Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Agnes Elias Hokororo (13 total)

MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ahadi ya ujenzi wa barabara ya Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi hadi Nachingwea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini TANROADS ilikamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mtwara -Tandahimba – Newala - Masasi hadi Nachingwea yenye urefu wa kilometa 255 mwaka 2015. Mpango wa Serikali ni kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu kulinganana upatikanaji wa fedha. Hadi sasa Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi huo katika sehemu ya Mtwara hadi Mnivata yenye urefu wa kilomita 50 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 89.591.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na mipango ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu iliyobaki ya Mnivata – Tandahimba – Newala - Masasi hadi Nachingwea kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021 jumla ya Shilingi Bilioni 10 zilitengwa kwa ajili ya malipo ya mkandarasi wa barabara kwa sehemu ya kwanza ya Mtwara - Mnivata na kuanza maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya Mnivata - Tandahimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara nchini imeendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hiyo ili kuhakikisha kuwa inapitika kwa majira yote. Pia napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa, baada ya Mheshimiwa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu wa Tano kuiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kutukopesha fedha za ujenzi wa sehemu hii ya Mnivata – Tandahimba – Newala - Masasi yenye urefu wa kilometa 160, benki hiyo tayari imetembelea barabara hiyo na kuna dalili nzuri benki hiyo kugharamia ujenzi wa sehemu hiyo ya barabara. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafufua Viwanda vya Korosho vilivyopo katika Wilaya za Masasi na Newala ili kuchakata korosho ghafi na kuongeza bei ya zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya za Masasi na Newala zilikuwa na viwanda vitatu vitatu vya kubangua korosho vilivyokuwa vikimilikiwa na Serikali na hatimaye kubinafsishwa. Viwanda hivyo ni Masasi Cashew Factory, Newala l Cashew Factory na Newala ll Cashew Factory.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Korosho cha Masasi kilichopo Masasi kilibinafsishwa na kuuzwa kwa Kampuni ya BUCCO Investments Holdings Limited ambayo ilishindwa kukiendeleza kutokana na Benki ya CRDB kuzuia mali za kiwanda baada ya kiwanda kushindwa kurejesha mkopo waliokopa. Hatimaye Kiwanda kiliuzwa na Benki ya CRDB kwa Kampuni ya Micronix Export Trading Co. Ltd kwa njia ya mnada. Kampuni ya BUCCO Investments Holdings Limited hawakuridhika na utaratibu uliotumika kuuza kiwanda hicho. Walifungua kesi mahakamani na kuishtaki Benki ya CRDB. Kesi hiyo bado ipo mahakamani hivyo uendelezaji wa kiwanda hicho umesimama kusubiri maamuzi ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Newala I Cashew Factory kilinunuliwa na Kampuni ya Micronics System Ltd, kiwanda hiki kinaendelea kufanya kazi. Kiwanda cha Newala II Cashew Factory kilinunuliwa na Kampuni ya Agrofocus (T) Ltd. Tangu kibinafsishwe, Kiwanda hicho hakijawahi kufanya kazi. Hivyo, mwaka 2019 kilirudishwa katika umiliki wa Serikali chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Kiwanda hicho kama vilivyo viwanda vingine vilivyorudishwa Serikalini kipo katika utaratibu wa kupatiwa mwekezaji mwingine mwenye uwezo wa kukiendeleza.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kusafisha na kuongeza kina cha Bwawa la Maji Lukuledi-Masasi linalohudumia Vijiji vya Lukuledi, Nambawala, Mraushi, Mwangawaleo na Ndomoni?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha maeneo mbalimbali yanapata huduma ya maji ya uhakika na kipaumbele ni maji kwa matumizi ya nyumbani ambapo Vijiji vya Lukuledi, Ndomoni na Nambawala vinapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kufikisha maji Kijiji cha Mraushi pamoja na Kitongoji cha Mwangawaleo, utekelezaji unaendelea ambapo utahusisha ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilometa sita, vituo vya kuchotea maji 16 na ujenzi wa tanki la lita 100,000 kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Vijiji vya Lukuledi, Nambawala, Mraushi na Ndomoni wanatumia maji ya Bwawa la Lukuledi. Hivyo, kutokana na umuhimu huo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itakamilisha usanifu na kuanza ukarabati wa bwawa hilo ili liwe na uwezo wa kuhifadhi maji mengi ya kukidhi mahitaji ya shughuli hizo za maendeleo.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta teknolojia mbadala ili kunusuru afya za wananchi wanaotumia zebaki kwa matumizi mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na taasisi zake, ipo kwenye mpango wa kutafuta teknolojia mbadala na tayari vikao vya pamoja na taasisi zinazohusika na uchimbaji wa dhahabu vinafanyika ili kupata teknolojia isiyohitaji zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu na hivyo kuondoa athari za kiafya kwa jamii na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa elimu juu ya matumizi sahihi, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa katika siku za usoni matumizi ya zebaki ni dhamira ya Serikali katika kulinda afya ya jamii na mazingira. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kumaliza tatizo la maji safi na salama Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyumbu Mkoani Mtwara?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji 26 ambapo miradi 14 imekamilika na miradi 12 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Aidha, Serikali imeanza ujenzi wa mradi wa maji wa miji 28, ambapo Mkoa wa Mtwara miradi inayotekelezwa ni mradi wa maji Makonde na Nanyumbu. Utekelezaji huu unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2024 na utanufaisha wananchi zaidi ya 500,000 wa Wilaya za Newala, Tandahimba na Nanyumbu.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, kwa nini huduma za afya kwa Watoto Njiti zinatozwa fedha ilihali Sera ya Afya inaelekeza huduma bure kwa Watoto chini ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa huduma za afya kwa watoto chini ya miaka Mitano wakiwepo Watoto Njiti kwa vituo vya Serikali na vile vya binafsi vilivyo na ubia na Serikali ni bure na ni takwa la kisera.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utamaliza utata huu kwa wananchi wanaotibiwa katika vituo binafsi vya huduma za afya.
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kubadilisha Sheria ya Mirathi ya Kiserikali ya mwaka 1925 na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la mirathi hushughulikiwa na sheria tofauti Tatu ambazo ni Sheria ya Kiislam, Sheria ya Kimila na kwa wale wasiotumia sheria hizo, Sheria ya Mirathi ya India ya mwaka 1925 (Indian Succession Act, 1925) ikiwa ni miongoni mwa sheria tulizorithi kupitia Sheria ya The Judicature and Application of Law (JALA) Sura ya 358.

Mheshimiwa Spika, aidha, sheria hizi katika kushughulikia suala la mirathi hutumika sambaba na Sheria ya Usimamizi wa Mirathi, Sura ya 352 ambayo ndiyo sheria mahsusi katika kushughulikia usimamizi wa mirathi yote nchi.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeshaelekeza Tume ya Kurekebisha Sheria nchini kufanyia utafiti wa sheria zote zikiwemo Sheria za Mirathi ili kuziboresha na kuondoa vifungu ambavyo vinakiuka misingi ya haki na usawa. Kuhusu Sheria ya Ndoa, Serikali imeshaandaa mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo na inatarajia kuyawasilisha katika Bunge hili linaloendelea. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani kufanya utafiti na kurasimisha pombe ya mwiki inayotokana na mabibo ili kuongeza thamani ya zao la korosho?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto kadhaa zinazowakabili wazalishaji wa pombe za kienyeji hivyo kushindwa kukidhi matakwa ya viwango na kukosa ithibati ya ubora, Serikali kupitia Shirika la Viwago Tanzania (TBS) pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) imeweka utaratibu wa kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa pombe za kienyeji kuhusu matumizi ya teknolojia bora na matumizi sahihi ya viwango katika kuzalisha pombe za kienyeji ikiwemo pombe aina ya mwiki ili ziweze kukidhi viwango vinavyokubalika na hivyo kuruhusiwa kuingia sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Oktoba, 2022, jumla ya leseni 43 za ubora zimetolewa kwa bidhaa mbalimbali za pombe za kienyeji, na maombi mengine mapya 22 yapo kwenye hatua mbalimbali za tathimini kuelekea kwenye kupata ithibati ya ubora. Aidha, Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania itaendelea kutengeneza viwango vya pombe za kienyeji kwa kadri mahitaji yatakavyojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, kwa kiasi gani vijana wa Mtwara wamenufaika na programu ya kukuza ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum Mtwara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Mtwara jumla ya vijana 1,663 wamenufaika kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi. Kati ya vijana hao, 891 wamenufaika kupitia mafunzo ya uanagenzi katika fani za uashi, uchomeleaji, ufundi bomba, ufundi magari, ufundi rangi, umeme wa majumbani, umeme wa magari, upishi, useremala, na ushonaji.

Mheshimiwa Spika, aidha, vijana 772 wamenufaika na Mpango wa Urasimishaji Ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na kupewa vyeti katika fani za useremala, uashi, ufundi magari, uungaji na uchomeleaji vyuma, ufundi umeme, ubunifu wa mavazi na teknolojia ya nguo, uandaaji na upishi wa vyakula, utandazaji na ufungaji mabomba.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuharakisha uwekaji samani kwenye maktaba na maabara Chuo cha FETA Mikindani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) inaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia katika Kampasi zake ikiwemo ujenzi wa maabara na maktaba katika kampasi ya Mikindani. Pindi tuu ujenzi wa majengo hayo ya maktaba na maabara yatakapokamilika katika kampasi ya Mikindani, Serikali itaweka samani kwenye miundombinu hiyo muhimu. (Makofi)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza siku za likizo kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa likizo ya uzazi kwa watumishi kwa mujibu wa Kanuni H12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2009 ambapo pamoja na Kanuni Pili ya Kanuni ya 12 inabainisha kuwa muda wa likizo ya uzazi kwa mtumishi mwanamke ni siku 84 ambazo hutolewa mara moja katika kipindi cha miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuongeza siku za likizo pale mtumishi anapojifungua mtoto njiti, suala hili halijawekewa utaratibu wa kikanuni kutokana na taratibu wa uendeshaji wa shughuli za Serikali. Hivyo, Mtumishi (Mzazi) anaweza kuomba ruhusa ya kawaida kutoka kwa Mwajiri wake inapotokea changamoto kama hiyo.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kupitia SIDO kutoa mashine ndogo na rahisi kwa vikundi vya wanawake vya ubanguaji korosho Mkoani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imeanza kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa na kuuzwa nje ya nchi zikiwa zimebanguliwa (kernel). Lengo kuu ni kuongeza thamani katika zao, kipato kwa wakulima na ajira kwa vijana na wanawake.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika kutekeleza mpango huo Serikali imenunua mashine 100 za kubangua korosho zilizotengenezwa na wajasiriamali walio chini ya mwamvuli wa SIDO na kuzigawa kwa vikundi 22; vikundi 15 vya Mkoa wa Mtwara na Lindi vikundi saba ambapo jumla ya wanawake 241 na wanaume 18 wamenufaika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania inaendelea kuhamasisha watengenezaji na wauzaji wa mashine za kubangua korosho ikiwa ni pamoja na SIDO, CAMARTEC na TIRDO ili kurahisisha upatikanaji wa mashine hizo.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-

Je kuna Sheria ya Huduma ya Afya inayosimamia utoaji na upatikanaji wa huduma za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya inasimamia Sheria zifuatazo thelathini zinazolenga kusimamia ubora, utoaji wa huduma, maadili ya kitaaluma, kiutumishi na upatikanaji wa huduma za afya nchini, ahsante.