Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Amina Daud Hassan (4 total)

MHE. AMINA D. HASSAN aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaondoa tatizo la ucheleweshaji wa malipo ya mafao kwa wastaafu wanachama wa NSSF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daud Hassan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikihakikisha kuwa wastaafu wote wanalipwa mafao yao ya pensheni kwa mujibu wa Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini pindi wanapostaafu. Aidha, ili mstaafu aweze kulipwa mafao ya pensheni ni lazima awe amekidhi vigezo vifuatavyo:-

Mosi, awe ametimiza umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria, ambapo ni miaka 55 hadi 59 kwa hiari na miaka 60 kwa lazima. Pili, awe amechangia kwenye Mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi 180 au miaka 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii yaani NSSF wastaafu wote wanaokidhi vigezo na kuwasilisha taarifa zote zinazohitajika hulipwa mafao ya pensheni kwa wakati pasipo kuchelewa. Mwanachama akiwasilisha maombi ya kuomba kulipwa mafao na akawasilisha nyaraka husika, mwanachama atalipwa mafao yake ndani ya siku 30. Aidha, malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu hulipwa tarehe 25 ya kila mwezi moja kwa moja kwenye akaunti za wastaafu na hadi sasa hakuna malimbikizo yoyote ya mafao ya pensheni kwa wastaafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai, 2020 – Machi, 2021, jumla ya wanachama 93,861 wamelipwa mafao mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 377.8. Aidha, tunawasihi waajiri kuwasilisha michango ya watumishi wao kila mwezi kwa wakati na ninawasihi wastaafu kuhakikisha wanawasilisha nyaraka zote zinazotakiwa kwa mwanachama ili kuwezeshwa kulipwa mafao na kuondoa ucheleweshaji unaoweza kujitokeza katika kuandaa mafao ya wastaafu.
MHE. AMINA DAUDI HASSAN aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutoa elimu kwa Wanawake kuepuka ndoa za siri ambazo zina changamoto ya malezi ya familia?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daudi Hassan, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa ndoa ni Taasisi muhimu katika kuimarisha haki na ustawi wa familia. Hivyo, Serikali kupitia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 eneo namba nne linalohusu malezi na mahusiano ya familia imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu malezi chanya na mahusiano ndani ya familia ili kuwa na familia inayozingatia maadili mema.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji, Usimamizi na Uratibu wa Mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa na Familia ambao utasaidia kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia taratibu za ufungaji wa ndoa pamoja na kuyajengea mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia uwezo ili kuendelea kutoa elimu katika jamii.
MHE. AMINA DAUD HASSAN aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kufuatilia miradi ya TASAF iliyokamilika ili kuhakiki uendelevu wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daud Hassan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kuhakikisha kuwa miradi ya TASAF inakuwa endelevu, jamii huunda kamati ya matunzo na ukarabati ambayo jukumu lake ni kuweka sheria na taratibu za kusimamia matunzo na kuendeleza miradi hiyo. Mradi unapokamilika hubaki chini ya uangalizi wa wataalamu na TASAF wakishirikana na Halmashauri husika kwa kipindi cha miezi sita na baadaye mradi huo hukabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika ambayo huendelea na jukumu la usimamizi, uendeshaji na matengenezo kwa kushirikiana na idara au taasisi inayohusika na miradi hiyo.
MHE. AMINA DAUDI HASSAN aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutenga fedha ya mabadiliko ya tabianchi kusaidia wananchi wenye visima vya maji chumvi Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daudi Hassan, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, inatekeleza miradi mbali mbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa pande mbili za Muungano ambayo inahusika na uchimbaji wa visima. Kwa upande wa Zanzibar, Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo ya Ikolojia Vijijini (EBBAR) umechimba visima sita katika Wilaya ya Kaskazini “A”. Pia, Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) umechimba visima viwili katika Shehia ya Maziwa Ng’ombe na Shehia ya Kiuyu katika Kisiwa cha Pemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.