Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kasalali Emmanuel Mageni (33 total)

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na majibu mazuri ya Serikali, kwa kuwa swali hili limeulizwa kwa muda mrefu, kuanzia katika Mkutano wa Tatu, ambapo Mheshimiwa Kiswaga na mimi Mbunge wa Sumve tuliuliza na tukapata majibu ya namna hii hii.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kulifanyia kazi jambo hili na kuanza taratibu za manunuzi ili barabara hii ijengwe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa barabara hii unaendana sambamba/unaathiriana na ujenzi wa reli ya kiwango cha standard gauge kutokea Isaka kwenda Mwanza kwa sababu, barabara hii kwa usanifu mpya inapita eneo tofauti na barabara iliyopo inapita na reli hii ikishajengwa, ina maana hakutakuwa na njia tena ya kupita kutoka Kwimba kwenda Magu.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati iharakishe ujenzi wa barabara hii, ili kuepuka kufunga njia ya kutoka Kwimba kwenda Magu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara hii tuliyoitaja kwa kiwango cha lami. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itajengwa na sisi kwa upande wa Wizara tayari tumeshakamilisha taratibu zote ili fedha itakapopatikana basi tuanze utaratibu wa kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa suala la barabara hii aliyoitaja kuingiliana na reli hii ya kisasa ya SGR, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, yote hayo yalizingatiwa kwenye usanifu na kwa hiyo, tumuhakikishie kwamba, hakutatokea hiyo changamoto anayoisema kati ya muingiliano wa hizo barabara na hiyo reli. Cha msingi tu avute subira kwamba wakati reli imeshaanza kujengwa hiyo ya SGR kati ya Isaka na Mwanza, lakini fedha ikipatikana mara moja pia barabara hii itajengwa ili basi hii miundombinu yote iende sambamba kuyafungua hayo maeneo. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hali ilivyo katika Jimbo la Busega inafanana kabisa na hali ilivyo katika Jimbo la Sumve. Katika Kata ya Mwabomba wananchi wamejenga maboma katika Vijiji vya Mwambomba, Mulula na Ngogo na mpaka sasa maboma haya hayajamaliziwa, ni maboma ya zahanati. Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itamalizia maboma haya ili wananchi wa Kata ya Mwabomba na wenyewe wapate huduma ya afya kama yalivyo maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata hii ya Mwabomba katika Jimbo hili la Sumve, ni kweli kwamba wananchi wameendelea kuchanga nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa maboma ya zahanati na katika vijiji hivi vitatu, kwanza niwapongeze sana kwa kutoa nguvu zao na kujenga maboma haya kuonesha kwamba kimsingi wana uhitaji mkubwa wa huduma za afya. Ndiyo maana Serikali imeendelea kutambua na kuthamini sana nguvu za wananchi kwa kutenga fedha kwa ajili ya kila jimbo kupelekewa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma haya ya zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika Jimbo la Sumve pia, nimhakikishie Mheshimiwa Kasalali kwamba fedha zimetengwa kwa mwaka ujao wa fedha, maboma matatu, ambayo yanahitaji kwenda kukamilishwa yatakwenda kukamilishwa. Nimweleze Mbunge, kwa kuwa vipaumbele ni haya maboma matatu na tayari milioni 150 zimetengwa kwa ajili ya maboma hayo, kwa hiyo tatizo hilo limeshapatiwa majawabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni endelevu. Katika kila mwaka wa fedha tutaendelea kuhakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma yote yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuendelea kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wetu.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa barabara hii ni ya muhimu sana kwenye uchumi wa nchi yetu na uchumi wa Kanda wa Ziwa, kwasababu inapunguza umbali wa kutoa Shinyanga mpaka Mkoa wa Mara kuelekea nchi jirani ya Kenya, kwa zaidi ya kilometa 73 na Serikali imekuwa ikiahidi ujenzi wa barabara hii katika Awamu kuanzi ya Tatu mpaka Awamu ya sasa na Wananchi wa Wilaya ya Kwimba wanahitaji kuunganishwa na Makao Makuu yao mkoa wao kwa barabara ya kiwango cha lami.

Je, ni lini sasa Serikali itaachana na maneno ya kutafuta pesa na kuanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara inayoanzia Fulo kupitia Nyambiti mpaka Malia yenye urefu wa kilometa 73 pia ni barabara muhimu sana kwenye uchumi wa Wilaya ya Kwimba na barabara hii imeahidiwa kwenye ukurasa wa 77 wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanza kufanyiwa upembuzi yakinifu na hatimaye kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika Awamu ya Tano iliyopita taratibu za ujenzi kwa kiwango cha lami umeanza na ndiyo maana tumekamilisha usanifu wa kina mwaka 2019 kwa hiyo si tu zimekuwa ni ahadi lakini tayari tumeshaanza utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Sumve kwamba barabara aliyoitaja ya Fulo Nyambiti Malia ameisema mwenyewe kuwa imeainishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi na nimuhakikishie katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita kama tulivyosema imeanishwa kwenye ilani, lakini pia imeongelewa na Mheshimiwa Rais wakati analihutubia Bunge hapa ni kati ya barabara ambazo zitafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mbunge na Wananchi wa Sumve kwamba tutatekeleza kama tulivyopanga ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa hali ilivyo katika eneo la Makanya huko Same inafanana moja kwa moja na hali ilivyo katika Kata za Mwabomba na Mwandu katika Jimbo la Sumve, ambapo barabara za kutokea Mwabomba kupitia Chamva - Mulula mpaka Manawa hazipitiki katika kipindi chote cha mvua:-

Je, lini sasa Serikali itaamua kuzijenga kwa kiwango barabara hizi ili ziweze kupitika katika mwaka wote ili watu hawa waweze kufanya shughuli zao za maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Kasalali Mageni ameainisha maeneo ya Kata kadhaa, kama nne hapa ambazo hazipitiki kabisa. Nami tu niwaagize TARURA Makao Makuu, ninaamini hapa wananisikiliza, wakafanye tathmini kama ambavyo nimeagiza katika eneo la Same ili walete hiyo taarifa. Kwa sababu sasa hivi tunahitaji tathmini za kina ili tuhakikishe hizi barabara tusiwe tunazungumza tu hapa, tunaleta maneno maneno. Tuzungumze kwa data na tuhakikishe kabisa kila barabara, hususan zile ambazo hazipitiki kabisa tunazitengea fedha na kila fedha inayopatikana inajenga ili kuhakikisha barabara zote zinapitika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nilichukue hilo jambo na tayari nimeshaagiza sasa hivi, watafanya tathmini na nitaleta majibu kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru, kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kuanza upembuzi yakinifu tangu mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021 na leo mwaka 2021/2022 lakini upembuzi yakinifu huu hauishi na umechukua zaidi ya miaka mitatu kwa mradi huu wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye Miji ya Malya, Sumve na Malampaka.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuwaambia uhalisia watu wa Sumve ili wajue ni lini wanapata maji haya ya bomba kutoka Ziwa Victoria?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria yameshafika kwenye Mji wa Ngudu na Serikali imejenga pale tenki la maji la lita milioni mbili na Naibu Waziri aliwahi kutembelea tukiwa naye; na katika mradi ule usanifu unaonesha maji yanatakiwa yafike katika Jimbo la Sumve katika Kata za Lyoma, Malya, Mwagi, Nyambiti na Wala.

Je, Serikali inasema nini kuhusu kusambaza maji haya ya bomba kwenye Kata hizo za Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Emmanuel kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mradi wa maji wa Ziwa Victoria kufikia Kata ambazo zipo ndani ya Jimbo la Sumve, tayari Wizara inaendelea kuona uwezekano wa kukamilisha hilo na mara fedha itakapopatikana suala hili tunakwenda kulitimiza.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili tenki ambalo limekamilika usambazaji wa maji katika maeneo yale ya wakazi, suala hili tayari linafanyiwa kazi. Wizara tumeshaagiza mamlaka husika pale Mwanza na wataendelea kufanyia kazi kwa haraka sana kwa sababu tayari fedha nyingi ya Serikali imeshatumika, hivyo tunahitaji kuona kwamba wananchi wale wanakwenda kunufaika na kufaidi maji haya ambayo tunatarajia yatoke bombani.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru, kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kuanza upembuzi yakinifu tangu mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021 na leo mwaka 2021/2022 lakini upembuzi yakinifu huu hauishi na umechukua zaidi ya miaka mitatu kwa mradi huu wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye Miji ya Malya, Sumve na Malampaka.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuwaambia uhalisia watu wa Sumve ili wajue ni lini wanapata maji haya ya bomba kutoka Ziwa Victoria?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria yameshafika kwenye Mji wa Ngudu na Serikali imejenga pale tenki la maji la lita milioni mbili na Naibu Waziri aliwahi kutembelea tukiwa naye; na katika mradi ule usanifu unaonesha maji yanatakiwa yafike katika Jimbo la Sumve katika Kata za Lyoma, Malya, Mwagi, Nyambiti na Wala.

Je, Serikali inasema nini kuhusu kusambaza maji haya ya bomba kwenye Kata hizo za Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Emmanuel kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mradi wa maji wa Ziwa Victoria kufikia Kata ambazo zipo ndani ya Jimbo la Sumve, tayari Wizara inaendelea kuona uwezekano wa kukamilisha hilo na mara fedha itakapopatikana suala hili tunakwenda kulitimiza.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili tenki ambalo limekamilika usambazaji wa maji katika maeneo yale ya wakazi, suala hili tayari linafanyiwa kazi. Wizara tumeshaagiza mamlaka husika pale Mwanza na wataendelea kufanyia kazi kwa haraka sana kwa sababu tayari fedha nyingi ya Serikali imeshatumika, hivyo tunahitaji kuona kwamba wananchi wale wanakwenda kunufaika na kufaidi maji haya ambayo tunatarajia yatoke bombani.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa bajeti ya dawa ya Serikali imeongezeka kama ambavyo taarifa zinaonyesha kutoka shilingi bilioni 31 mpaka shilingi bilioni 270 na kwenye makabrasha ya Serikali inaonekana upatikanaji wa dawa umeongezeka kwa kiwango kikubwa lakini uhalisia kwenye Vituo vya Afya na Zahanati siyo sawa na hizi taarifa kwa sababu bado kwenye Jimbo la Sumve katika Vituo vya Afya na Zahanati tatizo la upatikanaji wa dawa bado ni kubwa sana: - (Makofi)

Je, Wizara haioni sasa umefika wakati muafaka wa kutengeneza utaratibu mahususi ambao utaisaidia Serikali kwenda kutatua tatizo hili kwa uhalisia kwa kupata taarifa halisi kutoka kwenye vituo na siyo makabrasha ambayo yanapatikana kwa wataalam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Kasalali Mageni ame-suggest jambo jema ambapo ukiangalia katika hotuba ya Wizara ya Afya wakati wanaisoma hapa pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye Idara ya Afya ambayo sisi tunasimamia, katika moja ya changamoto ambayo imekuwa ikitukumba ni kwamba Serikali imekuwa ikipeleka dawa lakini haziwafikii walengwa kama ambavyo imekusudiwa. Sababu kubwa ilikuwa ni baadhi ya watumishi, sio wote, kutokuwa waaminifu; aidha kwa kuuza zile dawa ama wengine kutokuzitumia mpaka zina-expire, matokea yake wale wagonjwa wanaotakiwa wapatiwe zile huduma za kimsingi wanashindwa kuzipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hizi Serikali tuko katika hatua za mwisho za kuandaa mfumo ambao sasa hivi utakuwa unajua dawa inayoingia na dawa inayotoka kiteknolojia. Kwa hiyo, naamini hiyo ndio itakuwa mojawapo ya suluhisho la kuondoa hii changamoto iliyopo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa swali la aina hii limeshaulizwa na Mheshimiwa Shanifu Mansour, Mbunge wa Kwimba na swali la aina hii liliulizwa na Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Magu. Pia mimi mwenyewe niliwahi kuuliza swali la nyongeza kwenye swali la aina hii. Serikali kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri aliyetoa majibu leo, ilitoa majibu tofauti na iliyoyatoa leo kwa sababu, ilisema imeshatenga pesa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kilometa 10 katika mwaka huu wa bajeti na katika bajeti hiyo ilionekana. Sasa nataka kuuliza swali na kufahamu, je, Serikali katika ujenzi wa barabara hii inafahamu ni nini inahitaji kuwajibu watu wa Kwimba na Sumve au tunajibu tu ili muda uishe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; barabara hii imeshafanyiwa usanifu, kama majibu ya Serikali yalivyotolewa na kwa mujibu wa usanifu barabara hii, barabara mpya iliyosanifiwa itapita sehemu tofauti na inapopita barabara ya sasa katika eneo la Nkalalo ambapo kuna ujenzi wa reli ya SGR. Kwa sababu kwa mujibu wa ujenzi wa reli hii, hakuna barabara inaruhusiwa inaruhusiwa kupita juu ya reli. Ina maana reli hii ikimalizika kujengwa njia ya kutokea Kwimba kwenda Magu itakuwa imefungwa. Je, Serikali haioni kuna udharura wa kuanza ujenzi wa barabara hii ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo kutokea Kwimba kwenda Magu na kuiunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na Mkoa wa Mwanza kwa barabara ya lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Mageni Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika bajeti tuliyopitisha na bado sijaiondoa, tulitenga bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Katika jibu la msingi nimesema Serikali inaendelea kutafuta fedha na fedha ndio hii kwamba, tutakapopata sasa tutakuwa tunaanza ujenzi kwa sababu, hatujaanza, lakini ipo kwenye mpango na bado mpango huo haujafutwa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hakuna majibu tofauti, majibu ni hayo na ndio bajeti tuliyopitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, huu udharura anaousema Mheshimiwa Mbunge, naomba nimhakikishie kwamba, kama Wizara tunalichukua na wataalam watakwenda kufanya tathmini na kuangalia kama kinachosemwa kina ukweli, basi tutachukua ushauri na kulifanyia kazi kama kutakuwa na udharura huo. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hali ilivyo maeneo ya Jimbo la Nyang’hwale inafanana na kabisa na hali ilivyo kwenye Jimbo la Sumve ambalo lina Kituo cha Afya cha Nyambiti ambacho kilibadilishwa kilikuwa zahanati na kituo hicho cha afya kina hudumia kata 13 za Jimbo la Sumve ambazo zina wakazi zaidi ya laki mbili na kituo kile hakina majengo kama ya upasuaji mahabara na majengo ya muhimu ambayo yangesaidia katika kutoa huduma stahiki ya afya kwa watu wale. Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha watu wa Jimbo la Sumve katika kituo cha afya cha nyambiti na wenyewe wanapata huduma nzuri kama ilivyo katika vituo vingine vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni Mbunge wa Jimbo la Sumve kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla katika halmashauri zetu na katika majimbo yetu tuna vituo vya afya ambavyo vina majengo pungufu kama nilivyotangulia kujibu katika jibu langu lililopita na mpango wa Serikali ni kuhakikisha standard ya vituo vya afya inafikiwa kwa maana ya kuwa na majengo yale yote ya muhimu yanayofanya kituo kile kiwe na hadhi ya kuwa kituo cha afya. Kwa hiyo, kuwepo kituo hiki cha afya cha Nyambiti katika jimbo hili Mheshimiwa Mbunge naomba nimuhakikishie kwamba tutafanya tathimini pia kuona umetupa taarifa kwamba hakuna majengo ya upasuaji na mahabara na tunajua ni muhimu na yanahudumia zaidi ya kata 13 ni moja ya kituo cha afya cha kimkakati na ninajua ulikihainisha kwa hiyo tukitafuta fedha tutahakikisha tunaipa kipaumbele kujenga majengo hayo ili wananchi wale wote wapate huduma bora za kituo cha afya.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, hali ilivyo katika Jimbo la Kilwa inafanana kabisa na hali ilivyo kwenye Jimbo la Sumve ambapo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote wakiongozana na Naibu Waziri walikuja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa minara katika Kata za Bugando, Mwandu na Lyoma na ujenzi huo leo ni mwaka mzima haujakamilika.

Je, Wizara haioni sasa kuna umuhimu wa kuharakisha ujenzi huu ili watu wa kata hizo waanze kupata mawasiliano kama ilivyo kwenye kata zingine?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, labda kwanza niongee kwamba ujenzi wa minara hii unahitaji vifaa ambayo tunaviingiza kutoka nje ya nchi na kwa sababu ya changamoto ambayo ilikuwepo ya UVIKO-19 uzalishaji wa vifaa hivi katika nchi ambazo tulikuwa tunaagiza ulipungua kwa kiasi kikubwa sana. Kwa hiyo, nina uhakika kabisa, na hii sio changamoto ya Sumve kuna maeneo mengi, na Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamelalamika minara katika maeneo yao bado haijasimama kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nitoe taarifa kuanzia sasa mpaka mwezi wa nne tunaenda kuhakikisha minara 288 inawashwa. Hivyo, baada ya kuwasha minara hii baadaye sasa ndio tutajua kwamba changamoto bado imebaki maeneo gani, ili tuweze kuchukua hatua. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika Jimbo la Sumve, jimbo zima hakuna Kituo cha Polisi ambacho kina sifa ya kutunza silaha. Serikali kupitia Mawaziri mbalimbali wa Mambo ya Ndani imeshaahidi kuboresha Kituo cha Polisi cha Nyambiti ili kiweze kujengewa jengo la kutunza silaha.

Je, Serikali haioni kwamba umefika wakati sasa wa kuhakikisha kwamba Jimbo la Sumve na lenyewe linakuwa na Kituo cha Polisi chenye sifa ya kuwalinda watu wa Sumve muda wote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wowote Serikali ya Chama cha Mapinduzi iko tayari kuwahudumia wananchi wake kwa njia zote za kiusalama. Jimbo la Sumve ni Jimbo moja katika Wilaya ya Kwimba, kwa hiyo, matarajio yangu ni kwamba kama pana haja ya kuanzisha Kituo cha Polisi cha hadhi ya Tarafa na kikawa na majengo stahiki kinaweza kutunza silaha. Naomba kupitia Bunge lako Tukufu nimwahidi Mheshimiwa Kasalali kwamba baada ya Bunge hili katika ziara yangu Kanda ya Ziwa nipo tayari kutembelea eneo lake ili kuona namna ambavyo tunaweza tukashughulikia suala la kuimarisha usalama katika eneo lake. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Kwa kuwa taratibu za kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kulipatikana Halmashauri ya Sumve ambayo ndio ina Jimbo la Sumve zimeshakamilika katika ngazi zote mpaka ngazi ya mkoa na tunasubiri tamko la ngazi ya juu kupatikana kwa Halmashauri ya Wilaya Sumve. Je, nini tamko la Wizara kuhusu upatikanaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumve ambayo ni tamanio kubwa la watu wa Sumve na itasaidia sana kusogeza huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kugawa maeneo mapya ya utawala tayari zimepokelewa kwa halmashauri zote ambazo zimewasilisha kupitia utaratibu wa kisheria na kanuni na tathmini inaendelea. Mara baada ya kukamilisha tathmini hizo mamlaka husika itafanya maamuzi ya kugawa ama kutoa muda kwa ajili ya kuboresha maeneo ambayo yatakuwa na upungufu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo lipo na linafanyiwa kazi. Niwaombe kuwa na subra ili muda ukifika basi mtapata majibu ya maamuzi ya Serikali.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa shule ya Sekondari ya Sumve ni moja ya shule kongwe ambayo ina historia kubwa sana kwenye nchi yetu ambapo mama Maria Nyerere alipata elimu yake pale na ni shule ambayo imechakaa sana. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuipa kipaumbele shule hii ya Sumve Sekondari katika kuanza ukarabati wa shule kongwe katika bajeti inayokuja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kumjibu kwa kifupi sana Mheshimiwa Kasalali kwa swali lake; ni kwamba shule aliyoitaja Sumve ambayo ina historia kubwa amesema tuipe kipaumbele basi na mimi nilipokee ombi lake tutazingatia, tutampa kipaumbele na kama tutakavyowapa Wabunge wote katika Bunge hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Je, Serikali haioni kwamba, umefika wakati sasa wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa mazao ya choroko na dengu kwa kutoa pembejeo na mafunzo kwa wakulima badala ya ambavyo sasa Serikali imewekeza zaidi kwenye kusimamia mauzo badala ya kusimamia uzalishaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kasalali kwa namna ambavyo amekuwa akiyasimamia mazao haya, hii ni hoja yake ambayo amekuwa akiisema mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie mbele ya Bunge hili ya kwamba, tutaendelea kuyapa kipaumbele mazao yote, katika maoni na ushauri ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema tumeupokea tutakwenda kuufanyia kazi ili mwisho wa siku wakulima wa choroko na dengu pia walime kwa tija na masoko ya uhakika wayapate pia. (Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na namshukuru pia Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; Serikali imekiri kwamba imeanza mchakato na inagawa mbegu bora za kilimo cha alizeti kwa wakulima. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha mbegu hizi zinafika kwenye Jimbo la Sumve kwenye Kata za Lyoma na Malya ambazo zimeonyesha uwezo mkubwa wa kuzalisha alizeti kuliko maeneo mengi ya nchi hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; uzalishaji wa mazao haya ya alizeti na upelekaji wa mbegu bora unategemea pia upatikanaji wa mbolea. Katika Jimbo la Sumve mbolea ya ruzuku ambayo tunaitegemea sana kwa mazao haya mpaka sasa haipatikani. Je, ni nini tamko la Serikali juu ya upatikanaji wa mbolea hii ya ruzuku ambayo imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa wakulima wetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu mbegu bora za alizeti kuwafikia wakulima wake, nikitoka hapa nakwenda kumpigia simu na kumwelekeza Mtendaji Mkuu wa ASA ahakikishe wakulima wa Sumve na wenyewe wanapata mbegu bora hii ya alizeti.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mbolea, ni kweli kumekuwepo na changamoto katika mfumo wa usambazaji, lakini tumeshatoa maelekezo kwa ndugu zetu wa CPB ambao wanashirikiana na wadau wengine kuhakikisha kwamba mbolea hii inawafikia wakulima kwa wakati. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, zilikuwepo changamoto, tumeendelea kuzifanyia kazi na muda sio mrefu CPB pamoja na mawakala wengine watasaidia ufikishaji wa mbolea kwa wakulima pasipo na usumbufu wowote kwa wakulima wetu wa Tanzania.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuwa hali ilivyo Kilombero inafanana kabisa na ilivyo katika Jimbo la Sumve katika eneo la Bungulwa ambapo Halmashauri tumeshaleta andiko la kujenga soko la kisasa katika mnada wa Bungulwa.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuleta pesa ili mradi huu muhimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ufanyike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, anasema Halmashauri yake imeshaleta andiko katika ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa sasa anachohitaji tu ni kwamba fedha sasa itolewe kwa ajili ya soko hilo. Mimi tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kupitia hilo andiko na kuangalia namna bora ambayo tunaweza tukatafuta fedha kuhakikisha kwamba tunaleta katika Halmashauri yake.

Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo commitment ya Serikali, ahsante.(Makofi)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, Barabara hii ya Fulo kupitia Nyambiti mpaka Malya ni barabara ya muhimu sana kwenye uchumi wa Serengeti ya Kusini, na ni barabara ambayo Serikali imekuwa ikiahidi kuendelea kutafuta pesa, wakati huo Serikali ikitambua Jimbo la Sumve hatuna hata milimita moja ya lami.

Je, ni lini sasa seriously pesa hizi zitapatikana, mkafanya upembuzi yakinifu na kuanza kuijenga barabara hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara yenye urefu wa kilometa 71 inayotokea Magu inapita Bukwimba – Nkalalo – Ngudu mpaka Hungumalwa nimekuwa nikiiombea kila mara ijengwe kwa kiwango cha lami na Serikali mlijibu kwamba sasa mmejipanga kuijenga katika bajeti hii.

Je, sasa ni lini ujenzi huo unaanza au inaendelea kupewa ahadi kama ambavyo imekuwa kawaida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nakubaliana naye, barabara hii bado haijafanyiwa usanifu ; na nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna barabara mbili tu ambazo zilikuwa bado hazijafanyiwa usanifu katika Mkoa wa mwanza ikiwepo hii. Tumeshamwagiza Meneja wa Mkoa aangalie kama kutatokea saving yeyote kwenye hela ya maendeleo, hii barabara tuanze. Tukuhakikishie barabara hii lazima itafanyiwa usanifu katika kipindi cha mwaka wa bajeti huu tunaokwenda na mpango wa sasa.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, barabara ya Hungumalwa hadi Magu, Mheshimiwa Mbunge nishahidi, Waziri ameongea naye na tumeshaahidi. Tayari Meneja wa Mkoa ameelekezwa aitangaze kuianza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; hospitali mpya ya Wilaya ya Kwimba iliyoko Icheja ina upungufu mkubwa wa miundombinu ambapo hakuna wodi za Watoto na akina mama na huduma mbalimbali hazipatikani, hivyo kupelekea usumbufu mkubwa kwa wagonjwa kuhitaji kupata huduma katika Hospitali mpya na huduma zingine katika kituo cha afya cha Ngudu, ambapo husababisha gharama kubwa sana za matibabu kwa wagonjwa.

Je, ni lini Serikali sasa itapeleka pesa za kutosha ili kukamilisha huduma za msingi zipatikane katika jengo moja kwenye hospitali mpya ya Icheja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyogeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Jimbo la Sumve kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa hospitali zetu za Halmashauri unakwenda kwa awamu, na kila baada ya awamu majengo kadhaa yanayokamilika yanaanza kutumika na majengo mengine yanapelekewa fedha kwa ajili ya ujenzi na kuanza kutumika. Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Halmashauri hii ya Kwimba ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zimewekwa kwenye bajeti, kuongezewa fedha ili miundombinu mingine ikamilike kwa ajili ya kutoa huduma, ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba na watumishi katika zahanati ya Mwashilalage katika Jimbo la Sumve ambayo ujenzi wake umeshakamilika kwa muda sasa na mahitaji ya watumishi na vifaa tiba ni ya hali ya juu kutokana na kwamba kata nzima ya Sumve haina zahanati yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni, Mbunge wa Jimbo la Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vifaa tiba na watumishi vyote viko kwenye mpango na viko tayari. Watumishi wanaendelea kuajiriwa hivi sasa na matarajio ya Serikali ifikapo Julai, watumishi watapelekwa kwenye vituo vyetu na tutahakikisha tunatoa kipaumbele kwenye zahanati ambayo Mheshimiwa Mageni Kasalali ameongelea.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na vifaa tiba mwaka ujao wa fedha tumetenga 69.95 bilioni kwa ajili ya vifaa tiba na tutahakikisha pia vinapelekwa kwenye zahanati hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mpaka sasa haina gari hata moja la uhakika la wagonjwa; na ni Halmashari ya Wilaya ambayo imeundwa na majimbo mawili; Jimbo la Kwimba na la Sumve. Mpaka sasa kwenye Jimbo la Sumve hakuna kabisa ambulance: Mheshimiwa Waziri huoni kwamba umefika wakati wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba yenye majimbo mawili na Halmashauri zote zenye majimbo mawili kugawiwa ambulance kwa kuzingatia kwamba kila Jimbo lipate ambulance yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasalali Mageni Mbunge wa Jimbo la Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nipokee taarifa ya Halmashauri hii ya Kwimba kwamba haina gari la uhakika hata moja la wagonjwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wetu wanapata uhakika wa huduma za rufaa na dharura. Kwa hiyo, tutahakikisha tunapata gari kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kugawa magari mawili kwenye Halmashauri zenye majimbo mawili, tutafanya tathmini kulingana na uhitaji kwa kadri ya vigezo vya kitaalamu na tutaona, ziko Halmashauri zitapata magari zaidi ya moja na pia ziko Halmashauri ambazo zinaweza zikapata gari moja. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa barabara hii ni ya muhimu sana kwenye utalii wa Serengeti ya Kusini na vipande vya kuanzia Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiti mpaka Maswa vimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na baadhi ya maeneo yameshaanza kujengwa. Lakini kipande cha kutokea Maswa – Malya – Nyambiti – Fulo havijawahi kufanyiwa upembuzi yakinifu na imekuwa ni ahadi kila mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haioni sasa kwamba kuna umuhimu wa kulichukulia jambo hili kwa ukubwa wake na kufanya upembuzi yakinifu na hatimaye kuijenga kwa lami barabara hii ili watu wa Jimbo la Sumve na Mkoa wa Mwanza na wenyewe wafaidi matunda ya utalii ambayo Serikali imeshaanza kufanya juhudi kubwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa barabara pacha ya barabara hii ni barabara inayotokea Magu kupitia Bukwimba – Ngudu – Hungumalwa; na barabara hii yenye urefu wa kilometa 71 tumekuwa kila siku tukiizungumza na Serikali katika bajeti inayoisha Juni imepanga kujenga kilometa 10 lakini hakuna dalili zozote za kuanza kujenga.

Je, nini tamko la Serikali kuhusu barabara hii ya muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Kwimba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo ameulizia ambayo ipo kwenye swali la msingi nimesema Serikali itahakikisha kwamba kwanza tunaifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kama ambavyo imeainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo tunaitekeleza. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba kazi hiyo tutaifanya kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, barabara aliyoitaja ya Hungumalwa – Ngudu – Magu, barabara hii usanifu wa kina umeshapatikana na ipo kwenye mpango kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba mipango ipo na tuna hakika kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo tumeainisha. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Serikali inayo mpango wa kuleta maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria hapa Dodoma lakini ambako Ziwa Victoria lipo katika Mkoa wa Mwanza kwenye Jimbo la Sumve hakuna maji ya uhakika ya bomba kutoka Ziwa Victoria. Serikali imekuwa ikiahidi kwamba itatupelekea maji hayo kwa bajeti mbili mfululiozo.

Je, ni lini sasa Serikali itapeleka maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria katika Jimbo la Sumve?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na nimwambie tu kwamba baada ya dhiki sio dhiki, baada ya dhiki ni faraja. Jitihada kubwa zimefanyika katika Mkoa wa Mwanza Majimbo yote yamefikiwa na uwekezaji wa mradi wa Ziwa Victoria kasoro Jimbo la Sumve.

Mheshimiwa Spika, ni muda muafaka sasa katika bajeti yetu hii tunayokwenda nayo 2022/2023 kuhakikisha tunapeleka sasa maji ya Ziwa Victoria katika Jimbo lako la Sumve.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Barabara ya kutoka Haydom mpaka Katesh ni mwendelezo wa barabara ya kutokea Fulo au Bujingwa kupitia Nyambiti mpaka Mari ambayo imekuwa ikiahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali kwenye ilani mbalimbali za uchaguzi; je, ni lini sasa barabara hii inaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, kama nilivyosema barabara hii iko kwenye mpango wa kuijenga; kwa hiyo mara fedha itakapokuwa imepatikana barabara hii sasa tutaanza kuijenga kama tulivyoahidi.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, mbali na Serikali kutoa ajira nyingi, Jimbo la Sumve limeendelea kuwa na tatizo la upungufu mkubwa wa watumishi hasa katika sekta ya elimu, kiasi kwamba Shule kama Nyang’enge, Bukala zina walimu kati ya watano mpaka saba.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kutoa upendeleo maalumu katika ajira zinazofuata kwa Jimbo la Sumve ili kukidhi mahitaji ya walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilikuwa nimeshasema awali kwamba katika kipindi hiki cha miaka miwili ya uongozi wa Doctor Samia Suluhu Hassan, Serikali imejitahidi sana kuhakikisha inaajiri walimu wengi, na ninyi ni mashahidi kwenye halmashauri zenu Waheshimiwa Wabunge mmepata walimu wa kutosha. Kwenye hizi ajira mpya tutahakikisha Sumve pia nanyi mnapata Mheshimiwa Mbunge.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni lini sasa Serikali itatekelea mapendekezo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ya ujenzi wa vituo vya afya katika Kata za Mwabomba na Bugando?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeshatafuta fedha ya kuweza kuangalia ujenzi au kuanza ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo ya kimkakati hapa nchini. Tutaangalia vilevile Kwimba imetengewa kiasi gani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya hivi ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa kikokotoo ni kwa ajili ya watumishi na wastaafu; na uhalisia ni kwamba watumishi na wastaafu hawakitaki kikokotoo hiki: Ni lini Serikali italeta Muswada hapa wa kufuta kikokotoo hiki ili kuondoa kero kwa watumishi na wastaafu ambao hawakitaki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, no research no right to speak. Katika uhalisia wa actuarial report na utafiti uliofanyika, unufaikaji wa wanachama ni asilimia 81 ya wanachama wote, na asilimia 19, nadhani kama mtu atakuwa na hoja na hakubaliani, naye afanye utafiti na atuambie. Sisi tutaendelea kutoa elimu. Kwa kufanya hivyo, kwa sababu inaonekana suala linaanzia pengine kutokuwa na picha ya pamoja, tutaona umuhimu wa kuweka semina kwa ajili ya Wabunge ili kuweza kupata uelewa wa pamoja na kuwasaidia vizuri wanachama wetu kuliko kuwapotosha, ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Je, ni nini mpango wa Serikali katika kufufua viwanda vilivyotelekezwa kwa muda mrefu kikiwemo kiwanda cha kuchambua pamba cha Nyambiti kinachopatikana katika Kijiji cha Mwabilanda katika Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni kweli moja ya maeneo ambayo Serikali tunaweka mkazo sasa ni kuona tunafufua viwanda ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa, na baadhi ya maeneo au viwanda hivyo wale wawekezaji tuliowabinafsia hawajavifufua au kuviendeleza au wanafanya tofauti na mkataba tuliowapa. Pamoja na viwanda vingine, hiki pia kipo kwenye mpango huo ambapo tunaendelea kutafuta wawekezaji au kuhakikisha wale ambao tumewakabidhi kwa sasa, waweze kuviendeleza kulingana na mikataba ambayo tulikuwa tumeingia nao, nakushukuru.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwanza ili kuweka kumbukumbu sawa naomba nirekebishe jina langu kama lilivyotajwa na Mheshimiwa Waziri, mimi ninaitwa Mheshimiwa Kasalali na sio Kasasali.

Mheshimiwa Spika, baada ya marekebisho hayo, naomba niishukuru Serikali kwa majibu mazuri na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa utayari wake alipokuja kwenye Jimbo la Sumve kusikiliza changamoto zetu.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa kumeibuka aina mpya ya kangomba katika sekta ya mawasiliano ambapo kampuni za simu mara baada ya kufanya utafiti wa maeneo ambayo wataweka minara wamekuwa wakishirikiana na wajanja wachache wanaokwenda kuyatwaa maeneo haya kwa kuwalaghai wamiliki na hatimaye wao kuingia kwenye orodha ya watu wanaopangishwa na minara hiyo ya simu.

Je, nini tamko la Serikali juu ya ulaghai huu ambao umekuwa ukifanywa kupitia makampuni ya simu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Kata za Wala, Mwabomba na Maligisu hali ya mawasiliano ni mbaya sana na Serikali imesema inao mpango wa kupeleka mawasiliano katika maeneo hayo. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kupeleka mawasiliano haraka sana katika kata hizo ili kurahisisha mawasiliano kwa watu hawa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kuomba radhi kwa kukosea jina la Mheshimiwa Mbunge. Napenda sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi, kuna maeneo ndani ya jimbo hili bado kuna changamoto na ndio maana Serikali tunaenda kufanya tathmini ili tujiridhishe ni hatua gani ambazo tunazichukua aidha kama ni kujenga mnara au kuongeza nguvu. Lengo ni kwamba mawasiliano ndani ya Jimbo hilo la Sumve yaweze kuimarishwa.

Mheshimiwa Spika, kwa swali la ulaghai. Nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa picha ambayo nimeiona nikiwa nafanya ziara. Kumekuwa na maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kweli, watoa huduma kuhusishwa na jambo kama hili.

Mheshimiwa Spika, lazima nikiri kwamba sina uhakika na uthibitisho wa namna ambavyo watoa huduma wanashiriki, isipokuwa naamini kwamba kuna wajanja ambao wanahisi kwamba eneo fulani linakwenda kujengwa mnara basi wao wanawahi kwenda kulinunua ili baadaye wao ndio waweze kulipwa.

Mheshimiwa Spika, pia ninaamini kwamba kwa kushirikiana na Ofisi ya Halmashauri kwa sababu tulishatoa maelekezo, ujenzi wa minara ni lazima Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ihusishwe katika hatua zote ili kuhakikisha kwamba tumeondokana na migogoro ambayo inaweza ikatokea kwa sababu ya ujenzi wa minara.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; bodaboda maeneo ya vijijini ndiyo chombo kikuu cha usafiri kinachotumika kubeba wagonjwa kuwapeleka hospitali; na ili mgonjwa abebwe kwenye bodaboda inabidi abebwe mishikaki, awepo mtu wa kumshikilia, lakini Sheria ya Usalama Barabarani inazuia jambo hilo.

Nini tamko la Serikali juu ya watu wa vijijini wanaotumia bodaboda kupeleka wagonjwa hospitali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kiukweli ni hatari sana watu kutumia bodaboda kwa utaratibu wa mishikaki, na kwa mujibu wa sheria ni hatari kwa usalama wao na maisha yao, na nikiwa Naibu Waziri kwenye Wizara yenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao, siwezi kutoa kauli ya kuhalalisha jambo ambalo linaweza likahatarisha usalama wa maisha wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wetu, kama wanaona bodaboda ni chombo, kwa sababu ina magurudumu mawili, tunaweza tukashauri wakatumia chombo kilicho na magurudumu mawili kama baiskeli kuliko kutumia bodaboda ambayo katika kubadili gia, hawa wawili wote wanaweza wakajikuta wamedondoka na wakaathirika kiafya kinyume cha matarajio ya ndugu yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nishauri tu kwamba tuendelee kuimarisha maeneo yetu na kwa namna ambavyo nchi yetu inazidi kuimarika, bila shaka muda mfupi ujao maeneo mengi yatakuwa na usafiri, kwa mfano magari ya michomko, yapo mpaka vijijini, japo hayaruhusiwi kubeba abiria, lakini tumeyavumilia kwa sababu ya mazingira yale, lakini kwenye boda boda ni hatari, hatuwezi kuruhusu jambo hilo.

SPIKA: Kwenye baiskeli ni sawa? (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimesema baiskeli kwa sababu ya mwendo wa baiskeli, lakini kiti cha baiskeli kinabeba mtu mmoja tu. Mwendo wake ni mdogo, anatumia nguvu kazi ya yeye mwenyewe, lakini boda boda ni machine, ni engine sasa ile ni hatari kwa sababu ya ule mwendo wake na kadharika. Baiskeli kumbeba mgonjwa na ndio usafiri tumekuwa tukiutumia maeneo mengi ya vijijini. Tumetumia baiskeli za kwenda taratibu, lakini hii ya bodaboda ni hatari hata sio kwa mgonjwa hata wazima, tunawashauri wasitumie usafiri huo kama mshikaki.

SPIKA: Mimi nilitaka kuelewa tu sehemu ndogo, yaani kwamba kwenye baiskeli yule anayeendesha baiskeli akibeba watu wawili zaidi ni sawa?

NAIBU WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Hapana, kusudio langu abebe mtu mmoja na kile kiti kina uwezo wa kubeba mtu mmoja. Mwendo wake ndio nilisema kwa sababu ya tahadhari anayoisema Mheshimiwa Mbunge kwamba mgonjwa anatakiwa apate mtu wa kum-support kwa mwendo wa pikipiki hilo haliwezekani, lakini kwa baiskeli mwendo ule ni mdogo na familia nyingi zimekuwa zikibeba watu hao kwa baiskeli na wanafika, lakini sio pia mshikaki lakini hata kile kiti hakiwezi kubeba mshikaki.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Je, ni lini sasa Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya cha Nyambiti ambapo imekuwa ikiahidi kila mara tunapouliza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itapeleka fedha katika kituo hiki cha afya alichokitaja Mheshimiwa Kasalali Mageni kule Jimboni Sumve kadri ya uapatikanaji wa fedha, lakini tutatuma timu iweze kuangalia pia ukubwa wa eneo lililopo pia na majengo ambayo yanahitaji kufanyiwa upanuzi halafu tuweze kupata taarifa kamili na kutafuta fedha hizo.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kutosha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati katika Kijiji cha Chamva ili hali fedha iliyokuwa imetumwa awali haikutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, maeneo yote ambayo Serikali ilipeleka milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma, kwanza maelekezo ilikuwa ni kwamba boma liwe limefikia hatua ya linter. Pia, kwa tathimini zetu kwa kiasi kikubwa milioni 50 ilikuwa inatakiwa kukamilisha boma. Sasa kama eneo hili la Chamva fedha ilipelekwa lakini boma halikukamilika, kwanza tunataka Mkurugenzi wa Halmashauri atupatie taarifa rasmi kwa nini milioni 50 hazikutosha kukamilisha boma, tujiridhishe na matumizi sahihi ya fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, pili, wanatakiwa kutenga fedha kwenye mapato ya ndani ili kuhakikisha kwamba wanakamilisha jengo la Zahanati ya Chamva. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Hili suala la wazee waliopigana vita vyetu kuidai Serikali limekuwa ni suala la muda mrefu na limekuwa kila siku likitolewa majibu: Je, ni lini sasa Serikali inaliahidi Bunge hili kwamba suala la wazee hawa litatolewa majibu ya mwisho na kutatuliwa liishe kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikirejea majibu yangu ya swali la msingi, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ni kwamba wako wazee 272. Sasa kama wapo wazee wengine ambao kwa bahati mbaya wanaamini kwamba wana madai ya msingi, lakini hawamo kwenye orodha hii, tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili wazee hawa wahahakikiwe taarifa zao, ikithibitika kwamba wanastahili Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itawalipa hizo haki stahiki, ashante sana.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru mradi wa maji wa Isunga Kadashi ni moja ya miradi ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri aliitembelea katika Jimbo la Sumve na tukaahidiwa kwamba mradi ule utaanza kutoa maji ndani ya miezi miwili, lakini hadi sasa ninapozungumza ni zaidi ya mwaka sasa umepita na mradi ule hautoi maji.

Je nini tamko la Serikali kuhusu kitendo hicho ambacho kinapelekea watu wa Kijiji cha Isunga kutokupata maji kwa muda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tamko la Serikali kwenye mradi ambao mimi na Mheshimiwa Mbunge tuliutembelea ni kufuatilia na kuhakikisha maji yanatoka, Mheshimiwa Mbunge naomba niwe nimelipokea nilifanyie kazi kwa nini maji hayajatoka hadi sasa. (Makofi)