Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Festo Richard Sanga (6 total)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Makete naomba kuuliza kuhusu ujenzi wa barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya kutoka Chimala – Matamba – Kitulo kilometa 51, ilikuwa ni ahadi ya Waziri Mkuu mstaafu, kwa muda wa miaka 10 hadi sasa haijatekelezwa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete ni kati ya barabara ambazo zimetajwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia ukurasa wa 72 – 76. Pia katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Rais ameeleza kwamba katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani hii pamoja na ahadi alizozitoa atahakikisha kwamba anajenga na kukamilisha barabara zote ambazo zinaendelea zenye urefu wa kilometa 2,500 lakini pia ataanza ujenzi na kukamilisha barabara zenye urefu wa kilometa 6,006 na barabara hii ya Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete ni kati ya barabara ambazo zimetajwa ama zimetolewa ahadi na mwenyewe Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, nimpe uhakika kwamba barabara hiyo itajengwa na kukamilika.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Majibu ya Serikali hayajaniridhisha kwa sababu wananchi wetu kwenye zoezi hili la kuweka beacon walishirikishwa kuweka beacon tu, hawakushirikishwa kwenye mipaka itawekwa maeneo gani.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili tuongozane kwenda Makete tukawape majibu wananchi wetu na kurudia zoezi la kuweka beacon? Kwa sababu zoezi hili limesababisha wananchi wangu wengi saa hizi wako ndani lakini sehemu ya shule zimewekwa beacon…

SPIKA: Mheshimiwa Festo…

MHE. FESTO R. SANGA: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari twende wote?

SPIKA: Nisikilize kwanza; swali lako halijaeleweka kabisa, kwamba wananchi wako wlaishirikishwa kuweka beacon lakini hawakushirikishwa mahali pa kuweka, sasa…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, kilichotokea wananchi wamefika wamekuta watu wa kutoka Serikalini wanaweka beacon, hawajaambiwa kwamba ni eneo hili la mpaka au wapi. Kilichotokea nyumba nyingi za wananchi ziko ndani ya hifadhi, kitu ambacho hakikuwepo, siku za nyuma mipaka ilikuwa mbali. Leo hii wananchi wangu wengi wako ndani ni kwa sababu ya hilo jambo. Sasa ninachomuomba Naibu Waziri tuongozane baada ya hili Bunge twende Makete akawape wajibu wananchi wetu turudie zoezi; hicho ndicho ninachomwomba. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara iko tayari kuhudumia wateja wa aina yoyote akiwemo Mheshimiwa Sanga, hivyo naahidi baada ya Bunge lako Tukufu nitaongozana naye nikiwa na wataalam kwenda kuonesha hiyo mipaka ili wananchi watambue mipaka ya hifadhi ni ipi na iendelee kuheshimiwa. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo. Kwa kuwa na sisi watu wa Makete tuna changamoto ya hospitali ya wilaya toka mwaka 1982 kituo cha afya kilivyopandishwa hadhi kuwa hospitali ya wilaya, hadi sasa hatuna hospitali ya wilaya. Je, ni lini Hospitali ya Wilaya ya Makete itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/2021, kiasi cha shilingi bilioni 27 kimetengwa kwa ajili ya kujenga hospitali za halmashauri zile ambazo ni chakavu, tutajenga hospitali za halmashauri mpya na Halmashauri ya Makete ni miongoni mwa halmashauri ambazo tutakwenda kutenga fedha na kuhakikisha kwamba ujenzi wa hospitali ya halmashauri unaanza.
MHE. FESTO T. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza. Naomba kuuliza, changamoto ya barabara ya Kilindi – Gairo ni sawasawa kabisa na changamoto ya kutoka Isyonji Mbeya kuelekea Kitulo Makete, barabara ambayo ina urefu wa kilometa 97.6 na kwa muda mrefu imekuwa na changamoto wananchi wetu wa Makete wamekuwa wakipata changamoto.

Naomba kuuliza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa sababu ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano mfululizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Tuntemeke Sanga, Mbunge wa Makete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Sanga amekuwa anaifuatilia sana hii barabara ya Isyonje – Kitulo – Makete na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Sanga, Mbunge wa Makete kwamba barabara hii iko kwenye mpango wa ujenzi wa kiwango cha lami, kwa hiyo, labda tusubiri bajeti itakapopitishwa nadhani tutapata majibu sahihi zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, swali langu lilikuwa linaendana na haya mahusiano kati ya bodaboda na Trafiki na kule Makete mahusiano ya bodaboda na traffic ni kama Refa ambaye yuko uwanjani ana kadi nyekundu tu, mahusiano yao ni mabaya sana kwa kiwango ambacho Traffic wanatoza faini ya shilingi laki mbili, tofauti na utaratibu wa kawaida. Tumejaribu kufanya vikao vya negotiation kati ya sisi na watu wa Trafiki lakini imeshindikana. Pili, Traffic wanafuata bodaboda wangu mashambani kule Matamba, kule Makete, kitu ambacho ni kunyume na utaratibu. Sasa je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatupa kauli gani na maelekezo yapi kwa Trafiki Mkoa wa Njombe hususani Wilaya ya Makete dhidi ya vitendo viovu ambavyo vinafanywa na wao dhidi ya bodaboda wa Makete? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba sasa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utaratibu wetu kwenye PGO na utaratibu uliowekwa kwenye ile sheria au kanuni ya 168 ambayo imefanyiwa mabadiliko mwaka 2002, umesema ni Shilingi elfu thelathini, sasa kama kutatokezea askari au yoyote ambaye anayehusika na hili akawatoza watu zaidi ya kiwango kilichowekwa maana huyo anafanya kosa kwa mujibu wa taratibu kwa mujibu wa Sheria.

Mheshimiwa Spika, watu kuwafuata huko, unajua mtu anapokuwa mhalifu kwa mujibu wa utaratibu vyombo vinavyohusika kumkamata vina uwezo wa kumfuta popote alipo endapo amefanya makosa, lakini sasa hiyo namna ya kumfuata nayo ina utaratibu wake. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, kama kutakuwa kuna askari amechukua zaidi ya hizo, maana huyo anavunja sheria, nadhani Mheshimiwa tushirikiane katika hili kuweza kuwakamata na kama tunawajua tuwalete katika ofisi yetu, tujue namna ya kuwashughulikia kwa mujibu wa taratibu. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nilikuwa napenda kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Makete ya mwaka 2014 na Makete ya sasa ni ya tofauti sana. Kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imejengwa lami ambayo imefika hadi Makete, na kwa hiyo mabasi kutoka Dar es salaam na mikoa mingine tayari yameshaanza kuingia Makete.

Je, Serikali ipo tayari kutupatia fedha kutoka kwenye mpango wa miradi ya kimkakati ili Makete ipate kituo cha mabasi kizuri ambacho kinaendana na uhitaji mkubwa wa sasa ambao tunao?

Mheshimiwa Spika, jambo la pili; nakuomba Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili kama utakuwa tayari twende Makete kwa ajili ya kuangalia ukubwa wa uhitaji wa kituo cha mabasi pale ndani ya Wilaya ya Makete. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Festo Richard Sanga kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kuwatetea wananchi wa Jimbo la Makete katika miradi mbalimbali ya kiuchumi pamoja na ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, pili, nimhakikishie kwamba Serikali inatambua kwamba baada ya utekelezaji mzuri wa Ilani na barabara ya lami kutoka Njombe kwenda Makete, ambayo pia itatoka Makete kwenda Mbeya Mji wa Makete utafunguka na una kila sababu ya kupata stendi ya kisasa ya mabasi. Ndiyo maana katika katika jibu la msingi, na ninaomba niendelee kusisitiza, kwamba tunawashauri Halmashauri ya Makete, waandae andiko la kimkakati la ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa ambalo litaonesha business plan yake na uwezo wa kulipa fedha zile ili tuweze kutafuta vyanzo vya fedha, iwe Serikalini au kwa wadau mbalimbali, lakini pia na mapato ya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, tatu; nipo tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili. Naomba tukae ili tupange ratiba yetu tufike pale; pamoja na mambo mengine tuangalie ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi. Ahsante.