Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amina Daud Hassan (6 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa mzima na kuendelea na Bunge lako Tukufu salama.

Nampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuleta bajeti hii yenye faida kwa Watanzania, vilevile na Rais wa Zanzibar kwa kuwasilisha bajeti yake yenye muono wa uchumi wa bluu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake na watendaji wake wote kwa kazi nzuri waliyoifanya kukamilisha bajeti hii yenye mashiko, bajeti hii imebeba sekta tofauti tofauti na mimi nichangie sekta ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na inathamini mchango wa sekta ya umma na binafsi katika kukuza pato la Taifa kwa kupunguza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane. Kodi ya wafanyakazi kwa kiwango kimepunguzwa kutoka asilimia 11 mwaka 2015. Serikali imetenga shilingi bilioni 449 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 926,619. Natoa hongera sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo vya kodi, ada na tozo mbalimbali nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kupendekeza na kufanya marekebisho ya vyanzo vya kodi hizi ikiwemo tozo na ada ikiwemo tozo na ada zitokanazo chini ya Sheria ya Ajira na usimamizi wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Madiwani kwa kuwa awamu ya tano na ya sita imejenga utaratibu na uzoefu wa kukaa pamoja katika sekta zisizo za Muungano, namuomba Waziri wa Fedha akae na Waziri mwenzake wa Zanzibar haya mambo mazuri yanakwenda kukivusha Chama chetu cha Mapinduzi mwaka 2025, tuhakikishe nayo yanakwenda kufanyika na upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka posho kwa Madiwani wa Tanzania Bara basi tuhakikishe na upande wa Zanzibar yanakwenda kufanyika lakini ni ndogo mno, kwa hivyo ni vyema iongezwe ili waweze kufanya kazi kwa weledi zaidi na kudumisha Muungano wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. AMINA DAUDI HASSAN: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha nyingi katika Wizara ya Maji ili kuhakikisha maji yanapatikana na kumtua mama ndoo kichwani katika kutafuta maji.

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Waziri wa Maji na Naibu wake kwa kuaminiwa na Rais kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuendeleza malengo ya Rais wetu kuwa wanahakikisha maji yanapatikana.

Mheshimiwa Spika, mimi nijikite katika suala la uchimbaji wa mabwawa na visima nchini, naishauri Serikali iongeze fedha katika uchimbaji wa mabwawa na visima ili kutatua tatizo la maji katika maeneo ambayo hayana vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, lingine kuna maeneo ambayo maji yanaharibika kwa kuwa hakuna usimamizi katika maeneo ya vyanzo vya maji. Niiombe Serikali isimamie na kulinda maeneo hayo kwa kuweka walinzi ili kulinda maji ambayo ni uhai.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka miwili ya uongozi wake makini unaoleta mageuzi makubwa kielimu, kisiasa, kijamii katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na Naibu wake na watendaji wake kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu nauelekeza kwenye mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuangalia sekta mbalimbali. Nampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maendeleo anayozidi kuyatoa kwani shilingi bilioni 1.0 zimewekwa kwenye mfuko wa walemavu kwa ajili ya kusaidia vifaa vinavyohitajika, pia fedha hizo zitatumika kwa Mfuko wa Wabunge wa Kundi la Watu Wenye Ulemavu mchango kwa watoto wanaolelewa kwenye vituo maalum.

Mheshimiwa Spika, tunaomba makampuni binafsi kuchangia mfuko huu kwa kusaidia makundi haya maalum pamoja na programu zinazotolewa chini ya TASAF.

Mheshimiwa Spika, kuhusu elimu naipongeza Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza jambo la kihistoria kwa kuwafutia ada wanafunzi wa kidato cha tano na sita na kufanya wasome kwa utulivu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga fedha ya kugharimia programu hiyo ambapo hadi mwezi Aprili, 2023 jumla ya shilingi bilioni 661.9 zimetolewa. Pia kutokana na mabadiliko ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014 Toleo la mwaka 2023 na mabadiliko ya mitaala yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita Serikali imepanga kutoa elimu ambayo itamuwezesha mwanafunzi kujiajri au kuajiriwa.

Mheshimiwa Spika, pendekezo la Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhusu kuondolewa kwa ada ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na kupangiwa na Serikali kujiunga vyuo vya ufundi vya Dar es Salaam Institute, DIT, MUST na ATC ili kuongeza idadi ya wataalam wenye ujuzi na elimu inayohitajika katika zama hizi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uzalishaji; ongezeko la bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294.0 mwaka 2021 mpaka shilingi bilioni 954.4 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kufikia shilingi bilioni 970.8 kwa mwaka wa fedha 2023 ongezeko hilo limesababisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo na kuanzishwa kwa mashamba makubwa ya pamoja.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali imeendelea kusimamia usalama wa chakula kwa kujenga maghala 16 na vihenge 20 kwa ajili ya kuhifadhj mazao.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Rais kwa kazi kubwa anayofanya katika kuisaidia sekta ya uvuvi. Pia nimpongeze Waziri na Naibu pamoja na uongozi kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kuhusu zao la samaki ambalo wananchi wa maeneo ya maziwa na bahari wanategemea sana kwa kufanya biashara ya Samaki. Kwa vile samaki wanawategemea kufanya biashara naiomba Serikali iwawezeshe wavuvi kwa kuwanunulia vyombo vya kuvulia ili waweze kukuza zao hili, na wananchi waweze kukuwa kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichangie kuhusu leseni kuwa inaleta changamoto katika maeneo ya pwani, hivyo niiombe Serikali iweke njia rahisi ya kupata leseni ili kuondoa changamoto hii ili wananchi waweze kufanya biashara hii na kujipatia kipato na kuongeza mapato katika Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu; katika kuudumisha Muungano wetu namuomba Waziri wa Wizara ya Uvuvi awe na mawasiliano mazuri na Wizara ya Uvuvi Zanzibar ili kuwafanya wavuvi wadogo wadogo kupata kipato na kuongeza uchumi wa nchi yetu na pia kuiunga mkono dhana ya uchumi wa buluu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika hoja ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kuweza kusimama katika Bunge lako hili tukufu ikiwa ni mara yangu ya kwanza nikiwa na afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika Taifa letu. Vilevile nimpongeze Waziri na Naibu wake pamoja na watendaji wake kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nichangie kuhusu ukatili wa watoto mitandaoni; tumeona mara nyingi video za utupu zikisambazwa katika mitandao ya kijamii na matukio mbalimbali ya video na ngono za watoto na wanawake zikisambazwa katika mitandao ya kijamii kwa makusudi kabisa. Udhalilishaji huu unaleta madhara ya kisaikolojia na kusababisha hata kifo au kupoteza mwelekeo wa maisha katika jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukatili huu wa wanawake na watoto unaonekana kuathiri makuzi na mila za desturi zetu za jamii ya Kitanzania. Udhalilishaji huu umeonekana ni fimbo ya kuwapigia wanawake pindi wanapoomba ajira au nyadhifa fulani kwa makusudi au kwa wivu au kwa wivu wa mapenzi. Kwa mfano, baadhi ya wasanii, wanamuziki na maigizo wanawake hapa nchini hudhalilishwa katika mitandao yao ya kijamii wao wenyewe, haya ni matukio yasiyo ya kawaida.

Ninaiomba Serikali iangalie vizuri na iweke sheria kali kwa wale ambao wanahusiana na kadhia hii. Natoa wito kwa Serikali na asasi za kiraia kuzungumzia madhara na vitendo kama hivi vya ukatili wa kijinsia na kutoa elimu hasa katika kizazi cha sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusu wamachinga; naipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwamba kwa kulitambua kundi hili la wamachinga kwamba ni wafanyabiashara wadogowadogo ambao ndio wanaoleta pato katika Taifa letu. Sambamba na hilo nampongeza sana Rais kwamba wamachinga wawekewe maeneo rafiki ili waweze kufanya biashara zao bila ya kubughudhiwa na mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake na makusudi na mapenzi yake kwa Watanzania kwamba ameamua kutoa shilingi milioni 10 kwa kila Mkoa ili waweze kuwaendeleza wamachinga ambao ni wafanyabiashara wadogo wadogo kati yao na wanawake humo wamo, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. AMINA DAUD HASSAN: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia makadirio na mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Taifa letu kwa kutuletea utalii kupitia Royal Tour. Pia nampongeza Waziri na Naibu wake pamoja na watendaji wake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, tuzidi kuitangaza Tanzania kupitia watalii wanaokuja Zanzibar wanaokwenda Jozani kuna wanyama adimu kama kima punju vilevile kuna utalii wa kuzamia mbizi upo Paje na utalii wa culture na mila na desturi na utamaduni wetu. Mfano mapishi, ustaarabu wa mapokezi mazuri ya wageni pia tuishukuru Serikali kwa watalii wanakwenda kutembelea mikoa ya Tanzania Bara wanamalizia kuja Zanzibar ili kuweza kuona vivutio vizuri ambavyo vinapatikana Zanzibar kama hoteli iliyopo baharini Pemba, na hoteli mbalimbali kubwa.
Mheshimiwa Spika, ushirikishwaji wa private sector, tunamshukuru Bakhresa kwa kuleta meli zake ili kuweza kuwapatia na kuwasafirisha watalii kwa urahisi na kuweza kufika Tanzania Bara kwenda kuona Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kadhalika na kwenda visiwani bila ya shida yoyote.

Mheshimiwa Spika, natoa wito na kuishauri Serikali iweze kuiongezea bajeti Wizara hii ili iweze kuongeza miundombinu rafiki kwa watalii wetu ambao wanatarajiwa kuja kwa wingi sana. Kwa mfano, barabara, kuongeza hoteli ya nyota tano, kuongeza usafiri wa anga na baharini ili kuweza kumudu ongezeko la utalii, na hata watalii wanapokuja kwetu waone raha kama wapo nyumbani kwao, lakini vilevile nchi yetu itaimarika na kuongezeka kwa pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.