Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eric James Shigongo (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili. Naishukuru familia yangu, Wajumbe wote na wananchi wote wa Buchosa walionipa nafasi ya kuwa hapa, Chama changu Cha Mapinduzi, Mwenyekiti, Katibu wa Chama chetu cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nachukua nafasi hii kuwashukuru sana viongozi wa nchi yetu waliotangulia ambao kwa uwepo wao, maisha yangu leo ni bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yetu leo hapa ni kujadili hotuba mbili za Mheshimiwa Rais. Nami nimepata bahati ya kuzisoma kama walivyozisoma wenzangu wote, nimezisoma na nimezielewa. Katika kuzisoma kuna kitu kimoja kikubwa nilichokigundua kwamba Mheshimiwa Rais anawaamini sana Wabunge wake na anaamini kwamba hakuna kiongozi duniani anayefanikiwa peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Musa alichagua wazee; Yesu Kristo alikuwa na wanafunzi wake 12; na Mtume Muhammad alikuwa na Maswahaba wake. Kwa hiyo, sisi hapa ndani ni Maswahaba wa Mheshimiwa Rais, ametuamini, amekuja kutusomea hotuba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusoma, nimekumbuka kitabu kimoja nilikisoma kinaitwa Checklist Manifesto. Kwa wale ambao wamekisoma watagundua kwamba hotuba hizi mbili za Mheshimiwa Rais ni Checklist Manifesto mbili; ya kwanza ilikuwa ya 2015 – 2020 ambayo inaonyesha mambo ambayo Mheshimiwa Rais alitaka kuyafanya kwenye kipindi cha miaka mitano. Nikiwauliza kwenye Checklist Manifesto, kazi yako ni ku-list mambo yako, unatiki moja baada ya lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikikuuliza wewe na Waheshimiwa Wabunge kwamba kwenye miundombinu, Mheshimiwa Rais ametiki au hajatiki?

WABUNGE FULANI: Ametiki! (Makofi)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwauliza kwenye umeme, Mheshimiwa Rais ametiki, hajatiki? Kwenye barabara, ametiki hajatiki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mengi yametikika. Sasa tuna Cheklist Manifesto ya pili ya mwaka 2020 – 2025, ni checklist ngumu zaidi ya checklist tuliyomaliza. Ni ngumu kwa sababu nchi yetu iko kwenye uchumi wa kati. Ni checklist ambayo siyo rahisi kama iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuja kwenu na nazungumza mbele yako na mbele ya Watanzania wote kuwakumbusha kwamba kasi tuliyonayo ni kubwa. Mengi yamefanyika, kazi kubwa imefanyika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote, lakini nataka niwakumbushe kwamba kazi tuliyonayo mbele ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu mmoja aliwahi kusema kwamba the smallest of implementation is better than the biggest of intensions. Kama hatutatekeleza hotuba hii, tukabaki na mazungumzo ya hotuba nzuri, hakika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais itabaki ni intensions peke yake, hakuna matokeo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea private sector. Kwenye private sector hatuna hotuba nyingi sana, tuna utendaji peke yake. Nazungumza hapa nikiwaomba Waheshimiwa Wabunge, katika Checklist Manifesto ya pili 2025, tufanye kazi, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, tusimvunje moyo Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma katika hotuba yake, ukurasa siukumbuki vizuri, lakini amesema kwamba mazao ya bahari yangeweza kuiingizia nchi yetu shilingi bilioni 320 na kitu hivi kwa mwaka. Tunazozipata ni kidogo mno kwa sababu tulishindwa kudhibiti na kusimamia vizuri, (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia nyuma ya statement hiyo kwa mimi mwanafasihi, nagundua kwamba Mheshimiwa Rais alikuwa na manung’uniko, alikuwa na masikitiko. Nawaomba Waheshimiwa Mawaziri walioko hapa ambao mmepewa jukumu, mmefanya kazi nzuri sana kwenye checklist manifesto ya kwanza. Mmeaminiwa, fanyeni kazi, tumikeni, tengenezeni historia, tuko hapa kujenga historia yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wetu watakapokuja baada ya miaka 20 waseme maisha yao ni bora sana kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa kaka yangu Majaliwa. Watoto wetu wasimame waseme maisha yao ni bora kwa sababu sisi tulioko ndani ya ukumbi huu leo tutafanya maamuzi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kuwaomba ndugu zangu, Watanzania wanatuamini, dunia inatutazama, tutakachokifanya hapa ndani katika kipindi cha 2025 ni kufanya maamuzi ambayo tutatekeleza ndoto ya Mheshimiwa Rais wetu. Viwanda ni ndoto ya Rais wetu lakini hakuna viwanda bila kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikomee hapo. Ahsanteni sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kusimama tena ndani ya Bunge hili Tukufu kutoa mchango wangu ndani kwa Taifa langu. Naomba tu niishukuru sana familia yangu, wapiga kura wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya kunileta hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa matumaini. Najua nasikilizwa hap ana watu hapa ndani, lakini najua nasikilizwa na Watanzania sehemu mbalimbali ya nchi yetu. Naomba tu niseme hivi, nina matumaini makubwa kwa nchi yangu leo kuliko ilivyokuwa jana. My hope for this country is greater today than it was yesterday. Nataka niwaambie Watanzania wanaonisikiliza kwamba tunakokwenda ni kuzuri sana.

Sasa nina bahati ya kuwa hapa ndani leo, tangu nimeingia nasikiliza watu wanaongea, nasikiliza napata muda wa kujifunza. Namshukuru Mungu niko hapa ndani nashiriki, zamani nilikuwa nawaangalia mnaongea nikiwa nje. Najifunza kitu kimoja kikubwa sana. Ukiwa hapa ndani kuna wakati uweke fence kwenye akili yako, ujiwekee fence, useme hiki hakiwezi kuingia kwenye kichwa changu, hiki kinaweza kikaingia maana kuna mtu anaongea kitu halafu najiuliza hivi huyu hajui yanayoendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inakua, tena inakua kwa kasi! Nani hajui tulipotoka? Nani hajui?

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe Taarifa Mheshimiwa Mbunge Eric Shigongo anayeongea kwamba katika Bunge hili sisi tuko kwa niaba ya wananchi tunatoa mawazo yetu na ya wananchi, kwa hiyo pana uhuru wa mawazo yote tunayoongea ni sahihi mahali hapa. Mwisho wa siku tunakuja na kitu kimoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shigongo hajamtaja mtu, endelea tu.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hiyo sijaipokea kwa sababu sijamtaja mtu yeyote. Nataka niwaeleze Watanzania na niwaeleze watu wote walioko hapa ndani kwamba mnapoamua kujenga uchumi kuna transition period. Kuna kipindi cha mpito lazima mpite. Hata ukisoma historia ya China wakati wa Mao Tse Tung kulikuwa na kipindi kigumu sana walikipitia wale watu hatimae wakafika walipo leo. Yawezekana tunapita lakini tumeshaanza kupita kwenye transition hivi sasa mambo yanaenda kuwa safi. Nataka kuwaambia Watanzania wanaonisikiliza kwamba ya kwamba wawe na matumaini, wawe na imani na kiongozi wetu mkuu, wawe na Imani na Bunge hili ya kwamba tunakokwenda ni kuzuri na kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nichangie Mpango wa Mwaka mmoja na wa Miaka Mitano. Nasema hivi; nitachangia eneo la digital economy, uchumi wa kidijitali. Eneo la viwanda na nikipata nafasi nitachangia eneo la mitaala yetu ya elimu kwa ajili ya watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia nizungumze mambo matatu tu ya muhimu kwamba we are a blessed country. Tanzania kama Tanzania ni nchi iliyobarikiwa sana. Kuna mtu alisema kwamba Mungu wakati anaumba dunia inawezekana siku ya saba alikuwa yuko Tanzania, maliasili zote aliziacha hapa wakati anakung’uta kung’uta mavazi yake ili arejee alikung’uta kila kitu akaacha hapa. Kaacha gesi, makaa ya mawe, almasi, dhahabu na kadhalika. Wakati anaondoka wanasema akadondosha handkerchief yake pale Arusha kadondosha Tanzanite pale haipo sehemu nyingine duniani. This is a blessed country, tukusanyikeni hapa tuzungumze namna ya kutumia utajiri wetu kupeleka Taifa letu mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kulizungumzia ni uchumi wa kati. Hatujafika kwenye uchumi wa kati accidentally, hatujafika kwa bahati mbaya. Kuna mambo tuliyafanya yametufikisha hapo. Mambo hayo tuliyoyafanya tunayajua, basi tukayafanye mara mbili zaidi tulivyokuwa tukifanya zamani. Tutapanda kutoka uchumi wa kati wa chini kwenda uchumi wa kati wa juu, hili linawezekana. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu linahusu kufanya kazi kwa juhudi kubwa. Haukuwepo Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza hapa nikawakumbusha Wabunge juu ya checklist manifesto, kuandaa mpango kama huu uliokuja halafu mnakuwa mna-tick kimoja kimoja mnachokifanya baadaye kwenye siku ya pili au mwaka wa pili mnahama na yale ambayo hamkuyatimiza huko nyuma. Lazima tuwe na checklist manifesto ya namna ya kutekeleza mambo yote tunayoyapanga kwenye mpango huu na tuanze moja baada ya lingine na tupange vipaumbele vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Afrika huwa inateseka na tatizo kubwa sana la kupanga priorities. Sisi tukatae, sisi tuwe watu tunapanga priorities zetu sawasawa, tunaanzia hapa kwa sababu ni muhimu, tunakuja hapa, tunakwenda hapa, tunakwenda pale. Watu tufanye kazi, Rais wetu anafanya kazi sana. Tuna Rais mchapa kazi, Rais visionary, lazima tumuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais huyu hana maneno mengi na hazungumzi sana. Mfano, juzi alikuwa Mwanza akasema huko Dar-Es-Salaam nikija nikute shule imejengwa; imejengwa haijajengwa?

WABUNGE FULANI: Imejengwa.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo ndiye Rais tuliye naye tufananye nae Watanzania wote tufanye kazi kwa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda kusoma vitabu. Kaka yangu Waziri wa Sheria aliwahi kuniambia msemo mmoja niurudie hapa, akasema ili ufanikiwe lazima uwe na kitu kinaitwa Bibliophilia, yaani usome sana vitabu. Sijasoma sana lakini napenda kusoma sana vitabu. Nimesoma kitabu cha Jack Welch, Jack Welch is a number one general manager in the history of the world. Huyu ndio aliyeitoa General Electric kwenye kufilisika mpaka kuwa number one company in America.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jack Welch alisema ili uongoze watu lazima ufanye mambo mawili. La kwanza uwaongoze kwa compassion, kwa kuwasukuma au uwaongoze kwa persuasion, kwa kuwasihi na kuwabembeleza wafanye kazi. Hapa Tanzania na Afrika Jack Walsh angekuja kufanya kazi hapa angefilisika. Kwa sababu hapa Tanzania ukitaka kuwapeleka watu kwa kuwabembeleza kazi haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina kampuni binafsi; nilijaribu persuasion ikanishinda nikaamua kutumia compassion kwamba anayetaka kusukumwa anasukumwa anafanya kazi anayetaka kubembelezwa anabembelezwa anafanya kazi. Hapa Afrika mambo yote mawili yafanye kazi. Rais wetu anataka kazi. Ukipewa jukumu lifanye kwa nguvu zote ndiyo tunaweza kutoka hapa tulipo kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye digital economy. China wamegundua kwamba, manufacturing imeanza ku-decline, imeanza kushuka, ndiyo maana wakaamua sasa tuwekeze kwenye digital economy, uchumi wa kidigitali, ndio maana wanakimbia kwenye mambo ya 5G tunayaona. Sasa hivi duniani hapa China inaongoza katika mambo ya digital, kwa nini alifanya hivyo? Wanataka ku-cover lile gap ambalo litatokea manufacturing itakapo- fail.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hakuna ubaya kwa sisi kujikita kwenye kutengeneza viwanda, ni sawa kabisa, lakini hebu tuelekezeni na akili yetu upande wa pili kwenye digital economy. Kwa nini tunaacha nchi jirani hapa zinajivuna kama zenyewe ndiyo Silicon Valley ya East Africa? Tuna vijana wana akili hapa Tanzania sijawahi kuona. Wanagundua vitu vingi, lakini hawana mtaji hawa watoto, wanatoka UDOM hapo; wamejifunza mambo makubwa kabisa ya kuleta solution kwa changamoto tulizonazo lakini hawana capital na hawawezi wakaenda benki leo na idea akapewa mkopo, haiwezekani, benki zetu sio rafiki wa masikini. Sasa kama tunaweza kukopesha fedha kwa kijiji milioni 50, kama tunaweza kupeleka pesa kwenye halmashauri kuna shida gani hawa vijana wetu wakapewa guarantee ndogo tu kwa benki kwamba, you have the best idea, sisi tutaku-sponsor wewe utengeneze application yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest, mimi nina run media company. Pale kwetu tuna online radio, tulihangaika sana tulipopata kazi ya kuweka redio kwenye mabasi ya mwendokasi pale Dar-Es-Salaam, tulikosa technology. Tukapata South African partner halafu akajitoa, tukabaki tumekwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huwezi ukaamini waliotupa solution hiyo ni vijana wamemaliza UDOM hapa? Vijana wale wametengeneza king’amuzi cha kwao ambacho kinanasa matangazo kutoka ofisini kwetu mpaka kwenye mabasi yote ya mwendokasi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Watanzania let us trust our children, tuwaamini na tuwawezeshe watoto wetu.

MWENYEKITI: Ahsante sana ni kengele ya pili.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekit, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nasimama hapa jioni hii ya leo kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa msiba mkubwa ambao umelipata Taifa letu. Natoa pole kwako wewe mwenyewe Naibu Spika na Spika wa Bunge letu. Natoa pole kwa Wabunge na Watanzania wote kwa msiba huu uliotupata. Ni msiba mkubwa ambao kwa kweli umetutikisa, lakini nashukuru kwamba tunaendelea vizuri kama Taifa. Ni jambo la kumshukuru Mungu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya Ijumaa tarehe 26 nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu kutoka Australia. Alinipigia simu kutoka Australia akiniambia kwamba, ameshuhudia bendera katika taifa lile zikipepea nusu mlingoti. Nilifurahi sana moyoni mwangu nilipojua kwamba bendera ile ilikuwa inapepea nusu mlingoti kwa sababu ya rais wangu Hayati John Pombe Magufuli. Ni jambo la kujivunia sana na kwa kweli sio jambo dogo kijana kutoka Chato kufanya bendera za dunia hii zipepee nusu mlingoti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kama raia wa nchi hii ambaye nina kila sababu ya kujivuna kuwa na kiongozi kama Mheshimiwa Magufuli ambaye alijitoa sadaka, alijitoa uhai wake, alijitoa nafsi yake kwa ajili ya Watanzania masikini wa nchi hii. Amefanya mambo mengi ambayo siwezi kuyataja yote, wote mnayafahamu. Ameuthibitishia ulimwengu ya kwamba Tanzania inaweza kuendesha mambo yake bila kumtegemea mzungu. Tanzania inaweza kujenga reli yake yenyewe bila kutegemea mkopo. Tanzania inaweza kujenga bwawa la umeme bila kutegemea msaada wa mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jambo kubwa. Kwa miaka mingi sana tumeishi tukiamini ya kwamba sisi ni watu masikini, hatuwezi kufanya lolote bila msaada wa mzungu, lakini Mheshimiwa John Pombe Magufuli amezunguka nchi hii akiwaambia Watanzania nchi hii ni tajiri. Nimesimama hapa leo napeleka ujumbe kwa dunia nzima wapate kuelewa ya kwamba, mimi Erick Shigongo sitoki Taifa masikini, ninatoka Taifa tajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilifika mahali anakuja mzungu hapa mbeba mizigo tu kule, lakini ukimuona unaona kwamba ni msaada. Sisi Watanzania, sisi waafrika, tunao uwezo wa kujiletea mabadiliko wenyewe bila kumtegemea mzungu wala mtu mwingine yeyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inakwenda kwa kasi. Nchi yetu leo iko kwenye uchumi wa kati. Ni kweli, ziko nchi zilizoingia uchumi wa kati, lakini baadaye zikarudi nyuma kuwa masikini tena. Kama Watanzania tunapaswa kujituma, kuteseka, kutimiza ndoto za Rais wetu, Hayati John Pombe Magufuli, ambaye ametangulia mbele za haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufikiria kwa dakika moja, wakati Mheshimiwa anatuacha alikuwa anafikiria nini akilini mwake. Najua alikuwa anafikiria angetamani kuona Daraja la Busisi magari yanapita, angetamani kuona treni inapita pale TAZARA, treni inaenda kwa kasi kwenda Morogoro, hayo yote hayakutokea. Mahali fulani naamini ya kwamba, alikuwa ana disappointment kwa sababu ameondoka mapema. Kazi yetu sisi tuliobaki ni kumpa furaha Rais wetu, ni kumpa furaha Hayati Magufuli huko aliko kwa kuyatimiza haya mambo aliyokuwa ameyaanzisha, na inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, azimio la pili ni la Mheshimiwa Rais Suluhu Hassan ambaye, kwa kweli nataka nikuhakikishie moyoni mwangu sina hofu hata kidogo wala sina wasiwasi. Matumaini yangu ni makubwa sana leo kwa sababu naamini uwezo wa mwanamke. Wanawake wana uwezo mkubwa sana, wanaume naomba tukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanasayansi walifanya utafiti katika Chuo Kikuu cha Havard wakagundua ya kwamba, mwanamke ana-emotional intelligence kubwa kuliko mwanaume, na ndiyo maana anaweza kufanya kazi tano kwa wakati mmoja, mwanaume ukipewa kazi moja unateseka. Kama hiyo ni kweli nina uhakika nchi yangu iko katika mikono salama, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atalivusha Taifa hili mpaka kwenye uchumi wa juu kabisa badala ya uchumi wa kati. Tumempata na Makamu wa Rais mtaratibu, mnyenyekevu, wote hapa tumetoa kura asilimia 100. Huyu mtu atamsaidia Rais wetu kutumiza ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisiongee mambo mengi. Nataka niwaombe wote pamoja tumuunge mkono Rais wetu kuipeleka nchi yetu mahali inapotakiwa kwenda. Ahsanteni kwa kunisikiliza, naunga mkono hoja. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili kuzungumza suala la marekebisho haya ya sheria.

Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani nyingi sana kwa Kamati kwa kutambua jambo ambalo nilizungumza wakati wa bajeti ya Wizara ya Elimu, suala la RPL (Recognition of Prior Learning) nimelikuta na limejadiliwa. Napongeza sana Kamati nzima, Mwenyekiti na Wajumbe wote kwa kutambua jambo hili. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri dada yangu Ndalichako hatimaye kuona kuna umuhimu wa kuanza kuliona jambo la RPL kama ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sina mambo mengi sana ya kusema zaidi ya pongezi hizo. Isipokuwa, ukienda kwenye ukurasa wa 12 pameandikwa amendment of Section 2(31) naomba niisome, inasema “The principal Act is amended in Section 2 by inserting in their appropriate alphabetical order the following new definitions. Recognition of Prior learning means the process of evaluating skills and knowledge acquired outside the classroom for the purpose of recognizing competence against a given set of standards, competence or learning outcome”.

Mheshimiwa Spika, jambo hili nililizungumza wakati ule, wakati wa bajeti na nakumbuka kama nilishikilia shilingi ya Mheshimiwa Waziri. Wako watu katika Taifa hili ambao aidha kwa vipaji au kwa practical experience wameweza kufanya mambo makubwa sana. Nitatoa mfano wa mtu mmoja kule Iringa alifanikiwa kuzalisha umeme na kusambaza kwenye kijiji chake bila elimu formal, bila kupita darasani. Nakumbuka aliitwa Ikulu wakati ule na Hayati na kuzawadiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini nitoe mfano wa mtoto mmoja hapa wa kidato cha nne ambaye ametengeneza bulb yake ambayo ameweza kuiamuru kwa maneno ikazima au kuwaka. Hapa ndani ya Bunge lako tukufu wako watu ambao wanaweza kukutajia mpaka mifano, hawana hiyo elimu kubwa lakini wanafanya mambo makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Mheshimiwa Kibajaji kwa uwezo wake wa ku-present mada hapa Bungeni angeweza kusomea public speaking na akatambuliwa na akasoma na akapata shahada kabisa ya mawasiliano ya Umma bila shida yoyote kwa uwezo tu wa kuzungumza alionao.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jumanne Kishimba kwa namna alivyofanya toka zero mpaka ku-own companies na elimu yake ya darasa la saba angeweza kabisa kwa utaratibu huu kuruhusiwa kusoma hata business administration.

Mheshimiwa Spika, wewe ni Mgogo unamkumbuka Ukwe Zawose. Ukwe Zawose alikuwa ni kipofu mtaalam wa kupiga ngoma lakini alikwenda Finland akapiga ngoma kwenye chuo kikuu kimoja kwa sababu ya utaalam wake wa kupiga ngoma wakamu-award PHD. Kwa hiyo, ninapoona mambo haya yanaanza kutambuliwa naanza kuona sasa tunaanza kuelekea mahali pazuri kielimu kwenye Taifa langu. Nataka nchi yangu isifunge ilango kwa watu ambao hawakupita kwenye formal education kuweza kupata elimu ya juu. Hiyo ndiyo hoja yangu na hilo ndiyo jambo ambalo nimeliongelea sana kwamba ninapozungumza hapa simaanishi ku-challenge legal framework. Isipokuwa namaanisha kufungua milango kama ulivyofunguliwa kwangu.

Mheshimiwa Spika, ushuhuda wangu sitaki kuurudia tena leo wote mnaufahamu nilishauzungumza Bungeni hapa. Elimu yangu ya darasa la saba kwa kipaji cha kuandika nikapelekwa Chuo Kikuu nikafauli na nikamaliza. Nilipokwenda University of Dar es Salaam ku-apply for masters nikakataliwa kwa sababu sina cheti cha form four. Sasa hii form four hii ndiyo ninayoiongelea leo. Lakini nimeenda Open University nimekuwa accepted, sasa hivi nafanya Masters ya Mass Communication hawajaniuliza cheti cha form four.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kipengele hiki nilichokisoma kimetambua kwamba wako watu wenye elimu ya vitendo lakini hawama elimu formal…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nimalizie kidogo tu. Ukienda kwenye sehemu ya 35 hapa mwisho nilikuwa na mapendekezo ambayo baadaye…

SPIKA: 31…

MHE. ERIC J. SHIGONGO: …31 hapo nilikuwa nasoma lakini ukija 35 amendment Section 24 ukienda hapo kuna kipengele M. Ningependekeza, wameandika hivi “prescribing procedures for recognition of prior learning and…” hapo ningeomba tuongeze kipengele ambacho kinamtaka mtu ambaye ametambuliwa na aidha TCU au NACTE akasome popote pale bila kuuliza cheti cha Form Four. Ndiyo hoja yangu. Naomba kuwasilisha.