Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amina Daud Hassan (7 total)

MHE. AMINA D. HASSAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; pamoja na majibu yake mazuri Naibu Waziri aliyonipa, nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni lini hasa Serikali itaanza kulipa mafao ya wanachama ambao wana miaka zaidi ya mitatu wanafuatilia masuala yao hawajafanikiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, pili je, Serikali inamkakati gani kuhakikisha kwamba wastaafu wanalipwa kwa wakati ili isiathiri dhamani ya fedha ambayo wanalipwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Amina Daud Hassan kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni lini Serikali itakamilisha ulipaji wa Wawanachama ambao wana miaka mitatu sasa ambapo hawajaweza kulipwa mafao yao. Nimakikishie Mheshimiwa Mbunge kwanza nimpongeze kwa kufuatilia hasa kuhusu wananchi wake katika matatizo hayo ambayo wanayapata labda pengine ya kuwacheleweshea malipo. Lakini zaidi niweze kumuambia Mheshimiwa Mbunge mpaka sasa mfuko wetu hauna madeni kwa maana ya kwamba wastaafu wote ambao wamewasilisha nyaraka zao zenye usahihi ndani ya siku 30 anakuwa ameshalipwa malipo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa kama kuna mwananchi wake ambao amewasema zaidi ya miaka mitatu pengine hawajaweza kulipwa mafao yao niombe tu niwasiliane naye, nipate hizo details ili niweze kushughulikia waweze kulipwa kwa sababu ni haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha malipo haya yanalipwa kwa wakati. Tayari Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kwa maelekezo yake, tumekwisha kuanza kufanya kazi ya kuchunguza madai, lakini pia kuweza kuangalia kwa undani tija ya fedha ambazo zinapatikana katika mfuko, zaidi ya hapo uwekezaji unaofanywa pia na mfuko na tatu tunaenda katika kufanya uchunguzi wa madai yote ambayo yalikuwa ya awali kama yapo kuweza kujihakikishia kwamba yanafanyiwa uchunguzi na baada ya kujiridhisha tuweze kuwalipa madeni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika huo mkakati ambao upo mkubwa kwa sasa tunasubiri actuarial report ambao Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu amekua akiisimamia kwa kipindi chote na actuarial report itatoa taarifa kwa ujumla jinsi status ya mifuko hii na namna gani ambavyo itajiendesha kwa faida zaidi kama jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais jana katika hotuba yake aligusia na kuweza kueleza namna gani ambavyo mashirika ya umma, lakini taasisi na mifuko iweze kujiendesha kwa faida. Kwa hiyo hili Mheshimiwa Mbunge, tunakuakikishia kwamba halitavuka miezi miwili tutakuwa tumekwisha kumalima kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu
Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tumekuwa tukifanya uhakiki wa wastaafu kwenye mifuko hii, moja ya matatizo ambayo tumeyagundua ni hayo ambayo Mheshimiwa Naibu Spika umeayazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, wastaafu wamekua wakisumbuliwa sana kuleta nyaraka na wakati mwingine mstaafu anadaiwa alete nyaraka za miaka 20 iliyopita na wakati amestaafu nyaraka hizo zikiwa kwenye Ofisi za Serikali, tumeshatoa maelekezo kwa mifuko yote na hasa sheria inasema wajibu wa kufuatilia michango na nyaraka ni wamifuko na siyo mstaafu mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kazi yetu kwa sasa ni kusimamia watendaji wa hii mifuko wanatekeleza maagizo hayo tuliyoyatoa na kama kutakuwa na mstaafu anasumbuliwa yeye sasa ndiyo haangaike na ma-file wakati ni wajibu wa mwajiri na wajibu wa mifuko, tunaomba Waheshimiwa Wabunge tupeane taarifa na tutachukua hatua kwa hao watendaji ambao hawazingatii huduma bora. (Makofi)
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa tunayo makampuni mengi ya binafsi katika nchi yetu: -

Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa kuwa na Sheria ya Makampuni Binafsi ya ulinzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi ni kwamba mashauriano yanaendelea baina ya Serikali zetu mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili turidhiane. Kwa sababu suala hili linagusa Muungano, hatuwezi kulifanya upande mmoja wa Muungano tukasema tumekamilisha.

Mara taratibu hizo zitakapokamilika, then tutapeleka Muswada kwa ajili ya kupitiwa na kuridhiwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kwa kuniona na kunipa nafasi hii. Kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Uzing’ambwa kipo ndani ya kisiwa ambacho kimejitenga na vijiji vingine na kufungwa kwa kituo hiki kumeleta kero kubwa kwa wananchi wa eneo hili pindi wanapohitaji msaada wa Kituo cha Polisi. Je, Serikali haioni kuna haja ya dharura ya kufungua kituo hiki kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa vijiji hivi viwili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Daudi Hassan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoahidi majuzi kwamba tarehe 22 na 23 nitakuwa Zanzibar pamoja na mambo mengine kukagua Vituo vya Polisi vya Chumbuni, niko tayari kuungana na Mheshimiwa Amina kuangalia kituo chake hiki ili kuona uwezekano wa kukifanyia matengenezo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. AMINA DAUDI HASSAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya Ndoa ili iweze kupunguza changamoto ya ndoa za siri na za utotoni?(Makofi)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amkina Daudi Hassan, kuhusu Sheria ya Ndoa na Marekebisho yake.

Mheshimiwa Spika, wiki ijayo Kamati ya Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Sheria na Katiba zinaketi kikao kwa ajili ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Ndoa. Hivyo, basi tumepokea hoja yake, tunaenda kuwasilisha tujumuishe ili vijadiliwe pamoja. (Makofi)
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la nyongeza, ahsante Naibu Waziri kwa majibu ya Serikali mazuri na nina maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaongezea ruzuku wawezeshaji wakati wa malipo wakati wa masafa marefu ya kuwafikia walengwa?

Na swali la pili; shilingi 24,000 ni kidogo sana kwa wakati huu tulionao; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaongezea ruzuku wanufaika wa mfuko wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amina Daud Hassan kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la kwanza juu ya kuongeza ruzuku; nataka nimhakikishie Mheshimiwa Amina, kwamba Serikali iko katika mchakato ikijadiliana na wadau mbalimbali wakiwemo wahisani wetu juu ya maslahi na utaratibu mzima wa miradi hii ya TASAF, hivyo hii ni moja ya agenda ambayo inakwenda katika mjadala. Juu ya jambo la udogo wa pesa inayotolewa; niseme Serikali imesikia jambo hili na katika mjadala unaoendelea kama nilivyoeleza katika swala la kwanza la nyongeza, ni kwamba Serikali nao wanajadiliana kuona jinsi gani tunaweza kuangalia kuongezea ruzuku kidogo kwa wafaidika ili kuweka mazingira mazuri ya wao kufaidika na mradi huo; ahsante sana.
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utapeli hata hapa kwetu Tanzania unafanyika kwa kuomba michango na kadhalika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na TCRA ili kuweza kuwaelewa wahalifu hawa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA
YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi. Ni kwamba Serikali ina mkakati maalum na zaidi ya hapo Serikali kwa kushirikiana na Vyombo vya Dola vinaendelea kuratibu na kufatilia mienendo yote ya matumizi ya simu na zile ambazo zinahusika katika utapeli basi huwa zinakamatwa na baadae tunazifungia, sambamba na hilo tunaendelea kutoa elimu kwa Watanzania ili kuelewa pale ambapo simu za namna hii zinapowafikia ili wajue kwamba ni hatua gani waweze kuchukua kwa kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania - TCRA.
MHE. AMINA DAUDI HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Swali la kwanza; licha ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za hindi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Zanzibar, je, haioni haja ya kujenga kuta kandokando ya bahari ili kuzuia uendelezaji wa athari za mabadiliko ya tabianchi? Mfano kama Nungwi, Jambiani, Paje na vijiji vingine vyote vyenye fukwe ya bahari? Ahsante .
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mpango kabambe na mipango mingi ya kuhakikisha kwamba, tunakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo ya fukwe, ama maeneo haya ya ukanda wa Bahari, hasa katika Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tumekuwa tunahamasisha jamii ambazo zinaishi humu pembezoni mwa bahari, hasa maeneo ya ufukwe, kwanza kurejesha ama kupanda mikoko ambayo ilikuwepo lakini imekatwa, lakini hatua nyingine ambayo tumeichukua kama sehemu ya mpango kabambe wa Serikali ni kuendelea kuwaambia wananchi kwamba, wasiendelee kutupa taka hatarishi, lakini vilevile kufanya shughuli za uchimbaji wa mchanga katika maeneo haya ya fukwe. Kikubwa zaidi tumekuwa tuykiwaeleza shughuli za uvuvi, lakini pia shughuli za ulimaji ama uvunaji wa mwani zisiharibu fukwe zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa suala la ujenzi wa kingo ama kuta za kuzuia maji ya bahari au maji ya chumvi yasiingie maeneo mengine, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshaanza ujenzi wa ukuta kwa upande wa Tanzania Bara katika Mkoa wa Mtwara katika maeneo ya Mikindani, lakini kwa upande wa Kusini Pemba katika eneo linaitwa Sepwese, tayari tumeshaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maeneo ya Paje, Jambiani, Bwejuu, Nungwi na maeneo mengine, cha kwanza tunaenda kufanya utafiti kujua ni aina gani ya ukuta ambao unatakiwa, lakini tumwambie Mheshimiwa tunakwenda kutafuta fedha, ili tuone namna ambavyo tunakwenda kujenga hizi kuta ambazo zita-control uingiaji wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.