Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shanif Mansoor Jamal (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana umenipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyo mbele yetu. Kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema niweze kusimama kwenye Bunge lako Tukufu nichangie hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba nitoe pole kwa Mama Janet Magufuli, watoto, familia na Watanzania wote ambao tumepata msiba mkubwa wa kuondokewa na Rais wetu wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Kamati yake ya Mazishi kwa kutenda haki kumpa heshima zote ambazo Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alilikuwa anastahili, tangu siku ilipotangazwa…

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mansoor, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nafikiri wote tunajua kwamba tumepewa dakika chache, dakika tano, dakika saba. iti chako kilishatoa mwongozo kwamba kutoa pole na pongezi tushafanya kama Bunge hapa ndani wasifanye repetition. Sasa kama Mbunge anaona dakika ni nyingi kwake atupunguzie wengine walau tuweze kuchangia kwa manufaa ya Taifa hili. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ni kweli, niliwasomea Kanuni hapa, nadhani ni Kanuni ya 175, naomba tuipitie Kanuni hiyo inasema nini kwa sababu wakati ule nilieleza kwa kirefu, Mbunge ambaye anaanza moja kwa moja kwenye hoja tunaweza kupeleka ujumbe huko nje kama hajali hivi ama yeye hataki kutoa pongezi au hataki kutoa pole lakini huyo ndiye atakayekuwa anafuata Kanuni zetu zinavyosema. Kwa hiyo, tukitaka kuzungumza hayo tutafute hoja ambayo hayo tunaweza kuyasema kwa namna tofauti kuliko kuzisema moja kwa moja kwa sababu Kanuni tuliyotunga wenyewe hii hapa 175 inatutaka tufuate utaratibu huo. Karibu umalizie mchango wako Mheshimiwa Shanif Jamal.

MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naongea kwa niaba ya wananchi wa Kwimba na hapa ndiyo sehemu ya kusema pole kwa wanafamilia.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shanif tuelewanie vizuri, humu ndani kila mtu ni mwakilishi wa watu fulani lakini Kanuni tulizozitunga zinasema hivyo, kwa hiyo tufufate tu Kanuni , endelea na hoja yako. (Makofi)

MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na hoja kwamba siku ya msiba wakati mazishi yalikuwa yanafanyika Kitaifa Dodoma, nakata Bunge hili litambue kwamba watu takribani bilioni 4 walikuwa wanafuatilia kwenye runinga mbalimbali mazishi ya Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Maana yake ni kwamba Rais wetu alikuwa anapendwa na watu wengi sana ulimwenguni, ni Rais wa kipekee, ni Rais wa mfano. Kwa hiyo, mimi nimeona ni vema niseme hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wananchi wa Jimbo la Kwimba tunamshukuru sana Rais wa Awamu ya Tano kwa mambo makubwa mengi ambayo amewafanyia wananchi wa Tanzania. Niseme machache tu, la kwanza ametupa elimu bila malipo, wananchi wa Kwimba tunamshukuru sana, watoto wetu wanakwenda shule mpaka sekondari bila malipo. La pili, nataka nishukuru SGR inayojengwa itapita kwenye Wilaya ya Kwimba, italeta uchumi kwenye maeneo yetu, mambo ni mengi ametufanyia Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano. Pia ametoa heshima kwa Machinga, wafanyabiashara wadogo wadogo miaka hii mitano hawasumbuliwi, hawakimbizwi wana heshima. Hii heshima yote ametuletea Rais wetu wa Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuapishwa kwa Mujibu wa Katiba kuwa Rais wetu wa Awamu ya Sita. Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametoa hotuba mbalimbali za maelekezo. Hotuba aliyotoa siku ya kuapishwa Mawaziri aliongea takriban dakika 87 na kuendelea, alikuwa anatoa maelekezo kwa kila Wizara, hiyo ilikuwa ni hotuba ya darasa. Naomba hotuba hiyo ingeletwa hapa Bungeni ikatusaidia wakati tunachangia Wizara ili tuendane na maelekezo ambayo Rais wetu mama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa kwa Wizara mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii pia kuongea kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba niseme mambo machache. La kwanza, Jimbo la Kwimba tumekuwa na miradi mingi ya maji ambayo imetekelezwa na imeshamalizika, lakini tatizo kubwa tulilonalo, tumejengewa tenki la lita milioni mbili la maji ambalo linategemewa maji yatoke Ziwa Victoria yapande juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu ni kwamba bomba linaloleta maji kwenye hilo tenki limeharibika siku nyingi, leo ni takribani miezi sita. Tenki limekamilika la lita milioni mbili ili litoe huduma kwa wananchi wa Mji wa Ngudu na maeneo mengine, leo maji hayajafika, wananchi wa Jimbo la Kwimba wanateseka kwa maji, kwa sababu ya bomba hilo limeharibika. KASHWASA, wameshapeleka maombi kwenye Wizara ya Maji kuomba wasaidiwe ili waweze kukamilisha. Nina imani na Mheshimiwa Waziri Aweso, kilio chetu ameshakisikia, tunaomba atusaidie wananchi wa Kwimba wapate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la barabara. Tuna barabara ya lami ya Hungumarwa - Ngudu - Magu, sasa ni miaka mitano barabara yetu tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, lakini hatujui lini Wizara ya Ujenzi itatangaza hiyo barabara. Tunaomba tupate mwelekeo, Wizara ya Ujenzi ituambie lini itatangaza?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umenipa nafasi ili nichangie hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema niweze kusimama kwenye Bunge hili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii vile vile kumpongeza Waziri wa Fedha kwa hotuba nzuri aliyowasilisha hapa Bungeni, imeleta matumaini kwa Watanzania na ina mambo mengi. Kabla sijaanza kuchangia hotuba hii ya bajeti ya mwaka ujao, ninaomba nichangie bajeti ambayo inaelekea kuisha tarehe 30 Juni, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa kwa bajeti hii ambayo inaendelea sasa hivi. Pamoja na misukosuko ya kiuchumi ya kidunia ameweza kufanya kazi nzuri na miradi yote ya kimkakati imeweza kupata fedha. Ukienda kwenye Mradi wa Bwawa la Nyerere kazi inaendelea, ukifika kwenye Reli ya Kati kazi inaendelea, ukifika Daraja la Magufuli kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni machache nimeona niyaseme kwamba, kazi nzuri wanafanya pamoja na misukosuko ya kiuchumi pia kuna masuala ya kulipa mishahara kwa watumishi hawajakopa, tukiangalia nchi zingine jirani wanakopa mishahara ya watumishi lakini Serikali yetu haijakopa inalipa mshahara ndani ya wakati, nawapongeza sana. Pia fedha za elimu bila malipo kila mwezi wanapeleka fedha bila kuchelewa, hiyo nayo inasaidia watoto wetu wapate elimu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio ya Kitaifa pia Jimbo la Kwimba tumekuwa na miradi mingi sana imetekelezwa nitaomba niseme machache. Kwanza ni kwenye suala la afya, kwenye masuala ya afya sisi tumepata Hospitali ya Wilaya mpya imejengwa sasa hivi inatoa huduma, tumejengewa vituo vya afya viwili ambavyo vyote vinaelekea kuisha mwezi huu, tumepata zahanati nne zimekamilika, tukienda kwenye elimu madarasa yamejengwa sasa hivi watoto wakiingia shuleni hawakai chini kuna madarasa kuna madawati ya kutosha, tuna Chuo cha VETA kimekamilika kinaanza kutoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye masuala ya maji kuna mradi wa Hungumalwa ambao unaelekea kuisha kukamilika mwezi wa Desemba mwaka huu, tukienda kwenye maji tena tuna mradi wa Nyamilama nao unaelekea kukamilika ndani ya mwezi wa Desemba, tuna mradi wa Jojilo Maleve imekamilika maji yanatoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme taarifa ya maji ni kwamba Jimbo la Kwimba tuna Kata 15 kwa sasa hivi miradi hii ikikamilika tutakuwa tumeshapata maji ya Ziwa Victoria, maji safi na salama kwenye Kata 14. Mwakani kuna mradi wa maji wa kupeleka Malampaka - Malya itapeleka kwenye Kata moja inaitwa Mwankulwe. Maana yake Jimbo la Kwimba hadi kufika mwakani tutakuwa tuna maji salama safi Kata zote. Ahsante sana Serikali kwa kazi nzuri ambayo mnatufanyia wananchi wa Jimbo la Kwimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nielekeze kutoa mchango wangu kwenye bajeti ijayo, nianze na suala la Kilimo. Mheshimiwa Waziri kama unavyofahamu Jimbo la Kwimba ni Jimbo la Wakulima na Wafugaji. Sisi wananchi wa Jimbo la Kwimba wote ni wakulima, tuna zao la Pamba limekuwa na changamoto mwaka jana, wakati wa msimu mbegu zilichelewa kupatikana, mbolea yule mzabuni aliyechaguliwa na Serikali hakuonekana kabisa kwenye Wilaya yetu, ilibidi tuende Halmashauri, ilibidi ikodoshwe gari kwenda kuchukua mbegu, kuchukua mbolea Mwanza Mjini, tumepata shida sana kwenye mbolea haikufika dani ya muda, wakulima pia ilibidi waende kufuata mbolea Mjini. Kwa hiyo, mimi naomba mwaka huu Serikali itusaidie angalau mbegu na mbolea zifike ndani ya wakati ili wananchi wa Kwimba weweze kulima vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kama Mheshimiwa Waziri umependekeza kwenye hotuba yako kwamba unataka kupunguza ushuru wa forodha, unataka kufanya asilimia 35 ifike asilimia 10 na kwenye mafuta ya kula unataka kufanya kutoka asilimia 35 ifike asilimia 25. Mheshimiwa Waziri kwa kweli mimi sikubaliani na hiyo hoja, ningeomba hilo suala ungeliacha kama lilivyo kwa sababu inaenda tofauti kabisa na malengo ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo ilikuja na bajeti yao wanasema mambo mengine ya kuboresha na sisi hapa tunakinzana. Mimi ningeshauri hili suala uliache kama lilivyo pia usaidie wale wanaotaka kuagiza mafuta ya kula na ngano wanunue kwanza mafuta yaliyoko ndani ya nchi na pia ngano wanunue ambayo iko ndani ya nchi inazalishwa ndiyo wapate kibali cha kuagiza nje. Wasipate kibali cha kuagiza bila kuwa na mchango wa kununua mazao yanayozalishwa ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kusema ni kwenye suala la umeme. Suala la umeme napongeza sana Serikali kwamba bajeti ya mwaka kesho tutakuwa tumepeleka umeme vijiji vyote, sasa tunaanza kupeleka umeme kwenye vitongoji. Nawapongeza sana Serikali kwa maamuzi haya, lakini tatizo tulilonalo ni kwamba wananchi wetu wana uwezo wa kulipa umeme? Mimi ningeshauri na kupendekeza kwa Serikali kwamba waangalie gharama za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwamba hzi gharama za umeme zilipokuwa zimepangwa na EWURA ilikuwa wakati ule tulikuwa tuna jenereta za Diesel kama mfano Kigoma ilikuwa inatumia majenereta ya diesel, kwa hiyo gharama ya uzalishaji ya umeme ilikuwa juu. Sasa hivi tunazalisha umeme kwa kutumia gesi na mabwawa kwa hiyo bei imeshuka mimi ningependa sana Serikali iangalie tunawapelekea wananchi umeme lakini wana uwezo wa kulipa umeme? Nashauri tupunguze bei ya umeme ili wananchi kwenye vitongoji waweze kuunganishwa na umeme, tusije tukafikisha nguzo lakini haziendi kwenye nyumba kwa sababu hakuna uwezo. Kwa hiyo, lazima tuandae uwezo wa wananchi kupata umeme na kutumia umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ningependa kulisemea ni la barabara. Siku chache zilizopita Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitoa tamko hapa Bungeni wakati wa Wizara ya Ujenzi. Tunayo barabara yetu ya Hungumalwa - Ngudu kuelekea Magu tunataka ijengwe kwa lami. Miaka mingi tumeomba hiyo barabara tukaambiwa na Waziri wa Fedha kwamba kuna fedha za African Development Bank anazifuatilia, akizipata hiyo Barabara ya Hungumalwa-Ngudu kueleka Magu ataitangaza. Bajeti yake ambayo amewasilisha Mheshimiwa Waziri tumeona hiyo kwamba fedha za African Development Bank zipo zimekuja. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri wakati unafanya wind up ya hotuba yako, tuambie lini unatangaza barabara yetu ya Hungumalwa inajengwa kwa lami, lini unatangaza, hilo tamko lako tunalisubiri siku una-wind up hotuba yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwamba Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza tumebaki peke yetu hatuna barabara inayotuunganisha kwenye Mkoa kwa lami. Tunayo barabara ya kutoka Ngudu kwenda Jojilo kwenda Mabuki iko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kujengwa kwa lami. Tunaomba hiyo barabara pia ifanyiwe utaratibu wa kujengwa kwa sababu Wilaya haiwezi kuwa haina barabara ya lami kwenda kwenye Mkoa. Wilaya zote zinaunganishwa na lami lakini Wilaya ya Kwimba imebaki peke yake tunaomba angalau na hilo pia walifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la kimkoa, Mkoa wa Mwanza tumekuwa na kero ya jengo la abiria kwenye uwanja wa ndege, miaka mingi tumekuwa na kero, tumekuwa tukisemea. Kuna jengo la abiria limejengwa limekuwa na mapungufu, hilo jengo wameshakabidhiwa Tanzania Airport Authority kwamba waliboreshe, wakamilishe. Tunaomba sana uwanja wetu wa ndege uboreshwe na hilo jengo likamilike. Tunaomba Serikali ituambie lini TAA watakamilisha hilo jengo ili liweze kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na wageni wetu wanaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu Airport ya Mwanza ndio sura ya Mwanza. Mgeni anapokuja anakutana na ile jengo ambalo limekaa pale halikamiliki, limekaa kaa tu pale, tunaomba hilo jengo nalo lipate kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu, nakushukuru sana kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kipekee ya upendeleo niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukuwe nafasi hii pia ku-declare interest mimi ni mdau kwenye biashara ya mafuta na mdau mkubwa kwa Wizara ya Nishati. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri sana ambayo ameitoa leo hapa pia naomba nichukuwe nafasi hii kuunga mkono hotuba yake mia kwa mia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mie nitachangia maeneo machache la kwanza ningeomba kuchangia kwenye sehemu ya REA III. Mpango wa kuusambaza umeme vijijini, kwenye Jimbo la Kwimba umeanza miaka mingi 2013 REA round III, ilianza kuna vijiji tulikuwa tumekubaliana tulipewa orodha kwamba vitapata umeme kwenye miaka miwili ya 2019 na 2020.

Mheshimiwa Spika, mpango wa REA III kwenye Jimbo la Kwimba unasuasua sana kuna maeneo mkandarasi anasuasua sana wameweka nguzo lakini waya bado hajasambaza umeme kwa kweli unaenda kwa suasua sana kwa wananchi, pia kuwaunganisha wananchi pia imekuwa ni changamoto kwa sababu ukienda kwenye REA unaambiwa elfu 27 wananchi wakienda kwenye Ofisi ya TANESCO waambiwa 177,000 kwa kweli ni mkanganyiko mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ningeomba Mheshimiwa Waziri aliweke wazi kwamba Jimbo la Kwimba ni jimbo ambali lina vijiji 59 ina mitaa 14 lakini ni sehemu ambayo kama kijiji kwa hiyo inatakiwa iwe ni bei ya 27,000 lakini kuna maeneo wananchi wanatozwa 177,000 wanashindwa kulipa na pia kuunganisha wananachi wengi sana wameshalipia lakini kuunganisha umeme pia ni shida sana.

Mheshimiwa Spika, ningeshauri pia kwamba TANESCO kila mradi ukisoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amewapa TANESCO watafanya, lakini TANESCO naona kama uwezo wao utakuwa umekuwa ni mdogo sana kwa sababu kila mradi TANESCO unatekeleza. Ningeshauri pia maeneo mengine tuweke wakandarasi waweze kusaidiana na TANESCO tukiwapa TANESCO kazi zote hizi za kuunganisha wananchi nyumbani kwao itakuwa ni shida sana ningeshauri pia wakandarasi wengine waweze kuunganisha wananchi wapate umeme kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, TANESCO nafikiri out-stress hawana watumishi wa kutosha wapo lakini hawatoshi kwa sababu kazi ni kubwa tunataka tufike vijiji vyote vipate umeme awamu hii sasa maana yake lazima tufanye kazi ya ziada.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la REA ningeomba hilo walifanyie kazi lakini pia maeneo mengi wanaweka nguzo za miti lakini kwetu kwenye Jimbo la Kwimba kuna maeneo wakati mvua ikinyesha maji yanapita nguzo zinaanguka wanarudia kazi ya marudio imekuwa nyingi sana. Ningeshauri kwamba kuna maeneo wanaona ni korofi waweke nguzo za zege kwa nini wanarudia kwa hiyo watu wanapenda kufanya kazi ya marudio maana yake labda inalipa posho kwa hiyo watu wacha turudie lakini wananchi pia wanapata shida. Umeme unakatika mara kwa mara kwa sababu ya nguzo zimeanguka mimi ningeshauri maeneo korofi mengine waweke nguzo za zege angalau kazi isiwe ya kurudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ningependa kuisemea ni sehemu ya EWURA nimeshasema kwamba ni mdau kwenye sheria ya EWURA ningeomba kama ungeweza kukubali ungeagiza Serikali walete sheria EWURA ifunguliwe upya hapa Bungeni tuanze kuiangalia upya kwa sababu sheria EWURA tuliunga miaka 20 iliyopita. Sasa hivi sheria EWURA imekuwa ni sheria kandamizi kwa vituo vya mafuta, imekuwa kandamizi kwenye kuendeleza sekta ya mafuta kwa sababu faini zao zimekuwa ni kubwa sana kwenye vituo ambavyo kwa kweli vituo vinashindwa kulipa vinakula mtaji. Tunataka vituo viende mpaka vijijini lakini masharti na kanuni za EWURA hazitafanya mtu apeleke kituo kwenye Kijiji kwa sababu gharama zao ni kubwa sana kwanza kupata kibali ni gharama mazingira ukienda vibali ni vingi sana ningeomba suala hili la EWURA tuliangalie kwa upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza EWURA wamekamata maji, nishati, mafuta nao wamezidiwa, ningeshauri hii sheria iangaliwe upya labda tuwe na taasisi inasimamia maji peke yake, kuna taasisi inasimamia nishati peke yake, kuna taasisi inasimamia mafuta peke yake. Kwa hiyo, sasa hivi ukiangalia Bodi wa EWURA pia inateuliwa na Waziri wa Maji lakini huku Waziri wa Nishati nae anatakiwa afanye kazi na wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, inakuwa ni ngumu sana ningeshauri EWURA tungeweza kuifumua upya tena sheria yake tukawa na taasisi tofauti tofauti. Mfano nilikwambia juzi EWURA wametangaza kwamba gari ya abiria ikiingia kwenye kituo utatozwa faini milioni 7 kwenye kituo, sasa mwenye kituo una makosa gani kama basi imeingia na abiria anataka mafuta unatozwa wewe milioni 7. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, milioni saba ni pesa nyingi sana kwenye kituo, labda uuze lita laki moja ndio upate milioni 7 hiyo, maana yake hizi faini wanazitoa wapi sijui ningeomba tuliangalie hili kwa undani sana kwamba hizi faini zimekuwa ni kubwa sana mfano ukikutwa na kosa na EWURA unatozwa faini ya milioni tano kosa la pili milioni 10 kosa la tatu milioni 20 kosa ya nne unafungiwa sasa hizo pesa ni nyingi sana ningeomba suala hili la EWURA tuliangalie upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uliagize waambie wakuletee faini wanazozitoza EWURA utashanga kituo huwezi kuendesha hii sekta ya mafuta kutoa huduma vijijini inataka iwe tuboreshe huduma ya mafuta ipatikane mpaka vijijini haitafika huko kwa sababu masharti haya hatutafikisha huko tuisaidie Serikali tuangalie utaratibu mpya wa kupata vibali vya kujenga pia vibali vya kujenga vijijini pia vina masharti kibao unawaambia milioni 2 ulipie mazingira pia umpe usafiri wa kufika kwenye eneo husika kwelli vibali ni vingi sana hatupata maendeleo kwenye sekta hii, ningeshauri hilo kwamba EWURA tuliangalie upya ili tuweze kufanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sehemu ya tatu ningependa kuchangia ni sehemu ya vina saba nawashukuru sana Serikali wamefanya maamuzi mazuri kwamba TBS wasimamie vina saba waweke TBS, lakini sheria ya TBS ni kusimamia ubora wa mafuta kwenye sheria yao hawana sheria ya kusema pia vina saba ni sehemu ya kazi yao. Kwa hiyo, muhimu sana tuangalie hiyo sheria ya TBS kama inawaruhusu kufanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Spika, pia suala lingine pia tumelisema sana kwamba GFI alikuwa ni mkandarasi wa nje alipata gharama kubwa lakini lazima tujuwe GFI alikuwa ni mwekezaji ni kampuni ya kitanzania, GFI ni Tanzania Limited ni kampuni ambayo inalipa kodi ndani ya nchi yetu. Lazima tulijue hili kwa sababu hawa ni wawekezaji sisi tunataka Mheshimiwa Rais amesema anataka wawekezaji waje ndani ya nchi basi tuwe na utaratibu wa kuwatoa kwenye mikataba kwa sababu tunataka wawekezaji waje watulipe kodi GFI atalipa kodi kila mwezi analipa VAT analipa kodi ya mapato, TBS hizo atalipa.

Mheshimiwa Spika, tumeamua tunaenda huko lakini ninachosema tuwe na process ya kuachana na mtu kwa utaratibu hilo ndio nimeona niliseme mimi kuhusu vina saba napongeza Serikali kwa maamuzi kwamba TBS wafanye lakini pia utaratibu mwingine ni kwamba TBS sasa hivi wananunua vina saba, kwa walewale wazungu wako na ubia na GFI. Kwa hiyo, lazima wajibadilishe pia. Watafute tenda watangaze wanunue kwa utaratibu wa Serikali sasa hivi inanunuliwa bila kufuata utaratibu kwa hivi ni muhimu ningeshauri Serikali wafanye utaratibu TBS wanunue kwa utaratibu wa PPRA wafuate sheria zote za nchi ili tupate unafuu, unafuu wa vina saba tunapoelekea kwamba tu-save pesa kwenye gharama za vina saba ili tupate pesa kwenye TARURA basi tufike pale kwenye lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nakushuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi, afya njema niweze kusimama hapa kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya miaka miwili ya utawala wake, kwa kweli miradi yote ya kimkakati inatekelezwa na pia miradi mipya ameanzisha kwa kweli tumamshukuru sana na tunampongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii tena kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutuletea miradi mingi kwenye Jimbo la Kwimba katika kipindi hiki cha miaka miwili lakini niseme michache tu. Kwa kipindi cha mwaka mmoja huu tumepata hospitali mpya ya Wilaya, vituo vya afya viwili vipya. Kwenye masuala ya maji tumepata miradi mitatu mikubwa ya maji Hungumalwa sasa hivi tuna maji ya bilioni nne, Shibumulo pia kuna mradi wa maji unajengwa pale. Mambo haya niyaseme kwa sababu kwenye Jimbo la Kwimba tuna Kata 15 sasa hivi Kata 14 tuna maji ya Ziwa Victoria yote ni kwa sababu ya mafanikio ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Tumebakiza Kata moja tu ambayo tunategemea mwaka ujao tutapata maji, maana yake Jimbo la Kwimba wananchi wote wanapata maji safi na salama ya Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda hautoshi nimesema miradi michache. Naomba nichukue nafsi hii kwenda kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ya matumaini uliyoisema hapa tunakupongeza sana. Mheshimiwa Waziri, tunakupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya wewe, Naibu wako, Watendaji wako wote wa Wizara ya Nishati, hongereni sana kwa kazi nzuri sana mnayoifanya. Vilevile, nichukue nafasi hii kupongeza taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara yako, wanafanya kazi nzuri inaonekana. Kwa kweli mwaka huu Mheshimiwa Waziri umekuja hapa hakuna kelele kwenye Wizara ya Nishati lakini nakumbuka mwaka jana ulipofika hapa kulikuwa na kelele nyingi kwenye Wizara ya Nishati, mwaka huu kidogo pametulia.

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri nikupongeze kwa maonesho ya mwaka huu yaliyofanyika kwenye viwanja vya Bunge pale nje, kwenye maonesho ya nishati. Nimefika pale nimekutana na watu wa REA na maeneo mengine mbalimbali, kwa kweli maonesho ni mazuri sana. Pia, teknolojia mliyotumia kutoka viwanja vya Bunge mmenipeleka mpaka Julius Nyerere nimefika kwenye bwawa pale nashukuru sana nimepaona sina cha kusema. Niseme tu hongereni sana kwa kazi kubwa mnayoifanya kwenye bwawa, endeleeni Mungu awatangulie kuhakikisha kwamba mradi ule kama ulivyosema kwenye hotuba yako kwamba mwaka ujao mradi utakamilika nawatakia kila la kheri ule mradi ukamilike.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nitaongea hoja mbili tu. Hoja ya kwanza nitaongelea kuhusu REA. Mimi nawapongeza sana REA wanafanya kazi nzuri. Jimbo la Kwimba mimi nimebakiza Kata mbili ambazo ni Kikubiji na Mhande ambapo sasa hivi ndiko wanakofanya kazi, wamesema mpaka Agosti mwaka huu watakuwa wamemaliza kuunganisha umeme kwenye vijiji vyote. Ninashukuru Jimbo la Kwimba mpaka Desemba tutakuwa tuna umeme kwenye vijiji vyote, nashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, changamoto tunazopata ni kwamba wanaunganisha vijiji vingi lakini tatizo liko kwenye vitongoji ambavyo vimebaki, kwa sababu watu wameshaona utamu wa kupata umeme jirani sasa wanataka na wao wapate umeme, hiyo changamoto ni kubwa Mheshimiwa Waziri kama ulivyosema kwenye hotuba yako kwamba utatuunganishia vitongoji 15 kwa mwaka ujao kwa kweli kwenye mahitaji ya Jimbo la Kwimba haitoshi nafikiri na wengine pia haitatosha, mimi ninashauri kwamba hivi vitongoji 15 havitatosha tunaomba uongeze angalau vifike hata kwenye vitongoji 50 kwa mwaka kesho kuunganisha kwa kila Jimbo angalau tutakuwa tumepunguza kero kwa wananchi. Hilo ni ombi langu kuja kwako kwamba tunaomba utusaidie kuongeza vitongoji angalau vifike 50 kwa mwaka kesho.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ningependa kulizungumzia hapa ni kwamba Jimbo la Kwimba tuliahidiwa kuletewa taa za barabara za REA, nina Mji wa Ngudu pale nina lami kilomita nne inaelekea kilomita tano lakini hakuna taa hata moja ya barabarani.

Mheshimiwa Spika, tunaomba angalau tuliahidiwa taa 200 tutaletewa ili angalau na miji yetu ipendeze kidogo kwa sababu sasa umeme uko vijijini, umeme uko kwenye miji, kwenye nyumba za watu lakini barabara ni giza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeomba wakati wa majumuisho basi unisaidie angalau kunipatia hata taa hizo 200 za barabara angalau miji yangu ya Hungumalwa, Shilima, Ngudu, Gojiro, Malege na Milama angalau vipate taa za barabara. Mheshimiwa Waziri naomba utusaidie kwenye taa za barabara.

Mheshimiwa Spika, lingine Mheshimiwa Waziri ningependa kulizungumzia sasa hivi hapa ni suala la EWURA. EWURA wanafanya kazi nzuri sana lakini Mheshimiwa Waziri Sheria na Kanuni za EWURA zimepitwa na wakati. EWURA ilianzishwa na Sheria na Kanuni ambazo wakati ule tulikuwa hatuna bulk procurement system.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa sasa hivi Kanuni na Sheria wanazozitumia EWURA zimepitwa na wakati kwa sababu kwa mfano, ukienda mimi naomba ni-declare kwamba ni mdau wa Wizara, hii naji-declare kwamba EWURA wanapofanya vipimo vya vinasaba kwenye vituo, wamakuta wanaenda tofauti na sera za sasa hivi za Mheshimiwa Rais kwamba kazi iendelee wao wakifika wakikuta kuna tatizo kwenye kisima kimoja cha tenki wanafunga kituo kizima maana yake hawaendani na sera ya Mheshimiwa Rais ya kazi iendelee wao wanafanya kazi ifungwe.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri hivi vituo kufungwa ni kero na wakati unakuta Mheshimiwa Waziri ni kwamba kwenye kituo umekuta kuna mafuta aina tatu, unakuta tatizo lipo kwenye tenki moja lakini unafunga kituo kizima, sasa kile kituo ukikifunga maana yake mfanyabiashara yule amewekeza, ana madeni ya benki ana wafanyakazi wanafanya kazi halafu zile faini ni kubwa. Zile faini ni kubwa sana kwa hiyo, mimi ningeshauri hizi Sheria na Kanuni ziangaliwe upya kwamba zitatusaidiaje.

Mheshimiwa Spika, jingine Mheshimiwa Waziri niseme kwenye suala la EWURA kuna suala la ki-technical wanafanyafaga kukagua Research Octane Number (RON) inatengenezwa kwenye refinery haitengenezwi kwenye depo wa la kwenye kituo RON inatoka kwenye kiwanda so wanakuja wanapima RON wakipima RON ni neno la kitaalamu unakuta RON haiko sawa, isipokuwa sawa unapigwa penati ya milioni saba, milioni 20, unafungiwa kituo.

Mheshimiwa Spika, hili suala la RON linatengenezwa kwenye refinery haitengenezwi Tanzania, sasa mtu mwenye kituo ana makosa gani kama RON iko tofauti? Maana yake wakati meli au wakati shehena imetoka kwenye refinery imekuja Dar es Salaam watu wa TBS wanaopima mafuta hayo wana makosa hawakufanya ukaguzi vizuri pale, yale mafuta yameshuka mpaka kwenye vituo, kwa hiyo mwenye depo hawezi kubadilisha RON, mwenye kituo hawezi kubadilisha RON.

Mheshimiwa Spika, RON inatengenezwa kwenye kiwanda, kwenye refinery. Kwa hiyo, mimi ningeshauri hizi kanuni na sheria za EWURA mziangalie upya zilianzishwa wakati hakuna bulk procurement, kazi wanafanya nzuri lakini sheria hizi ndiyo zimewabana.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu ndiyo huu tu ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nichangie hoja, ahsante sana. Naunga mkono hoja asilimia mia, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwenye hotuba hii ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri yenye matumaini kwa wananchi ambayo ameitoa hapa mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kuchangia katika maeneo machache matatu. La kwanza, ningependa kuchangia sehemu ya umeme vijijini REA. REA ni changamoto kubwa tuliyonayo sisi wananchi wa Jimbo la Kwimba. Tuna vijiji takribani 32 tunasubiri kupata umeme. Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatangaza kwamba umeme utafikishwa mwaka huu mwishoni lakini bado kuna changamoto, ukimfuatilia mkandarasi amemaliza vijiji vinne kupata umeme, lakini hivyo vijiji vinne ambavyo ameshavimaliza bado hajawasha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli shughuli ya umeme vijijini inaenda taratibu sana, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri aweke nguvu ya ziada, umeme vijijini ni siasa. Ni siasa kwetu sisi huko vijijini, hivyo, tunaomba tupate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kusema kwenye bajeti ya mwaka huu mahitaji ya kupeleka umeme vijijini kwenye bajeti yake Mheshimiwa Waziri amesema mahitaji ni shilingi trilioni 1.24, lakini fedha alizozitenga ni bilioni 164, ni asilimia 15 tu. Nasema hizi fedha ni ndogo sana anatakiwa aongeze bidii kwa sababu maana yake tutapata umeme vijijini asilimia 15 tu kwa mwaka ujao. Ningeomba sana hizi fedha za kupeleka umeme vijijini zingeongezwa kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili pia kuna changamoto wakandarasi wanasema hata Mheshimiwa Waziri alitwambia kwamba kuna changamoto, vifaa vimepanda bei, wanaboresha mikataba na wakandarasi. Naomba tupate mwelekeo wa Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake wakati anatupa majibu, atuambie wakandarasi hawa anafunga nao mkataba lini, watarekebisha lini, ili hawa wakandarasi waweze kuendelea na kazi kwa speed kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la subsidy, suala la shilingi bilioni 100 ambayo Serikali imetoa kwenye mafuta. Naomba ku-declare interest mimi ni mdau, nataka nipongeze Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo imefanya ya kutoa msaada kupunguza makali ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii subsidy ya bilioni 100 iliyotolewa kwenye mwezi Juni ina changamoto nyingi sana ambazo imekuja nazo, wafanyabiashara wa mafuta, kuna mafuta yamekaa kwenye maghala ambayo yalishalipiwa kodi sasa hivi yale mafuta yote yaliyokwishalipiwa kodi sasa inabidi uuze kwa pungufu ya sh.300 ambayo ni subsidy. Kuna hasara kwenye kwa makampuni ya mafuta takribani shilingi bilioni 50 inapatikana hasara kwa makampuni ya mafuta ambayo yamekutwa na stock ya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba subsidy nasaidia kupunguza makali lakini kuna utaratibu, sasa maana yake mafuta ni biashara ni shughuli ambayo ni nyeti sana haitaki kuingiliwa sana. Maana yake sasa mwezi wa Sita tumeingilia mwezi wa Saba hatujui kinachoondelea, kutakuwa na utofauti tena, maana yake kuna mafuta utakuwa unalipia mwezi wa Sita utavuka nayo mwezi wa Saba. Sasa mwelekeo wa mwezi wa Saba haijulikani tena itategemea kwamba Makampuni tena yatapata hasara au itatokea nini. Mimi ningeshauri wazo la Serikali kupunguza makali ni mazuri lakini iwe endelevu, maana yake ifanyike kwa miezi mitatu au miezi sita. Kila miezi itakuwa ina changamoto yake. Kwa hiyo mimi ningependa kusema kwamba hii subsidy ni kitu kizuri lakini wakifanye kiwe kama Sera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshauri kwenye suala la subsidy kama inaendelea basi Mheshimiwa Waziri alivyosema kwenye hotuba yake kwamba ataka aanzishe stabilization fund, maana yake basi wangetangaza ingekuwa ni stabilization fund. Mfano, wangetoa fidia kwa miezi mitatu wakati mafuta yanapanda bei basi baadae wakati mafuta yakianza kushuka mwezi wa Agosti, Septemba, mafuta yakianza kushuka bei wanaanza kurudisha ile stabilization fund kurudisha hii fedha. Kwa hiyo, maana yake kuwe na sera na kuwe na utaratibu mzuri wa kuweka wazi kwamba hili suala litaendaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kulisema leo ni suala la Bulk Procurement Agency. Mimi niwapongeze, Bulk Procurement Agency wanafanya kazi nzuri sana, wanasimamia kuagiza mafuta kwa niaba ya Makampuni ya mafuta. Leo takribani miaka 11, Bulk Procurement Agency wanafanya kazi ya kuleta mafuta ndani ya nchi. Changamoto zipo lakini pia kazi nzuri wamefanya. Hapo nyuma nilisikia mara nyingi watu wakisema kwamba hii mafuta tungevunja Bulk Procurement tukaanza kufanya watu wafanye mafuta ya kuleta watu binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi duniani ambayo inaweza ikaacha mafuta ikafanywa na wafanyabiashara peke yao, lazima Serikali iwe na mkono wake isimamie, changamoto ipo lakini tunafanya kazi vizuri. Pia lazima tufahamu kwamba Bulk Procurement tender zinazotangazwa ndani ya nchi yetu zinaleta mafuta kwa ajili ya nchi nyingine Sita ambazo zimetuzunguka, nchi ya Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi, Uganda wanategemea mafuta yanayoletwa kwenye Bulk Procurement. Kwa hiyo, mimi ningeshauri Serikali wanapofanya maamuzi waangalie kwamba nchi hizi Sita pia zinategemea mafuta yanayoletwa ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo tunavyoboresha tuangalie na nchi hizi Sita ambazo zinatuzunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kulisema pia Tanzania tumetoa subsidy nchi zinazotuzunguka zote Sita hizi hazijatoa subsidy. Itafika sehemu tutaenda tutakuta nchi za jirani mafuta ni bei nafuu kuliko mafuta ya Tanzania. Kwa hiyo, lazima tuangalie tuwe tunaenda pamoja na nchi za jirani kwa sababu mafuta yote yanayoingia ndani ya nchi yetu yanaenda pia kwenye nchi ya jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kulisema ni kwenye Bulk Procurement tunafanya tendering ya meli takribani Nane au Tisa kwa mwezi. Naipongeza Serikali wamewapa uwezo TPDC toka mwaka jana Desemba, mwaka jana Oktoba wameanza kushiriki, naomba TPDC waongeze speed ya kushiriki, wanashiriki kwenye tender moja moja tu za diesel kwenye petroli TPDC hawashiriki sijui kwa nini. Mimi ningeomba sana na ningeishauri Serikali TPDC pia inatakiwa ishiriki kwa undani zaidi maana yake inatakiwa TPDC inavyoshiriki unakuta na bei zinashuka kidogo. Kwa hiyo, TPDC tungeomba muwape nguvu ya ziada, TPDC ishiriki kwenye tender za kila mwezi. Kuna tender Nane unakuta TPDC ana tender moja tu ndiyo anashiriki au mbili zingine zote anaziachia. Mimi ningeomba sana Mheshimiwa Waziri TPDC washiriki kwenye tender zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi ya kusema nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja. Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)