Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Festo Richard Sanga (2 total)

MHE. FESTO R. SANGA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarudia zoezi la kuweka alama za mipaka kwa kuwashirikisha wananchi ili kumaliza mgogoro uliopo wa mipaka kati ya Hifadhi ya Kitulo na wananchi wa Vijiji vya Misiwa, Makwalanga, Igofi na Nkondo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2016, Serikali ilishaweka alama za mipaka za kati kwenye maeneo ya Hifadhi ya Taifa Kitulo inayopakana na vijiji vya Misiwa, Mwakalanga, Igofi na mwaka 2018 katika Kijiji cha Nkondo.

Mheshimiwa Spika, zoezi hili la uwekaji wa alama lilishirikisha Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Makete, Waheshimiwa Madiwani, Serikali za Vijiji, wananchi kwa ngazi ya vijiji, pamoja na wataalam wa ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Makete. Elimu ilitolewa kwa wananchi kuhusu zoezi la uwekaji alama za mipaka kwenye vijiji hivi kabla ya uwekaji wa alama za mipaka hiyo. Baada ya utoaji wa elimu, wananchi walichagua wawakilishi watano katika kila kijiji ili kujiunga na timu ya watumishi kutoka Hifadhini na wataalam wa ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Makete, ili kufanya utambuzi wa eneo la mipaka na kuweka mipaka hiyo kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na.279 la Mwaka 2005 la uanzishwaji wa Hifadhi ya Taifa Kitulo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa kwamba maeneo hayo tajwa yalikwishawekewa alama za mipaka na zoezi hilo liliwashirikisha wananchi kikamilifu. Lengo kuu la zoezi hilo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa mipaka inaonekana bayana na pia shughuli za kibinadamu hazifanyiki ndani ya eneo la hifadhi.

Mheshimiwa Spika, ni imani yetu kwamba mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Taifa Kitulo na vijiji vilivyotajwa ulishapatiwa suluhu kwa kuzingatia Tangazo la Serikali na tunachokiomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano wao ili kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi.
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Stendi ya Mabasi Makete Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Festo Richard Sanga Mbunge wa Jimbo la Makete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Makete katika Mwaka wa Fedha 2013/2014 ilitenga eneo lenye ukubwa wa ekari 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2014/ 2015 Halmashauri ilianza ujenzi kwa gharama ya shilingi milioni 40; na katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Halmashauri imepanga kutenga fedha kwenye mapato ya ndani ili kuendelea na ujenzi wa kituo hicho

Mheshimiwa Spika, Serikali inaishauri Halmashauri ya Wilaya ya Makete kufanya tathimini ya ujenzi wa kituo cha mabasi na kuandaa andiko ili kutafuta vyanzo vya fedha kwa ajili ya ujenzi. Ahsante sana.