Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka (28 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wa kuchangia moja kwa moja ni mfupi ninachangia baadhi ya mambo kwa maandishi. Ninaunga mkono hoja. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake, pia ninampa pole Naibu Waziri Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kufiwa na mama, Mungu amrehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu ndiyo itafafanua mustakabali wa Taifa letu. Kwa hiyo, wote tu wadau. Ninaunga mkono hoja lakini ninatoa maoni na ushauri ambao Waziri akiufanyia kazi itasaidia sana. Nitajielekeza katika maeneo yafuatayo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka Na. 6 wa 2015 kuhusu elimu una mapungufu. Wakati ninaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais kwamba elimu ya msingi na sekondari ni bure, kwa maana italipiwa na Serikali ili kumpunguzia mzazi mzigo, ninashauri waraka huo uboreshwe. Ni wajibu wa jamii katika kuchangia elimu ili iwe bure huku miundombinu ikijengwa iweze kutekelezeka.
Hali ilivyo sasa inaonekana wajibu wa kuendeleza miundombinu umebaki tu kwa Serikali jambo ambalo ni mzigo mkubwa. Ushauri wangu ni kwamba wajibu wa kuchanga fedha za miundombinu elimu katika Kata uwe wa lazima katika jamii ili tusirudi nyuma. Momentum ya kuendeleza shule za Kata nazo ziwe na viwango. Duniani kote elimu huchangiwa na jamii, wazazi pekee hawawezi, Serikali pekee nayo ni vigumu kwa nchi kama yetu pamoja na nia nzuri sana ya Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumuunge mkono kwa kuhamasisha jamii ijenge madarasa, hosteli, maabara, ofisi, vyoo na kadhalika. Aidha, jamii ichangie madeski na mahitaji mengine ya kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya walimu wa sekondari katika Wilaya ya Muleba yanaonesha upungufu wa walimu wa sayansi wakati wa sanaa wametosha na kuzidi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Wizara itafute misaada ya walimu wote nje ya nchi ili shule ziwe na walimu. Mwaka 1960 Baba wa Taifa alitafuta msaada kutoka kwa Rais wa Marekani John Fitzgerald Kennedy walioitwa Peace Corps wakafundisha. Hatuwezi kuacha hii hali ambapo mwanafunzi anamaliza shule sekondari bila kumuona mwalimu wa hesabu. Naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza pia walimu wa ziada waondolewe katika shule za sekondari na pia kupelekwa shule za msingi ambazo bado hazina walimu wa kutosha. Aidha, katika manpower planning mahitaji ya walimu wa hesabu na sayansi zipewe kipaumbele. Walimu wanaweza kupewa retrovining program na kufundisha masomo yasiyo na walimu. Pia, unaweza ukaweka mobile teaching teams‟ za vipindi vya sayansi, walimu wachache waliopo wanatoka shule moja hadi nyingine. Pia kwa kuwa umeme na simu umesambaa uwezekano wa kutumia distant learning kutumia mtandao uangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litasaidia pia kuboresha viwango. Kwa vyovyote vile walimu wasiohitajika shuleni waondolewe. Muleba imekuwa na tatizo la baadhi ya walimu wa Kiswahili na Historia wasio na vipindi wanabaki kwenye majungu na kuvuruga utulivu na nidhamu shuleni. Hii imetokea shule ya sekondari Bureza ambapo baadhi ya walimu wasio na vipindi vya kutosha walivuruga nidhamu, jambo la kusikitisha baada ya ukaguzi kuliona hili na kupendekeza wahamishwe ni Mwalimu Mkuu aliyehamishwa katika mazingira yanayotakiwa kuchunguzwa. District Education Officer aeleze kwa nini ana muadhibu Mwalimu Mkuu anayefanya vizuri katika Wilaya nzima ili kuwafurahisha walimu wasio na nidhamu. Mheshimiwa Waziri afike Muleba aangalie hali duni ambayo tunayo hairidhishi na haitaleta tija wala matokeo mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya kuanza shule kwa hali tuliyonayo vijijini chekechea ianze na miaka 5 hadi 6 na shule ya msingi miaka 7 hadi 8 la sivyo, watoto wanakuwa wengi sana darasani na ukizingatia udogo wa watoto na uchache wa walimu, service ratios hazikubali inakuwa na shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ada elekezi katika shule binafsi, mjadala huu ni wa kushangaza, Wizara ya Elimu ina kazi nyingi na mimi sielewi kwa nini hili litusumbue. Wazazi wapewe elimu ya kutosha kuhusu ubora au mapungufu ya shule binafsi wanapopeleka watoto wao ili wapate value for money. Lakini kuchukulia shule binafsi kwamba ni biashara ni kushindwa kutambua elimu bora ilivyo huduma. Mimi sina mgongano wa maslahi lakini mdau katika sekta ya elimu. Niko katika taasisi ya Barbo Johnson Girls Education Trust- JOHA Trust inayomiliki shule mbili za sekondari; moja Dar es Salaam nyingine Bukoba. Shule hizi siyo biashara kama wengi wanavyodhani; shule hizi ni huduma kuwapa wasichana elimu bora. Shule ina utaratibu wa kutoa ufadhili kwa wasichana wenye vipaji lakini ambao hawana uwezo kulipa ada. Katika shule za JOHA trust ada inatofautiana kati ya wanafunzi kulingana na uwezo wao kiuchumi inaitwa assessed fees. Kuna wanafunzi wanapewa ufadhili wote na kuna wanalipa kinachoitwa fees zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hawa wanapewa ruzuku ya karibu milioni moja kwa sababu gharama halisi ni shilingi milioni 5.5 na full fees ni shilingi 4.5 milioni kwa sasa. Mheshimiwa Waziri awasikilize watoa elimu na kuwasaidia. Ni aibu kwa TRA kushinda kwenye shule kudai kodi badala ya utaratibu mzuri zaidi kwa kodi za lazima kukusanywa.
Hali ya sasa hivi imelalamikiwa sana na siyo rafiki kwa watu wanaosaidia kuelimisha Taifa letu. Kama kuna shule binafsi ambazo hazina viwango wazazi watazigundua. Kazi ya Wizara ni kutoa taarifa za ufaulu wa wanafunzi na hapa NECTA imefanya kazi nzuri ila ninashauri NECTA iwe inatangaza top 100 schools siyo top 10 maana shule zimekuwa nyingi, kwa hiyo top 10 ni kasumba ya mazoea. Tujue shule bora 100 kwa ujumla na katika vipindi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu viwe vinafanana. Mwisho ninashauri kuwa elimu pia inasimiko utamaduni, sasa kama vitabu viko tofauti tutajengaje utamaduni wa Taifa, culture harmony. Ninashauri utunzi wa vitabu ubaki kama ulivyo lakini Wizara iratibu na kuchagua vitabu vinavyofanya wanafunzi, kizazi au rika wawe na common reference point kupitia vitabu wavyosoma.
Mheshimiwa Spika naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba niungane na waliotangulia kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kuwa hapa leo katika Jumba hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kuanza kwa kusema kwamba naunga mkono hoja asilimia mia moja. Niwapongeze wananchi wa Tanzania kwamba katika uchaguzi uliopita Taifa limeibuka na kiongozi. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake na niwapongeze wananchi wa Tanzania kwa kumpa zana na silaha ya Urais. Maana ifike mahali tutofautishe kati ya urais na uongozi, vinaweza vikawa vitu viwili tofauti, inapokuwa kitu kimoja mambo yanaweza kwenda kwa kasi na inakuwa hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana pia Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri wetu Mkuu ambaye hakuna shaka anafanya kazi inayoonekana na sisi ambao tumepata bahati ya kumfahamu ni mtu ambaye anafanya kazi kwa umakini sana. Kwa hiyo, sina wasiwasi kabisa kwamba timu ya Baraza la Mawaziri ilivyopangwa kwa umakini Taifa hili linaweza likaiona neema na naona speed inaanza kuwapa wenzetu kiwewe. Wasiwe na kiwewe watulie kwa sababu kazi isipofanyika watu watalalamika kazi haifanyiki, sasa inapofanyika watu wanalalamika, hatuwezi kuwa na Taifa la walalamikaji tunataka Taifa la watu wa kujenga hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kuzungumzia kwamba Taifa letu sasa tunaingia katika awamu muhimu ambayo inatufafanua hata kwa ngazi za ulimwengu. Naomba nimpongeze sana Rais wetu kwamba katika diplomasia yake amefanya kitu ambacho wanadiplomasia wanakienzi sana, ameanzia kutembelea nchi jirani. Katika diplomosia iliyobobea hiyo ndiyo diplomasia kwa sababu unaanza kuwatembelea watu ambao wanaitwa your natural allies, watu ambao una maslahi nao kwa karibu sana. Kwa hiyo, ni jambo la kupongeza kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa bajeti iliyo mbele yetu nimeiangalia, nimeipitia kwa umakini sana, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba imekaa vizuri. Tunaposimama hapa kuchangia ni kuboresha hasa kwa upande wangu kuzungumzia mtazamo wa wananchi wa Muleba Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Muleba Kusini, hali yangu ilikuwa ngumu lakini mnaniona nimerejea mjengoni, ahsanteni sana Muleba Kusini. Waswahili wanasema ukweli ukidhihiri uongo hujitenga. Kwa hiyo, nimesimama hapa kwa mantiki hiyo na nataka kusema kwamba kazi inaendelea na tumeshapata watu wa kutuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mawaziri wamejipanga chini ya Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais na Mama Samia Suluhu ambaye ni kielelezo tosha kwamba wanawake tunaweza, naye nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninawawakilisha wakulima, wavuvi na wafugaji wa Muleba Kusini. Hali yao siyo nzuri sana, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nchemba alikuja akaona tuna matatizo ya wafugaji na wakulima. Hapa ninavyozungumza mifugo katika Mkoa wa Kagera iko kwenye hifadhi.
Kwa hiyo, naomba kabisa Mheshimiwa Waziri Mkuu na wewe utuwekee nguvu zako tuweze sasa kuhaulisha hii ardhi ambayo iko kwenye hifadhi ambazo zimepitwa na wakati tuweze kupata mahali pa kuchungia. Ni tatizo kubwa sana kwamba ukitaka kutoa mifugo ile kwenye hifadhi itabidi upeleke kwenye mashamba ya wakulima itazua migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo pia tusisahaulike sisi. Suala la mnyauko bado halijakaa sawasawa na magonjwa yanaibuka kila siku. Kituo chetu cha Utafiti cha Maruku kimesahaulika. Naomba Kituo cha Maruku kwa ajili ya Ukanda wa Mkoa wa Kagera kipewe kipaumbele na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hili utuunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo. Muleba ni wakulima wa maharage, migomba na nafaka mbalimbali lakini hatujawahi kuona vocha hata moja. Kwa hiyo, katika hili tumesahaulika na tunaposahaulika inakuwa njaa. Nakumbuka Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyestaafu aliwahi kunipa mahindi nipeleke Muleba, hii sio tabia yetu, lakini tukisahaulika katika uwezeshwaji, mambo yanakuwa magumu sana. Kwa hiyo, suala hili nalo tuliwekee mkazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikimbilie sasa kuzungumzia suala la miundombinu. Bahati nzuri nchi yetu sasa hivi inaendeshwa na wahandisi na mainjinia naona kila siku wanapangwa katika sehemu mbalimbali. Suala la reli halina mjadala, nchi haiwezi kuendelea bila reli. Nikizungumzia kwa mtazamo wa sehemu yoyote ile, ukienda nchi za Ulaya unakuta reli inafanana na mishipa ya damu, wanasema ni capillary system. Kwa sababu nchi ya kilimo kama haina reli haiwezi kushindana kwenye masoko ya dunia. Ukibeba mizigo, hususan mahindi, kahawa kwa ma-semi trailer huwezi kushindana katika uwanja wa dunia. Kwa hiyo, suala la reli lipewe mkazo, napongeza kwamba limepewa kipaumbele lakini tunazungumzia reli basically kwenda kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi watu wa Mkoa wa Kagera hususan Muleba Kusini, tunaomba kabisa Serikali hii Tukufu, chini ya Jemedari wetu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na chini ya Prime Minister, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, meli ya Ziwa Victoria imekuwa sasa lazima niseme aibu, imekuwa ni aibu ya Taifa wananchi wanasubiri meli. Wale watu walioangamia kwenye MV Bukoba wakiibuka leo zaidi ya miaka 20 baadaye hatujanunua meli jamani hatutapata mahali pa kukimbilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo niunganishe usalama katika Ziwa Victoria. Ziwa Victoria sasa hivi, wavuvi wenyewe ndiyo wameweka ulinzi wao shirikishi. Naomba sana Waziri wetu wa Mambo ya Ndani na hapa naomba Waziri Mkuu utuwekee nguvu kwamba ulinzi katika Ziwa Victoria uimarishwe kwa sababu wananchi wametelekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda siyo rafiki nikimbilie sasa suala la miundombinu hasa barabara. Nilishapiga magoti, kila jioni nasali tupate barabara ya kwenda kwenye Hospitali yetu Teule ya kutoka Muleba – Rubya. Hospitali Teule unapita kwenye mlima mkali na miamba, akina mama wanajifungua pale kwa sababu ya mtikisiko kwa ile barabara ilivyokuwa mbovu kwenye Mlima Kanyambogo. Sisi Muleba Kusini tupo tayari kuchapa kazi chini ya Jemedari wetu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na timu yake aliyoipanga na Waziri Mkuu lakini sasa msitusahau tuko mbali, lakini nashukuru kwamba Waziri Mkuu umshapita umeona wewe mwenyewe umbali wetu, kwa hiyo bila kuwekewa juhudi maalum mambo yatakuwa magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wale waliozungumzia suala la vijana na ajira. Tusipowawekea vijana wetu utaratibu wa ajira itakuwa vigumu. Sisi watu ambao tumeajiriwa tunapenda kuwaambia vijana wajiajiri, watajiajiri namna gani bila uwezeshwaji? Kwa hiyo, suala la kuwezesha vijana ni muhimu sana na uwezeshaji ni taasisi za Serikali kuweka mazingira wezeshi, siyo kuwa-harass wale vijana kama vyombo vya kuwafuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kulipa kodi, unamwezesha kijana, unaangalia accounts zake unaona kama kweli amepata faida, siyo kila mfanyabiashara anapata faida. Ifike mahali ijulikane kwamba mfanyabiashara pia anaweza akapata hasara na anapopata hasara itambuliwe. La sivyo vyombo vyetu vinaweza vikafunga small micro enterprises, viwanda vidogo vidogo vya vijana vikafungwa vyote kwa sababu ya harassment tukashindwa kwenda mbele kama Rais alivyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo ya kwangu na naomba niwasihi vijana kwamba dawa za kulevya ni hatari, UKIMWI ni hatari, lakini nasema na viroba ni hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme viroba ni hatari, navikemea Muleba Kusini, navikemea popote pale. Nilikuwa tayari kushindwa uchaguzi kama nikisema eti vijana wanywe viroba ndiyo wanipigie kura, wasinipigie kama ni mambo ya viroba. Kwa hiyo, suala la viroba ni hatari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ya Sweden, pombe inauzwa na Serikali, labda niseme maana yake Taifa hii limetusaidia sana. Katika nchi ya Sweden, Shirika la kuuza na kununua pombe Kali ni Shirika la Serikali, hili nalo tujifunze kutoka kwa hao wenzetu ambao wamepiga hatua katika yale ambayo yanatukwaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni wale ambao wanabeza juhudi za Rais, kwa mfano kusema mizigo imepungua bandarini, bandari yetu ya Dar es Salaam lazima tuiboreshe, kama mizigo imepungua ilikuwa hatuna faida nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda sio rafiki …
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha, naomba ukae.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja moja kwa moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kabisa kwa kusema kwamba naunga mkono hoja. Nampongeza sana mdogo wangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, amekaa vizuri na yameshasemwa mengi kwamba yeye ni mchezaji wa kukodisha. Nami nakubaliana na usemi huo. Maana yake ni kichwa, ametafutwa na sasa hivi nadhani nazi imepata mkunaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposimama hapa, baada ya kuyasema hayo, pia, nitoe masikitiko yangu makubwa kwa Naibu Waziri wake ambaye amempoteza mama na Waswahili wanasema, “aisifuye mvua, imemunyea.” Kwa hiyo, najua machungu anayopita, Mungu ailaze roho ya mama yetu, mahali pema Peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasimama hapa kwanza kabisa kama mdau wa elimu. Watu wengi wameshasema, wengine wanasema ni mgongano wa masilahi. Mimi sina mgongano wa masilahi ila I am interested party. Katika hili la elimu, natangaza kabisa, hii ni sekta ambayo Mwenyezi Mungu akinijalia maisha, ninalia nayo, nakufa nayo, nahangaika nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, maana yake Waheshimiwa Wabunge wote ambao mko ndani hapa, ni kwa sababu wazazi wetu katika nyakati mbalimbali na mazingira mbalimbali walitupeleka shule, ndiyo maana tuko hapa. Ni ufunguo wa maisha. Kwa hiyo, hii sekta ambayo tunaijadili leo, tunazungumza mustakabali wa Taifa hili na watoto wetu. Kwa hiyo, hapa ni lazima wachangie kwa uchungu; na wachangiaji wengi nasikia wanazungumza mambo yanatoka rohoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mfupi, siyo rafiki. Naomba nianze kwa kumwomba Mheshimiwa Waziri aangalie Waraka Na. 6 wa Elimu wa Mwaka 2015. Mheshimiwa Waziri unajua kwamba nilishawahi kuzungumza kwamba Waraka huu umeandikwa vizuri, lakini unatakiwa kuboreshwa. Ulivyoandikwa, sasa hivi ulivyokaa, sisi ambao tunawakilisha wananchi wetu katika mazingira ambayo bado elimu ni changamoto, unatuletea sintofahamu. Kwa sababu nimeona katika hotuba yako umefafanua jukumu la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, napongeza sana kwamba, Mheshimiwa Rais ameona yafaa kwamba Serikali ijaribu kutoa elimu bure kwa maana ya kwamba Serikali inagharamia elimu. Elimu unaposema iko bure inamaanisha, Serikali ndiyo inalipia elimu, wazazi wanakuwa wamepunguziwa mzigo. Kwa sababu kwamwe elimu haijawahi kuwa bure, lazima mlipaji apatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo basi, naomba nikupeleke kwenye Jimbo la Muleba Kusini ambalo limenituma hapa. Mheshimiwa Waziri, Waraka ule ulivyosimama, utakaposimama kujibu, naomba unipunguzie matatizo niliyonayo Muleba Kusini. Pale tuna Shule za Sekondari. Kwa mfano, tuna sekondari 44, wanafunzi 15,378, lakini hali ya shule zile bado madarasa hayatoshi, madawati hayatoshi, nyumba za Walimu hazitoshi, mabweni usizungumze, Maabara tunahangaika nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, ni muhimu sana Waraka ukatambua pia kwamba kwa kuwa sera yetu ya elimu ni bure, inamaanisha kwamba wazazi ndio wanatolewa mzigo wa kulazimisha watoto kushindwa kuja shule, lakini jamii inachangia. Nataka niseme kabisa kwamba ule Waraka una walakini sana kwa sababu unafanya kazi yetu iwe ngumu. Sijui wenzangu vipi, lakini Muleba Kusini watu wote wanashikilia elimu ni bure, hawataki kuchanga. Hawataki kuchanga katika hali ambayo Serikali Kuu haina fedha za kutosha kuweza kuenea na wengine wameshasema. (Makofi)
Kwa hiyo, kusudi tusijirudishe nyuma, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri, utakaposimama kujibu, ujaribu kutuelezea, utakavyotusaidia katika hili. Elimu ni bure, lakini pia lazima jamii ya Watanzania ilipe. Ni vizuri kwa sababu mwisho wa siku mtoto ni mali ya jamii, siyo mali ya mzazi. Mtoto ni mali ya jamaii, hilo nadhani nimelimaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimeshasema kwamba, mimi nimekuwa mdau wa elimu kwa muda mrefu; mimi ni Mwanaharakati wa Haki za akina mama, katika hilo wala sirudi nyuma, wala siombi radhi kwa mtu yeyote, ninasonga mbele. Sasa Wanawake ukiangalia, tumepiga hatua, lakini katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimeona hapa katika lile jedwali.
Katika udahili wa Vyuo Vikuu, bado wasichana ni asilimia 50. Bado hawajaweza kuwafikia wale wavulana. 7, 700 wasichana, wavulana wanaingia kwenye 15, 000 na zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona kwamba, bado changamoto ya mtoto wa kike bado iko unapozidi kupanda ngazi, ngazi za chini tuko sawasawa. Sasa shule zetu za Kata zimeleta mafanikio makubwa sana. Kama maendeleo yote, zimeleta changamoto! Shule za Kata ndizo tunataka kuhangaika nazo kwa sababu ndiyo mkombozi wa Taifa letu. Sasa hivi naipongeza Serikali ya CCM, imefanikisha kupunguza tatizo la Walimu katika shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nikupe mrejesho Mheshimiwa Waziri. Nikichukuwa Muleba tu, nilishasema ina shule za sekondari 44, ina wanafunzi 15,000 na Walimu wamepatikana. Katika Hesabu, tuna upungufu wa Walimu 86; na kuna shule 13 za sekondari Muleba, hazina Mwalimu wa Hesabu hata mmoja.
Katika hali hiyo, kama tunavyozungumza, shule ambayo haina Mwalimu wa Hesabu ni hatari sana. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hilo aliangalie, kama hajalifanyia kazi, lifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Biology, Muleba kuna shule nane hazina Mwalimu wa Biology, upungufu Walimu 47. Shule nane hazina Mwalimu wa Chemistry. Huwezi kutoa Mkemia pale! Huwezi kutoa Daktari pale! Shule 57 hazina walimu hao. Physics, hiyo ndiyo zahama kabisa! Walimu 80 wanakosekana. Shule 18 hazina Mwalimu wa Physics na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naendelea; Kiswahili, Muleba tumeletewa Walimu wa Kiswahili 85 wa ziada. Walimu 85 wa ziada wa Kiswahili, Walimu 80 wa ziada wa Historia, Walimu 30 wa ziada wa Jiografia. Napendekeza kwamba, haya ni maendeleo, lakini maendeleo yanataka mrejesho from the field. Nataka nipendekeze kwamba, baadhi ya Walimu hawa wangeweza kufanyiwa retraining wakatusaidia katika masomo mengine ambayo hayapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza pia kwamba Walimu hawa wanaweza wakapelekwa Shule za Msingi. Hii kasumba kwamba wanaotoka Chuo Kikuu wataishia Shule za Sekondari, nayo tuondokane nao. Pia nataka kusema kwamba shule inapokuwa haina Mwalimu wa Hesabu, hiyo ni crisis. Mwalimu Nyerere, sisi tulifundishwa na wamarekani, tulifundishwa na Walimu kutoka India. Mimi nafikiria kwamba…
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya kwanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini ni kengele ya kwanza. Niombe tu Mheshimiwa Waziri utakapo simama au utakapojiandaa na timu yako nzuri ya Makatibu Wakuu waliobobea katika elimu, mwangalie namna ya kutafuta misaada kutoka nje. Nadhani hatuwatendei watoto haki. Mtoto anamaliza Form Four hajawahi kukutana na Mwalimu wa Hesabu! Kwa kweli hapo tutakuwa hatuwatendei haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamesema mengi kuhusu shule binafisi. Mimi ninashiriki katika Taasisi zinazoendesha shule binafisi. Yameshasemwa mengi; elimu ni ya ghali, inaweza ikawa bure kwa sababu Serikali nzuri inaisimamia, lakini elimu ni ya ghali. Sasa hizi shule ambazo tunataka, wazazi wanafanya bidii, wanajiongeza. Nafikiria ifike mahali wazazi na wenyewe tutambue mchango wao. Sisi kama viongozi kusimama hapa na kusema tunaweka ada elekezi wakati wazazi wako tayari kulipa, kwani wazazi ni wajinga? Kwani wazazi hawana akili? (Makafi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia mtu, akasema kwamba Sukari ni pendekezo, lakini huwezi kulinganisha elimu na sukari; ni bidhaa tofauti. Ni bidhaa tofauti kabisa, ziko katika masoko tofauti na mtu yeyote anayeelewa elimu, anajua kwamba elimu ni huduma. Katika shule nzuri, elimu ni huduma, haiwezi kuwa biashara. Wengi wanasema; mimi nikitaka biashara nitauza Bia na kaka yangu Rugemalila, sitahangaika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitaka biashara sitahangaika na shule; shule siyo biashara. Ukitaka biashara unakwenda kwenye fast moving items; unauza bia, unauza nini na mambo yanakuwa mazuri. Elimu ni huduma! Sasa wale wanaotoa huduma, tuwatambue mchango wao, tuwaenzi. Katika nchi nyingine, wana utaratibu wa kupeleka fedha katika shule binafsi. Sasa sisi tuna utaratibu huu kidogo ambao unaweza kusema ni aibu kwa Taifa watu wa TRA kwenda kushinda kwenye shule wanatafuta kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo hayatusaidii, nayazungumza kwa dhati kabisa kwa sababu program tulionayo ni nzuri. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba hilo nilichangie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la haraka kama muda utaniruhusu, nizungumzie pia umuhimu…
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naomba nijue utaratibu ni dakika ngapi.
MWENYEKITI: Una dakika kumi.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi muda huu, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili kwa awamu hii kwa kikao hiki kwanza kabisa nianze na pongezi. Nawapongeza kwa dhati Wabunge wetu wapya wateule wa Mheshimiwa Rais ambao wameungana na sisi, uteuzi huo mimi mwenyewe umenifurahisha sana, natoa pongezi na nimefarijika sana kumuona Mwenyekiti wa Baraza la Wazazi wa CCM, Mheshimiwa Abdallah Bulembo akiwa na sisi. Hii ni waziwazi kwamba Mheshimiwa Rais anataka Bunge hili pia tuwe na weledi katika malezi ya vijana wetu, kwa hiyo hongereni sana. Pia nampongeza msomi mwenzangu, Mheshimiwa Profesa Kabudi ambaye na yeye ameungana na sisi na nitoe taarifa kwako Mheshimiwa Mwenyekiti kwamba jana sisi katika Bunge Readers’Club tayari tumeshaanza kumfaidi aliweza kutoa mada ya matumaini yake katika Bunge hili. Kwa hiyo, tunaona kwamba uzoefu wetu katika fani ya sheria ambazo tunatunga unaendelea kuongezeka. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mama Anne Kilango Malecela ambaye anarejea nyumbani, waswahili wanasema mwenda kwao siyo mtoro, hapa ni nyumbani kwake. Natoa pia pongezi zangu kwa Mheshimiwa Dkt. Possi ambaye amepangiwa kazi nyingine ambaye sasa hivi ni Balozi katika Diplomasia. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mkuu wetu mpya wa Majeshi aliyeteuliwa na kutoa pongezi zangu, ziwekwe on record, kwa Jenerali Mwamunyange ambaye amemaliza kipindi chake kwa utekelezaji uliotukuka, hapo hatuna budi kabisa kusema kwamba tulikuwa katika mikono salama na leo tunaangalia ulinzi na usalama wa Taifa hili. Naendelea pia kutoa pongezi zangu kwa….
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Ndiyo, kwa sababu ni sehemu ya ulinzi na usalama kama unashangaa ni conceptual framework, maana yake mambo haya huu ndiyo ulinzi na usalama wenyewe huu, kwa sababu watu wanafikiria kwamba ulinzi na usalama ni mitutu ya bunduki hapana, ni amani, ni maendeleo, ni upendo, ni kufahamiana ni kutambuana na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sina budi kuwapongeza waliokuwa kwenye uchaguzi mdogo, naipongeza CCM na mimi mwenyewe najipongeza kwa kushinda kwa kishindo na wenzetu nasema kwamba kujikwaa siyo kuanguka, lakini wapiga kura kwa kweli walikwenda vizuri kwa sababu ulikuwa ni uchaguzi wa amani. Kule kwangu Muleba ninapozungumza hili sina budi kuwatambua kabisa wananchi wa Muleba Kata ya Kimwani na kumpongeza Ndugu Daudi Kiruma aliyeibuka mshindi akaleta ushindi wa CCM. Niwashukuru sana watu wote walioshiriki katika zoezi hili ambalo lilikwenda katika hali ya ustaarabu na demokrasia ya kisasa, nawapongeza sana, ngazi ya Taifa hawakututupa, ngazi ya Mkoa, Wilaya mpaka kwenye Kata. Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mkoa wa Kagera, mimi ni mwakilishi kutoka Mkoa wa Kagera na katika hali ya kuangalia hali ya ulinzi, usalama na ujirani mwema wetu mnajua kwamba tulipata tetemeko na kwa mara nyingine tena ninatoa shukrani kwa mchango wa Waheshimiwa Wabunge ambao mlitupa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara ya Mheshimiwa Rais ambaye tarehe Mosi, mwaka huu alikuja akasali na Wanakagera, akatufariji na sisi tulifarijika. Nilishangaa sana kuona watu ambao wazungu wanasema watoa machozi ya mamba (crocodile tears) wakijaribu kubeza ziara hiyo iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanakagera tulifarijika sana na hasa tuliweza kupata misaada mbalimbali. Mheshimiwa Rais alikuja amejipanga vizuri alikuja na Balozi wa Uingereza ambaye atasaidia katika kurekebisha miundombinu. Mambo haya siyo haba, tumeyashuhudia. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba katika suala la kumshukuru Rais kuja kututembelea na hata Mheshimiwa Jenista aliandamana naye Mawaziri kadhaa walikuwepo pale nawashukuruni sana na changamoto waliziona. Sasa kitu kikubwa ambacho napenda kusema kinahusiana na mada ya sasa hivi ni kwamba makazi kwa wananchi wa Kagera yanaendelea kuwa ya wasiwasi kwa sababu watu ambao nyumba zao ziliporomoka wengi bado wako katika hali hatarishi kiulinzi na kiusalama. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nichukue nafasi hii kuomba kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama pia iangalie jambo hili kwa mapana yake na kuangalia sasa tunapojipanga na Waheshimiwa Mawaziri Serikali mnapojipanga, mnawasaidiaje wananchi ambao sasa hivi bado wanaendelea kuwa nje kwa sababu hawana makazi. Mheshimiwa Rais alifafanua vizuri sana, mimi naweza nikasema kwamba nimeshughulikia mambo ya maafa kwa ngazi za Kimataifa, Serikali huwa haijengi nyumba hata na Japan hawajengi nyumba hiyo ni international standard, jambo hili linaonekana geni kwa watu wengi lakini ndivyo zilivyo sheria za kimataifa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi ambalo tunaweka mezani kuwasaidia wale wahanga sasa kupata vifaa vya ujenzi kwa bei nafuu, ni suala la kiusalama na kiulinzi na kimiundombinu kwamba sasa hivi mtu ambaye nyumba yake imeporomoka sasa analipa kodi ya VAT kwenye mabati, kwenye simenti, kitu hiki kina ukakasi na tukiangalie sasa kwa mapana marefu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, dakika ngapi sasa hizi tano, bado ninazo tano, sawasawa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika zangu tano ambazo sasa zimebaki, naomba nianze na suala la ulinzi na usalama kabisa ambalo limeongelewa sana na watu, na ninaomba nikabidhi kwa rekodi ya Hansard, naomba nikabidhi barua ya Makamu wa Rais wa nchi ya tarehe 30, Mei alipositisha zoezi la kufukuza mifugo kutoka kwenye Mapori ya Akiba na Hifadhi nyingine ndogo ndogo. Kuna barua hapa naomba ipokelewe, wahudumu nisaidie, iwe kwenye rekodi za Hansard, sasa hao watu ambao wanaendelea kukiuka maagizo ya Makamu wa Rais wa Nchi kwamba zoezi hili limesitishwa wakati Serikali inajipanga watuambie wenyewe mamlaka yao wanayapata wapi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza sasa hivi, katika Wilaya ya Misenye kuna watu sasa hivi wanachomewa nyumba zao, kuna wafugaji ambao wanahangaishwa, kuna wafugaji wengine Wabunge wengine nimesikia mnasema watu wameuawa, ninaomba tusipopata maelezo ya kutosha basi Bunge hili liazimie kwamba tuwe na Judicial Enquiry katika vifo vinavyoendelea kwa wafugaji. Kwa sababu, haiwezi kukubalika, tuliona Operesheni Tokomeza ilipotufikisha, sasa inakuaje watu wanapigwa risasi na Maafisa Wanyamapori na inakuwa business as usual, jambo hili haliwezi kukubalika naomba barua ya Makamu iwe sehemu ya Hansard. Kama imefichwa iliandikwa kwa Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Bara wote, ninayo hapa naiweka for the record.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nisisitize, mimi kwangu Muleba tuna tatizo la usalama wa wavuvi, wavuvi wangu wanahangaishwa. Naomba Serikali itufafanulie, ulinzi wa wavuvi, wavuvi ni kama wametelekezwa inabidi walipe wao vituo vya Polisi, wajitafutie zana na mambo kama hayo. Kwa hiyo, naomba Kamati ya Ulinzi na Usalama ije itutembelee na akina mama katika Kamati ile na ninyi wawabebe kama wanavyonibeba mimi kuingia kwenye mitumbwi maana yake kule hakuna hata gatiza kuweza kupaki boti, ni suala la ulinzi na usalama ni suala nyeti, naomba lifanyiwe kazi kwa mtazamo huo. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ulinzi na usalama pia kuna suala la chakula. Kule kwangu Muleba sisi ni wakulima, tunafanya kazi kwa bidii lakini tulikuwa na ukame, kuna upungufu wa chakula, kwa hiyo chakula hakitoshi, na penyewe tuangaliwe kwa mtizamo huo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza wewe na timu yako jinsi unavyotuongoza. Pia nampongeza Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi nzuri aliyoifanya inayoonekana kwenye Mpango wa Miaka Mitano aliouleta. Aidha, naipongeza Kamati ya Bajeti kwa maoni yao yanayoleta nuru zaidi katika mikakati ya Maendeleo iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuokoa muda nitachangia kwa kuuliza maswali ya kimkakati (strategic questions) ambayo naamini yakijibiwa yataboresha Mpango mzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi sasa imepata Rais ambaye pia ni Kiongozi. Kwa hiyo, tuna mtu wa kutuonesha njia ili tujue tunakwenda wapi. Juhudi za Kinabii ambazo Rais, John Pombe Magufuli (JPM) anafanya nchi yetu inaweza sasa kuwa na mpango na kuutekeleza. Pia ninapochangia kwa kuuliza maswali naamini Mheshimiwa Waziri atayafanyia kazi na yale yanayohitaji mwongozo wa Kiongozi wa nchi atayawakilisha. Kwa mantiki hiyo, nauliza kimkakati yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, aya ya 12; kama mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 9.8 mwaka 2011 hadi alimilia 5.6 mwaka 2015, kwa nini riba katika mabenki yetu yote imebaki juu sana? Riba kubwa ya tarakimu mbili haiwezi kusaidia kusukuma shughuli za uzalishaji katika sekta husika (productive investments) riba za tarakimu mbili ni kwa wachuuzi wasiochangia uzalishaji mali na uwekezaji. Nini mkakati wa Serikali kutatua changamoto hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, aya ya 14; umaskini; ni jambo jema kwamba kama Taifa tumepunguza umaskini. Hata hivyo, ili jambo hili liaminike takwimu za umaskini ziwe zinatolewa kimkoa na kiwilaya ili mikakati iwekwe kulingana na eneo husika, ili mikakati iwekwe kulingana na eneo husika. Katika Jimbo langu la Muleba Kusini hali ya umaskini imeongezeka. Katika Jimbo langu Tunahitaji mikakati maalum inayohusu maisha na shughuli zetu, Mpango wa Miaka Mitano unahitaji kugatuliwa kwenda ngazi za wilaya na hata vijiji ili tupambane vizuri na hali halisi na kuweza kuboresha maisha yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja linalochangia Wilaya kama Muleba kubaki nyuma kimaendeleo ni kwa Taifa kutokuwa na specific program za Wilaya kubwa kieneo (geographic size) na wingi wa watu population size. Kwa Tanzania bara mgao wa fedha za maendeleo hauzingatii vigezo hivyo. Kwa hiyo, bajeti ya maendeleo inawasaidia zaidi wenye maeneo madogo kuliko wenye maeneo makubwa na watu wengi. Matokeo ni kugawa Mikoa, Wilaya, Vijiji na Majimbo vipande vipande, yaani hivi sasa kwa mtazamo wa kiuchumi kuna utitiri wa maeneo ya utawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la wazi kwamba, maeneo ya utawala yakiongezeka na gharama za uendeshaji wa Serikali zitaongezeka. Ingawaje kuna sehemu ambapo ugawaji wa maeneo yataleta ufanisi tusisahau kuwa teknolojia ya mawasiliano, usafiri na miundombinu bora inaondoa umuhimu huo. Kwa mfano, ilikuwa inachukua masaa 36 kuendesha gari kutoka Dar es salaam kwenda Bukoba, hivi sasa ni masaa 16. Kwa hiyo, kinachotakiwa ni mpango mkakati wa kuwa na Mipango ya Maendeleo ya Miaka Mitano na bajeti za kuitekeleza iliyojikita na inayozingatia na yenye uwiano wa ukubwa wa eneo na wingi wa watu waliomo kwa Tanzania Bara. Bila hivyo utakuta umaskini unaongezeka katika Mikoa na Wilaya kubwa.
Hii ni tofauti kabisa na malengo ya kuiendeleza Tanzania kwa misingi ya usawa iliyokuwa wenye Mpango wa Maendeleo wa Kwanza wa 1964-1963 (1st Year Development Plan) Mikoa kama Kagera ilitakiwa kupiga mark time kusubiri wengine, sasa imerudi nyuma na inashika mkia.
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unatakiwa kuwa na uchambuzi huu wa usalama na uwiano wa maendeleo ya mikoa- (regional equality). Bila hivyo umaskini na kutokuwa na usawa vinaweza kuwa chanzo cha vurugu na kuharibu amani na utulivu wa nchi yetu. Mheshimiwa Rais Magufuli, ana uwezo na upeo wa kurekebisha hali hii isiyoridhisha aliyoirithi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Uwekezaji (Ibara ya 28); Mpango unakiri kuwa uwekezaji wa sekta binafsi haukufikia malengo. Hili ni jambo zito linalohitaji kuchunguzwa kwa kina. Haitoshi na ni kujidanganya kujivunia uwepo wa rasilimali nyingi chini bila kuwa na uwezo kifedha, kiteknolojia na kiutawala (managerial capacity) kuziendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Maendeleo unahitaji kuweka bayana mikakati ya kuondoa balaa hili, kuwa na rasilimali ardhi bila uwezo wa kuitumia. Badala ya mashamba tuna mapori, tuna rasilimali maji, lakini samaki wanavunwa na Mataifa mengine kwa sababu ya uvuvi duni. Tuna rasilimali misitu lakini hatuna wataalam wa kuvuna misitu na kutengeneza fenicha za kuuza nje, tunaishia kuuza magogo na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya Matokeo Makubwa Sasa; jambo hili linahitaji kuangaliwa kwa kina lisijekutwa ni jipu. Mishahara mikubwa inayodaiwa kulipwa kwa Watendaji wa Sekretarieti hiyo ni vyema iwekwe wazi na katika kufanya hivyo sera na mpango wa mishahara endelevu ufafanuliwe kwa wote. Gharama za uendeshaji zikizidi mapato hatuwezi kwenda mbele, tutakwamba. Naunga Mkono uamuzi wa Mheshimiwa Rais, kutangaza mshahara wake na kupendekeza suala la mishahara mikubwa sana kuangaliwa upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu; kinachohitajika ni reli, reli, reli kila mahali. Bila hivyo ni vigumu kuendelea na kushindana katika kilimo. Aidha, barabara za vijijini (access roads) zipewe kipaumbele. Barabara ya Muleba – Kinyambogo - Rubya. Kwa kiwango cha lami ni mfano hai wa jinsi barabara za vijijini zinavyosahaulika. Naamini Mheshimiwa Magufuli atatusaidia kutekeleza jambo hili ambalo alilifanyia kazi alipokuwa Waziri wa Ujenzi.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naamini maswali yangu yakijibiwa tutafanya maendeleo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naomba niungane na Wabunge walio wengi walionipa pole katika mkasa ulionipata huko kwetu Wilaya ya Muleba kufiwa na Katibu wa UWT Bi. Paulina Francis aliyekuwa shujaa wa chama tawala na kwa kweli Wabunge wa Kagera tulio wengi humu ametusaidia, kwa hiyo, nasema kwamba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na waliotangulia kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Timu yake, Waziri wa Nchi na Manaibu na Makatibu Wakuu wao kazi wanayofanya inaonekana na kwa kweli ni nzuri inatia moyo na ni kazi ambayo inakwenda kwa ufanisi mkubwa, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nitakayoyasema ni kwa nia na mantiki ya kuboresha kwa sababu kazi ya Bunge ni kutathmini kazi za Serikali, kutoa maoni na kutoa ushauri, kwa hiyo, ieleweke hivyo lakini kazi ni nzuri. Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa muda mfupi ameonesha kwamba mambo yanawezekana. Kama alivyosema Mwalimu Nyerere it can be done, you play your part. Kwa hiyo, sasa sisi hapa kazi yetu tuna-play our part kwa kuonyesha zile changamoto ambazo tungeomba Waziri Mkuu kwa nafasi yake na nyingine ni za kisekta aandamane na wale watendaji wengine kuziboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mantiki hiyo basi naomba kabisa nianze na sekta muhimu sana, mimi ni mwakilishi wa wakulima, wavuvi na wafugaji. Wafugaji bado suala lao la ardhi ni kizungumkuti katika mikoa ya ziwa. Nasimama hapa tusisahau tulipotoka. Sasa hivi baada ya kuondolewa kwenye hifadhi kwa sababu ya kuzilinda, wengi wanahangaika na suala la ardhi ya ufugaji bado halijakamilika, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aweke nguvu yake mwenyewe kuhakikisha kwamba tunahitimisha jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa pia niko hapa kuwakilisha wavuvi, Mheshimiwa Chegeni ambaye amenitangulia kuzungumza hapa amezungumzia sintofahamu na kwa kweli dhahama iliyowakuta wavuvi naomba nipaze sauti kwa kusema kulinda ziwa ni lazima na ni wajibu wa kila mtu, lakini tunavyolinda ziwa nayo ni muhimu kwa sababu tunapigana na umaskini hatupigani na maskini. Wavuvi walio wengi kipato chao ni cha chini, nyavu zao ziliharibiwa kwa fujo na kwa kukomoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kabisa katika suala hili la kukomoana, Watanzania tuna tabia mbaya ya kukomoana. Mtu anapopata madaraka anamkomoa mwenzake hii haitaleta maendeleo. Kwa hiyo, nataka niseme kabisa kwamba wavuvi walikomolewa, sasa katika kukomoa wavuvi unasababisha ajira zikapotea. Kwa hiyo, hii dhana ya ajira kwa vijana, vijana walio wengi mikoa ya ziwa hususani Muleba Kusini wote wako ziwani ndiyo wanapata ajira. Sasa unaharibu zana zao za kazi badala ya kulinda ziwa, yaani mtu anaweza kusema kwamba ni total confusion sasa hapo unataka nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unakuta kwamba hili suala la watu kupata nafasi na kuzitumia kukomoa wenzao napenda kabisa niseme kwamba linatuharibia pale ambapo tungekwenda vizuri zaidi. Kwa hiyo, waliohusika na ukomoaji huu naomba wachukuliwe hatua stahiki kusudi isije ikajirudia tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la kahawa, wakulima Mheshimiwa Waziri Mkuu atambue kwamba wakulima wamenituma wako kwenye msiba mkubwa sana wakulima wa kahawa, kwa sababu utaratibu huu wa stakabadhi ghalani ambao ni utaratibu mzuri lakini una mazingira yake. Nikizungumza tu kama mtaalam wa sekta hizi ni kwamba kahawa iko tofauti na korosho. Unapouza kahawa wewe unayeuza kahawa ndiyo unahangaika nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba ni bias market, wale wanaonunua kahawa kuna kahawa nyingi duniani imefurika inabidi uwabembeleze. Unapouza korosho ni sellers market wewe mwenye mzigo ndiyo unatamba. Sasa naunga mkono kabisa nia ya Serikali ya kufufua ushirika. Katika hilo na kwa uelewa wangu naliunga mkono kwa dhati, lakini sasa ushirika tunaufufua vipi hatuwezi kuufufua kwa kukomoa wakulima sasa na kuwaambia kwamba lazima wote wauze kahawa yao kwa ushirika ambao haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake lazima tukiri kwamba ushirika ulishakufa wengine vyama vya msingi vingine vilishafungwa, kuna buibui na popo kule kwenye stoo, sasa hatujajipanga tunasema kwamba wanunuzi binafsi wasinunue. Naungana kabisa na dhana kwamba wanunuzi binafsi hawawezi kuendeleza wakulima wadogo wadogo, hili nalijua, nalijua tu kama economist nalijua kabisa, lakini sasa tutafufuaje ushirika wetu kusudi uwe na tija na uweze kuleta huduma stahiki kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muleba kule kwetu na Kagera kwa ujumla na naamini sehemu nyingine nyingi hata na majirani zangu Kigoma nasikia nao wako hoi. Sasa katika hali hiyo tunataka kusema kwamba suala la kufufua ushirika lisitangazwe kama tukio ni mchakato unaohitaji ulezi wa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala ambalo lisimamiwe na Waziri wa Sekta najua kwamba anafanya kazi yake kwa bidii, lakini anahitaji nguvu za Mheshimiwa Waziri Mkuu, hata na za Mheshimiwa Rais katika kuliongoza suala hili liende vizuri. Hali ilivyo sasa hivi wametangaza shilingi elfu moja kwa kilo wakati watu wanaweza kuuza elfu mbili jamani hata na sisi Wabunge humu posho yetu ikipunguzwa ghafla tutakubali? Kwa hiyo, hii ni dhahama kabisa, hivyo, naomba suala hili lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kabisa kwamba suala la miundombinu ni muhimu, suala la maji limeshaongelewa, nami naona kwamba tuweke mfuko wa maji, tuweke fedha stahiki lakini sina budi pia kumwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aangalie suala la barabara. Barabara hizi baada ya TARURA kuundwa tunaweza kujikuta katika hali ambapo wanaweza wakachukua fedha zote wakaweka kwenye barabara moja au daraja moja nyingine zikasimama kwa sababu hakuna usimamizi wa Halmashauri. Kwa hiyo suala la TARURA kuripoti kwenye Halmashauri limezungumziwa na wengi na naomba niliunge mkono na nilisisitize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu barabara ya kwenda Lubya wameshaitisha tenda mara tatu; mara ya kwanza wakasema kandarasi hakupatikana; mara ya pili kandarasi alipatikana baadaye wakasema mwenzake amejitoa; mara ya tatu mchakato unaendelea. Kwa hiyo, badala ya kupata barabara ambayo Mheshimiwa Rais ameisimamia, ni ahadi yake, sasa tupo kwenye mchezo wa kuchezeana na kukomoana. Nataka nisisitize suala la kukomoana kwamba halitajenga ustawi mzuri wa Taifa hili, litaturudisha nyuma na ndio tatizo ambalo naliona katika sekta nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa niseme kwamba ajira kwa vijana ni muhimu, lakini katika biashara zao lazima wale wa Serikali wawalee wale vijana. TRA hawawezi kuja wanafunga kila duka bila kuuliza wanakuja na minyororo wanafunga biashara. Sasa unapofunga biashara inamaanisha kwamba unaharibu ajira, kodi lazima zilipwe lakini sasa uweke utaratibu, you must go through the pain ya kuweka utaratibu sio kutafuta shortcut kwa kufunga badala ya kulea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba vyombo vyote vya Serikali Mheshimiwa Waziri Mkuu yeye ndiye ana sera na naona kuna Katibu Mkuu wa Sera hapa Profesa Kamuzola, watusaidie kusaidia kwamba regulatory authorities zote hazikomoi bali zinalea/zinajenga. Wazungu wanasema Roma haikujengwa kwa siku moja, mambo mengine ni polepole, kodi lazima zilipwe lakini pia kodi ziwe na mahesabu ambayo yamehakikiwa na auditors. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi za Ulaya kila mtu analipa kodi, lakini kila mtu anaweza audited accounts kwamba kipato changu ni hiki na kodi yangu ni hii, lakini sasa unakuta mtu hajawahi kufanya biashara hata kidogo lakini anaona kwamba kila biashara ina faida, sio kila biashara ina faida. Kuna biashara zingine zina hasara, kazi ya Serikali ni kuzilea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio mchango wangu lakini naunga mkono hoja na namalizia kwa kumpongeza Waziri Mkuu na kumkaribisha kuja Muleba, Muleba Mheshimiwa Waziri Mkuu nimemkaribisha lakini bado hatujamwona, tunamsubiri kwa hamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kabisa kwa kusema kwamba mimi hapa si kawaida yangu kukamata shilingi lakini katika hili ninaanza nalo kabisa.

Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla anafanya kazi nzuri na kwa utaalam. Mimi najua kwamba yeye ni Doctor of Medicine daktari wa binadamu, sasa daktari wa binadamu napenda kuamini kwamba kitu muhimu kuliko vyote kwake itakuwa ni kuliunda maisha ya binadamu. Sasa hali halisi katika hifadhi zetu kwa kweli namuangusha Mheshimiwa Waziri huyu ambaye tuna matumanini naye makubwa Kwa sababu hali ya hifadhi haijakaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, tutakuwa tunajidanganya katika taifa hili ambalo kwa kweli linaongozwa na Mheshimiwa Rais anayesifika dunia nzima kwa kutetea wanyonge sasa watu/ majirani wa hifadhi si wanyonge? Maana yake ukweli ni kwamba hadi tunapozungumza sasa hivi kuna sintofahamu karibu na vijiji jiraniya hifadhi, mapori ya akiba na game controlled areas kwa kweli hali yao sio nzuri, na ni wajibu wa sisi Wabunge kuyasema mambo kama yalivyo kusudi Serikali mpate taarifa muweze kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka juzi Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa mfano alisitisha zoezi la kutoa mifugo kwenye hifadhi kusudi Serikali ijipange watafute maeneo ya wafugaji. Suala hili halikufanyika; kwa hiyo maafisa wanyamapori na ninazungumza jambo ambalo nalijua kabisa, maana mimi katika jimbo langu Muleba Kusini tuna mapori ya Biharamulo, Buligi, Kimisi na kadhalika. Yanatokea kule kwa kweli wananchi hawawezi kutuelewa yasipofika katika Bunge hili na ninavyosikia taarifa za Tarime na kwingineko hali si nzuri; sasa tatizo ni nini na tufanye nini?

Mheshimiwa Spika, mimi ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba atambue kwamba dhana ya misitu ya akiba iliyo nyingi imepitwa na wakati kwa Mkoa wa Kagera, naomba kabisa Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa utueleze una programu gani ya kuendeleza utalii, misitu na hifadhi katika mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba kule achana na dhana ya Mapori ya Akiba ya Biharamulo na Kimisi na Buligi tangaza national park. Ukituletea programu ya kutangaza national park utakuwa na comprehensive program ya kufanya kazi na kuondokana na matatizo tuliyonayo sasa hivi, kwa sababu hizi shoroba ambazo nasikia mnaziweka hiyo ni kazi ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi. Tatizo linatokana na watu wa maliasili kujipimia ardhi, hamna mamlaka hayo, mimi najua na nilikuwa Waziri wa ardhi miaka mine, hayo mamlaka hamna. Tatizo linaanza kwa watu wa maliasili kuchukua kazi za surveyor ambaye yuko Wizara ya ardhi wanajipia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, hapa Kisarawe kuna msitu wa Kazimzumbwe imekuwa ni mtafaruku mkubwa sana kwa sababu walikosea wale watu wa Maliasili, wali- shift mpaka na Gurumeti ni hayo hayo.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kusema kwamba kusudi tuende mbele, Mheshimiwa Waziri Kigwangala mimi nina imani naye lakini sasa hivi nimemkumbusha fani yake kwamba wajibu ni kuanza kulinda maisha ya binadamu. Sasa hatuwezi kukubalika tukionekana kwamba tunalindaje raia wetu.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nishauri kwamba kwanza tu-certify mipaka na Waziri wa Ardhi amsaidie Waziri wa Maliasili ku-certify mipaka tujue hifadhi ni nini na wanyama hawa lazima wapate maji. Kwa mfano pale Serengeti kuna sehemu kwamba Serengeti haifikii Ziwa Victoria, shoroba za wanayama kufikia maji nazo ni muhimu. Nimesema kwa mfano kule Nyakabango kuna ushoroba kati ya Chato na Muleba kule kwangu tumeweka ushoroba wakati wa kiangazi lazima nyati waende kunywa maji kwenye ziwa.

Mheshimiwa Spika, sasa unaweza ukakuta njia kama hizo za wanyama zinawekwa, lakini ziwekwe kwa mujibu wa sheria na si kwa wanyamapori kupima mipaka kwa macho. Kwamba wanakaa hapo wanaamua kama mpaka unapitia hapa unapitia pale.

Mimi naomba kusema kwamba tuna hifadhi kusudi tupate mapato. Sisi kwa upande wa Kagera programu tunayohitaji sasa tunataka national park ili na sisi tuweze kupata watalii, maana sasa hivi wale maafisa wanyamapori wako mule wanachoma mkaa tu wala hakuna hifadhi yoyote utakayoweza kukamilisha. Unatoa mifugo, watu wanahangaika, lakini wale wanaendelea na biashara ya mkaa, kwa hiyo unakuta kwamba mazingira yanazidi kuharibika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kusema kwamba jambo hili ninaposema natoa shilingi naamini kwamba tunaweza kupata sasa mkakati wa kuendeleza kwa mfano upande wa Kagera tuna mifugo mingi.

Mheshimiwa Spika, hii tabia mbaya kila mtu anaitwa Mnyaruanda, Mganda, Mnyamkole, Mkenya, Mloita kama ni Wamasai wanasema wewe ni Mloita, kwa hiyo, ukienda kule Loliondo wanasema huyu ni Mloita huyu, ukienda Tarime unakuwa Mkenya, ukija Kagera kama mimi ndio Mnyamlenge asili. Sasa mambo hayo hayawezi kujenga Taifa hili, Taifa hili ni makabila mbalimbali na si dhana ya viongozi wa nchi hii wala chama tawala ninavyokielewa mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilitaka kusema kwamba tuenda scientifically, twende na programu na nishauri kwamba tuachane na biashara ya operesheni, hizi operesheni hatuna maslahi nazo, ni mabo ya kushtukiza ni mambo ya haraka na unakuwa huna proper program. Kwa hiyo nimeona niyaseme haya yawe on record.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kusema kwamba ninaposema tuwe na development program zitaondoa matatizo yote haya na wafugaji ambao kimsingi ndio problem kati ya hifadhi na wafugaji wapewe ardhi.

Mheshimiwa Spika, huwezi kuendeleza mifugo au utalii kama huna proper land demarcations. Sasa watalii kwa mfano wanapokuja kuangalia wanyama ndani ya hifadhi wanaona na watu wanachunga ng’ombe, hiyo nayo haitusaidii, inaweza ikafukuza watalii.

Mheshimiwa Spika, wanakuja kuangalia simba, nyati na faru, that is granted, lakini sasa hawa watu ambao wafugaji ardhi zao ambazo wametengewa ziko wapi? Tangu mwaka juzi, Serikali hii ya Awamu ya Tano naishukuru sana walitoa miezi kumi kwa Mawaziri kadhaa hapa kutafuta ardhi za ufugaji, hiyo kazi haikufanyika kilichotokea watu wakaja kuondolewa kwenye hifadhi kama operation na kwa kweli kwa mateso makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, niseme pia na niwe on record, ni utawala wa sheria. Kama mtu ameshinda mahakamani na unatakiwa arudishiwe mifugo yake ni lazima irudishwe, kama haipo lazima inunuliwe Serikali hapo ni lazima kuwajibika, ndiko kuwajibika kwenyewe huko, kuwajibika hakuwezi kuwa sehemu tu ya wananchi na Serikali nayo ni lazima iwajibike pale ambapo kosa limefanywa na watendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Muleba Kusini naomba nitaarifu kama tabia hii iko sehemu nyingine, kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Ndani lazima mtambue kwamba OCD maana yake ni Officer Command District, kwa hiyo officer wa Biharamulo OCD wa Biharamulo hawezi kuja kumkamata mtu wa Muleba bila OCD wa Muleba kujua kwa mfano. Kwa hiyo unakuta kwamba ni uvunjivu kunakuwa na ka-group la watu kanajiandaa kula rushwa na kutesa wananchi. Sasa jambo hili kwa sababu wananchi wengi hawaelewi sheria hii vizuri unashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kwangu wametoka Biharamulo kuja kuwakamata watu katika kata zangu za Nyakabango, Karambi, unasikia kwamba tumekamatwa na watu wa Biharamulo watu wa Biharamulo watawakamataje bila kufika kwa OCD wa Muleba? Kwa hiyo, ni matatizo kama hayo ambayo kwa kweli ni lazima niseme ukweli, na msema ukweli ni mpenzi wa Mungu jamani. Kwa mantiki hiyo nasema kwamba tusiharibiane utawala bora kwa sababu ya wale tuliowaweka chini tunapokwenda sisi wanatupa taarifa nzuri. Mheshimiwa Waziri nakukaribisha uje Muleba ujionee mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, mtu anatoka Buharamulo kuja kumkamata mwananchi tena Diwani, anakamatwa anapelekwa mahakamani anasumbuliwa kabisa yaani huwezi kuamini. Mimi nikienda kama Mbunge wanaponisimulia wakati mwingine hata na mimi nashindwa kuamini, kwamba hii haiwezi kutokea lakini ndivyo inavyotokea. Kwa hiyo, unakuta ni network ya watu kwa hiyo Mheshimiwa Waziri mimi suingi mkono hoja nangojea majibu ya Waziri, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nami sina budi kuungana na wachangiaji wa hapo awali kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpango na Naibu, Mheshimiwa Dkt. Kijaji na Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii ya Fedha ambayo kwa kweli ndiyo inakutanisha Serikali yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kusema kwamba mpango ni mzuri na kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, naomba kusema kwamba, mapendekezo yangu yanaenda moja kwa moja na Kamati yetu ya Bajeti ambayo sina budi kumpongeza Mwenyekiti wetu mahiri na Makamu wake, Mama Hawa Ghasia na Mheshimiwa Jitu. Kwa kweli, wanatuongoza vizuri na andiko lenyewe mnaliona kwamba limekaa vizuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, lililobaki ni Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Makamu wake ambao tunakutana nao mara kwa mara kutusaidia tu na sisi tuongeze zaidi yale tunayoyasema kwa namna ya ku-amplify. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, Mheshimiwa Waziri naunga mkono hoja iliyo mbele yetu, lakini nataka kufafanua mambo yafuatayo. Tuanze kabisa na Wizara yenyewe ya Fedha. Hii ni Wizara muhimu sana. Sina budi kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuunganisha Fedha na Mipango, lakini naanza kuwa na wasiwasi nikiona mipango inafifia chini ya fedha. Nami kama mchumi, nakuwa na wasiwasi mkubwa sana nisipolisema hili kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie jinsi atakavyolinda capacity ya National Plan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa na naomba ieleweke kwamba bila kuwa na Commission for National Economic Planning itakuwa vigumu sana kujua tunakokwenda. Tunaweza tukajikuta katika mchezo wa juhudi bila maarifa na Mwalimu Nyerere alionya dhidi ya mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana suala hili la hatima ya National Plan Commission, sasa hivi ikiwa inafanya kazi vizuri ndani ya Wizara hiyo sio shida, lakini inakuwa na enabling legal framework ambayo inaruhusu mambo ya mipango kufanyika. Hili naomba liwe mezani na Mheshimiwa Waziri atufafanulie sasa kwamba anajipangaje? Dhana ya Commission for National Economic Planning tunailindaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; kwa kuwa tunangalia sasa bajeti ya Serikali, kuna suala zima la Mamlaka ya Waziri mwenyewe huyu. Nimefurahi sana; na kama Mwanakamati wa Bajeti tunaipongeza Serikali kwamba hatimaye wamekubaliana na mapendekezo ya siku nyingi ya Kamati kwamba, Waziri wa Fedha arejeshewe mamlaka yake ya uamuzi wa kusamehe kodi pale inapostahili, hususan katika mikataba ya wahisani au miradi maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tupendekeze kama Kamati ilivyopendekeza kwamba mamlaka yake yasikomee kwenye miradi ya Serikali, lazima pia na Serikali ielewe kwamba, Halmashauri nazo ziweze kupata msamaha huu. Kwa hiyo, nafikiri mamlaka haya pia yawe total, yasiishie tu miradi ya Serikali, lakini yaende hata kwenye Halmashauri na miradi mingine inayoweza kupatikana yenye National interest.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kinachogomba ni lazima tuaminiane. Ifike mahali kama mtu amepewa dhamana ya Waziri wa Fedha, afanye kazi hiyo, tumwamini kwa sababu, tunajua kwamba atafanya in National interest. Tukiondoa mamlaka yake kisheria, anakwama na sisi tunakwama. Hilo naomba niliweke wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna dhana nzima ya ukuaji wa uchumi. Tunapongezana kwamba Tanzania ni kati ya nchi zinazokua kwa haraka, lakini mwisho wa siku ukuaji huu ni lazima uonekane pia kwa sura ya fedha za wananchi mifukoni au siyo? Kwa hiyo, sasa hivi wananchi walio wengi nadhani ni halali kusema kwamba hali yao siyo nzuri. Kama yale ninayoyaona Muleba Kusini kule kwangu kwa wale walionituma hapa, kwa kweli hali ni ngumu. Sasa tunafanyaje kusaidia wananchi wetu na wenyewe kuwa na ukwasi wa kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi kusema uchumi unakua, lakini hauonekani mifukoni mwa watu. Kuna njia mbili za kuboresha vipato vya wananchi. Njia moja ni direct income; Mheshimiwa Waziri hili analijua, lakini nyingine ni social income.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, unapoleta dhana ya elimu bure, hiyo, ni njia moja ya kuboresha ukwasi wa wananchi, hawana haja tena ya kufanya michango. Sasa zile direct income zime-shrink. Mheshimiwa Waziri anajua, ni Mchumi, zime-shrink kiasi cha kwamba social incomes zinakuwa na impact kidogo. Kwa hiyo, sasa hivi tuko kwenye shule za msingi, kule kwangu Muleba Kusini watoto wamekuja, lakini hawajanywa uji, hawajapata chakula kwa sababu vipato vya wazazi havitoshi. Kwa hiyo, nataka kusema sasa suala la kuboresha ukwasi kwa kaya ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi zinakua. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri lazima pia ajue kuwa kuna indirect taxes, hasa tozo. Kwa mfano, kule kwangu Muleba sasa hivi bado naendelea kusema kwamba huwezi kuwasaidia wananchi kama hawauzi kahawa yao kwa haraka na kwa bei nzuri. Kwa hiyo, bado suala la kahawa ni kizungumkuti na unakuta kwamba sasa mwananchi anakwenda kubebeshwa mzigo wa kulipa madeni ya ushirika ambayo hakuhusika nayo. Hii ni njia moja ya kumdanganya mapato yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kahawa kwa mfano, Sh.400/= zitakwenda kulipia deni ambalo wananchi walikuwa hawahusiki nalo. Namna hiyo, unawanyima yale mapato yao ambayo wangeyapata kama direct icome. Kwa hiyo, suala hili la kuboresha ukwasi wa wananchi ni sehemu kubwa ambayo Mheshimiwa Waziri atakapokuja, atuambie mikakati yake na hapo anahitaji wapangaji wake, Wachumi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyo mbele yetu, Kamati imeichambua kwa kweli kwa ufanisi mkubwa, lakini ukiangalia Deni la Taifa lilipofika hapa, naomba niseme kabisa, hii dhana ya kwamba deni ni himilivu, Mheshimiwa Waziri aje atuambie uhimilivu wake wakati linaswaga 49% ya mapato ya ndani. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba fedha nyingi zinapokwenda ku-service deni, hapo uhimilivu unaanza kuwa wa mashaka. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri a tuletee mikakati mizuri au majibu mazuri ya kutufanya comfortable, kutupa faraja kujua kwamba hili deni jamani tumejisahau wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati inaonesha kabisa kwamba uwezo; tunakopa zaidi, tunaendelea kutegemea kukopa, tunakusanya mapato ya ndani lakini yanaenda kwenye matumizi. Maendeleo yatakwama kwa sababu tunakopa na mikopo mingi ni mikopo ya kibiashara. Mheshimiwa Waziri ni lazima mkakati utafutwe kurudi kwenye mikopo ya bei nafuu ikiwemo kutafuta guarantees kutafuta ubia katika miradi mikubwa. Hata na Marekani mambo makubwa yamefanywa kwa ubia; Equity financing yamefanywa kwa government guarantees. Tukienda kichwa kichwa kwamba tunajitegemea, tunaweza kuja kuangukia pua. Nafikiri suala hili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku nchi hii imesimama kwenye dhana ya Siasa ni Kilimo katika; katika nchi hii mtu ni afya; hiyo ndiyo miradi ambayo tumeiona. Sasa nimeshangaa sana kuona Mfuko wa Maji nao umepata hatima ya kutokupata fedha zote ambazo tunakusanya ambazo zimepangiwa. Tukisahau maji, tumesahau kila kitu. Maana yake kama nilivyosema, afya; maji ndiyo uhai na afya ni kitu muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyotangazwa hapo awali, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Hafla ya jioni ambapo tunakusanya fedha. Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru sana kwa kuweka nguvu sasa katika kuboresha dhana ya usafi katika shule. Nataka niseme kwamba na mtoto wa kiume hatumsahau. Choo bora kinachojengwa kitajengwa pia na kwa watoto wa kiume na wenyewe watakuwa na sehemu yao na mtoto wa kike wana sehemu yao. Kwa hiyo, hili nalo nimeona nilifafanue. Tunamlenga mto wa kike lakini hatutaki kumwacha mwenzake nyuma. Kwa hiyo, tunakwenda pamoja kama tulivyo hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekti, nataka kusema kwamba Kamati ya Bajeti imefafanua mambo vizuri na sisi tunaongezea kama tulivyofanya, lakini hii dhana ya Mfuko Mkuu wa Serikali ni dhana nzuri, lakini kwani lazima imaanishe kwamba fedha zote hata zilizokusanywa na Halmashauri zije kwanza Hazina? Mfuko Mkuu wa Serikali kwangu mimi naona ni concept. Mheshimiwa Waziri nadhani anahitaji concept, wakati wote kweli Serikali Kuu tunakusanya nini? Siyo fedha zote zije pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. Naomba nianze kwa kuungana na walionitangulia kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wa TAMISEMI na Utumishi na Utawala Bora kwa kazi nzuri wanazofanya chini ya Ofisi ya Rais. Suala la utawala bora ni mtambuka na nyeti na ndiyo maana labda Wizara hizi zipo chini ya Ofisi ya Rais, kwa hiyo, hapa tunazungumzia mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo basi, nianze tu kwa kueleza kwamba mapema mwaka huu nilikuwa na changamoto za kiafya nikaenda kutibiwa Marekani nikapata nafasi kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katika maongozi yetu, alinipongeza sana na alisema maeneo yafuatavyo, namnukuu, alisema: “You know Anna Tanzania is unique”. Ina maana kwamba Tanzania ni nchi ya pekee. Akasema kwa sababu katika katika nchi za Afrika ni nchi ambayo ina utamaduni na inaonyesha kwamba ina uwezo wa kuwa na changamoto zake na ikazitatua yenyewe. Hayo ni maneno ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Kiingereza anaitwa Secretary General of the United Nations, kuna wenzetu hapa walikuwa wanataka kukusikia Kiingereza chake. Tulipofika hapa katika dhana nzima ya utawala bora, sina budi kuwapongeza majemedari wetu Waheshimiwa Mawaziri ambao wana dhamana ya sekta hizi na Mheshimiwa Rais kwamba tulipofika si haba. Hii ndiyo salamu ambayo naileta kutoka kwa marafiki zangu na watu wengine ambao niko nao, juzi juzi nimetoka nchi za Nordic tulipofika si hapa. Ukiangalia Rais alipoanzia katika kuleta utawala bora tulianza na janga la madawa ya kulevya…

MBUNGE FULANI: Aaaaa.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Kwa vyovyote mawazo yako juu ya mtu ni ya kwako lakini huwezi kusema mtu anayekuja kupambana na madawa ya kulevya atapata marafiki, hilo ni la kwanza na dunia inalitambua. Tukaingia katika changamoto ya mikataba mibovu iliyokuwa inatuumiza sana kwenye madini tukalikamilisha na mengine yanakuja. Kwa hiyo, katika dhana ya utawala bora, nafikiria Taifa zima bila kuangalia itikadi ya mtu tunatakiwa tuwe pamoja kuhakikisha kwamba tunaimarisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe kwa maumbile yangu (by inclination) ni mtu ambaye napenda sana hoja, ushindani na upinzani kama ikiwa lazima. Tunapozungumzia utawala bora lazima pia tuzungumzie upinzani bora maana hatuwezi kuwa na utawala bora kama hatuna upinzani bora, kwa sababu upinzani bora ndiyo utaleta utawala bora. Kwa hiyo, nataka kusema tunapokaa hapa wakati mwingine tunasahau context ya tunachotaka kufanya hapa.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa, kidogo tusikie taarifa, Mheshimiwa Mwakagenda.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuumpa taarifa mzungumzaji anayeongea ambaye ni Profesa Mbobevu katika nchi hii. Nataka kumpa taarifa kwamba alipokuwa anaongea na huyo Kiongozi wa UN angemueleza kwamba upinzani bora unahitaji fairness. Kwa hiyo, nilifikiri kwamba angemsaidia na kumpa uwazi wa kinachofanyika katika Taifa letu. Mheshimiwa Profesa nataka nikukumbushe nawe ulikuwa Waziri wa awamu zilizopita na madawa hayo hayo yalikuwepo wakati wewe ukiwa Waziri. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa, taarifa hiyo.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mwakagenda kwa hiyo perspective yake. Nimeshasema mimi ni mtu ambaye nakaribisha mawazo mbadala ila naweza kumhakikishia maongezi yangu na Katibu Mkuu yaligusa mambo yote hayo na zaidi. Cha msingi ni kwamba Tanzania is unique, tulipofika ni pazuri na tujipongeze na Rais wetu anakwenda vizuri Mheshimiwa Mwakagenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde dakika zangu alizozichukua Mheshimiwa Mwakagenda. Baba Mtakatifu Francis katika kazi yake ya kujaribu ku-promote utawala bora na uongozi wa kiroho alikuwa katika nchi za Uarabuni alifika Dubai, alitoa nasaha ambazo kwa ukosefu muda sitaweza kuzisoma hapa lakini naomba nikabidhi nyaraka hii kama sehemu ya Hansard ya hotoba yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba Mtakafitu anasema ni lazima tujue changamoto zipo, tatizo siyo changamoto, tatizo siyo watu wanakusema, tatizo siyo kwamba watu wanakuonea, tatizo ni wewe una-respond namna gani? Kwa hiyo, usikubali mtu yeyote aku-pull down, wewe weka hoja mezani, nyaraka hii naikabidhi ili isaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukiona kwenye mitandao Baba Mtakatifu anahakangaika na wenzetu wa South Sudan. South Sudan watu hawaelewani, sasa Baba Mtakatifu ameamua kuwapigia magoti, mtaona kwenye mitandao nadhani ina-trend, utawala bora pia unaamanisha dhamira zetu, kama unataka utawala bora lazima uangalie pia dhamira zetu. Kwa mantiki hiyo basi na kwa sifa tulizonazo tusizipoteze kwa kuokosa nation dialog. Ni kwa mantiki hiyo basi nataka kuchangia ifuatavyo:-

Mhehimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa utawala bora utataka utawala wa sheria na haki. Utawala bora lazima utokane na sheria na haki, sheria peke yake bila haki haiwezi kuleta utawala bora. Kwa mantiki hiyo, nataka kusema kwamba suala la haki Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, naomba liangaliwe kwa umakini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka (DPP) ni lazima ijiangalie pia kwa sababu huwezi kuwaweka watu gerezani bila kusikiliza kesi zao ukasema nina utawala bora. Hiyo naiweka kwa perspective niliyosema kwamba hapa tunachangia, hili ni Bunge la Jamhuri, tatizo letu hapa huwa ni ideologies zinatufanya tunashindwa kwenda forward. Kama mtu unatuhumiwa una makosa ni sawa lakini wachunguzi kama hawajawa na ushahidi, kusudi tukae vizuri mbele ya Mataifa na majirani wanaotuangalia na humu ndani, naomba suala hilo tuliangalie na nalisema hili bila kuwa na usabiki wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa, muda wako umeisha.

WABUNGE FULANI: Aaaaaa.

MBUNGE FULANI: Mwongezee.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Dakika tano, bado jamani, sijui kama nimeongea dakika tano. Kama nimemaliza dakika zangu nitaweka…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tibaijuka, kwa sababu Kanuni pia zinatambua watu fulani ambao wametoa mchango mkubwa kwa nchi hii na kwa Bunge hili, kwa hiyo, nakuongezea dakika tano. (Makofi/Kicheko)

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa heshima hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, naomba niende haraka na nitaweka hapa mchango wangu kama ulivyoandikwa, kwa sababu mimi ni Profesa nimeandika uingie wote kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya muhimu ya kusema, niende kwenye suala la kuwezesha watu wetu katika utawala bora, kuna suala la kuwalipa wakandarasi wa ndani. Wakandarasi wa ndani sasa hivi Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa nalileta kwenu ni suala la utawala bora kwa sababu wasipolipwa fedha hawawezi kufanya kazi, hatuwezi kujijengea uwezo, tutabaki na Wachina peke yao. Kwa sababu ya muda umekuwa mfupi nimelifafanua katika hotuba yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nikupe nyaraka nyingine ambapo kuna kitu kinaitwa Ilani ya Usafi. Utawala bora pia ni mkono wa Serikali wa kushoto kujua wa kulia unafanya nini. Sasa hivi kuna tabia mbaya, naomba niseme kwamba Maafisa Afya na Mazingira wanakwenda kwenye shule binafsi na hapa na-declare interest kwa sababu nina shule, wanategemea uwape bahasha kama bahasha haipo imekula kwako, unakuta unaandikiwa Ilani Chafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikukabidhi Ilani moja hapa ambayo imeandikwa kwenye Shule ya Wasichana ya Barbro ambayo huwa naisaidia, inasema tuong’oe vyoo (WCs) kama hivi hapa Bungeni tuweke vyoo vya kuchuchumaa. Hata hivyo, Bwana Afya hajui kwamba kwa wanawake kuchuchumaa inaweza pia ikaeneza UTI, hapa ndipo tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalileta jambo hili hapa mtu atashangaa kuwa ni la kisekta, siyo la kisekta ni la kiutawala bora. Sheria ya Elimu ndiyo inatawala shule, watu wa mazingira na watu wengine wale wakitaka kuingia kwenye shule lazima waende na Mkaguzi wa Shule, vitu kama hivi havifanyiki vinatuletea matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijakaa hili lazima niliseme ni muhumu sana, naomba sana Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa na nadhani na Mheshimiwa Rais pia atatusikia ni kuhusu suala la watumishi walioachishwa kazi kwa sababu walidai kwamba wamemaliza form four wakati hawakumaliza, naomba tena Mheshimiwa Rais atumie huruma na hekima yake kuliangalia upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa nafasi yangu ukiniuliza nasema kuna wengine walijaza form wakisema kwamba wana form four kwa sababu mabosi wao waliwaambia jaza form four. Tuje humu Bungeni, Mheshimiwa Lusinde leo sijui kama yupo au hayupo yeye huwa anapenda kujiita darasa la saba lakini namjua ana-masters ni kwamba hana cheti tu. Unaona ni persepective tu huwezi kusema Mheshimiwa Lusinde ni darasa la saba siyo darasa la saba huyu, kwa elimu yake ana-masters na zaidi lakini kwa sababu ya certification ndiyo tusema darasa la saba, sisi tumekwama kwenye certification tunashindwa kwenda mbele. Kwa hiyo, naomba niseme jamani, jamani suala hili ni muhimu sana kuangaliwa upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kutunza vyeti, siyo kazi ya individual. Ni kazi ya NACTE, BRELA, Wizara ya Ardhi na wengine. Sisi raia hatuna safe ambayo ni fireproof kwa mfano. Kwa hiyo, cheti changu kikiungua nakwenda NACTE kuomba cheti changu. Sasa nina kesi za watu ambao ni Maprofesa, wamesimamishwa kazi katika Vyuo Vikuu kwa sababu walipoteza vyeti vya Form Four. This is not serious. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nitaleta kwa maandishi. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa FAO wa Kuzuia Uvuvi Haramu kupitia Bandari za Nchi Wanachama pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (The Framework Agreement on the Establishment of International Solar Alliance)
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mimi pia naomba niungane na waliotangulia kuwapongezeni Waheshimiwa Mawaziri wote wawili waliotuletea mikataba hii ya Kimataifa kusudi na sisi tuweze kuiridhia. Katika uchangiaji wangu, ni jambo zuri na wote kama ilivyosema, hasa ule mkataba wa FAO, nataka kusema kwamba ni mkataba umekuwepo kwa muda mrefu mimi nimeushuhudia wakifanyiwa kazi bado niko huko Umoja wa Mataifa. Sasa niseme kwamba labda ni muhimu sana kusema, kwamba kwa kuwa tumechelewa kidogo kuridhia mikataba hii mimi nimefarijika sana kuona kwamba katika Bunge hili Tukufu inaonekana pande zote tunakubaliana kwamba turidhie, kwa hiyo naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa katika kuridhia hilo na Serikali katika kutupa taarifa nina mambo mawili ya kusema. Kwanza naomba Mheshimiwa Waziri wetu wa Mifugo na Uvuvi ajaribu kuangalia kwa wenzake hali tuliyo nayo huko katika bahari kuu. Maana ninachofahamu mimi ni kwamba sisi Tanzania tuna haki ya kupewa eneo zaidi katika bahari kuu ambayo bado tunalidai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi hiyo imekwama kule Umoja wa Mataifa na nadhani sasa Mheshimiwa Waziri Mpina wewe ndiwe mhamasishaji, wewe ndiwe mwenye samaki, wewe ndiwe mwenye viumbe kule baharini. Nadhani ni muhimu kuangalia mchakato wa kudai extended continental shelf ya Tanzania umefikia wapi. Kazi naifahamu kwa sababu mwaka 2012 nikiwa Waziri wa Ardhi niliwakilisha Umoja wa Mataifa New York kwenye kamati husika ya International Convention on the Taw of The Sea, kudai eneo letu. Sasa tusipoangalia tunaweza tukaridhia mikataba hii lakini kuna sheria zinazotawala utawala wa maji duniani, International Law of the Sea. Labda ingekuwa ni vizuri kulijulisha Bunge hili mchakato huo umefikia wapi.

Mheshimiwa Spika, labda kwa kufafanua zaidi; ni kwamba tumesikia hapa, na kamati imezungumza vizuri, kwamba exclusive economic zone ni nautical mile 200 unapewa baada ya maji yako (territorial waters). Lakini Tanzania kwa sababu ya mito yetu, hususan Mito ya Rufiji, Pangani, Wami; ndiyo inalisha viumbe baharibini. Kwa sababu hiyo tunastahili kupewa nautical mile 150 zaidi ndani ya bahari.

Mheshimiwa Spika, sasa hiyo ni hazina kubwa ya Taifa, na ninadhani kwamba Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi aangalie na wenzake wanaohusika hususani Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Waziri wa Ardhi kwamba hatupotezi hazina hiyo, kwa sababu unapopeleka maombi Umoja wa Mataifa kuna muda usipofatilia unaweza ukaondolewa kwenye orodha. Kwa hiy ni jambo ambalo nimeona kwamba niliseme na huu ni wakati wake.

Mheshimiwa Spika, tunaporidhia mkataba huu pia tujue utawala wa bahari duniani na tutaweza kudhibiti huo uvuvi haramu katika bahari zetu. Suala la uvuvi haramu nadhani ni suala ambalo wote tunakubaliana kwamba ni suala hatari lakini pia ni suala la teknolojia na sisi kama nchi inayoendelea wakati mwingine tufaidike kwa kuomba misaada pale tunapohitaji. Kwa sababu uwezo pia wa kudhibiti hizi meli kubwa, gharama inayohitajika na teknolojia inayohitajika unaweza kukuta kwamba hatuna. Tukisharidhia mkataba kama huu na sisi basi; na imesemwa na wengine; tunaweza pia kuomba msaada wa wataalamu, vifaa na fedha za kutusaidia kuhakikisha kwamba hapa kwenye bahari yetu kuu si inakuwa shamba la bibi, kwamba kila mtu anafanya anachotaka na hasa uchafuzi wa sumu zinazotupwa katika bahari yetu.

Mheshimiwa Spika, ilifikia kuna mahali pale wala siendi mbali pale Kawe Beach waliwahi kutupa magunia ya sumu hatari kwa hiyo unakuta vitu kama hivi wanaendelea kwa sababu hatujajua...

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Ndio taarifa tafadhali Mheshimiwa Zungu

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Profesa. Kwanza nimpongeze kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha extended ya continental shelf ya Tanzania na kupata hizo km 150. Juzi mimi nilikuwa umoja wa mataifa tumelifatilia hili suala tuko katika namba 59 ya shauri la Umoja wa Mataifa na limekaa vizuri. Tatizo vikao vya Umoja wa Mataifa havikai kutokana nchi wanachama ambao wako kwenye commission ile wanatakiwa walipiwe gharama zao za kuhudhuria vikao na nchi zao kwa vile nchi zao hazilipi gharama ile commission haikai. Kwa kutokukaa justice delayed justice denied tunakosa haki yetu.

Mheshimiwa Spika, vilevile Kenya nao wana shauri na Somalia na shauri lile linaweza likatuathiri kama Somalia wakishinda kutokana na mpaka kati ya Kenya na Pemba. Kwa hiyo nilitaka nimpe taarifa tu kwamba suala liko vizuri Serikali wanalifuatilia na kamati tuko karibu nao kuhakikisha haki ya Tanzania inapatikana. (Makofi)

SPIKA: Asante sana ni kweli Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje alikuwa UN kwenye General Assembly akifatana na Waziri wa Mambo ya Nje hivi juzi tu. Mheshimiwa Profesa Tibaijuka endelea na mchango wako.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nchi za Nje na nimefarijika kusikia kwamba suala hilo linafatiliwa ni muhimu sana. Sasa nikirudi kwenye uwezo wetu wa kutekeleza hii mikataba tukishasaini. Sisi ni nchi inayoendelea, bado tuna haki ya kupata msaada wa hao wenzetu waliotangulia. Kwa kweli wenyewe kwa sababu ya teknolojia zao ndio wana uwezo wa kuchafua na kutumia hizi mbinu haramu ambazo zinakuwa na athari kubwa. Kwa hiyo tusibaki nyuma, Mheshimiwa Waziri usibaki nyuma katika kuweka sasa ufatiliaji ambao ni chanya. Kuna ufatiliaji mwingine ni urasimu tu mtu hana vifaa atakaa anasumbua meli anaweza akaleta kero.

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiria kwamba tufanye kazi kwa weledi kwa sababu tunaposema tuweke watu wa kudhibiti, je, wana uwezo wa kudhibiti? Wanakuja kufanya juhudi au kama Mwalimu Nyerere alivyosema, kwamba ni juhudi bila maarifa. Suala hili ni muhimu sana hasa katika vyombo tunavyojiwekea kudhibiti.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili nirudi sasa kwa haraka kwenye suala la mkataba wa umeme wa jua. Umeme wa solar huu na umeme wa jua ni kitu kizuri sana. Naomba kusema kwamba sisi kitu kimoja kinachotukwaza kama taifa linaloendelea na kama taifa lenye vijana na vijana ambao hawana ajira ni kushindwa kuweka utaratibu kwa vijana kuunda kampuni za solar zitakazoweza kuleta teknolojia katika nyumba na kutoa huduma.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nirudi sasa kwa haraka kwenye suala la mkataba wa umeme wa jua. Umeme wa solar huu na umeme wa jua ni kitu kizuri sana. Naomba kusema kwamba lakini sisi kitu kimoja kinachotukwaza kama Taifa linaloendelea na kama Taifa lenye vijana na vijana ambao hawana ajira ni kule kushindwa kuweka utaratibu kwa vijana kuunda makampuni ya solar yatakayoweza kuleta teknolojia katika majumba na kutoa huduma. Kutegemea TANESCO bila kutumia solar ni kutwanga maji kwenye kinu kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, nafikiri ingekuwa ni bora Mheshimiwa Waziri akatueleza sasa anavyojaribu kusaidia vijana wetu hawa ambao tunawaambia wajiajiri wakati sisi tumeajiriwa, lakini hatuwawekei utaratibu wa kwa mfano kuunda kampuni mahususi ambazo zitaweza kueneza umeme wa solar; vijana wanamaliza Engineering wapo kule mijini hawana kazi.

Mheshimiwa Spika, nadhani tunaposaini mkataba kama huu ni fursa muafaka pia kuwapatia teknolojia, lakini na huduma inayotakiwa maana yake unaposambaza kitu kipya kina ukakasi, ukiwaambia watu tukufungie solar yeye anaona nyaya za TANESCO zinapita juu anaona unamsumbua kama unamfanyia shamba la majaribio, kwa hiyo mtu anataka kitu ambacho ana uzoefu nacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukiwa na vijana ambao wanaweka makampuni ya kuhakikisha kwamba yanapata soko, sasa kazi yetu nini? Kazi yetu ni halmashauri, kuweka sehemu ili ziwape masoko inaitwa public procurement ambayo ni lazima iwezeshe dissemination ya teknolojia, teknolojia mpya haiwezi kusambaa kama haina Public Procurement Policy inayoi-support yaani kwamba kule kununua kwa upendeleo kabisa kampuni za vijana, ndiyo tutaweza kuondokana na hii ngonjera ya umeme wa solar umeme wa solar, lakini watu hawapo tayari kuwa kwenye majaribio, tuwawekee uwezeshaji.

Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mchango wangu, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, na mimi sina budi kwanza kabisa kuungana na Bunge zima kumpa pole sana familia ya Mheshimiwa Tundu Lissu kwa kufiwa na Marehemu Christina ambaye alikuwa ni mwanafunzi wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ilikuwa ni pigo sana, poleni sana.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpogeze sana Mheshimiwa Waziri Mwakyembe kwa hotuba yake ambapo ametuelezea kabisa hatua kubwa ambazo zimeshafanyika na zinazoendelea kufanyika katika kuboresha hali ya utawala wa sheria na Katiba katika Nchi hii. Nashangaa sana na naomba niongee kwa mtazamo wangu kama mchumi, mtu ambaye naelewa hali halisi inayokabili utawala wa sheria. Mwanamapinduzi Karl Marx alisema nanukuu kwamba economics drives oolitics na akasema Karl Marx kwamba power makes law, maana yake ni kwamba uchumi unaendesha siasa na akasema mamlaka, madaraka pia hutengeneza sheria, mwisho wa kunukuu, huyo ni Karl Marx siyo Anna Tibaijuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa hivi nilisema awali na narudia tena, nchi yetu imebahatika, Watanzania wamekaa wakamchagua Rais ambaye ni kiongozi wa nchi naomba tumpe support, Waheshimiwa wenzetu ambao kazi yao ni kuja kutusimamia sisi, wana haki ya kusema wanayoyasema, pia tuna haki ya kuyawekea context yake kusudi yaeleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa uelewa wangu wa mambo, nchi yetu sasa hivi ina nafasi ya kurekebisha yale ambayo yalikuwa yametushinda kusudi twende mbele. Kwa hiyo, Upinzani ukifilisika ukabaki sasa kukemea kwa sababu lazima useme kitu, Bunge linageuka kijiwe. Bungeni hapa hatuleti hoja za vijiweni. Kwa mfano kusema kwamba Tanganyika inainyonya Zanzibar inainyonya katika lipi? Hili ni jambo la kujiuliza! Nimejiuliza kama mchumi tena mchumi kazi yangu ya kwanza ninyi mnanijua nilikuwa kwenye Shirika la Makazi Duniani, hamjui kwamba nilikuwa kwenye Shirika la Biashara la Dunia (UNCTAD) nikisimamia…..
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, linda muda wangu, kwanza kabisa kwa wale wanaosema nimeiba hapa mtaisoma namba, mimi siyo mtu wa kutishwa na vitu vya hovyo hovyo!
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimkiwa Spika, kama kuna mtu anafikiria kwamba mimi naweza nikatishwa hoja za hovyo hovyo huyo asome namba. Soma namba nasimama hapa nataka nitetee vitu ambavyo kwa kawaida watu tunanyamaza lakini sasa mtu anapopotosha hoja inaweza ikaleta hatari.
Mheshimiwa Spika, Tanganyika kwa mtazamo wa kiuchumi, haiwezi kuinyonya Zanzibar kwa mtazamo wa kiuchumi wa haraka. Nimeona niseme hili kwa sababu sheria na Katiba ya nchi yetu nimeona Mheshimiwa amezungumzia Katiba mpya mambo ambayo nilitaka kuyaainisha hapa, kuna suala la Katiba Mpya, Katiba Mpya tuliifanyia kazi wote tukawa tumekwama na Waziri ameainisha.
Mheshimiwa Spika, tunapoleta hoja zetu, tuzilete kwenye mantiki ambayo sasa haipotoshi umma wa Watanzania na kuleta vurugu katika nchi hii. Kisiwa cha Zanzibar nilisema wakati wa Bunge la Katiba na narudia, Kisiwa cha Zanzibar huwezi kusimama ukasema itakuwa Singapore, itakuwa Singapore vipi haina bandari, Comoro ina hali gani?, Commoro ina hali gani?
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walizungumza bila mpangilio)
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, naendelea kuchangia. Katika dunia ya ustaarabu unasikia hoja, Mheshimiwa Lissu amesoma hapa angeweza kuzomewa lakini wastaarabu wakamsikiliza wamekomaa kisiasa. Sasa ninyi mkianza kupiga kelele ilimradi kelele zote naomba muda wangu ulindwe.(Makofi)
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, suala la Zanzibar tulijadili kwa umakini, tulijadili kwa ukweli, tulijadili kwa haki lakini siyo kwa hoja za vijiweni hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, inapokuja suala la uhuru wa mahakama, wananchi wangu wa Muleba Kusini wa Kata ya Mgunda na Kata ya Karami wako katika hali ngumu. Hakimu pale anakula rushwa ya waziwazi, hatuwezi kusema kwamba Mkuu wa Wilaya ambaye anasimamia maadili ya Mahakimu au Mkuu wa Mkoa ambaye anaangalia aache mambo yaende kama yanavyokwenda. Uhuru wa mhimili wa mahakama haumaanishi kwamba wafanye wanavyotaka na wenyewe wanapofanya kosa lazima sheria itafuata mkondo wake.
Hivyo, suala hili naomba niliweke mbele na Mheshimiwa Waziri utakaposimama kwa sababu tunakutegemea wewe kwamba uwajibishwaji wa mawakili, mahakimu katika sehemu nyingi hasa Mahakama za Mwanzo imekuwa ni mgogoro na shida kubwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Muleba Kusini hali yetu siyo nzuri, tumeshahangaika, hatujui mahali pa kwenda naomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama utuambie unavyoweza na jinsi mhimili huu utakavyoweza kusimamia utendaji na uadilifu wa Mahakimu hasa wa Mahakama za Mwanzo. Wamejifanya miungu watu, wanashirikiana wakati mwingine na polisi ambao siyo waaminifu kubambikiza watu kesi na mtu yoyote anayekubali kubambikizwa kesi au kubambikizwa hivi vitu vya hovyo hovyo, mtu dhaifu lazima tusimamie wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, hilo nimelisema naomba kabisa lishughulikiwe na kwa upande wa Muleba Kusini tuko katika hali ngumu, tunahitaji Mheshimiwa Waziri uwasiliane na mahakama utusaidie.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninataka niliseme, tunapozungumzia sheria na Katiba, utawala wa sheria pia, hauondoi mamlaka ya watendaji wa Serikali kufanya kazi yao kama Mheshimiwa Rais anavyofanya kazi yake kwa speed kusudi twende mbele. Kwa sababu sasa you can not have your cake and eat it, hapa naona kuna hoja za mtu kula keki yake na anataka abaki na keki yake. Serikali ilipofanya kazi polepole wakasema Serikali ni dhaifu, nikasikia kauli kwamba Rais huyu ni dhaifu, Rais anapofanyakazi anasimama mtu anasema Rais anakwenda kiimla, please, mbona tunapingana? Nataka kusema kwamba tunapozungumzia sheria tusiwa-confuse wananchi wetu kwa kusema kwamba Serikali inaendesha kiimla, hakuna Serikali inayokwenda kiimla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho naomba nichangie kwa kusema kwamba, hali za mahakama hususani Muleba na Kagera nyingi zipo katika hali mbaya. Majengo yamechakaa, majengo hayatoshi yanatakiwa yafanyiwe ukarabati. Kwa hiyo, tunapogawa fedha sasa, tunapoimarisha sheria, justice delayed, justice denied kama hakuna vifaa vya kutosha katika Mahakama haiwezekani! Nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye tayari ameshawawezesha muhimili huu wa mahakama ili kusudi waweze kupata fedha wanazozihitaji na kesi ziende haraka.
Kwa hiyo, nataka kusema kwamba kwa upande wa mtizamo wa muhimili huu wa sheria inatulinda wote, hayo tunayoyasema hapa Bungeni ni kwa sababu tunalindwa na sharia, unapotuhumiwa unasimamia haki yako! Hizi kelele za chura haziwezi kumzuia ng‘ombe kunywa maji! Hiyo naomba niseme kabisa. Haziwezi kumzuia ng‘ombe kunywa maji (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nifafanue kwa sababu naelewa mambo mengi. Nilipokuwa Kenya nilishuhudia Rais Mheshimiwa Mwai Kibaki alisimamisha Majaji 23 kwa siku moja, kwa hiyo lazima watu wawajibishwe, lazima kuwe na unautaratibu wa kuwawajibisha watendaji wa Mahakama. Hivyo, msiwa-confuse wananchi, msiwadanganye, mlete hoja, wengi wetu tunazipenda tutazisikiliza lakini ziwe na mashiko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, nami naomba niungane na waliotangulia kukupongeza wewe na timu yako, Makamu wako na Katibu wa Bunge kwa jinsi mnavyotuendesha. Mimi mwenyewe hapa nasimama kwa nguvu za Mwenyezi Mungu nikiamini kabisa kwamba Bunge litakapokutana Novemba, 2020, nitakuwa nimeng’atuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa muda ambao tumekaa pamoja na hasa nikijielekeza kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye tunajadili hotuba yake. Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa karibu sana na sisi watu wa mbali, wa Kagera, ametembelea Jimbo langu. Juzijuzi kama mlezi wa Chama cha Mapinduzi, Mkoa wa Kagera alikuja kututembelea na kuangalia hali yetu. Naomba tumpigie makofi Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni nzuri, mipango ni mizuri lakini nyakati zenyewe ndiyo siyo rafiki. Kwa hiyo, nami sina budi kuungana na Wabunge wengi, wanasema the time demand action, Corona ni tukio ambalo limetokea na huwa linatokea miaka mia moja mia moja ukiangalia historia ya pandemic. Mara ya mwisho limetokea 1918/1920, Spanish Influenza ambayo iliua watu takribani milioni 15, 20 au hata zaidi maana takwimu zinatofautiana na sasa hapa tuna hii pandemic.

Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye suala hili kwa sababu ni muhimu sana na lina demand kwamba tuliangalie kama Bunge. Uwezo wetu Afrika ku-respond kwa mambo ambayo nayaona kwenye mtandao yaliyotokea China, London St. Thomas ambapo Mwalimu wetu Nyerere alitibiwa na umauti umemkuta pale, wagonjwa wamelala chini na hata St. Mary’s. Juzi nimemuona Meya wa New York akilia hana ventilators sisi ventilators hatutaweza kuzipata.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nirudie alichokisema kwa ufupi sana Mheshimiwa Ngeleja kwamba sisi ni lazima tuwe na mpango mbadala ambao unajikita katika jamii yetu. Lazima tuhimize kunawa lakini tunapozungumza hapa kuna hospitali zingine hazina maji. Kunawa ni lazima lakini wananchi wetu wengine hawana maji. Kwa hiyo, huwezi kusema kwamba mkakati ni kunawa wakati unajua nusu ya watu hawana maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisemi kwamba tusinawe nasema kwamba ikiwa zahma ikitufikia kama tunavyoiona kule itakuwa kizungumkuti. Hapa ndipo naungana kabisa na kumpongeza Rais wetu tunaanza na sala kwa sababu lazima tukiri kwamba mpaka sasa hivi Mungu ametuhurumia, tumshukuru Mungu jamani. Ametuhurumia kwa sababu yale yanayotokea yangefika hapa hatuna uwezo wa ku-respond. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa nachotaka kupendekeza, hapa ndipo nasema jamii inahitaji survival strategies ambapo kujiuliza tiba zetu mbadala (za asilia) ziko wapi? Hakuna jamii yoyote itakayokaa na kusubiri kifo lazima itajihami. Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu asipopitisha dude hili mbali tukafikia pale walipofika ni lazima tuangalie makabila yetu mbalimbali maana yana mbinu mbalimbali za kukabiliana na homa za mapafu.

Mheshimiwa Spika, wanasema Covid19 ni mpya lakini siyo mara ya kwanza kwa virus kama hivi kutokea. Kufukiza ni muhimu lakini unahitaji mkaa na kuni. Kwa hiyo, ni lazima sisi kama Serikali tuhakikishe watu wanapata mkaa yaani wawe nao karibu, watu wawe na sigiri, wawe na kuni karibu maana katika tiba zetu nyingi asilia inabidi uwe karibu na joto.

Mheshimiwa Spika, nataka kuomba Wizara ya Afya na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile nimeshamwandikia barua rasmi nikimweleza kwamba ni lazima tuangalie pia option B. Sisemi kwamba tusitekeleze option A, tuvae mask, tutafute ventilators lakini kama watu wengi watakuwa wameambukizwa ni lazima tuangalie namna ya kuwaokoa na mimi naamini kwamba wataokoka. Nimeangalia figures leo, Ghana sasa hivi wameshapona watu 33 wakati Holland hakuna hata mtu mmoja amepona kwa sababu wao wamerudi kwenye muarobaini, wanafukiza wagonjwa na wanapona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mambo haya naomba kusema kwamba Wazungu hapo wametupoteza. Tuna kasumba nyingi na huwezi kuwalaumu Madaktari wetu, wengi wamekuwa trained kwenye western tradition; oxford tradition, wanabeza mambo yetu kana kwamba sisi kabla ya Wazungu kuja tulikuwa hatuishi au tulikuwa hatuugui. Kwa hiyo, tiba mbadala ni kitu muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona niliseme hili kwa sababu ni survival strategy, ni lazima Serikali sasa isaidie. Kule kwangu kuna barrier fulani wanazuia watu wa mkaa, sijui wanataka watu wapikie nini! Unamwuliza mtu wa mkaa; mtu haruhusiwi kuwa na mkaa wake wa kupikia kwa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba nionavyo mimi katika kukabiliana na hili Covid- 19 ni kwamba tuangalie Plan A na Plan B. Plan A ni hii ambayo tunayo standard procedure, hospitali; Plan B ni kwamba kama tukizidiwa, lazima tupeane maarifa; Wagogo wanafanyaje? Wapogoro wanafanyaje? Wanyakyusa wananyaje? Wahaya tunafanyaje? Kwa sababu hii knowledge ipo, ni indigenous knowledge, lakini inakuwa ignored watu tumekuwa brainwashed. Sasa sisi na wengine wengi humu ni vijana siwalaumu, ninyi hamkukulia vijijini. Sisi tumelelewa na wazee, tumeshuhudia haya mambo. Sasa watoto wa mjini hawayajui haya mambo kwamba Plan B iwepo kusudi Afrika iweze ku- survive. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaposema hivyo, niseme pia, magonjwa mengine tusiyasahau, kwa sababu na yenyewe yatakuja kukuza hili tatizo. Kule kwangu Muleba, kule kwenye Hospitali ya Wilaya hatuna damu salama. Kwa hiyo, kuna wanawake watatu walipoteza maisha wakiwa wanajifungua kwa kukosa damu salama. Kwa hiyo, naomba hili nalo liangaliwe. Kwa sababu tusipoweka mambo ya kulinda sehemu nyingine ambazo zitatuletea matatizo, hata na hii Corona Virus, kama Mungu akitusaidia; na vile vile tusali; na tunaposali hata nyumbani unaweza ukasali, sio lazima uwe na mkusanyiko mkubwa kusali, lakini Mungu yupo kila mahali, au sio! Hata na hapa Bungeni tunaweza tukasali, mahali popote ni mahali pa ibada.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani hilo nimelisema, lakini nawasiliana na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, nimeshamwona, nami najaribu kutoa mawazo kwa sababu the time reminds it. Ni dhana kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda ni mfupi, hilo nadhani tutaendelea na naomba nimpongeze Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwa kweli naona kama ni Jemedari. Namsikia kila siku anatangaza, yaani she is doing a great job. Sasa tumsaidie na sisi katika kutafuta hii Plan B.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, ni dakika saba, nimeweka stop watch hapa. Ni dakika saba. Nimeweka stop watch, ninayo hapa dakika ya nane sasa. (Makofi)

SPIKA: Basi malizia, inaelekea stop watch ya Katibu wangu ina matatizo.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, katika dakika zangu hizo mbili kwa ruhusa yako, niendelee. Kitu kingine ambacho nataka kuongea na ni cha kimkakati, tunampongeza Mheshimiwa Rais wetu, anafanya kazi nzuri sana, lakini naomba kwa kupitia Bunge lako hili Tukufu nipeleke maombi maalum kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Program ya NIDA kwa sasa hivi ni kama imefeli.

Mheshimiwa Spika, NIDA kama ilivyo sasa hivi, imekuwa kero kubwa kwa wananchi kwa sababu simu zao zimefungwa. Sasa sijui ninyi wenzangu huko kwenu mkoje, lakini kule kwangu Muleba, watu simu zao zimefungwa na mtu ambaye umemfungia simu, hata kama umefanya mambo mazuri mangapi atakuona kwamba umemharibia. Kwa hiyo, naomba kitu hiki kilipofika; na zoezi lenyewe la NIDa ni zuri lakini mkakati ndiyo kwa kweli haujitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba Afisa Uhamiaji wanaodhibiti uhakiki wa hizi namba, warudishe na wakasimu madaraka yao kwa Watendaji wa Vijiji. Kwa sababu mtu atakayejua kama mimi ni Mnyarwanda au ni Mtanzania ni kijiji changu au siyo! Haiwezi kuwa ni mtoto mdogo, migration officer namkuta kwenye Wilaya eti ndio anasema mimi sio Mtanzania. Kwa hiyo, unakuta hizi ni kero kwa wananchi na kwa upande wa Muleba na mikoa ya pembezoni. Huko pembezoni kwa kweli imekuwa kero kubwa. Sisi kwa upenzi wa Rais wetu lazima tutoe feedback ya hali halisi ilivyo. Kwa hiyo, hilo naona niliseme kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kwa kupitia ofisi yako, nashukuru kwamba umemwandikia Mheshimiwa Jenista Mhagama, nakukabidhi hoja yangu binafsi ambayo nimehangaika nayo tangu Bunge la Kumi. Naomba kabisa Bunge lako tukufu, kwa kuwa naamini kabisa wewe unaendelea kabisa, tutakuwa nawe katika Bunge linalofuata, Mheshimiwa Jenista Mhagama naomba record ya Hansard irekodi kwamba nimekukabidhi hoja yangu binafsi, kwa sababu najua kwamba Mheshimiwa Spika, alikukabidhi hoja ile.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Waunge, hoja hiyo ilikuwa inasema hivi, baada ya kukumbwa na tatizo la ESCRO nikajikuta katika situation ambapo nahukumiwa na Bunge, niko ndani ya Bunge, ni Mbunge na siruhusuwi kusimama kujitetea. Nikaona tuna upungufu mkubwa sana katika mfumo wetu. Kwa hiyo, nimehangaika na hoja binafsi na Muswada binafsi.

Mheshimiwa Spika, Bunge la Mheshimiwa Makinda wakasema hatuna wakati; Bunge lako hili wakati haukupatikana, lakini angalau umepiga hatua umeikabidhi Serikalini. Kwa hiyo, naomba niikabidhi rasmi for the sake of the record nina historia kwamba ionekane kwamba Muswada binafsi, lazima Wabunge wawe na uwezo wa kuandika Miswada binafsi. Kazi ya Mbunge ni kutunga sheria, siyo lazima kujadili tu sheria zinazoletwa na Serikali, mwisho wa siku lazima Serikali itakuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jambo kubwa na la msingi ili kuboresha demokrasia yetu. Nadhani muda wangu umekwisha. Nakushukuru kwa kunivumilia. Nawashukuru sana wananchi wa Muleba Kusini kwa kunipa nafasi kuwa na ninyi katika Bunge hili. Miaka 10 nimejifunza mengi, naenda kuandika vitabu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, unafanya kazi nzuri. (Makofi)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi sina budi kuungana na wachangiaji wa awali kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa kazi nzuri. Ni pacha wangu kabisa lakini pia ni mwanangu, kwa lugha ya upendeleo naona kwamba tuna sababu sasa baada ya kuangalia andiko lake hili, ni kwamba kweli tunaingia katika awamu ya viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kusema kwamba mpango uliopo mbele yetu ukitekelezwa na ninaona kila nia ya kuutekeleza, utatupeleka mbele. Napenda tu nisimame hapa kuchangia kwa kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini na ninafahamu kabisa kinadharia kama mwanauchumi kwamba ili uwe na viwanda na Mheshimiwa Waziri analijua na atakaposimama kujibu atueleze, ni lazima viwanda vinaendana na kilimo, maana yake wanasema ni Agricultural Development na industrialization, hivi vina kwenda pamoja. Huwezi kuendeleza viwanda kama hujaendeleza kilimo. Hutapata malighafi ya ku-feed hivyo viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wachangiaji wengine, na mimi naomba nisisitize kwamba ni lazima tuwe na malighafi. Sasa mazao ambayo unayo, kwa mfano zao la sukari, mchele na alizeti; ukiniuliza mimi kwa uelewa wangu wa mambo kama mchumi, nitasema kwamba Taifa hili halina sababu yoyote isipokuwa katika hali ya dharura kukubali kuingiza sukari, mchele au alizeti kutoka nje. Kwa sababu mafuta, kama unataka industrialization na hii inaitwa nascent industrial development. Lazima uwe na mkakati wa kulinda viwanda. Kila nchi zimelinda, Marekani, Uingereza na Ulaya imelinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha zaidi sasa, Jumuiya ya Kimataifa katika WTO inatulinda sisi tulinde mazao haya. Mheshimiwa Waziri utakaposimama, una mwambata wako yuko Geneva ambaye anafuatilia mambo haya katika World Trade Organisation, under special and differential treatment for least developed countries. Mazao haya yamelindwa na Sheria za Kimataifa. World Bank wanapokuja hapa kutuambia tufungue milango, wanakuwa wanatuonea.
Kwa hiyo, katika zana ya biashara, hili nalo naomba lieleweke na Mheshimiwa Waziri utufafanulie utakavyofuatilia sasa na waambata wako wa biashara walioko Geneva ambao wanafuatilia mazungumzo ya Kimataifa kuhusu biashara duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri jambo hili litatusaidia sisi, kwa mfano mimi nasimama hapa kuzungumzia viwanda na biashara nikitoka pembezoni, Mkoa wa Kagera. Nadhani alikuwa Mheshimiwa Kubenea. Hapa ni lazima niseme kwamba na-declare interest nakubaliana na Mheshimiwa Kubenea kabisa kwamba sikuona mkakati wako kwa mikoa ya pembezoni. Watu wanasema Rwanda ni nchi ambayo haina bandari, lakini Kagera, Kigoma na Katavi ni mikoa ambayo haina bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwe na mkakati wa kusaidia mikoa ya mbali kuweza kufika bandarini. Mimi nafikiria suala ambalo Mheshimiwa Rais amelitilia mkazo na tunashukuru kumuunga mkono kwa nia yote, ni suala la hii standard gauge na reli inajengwa. Na mimi naomba niseme, reli hiyo ni lazima pia iwe na spur au mikondo inayoingia mikoa mingine ya pembezoni itakapokuwa inapita kusudi wote tuweze kuzifikia bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima hapa nikiri kwamba, Rais Museveni nataka nimpongeze kabisa, hatua hii tuliyofikia kwamba bomba la gesi sasa litapita Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua na naweza nikatoa taarifa kabisa kwamba Rais Museveni ilikuwa ni azma yake kwa sababu alikaa hapa Tanzania kama mkimbizi, alikaa Muleba pale kwako Mheshimiwa Waziri, Muleba Kaskazini, ndiye alikuwa anakaa pale anapigania uhuru. Sasa unaona kwamba ametoa shukrani, anatukumbuka na katika hilo lazima tumpongeze na tujipongeze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali hiyo, tujipange sasa. Sisi walio wengi ni wakulima, wavuvi na wafugaji, na sisi ndio viwanda. Hivyo viwanda vitahitaji malighafi. Sasa mnatuwezeshaje? Mnatuwezesha kwa miundombinu, lakini pia mnatuwezesha kwa mifumo ya kuweza kuwafanya waingie kwenye uzalishaji wa kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema sukari isiingie, sukari ikiingia itaua viwanda vya sukari. Hata mtoto wa shule anajua hilo. Ili kusudi Watanzania wapate sukari ni lazima Wizara ya Kilimo iwe na utaratibu wa kuingiza sukari, lakini siyo kutumia wafanyabiashara. Wafanyabiashara wale ukiwapa nafasi wataingiza sukari ya zaidi na viwanda vyetu ndani vitakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kabisa kwa mfano kiwanda cha Kagera sasa hivi hakizalishi kwa sababu mvua ni nyingi, mashine haziwezi kuvuna muwa, vitu kama hivyo.
Kwa hiyo, nataka kusema kwamba itatosha kabisa kwa sisi kuwasaidia wavuvi wetu wapate viwanda. Wavuvi sasa hivi wanahangaika kwa sababu ya nyavu, lakini pia na viwanda vya samaki vingi viko katika mikono ya watu binafsi. Mheshimiwa Waziri naomba uviangalie pia viwanda vya samaki, vinawezeshaje wavuvi? Viwanda vya samaki wenyewe havina utaratibu wowote wa kusaidia wavuvi, lakini utakuta hawapati bei wanayostahili na wakati mwingine mauzo hayaendi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishajipanga ndani, sasa tunajipanga nje; na dunia ya Kimataifa inatusubiri. Nimeona Mheshimiwa Waziri umezungumzia vizuri AGOA (African Growth Opportunity Act), lakini kama unavyojua, Tanzania inasuasua na AGOA. Hatupati faida yoyote. Ninaweza nikasema kabisa, nilipokuwa bado Umoja wa Mataifa kwenye Shirika la Biashara nilipoanzia kazi, Ulaya wametupa pia, AGOA ya Ulaya inaitwa ABA (All But Arms), unaweza ukaingiza kitu chochote Ulaya isipokuwa silaha. Hii ni trade offer waliyotupa, lakini kwa sababau hatujajiandaa…
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kengele ya kwanza eeh? (Makofi)
Sasa nataka kusema hivi, vijana wetu sasa; trade presupposes exchange of goods and services, yaani ni lazima muwe mnabadilishana kitu. Sasa vijana wetu wanapokuja kufanya biashara, tumewawezeshaje vijana wetu?
Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, naomba nisikie mkakati wako wa kuwasaidia vijana waanze kufanya biashara. Wale ambao wamemaliza darasa la saba lakini wana ujanja unaweza wakapewa hata tuition ya kuzungumza kiingereza kusudi waweze kwenda kufanya biashara, maana yake huwezi kufanya biashara za Kimataifa na wewe hujui lugha. Hiyo nayo tusidanganyane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina hawa sasa hivi wanajifundisha kiingereza kila mahali. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba kwa upande wa biashara, tujue yaani tunajiandaaje na masoko? Vijana wetu wanapomaliza form four, form six, chuo kikuu, napenda kuona mkakati Mheshimiwa Waziri unaposimama hapa kujibu, utuambie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kabla kengele haijanigongea, Mkoa wa Kagera sisi tuko mbali; nimeshangaa kuona kwamba Omukajunguti haijatajwa hapa. Pale Mheshimiwa Rais Magufuli, alituahidi kwamba ataweka Export Processing Zone.
Sasa napenda kujua kwamba hii Export Processing Zone ambayo itatukomboa sisi Wanakagera kuweza kuingia kwenye horticulture kwenda kuuza mboga (vegetables), kama huna ndege huwezi. Kule Kilimanjaro wanafanya kwasababu kule kuna airport. Sasa kule Bukoba, huwezi. Hata ukienda kule kila kitu kwetu ni green lakini hamna miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huo ndiyo mchango wangu. Tunapozungumzia viwanda na biashara, Serikali hii imejipanga, napongeza sana juhudi za Serikali, naunga mkono hoja, lakini na mimi nimechangia kinadharia kwa kusema kwamba inaendana na sekta nyingine. Huwezi kuzungumza viwanda na biashara in a vacuum, lazima uangalie kwamba itakwendaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, naunga mkono hoja na kumpongeza mwanangu Mheshimiwa Mwijage, amefanya kazi nzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Tangu awali hapa ngoja niseme kabisa kwamba Bajeti iliyopo mbele yetu inastahili na ninaiunga mkono kabisa, ila sasa nachangia kwa mtazamo wa mwananchi wa Muleba Kusini na hasa Halmashauri ya Muleba kwa ujumla wake.
Imeshasemwa hapa kwamba kwa sisi ambao tunatoka kwenye Halmashauri ambazo ni kubwa na Majimbo makubwa, tuko katika hali ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Simbachawene atakaposimama hapa kufafanua, ajaribu kuoanisha mgao wa fedha zilizogawiwa na wingi wa watu na ukubwa wa eneo. Kwa maneno mengine, tunataka weighted average; kwa sababu haitoshi kusema fedha kadhaa zinapelekwa mahali, ni lazima uangalie per capita; wale wananchi walio mle wanapata kiasi gani? Uone kama zinatosha kusukuma maendeleo au hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya hivyo, tunajikuta katika hii pressure inayozidi kuongezeka ya kugawa Mikoa, Majimbo na Wilaya lakini mwisho wa siku tunakuwa na viongozi ambao sasa hawana OC ya kufanyia kazi, hili ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kutusaidia kama siyo sasa huko anapokwenda kuliangalia jambo hili, ni la muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Muleba ndiyo kubwa katika Mkoa wa Kagera, ina Kilomita za mraba 10,500, theluthi mbili zikiwa ni maji, mimi hapa nina Kata 25; nina wananchi 600,000; nina wapigakura 264,000 na kadhalika na kadhalika. Sasa katika hali hiyo bajeti ambayo iko mbele yetu, kitu cha kwanza nakubaliana na Serikali. Serikali haiwezi kugawa fedha ambazo hazipo. Sisi kama Wabunge tunapenda sana kusema kwamba tuongeze bajeti, lakini nimeangalia katika majedwali ambayo Waziri ameleta hapa na yamekaa vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia jedwali namba 11, linaonyesha vitu muhimu. Kitu kinachokosa ni uwiano na wananchi katika lile eneo husika, hilo halipo. Isipokuwa utaona kwamba kwa ruzuku ambazo zimekwenda, kwa mfano kwenye Road Fund. Road Fund nadhani kila Mbunge hapa anaitegemea sana, lakini ni asilimia 5.25 ya fedha ambazo zililipwa zilizopelekwa kule.
Sasa unaona kwamba unapokuwa katika hali ya kupanga bajeti kubwa, watu wakawa na matumaini, Halmashauri zikafikia kwamba fedha zitatoka katika bajeti kuu, fedha hizo zisipokwenda tunarudi nyuma. Kwa hiyo, napendekeza kwa Mheshimiwa Waziri alifikirie hili atakapokuwa anajumuisha (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru zaidi na hapa ninapoangalia, Waziri wetu wa Utawala Bora na decentralization, dhana nzima ya kugatua madaraka ni kupeleka wajibu kwa hawa watu. Wajibu huwezi kupeleka wajibu bila kuwapa watu uhuru na kuwaamini. Nimemshukuru sana Waziri Mkuu aliposimama hapa na kusema sasa bajeti chini ya shilingi bilioni moja itaweza kuamuliwa yaani mikataba itaweza kuamuliwa kwenye Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia na Mawaziri wetu mwangalie suala la ajira kwa mfano, process ya kuwaajiri watu kwenye Halmashauri, eti watu wanatoka Dar es Salaam kuwaajiri Watendaji wa Vijiji Muleba. Jamani, mambo mengine Mheshimiwa Mwalimu Nyerere alisema kuna maendeleo ambayo hayahitaji pesa. Mtu atoke Dar es Salaam kusimamia eti kumwajiri Mtendaji wa Kijiji. Sehemu nyingine Kiswahili ni lugha ya Taifa, lakini sehemu nyingine Mtendaji wa Kijiji ni vizuri pia akajua mazingira ya pale ambapo anaajiriwa. Kwa hiyo, unaona mantiki ya kuwa na Serikali za Mitaa ni nini. Kama tutaendelea na control ya namna hii, maana yake hii central control inafuta dhana nzima ya decentrelization. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu limezungumziwa sana, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameshavuna a low hanging fruit. Kwa kutamka tu elimu bure, watoto walioandikishwa wameongezeka kwa asilimia 32. Nimeona hapa Mheshimiwa Waziri ameleta takwimu ziko very clear. Watoto walioandikishwa Darasa la Kwanza wameongezeka kwa 32%; kutoka bilioni 1.3 mpaka bilioni 1.8; ni maendeleo makubwa. Katika Mkoa wa Kagera wameongezeka kwa 44% na Muleba kwangu wameongezeka kwa 69% kwa tamko tu yaani hii ndiyo Mwalimu Nyerere alisema mendeleo yasiyohitaji pesa. Watoto kuletwa shuleni ni maendeleo, hayo tumeyaona. Sasa mtu anaposimama hapa kusema kwamba elimu bure haijaleta tija, huyo hawezi kuwa anakwenda na takwimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa ufahamu wangu wa mambo nasema kwamba indicators ya mafanikio ndiyo hizo kwamba watoto wameletwa shule. Sasa sisi tuwezeshwe na wahusika Mawaziri, tujitegemee. Kuna dhana ya kujitegemea. Hii notion kwamba Serikali italeta fedha, Serikali haiwezi kuleta fedha ambayo haina, hilo nalo tulijue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama Halmashauri nimeona kuna Halmashauri nyingine zimekopa, zimekuwa pro-active zimekazana. Halmashauri nyingine zimesubiri kwa sababu tunakosa mwongozo. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utuletee mwongozo kuhusu waraka wa hii dhana ya elimu bure. Elimu bure haitaweza kujenga madarasa yote, haitaweza kujenga maabara zote, lakini wananchi tuko katika hali ngumu au siyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu niko katika hali ngumu. Siwezi kusimama Muleba nikawaambia wananchi wachangie, wakati wanasema kwamba Serikali imesema kila kitu ni bure. Nafikiri ingekuwa ni vizuri tukapata waraka sasa kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Elimu kufafanua responsibility ya mzazi ni nini na responsibility ya Serikali ni nini. Katika hili niseme waraka ambao ulitolewa na Wizara mwezi Disemba ulisema wazazi wanagharamia chakula, mimi kama mwalimu wa siku nyingi, naomba kama mtu mwenye umri hapa, maana yake na sisi wazee tuna kitu cha kuwaambia hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikisoma primary enzi za mkoloni, hakuna mtoto alikuwa anaruhusiwa kwenda shuleni bila chakula. Kulikuwa hakuna hotpot, hakuna kitu chochote, lakini mama anachemsha kiazi unakwenda nacho; mama anachemsha muhogo unakwenda nao; mama anakupa kipande cha ndizi, unakwenda nacho. Sasa sisi tumekuwa Taifa, watoto wanashinda na njaa. Eti watoto watasomaje hawajala kitu chochote? It is not serious! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, nafikiri tungepata waraka ukafafanua mambo, sisi tuko tayari kuwajibika; Muleba Kusini tuko tayari kuwajibika lakini sasa ngazi za juu zisituchanganye. Mnatuchanganya kwa kusema kwamba mambo yote yatafanywa bure wakati uwezo wa kufanya bure hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu na ninautoa nikiunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kabisa kwa sababu najua kwamba ndivyo hali ilivyo. (Makofi)
Mwisho kabisa, watoto wa miaka minne kwenda kwenye chekechea, Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie, labda umri ungepanda kidogo, kwa sababu watoto wanakuwa wengi, madarasa hayapo, walimu hawapo, service ratios haziwezi! Sasa unakusanya watoto wadogo 50 au 80 kwa mwalimu mmoja, ataweza kufanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi nyingine unasema kwamba watoto wawe miaka mitano au sita au saba kwa sababu inapunguza pressure kusudi uweze kujiandaa na kuweka services zinazohitajika.
Baada ya kusema yote hayo, naunga mkono hoja moja kwa moja, Muleba Kusini usitusahau Mheshimiwa Waziri, karibu ututembelee. Na wewe Mheshimiwa Mama Angellah Kairuki, njoo ututembelee, uje uangalie sasa Watendaji wa Vijiji walioajiriwa kutoka Dar es Salaam, kwa kweli ni kizungumkuti! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mimi kwanza kabisa naomba niseme kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Mindombinu na naomba kabisa nianze kwa kuunga mkono taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Dkt. Norman Sigalla na pia naomba nianze kusema kwamba mimi naunga mkono hoja ambayo iko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, amejitahidi kadri alivyoweza, lakini na sisi kazi yetu hapa ni kuboresha. Kwa hiyo, naomba nizungumze kwa mtizamo huo wa kuboresha yaani positive and forward looking contribution. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi iliyo mbele yetu ni kubwa. Nimewahi kusema na kila nitakaposimama nitarudia, kwamba nchi yetu imebarikiwa, tumepata kiongozi ambaye sasa anatuingiza katika mapambano mapya ya kupigana na umaskini. Umaskini huu unamaanisha kwamba tunasomesha watoto, lakini watoto hawawezi kupata ajira kwa sababu hatujajipanga vizuri kuweka miundombinu ambayo itaweza kubadilisha hali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na pia cabinet nzima, Baraza la Mawaziri na Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba, sekta hii sasa ipewe angalau asilimia 16 ya bajeti ya Serikali. Lakini Kamati yetu ilipendekeza na niomba nisisitize kwamba hazitoshi na ushahidi kwamba hazitoshi Waheshimiwa Wabunge wote mnaposimama kila mmoja unaona kwamba, anasema mambo ya msingi ambayo ni pungufu. Barabara zinatakiwa zijengwe maeneo mbalimbali nchini kote na kila mmoja wetu hapa anastahili. Anastahili reli, reli inatakiwa kwenda katika kila Wilaya, anastahili bandari, lazima ziwe kila mahali na kadhalika, lakini sasa bajeti haitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi mchango wangu nataka kusema kwamba wananchi wa Muleba Kusini ambao wamenituma hapa kwa mara nyingine na wenyewe wana matarajio yao. Matarajio yao ni kwamba, Hospitali yetu Teule ya Rubya, Hospitali ya Wilaya, iko milimani na huwezi kuifikia bila kupita Mlima wa Kanyambogo. Kwa hiyo, siwezi kurudi nyumbani kwa wananchi wa Muleba Kusini kwa kujiamini kama sijaweza kuwahakikishia kwamba Mheshimiwa Waziri utakaposimama utatwambia hatima ya barabara ya lami kutoka Muleba kupita Kanyambogo kwenda Hospitali Teule ya Rubya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa ridhaa yako nimkabidhi Mheshimiwa Waziri tender iliyoitishwa na TANROADS chini ya Waziri wetu wa Ujenzi wa zamani ambaye sasahivi anaongoza nchi ambayo ilikuwa kwenye Gazeti la Daily News la tarehe 13 Septemba, 2013. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi aliitisha tender ya kujenga barabara ya lami kutoka Muleba kupitia Kanyambogo kwenda Rubya. Nimeona sasa hivi Mheshimiwa Waziri hujasahau kabisa, lakini umeweka kwamba ni ya changarawe. Kwa mlima wa Kanyambogo kuweka changarawe pale ni kutwanga maji kwenye kinu. Unaweka kifusi asubuhi, jioni kimeshaporomoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu imeshauri kabisa kwamba pamoja na ukosefu wa fedha TANROADS wajitahidi kuachana na mambo ya changarawe na kokoto, hawa ni watu wa lami ni watu wa viwango, watusaidie; sisi kazi yetu ni kuwatafutia fedha wanazostahili. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba jambo hili ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasahivi Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, amemaliza kazi yake. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati akiwa kwenye kampeni pale Muleba alituahidi na mimi naamini ni mtu wa ahadi, kwamba sasa hili litatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sisi wanawake wa Tanzania tunajivunia sana na tunampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu na alipopita Muleba akiwa kwenye kampeni aliahidi barabara ya lami kutoka Lunazi kwenda Ziwa la Burigi. Ziwa la Burigi ni ziwa (unique) la kipekee katika nchi yetu, lakini amini usiamini miaka 55 baada ya Uhuru hakuna barabara yoyote inayokwenda Ziwa Burigi ambalo ni unique ecosystem. Kwa hiyo, naomba kabisa hili nalo liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa kwa mchango wangu naweza nikasema mambo mengi. Watu wamezungumzia meli nimeshazungumza, kiwanja cha ndege cha Omkajunguti kuikomboa Kagera kutokana na umaskini imeshazungumzwa, naomba nikazie. Lakini pia kama mtu ambaye ninatoka Kanda ya Ziwa, reli ya kati imezungumziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tunapozungumza reli tuangalie sasa kumuwezesha pia Waziri wetu…
WENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa hisani hii. Kwanza kabisa naomba niseme nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Engineer Lwenge na timu yake kwa kazi nzuri ambayo amefanya, kitabu chenyewe kinajieleza, naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama mwanamke naomba nisimame nizungumze kama Mwenyekiti na samahani kwa hili kama wewe na wenzako mtaona haifai, lakini naamini kama wanaume mngekuwa mnateka maji, tungekuwa tumeshaondokana na tatizo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hapa tunaposimama leo kuzungumzia suala la maji tunazungumzia pia ajenda ya ukombozi wa mwanamke jamani! Miaka 55 baada ya uhuru huko vijijini hali ni tete na wote tunafahamu. Kwa hiyo, nafikiria hapa tukiangalia kazi nzuri ambayo iko mbele yetu, sasa mikakati ya kuanza kusambaza maji, watu wamezungumza hapa kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kimkakati kwa sababu muda sio rafiki. Ni kwamba ili tuweze kuwafikishia Watanzania huduma hii ya maji maana maji ni huduma, lakini sasa hivi imekuwa biashara na biashara hiyo wanaonunua maji ni wanawake, ndoo ya maji inaweza hata ikafika sh. 1,000/= au sh. 500/=, kama huna mahali pa kuchota maji inabidi ununue maji. Kwa hiyo, unakuta kwamba mzigo wa mwanamke unazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabisa, kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri, nimeona katika Ibara ya 253 ya hotuba hii anazungumzia ushiriki wa sekta binafsi. Nataka kusema kwamba, juhudi za Serikali ni nzuri lakini suala hili ni gumu, hata tungeunda wakala wa maji jambo ambalo nalo linafikirika na wengi wamechangia bado utakuta kwamba Serikali peke yake haitaweza kuwafikishia Watanzania maji kwa haraka tunayoitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Sekta binafsi, Mheshimiwa Waziri nadhani atakaposimama labda angetuambia afafanue kidogo jinsi anavyopanga kushawishi sekta binafsi kushirikiana na Serikali na halmashauri zetu katika kusambaza maji kwa haraka zaidi, hili jambo ni muhimu sana. Kule kwangu Muleba Kusini ambao ndio wajibu wangu hapa, nimeangalia Mheshimiwa Waziri bajeti na mpango aliotupangia nasikitika kusema kwamba haitoshi kabisa. Ninaposikitika hivi nadhani na wengine wengi humu ndani wanasikitika. Ndiyo maana angekuja basi na mkakati wa kutukomboa sisi akatuonesha jinsi tunavyoweza kutafuta wawekezaji kwa sababu maji mwisho wa siku watu wanachangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uwekezaji katika maji huu unahitaji pia Serikali iangalie, ni lazima bei ziwe zinaweza kulipika. Kwa hiyo, sasa hivi nafikiria kwamba suala hili lingetusaidia sana. Kwa hiyo, katika miradi yako ya umwagiliaji Muleba, nasikitika kusema kwamba, miradi iliyowekwa awamu zilizopita fedha hiyo ni kama ilipotea, hakuna mradi unaofanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Pia nimpongeze Mheshimiwa Balozi Mahiga, Naibu Waziri wake pamoja na Watendaji wake kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masuala kadhaa pamoja na kuunga mkono hoja, nitaomba yajibiwe au kama bado yafanyiwe kazi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, diplomasia imejikita katika misingi ya reciprocity. Tupewe ufafanuzi kama kweli Balozi wa nchi za nje hawataruhusiwa tena kwenda mikoani bila kibali cha Wizara ya Mambo ya Nje. Naamini jambo hili haliwezi kuwa kweli, hii maana yake watu hawatakuwa na uhuru kamili kufanya kazi zao halali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakiamua ku-retaliate na kuweka sharti hili kwa Mabalozi wetu walio nchi zao inaweza kutuumiza. Nitaelewa kama kwa sababu ya usalama Mabalozi na Maofisa wao watatakiwa kutoa taarifa ya safari zao nje ya Dar es Salaam ili Serikali ikibidi iwawekee ulinzi, hiyo inaeleweka, lakini hivi sasa ni kama suala hili limepotoshwa na Wapinzani kudai wanahitaji ruhusa. Mheshimiwa Waziri atufafanulie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Balozi zetu ziruhusiwe kubaki na maduhuli wanayoyakusanya ili kupata fedha za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya ya Afrika Mashariki imeendelea kutoeleweka vizuri kwa wananchi, ingekuwa vizuri kupata kitabu cha maswali na majibu (Q and A) kuhusu maana ya ushirikiano – sekta kwa sekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya nchi hii yote bado haijakamilika. Mpaka kati ya Uganda na Tanzania huko Kagera, uliowahi kusababisha vita hadi leo haujakamilika. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi atueleze ni lini wanakamilisha zoezi hilo. Nilijaribu kulikamilisha nilipokuwa Waziri wa Ardhi, lakini jukumu la mwisho ni Waziri wa Mambo ya Nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa Mwenyekiti wa Governing Council ya UN–Habitant kati ya 2006 – 2008. Katika wadhifa huo alikuwa Co–Chair wa World Urban Forum ya Vancouver Canada 2006. Kwa kuwa, mkutano wa Habitant III, utafanyika Oktoba Ecuador ni mkutano unaotokea kila baada ya miaka 20. Mheshimiwa Waziri unashauriwa ku-check kuona kama Rais anaweza kuhudhuria mkutano huo. Kwa hivi sasa Mheshimiwa Rais wetu tayari anasifika duniani, akihudhuria Habitant III jambo hilo Kidiplomasia litaendelea kumsimika kama “Purposeful Traveller”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maoni yangu kama yakionekana yanafaa yafanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kutupa dakika tano tano kuonesha kwamba ni dakika za majeruhi. Katika dakika tano sijui nitasema nini! Bora niseme tu kwamba naunga mkono hoja ila ningependa yafuatayo yazingatiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa suala zima la kupeleka ukusanyaji wa kodi ya majengo TRA kunaleta ukakasi mkubwa. Hili nalisema kwa sababu ya utaalamu wangu kama mchumi, kimsingi naona halitekelezeki, kwa sababu litaleta mtafaruku mkubwa sana katika kugatua madaraka kwenda katika ngazi za Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili naomba mlione, najua wengi labda hatujalitafakari vizuri, lakini naomba kwa sababu nina dakika tano nalisema kama lilivyo, tukipata nafasi tutalifafanua, halitekelezeki litatuletea matatizo makubwa. Ninavyomjua Mheshimiwa Rais wetu yuko katika „Hapa Kazi Tu‟ hatuwezi kurudi kwenye mwaka 1972 Mwalimu Nyerere alipoondoa mamlaka za Native Authorities ilikuja kuleta ukakasi akabadilisha mwenyewe mwaka 1982 na alibadilisha kwa kuomba radhi. Mimi ni mtu mzima ni lazima niwaambie mambo yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Waziri ambaye ameleta hotuba nzuri, mambo ni mazuri lakini muda ni mfupi; kuna suala la mitumba.
Mimi hapa nawakilisha Mkoa wa Kagera imeshasemwa umefilisika. Mkoa wa Kagera watu wanafikiria kwamba, una fedha, hauna fedha. Kwa hiyo, lile andiko lako ulilotuletea Mheshimiwa Waziri liko sahihi, labda utuandalie semina watu waweze kukuelewa unavyopima umaskini, kwa sababu umaskini unaweza kuwa na hela leo kesho ukafilisika mambo yakawa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mitumba ndiyo imeondoa aibu iliyokuwa inatukuta wakati Mheshimiwa Salim akiwa Waziri Mkuu watoto walikuwa wanavaa plastic bags! Mimi ni mtu mzima nimeyaona kwa macho! Kwa hiyo, nafikiria kwamba, mitumba viwanda tuvijenge, lakini tuende taratibu. Wanasema safari ndefu inaanza na hatua ya kwanza. Tusianze kujitutumua tukaleta matatizo makubwa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji limeshazungumziwa na mimi nakubali kwamba, hizo shilingi 50 ambazo zimependekezwa na Kamati ziwekwe zitusaidie. Akina mama wanateseka na ninarudia tena, haya maji mngekuwa mnachota wanaume mambo yangekuwa yameshakuwa mazuri zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu ni la utata sana. Watu wanasema kwamba mtu atangaze mgongano wa maslahi! Mimi nilishawaambia mimi ni mdau wa elimu, sina mgongano wowote wa maslahi. Kuwaambia kwamba kodi ambazo zimewekwa kwenye shule binafsi ni sawasawa na kuziua hizi shule binafsi. Kwa hiyo, ni lazima tuziangalie hizi shule binafsi tuziwekee uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA wanafanya kazi nzuri, lakini TRA siyo panacea, anasema mzungu. TRA is not a panacea for all our problems! Hawawezi kumaliza matatizo yote. Tusiwabebeshe mzigo ambao utawashinda. Wafanye kazi na Halmashauri na Halmashauri tuzibane. Hata ya kwangu ya Muleba inanipa headache kabisa, lakini nafikiria kwamba, mchango wangu ni kuiimarisha ile Halmashauri na siyo kuiondolea mapato yake na siyo kuiondolea kuiwezesha. Kwa hiyo, suala la kuwezesha ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda na biashara; nimeona bajeti ilipokwenda, iko kwenye miundombinu na hilo nashukuru, lakini kilimo na viwanda na miundombinu vinakwenda pamoja. Suala la kilimo, kwa mfano Mkoa wa Kagera, kodi za kahawa ziko palepale. Hapo Mheshimiwa Waziri utakaposimama utuambie maana Mheshimiwa Rais mwenyewe ndani ya jumba hili alizungumzia kodi 27 kwenye kahawa. Sasa kwenye kitabu chako naona kahawa ni kama haipo. Mkulima wa kahawa ataachaje kupeleka kahawa Uganda kama unamuacha alivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nimepewa dakika tano, ninakushukuru sana, lakini ninasema kwamba bajeti iliyo mbele yetu italeta ukakasi tutakapofika kwenye Finance Bill! Hatujafika kule, lakini itabidi tupewe muda tuangalie mambo yanayopendekezwa kwa kweli mengine yana-far reaching implications, hayawezi kuruhusiwa kwenda hivi yatatuletea matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sijui kama muda bado upo, lakini ninasisitiza suala la mitumba, ninyi hamjawahi kuwaona watoto ambao hawajavaa nguo, mimi nimewaona kwa hiyo, lazima tuwalinde kabisa tuende pole pole, viwanda tuvijenge, lakini wanasema subira yavuta kheri. Nashukuru sana kwa kunipa muda.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adimu. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwapongeza kwa kazi nzuri ambayo mmefanya, mimi sikuwepo nilipata changamoto za kiafya lakini Alhamdulillah sasa nimerejea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama hapa mimi kama Mbunge wa Muleba Kusini iliyopo katika Mkoa wa Kagera. Kama mnavyojua mapori ya hifadhi na sehemu ambazo zina mvua za kutosha ziko katika Mikoa ya Kagera na Geita, kwa kweli tuko katika hali ngumu. Mheshimiwa Waziri na timu yake nawapongeza lakini kwa sababu ni mwanafunzi mwenzangu, research methodology tuliisoma wote, leo naomba aniruhusu niende kiutafiti. Nina nyaraka 10 (annexes) ambazo nitaomba Mheshimiwa Waziri azifanyie kazi asije akaniweka katika hali ngumu ya mimi kuondoa shilingi hapo kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii tuna migogoro ya wakulima na wafugaji, asilimia 28 ya nchi hii sasa hivi ni hifadhi. Mheshimiwa Profesa ambaye anafanya kazi nzuri, anatambua kabisa kwamba neno la Kiingereza la kutumia hapa ni untenable, kwamba hali hii haiwezekani kuendelea kama ilivyo business as usual, asilimia 28 ya Tanzania inaendelea kuwa hifadhi wakati watu hawana mahali pa kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kinadharia, haiwezekani Wabunge wengi wamechangia hapa na wote tunaelekea huko haiwezekani, something has to give way. Haiwezekani kwa sababu watu wameongezeka, sasa naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba Mheshimiwa Waziri Nchemba tarehe 22 Desemba, 2015 mara baada ya kupewa jukumu la kuongoza Wizara ya Mifugo alikuja Ngara akakaa na wananchi, akaingia makubaliano, akaleta faraja, akatupa matumaini naomba nyaraka ya kwanza appendix no.1 Waziri airejee, sina muda wa kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyaraka hii, kilichotokea ni nini, Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye tunajivunia sana sisi akinamama, Samia Suluhu akaandika barua ambayo naomba niikabidhi kama appendix no. 2 akiagiza kwamba mifugo iendelee kuwa pale ilipo mpaka hapo Serikali inajipanga. Sisi tukawaambia wananchi kwamba Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Jemedari Dkt. Magufuli haiwezi kuwaacha wafugaji hoi, kwa hiyo barua ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ipo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka telegraphically, tarehe 11 Oktoba, 2016 Mheshimiwa Waziri huyu Profesa ndugu yangu, akatoa tamko hapa akawaambia kwamba kulingana na maelekezo ngazi za juu basi wafugaji wabaki pale walipo, wakati anajipanga, naomba niikabidhi iko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naogopa maana dakika kumi siyo nyingi lazima niende telegraphically. Sasa kilichotokea na kinachoendelea sasa hivi from nowhere ile Kamati ya Serikali iliyoundwa ya kutafuta maeneo mbadala kwa ufugaji, mara wakaibuka kuwafukuza wafugaji kutoka kwenye mapori ya akiba. Hii ni contradiction kabisa na kwa kuokoa muda natoa nyaraka hapa kumsaidia Ndugu yangu Profesa Maghembe aangalie mambo yaliyojiri. Kwa sababu yeye ni mwenzangu na jirani ya jirani yangu hapa Mama Kilango wanatoka Upareni. Nimeleta hapa picha za ng’ombe wa Ankole wanavyofanana wanapopita kwenye shamba, hakuna linalobaki. Huwezi kusema una- support kilimo kama mifugo itatolewa kwenye akiba kiholela huwezi, it is not possible.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mkulima miezi sita amehangaika, lakini kundi la ng’ombe likipita in five minutes shamba limekwisha, kwa hiyo ndiyo hali halisi. Kwa hiyo, tatizo hili siyo tu la wafugaji ni tatizo la wakulima, kwa sababu wakulima wale ng’ombe watamaliza hayo mazao yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuokoa muda kinachofuata sasa, mapendekezo ya wafugaji wamekaa na Serikali, Mheshimiwa Waziri anajua hilo. Serikali kwa ujumla Serikali inayofanya kazi ya matumaini sasa inakuwaje hiki kitu kinatushinda wakati tunakwenda kujenga standard gauge na vitu vingine vikubwa. Kwa hiyo, nataka kuweka hapa mapendekezo ya wafugaji wenyewe, let us take it from the horse’s mouth, wafugaji wenyewe wanasemaje, wafugaji hawa wanatii Serikali, hawakaidi Serikali lakini hawawezi bila ardhi, kama huna ardhi huwezi kufuga.

Mheshimiwa Mwneyekiti, kwa hiyo suala la kuwapatia wafugaji ardhi, appendix zinaendelea ninayo ya nane hapa ambayo na yenyewe Waziri ataifanyika kazi. Apppendix hii inaonyesha kabisa mapendekezo na wafugaji wanavyohangaika, wana vijana makini, tunahangaika nao sisi, sasa inaonekana Mheshimiwa Waziri anakuwa mbali hawamfikii kwa urahisi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kama yote haya hayakutosha, tunavyozungumza sasa hivi wafugaji wameporwa ng’ombe wao kwenye mapori. Kwa kumsaidia Waziri katika kuja kujibu kesho, mimi msimamo wangu unatoka kesho baada ya kusikia majibu na nyaraka zote hizi za Kiprofesa nilizoweka mezani hapa. Huyu siyo kwamba ni Profesa pia ni my classmate, he knows what I am talking about. Suala hili ni nyeti, suala hili ni la Usalama wa Taifa naomba lifanyiwe lifanyiwe kazi. Ng’ombe 2000 wameporwa maporini, mtu msanii mmoja anasema anaendesha eti mnada maporini. Sasa mnada nani ananunua ng’ombe porini? Wanauziana wao kwa wao, It is totally unacceptable (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haya mambo anataka tuseme ukweli, nami ninasimama hapa kwa imani kabisa kwamba Serikali haiwezi kushindwa kitu hiki. Mitandao ya Ma-game wapo kule kwenye mapori wanaendesha minada ya kisanii wanauziana wao, naomba Serikali, Mheshimiwa Waziri Serikali watuletee taarifa hawa ng’ombe wamewauza wamemuuzia nani na sasa hivi hao ng’ombe wapo wapi, maana yake itabidi wawapeleke, siyo wapo kwenye misitu hiyo hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema hivi sitaki sensation nimeleta facts hapa kwa imani kabisa kwamba Serikali itazifanyia kazi. Kwa sababu, bila kufanya hivyo you forget kuzungumza mambo ya wakulima na wafugaji, viwanda vitatoka wapi, viwanda vya ngozi kwa mfano, kama huna mifugo huwezi kuwa na viwanda vya ngozi! kwa hiyo lazima tuwawezeshe wafugaji wetu, wakulima wamewasukuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hapa katika Jimbo langu watu wengi hata mifugo hawana, lakini jirani zangu kutoka Geita, kutoka Simiyu wako kule na ni Watanzania wana haki ya kuwa kule. Sasa wanaendesha propaganda ooh, unajua yule Mama Tibaijuka ni Munyamulenge na yeye ana mifugo, maneno ya rejareja kutukatisha tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wenzetu Rwanda kule kwa Kagame ni ng’ombe 10 hakuna mchezo. Kule kwa Mseveni anauza maziwa Dubai, wenyewe wameshapiga hatua kwa nini, because of land tenure, wametoa maeneo ya kudumu kwa hiyo wana Small Ranching Associations. Hicho ndicho kilio chetu naomba Serikali itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio msimamo wangu, Waheshimiwa Wabunge wenzangu twende conceptually tui- support Serikali hii kwa kuleta facts, wale ambao wanalinda maslahi yao kwenye ma-game na kuniita majina, mimi hayo majina hayanitishi, yaani wanasema ukijaribu kutetea hoja wanasema huyu ana maslahi binafsi. Kwa hiyo, inakuwa characterization watu wengi wanaogopa. Watu wengi wanaogopa kusimamia jambo hili kwa kuogopa kwamba watasema hawa ndiyo wana mifugo, lakini nataka kusema kwamba tafadhali sana hali ni tete, na ni suala la Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi za ufugaji tuondokane na migogoro; nimezungumzia Mkoa wa Kagera lakini the same applied to sehemu nyingi Tanzania nzima. Naomba kuwasilisha nashukuru sana, kesho ndiyo nitajua baada ya kumsikiliza Profesa mwenzangu kama naunga mkono hoja au naondoka na shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupewa nafasi hii. Naanza kabisa kwa kutoa pongezi na kuunga mkono hoja hii, bajeti iliyo mbele yetu kwa kweli imetayarishwa kwa umakini mkubwa na inahitaji kuungwa mkono. Kwa hiyo ninaposimama hapa nataka kuboresha sehemu mbalimbali ambazo nadhani Mheshimiwa Waziri akiendelea kuzifanyia kazi bajeti hii itakuwa bora zaidi kabla haijakamilishwa.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuokoa muda nina vipengele mbalimbali ambavyo nitaviwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri kwa maandishi, Ibara kwa ukurasa, lakini kwa ufupi tu nianze kabisa na ukurasa wa pili, Ibara ya 4. Mambo yote aliyoorodhesha na matukio makubwa yametokea na namuunga mkono, hiyo nadhani Mheshimiwa Waziri na nimewaambia wapiga kura wangu hii si kwa hila bali kwa kusahau, tukio kubwa sana lilitokea tarehe 10 Septemba, 2016, Mkoa wa Kagera ulikumbwa na tetemeko kali. Katika tetemeko hilo watu wakapoteza maisha yao na watu wakapoteza mali zao.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru sisi wa kutoka Kagera kwamba Waziri Mkuu hakuchelewa, alikwenda kwenye mazishi na hatimaye Mawaziri mbalimbali walikuja pale kutufariji na ninyi Bunge Tukufu mkachanga mchango ambao umetusaidia kwa wale wahanga walioathirika. Nawashukuruni sana.

Mheshimiwa Spika, sasa hii ni bajeti, nilitegemea na naomba Mheshimiwa Waziri aone kwamba sisi wahanga wa tetemeko hatujioni katika bajeti hii, watu walioathirika tunaendelea kuwaleaje ili kuwasaidia kuondokana na kadhia iliyowakuta?

Mheshimiwa Spika, nina pendekezo kwa Mheshimiwa Waziri, kwamba ahimize viwanda na aviwezeshe kufungua factory outlets. Factory outlet nadhani anaelewa maana yake, ni viwanda vya vifaa vya ujenzi hususan Kiwanda cha Twiga, Dangote na hao watu wa Tanga na Mbeya wawe na maduka yao kule Mkoa wa Kagera. Zile zinaitwa factory outlets, ni concept ambayo anaielewa, ni sehemu moja ya kusaidia watu kuweza kujenga makazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipofika kule, yeye anahangaika na shule na miundombinu tunamshukuru, lakini sasa wananchi vifaa vya ujenzi inakuwa ni ngumu kupatikana. Nitoe mfano, mfuko wa cement ‘X’ factory pale Dar es Salaam Twiga ni Sh.9,000/=; unapofika Kagera ni Sh.15,000/=. Kwa hiyo, unaona kwamba mwananchi wa Kagera, huyu mhanga wa tetemeko hawezi kwenda mbele. Hilo naamini kwamba atalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo napenda ku-highlight katika orodha yangu ya vitu kadhaa ambavyo naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, kuna issue ya ukwasi katika uchumi wetu. Mheshimiwa Waziri, yeye ni mchumi mwenzangu na anajua kwamba ukwasi ndiyo damu inayoendesha uchumi. Katika hili wamejitahidi sana, naomba nimupongeze kwamba katika bajeti hii mabenki yatawezeshwa sasa. Wamepunguza vile viwango, yaani minimum reserve wanayoweka kule Benki Kuu.

Mheshimiwa Spika, kuna sekta moja ya fedha ambayo Mheshimiwa Waziri anayoisahau, nami hapa nitangaze mgongano wa maslahi au na-declare interest kwamba mimi ni mdau pia wa Sekta ya Bima kama vile wengi tulivyo wadau katika Sekta ya Benki. Maana yake ukiwa na hisa katika sekta hizi, tayari umeshakuwa mdau, au siyo?

Sasa bima hizi; unajua ukwasi katika bima ni mbaya sana na unaendana sambamba na mabenki. Kwa hiyo, nafikiria hapo angepaangalia namna ya kuwasaidia wasije wakafunga Makampuni ya Bima, badala ya kujenga Makampuni haya tukakuta tunarudi nyuma. Kwa hiyo, hilo nalo ni la kufanyia kazi katika bajeti yetu ambayo ni vizuri.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho naomba nipongeze, tumesikia mengi kuhusu vyeti feki, Mheshimiwa Rais amekamilisha mengi. Watu ambao walikuwa na vyeti feki, nadhani sheria imefuata mkondo wake. Katika bajeti hii kuna kitu ambacho nimekiona kimeni-strike, kumbe kulikuwa na madai feki katika Serikali! Watu walikuwa wanaidai Serikali vitu, kumbe madai yao hayakuwa halali! Naomba jambo hili tulinyooshee bango; watu wanaokwenda kuweka madai feki Serikalini, nao tuwajue, maana Tanzania ni nchi ya uwazi na ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tupo katika awamu ya uwazi na ukweli, kwa hiyo, watu kama hao waliokuwa wanakwenda kudai zaidi ya shilingi bilioni zaidi ya 900 ambazo wamezikomboa, wajulikane ni akina nani, kusudi wawe blacklisted wasiendelee kutusumbua katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia hapo hapo niongezee kwamba katika bajeti hii ambayo ina mambo mengi, kuna suala la wakulima. Ninaposimama hapa, Muleba Kusini sisi ni wakulima wa kahawa, ndizi, mpunga na maharage. Sasa ukiangalia ruzuku zinazokwenda kusaidia
wakulima, Mkoa wa Kagera nasikitika kwamba hazitufikii kabisa. Katika hali hiyo, wakulima unawasaidiaje? Naomba nimpongeze na nishukuru kwamba kodi kwenye kahawa imepunguzwa, lakini bado kuna msururu wa kodi kwenye kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi maboresho ambayo wamefanya, hizi kodi 17 zilizoondoka, zimeondoka kwa wale ambao ni wafanyabiashara wa kahawa na viwanda vya kahawa, lakini mkulima bado amebebeshwa mzigo. Naomba Mheshimiwa Waziri yeye ni mchumi, afanye analysis, aangalie cost breakdown aone kwamba mkulima tunamsaidiaje?

Mheshimiwa Spika, nina pendekezo, hii cess ambayo imesemwa kwamba mazao ya biashara yanabaki kwenye 3%, tumetoka 5% mpaka 3% tunashukuru. Nataka nipendekeze kwamba mazao ya biashara sasa hivi na mazao ya chakula, yaani tofauti ni academic. Kwa mkulima, analima mahindi na kahawa ili auze. Sasa yule wa kahawa ambaye amebeba Taifa hili miaka mingi au yule wa korosho; ninapozungumza kahawa naweza pia kwenda kwenye mazao mengine. Kwa mfano, wakulima wa pamba, wale ambao wamebeba Taifa hili tangu uwepo wake, sasa hivi ni wakati wa Taifa kuwarudishia kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napendekeza hiyo cess na yenyewe iteremshwe ifike kwenye kiwango kinachostahili, wakulima waonekane sawa. Hapo sina budi kushukuru sana ukombozi ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta kwamba mazao tani moja mtu anaruhusiwa, ni ruksa kabisa kuyatembeza. Huu ni ukombozi kwa mkulima, pia kutusaidia sisi Wabunge huko kwenye Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa napambana na Halmashauri, wanaweka barrier feki, inabidi niziondoe. Mambo ni mengi, lakini nitayawasilisha kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza kabisa Waziri wetu na Naibu wake ambao kama mnajua wamebobea pia katika nyanja za Kimataifa. Kwa hiyo, tunapowauliza habari za diplomasia ya uchumi, Wahaya tunasema, usimuulize mganga wa kienyeji kondoo kapita wapi? Kwa sababu anaelewa anachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongezeni kabisa kwamba hapa hatua tuliyopiga siyo haba na kazi kubwa ambayo inafanyika katika uwanja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kiasi cha kwamba sasa hili bomba lililokuwa linaenda Kenya tayari limeshaingia Tanzania, tunamshukuru sana. Hili ni jambo kubwa sana, siyo jambo la kuchukulia hivi hivi, linataka diplomisia ya kiuchumi ambayo inafanyika nyuma ya pazia, wanasema ni lobbying. Huwezi kupiga kelele ukafanya mapinduzi makubwa kama hayo. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili naomba nipongeze sana juhudi ambazo zinaendelea pia kupanua wigo wa nchi rafiki, nchi ambazo zimepiga hatua kama Uturuki, nimeiona ni nchi ambayo naifahamu sana, nimeifanyia kazi kule na imepiga hatua. Kwa hiyo, wakija kutusaidia, nalo siyo jambo dogo la kubeza, tunawapongezeni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa nina dakika tano mbali ya pongezi, naomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama, nami unitoe dukuduku kwa yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tuna tatizo la mipaka ya nchi hii ambayo haina mikataba (treaty). Nchi hii mwaka 1979 ilipigana vita Uganda kwa sababu ya kutokuwa na mpaka ambao una mkataba wa Kimataifa. Ninaomba nijue kabisa unachukua hatua gani kukamilisha jambo hili?

Jamani ndugu zangu naomba niwaambie, Rais Museveni akiondoka madarakani Uganda, msishangae tukienda pia kupigania huu mpaka. Kwa sababu ule mpaka ni one degree South of the Equator na ukifuata protocol hiyo, Tanzania itapoteza ardhi kubwa sana. Kwa hiyo, ni jambo ambalo lina utata, naomba nijue kama Mheshimiwa Waziri analifanyiaje kazi? Hii inaendelea kwenye mipaka sehemu kadhaa…


TAARIFA ....

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Lissu utafikiria na ungeamini kwamba anajua anachokiongea. Naweza kusema kwamba mimi kama mtaalam wa sekta, huyu hajui anachokiongelea sasa hivi Mheshimiwa Lissu. Kwa hiyo, siwezi kupokea taarifa ambayo haina knowledge. Ni lazima mpaka uwe na treaty. Hili tamko la African Union ni aspiration peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nayakataa, naomba niendelee, nitakuja kumwelewesha zaidi Mheshimiwa Lissu baadaye nimpe habari anayotakiwa kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama atueleze ni jinsi sasa Tanzania tutakavyojipambanua katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo Mwalimu Nyerere na Amir Jamal walileta heshima za nchi hii. Shirika la UNCTAD sikuliona hapa katika orodha ya watu unaowasiliana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Rais wetu amekazana tusiibiwe madini, lakini kama huna mashirika haya including South Center kule Geneva, taasisi ambayo ilianzishwa na Mwalimu Nyerere kupigania haki za mambo ambayo tulikuwa tumeonewa, tukaweza kufutiwa madeni. Sasa nataka kujua mkakati ulionao Mheshimiwa Waziri kuhusu UNCTAD kutusaidia kuondokana na hii kadhia ya mikataba mibovu ambapo tumekuwa tumeibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kwenda na International Diplomacy sisi ni Taifa change, hatutaweza kufika, Rais wetu amejidadavua kama Mwalimu Nyerere, anapigania haki ambazo tulikuwa tumepokonywa. Sasa ninyi mnamsaidiaje kuhakikisha kwamba hatutatengwa? Kwasababu pia inabidi twende kimkakati (strategically), tusije tukajikuta tunaingia katika hatari ya kutengwa. Ni jambo ambalo nadhani ni diplomasia ya kiuchumi ambayo nilifikiria kwamba Mheshimiwa Mchungaji Msigwa angekuwa anaifahamu, lakini sikusikia akiizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa dakika tano, nilikuwa nataka kusema kwamba Afrika Mashariki, sasa hivi Kenya wameridhia Mkataba wa EPA (Economic Partnership Agreement), napenda kusikia Waziri anajitayarishaje sasa kuhakikisha kwamba zile athari zinazoweza kutokana na hali kwamba nchi moja imeshasaini na sisi bado, ni ipi? Sisi ni nchi inayoendelea, tuko protected na World Trade Organization, lakini ni vizuri kwa Wizara ya Mambo ya Nje kuwa wamejipanga katika hili kwamba athari zitapoanza kuonekana sisi tutalindaje maslahi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa dakika hizi tano, yangu ndio hayo. Ninaunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Sina budi kuanza kwa kusema naunga mkono hoja tena kwa furaha kubwa sana. Ungekuwa unaruhusu kidedea humu tungesema neema, neema, neema imefunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imepata bahati nzuri, bahati kubwa kwamba hayawi hayawi yanakuwa, hatimaye makubaliano haya au mkataba huu ukawa umesainiwa na sasa hivi unaendelea kuwa mkataba unaitwa treaty. Kwa hiyo, naomba kwanza niseme kama Watanzania tujue tofauti ya mkataba huu na ile mikataba ya madini, mikataba ya madini, those are contracts, ile ni mikataba ya makampuni, lakini hii ni treaty maana yake makubaliano kati ya Serikali na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba kabisa kusema tusipotoshe Watanzania kwa sababu tunataka kutoa mawazo mbadala. Katika suala hili tuungane kama Taifa na kama Bunge, kwanza kumpongeza Rais wetu kwamba hapa ameingiza goli, hapa utake usitake goli limeingia na hongera sana, tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili mimi nimelifuatilia kwa muda mrefu na najua kwamba ilichukua muda. Haikuwa kitu rahisi kwa mtu kufanya maamuzi kutoa zile concessions kama tulivyoona pale Chongoleani kwa wale tuliokwenda kuwawakilisha. Katika hili nawashukuru sana kwamba na ninyi mlihakikisha kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Kamati mbalimbali tulishiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niungane kabisa na Taarifa ya Kamati kama ilivyotolewa. Niwapongeze sana kwa kufanyia kazi mkataba huu. Nimesikiliza sana mapendekezo na mimi nakubaliana nayo. Sasa nasimama hapa kuongezea tu yale ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, mimi bomba hili linapita katika kata sita za Jimbo langu. Bomba hili linapotoka Ngenge linaingia Burungula, likitoka Burungula linakwenda Mubunda, likitoka Mubunda linapiga kona liko Karambi, likitoka Karambi linaingia Kimwani, likitoka Kimwani linaingia Nyakabango likipinda likitafuta Chato. Kwa hiyo, jamani ni mambo makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa niaba ya wananchi na naungana na Waheshimiwa Wabunge wengine walionitangulia waliosema kwamba sisi kazi yetu ni nini, kazi yetu kwanza ni kuuelewa mkataba huu na kuusifu na kujua kwamba katika mkataba wa nchi kwa nchi ni give and take, huwezi kusema kwamba utachukua kila kitu uweze kuleta bomba Tanzania, au siyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, bomba hili lilikuwa na njia tatu na mnajua kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alikazana sana kulitoa Kenya kulileta huku, si kazi ndogo, naomba kabisa Bunge hili tumpigie makofi. Katika kulileta, katika mikataba, dhana ya treaty, dhana ya mikataba lazima uwe na concessions, sasa tuko katika kipindi ambacho tunaangalia mikataba yetu, hatutaki kuingia katika mikataba mibovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba mibovu inatokana na usiri, sasa tuko hapa tunajadili jambo na Kamati imeshaona mkataba unavyokwenda, sasa kuboresha, lakini watakapokuja wanaweza kuja wakasema tunapata nini. Mimi nilikuwepo Chongeleani, Tanga na Mheshimiwa Rais alisema faida tutakazozipata kwa hesabu ya haraka, mapipa 216,000 kwa siku na bei inaweza ikayumba lakini kwa bei ya chini tuliyoambiwa zilikuwa ni dola 12 kwa pipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kila siku tuna uwezo wa kupata dola 2,592,000, hapo utasema kwamba Dkt. Magufuli hakucheza jamani? Alicheza, kwa sababu mafuta haya sio ya kwetu, mafuta ni ya Waganda lakini na sisi tumeingia pale kwa sababu tumepata ushoroba, kwa hiyo tulinde amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuhimiza kwa wananchi wangu, tungependa amani. Sisi kazi yetu lazima tuwe na ulinzi shirikishi, ulinzi wa kitaalam lakini pia ulinzi shirikishi. Kulinda bomba hili litakuwa ni jukumu la Watanzania wote. Tumelipata kwa sababu ya utulivu ambao kwa kweli wahenga waliufanyia kazi na sisi tunaendeleza. Kwa hiyo, ulinzi ndicho kitu kikubwa ambacho nakiona hapa lakini pia na fursa na ajira ambazo Mheshimiwa Waziri ameshasema katika hotuba yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika suala la ulinzi naomba sasa tusiibue migogoro ya ardhi. Naposimama hapa kule kwangu kuna watu wanapima ardhi katika hizi kata nilizozitaja ambapo bomba linapita na mimi kama Mbunge wa eneo wala sina taarifa yoyote. Kwa hiyo, naomba jamani hapa Serikali, Mheshimiwa Waziri, msituchanganye na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo naomba utusimamie. Suala hili, Waheshimiwa Mawaziri, mimi ntakuwa mkweli, nikiona mnasuasua mimi nakimbia naenda kwa Waziri Mkuu, naamini watatusaidia huko ngazi za juu kama ikibidi lakini tusifike huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabisa katika upimaji wa ranchi, watu wanaosema wanapima ranchi katika maeneo ambapo bomba linapita wanatuchanganya. Wananchi sasa hivi kuna taharuki kubwa sana, wananchi wanalia kabisa nbagila bati twafa twafa. Sasa kilio kule twafa, twafa, wakati tunasubiri bomba, sasa bomba likija upimaji wa bomba utakwendaje? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamezungumzia fidia, fidia ni muhimu na wanaochanganya mambo ya ardhi, ile ardhi itatwaliwa kwa fidia kwa mujibu wa sheria inakuwa sasa bomba litapita katika ardhi ushoroba itakuwa ni mali ya Serikali, haitakuwa tena mali ya watu binafsi. Huwezi kupitisha bomba la Serikali katika ardhi ya watu binafsi, itatwaliwa ile ardhi lakini mimi mwenyewe kama nilivyosema, tutasimamia haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa hili na wewe utuwekee nguvu, hao watu ambao wako kule Muleba wanawachanganya wananchi, naomba Serikali, Mheshimiwa Waziri ananisikia, naomba watusaidie.


Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipofika Biharamulo alisema kwamba suala la mifugo ni ufugaji wa kisasa sasa, mambo ya kurandaranda na mifugo hakuna tena. Kwa hiyo, tunakwenda kupima ardhi lakini kwa taratibu. Huwezi kupima ardhi za vijiji bila kuzihawilisha kwanza. Mimi ninavyojua mchakato wa kuhawilisha ardhi mpaka Rais anatoa notice ya miezi mitatu, sasa hiyo notice ya kwenda kuipima Muleba imetoka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili pia niliwasilishe, na suala lenyewe ni tete tena linavuruga bomba la mafuta, maana yake ni kwamba linakwenda kuvuruga amani tunayoizungumzia. Naomba barua hii ambayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, pia kwa Mheshimiwa Mwijage yeye mdomo wake hawezi akasema zaidi hapa labda lakini mimi nalitaja wazi wazi hapa. Wananchi wa Muleba hawawezi kutuelewa mimi na Mwijage hatutaeleweka na Wabunge wengine hapa kutoka Mkoa wa Kagera tusipozungumza suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili pia litavuruga amani, linapandikiza mgogoro wa ardhi, sisi hatukubali na tunaomba Serikali itusaidie, naamini watendaji wamekurupuka, wamekwenda kule bila kufuata utaratibu naomba mtusaidie na naomba barua hii niiwasilishe kwako na iwe sehemu ya Hansard. Kusema kwamba huwezi kwenda kupima kata sita, kata kumi. Hata na kule Kaskazini pia wameathirika hata sisi wawakilishi wa wananchi hatuna habari, wananchi wanatupigia simu katika taharuki kubwa sana. Wakati Mheshimiwa Rais alipokuwa Biharamulo alifafanua…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tibaijuka malizia maelezo yako dakika moja.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kimsingi ni siku ya furaha, ni wale wanaotaka kutuharibia hao ndio tujadiliane nao lakini nadhani hili ni jambo jema limekuja Tanzania, vijana changamkeni, jifunze mgambo, mkalinde bomba la mafuta. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Wizara ya Kilimo kwa kujitahidi kutuletea mpango mzuri ambao kazi yetu sasa ni kujaribu kuonesha namna ya kuboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ibara ya 239 ukurasa wa 99 Mheshimiwa Waziri ameanza vizuri, ameanza kwa kuanza kwa kutupa mihimili minne ambayo sasa ataitumia katika kuendesha kilimo. Kwa umuhimu wake ninaomba ninukuu muhimili wa nne ukurasa wa 129 anasema anakwenda; “kuweka mfumo mpya wa usimamizi wa kilimo, kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa uendeshaji kibiashara na kuwezesha wakulima kuwa na sauti katika uendeshaji na biashara ya mazao yao.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kumpongeza sana Waziri kwa mkakati huu na kwa wale waliokuwa wanasema Waziri hatoshi mimi naomba nitofautiane nao, anatosha kabisa. Anatosha kwa sababu ametuonesha principles zake, sasa mimi naomba nioneshe matatizo ambayo nadhani yatakukwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza kabisa katika nchi hii labda wengi hatutambui kwamba mazao ya kimkakati kimsingi yanaendeshwa kwa sera za kikoloni ambapo mazao yale kimsingi sio mali ya wakulima, yanachukuliwa hususani kama mali ya Serikali. Jambo hili naomba litambulike na mimi nasimama hapa kwa niaba ya walionituma, wananchi wa Muleba Kusini na niseme kwamba Kagera kwa ujumla na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kilimo katika Jimbo langu la Muleba Kusini na kusema Ukanda wa Ziwa kwa ujumla ni taabani. Ni taabani kabisa ukweli ndio huo, hali si nzuri na tukiendelea hivi bila kumuunga mkono Mheshimiwa Waziri na kuleta mawazo ya kisasa, mawazo yanaweza kuleta mapinduzi katika kilimo tutaendelea kutaabika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoona katika Ibara ya 178 wanazungumzia kwamba hatimaye watafikiria mpango wa mkakati kama wa SAGCOT kwa ajili ya Kanda ya Ziwa, mwaka jana nilisema na ninarudia kusema kwamba umechelewa Mheshimiwa Waziri, nataka kujua hiyo LAPCOT (Lake Province Agricultural Growth Corridor) inaanza lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nchi yetu ilivyo ni vizuri kwamba SAGCOT iendelee na ni haki ni lazima tuipe nguvu lakini wakulima wa Kusini hawawalishi wakulima wa Kaskazini, hawawalishi Mikoa ya Ziwa, ninasimama hapa watu wamenituma hapa tena wananiamini kabisa neno mgomba hakuna neno mgomba katika kitabu hiki, jamani ndizi siyo chakula? tena sisi Wahaya tunasema kama ndizi haziko mezani na chakula hamna au siyo? Zao la ndizi/ mgomba umesahaulika kabisa this is not serious, hatuwezi kuwa na mpango wa kilimo ambao umesahau kabisa zao la mgomba! Hilo ni la kwanza naomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama mimi ninaimani na wewe uje uniambie imekwendaje Mheshimiwa Tizeba imekuwa Tizijuka umesahau kabisa? Maana yake majina haya yanashabihana kwa wale ambao hawajui lugha hizi, yaani tumekwendaje. Hiyo naomba Mheshimiwa Waziri lijibiwe tujue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mnyauko tulikuwa tunahangaika hapa na mnyauko, this is now forgotten completely hakuna hata neno lolote la kusaidia wakulima wa migomba nchi nzima, mind you hata Mbeya SAGCOT wako, hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili niongelee ushirika kwa haraka. Ushirika nilisema wakati tunajadili bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu mambo mengine ambayo ameyafanyia kazi naona vijana wa TRA wanaanza kujipanga upya nashukuru sana, lakini suala la ushirika msiuchukulie kama tukio, sasa hivi Mheshimiwa Tizeba huna uwezo wa kuingia Muleba kununua kahawa yote. Ulikwenda kule nakushukuru lakini nilisikiliza ile speech yako uliyoyasema yale hayawezi kumsadia bibi kizee kama mimi ana magunia yake mawili pale mlangoni unamuambia abebe magunia apeleke kwenye chama cha msingi ambacho hakipo, ambacho kitafunguliwa kimechelewa, wakati ana uwezo wa kununua direct farm gate price kuuza kahawa yake kwa mteja wakapeleka . (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani muangalie implications za vitu tunavyovipanga vingine havitekelezeki kwa mtu anayejua hali halisi ya kijijini, naomba Mheshimiwa Waziri unahitaji time, tukupe time ya mwaka huu uandae ushirika uje next year kutuambia direct purchase, farm gate price tunafunga na inayoeleweka kusudi tuweze kushiriki. Hii hii umeshtukiza mno it can’t work! Lazima niwe mkweli kwako kwamba hapa tunapozungumza wenzangu wa Kigoma watasema, lakini kahawa imevuka. Kwa hiyo mambo haya Waziri anaenda vizuri tumuwezeshe na mwisho kabisa tumpe wataalam wa ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Kilimo hana watalaam, huyu Waziri he is a general without an army! Maafisa Ugani wako chini ya Halmashauri, namshukuru sana Mheshimiwa Rais hatimaye Maafisa Ardhi wamerudishwa, Mabwana Shamba ni Wataalam wamesomea hizi fani, warudishwe kwenye Wizara mama waweze kuwajibika, sasa hivi wanafanya wanalotaka huko. Kwa hiyo, Maafisa Ugani hawapo nadhani tutakwama kwa mambo haya. Kwa hayo mambo matatu na utafiti ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbegu hasa nimeona hapa Agricultural Seed Agency na wenyewe wanazo tani 700 wakati nyingine zote zinatoka nje, ninaomba uwezeshe agricultural seed agency kununua sasa mbegu kwa ajili ya distribution kwa wakulima, huo ni ushauri wangu, nafikiria kwamba Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri, lakini mfumo alionao hauwezi kumruhusu kwenda mbele. Kwa sababu kama wakulima wanamiliki mazao yao basi tuwape nafasi hawa watu wakulima ambao wako kwenye fair trade watu wa kahawa ambao wako kwenye fair trade, organic trade wale waruhusu hawana haja ya kuja kwenye mnada wa Moshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnada wa Moshi kile ni kituo cha mazao tu mnada huko London na New York, kama unataka kupata bei nzuri auction zipo London zipo New York pale Moshi tunafanya coordination tu na coordination inaweza ikafanyika pia kwa kutumia farm records. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiria kwamba wataalam wako Mheshimiwa Waziri wakupe proper analysis ya mambo yalivyo wengine humu tunayaelewa, tuko tayari hata kusaidia, lakini ukija na vitu ambavyo havitekelezeki, kwa mfano ukisema kwamba kwa dharura unazuia watu kuwasaidia wakulima itakuwa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache atakaporudi naamini kwamba tutaelewana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nampongeza Waziri na timu yake kwa hotuba na bajeti nzuri. Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii kwa wapiga kura wangu ambao huko Muleba Kusini ni ama wakulima ama wafugaji ama wavuvi, nitachangia vitu muhimu katika sekta hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo huko Muleba Serikali ni kama imetusahau, hatuna wala hatuoni jitihada za Serikali kuwaendeleza wakulima wa kahawa na wakulima wa migomba, maharage, mihogo, viazi vitamu na kadhalika. Nasema hivi nikiwa pia shahidi kwani nami ni mkulima. Sijamwona bwana shamba wa Wilaya akipita kuangalia hali ya mazao. Rais wetu mpendwa ameelekeza msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Sijui tatizo la hawa Mabwana Shamba ofisi na Mabwana Shamba mashamba, Mheshimiwa Waziri anatusaidiaje na je, tatizo lao ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri awasikilize nao wamweleze tatizo lao, wakulima hatuna msaada sana wa Ofisi ya Kilimo Wilayani. Haigawi pembejeo, haitoi utaalam, haitutembelei kujua tatizo ni nini. Serikali, tena ya Awamu ya Tano itusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wanahitaji ardhi, lakini watu wameongezeka na ardhi inazidi kupungua kwa uwingi wetu na uwingi wa mifugo. Kwa hiyo, land pressure, uhaba wa ardhi hivi sasa ni mojawapo ya matatizo yanayoikabili nchi hii. Juhudi za Rais wetu kuendeleza viwanda zitasaidia kupunguza land pressure kwani vijana watapata ajira viwandani, kwa sasa viwanda bado, pamoja na hatua nzuri za uhamasishaji zinazoendelea. Kwa hiyo, vijana wanahitaji kupewa ardhi, ili wajiajiri katika kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itueleze ina mpango gani kuorodhesha vijana wote wasio na ardhi waume kwa wake ili wapewe ardhi na kujiajiri katika kilimo. Kuwaacha wazazi peke yao ndiyo wahangaike kuwapatia vijana wao ardhi kuanzisha mashamba ya kisasa haitasaidia. Mheshimiwa Waziri anatambua bila kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na umwagiliaji viwanda vitashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna viwanda bila malighafi na malighafi inatokana na kilimo. Naomba Serikali na Waziri anapohitimisha anieleze mpango wa kuwapatia ardhi vijana wa Kata za Muleba ambazo ni Kushasha, Ijumbi, Nshamba, Biinabo, Ikondo na Kibanga, Bereza na Muleba kuhamishwa na kupewa mashamba ukanda wa Ziwa Burigi. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hili alichukue na kulifanyia kazi. Vijana katika Kata hizi wana haki ya kuhamia Mjini kwani hawana pa kwenda, hawajakataa kulima ni landless, hawajawezeshwa, tunaomba youth resettlement program ndiyo hali halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake Muleba hatumiliki mashamba ya migomba au vibanja, ni mali za ukoo kwa kawaida, lakini wanawake tuna jukumu la kulima mfano mahindi, maharage, karanga, kwenye grass lands au nyeya. Sasa uhaba wa ardhi umefanya mashamba ya migomba pamoja na miti kupanuliwa hadi kwenye hizo nyeya, matokeo yake wanawake uchumi wao na lishe vinakosekana kwenye familia kwa kukosa mikunde, legumes, ambayo inatoa protini, isitoshe zile sehemu ndogo zilizobaki wanapolima na mifugo nayo haina sehemu za malisho. Mheshimiwa Waziri naomba atueleze ana utaratibu gani kuwapatia wafugaji maeneo ya kuendeleza ufugaji wa kisasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji hawana maeneo, wapo kwenye mapori ya akiba siyo kwa kupenda, bali kuepuka migogoro na wakulima. Nasikitika kutamka bayana kwani Serikali na hasa ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, jambo hili ama hajaonekana kulielewa au anaamini propaganda za wanaonufaika kwa kudai rushwa kutoka kwa wafugaji katika mapori ya akiba kwamba, mifugo ni ya Wanyarwanda na Waganda huko Kagera. Naomba Serikali ilete taarifa zake katika jambo hili katika uwazi ili ukweli ambao Rais anahimiza ujulikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtandao muovu unaoeneza propaganda hizi na wananchi tuko tayari kueleza ukweli. Tanzania ya viwanda haiwezi kushamiri bila kupunguza eneo la hifadhi kutoka asilimia 28 ya sasa na kugawa kiasi cha kutosha kwa wafugaji ili wapewe hati ya ardhi kukopesheka na kuanzishwa small scale ranching association. Hakuna njia nyingine, kupora mali za wafugaji kwa kutaifisha mifugo yao bila kutuonesha hiyo mifugo imenunuliwa na nani na imehamishwa kwenda wapi baada ya kunadiwa huko porini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutuhadaa, kusababisha umaskini badala ya kuuondoa. Kuswaga mifugo kutoka mapori ya akiba kuzingatie agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa Wakuu wa Mikoa kwamba, wabaini maeneo ya ufugaji kabla ya zoezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, wavuvi wasisumbuliwe na nyavu ndogo wakati hawahusiki na viwanda vinavyozitengeneza na kuziingiza nchini. Ziwa Victoria ni hazina ambayo haijapewa kipaumbele. Mheshimiwa Waziri anajua usalama wa wavuvi hautoshi, majambazi yanapora na kuua. Serikali inaombwa kuendelea kutumia vyombo vyake katika eneo hilo. Aidha, utaalam wa ufugaji wa samaki katika ziwa lenyewe bila kuathiri mazingira ni jambo ambalo litahitaji utafiti wa Serikali kuonesha njia kama sehemu ya kuendeleza viwanda vya samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nfasi. Naomba nianze kabisa kuungana na Taifa kwa ujumla katika simanzi kubwa iliyotukuta kuondokewa na mojawapo ya Mtanzania maarufu aliyefanya mambo mengi, Dkt. Reginald Abrahamu Mengi. Nachukua nafasi hii kutoa pole sana kwa wanafamilia na pia kumshukuru sana kwa msaada wake alioutoa kwa watu mbalimbali, hususan kwa sisi ambao tunashughulikia elimu bora kwa wasichana ambao hawana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mengi alikuwa ni mtu mkarimu na waswahili wanasema kutoa ni moyo sio utajiri. Kwa hiyo, tunaomba sana familia yake iyachukue kama yalivyokuja na Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kusema kwamba, pigo kubwa kwa sababu, siku kadhaa zilizopita wakati Marehemu Ruge Mutahaba amefariki, pia na Ephraim Kibonde wote tulikuwa katika chumba kimoja pale Karimjee, lakini hizo ndizo njia za Mwenyezi Mungu ni pigo kubwa kwa Taifa. Na ninasimama hapa kwa majonzi makubwa leo, jana tumempoteza Prof. Robert Mabele wa Chuo Kikuu cha Dar- es-Salaam na yeye nichukue nafasi hii kumshukuru kwa mchango wake katika kufundisha wachumi wengi ndani ya chumba hiki, nadhani na Waziri wetu wa Fedha ni wanafunzi wake kwa hiyo, ni pigo kubwa kwa Taifa, Mwenyezi Mungu amrehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana sasa niende kwenye ajenda, nianze kuungana pia na wengine kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Ummy na Makamu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mheshimiwa Dkt. Ndugulile alipata nafasi kunitembelea kule na kwa sababu yeye ni daktari mambo ya Muleba aliyaona kwa karibu na alifuata hata na Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu ulifika pale Rubya Hospital ukatembelea hospitali teule ya wilaya, kwa hiyo, naomba nianzie hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa nchi hii katika kutoa huduma ya afya ambayo sina budi kupongeza juhudi kubwa ambazo zimefanyika katika Awamu ya Tano. Juhudi ambazo tumesikia wakati Waziri Jafo anaorodhesha hospitali ambazo tumejenga za wilaya ni jambo la kujivunia. Mwemyewe kwa upande wa Muleba Kusini tunashukuru kwamba, vituo vya afya viwili Kimea na Kaigara vimeimarishwa, upasuaji sasa hivi unaendelea. Jambo hili kwa kweli, tunashukuru sana juhudi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Rubya naomba niseme kwamba, nikiiangalia Rubya kwa karibu, lakini na hospitali nyingine kwa ujumla hizi zinaitwa designated hospitals. Utaratibu wa public private partnership naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba, ni utaratibu muhimu sana. Na tunapoboresha hospitali za Serikali tusisahau pia umuhimu wa kuhakikisha kwamba, zole ambazo tulikuwanazo nazo tunalinda uwezo wake kwa sababu, isije ikawa ni wazungu wanesema, you rob Peter to pay Paul; tusimuibie Paulo kumlipa Petro, hapa inatkiwa balance.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba sana Mheshimiwa Waziri anapojumuisha tusikie mkakati alionao kuhakikisha kwamba, hizo hospitali tulizokuwanazo zinaendelea pia, kufaidika na hii partnership iliyokuwepo la sivyo tunaweza tukajikuta kwamba, hospitali zinadidimia. Sina budi kusema kwamba, hospitali sio majengo, hospitali ni huduma na katika hili niunganishe hapohapo kusema kwamba, Mheshimiwa Waziri pia, aangalie hali halisi ya referral hospital zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza sana juhudi za Serikali ya Awamu ya Nne iliyokamilisha Hospitali ya Mloganzila, lakini Mloganzila hospitali majengo, hakuna Hospital town pale kwa ajili ya madaktari kukaa karibu na hospitali. Na hata huyo Profesa Mabele ambaye namsema kafia Mloganzila nilikwenda kumuangalia tu juzi nikakuta kwamba, kama kuna dharura daktari anafikaje Mloganzila? Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kufanya uwekezaji kuhakikisha kwamba, kituo kinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye Hospitali ya Rubya ninaomba sana Mheshimiwa Waziri Ummy unapafahamu, ulikuwa unataka kuleta mashine ya viral load kwa ajili ya upimaji. Sasa hivi mashine hiyo tunasikia kwamba, imehamishwa imepelekwa Bukoba na vifaa vingine. Hata na watumishi wa maabara tunapozungumza hospitali haina any degree holder kwenye pharmacy.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hospitali inayohudumia wilaya, wakazi laki saba. Kama una wananchi 700,000, huna maabara ambayo ina a qualified technician unaona kwamba, hapo huwezi kwa kweli, kutoa huduma inayostahiki. Kitengo cha meno pale kiko katika hali mbaya kwa hiyo, nafikiria kwamba, Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri mnayoifanya na utaalamu mlionao ni muhimu sana kwamba, pia, kuweko na uboreshaji tuhakikishe kwamba, hospitali zetu za zamani hazitasambaratika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mwisho kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nataka kuweka mkazo kwa mchango wangu kuhusu umuhimu wa utawala wa sheria na haki, utaratibu wa kukamata watu kwa tuhuma ambazo DPP hana ushahidi si sawa kabisa. Kuwaweka watu rumande kwa muda mrefu halafu mchezo wa “uchunguzi haujakamilika” si sawa kabisa, ni uonevu, hakika. Kama mtu anatuhumiwa kutenda kosa uchunguzi ufanyike na sheria ichukue mkondo wake lakini mtindo mpya wa kubambikiziwa mtu kesi au charge ambazo hazina dhamana kusudi asote rumande miaka nenda, miaka rudi, si haki, si sawa na ni kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, magereza zimejaa watu ambao wametuhumiwa makosa ya kawaida mfano,traffic case lakini wamenyimwa dhamana wako jela miezi hata miaka. KatikaGereza la Muleba nimeshuhudia wanawake waliowekwa mahabusu ili wapishe waume zao kuuza mashamba ya familia. Nimeshuhudia watu walio mahabusu muda mrefu kwa sababu ya ugomvi. Hata kesi za mauaji inabidi ziwekewe mkazo na uchunguzi ufanyike na Nolle prosequi zitoke kwa muda muafaka na zisipotoka basi kesi zisikilizwe kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mhimili wa Mahakama uko huru na ni muhimu sana uhuru huo udumishwe. Mhimili wa Mahakama sharti ujitathimini. Tunashuhudia baadhi ya Mahakimu hasa ngazi za Mahakimu waMwanzo na Wilaya wakila rushwa za waziwazi, unakuta Hakimu Mkazi anafanya mtandao na viongozi wenyeji wenye uwezo kuwanyanyasa wananchi kwa kubuni kesi ambazo zinahukumiwa na mtu anashindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nililalamikia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Mubunda huko Muleba, Ndugu Omar Musa kwa tabia yake mbaya kutoa hukumu kwa dhuluma. Hakimu huyu alipokuwa Mahakama ya Mwanzo, Kashasha, Wilayani Muleba alisababisha mtoto kumfunga mama yake mzazi katika mgogoro wa shamba. Nililazimika kulipa faini aliyoikosa huyo mama iliatoke mahabusu lakini huyo mama alikufa siku mbili baadaye kwa huzuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hakimu huyo alipohamishiwa Mubunda akajiingiza katika kesi za Diwani wa Kata ya Kashurunga, Ndugu Khalid Swalehe na kuwafunga Mwalimu Mkuu wa Shule huko Kimeyo na mke wake na baadaye Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkomero katika mgogoro wa eneo la ardhi ya shule. Diwani anataka kupora eneo la shule na mwalimu na mke wake na Mwenyekiti wanatetea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa juhudi zangu kutetea suala hili hadi leo zimeshindwa. Nimeambulia kutolewa tamko la Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) juu ya matamshi ya Mbunge wa Muleba Kusini dhidi ya Mahakama isiyo na tarehe lakini iliyosainiwa na Rais wa chama hicho, Jaji Wilberforce Samson Luhwago.Ni tamko la pages saba linanilaani mimi kwa kulalamikia Mhimili wa Mahakama mara kwa mara na hatimaye kulalamika katika mkutano wa hadhara mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naambatisha tamko hilo ili liwe sehemu ya Hansard ya mchango wangu. Yaani mimi mtu wa kawaida ninatolewa tamko na Chama cha Mahakimu na Majaji kwa kufanya kazi yangu ya Ubunge ambayo ni kutetea wananchi na kuijulisha Serikali na Mhimili wa Mahakama juu ya mapungufu waliyonayo ili wayafanyie kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maelezo juu ya suala hili na hatma yangu nikiwa na kesi Mahakamani nani ataisikiliza kwani tamko hilo lilidaiwa ni la Majaji na Mahakimu wote. Kwa dharau kabisa hadi leo Hakimu Omar Musa bado hajahamishwa kutoka Mubunda hivyo kunipa kazi ya ziada kuwatuliza wananchi wenye hasira wasifanye fujo. Naomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitolee ufafanuzi jambo hili na kunielekeza juu ya utaratibu wa kusikiliza kesi zangu zinapokuwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Mhimili huu katika kujitathmini waangalie mtindo mpya wa baadhi ya Mahakimu wasio waadilifu kufanya kazi na Mawakili wasio waadilifu. Kwa hiyo, mtuhumiwa unaelekezwa na Hakimu kama unataka kushinda kesi kamlete advocate fulani. Mhimili huu ujitathmini kwani changamoto za rushwa zinawaumiza watu ambao niinnocent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nianze kwa kuungana na Taifa zima kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Dkt. Reginald Mengi kilichotikisa Taifa zima. Dkt. Mengi amefanya mengi katika Taifa hili, hivyo tumuenzi kwa kuendeleza mema na wema wake. Aidha, kifo chake kimetokea kikifuatana na cha kijana mahiri Ruge Mutahaba na Ephraim Kibonde. Ni pigo kubwa pia jana tu tumempoteza Mtanzania mwingine Prof. Robert Mabele kilichotokea Hospitali ya Mloganzila. Profesa Mabele amewafundisha wengi na hata Waziri wetu wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango ni mwanafunzi wake. Tuwaombee wote pumziko la milele.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite katika hoja ya leo ya afya. Nami naungana na wengi kupongeza kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na msaidizi wake Mheshimiwa Dkt. Ndugulile. Wote wametembelea Wilaya ya Muleba na kuona maendeleo na changamoto ambazo naomba niziorodheshe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajua tuna Hospitali Teule ya Wilaya ya Rubya, aliitembelea. Tatizo ni kwamba utaratibu wa PPP katika kutoa huduma unaweza kuleta mkanganyiko ikiwa utaratibu wa kulinda uwezo uliojengwa hautawekwa bayana. Hospitali Teule ya Rubya imepoteza wafanyakazi muhimu na vifaa, wamehamishwa. Kwa hiyo, hakuna degree holder tena katika ukurasa wa tatu utaona hakuna maabara wala generator.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mashine ya viral load imehamishwa na kwenda Bukoba. Hii inadhoofisha uwezo wa hospitali teule kuhudumia wananchi takriban 700,000 katika Wilaya. Upanuzi wa hospitali mpya usimaanishe kudhoofisha zile za zamani. Naomba kujua mkakati wa kuepusha jambo hili, tusipoteze uwezo uliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rubya pia kitengo chake cha meno hakitoshi kabisa, ni kama hakipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile uboreshaji wa vituo vya afya viwili; Kaigara na Kimeya tumeshuhudia na sasa upasuaji unaendelea. Hata hivyo, bado kuna upungufu wa maboma. Ninaomba jambo hili liangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ujenzi wa zahanati kadhaa kwa nguvu za wananchi unaendelea karibu katika kata zote. Tatizo ni fedha za kununua vifaa vya viwandani; saruji, nondo, vioo na kadhalika. Naomba Wizara iangalie jinsi gani ya kupata fedha kukamilisha ujenzi wa zahanati hizo ikiwemo zifuatazo: Buhangaza, Buganguzi, Kishando – Muleba, Burunguna, Muzinga – Nshamba, Kashanda – Kubirizi, Kasindaga – Kata Kamombi – Kangazo – Nyakabango.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaona kwamba mahitaji ni makubwa sana. Bila Wizara ya Afya na TAMISEMI kutuwekea nguvu itakuwa vigumu kumaliza zahanati hizi. Eneo linalohudumiwa ni kubwa. Sina budi kuwashukuru TANAPA kutusaidia katika ujenzi wa zahanati kisiwa cha Ikuza. Ni Ukombozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy kutusaida kupata ambulance ya Hospitali ya Rubya. Pia, tunazo kwenye vituo vyetu vya afya, lakini wakati mwingine ambulance inasimama kwa sababu ya kukosa dereva. Ni suala la TAMISEMI, lakini ninaamini Wizara ya Afya ni mdau mkubwa katika jambo hili. Jamani hospitali kusimama kwa sababu tu hakuna dereva! Kama haupo utaratibu, tunaomba mwongozo utolewe wa kumewezesha Mkurugenzi kuhakikisha kamwe ambulance haisimami kwa kukosa dereva.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ajira kwa Madaktari na Wauguzi. Ni jambo la kushangaza kuwa baadhi ya Madaktari wanahitimu lakini wanahangaika kutafuta ajira na wengine kukata tamaa na kwenda nje ya nchi. Ninaomba kujua, hivi sasa tuna Madaktari wangapi ambao bado hawajaajiriwa, huku uhaba wa Madaktrai na Wauguzi mbalimbali wakiwa hawatoshi katika hospitali zetu. Naomba mkakati wa manpower planning kwa Sekta hii uwekwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mloganzila imekamilika na ninapongeza juhudi za Awamu ya Nne zilizoijenga, lakini naamini ni muhimu sasa kuwa na mpango wa kujenga hospitali town. Hivi sasa madaktari hawana makazi na sijui kama dharura ikitokea itakuwaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, MSD ya Kanda ya Ziwa Magharibi ipo Muleba. Mheshimiwa Waziri anajua kulikuwepo na tetesi kwamba itahamishwa kwenda Bukoba. Mheshimiwa Waziri Dkt. Ndugulile alitembelea MSD hiyo na kuona athari za kuihamisha. Aidha, mantiki ya kuiweka Muleba ni kwa kuwa ni katikati ya eneo la huduma; Kagera, Geita na Kigoma Kaskazini. Naomba hofu hii ya kuhamisha MSD ya Kanda iondolewe ili maendeleo yaliyopangwa yaendelee. Eneo la kutosha ekari tano zimetolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bima ya Afya ni mkombozi na tunapongeza maendeleo yake. Changamoto zinazojitokeza ni ngazi ya referral system. Inaonekana hakuna manual ya recommended drugs kwa Hospitali za Rufaa. Hicho hicho cha hospitali za kawaida ndicho kinatumika Hospitali za Rufaa. Hii ina ukakasi, kwani Hospitali za Rufaa zina utaalamu zaidi na wanaweza kukubadilishia dawa. Sasa kuna Wakaguzi wa NHIF na uthibiti wa abuse, ni muhimu kwa sababu wakaguzi hao wanaweza wasikubaliane na daktari bingwa, inaleta ukakasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nilimwomba Mheshimiwa Waziri Ummy atambue Hospitali ya Mkoa ya Bukoba haikidhi viwango vya referral kutoka Hospitali Teule ya Rubya. Kwa hiyo, Bima ya Mkoa wa Kagera referral iwe Bugando, hata kwa Bima ya jamii, yaani zahanati - wilaya - Bugando hadi Rubya Hospitali ya Mkoa itakapoboreshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri huduma za saratani ziendelee kuboreshwa. Tunapongeza Ocean Road na Bugando kwa huduma zao lakini hazitoshi. Pia tuwekeze katika kuzuia kuenea kwa saratani, tupime afya, tusingojee mionzi. Prevention is better than cure. Inahitaji Wizara kupiga kampeni ya rollback cancer.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami kwa dakika tano nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpango, Naibu wake na Watendaji kwa ujumla kwa kazi nzuri waliyofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Hawa Ghasia nilipata nafasi kushiriki katika Kamati, kwa hiyo, nita-summarize tu. Nampongeza Waziri kwamba mambo mengi ambayo tulikuwa tunazungumza ameshayafanyia amendment, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Serikali ya Awamu ya Tano hii ni bajeti yao ya pili na unaona kwamba tunafanya maendeleo progressively. Mimi yangu sasa ni recommendations ambazo Mheshimiwa Waziri nimempa kwa kirefu, mambo mengine kimaandishi, lakini haya tu naya- highlight.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha kwanza ili kusudi tuwe na uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na stable tax regime, yaani hali ya kodi iwe imetulia. Kwa hiyo, naomba kabisa kadri tunavyoendelea tusiwe tunabadilisha sheria mara kwa mara ile misingi yake. Tubadilishe viwango lakini siyo misingi ya sheria kwa sababu Mwekezaji akija ataangalia kama sheria iko stable au kama inayumba. Hilo ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha pili naomba nitoe ufafanuzi, wachangiaji wengi hapa wamezungumzia habari ya mafuta, napongeza Waziri na Serikali kwamba wamependekeza kama ilivyopendekezwa na imekaa vizuri. Huwezi kuwa na tofauti kubwa kati ya mafuta na diesel. Watu wa pembezoni Mkoa wa Kagera, Kigoma na kadhalika tulikuwa tunapata tabu sana, watu walikuwa wanachakachua mafuta, vituo vya petrol vilikuwa vimekaa pale Chalinze, sasa hivi vituo vya petrol vile vimeyeyuka vimekwenda wapi? Kazi yao ilikuwa ni kuchakachua, walikuwa wanaharibu magari, wanaharibu vifaa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwa dakika tano……

T A A R I F A . . .

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Taarifa nimeikataa kwa sababu kule kwangu shida yetu ni magari yasiharibike, engine zisiharibike.

Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaambie, ninaowazungumzia mimi ndiyo Mwakilishi wao, hata viwanda kama Kagera Sugar karibu isimame kwa sababu diesel ilikuwa inachakachuliwa. Kwa hiyo, uchakachuaji ni mkubwa, jambo hili ni zuri msilete siasa ambazo hazitufikishi mahali popote. Kwa hiyo, mafuta ya petrol ilivyokaa kwenye bajeti imekaa poa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la withholding tax. Mheshimiwa Waziri naomba ufafanuzi bila shaka utatolewa kama Mheshimiwa alivyosema kwenye Kamati ilivyokaa hapa kwenye sheria, tuweze kujua walipaji wa withholding tax itakwendaje iko clause ya 18.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu samaki, mimi nawakilisha wavuvi hapa, hili nimeambiwa na nimeahidiwa kwamba sasa ile regulation ya samaki itabadilika iwe kwa shilingi siyo kwa dola tena. Kwa hiyo, wapiga kura wa Muleba na wavuvi wengine kwa ujumla Tanzania waliokuwa wanalipishwa kwa dola suala hili sasa linaondoka na tunashukuru sana kwamba Waziri ameshatangaza hili. Kwa hiyo, Waziri wa Uvuvi basi asichelewe kubadilisha suala hili kwa sababu linatesa sana wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwango vya kodi. Sisi hapa ni waajiriwa tunalipa asilimia 30 ya kodi katika mapato yetu. Rais wetu sasa hivi anapambana na hawa watu waliokuwa wanachukua madini yetu kwa bei poa. Napendekeza na pendekezo hili nimempa Mheshimiwa Waziri huko tunakokwenda going forward, progressive tax system iingie hapo, watu wanaovuna madini, sisi tupate asilimia 51 ya corporate tax wanayopata. Viwango visilingane, hiyo inaitwa progressive taxation, kwa sababu sasa mfanyakazi asilimia 30, mtu wa mgodi asilimia 30, watu wa mafuta asilimia 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi nyingine haiko hivyo na Mheshimiwa Waziri anajua ninaloliongelea, naomba lifanyiwe kazi. Tuwe na progressive taxation wale wanaovuna madini yetu tuweze kupata faida kubwa, sasa hivi wakati Rais anapambana na sisi tumuunge mkono katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo naweza kusema ni suala la kuwapa haki wafanyabiashara. Kama nimezungumza tax regime katika ile tax appeals process, kama TRA wakibishana na Mlipa Kodi ni muhimu sana ionekane kwamba anaweza akapata haki huko anakokwenda. Kwa hiyo, unapokuwa na mgogoro lazima unakuwa na status quo inakuwa maintained. Kwa hiyo, kuna vipengele vingine vinaweza kuleta ukakasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo maelezo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.