Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Festo Richard Sanga (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge hili, nipende kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa nafasi niliyoipata. Pia niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Makete kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mbunge wao. Kubwa zaidi nimpongeze Mheshimiwa Rais na Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa walioupata, ni kitu ambacho mimi kama Mbunge kwa kweli niseme hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais naomba kuchangia mambo matatu. Jambo la kwanza naomba kuchangia kwenye sekta ya barabara. Tumeona jitihada za Rais akipambana kuhakikisha kwamba barabara zinajengwa kwenye kila kona ya nchi hii, wilaya na kila mkoa. Kwa kule Makete sisi tumepata barabara kutoka Njombe kuelekea Makete ambayo imekamilika kwa kiwango cha lami. Naomba kuishauri na kuiomba Serikali tuna barabara ya kutoka Makete kuelekea Mbeya, moja kati ya barabara ambazo zimebeba msingi wa uchumi wa Wilaya ya Makete, nawaomba na nawasihi sana wahusika ambao ni Wizara ya Ujenzi waiangalie barabara hii kwa jicho la karibu ili wananchi wa Makete waweze kupata huduma hiyo ya barabara ya lami, kwa sababu uchumi wa Makete unakua lakini unakwamishwa na barabara hiyo ambayo kwa kweli ni barabara muhimu wa Wilaya ya Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naomba nichangie kwenye sekta ya kilimo. Sisi Makete ni wilaya ya kazi kama ambavyo wananchi wengi wa Tanzania wanafahamu wananchi wa Makete ni watu wa kazi. Kwenye kilimo Mheshimiwa Rais ameonyesha kwenye hotuba kwamba ana lengo la kuboresha kilimo. Changamoto ya kwanza kwa wananchi wa Makete tunalia na lumbesa kwa ajili ya wananchi wetu na wakulima wetu wa Makete. Wakulima wanalima lakini tatizo la lumbesa kwa wananchi wetu ni kubwa. Naishauri Serikali mambo matatu; ushauri wa kwanza kwenye Serikali ni jambo moja, kwanza Wakala wa Vipimo waoneshe kipimo kipi ni rasmi kwa ajili ya kuuzia mazao yetu ya mahindi pamoja na viazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naomba Wizara husika ya Kilimo waanzishe sales point (vituo vya kuuzia) ili wakulima wetu waweze kuwa controlled kwenye biashara kuondokana na suala la lumbesa. Lumbesa ni kilio, wananchi wangu wa Matamba, Makete na Ujuni wanalia na lumbesa, tunaomba sana ili tuweze kumboresha mkulima huyu lazima tuondoe suala la lumbesa na nawasihi na kuwaomba sana Wizara husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la tatu, naomba kuchangia kwenye suala la mapato. Rais amezungumza mambo mengi sana; hapa tuna mambo ya ujenzi wa barabara, tuna mambo ya umeme, tuna mambo mengi ya kiuchumi ambayo yanahitaji fedha, lakini kuna eneo moja ambalo tumeliacha kwa muda mrefu fedha nyingi zinapotea, nako ni kwenye suala la tozo, kwa maana ya kwamba non tax revenue. Rais amepambana kwa level yake, kwa maana ya kwamba ukiangalia kwenye eneo kama la vitambulisho vya wajasiriamali, mambo ya magawio saa hizi tumeanza kuyapata, naiomba na kuishauri Serikali waanzishe authority kwa maana non tax revenue authority ili iweze kukusanya tozo hizi ambazo zimekuwa zikipotea. Mambo ya fees na mengine yanapotea huko na wafanyabiashara wetu wengi wanahangaika kuona kwamba wanafuatwa fuatwa sana na watu ambao ni wa tozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ili tuwasaidie wafanyabiashara, ukifuatilia wafanyabiashara wengi ndani ya nchi yetu ya Tanzania wanaotaka kuanzisha biashara ndogondogo, wanafuatwa na watu wa tozo wengi wengi sana, mtu anaanzisha biashara, hajatulia anaingia mtu wa TBS, anaingia mtu wa NEMC, anaingia mtu wa OSHA, anaingia mtu wa Fire, anaingia mtu wa TFDA, mfanyabiashara huyo ambaye tunatamani awe bilionea kama Rais anavyotaka, atawezaje kama hatuwezi kuanzisha kitu ambacho ni kimoja, tuweza kuweka single point, huyu mtu akilipa kwa pamoja Serikali itafute jinsi gani inaweza ikagawana hayo mapato, siyo kufunga safari kwa kwa mfanyabiashara mmoja watu 20 kwenye Serikali ile ile. Naisihi na naiomba Serikali ianzishe Non Tax Revenue Authority ili tuweze ku-control hizi tozo ndogondogo ambazo zinapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo niendelee kumpongeza Rais hata kwa wenzetu tulionao humu ndani ya Bunge, wa upande wa pili, ni kwa sababu Rais aliruhusu demokrasia kwenye nchi hii ndiyo maana na wao wapo. Ninachowasihi ni jambo moja, wawe watulivu, walikotoka wanalaumiwa na hapa wanatulaumu sisi, sasa hawajielewi walipo, wafanyiwe counseling tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kupewa nafasi ili niweze kuwasilisha mambo machache ya kuishauri Serikali. Vilevile niishukuru Serikali kwa Mpango huu wa Miaka Mitano na hata huu wa Mwaka Mmoja ambao umeletwa mbele yetu kwa ajili ya kuujadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie mambo matatu. Jambo la kwanza ambalo nataka kulizungumzia ni kwenye sekta ya elimu. Kwenye sekta ya elimu nataka kuzungumzia jambo moja. Rais wetu tuliye naye kwa sasa alikuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba, kila shule inakuwa na madawati. Mpango huu ambao Rais alituletea hatujauona nini ambacho Serikali inapanga kwenda kukifanya kuhakikisha kwamba, kila mwaka shule zinakuwa na uhakika wa madawati kuliko kuwa na huu mtindo wa zimamoto. Sijaona mpango wa kuona Serikali na sekta ya viwanda wakijadiliana kwamba, wana uwezo wa kujenga angalau kiwanda kimoja cha kimkakati Mkoa wa Njombe au mkoa wowote ambao unatoa malighafi kama mbao, ili Serikali iweze kupata madawati kwa uhakika kwa ajili ya shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukulia mfano mwaka 1985, Mwalimu Nyerere aliamua kujenga kiwanda cha Mgololo kwa ajili ya karatasi, ili shule zetu ziwe na uhakika wa kupata madaftari. Kiwanda hiki kilifanikiwa, lakini kwa sasa kwenye hili suala la madawati hatuoni jitihada zozote ambazo zinafanyika za makusudi za Serikali kuona inajenga kiwanda ambacho kinaweza kikasaidia kupata furniture mbalimbali kwa ajili ya Serikali yetu na kwa ajili ya shule zetu. Sisi watu wa Mkoa wa Njombe tuko tayari ku-offer maeneo kama haya ya viwanda kusaidia Serikali yetu iweze kupata haya mambo ya madawati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nichangie; wewe ni Mbunge wa Kongwa, NARCO ilianzishwa kwa ajili ya kuendesha hifadhi za Taifa, lakini tumeona NARCO ikijikita kwenye kutatua tu migogoro. Miaka inaenda, miaka inarudi hifadhi ya Kongwa pale toka Nyerere alivyoiacha ng’ombe ni walewale inawezekana na idadi imepungua, hakuna ng’ombe wanaoongezeka. NARCO inafanya kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, wewe kwako Kongwa pale, kuna eneo kubwa ambalo hata Watanzania wangetengewa tu sehemu kidogo tu wapewe vile vitalu wafuge, angalau tungeona kwamba, kuna jitihada zinafanyika. Leo ukienda pale Ruvu mradi wa zaidi ya bilioni
5.7 wa machinjio ya kisasa umekufa. NARCO wapo na mambo yanaendelea, wamejikita Misenyi, wamejikita Kagera kwenye kutatua migogoro ya wafugaji tu, lakini NARCO haina mkakati wowote ambao tunauona kwenye Mpango hapa ukurasa wa 89, Kuendeleza Ranch za Taifa. Maeneo yamebaki ni makubwa, hayana msaada wowote kwa Watanzania, ni vema wananchi wangegawiwa, waweze kufuga ili Serikali iweze kukusanya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kwenye sekta ya wafanyabiashara. Hivi ninavyozungumza wafanyabiashara Makete, akina mama mafundi cherehani wanaambiwa wawe na mashine ya EFD. Ni masikitiko makubwa kwamba huyu mtu ana kitenge anashona anaambiwa awe na mashine ya EFD. Kodi now is not to collect they are just trying to grab it kitu ambacho siyo kizuri kwa sababu wananchi wetu wana uchumi mdogo, wana tozo nyingi lakini pili ukamuaji wake umekuwa ni wa tofauti. Hata ng’ombe unayemkamua unatafuta jinsi ya kumkamua, unamlisha, unazungumza naye lakini sisi TRA yetu hawafanyi jambo hilo, wanakusanya kodi kwa nguvu. Pia naendelea kusisitiza tozo ni nyingi na zimegeuka kero kwa wafanyabiashara wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasihi na naomba TRA watafute mazingira bora na salama. Mbona Rais ametusaidia vitambulisho vya wajasiriamali vimeondoa kero za wafanyabiashara wetu kukamatwa mitaani na mgambo, watafute njia sahihi ya kukusanya kodi. Nashauri wakusanye kodi kwa utaratibu siyo kutuma tax force kama Mheshimiwa Nape alivyosema, wanaenda wanakamata maofisi ya watu na kompyuta za watu, huyo mtu utegemee kesho akusaidie tena kulipa kodi? Ni jambo ambalo linasikitisha, tunaomba TRA wasaidie wafanyabiashara wetu wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama ambavyo leo tuna vitabu vinavyoonyesha kwamba Wizara ya Kilimo kuna tozo ambazo imeziondoa kwa maana kwamba ni tozo kero, ndivyo tunavyotamani kwamba keshokutwa kwenye Bunge linalofuata au Bunge la mwakani tuje na kitabu kutoka TRA kinachosema hizi tozo ambazo ni za hovyo kwa wafanyabiashara zimepungua kwa sababu wafanyabiashara wetu wanaumizwa. Vijana wadogo ajira mtaani hamna wakitaka kufungua biashara TRA wameingia, watu wa OSHA wameingia, watu wa Bima wameingia, watu wa lift wameingia yaani hadi kukagua lift kukagua ni Sh.400,000 kwa mwaka, lift? Sasa huyu mtu ata-survive vipi na tunatamani tuendelee kukusanya kodi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali hii nchi itajengwa na wenye moyo ambao ni sisi lakini kama mkiendelea kubomoa wafanyabiashara wadogo hatuwezi kukusanya kodi. Mwisho wa siku tunachoomba Wizara husika watuletee takwimu kama idadi ya wafanyabiashara inaongezeka au inapungua kwenye taifa hili. Kwa sababu kila siku wafanyabiashara wanalia kutokana na changamoto za tozo, wapunguze tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mchango mwingine nitaleta kwa maandishi lakini kwa kweli Watanzania wana matumaini makubwa na Mpango huu, naunga mkono hoja. (Makofi)