema, lakini pia itasaidia kuanzisha viwanda vya magari katika nchi yetu. Kwa hiyo, itaongeza na kukuza uchumi kwa zaidi ya asilimia 100. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante. Taarifa hiyo.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali taarifa na mambo ni mengi ni mengi sana ambayo chuma kingetusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumalizia kwa kusema wenzetu Serikalini watusaidie. Mheshimiwa Engineer Chiwelesa amesema huyu mwekezaji kama hawezi basi aondolewe, lakini tunachoambiwa ni kwamba kuna tatizo la tax incentives au vivutio.

Sasa mimi nimeangalia vivutio vinavyoongelewa, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hivi vivutio vinavyoongelewa kwa mradi mkubwa wa aina hii tuangalie maslahi makubwa kwamba tukijenga hii infrastructure ambayo ni Liganga – Mchuchuma, power na steel, tukajenga na hizi reli, uchumi mkubwa wa eneo zima la Kusini utasisimka na tunaweza tukapata hii kodi ambayo tunaweza tukaisamehe hapa mwanzoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata ukiziangalia hizi kodi zinazoongelewa hapa tuliuliza swali hivi tunazipata leo? Kwa hii chuma kuwa bado hazijachimbwa? Tunazipata hizo kodi? Hatuzipati.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Kwa hiyo, tuliangalie kwa karibu nashukuru muda ni mfupi lakini naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na kunikumbuka ili nami niweze kutoa mchango kwenye muswada uliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja kwanza kwa kumpongeza sana Waziri wa Fedha na Mwanasheria Mkuu kwa kuja na Muswada huu. Muswada huu pamoja na kwamba mawanda yake yanaongelea zaidi mambo ambayo ni ya kuimarisha zaidi udhibiti ili Tanzania nayo isiwe ni sehemu ambayo labda utakatishaji unaweza kushamiri, lakini tukumbuke vilevile kwamba sheria hii inawahusu Watanzania wa kawaida, mmoja mmoja na wengine walio wengi. Kwa hiyo wengine leo watakuwa na mawazo kwamba labda sheria hii itawapa ahueni kwenye mambo fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kwanza kabisa, mimi naichukulia sheria hii kama ni mwendelezo wa yale ambayo tuliyaanza jana ya kuendelea ku-improve utoaji haki katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hili kosa la utakatishaji ni kubwa, lina madhara makubwa kwenye uchumi na tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba utakatishaji fedha ni jambo ambalo linapigwa vita kwa nguvu zote na udhibiti unakuwepo katika nchi. Pamoja na kusema hayo, nimeridhishwa na kufarijika na kuona marekebisho ambayo yamefanywa katika Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa ku-take into account mawazo mengi ya Kamati ambayo waliyatoa, yameturahisishia kazi na yanaonesha kabisa kwamba tuna ushirikiano mzuri katika kuendeleza suala hili la kupeleka sheria ambazo zina maslahi makubwa na mapana kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mawili tu ambayo napenda niyaongelee; moja ni kifungu cha tatu ambacho tafsiri yake imepanuliwa, imeongezwa, imebadilishwa na imeandikwa upya. Kifungu hiki cha tatu katika sheria ya zamani kulikuwa na hilo kosa linaloitwa kosa mtangulizi au la msingi (predicate offense).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wanaojua historia ya Muswada huu au sheria hii watagundua kwamba kwa muda mrefu makosa yaliyongezwa mpaka ikafika wakati kosa la kawaida kabisa na lenyewe linaweza lika-qualify kuwa ni utakatishaji. Hiyo ilisababisha matatizo makubwa, hisia mbaya dhidi ya Serikali yetu kwa kudhani kwamba kosa lolote unalolifanya linaweza likawa ni utakatishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu sasa umekuja na umetibu tatizo hilo. Nimefurahia kuona namna interpretation katika sheria mpya inavyojaribu kwa kusoma kifungu kile cha 12 ambapo sasa makosa haya yametenganishwa; kosa lile ambalo ndilo la msingi (predicate offense) na kosa lenyewe la utakatishaji, ni makosa ambayo sasa hayatakuwa pamoja. Huko nyuma tukumbuke kwamba makosa ya utakatishaji ni makosa ambayo hayana dhamana. Kwa hiyo ukweli ni kwamba pamoja na kudhibiti fedha haramu lakini mwisho wa siku vilevile kuna uwezekano wananchi wakaumia kama jambo hili lisingeangaliwa kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza, moja, ningependa kifungu namba 28B ambacho ni kipya ambacho kinaongelea eneo la wakurugenzi wa makampuni, mameneja, kwamba watakuwa-presumed kwamba wame- commit offense chini ya Sheria ya Anti-money Laundering iwapo hawatajitetea na kuonesha kwamba hawakuhusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uweze kujitetea kwamba haukuhusika unatakiwa upite katika mfumo wa kisheria na tukumbuke kwamba sheria hii isiangaliwe peke yake iangaliwe na sheria nyingine. Sheria hii na makosa katika sheria hii ni makosa ya kihujumu uchumi, kwa hiyo hayana dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri basi huko mbele Mwanasheria Mkuu angeliangalia hili baada ya kupitisha sheria tukaangalia na sheria nyingine ambazo zinaendana na hii ili ziweze kutoa matumaini makubwa zaidi ambayo Mheshimiwa Rais wetu ameahidi umma wa Watanzania na anaendelea kuyafanyia kazi kwa haraka sana katika utoaji wa sheria kama wote tunavyoona mambo yanavyobadilika na kuwa mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)