Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Agnes Elias Hokororo (7 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ni mara ya kwanza nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima. Pili, nitumie fursa hii kuwashukuru sana akina mama wa Mkoa wa Mtwara ambao wameniwezesha kurudi katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wetu mpendwa, jemedari bingwa, Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa katika maeneo yote; miundombinu, maji, elimu, afya na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa. Mojawapo ya nguzo ya mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa kama ilivyoainishwa kwenye Mpango huo ni ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Naiomba sana Serikali yetu Tukufu, ili kuwajumuisha wananchi wa Kanda ya Kusini, ni muhimu sana Mpango huu wa miaka mitano ukaingiza ujenzi wa reli ya Kusini. Kwa nini naiomba hii? Ujenzi wa reli ya Kusini ulitokana na Mradi wa Mtwara Corridor na mradi huu ulisainiwa na nchi nne; Tanzania, Msumbiji, Malawi na Zambia. Ulisainiwa mwaka 2000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muasisi wake ni hayati mpendwa wetu Rais Mkapa. Lengo lake lilikuwa kuiwezesha Bandari ya Mtwara. Bandari ya Mtwara imejengwa kwa bilioni 157 lakini juzi swali liliulizwa hapa na Waziri alikiri kwamba Bandari ya Mtwara kwa sasa inafanya kazi chini ya kiwango. Kumbe mradi huu wa Reli ya Kusini ukitekelezwa ina maana Bandari ya Mtwara itafanya kazi ile iliyokusudiwa kwenye huu mradi na miradi ya EPZA ambayo kwa sasa bado haijaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naiomba sana Serikali, kwenye huu Mpango wa miaka mitano ioneshe waziwazi ni lini mradi wa ujenzi wa reli ya Kusini utaanza na kukamilika ili kuwajumuisha wananchi wa Mikoa ya Ukanda wa Kusini katika ukuaji wa uchumi na maendeleo yao. Vinginevyo tutakuwa tu tunaendelea kushangilia lakini wananchi wa Ukanda wa Kusini kama maeneo haya muhimu katika ukuzaji wa nchi yetu hayatajumuishwa na wao watakuwa wanaendelea kushuhudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kabisa kwamba Serikali imeanza kutekeleza sehemu ya Mradi wa Mtwara Corridor, kama vile ujenzi wa barabara ya kutoka Mtwara mpaka Mbambabay umetekelezwa, lakini pamoja na huo ujenzi wa bandari, pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege, lakini pia pamoja na ujenzi wa Daraja la Umoja lile linalounganisha Tanzania na Msumbiji, lile Daraja la Mtambaswala. Sasa mambo haya yote ambayo Serikali ya Awamu ya Tano na zile zingine imeyatekeleza, hii miradi itaendelea kulala kwa sababu shughuli za kiuchumi zinategemea kwa kiasi kikubwa ujenzi wa mradi wa reli ya Kusini. Naamini Serikali yetu Tukufu itaweza kujumuisha Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kusini ili na sisi tuweze kushiriki kikamilifu katika ile dhana ya uchumi jumuishi, uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nijielekeze katika eneo la kilimo. Kama ambavyo mpango umeainisha kwamba asilimia 65 ya Watanzania wanapata riziki yao kwa kutegemea shughuli za kilimo. Lakini tunaona shughuli za kilimo zinachangia asilimia 27 tu ya GDP na asilimia 24 ya total export.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kinahitajika katika eneo hili; kwa kuwa wananchi wa Mikoa ya Kusini, hasa Mtwara, asilimia 98 ni wakulima, ili tujumuike pia katika ujenzi wa uchumi huu ambao wote tunauhitaji, naomba sana tujikite katika mapinduzi ya kiteknolojia. Wakulima wetu kwa sasa wanatumia jembe la mkono; kwa nini? Trekta ziko bei juu, milioni 45 mpaka milioni 60. Akinamama ambao wanashiriki kwa asilimia 75 kule mashambani na katika shughuli za kilimo hawawezi kununua trekta, mikopo yetu ya vikundi vya halmashauri...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa. Kengele imeshagonga.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kwa kuwa nami ni Mjumbe wa Kamati, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza na hoja ambazo pengine watu wamekuwa wakijiuliza, maana ukisikiliza nje ya sisi Wabunge, wapo baadhi ya wananchi katika makundi mbalimbali wanahoji pia kwamba kwa nini Waheshimiwa Wabunge hawa wawili ambao ni mashahidi walitokea mbele ya Kamati ama waliitwa kwenye Kamati yako ya Bunge?

Mheshimiwa Spika, naomba niliweke wazi hili kwa sababu pengine hawajui kwamba mashauri haya yote mawili yameshughulikiwa chini ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Sura ya 296. Kwa hiyo, siyo suala tu kwamba labda mhimili huu wa Bunge uliamua tu wenyewe bila kufuata sheria; ni kwamba ni suala la kisheria. Pia niwaambie wale ambao pengine wamepata mashaka kwamba masuala haya yote mawili yameshughulikiwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Bunge lako Tukufu linaendesha shughuli zake kwa kufuata Kanuni za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba nilieleze hili kwa sababu baadhi huko ukisilikiliza wanasema wameonewa, mtu kwa nini ameitwa? Kwa nini hakwenda huku? Kwa nini huku? Pengine wanadhani ni shinikizo la mtu mmoja, lakini kumbe huu ni utaratibu wa kibunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mashauri haya yote mawili kama ambavyo Mwenyekiti wa Kamati amewasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu, yote yameangukia katika Kanuni ya 85 - Utovu wa Nidhamu Uliokithiri.

Mheshimwia Spika, hapa pia naomba nianze na shauri lile la kwanza la Msheshimiwa Josephat Gwajima. Sote tunatambua kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa uhuru wa kuabudu, lakini uhuru huo wa kuabudu tunaopewa Watanzania na watu kuanzisha taasisi za kidini hupaswi kuvunja masharti ambayo Katiba hiyo imeweka na sheria nyingine za nchi yetu. Tunajua sote kwamba hakuna uhuru usio na mipaka; yaani haiwezekani mimi leo; na kwa sababu kuanzisha Kanisa au taasisi ya kidini mtu yeyote anaruhusiwa; haiwezekani leo nikatoa maneno ambayo yanavunja sheria nyingine za nchi tu kwa kisingizio cha uhuru wa kuabudu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa maneno ambayo yalisemwa na shahidi hayana shaka. Naomba niungane na Wabunge ambao wametangulia kwamba maneno yale yanaweza kuvunja amani na utulivu wa nchi yetu. Sasa tukiachia hiyo tukasema sasa kila mtu aamke tu, sidhani kama tunaweza tukaendelea kufurahia nchi yetu katika uwanda huu mpana wa utulivu ambao unamwezesha kila Mtanzania kufanya shughuli zake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge King hapo amesema, ukiacha ile mifano ya Kibwetere, tuliona pia kwenye maeneo mbalimbali; nakumbuka kama sikosei kule Kagera kuna mchungaji alitokea Kanisani akasema ameoteshwa aoe mke wa mwingine Kanisani, lakini tuliona Serikali pia ambaye ni Mkuu wa Wilaya alienda akachukua hatua kuhusiana na lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia yapo maeneo mengine. Kwa hiyo, kwa ufupi tu tuseme kwamba hili pia ambalo limefanywa na Mheshimiwa Gwajima kwa kisingizio kwamba alikuwa anasema yale maneno akiwa anahubiri waumini wake kwenye nchi 142; na kwa kuwa alikiri Tanzania ni miongoni mwa hizo nchi 142; kwa kufanya hivyo kwa kweli sioni kama kuna shaka kwamba alikuwa anajaribu kuizua Serikali kutekeleza wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwasihi Wabunge kuliunga mkono Azimio hili la Bunge ili kuendelea kuulinda utulivu wa nchi yetu, kuilinda amani ya nchi yetu na pia kuleta ustawi wa jamii zetu. Hii chanjo ambayo pengine watu wanahimizwa wasiende kuchanja, tuliambiwa wote ni kwa hiari, lakini pia mashaka yale mengine ambayo yametolewa na mzungumzaji yanaendelea kuwachanganya wananchi. Kwa sababu akisema daktari yeyote atakayebisha amepewa pesa, sasa tunaendelea kuwachanga wananchi. Kwamba hawa hawa Wabunge wanasema hii chanjo isichanjwe kwa sababu hakuna nafasi ambapo Mbunge anapofanya shughuli nyingine nje ya Bunge utasema sasa mimi Agness Hokororo sio Mbunge, nafanya kazi zangu kama mwananchi wa kawaida kwa sababu wote tumekula kiapo kwa mujibu wa Katiba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, ahsante Mheshimiwa.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Aweso na nina matumaini makubwa kwamba atafanya vizuri kwa sababu naye hakutoka Oysterbay wala Masaki na anajua taabu na shida za mama zake kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina mashaka pia na Naibu wake, Mheshimiwa Eng. Maryprisca, kwa sababu ni mama. Kwa hiyo, hata Mheshimiwa Rais anapohimiza suala la kumtua mama ndoo, yeye ni mama. Kwa hiyo, wote kwa kweli tuna matumaini na ninyi na tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu mwendelee kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru pia kwenye bajeti hii nimeona kuna miradi 84 na hiyo ni usanifu, ukarabati, uchimbaji wa visima katika Mkoa wa Mtwara, lakini naomba nijielekeze kwenye utekelezaji wa bajeti iliyopita 2020/2021. Kama ambavyo imeonekana kwenye hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri, utekelezaji wake ni asilimia 54 tu. Mkoa wa Mtwara kulipangwa shilingi bilioni 21 na zikapatikana ama zilizotumika ni shilingi bilioni sita tu, sawa na asilimia 39. Kwa hiyo, hapa changamoto kubwa ni suala la upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri kwenye hili eneo. Kwa sababu kwa sasa Mfuko wa Maji ambao ndiyo Wabunge wote wanautegemea na kila mmoja hapa kwenye eneo lake ana changamoto ya maji na fedha zile ambazo zinapelekwa ni shilingi 50/= ya mafuta, mimi naamini Waheshimiwa Wabunge kwa sababu tunaona bado kuna kadhia kubwa ya uhitaji wa maji, pengine mfuko huu uongezewe uwezo. Kama kwa bajeti ya mwaka 2020 iliweza kutekelezeka kwa asilimia 54, hatutegemei miujiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba mwaka huu zimetengwa shilingi bilioni 680 lakini kwa utaratibu huo huo kama fedha haitakwenda yote hatutegemei Mheshimiwa Aweso na wenzake kwamba watafanya miujiza kwa sababu hiyo iko kwenye imani zetu za kidini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya uwekezaji mdogo katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu unachangiwa na ukosefu wa fedha. Kwa hiyo, nadhani iko haja ya kuangalia vyanzo vingine ili sasa hili suala la maji litekelezeke kwa kipindi kifupi na Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuongea habari nyingine.

Mheshimiwa Spika, nijielekeze katika Mkoa wa Mtwara. Kama ambavyo nimetangulia kusema, kwamba upatikanaji wa fedha pia ndiyo ilikuwa changamoto, sisi wananchi wa Mkoa wa Mtwara, nikisema hapa habari ya kuokota, dada yangu, Mheshimiwa Tunza amesema, hamtuelewi. Maana yake, kwenye vile vyanzo vitatu vya chini ya ardhi na juu ya ardhi, sisi tunatumia kwa kiasi kikubwa maji yale mvua inaponyesha, iwe ni nyumba ya nyasi yale maji meusi au yale yanayotiririka juu ya ardhi, tunayakinga kwenye mashimo halafu wenye uwezo wanaweka shabu, tusio na uwezo tunayanywa vilevile. Ndiyo maana ya maji ya kuokota kaka yangu, Mheshimiwa Waziri Aweso. Hiyo inatusababisha kutumia pia fedha nyingi kwenye matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana, hii changamoto ya maji ya Mkoa wa Mtwara kwenye Wilaya za Tandahimba, Newala, Mtwara Vijijini, Masasi, Nanyumbu ndiyo mara 200, haitaweza kuondoka kama Serikali haitakuwa na dhamira ya dhati ya kuanza kutekeleza Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona huku kwenye bajeti iko ile shilingi bilioni sita, Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara Mikindani na vijiji vya jirani, vijiji 73 vya Jimbo la Nanyamba au Mtwara Vijijini, lakini bado kule Nanyumbu, Newala, Tandahimba, Masasi, Majimbo ya Lulindi na Ndanda kuna adha kubwa. Kila siku mama analazimika kwenda mtoni. Kama mto utakuwa umekauka, basi tufukue kisima tuweze kuchota maji. Hata ukiona hata rangi ya yale maji hutakunywa. Hutaweza, nina uhakika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaishauri Serikali ianze kutekeleza Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma. Wenzetu tunasikia; maji ya Ziwa Victoria, maji sijui ya nini, sisi chanzo cha uhakika tulichokuwa nacho ni Mto Ruvuma. Pamoja kwamba kuna mto wa pili ambao haukaushi maji, Mto Lukuledi, lakini bado pia huo utasaidia kwenye maeneo machache. Ili tunufaike wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara, ni muhimu sana kuona mradi wa chanzo cha Mto Ruvuma unatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mtwara una vijiji 809. Kwa sasa vijiji 450 ndiyo vinapata maji na siyo saa zote, yaani 450 ndiyo vinapata maji. Ndiyo hayo sasa ya mdundiko, ama ya kuchota angalau. Vijiji 359 havipati maji. Kwa hiyo, wakati Ilani inasema itakapofika 2025 vijijini ni asilimia 85, sisi hiyo ni ndoto, kwa sababu kwa sasa kwa upande wa vijijini ni asilimia hiyo ambayo tunasema ndiyo ya wataalam, inawezekana 58 au 59, hatuwezi tukafanya maajabu kwenye hii miaka mitano tukafika kwenye hiyo asilimia 85.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana ukiniuliza kipaumbele cha kwanza kwa Mkoa wa Mtwara, ni maji; cha pili, changamoto ni maji; cha tatu changamoto ni maji. Tunaiomba sana Serikali yetu sikivu ya Chama cha Mapinduzi ijielekeze kwenye hilo eneo ili nasi tutuliwe ndoo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naamini wote tunatambua kwamba afya ni sehemu muhimu ya kuimarisha mtaji watu hasa katika kuendana na sera yetu ya uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie kwenye upatikanaji wa dawa. Kama ambavyo Mheshimiwa Noah amechangia na katika bajeti hii imeonekana ni asilimia 26.6 tu ndio iliyopokelewa kwa bajeti ya mwaka uliopita 2021. Hata hivyo, kinachokwamisha zaidi ukiacha ule utaratibu ambao ni wa ununuzi wa madawa kupitia MSD wa dawa nyingi yaani bulk procurement inaonesha pia kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya utaratibu wa manunuzi ndio hasa umekuwa kikwazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika vituo vya afya ama zahanati ambapo wakati mwingine wanakuwa na fedha, lakini katika utaratibu wa manunuzi inaweza ikachukua miezi miwili mpaka mitatu huku wananchi wanaendelea kuumia. Ikikupendeza katika Bunge lako hili Tukufu inawezekana kufanyike utaratibu wa kubadilisha hata sehemu ndogo ya Sheria ya Manunuzi ili kuwaokoa wananchi wengi wanaosubiria dawa wakati kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya hiyo ingewezekana, sio kwa kusubiri huo utaratibu wa miezi miwili mpaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze katika Mkoa wa Mtwara. Kama ambavyo taarifa imeonesha katika hotuba ya bajeti kwamba Kamati imebainisha wazi upatikanaji wa fedha katika bajeti iliyopita ndio ilikuwa kwa kiwango si cha kuridhisha, lakini natambua kabisa kwamba kwa bajeti ya mwaka huu 2021/2022, bajeti ya Wizara ya Afya imeongezeka kwa asilimia 31 na ongezeko kubwa limeonekana katika miradi ya maendeleo. Naiomba sana Serikali yetu sikivu ijielekeze pia katika kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ambayo ni hospitali ya kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali hii ikikamilika itawanufaisha wananchi wa Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Ruvuma, Mkoa wa Lindi, lakini pia hata nchi jirani ya Msumbiji. Kwa sasa katika Mikoa hii ya kusini wananchi wote wanakwenda kufuata matibabu ya ngazi ya rufaa katika Hospitali ya Muhimbili, lakini Serikali ikikamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa inayojengwa pale Mtwara Mitengo ina maana hata mzigo ule wa Muhimbili utapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba yale yaliyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020 - 2025 inawezekana ikatekelezwa na iwapo Wizara itahakikisha hili inalitekeleza. Kwa sasa ujenzi wa hospitali hii umefikia asilimia 40, kwa hii miaka mitano naomba sana, kwa yale majengo tisa yaliyoanza ambayo kwa sasa kwa kweli inaonekana lakini haitawezekana kutoa huduma kama haitakamillishwa kama ilivyoelekezwa na Ilani ya chama changu Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Mtwara vituo vya kutolea huduma ya afya vipo 251 na katika hivyo tunazo zahanati 227 sawa na asilimia 22 tu, bado tupo chini na mahitaji ya zahanati yalitakiwa 985, lakini hadi sasa tunao ujenzi wa zahanati 28 ambao wananchi na halmashauri wamejitahidi. Naiomba Serikali ijitahidi kukamilisha haya maboma ili angalau haya 28 yakaongeze ile 227 na wananchi kwenye maeneo mbalimbali waweze kupata huduma ikiwemo kule Lukuledi, ule ujenzi wa zahanati na ikiwezekana iwe kituo cha Afya Chiroro na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara hii. Kwanza niungane na mzungumzaji aliyetangulia, Mheshimiwa Ungele kusisitiza barabara ya Masasi – Nachingwea ambayo ndio pia inakwenda mpaka Liwale.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingine huwa hatueleweki, lakini pia nina maswali madogo ambayo ninajiuliza na pengine Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa ufafanuzi atuambie. Sera ya barabara inasema ni lazima kuunganisha mkoa kwa mkoa, hivyo watuambie wameunganisha kwa kiwango cha lami Mkoa wa Mtwara na Lindi kutoka Liwale – Nachingwea na Masasi Lami imepita hewa gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu wakati mwingine hata tunajichanganya wenyewe, kama Serikali hii hii inasema masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, moja ya kigezo ambacho kinapaswa kuzingatiwa ni uimarishaji wa miundombinu ikiwemo barabara. Sasa maeneo ambayo yanatoka mazao ya korosho, huko Nachingwea, huko Liwale ambayo inapaswa sasa kuja kusafirishwa huku Bandari ya Mtwara na kipande cha Masasi – Nachingwea ni kilometa 45 tu. Nimepata bahati ya kusikia ahadi za viongozi, lakini pia kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tangu mwaka 2010 - 2015 na 2015 – 2020, lakini mpaka sasa barabara hiyo haijaguswa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hokororo, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.
T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Nataka nimpe taarifa mzungumzaji. Barabara ya Nachingwea – Masasi imefanyiwa upembuzi yakinifu mwaka 2014, lakini mpaka leo bado inatafutwa fedha ya kujenga.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnes Hokororo.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea na tena imeniwahi, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama upembuzi yakinifu ulikamilika tangu 2014 pamoja na kwamba ahadi ilikuwa ni ya miaka 20 sasa. Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie maana kwenye taarifa yake inasema Serikali inatafuta fedha na ikisema Serikali inatafuta fedha, hilo jambo ni kama halipo. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amekwenda Nachingwea, kimsingi hata sasa hivi kama ungenipa nafasi niongozane na Naibu Waziri ama yoyote kwenye Serikali. Ukiwa mjamzito kwenye barabara ile ya Masasi – Nachingwea unapata, sijui nisemeje?

WABUNGE FULANI: Unazaa.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, unazaa kabla ya wakati. Ile barabara nikiongea kwa lugha ya kikwetu si dhani kama nitaeleweka, lakini ni kwamba unakuwa unatingishika kuanzia unapoanza mpaka, hapa wiki iliyopita niliuliza swali, wakasema fedha imetengwa lakini tuendelee kusubiria. Jamani! Mkoa wa Mtwara na Mikoa hii ya Kusini niwakumbushe tu, kwamba ilihusika kikamilifu katika kuziletea ukombozi Nchi za Kusini mwa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa labda Serikali ama Waziri aje kutuambia, hivi ile barabara haitengezwi kwa sababu kuna vikosi vya majeshi kule? Kwa hiyo wananchi wote waendelee kuishi nao kijeshi! Sasa unasemaje uwezeshaji wananchi kiuchumi, miundombinu haijakamilika, ni kwa miaka 20 iko kwenye ahadi, upembuzi umekamilika, nini kikwazo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tunajua kwamba Nchi hii ni kubwa na Serikali ina mzigo mkubwa, lakini iko haja ya kuangalia maeneo ambayo kimsingi yameachwa nyuma kwa muda mrefu. Hawa wananchi sehemu ambayo na nilisema hapa uliponipa nafasi ya swali la nyongeza, sehemu ambayo nauli ilipaswa kuwa shilingi 750 wanalipa shilingi 6,000, huu mzigo unakwenda kwa mwananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Waziri atakapokuja hapa bila kutupa maelezo ya kutosha, mimi siwezi kupiga sarakasi kwa sababu najua, lakini tunakwendaje kwenye bajeti hii bila ya kuwa na matumaini kwamba angalau hicho kipande tutatengenezewa. Kwa sababu hii habari ya kutengenezwa kila mwaka ndio kila siku mvua ikija inaosha, mvua ikija inaosha, lini Serikali itaanza kutekeleza kipande cha kilometa 45 kuunganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru kwa kunipa nafasi, kwanza awali ya yote niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya na hasa kuwaunganisha watanzania wote wa mjini na vijijini kwenye mtandao wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa sababu imetambua kwamba umeme ni suala la msingi na wala si la luxury na kwa msingi huo inaendeleza ujenzi wa mradi wa umeme ambao unajulikana kwa jina la Mwalimu Nyerere ambao utazalisha megawatts nyingi na kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamesema mradi huo utatusaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na giza.

Mheshimiwa Spika, lakini Serikali pia inaendeleza mradi wa REA kwa sasa ni mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ambapo na hiyo inafanyika kwa nia njema ya kuwaunganisha wananchi vijijini wao waweze pia kupata umeme. Natambua juhudi zinazofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, lakini naomba tu nichangie kwa uchache sana katika Mkoa wa Mtwara ambapo ninawawakilisha wanawake wa Mkoa wa Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwamba katika Mkoa wa Mtwara bado tunavyo vijiji 281 ambavyo havina umeme, lakini natambua pia kwamba ipo jitihada Mheshimiwa Waziri anaifanya ya kuwapelekea vijiji hivi 281 umeme wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa pili, lakini ningeomba tu kwamba kwakuwa vijiji hivi ni vingi pengine wakandarasi wawili wasingetosha na ili pia mradi utekelezeke kwa haraka. Pengine wakandarasi wangeongezeka wangekuwa watatu kama ambavyo tuliahidiwa huko nyuma pengine vijiji hivi 281 vingefikiwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, niishukuru sana Serikali, huko nyuma kabla ya mwezi wa 3 Mkoa wa Mtwara ulikuwa na tatizo kubwa la kukatikakatika kwa umeme kwenye wilaya zote sita. Lakini Serikali ilituletea mashine mbili za kuchakata umeme, kila mojawapo ilikuwa na uwezo wa kuchakata megawati 4.3. Ninaishukuru sana Serikali kwa sababu, sasa kwenye wilaya nne umeme umekaa vizuri hauna tatizo kubwa la kukatikakatika. Changamoto imebaki katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu, huku kuna tatizo kubwa la kukatika kwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri kwa Serikali na kwa kuwa natambua ni Serikali sikivu. Kwa upande wa Masasi, ambako kumekuwa na tatizo kubwa la kukatika kwa umeme kwa sababu tu, umeme wake unaunganishwa kutoka Mkoa wa Ruvuma kule Madaba. Unatoka Madaba unapita Songea, unapita Namtumbo, unapita Tunduru, unakuja Mangaka ndio unakuja Masasi. Lakini pia, kuna njia nyingine inayotoka Mahumbika ambayo iko Mkoa wa Lindi. Kwa hiyo, hizo zote mbili haziwapatii wananchi wa Masasi umeme wa uhakika na hivyo wameendelea kuukosa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri, ili kuondoa tatizo hili kwa suluhisho la muda mfupi, Serikali ijenge line mpya kutoka Mahumbika kwenda Masasi na hii itaondoa tatizo la umeme ule wa Masasi kutumika njiani kabla haujafika Masasi. Lakini halikadhalika watu wa Nanyumbu waunganishwe pia kwenye gridi hiyo, ikiwezekana sasa hivi waunganishwe watu wa Nanyumbu kwenye gridi ya Mtwara, ambayo imeimarika itasaidia kuondokana na hilo tatizo. Lakini, pale Masasi tunacho kifaa ambacho wataalam wanajua tunakiita AVR Automatic Voltage Regulator tunacho pale Masasi. Lakini wakati mwingine pengine hakitusaidii kwa sababu, tayari ule umeme unapofika unakuwa umeshapungua nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali kifaa hiki AVR, kiwekwe Tunduru na kiwe kifaa kikubwa kisaidie sasa ule umeme wa Tunduru, lakini pamoja na Nanyumbu na Masasi kwa sasa ambao ndio tunatumia uwe ni umeme wa uhakika. Lakini kwa suluhisho la muda mrefu nilikuwa napendekeza pia, kwa sababu Mtwara tunatambua kuna gesi ambayo tayari imeshaanza kutumika. Kwa suluhisho la muda mrefu kwa Wilaya za Masasi na Nanyumbu ni vyema pia, kungejengwa bomba la gesi kutoka Mahumbika kuja Masasi, ambapo pia wanufaika watakuwa Wilaya za Masasi na Wilaya za Nanyumbu na kuendelea kwa sababu bado tutakuwa tunauhitaji huu umeme kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napendekeza hayo kwasababu, tunatambua kwamba kwa sasa, Serikali inafanya jitihada pia ya kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuweka viwanda mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara na hasa Masasi pia, kwa ajili ya kuchakata korosho, mabibo na yale mabibo yaliyokauka ambayo tumependekeza kutengenezwe spirit na viwanda vya mafuta ambapo kuna uhaba wa mafuta ya kula. Tunao ufuta na karanga kule, lakini wawekezaji hawa watakwama kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamechangia kutokana na kukosa umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu umeme ukiimarika kwa Serikali kuweka hayo masuluhisho ambayo nimeyapendekeza, hiyo changamoto itakuwa imeondoka. Na hivyo wawekezaji watavutika kuja kuwekeza katika Mkoa wa Mtwara katika wilaya zote kwa sababu ya uhakika na hivyo kutakuwa na shughuli za uzalishaji mali na wananchi wataondokana pia na umasikini ambao kwa namna moja au nyingine, wanashindwa kujikwamua kutokana na mazingira ambayo kimsingi Serikali yetu sikivu inaweza kuyatibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa tatizo la kukatika kwa umeme lililopo, inapelekea wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kuunguza vitu vyao na tunajua sote kwamba, hakuna utaratibu mwananchi mmoja mmoja anapofanya shughuli zake kama labda ana mashine, labda saluni, ama mashine ya kusaga, ama fridge wapo wakinamama wanaotengeneza ice cream, waweze kuuza na shughuli zingine zozote zinazohusisha umeme. Vifaa hivyo vimekuwa vikiungua kwa sababu, umeme unakuja na nguvu kubwa pengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wananchi wanaathirika kwa hiyo, wanapata hasara kubwa, lakini hata wale wafanyabiashara wanaouza hivyo vifaa vya umeme. Kwa sababu, kama wanapewa warrant ina maana kila siku wakiuza wanatakiwa warudishe ama wafidie, wakiuza wafidie. Kwa hiyo, kwa kiasi kikubwa hiyo imekuwa ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali, lakini na kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mtwara, ambapo ninaamini kabisa, Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi, inaweza ikalitibu hili tatizo kwa njia hiyo ya muda mfupi lakini pia kwa njia hiyo ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa umeme huu utakapokuwa umeimarika hata zile changamoto za Kituo cha Afya kama Nagaga na vingine kule Newala vitakuwa pia ambapo hawapati umeme wa kutosha, Newala, Nanyamba, Mtwara Vijijini, Jimbo la Ndanda, Lulindi ambako kumekuwa na tatizo la umeme usiokuwa wa uhakika basi hiyo changamoto itaondoka. Katika Wilaya ya Masasi pale mjini tunavyo vijiji 19 lakini pia, tuna mitaa kadhaa ambayo haijaunganishwa kabisa haina umeme. Ni imani… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa...

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba nami nijielekeze katika kuchangia Muswada wa Sheria, Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa mwaka 2021. Kwanza kabisa, nianze kuipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huu ambao kimsingi ndani yake una Sheria 13 na Sheria hizi zina nia ya kuziba mianya inayoweza kuathiri utekelezaji wa Sheria hizo 13 kwa maslahi mapana kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na timu yake kwa usikivu wakati wa majadiliano na Kamati lakini kwa ushirikiano mkubwa na ndiyo maana imewezesha Taarifa ya Kamati, kwamba kwenye jedwali la marekebisho kuna mambo mengi ambayo wameyachukua, lakini pia walikuwa tayari kuondoa hata vile vifungu ambavyo vilikuwa havioneshi uhalisia. Kwa hiyo, naomba nimpongeze sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na timu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, naomba pia niunge mkono maoni ya Kamati na niwasihi pia Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono maoni ya Kamati kwa nia ile ile njema ya kufanya marekebisho ya Sheria hizi 13 kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, wakati Sheria hizi 13 zinajadiliwa na Kamati, nitoe tu mfano eneo ambalo Kamati imezingatia. Ile Ibara ya 42 ya Muswada inayopendekeza uhiari wa kisheria wa kuanzisha mfumo wa matumizi ya TEHAMA. Kamati iliona kwamba jambo hili likiletwa kwa hiari kwa kuzingatia Sheria ya Utaratibu wa Ajira za Wageni Sura ya 436, litakuwa bado linaturudisha nyuma kama nchi, kama Taifa hasa kwa kuzingatia pia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Mpendwa wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ya kuondoa changamoto zinazoleta urasimu katika masuala ya uwekezaji. Hivyo hivyo ukiangalia katika mapendekezo yale ya Marekebisho ya Sheria ya Ibara ya 42 yalikuwa pia nayo yanaendeleza urasimu. Kwa sababu ukiweka uhiari, ina maana itawalazimu wageni sasa kwenda kwenye ofisi mbalimbali ambapo hiyo pia tunaona itaendeleza urasimu.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyojua ina maana itakuwa njoo leo, njoo kesho; kwa maneno mengine full of come tomorrow na hivyo itakuwa inakwambisha pia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita. Sasa hivi tunataka kama Taifa kurahisisha na kufanya mambo haya ya uwekezaji yawe kwa njia ambayo inamwezesha kila anayetamani kufikia kwenye hiyo azma mahali popote anapokuwa; nje ya nchi ama ndani ya nchi na hasa kwa wageni hata wanapokuwa kule nje, wahakikishe wameshatekeleza au wameshajisajili kwa kupitia huo mfumo wa TEHAMA ili kuondoa urasimu kama nilivyotangulia kusema.

Mheshimiwa Spika, nilianza kutangulia pia kumpongeza Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kama ambavyo inaonekana kwenye Ibara ya 58, marekebisho pia pale yalihusu Shirika la Posta kuwa shirika la kipekee la kusafirisha vifurushi kuanzia gramu 500 mpaka kilo 10, jambo ambalo kimsingi lingefunga sasa fursa za vijana, fursa za mawakala, fursa za vyombo mbalimbali vya usafirishaji na ajira kwa kimsingi huo kwa vijana ambao wamekuwa sasa wakitumia nafasi hiyo vizuri.

Mheshimiwa Spika, pia tunatambua sote kwamba Shirika la Posta bado halijajiandaa kikamilifu na hasa kwa kuzingatia pia miundombinu pamoja na upungufu wa watumishi. Kwa sababu pia zipo changamoto ambazo mpaka sasa hivi kwenye Shirika letu hilo la Posta bado hatujaweza kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa pia tunaishukuru sana Serikali kwa kuona ukweli ambao Kamati ilijielekeza kwao na hivyo kuamua kuondoa kabisa hilo jambo ambalo kimsingi nimeona ni la msingi kwetu. Kwa hiyo, bado naendelea kuwasihi Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono marekebisho ambayo yameletwa na Kamati kwenye Jedwali la Marekebisho ili sote kwa pamoja tuweze kupitisha marekebisho haya mbalimbali ya Sheria ya Muswada (Na.
4) kama ambavyo leo tunajadili.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)