Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by hon Hassan Seleman Mtenga (9 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, nianze kutoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais ambaye ni Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa ambazo anazifanya. Pili nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Waziri Mkuu lakini kwa pamoja niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Mtwara Mjini ambao wameniwezesha kufika kwenye Bunge hili kwa mara ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze kwenye maeneo mawili. Kabla sijaanza kuzungumza ni vema nikatoa shukrani kubwa sana, Jimbo la Mtwara Mjini tumepata miradi mingi sana. Tuna mradi wa Hospitali ya Rufaa ambayo itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 122, tuna barabara ya kiwango cha lami ambayo inatoka Mtwara - Masasi na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi nataka tuzungumze kuhusu Mtwara Corridor. Hii Mtwara Corridor inawezekana hatuielewi vizuri na italeta maendeleo gani. Mheshimiwa Rais amewekeza fedha kwenye bandari ya Mtwara takriban shilingi bilioni 157, lengo na madhumuni ni bandari ya Mtwara iweze kufanya kazi na ilete tija kwenye uchumi wa taifa. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais ameamua kutengeneza barabara ya kutoka Mtwara - Newala ambapo itakuwa ni kiunganisho kikubwa sana kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu umefanyika juu ya reli ya kutoka Mtwara hadi Mbambabay. Kama upembuzi yakinifu umefanyika na tunapozungumza upembuzi yakinifu ni kwamba tayari mamilioni ya shilingi yametumika kwenye kuangalia dhana nzima ya awali. Niishauri Serikali muda sasa umefika wa kutoa maamuzi ambayo yako sahihi ya kuanza kuijenga reli hii ambayo itaweza kutuletea uchumi kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia uchumi wa nchi, yako mambo matatu tunatakiwa tuyaangalie. Tunazungumzia barabara ambayo ni kiunganisho, viwanda ambacho ndiyo kiunganisho namba moja lakini lazima tuwe na watu kama hatutakuwa na watu hatutakuwa na mashamba na hatutakuwa walimaji. Kama hakuna barabara ambazo ziko sahihi hatutaweza kupitisha mazao yetu kwenye barabara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu niiombe tena Serikali, tuna barabara ya kutoka Mtwara - Dar es Salaam, kwa muda mrefu sasa imekuwa inafanyiwa service za mara kwa mara na kutengeneza barabara ya lami kilometa moja inatugharimu fedha nyingi sana. Barabara hii imekuwa inaharibika mara kwa mara kwa sababu malori yanayopita ni makubwa na yenye uzito mkubwa. Tuna kiwanda cha Dangote, cement yote zinasafirishwa kwa njia ya gari. Tuna zao la korosho ambapo zote zinasafirishwa kwa njia ya barabara. Tumejenga bandari na tumewekeza pale shilingi milioni 157 ni kitu gani kinashindikana bandari ya Mtwara isifanye kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la elimu ni vema nikampongeza sana Mheshimiwa Rais. Tunapozungumzia elimu bure kwenye shule za msingi na sekondari suala hili limeleta chachu kubwa kwa wananchi kwa ujumla wake. Hata hivyo, ni vema nikasema kuna mgawanyiko katika fedha ambazo tunazipeleka kwenye shule za sekondari na msingi. Mwanafunzi mmoja shule ya msingi anapelekewa Sh.6,000 na mwanafunzi mmoja kwenye shule ya sekondari anapata Sh.10,000…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga

MHE. HASSAN S. MTENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dooh, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Fedha kwa kutuletea Mpango ambao umekaa vizuri sana. Nina mambo ambayo nitayachangia kwenye maeneo zaidi ya matatu hasa tukianza kwenye miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunahitaji tuvuke na tupambane kuondoka kwenye umaskini kuingia kwenye suala zima la kimaendeleo hasa kwenye uchumi mkubwa tunapozungumza miundombinu hasa kwenye maunganisho ya nchi yetu Kusini mwa Tanzania, kule Mtwara, naishukuru sana Serikali kwa kutujengea daraja la Mtambaswala. Nataka nitoe angalizo, daraja hili limetengenezwa kwa gharama kubwa sana, lakini kwenye utengenezaji wake na matumizi ni tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nieleze uhalisia kutoka Mtwara kuelekea Masasi kuna kilometa zaidi ya 230, lakini kutoka Masasi kuelekea kwenye daraja la Mtambaswala kuna kilometa 130 lakini kutoka Mtambaswala kwenda border kuna kilometa 75. Ukitoka border kuelekea Beira Nampura pana kilometa zaidi ya 788. Hoja ni vipi? Ukitoka Mtwara kuelekea Ruvuma pana kilometa 70, kutoka Ruvuma Mpakani unaelekea Msimbwa Naplaya mpaka Nampura unatumia kilometa 445. Kama tungejenga daraja hili kupitia pale Mto Ruvuma tungeweza kufungua mawasiliano kati ya Msumbiji na Tanzania na Afrika Kusini kupitia Msumbiji kuja Tanzania. Sasa hivi wenzetu Afrika Kusini wakitaka kwenda kuuza magari wanapitia Zambia ambapo wanatumia zaidi ya kilometa 2,800 kuja Tanzania. Kwa hiyo nataka niseme hapa hapahitaji watu wenye degree wala maprofesa, ni suala la uamuzi sasa kwa Waziri mwenye dhamana alishughulikie hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nataka nimpongeze mdogo wangu Mheshimiwa Bashe. Mimi nasema Bashe ana akili kubwa sana. Pia nataka nishauri, kule kwetu Mtwara liko eneo moja linaitwa Kitele. Toka nazaliwa napata umri mpaka leo naingia uzeeni, liko eneo linamwaga maji chemchem, maji ya kutosha sana na eneo lile wakazi wa pale wanalima mpunga. Kwa kuwa mpunga ule unalimwa tofauti na viwango, hatuna scheme za umwagiliaji mpunga ule ni mzuri sana, lakini haukidhi mahitaji ya kibiashara. Sasa naiomba Wizara yenye dhamana, twende pale wakaangalie wajiwekeze ili tuweze sasa kuleta kilimo cha kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango nimeangalia kwenye suala la elimu. Kwanza niipongeze Serikali, imeweza kuwekeza kwenye mfumo wa elimu bila malipo tukisema elimu bure, hongera sana kwa Serikali yetu. Hata hivyo, bado kuna tatizo, shule za msingi katika kila pato la kichwa cha mwanafunzi tunapeleka shilingi 6,000, lakini kwenye shule za sekondari kila kichwa cha mwanafunzi tunapeleka shilingi 10,000, lakini fedha hizo tayari Wizara zinapeleka kukiwa na mgawanyiko wa matumizi. Utawala wana asilimia 10 kwenye fedha hiyo, michezo kuna asilimia 20 inagawanyika kwenye fedha hiyo, mitihani kuna asilimia 20 kwenye fedha hiyo, ukarabati kuna asilimia 20 kwenye fedha hiyo, vifaa kuna asilimia 30 kwenye fedha hiyo. Niombe fedha hii ni ndogo mno na fedha hii inasababisha sasa hivi Walimu wetu kufanya njia mbadala ya kuwafaulisha watoto ilimradi tu wasionekane kwamba wao hawana mafunzo kwenye zile shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule nyingi zimekuwa sasa wazazi wakiwa wanachangia, lakini kwenye uchangiaji wazazi wamefika mahali wanagoma. Wanasema Serikali inaleta fedha nyingi sana kwa sababu mnyumbulisho huu wazazi hawauelewi. Kwa hiyo niiombe Wizara yenye dhamana twende tujiwekeze sasa kwenye Sekta hii ya Elimu, kama tumekubali sasa Serikali kubeba mzigo wa elimu bila malipo basi twendeni sasa tuongeze ruzuku hii ambayo inapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nataka niguse kwenye suala la viwanda. Kusini tuna Kiwanda kikubwa sana cha Saruji cha Dangote. Kiwanda hiki kina wafanyakazi zaidi ya 6,000. Kimetoa ajira ya kutosha, lakini kiwanda hiki kinashindwa ku-move kwa sababu ya kodi za TRA. hHpa karibuni mlikuwa mnasikia kwamba Kiwanda cha Dangote kinataka kufungwa, lakini Kiwanda cha Dangote wamefika mahali sasa wamechoka wanataka kuondoka. Kwa mfuko wa saruji mmoja TRA wanachukua shilingi 3,000, mfuko unaouzwa shilingi 11,000 kwa bei ya jumla. Ukienda ndani ya kiwanda kile, maintenance ya kiwanda, mkanda mmoja unavyokatika wa mashine unatumia zaidi ya milioni 180 kuagiza mkanda mmoja wa mashine. Twendeni sasa tuangalie kama tunahitaji kuboresha uchumi huu wa Tanzania lazima tufike mahali sasa viwanda vyetu tuvisaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wawekezaji, kila tunapozungumza, sasa hivi nimeshazungumza na wawekezaji zaidi ya sita kutoka nje (investors) lakini wanasema kwamba Mtenga, hili suala kwenu haliwezekani. Ukitaka kufungua kiwanda, kuwa mwekezaji, shughuli yake ni kubwa mno. Mle kuna watu wapo zaidi ya nane au tisa, ukitaka kiwanda unamkuta NEMC, ukienda hapo NEMC mambo ya NEMC Mwenyezi Mungu mwenyewe anayafahamu. Pia kuna mtu anaitwa TBS, ndani ya kiwanda hicho hicho kimoja. Yuko mtu mmoja anaitwa TRA, lakini kuna janga kubwa la Kitaifa linaitwa NIDA, leo mwekezaji ametoka nje kadi ya NIDA anaipata wapi hapa Tanzania? Hili lazima tuliangalie, lakini kuna mtu anaitwa OSHA, pia mtu mwingine anaitwa Zimamoto. Vile vile Kuna kibali cha kuishi, hili nalo ni shughuli nyingine. Vibali vya kuishi leo kama kuna wawekezaji ambao tayari wana wafanyakazi wao wako wanafanya kazi, kwenda ku-renew kibali tu cha miaka miwili au mwaka mmoja wanachukua takriban zaidi ya miezi nane au tisa. Hebu tufike mahali kama kweli tunahitaji sasa, tufike mahali tubadilike ili tuingie kwenye uchumi mkubwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri hawa OSHA, NIDA na kadhalika kwenye Sekta hii ya Uwekezaji hebu wakae sehemu moja ili shughuli ile iwezekane kupatikana. Yuko hapa mtu mmoja anaitwa Mkurugenzi wa NEMC, yaani afadhali leo unaweza kumtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukampata kuliko Mkurugenzi wa NEMC. Tunakwenda wapi? Leo tunazungumza kwamba nchi yetu tunataka iwe nchi ya uchumi, lakini uchumi wetu tunazungumza viwanda, ni kitu ambacho hakiwezekani. Ukiangalia kwenye viwanda vyetu, wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwenye viwanda hivyo, mishahara yao wanayolipwa ni midogo. Serikali kama Serikali wanasema kuna viwango vya kima cha chini vimepangwa, sasa viwango vinavyopangwa vya kima cha chini tuangalie na kodi tunazowatoza wale watu na service za viwanda vyao wanavyofanya ili tufike mamlaka ya kuwabana wale juu ya mishahara yao ambao inalipwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshamaliza? Loh, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, nami nitangulize kutoa shukrani za dhati kwako kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu kwa kazi nyingi anazozifanya. Niwapongeze na Mawaziri ambao wamepata uteuzi hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie suala la Hifadhi ya Ngorongoro. Hifadhi yetu ya Ngorongoro ilianza rasmi mwaka 1954. Hifadhi hii wakati inaanzishwa kulikuwa na takriban watu kama 8,000. Watu 8,000 kwa wakati huo walikuwa ni wachache sana, lakini leo tunapozungumza hapa Bungeni kuna watu takriban 110,000. Sasa ni nini nataka nizungumze. Kama tunakwenda kuwa na hifadhi ina watu zaidi ya 110,000, hatuwezi kuiita hifadhi kwa kweli, tusidanganyane kwenye Bunge hili. Lakini hii ni rasilimali ya Taifa.

Mheshimiwa Spika,tukiangalia rekodi za mapato ya makusanyo ya fedha wenye Hifadhi yetu ya Ngorongoro; mwaka 2018 tulikusanya bilioni 143.

T A A R I F A

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Simwoni anayeomba taarifa, ni nani!

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, niko hapa.

SPIKA: Nimekuona tayari, Mheshimiwa Jafari Chege.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, sina budi na wala sina namna ya kumwondoa mchangiaji kwenye hoja yake ya msingi, naaka tu nimpe taarifa kwamba nje ya watu zaidi ya 100,000 wanaopatikana pale tunachozungumza ni pamoja na aina ya shughuli zinazofanyika kwenye ile hifadhi ya Ngorongoro. Mojawapo ikiwa ni kwamba miaka hiyo ambayo watu walikuwa ni zaidi ya 8,000 ng’ombe waliokuwa kwenye hifadhi walikadiriwa kuwa 12,000. Leo tunavyozungumza kuna ng’ombe zaidi ya laki moja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka nimpe taarifa ili aende akijua kwamba hayo yote yanafanyika kwenye Hifadhi ya Ngorongoro.

SPIKA: Sasa kabla sijakuuliza Mheshimiwa Mtenga uendelee na mchango wako, nilikuwa najizuia kidogo kusema kanuni zetu, maana nachukua muda wenu kidogo, nilikusudia kuwakumbusha baadaye. Kwa sababu usipomsikiliza Mbunge mwenzako kumaliza hoja yake, huenda hilo jambo, yaani unatakiwa umuingizie taarifa akiwa amemaliza kile anachokisema ili ujue kuwa kuna jambo amelisahau. kwa sababu pungufu ya hapo maana yake wewe unamuingizia taarifa yako, sasa haelewi kama mtiririko wake aendelee nao ama vipi.

Kwa hiyo tuwe wavumilivu kidogo. Leo taarifa zinaruhusiwa kabisa, wala msiwe na wasiwasi, lakini mwache yule mwenye hoja amalize ile hoja, anapokwenda kwenye hoja nyingine unagundua kwamba amesahau hii sasa ngoja nimuongeze, ndilo lengo hasa la hiyo kanuni yetu ya Taarifa.

Mheshimiwa Mtenga.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza niipokee taarifa, lakini nilikuwa nazungumzia mwaka 1820 mapato ya Ngorongoro yalikuwa bilioni 143. Tulipoingia 20…

SPIKA: Samahani, ulikusudia kusema 1820 au 2018.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ni mwaka 2018, Mheshimiwa Chege alinitoa kidogo kwenye mstari.

Mheshimiwa Spika, tulipoingia mwaka 2019 tukakuta tuna fedha ambazo tulizikusanya bilioni 124, lakini 2020 tukakusanya fedha bilioni 31.

Mheshimiwa Spika, sasa naziweka hizi record ili tuone jinsi hifadhi yetu inavyokwenda kuteketea na masuala ya mifugo pamoja na kaya ambazo zipo kwenye hifadhi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwenye hifadhi hii kuna kaya zaidi ya 22, lakini leo tunapotaka kuzungumzia watalii wanaoingia Ngorongoro imekuwa ni hali ya hatari. Watalii wanapoingia Ngorongoro kwanza lazima wakutane na ng’ombe, mbuzi pamoja na kondoo ndipo waingie huko ndani.

Mheshimiwa Spika, kibaya zaidi kuna vitu vinafichwa kwenye Ngorongoro. Leo kuna watu wanauawa na simba, wanazikwa usiku, haya hayazungumzwi. Wanafika mahali kuwazika watu hawa usiku Serikali isije ikaelewa na ikatambua kwamba wananchi wao wanauawa mbugani.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe ushauri na ushauri wangu, pale tunapozungumza kwamba tunataka hifadhi iwepo lazima tufike mahali tukubaliane kwamba hifadhi hii iwepo. Kwa sababu kwa mujibu wa sheria, kama hawa watu walikuwa 8,000, leo wako 110,000, wametokea wapi zaidi ya 102,000? Kwa mkataba upi unaozungumzwa? Lazima vitu hivi tuviangalie.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe angalizo moja. Kwetu kule Mtwara kulikuwa na mradi wa gesi. Mradi ule wa gesi ukazua mambo mengi sana, lakini kwenye Bunge hili ikasemwa kwamba mradi ule ni wa kitaifa na Serikali ikachukua maamuzi na gesi ile ikatoka Mtwara ikaja Kinyerezi – Dar es Salaam na sasa ndiyo imekuwa sehemu ya msaada wa umeme wa gesi ya Mtwara. Hakuna sehemu tulipozungumza kwamba sasa katika hii rasilimali tugawane mbavu, hakuna. Hata hivyo, huku tunapoelekea kwenye suala la Ngorongoro, leo kuna wafugaji wako mle ndani, twendeni kwa wale wafugaji wakaombe mifugo waliyokuwa nayo halafu wataowaona watu walio nyuma ya mifugo ile.

Mheshimiwa Spika, wale waliopo ndani ya Ngorongoro si wenye mifugo yao; na hili lipo, si kwamba ni jambo ambalo tunalizungumza tu hapa. Sasa kama kuna matajiri wako nje, wanafanya kazi wao kugeuka kuwa NGOs na NGOs sasa hivi ziko kule zinaelimisha watu jinsi ya kutohama.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la Ngorongoro tufike mahali kama Bunge tuchukue hatua. Hali ya Ngorongoro ni mbaya. Naishauri Serikali, hizi kaya 22 twendeni tuwatafutie makazi au tuwalipe fidia, hawa watu tuwaondoe kwa utaratibu.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu ambacho kipo ndani ya pazia; leo tunazungumza wenzetu wapo mle ndani, wanafuga; si wao tu, kuna wenzetu wa nchi Jirani wanafanya kila njia Ngorongoro ife na sisi tumejifungia humu Bungeni. Pia wako wenzetu wanatumika. Huko nje kuna matajiri, kwenye hoteli kuna matajiri kutoka Ngorongoro. Lazima tuelezane humu ndani. Wamekuja kufuata nini matajiri? Mbona hatujawaona Wamasai wamekuja na lubega wanasema mimi ndiye mwenye ng’ombe 200? Wanakuja matajiri hapa wanakaa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii inaumiza sana. Nimezungumza kwa uchungu kwa sababu Jimbo langu mimi la Mtwara Mjini ni Jimbo ambalo ni masikini, na ndiyo maana leo ninazungumza kwa ukali sana. Hata tukiangalia kwenye bajeti, mimi nimetoa gesi kuileta huku, kwenye bajeti, tuiangalie Arusha, sisi tunapata sawa na Arusha? Arusha sawa na Mtwara? Si vitu viwili tofauti? Mtwara haiwezi kuingia Arusha hata kwa mara 200 wala kwa mara 100, haiwezi kuingia Arusha, lakini tunapoingia kwenye kutafuta rasilimali ya Taifa, keki tunagawana sawasawa. Kuna haja gani sasa ya wenzetu kuzuia hiyo keki wao wanataka kuihujumu hiyo keki? Hili halikubaliki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale kuna Baraza la Wafugaji. Baraza lile la Wafugaji ndicho chanzo chote mnachoona kwenye mgogoro huu tuliokuwa nao. Ngorongoro wenyewe walikuwa wanawapa hela zaidi ya bilioni tatu kwa mwaka kuendesha shughuli zao. Zile bilioni tatu sasa ndizo zimegeuka kuwa chungu kwa Serikali. Tunapigwa na fedha zile ambazo tulikuwa tunawapa Baraza la Wafugaji.

Mheshimiwa Spika, kanuni sizijui sana, lakini kuna maneno ningesema hapa, naogopa sana unaweza ukanifukuza kutoka nje, ila nikuombe, kama walipeleka Mtwara kule vifaru, ma-bulldozer pamoja na vitu vingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HASSAN S. MTENGA: …kwamba rasilimali ile ya taifa iwe keki ya Taifa, tunaogopa nini? Au kwa sababu kuna matajiri?

Mheshimiwa Spika, ni vyema sasa, kama waling’ata jongoo Mtwara wang’ate hao jongoo na sehemu nyingine. Tukiiacha Ngorongoro kesho tutakwenda Mfinga Iringa, kesho kutwa watahamia Serengeti na mwaka ujao watakuja pale Mbeya; halafu tunakaa humu tunajifungia, tunaona ni vitu vya kawaida tu?

Mheshimiwa Spika, tufike mahali…

SPIKA: Dakika moja, malizia Mheshimiwa.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru sana. Zingekuwa mbili ningekushukuru zaidi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa namna moja au nyingine mgogoro ule hauwezi kwisha kwa mazungumzo kama wanavyodai, kwa sababu wenzetu wanatoka wanakwenda kule wanashawishi watu, leo hii wameshajipanga, wanasema njia zote tu-block, tuanze Maandamano pamoja na vitu vingine.

Sasa hawa ni wenzetu wanafanya vitu hivi. Huo mgogoro wanakwambia wewe uende ukazungumza, ukazungumze na nani? Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza, nimpongeze Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo kwa kweli imesheheni vipaumbele vyote vitakavyokwenda kurekebisha uhalisia wa maendeleo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimekuwa mtumishi wa CCM kwa muda mrefu sana na nimepitia nafasi mbambali mpaka hapa nilipofikia. Hapa niliposimama inawezekana nikazungumza nitakayoyazungumza sitoweza kusahau au sitaweza kumsahau Hayati John Pombe Magufuli. Hata hivyo, siyo tu Hayati Magufuli, tunao viongozi ambao wameondoka wako mbele za haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka wakati Sokoine anafariki takribani zaidi ya miaka ya 10 hakuna impact yoyote ambayo ilikuwa inaonyesha kwamba tumkumbuke kwa matendo yake. Tulikuwa tunasikiliza kwenye asasi mbalimbali wakiwa wanatukumbusha wanasiasa na Serikali jinsi ya kuenzi viongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri Hayati Magufuli amekuwa ni kiongozi bora Barani Afrika na ni kiongozi ambaye Marais wa Afrika walikuwa wanatamani kuiga mifano yake. Sasa ikitupendeza pale Morogoro roundabout twendeni tukaweke picha yake. Kwa legacy ambayo ameiacha Hayati Magufuli na kama Bunge hili kila Mbunge anayesimama anamzungumzia na sisi tufike mahali sasa tuwaonyeshe Watanzania kwamba tunamuunga mkono kwa vigezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze mdogo wangu Mheshimiwa Bashe. Tulipokuja Disemba kuapa nilikaa naye hapa kantini lakini nilimueleza kuhusu zao la korosho na TMX, namshukuru sana amekuwa msikivu na alituelewa watu wa Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema Wabunge wengine wakaijua TMX. Kule kwangu Mtwara zao kubwa la biashara ni korosho. Nilikuwa nasoma kwenye ripoti yao wanasema watakuja kuwa madali lakini udalali wao korosho zetu zitanunuliwa online. Makampuni yote ya korosho ambayo yako Tanzania hususani Mtwara, yana wazawa na matajiri wengine wapo Vietnam, India na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia TMX kufika mahali wao wakala number one, kinachotokea ni nini? Ni kwamba mfanyabiashara aliyeajiriwa yuko Mtwara tayari atakuwa amepoteza ajira kwa sababu korosho zitakuwa zinanunuliwa online. Kampuni ambayo iko India na iko Tanzania na hapa kuna wafanyakazi, kama wako 20 watapunguzwa atabakia mfanyakazi mmoja. Kwa hiyo, niipongeze Serikali kwa kuwa wasikivu na kukubaliana kwamba TMX sasa ifike mahala ikae pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimshukuru Waziri wa Maji. Waziri wa Maji alinitembelea Mtwara kuja kuangalia chujio na nikamueleza shida ya Mtwara siyo chujio ni maji na Serikali ikiweza kutupatia maji ya Mto Ruvuma tatizo la maji litakuwa limekwisha. Pia nikamueleza Waziri wa Maji kwamba mabomba yanayotumika hususani kwenye Jimbo la Mtwara Mjini yalifungwa na mkoloni, ni ya chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata leo kama mtaweka chujio likawa linafanya kazi lakini linapita kwenye bomba ambazo zina kutu. Kwa hiyo, maji yale hayatakuwa na usalama, yataendelea kuwa na ukakasi na chuma. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Maji atusaidie kwenye mpango wake kwa sababu ameshafika mahala amesema kwamba atatutengea fedha na upembuzi yakinifu utafanyika basi hilo naomba alisimamie kwa makini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tumekuwa tunazungumza ajira za vijana, kweli hili ni janga la kitaifa. Sisi Wabunge wa Mkoa wa Mtwara tuna maeneo mengi sana ya mapori na yanahitaji kufanyiwa kazi kwenye suala la kilimo lakini hatuwezi. Hii ni kutokana na jinsi tulivyowaandaa vijana wetu kwenye familia zetu hawawezi ku-compete na kwenda shamba kulima bila Serikali kuwekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe mfano, leo tunawatibu vijana ambao wanakula madawa ya kulevya kwa gharama kubwa sana lakini tunapeleka asilimia 10 kwa ajili ya vijana, akina mama na walemavu, twende sasa na mpango endelevu, wapo vijana wako tayari kwenda kulima shambani lakini Serikali ichukuwe hatua sasa ya kuwawezesha vijana hawa tuwapeleke mashambani wakalime kilimo cha kisasa ili sasa tuweze kutoa ajira zingine mpya tofauti na zile ambazo tunazungumza.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagongwa.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Kwanza nilikuwa namwangalia hapa Waziri wa Ujenzi, mara nyingi amekuwa anajishika kichwa, anajishika shavu, kwa kweli tunapaswa tumsaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwangu Mtwara tuna barabara ya Mnivata ya kilometa 160; Mnivata - Mtwara mpaka Masasi. Barabara ile kwenye bajeti humu tumetengewa shilingi bilioni tatu. Kwa hali ya kawaida ukipiga mahesabu ya kilometa moja kujenga barabara ya lami, lami standard nadhani ni zaidi ya shilingi bilioni moja na something.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hizi shilingi bilioni tatu tunakwenda kutengenezewa kilometa tatu. Barabara hii sasa ina miaka takribani 10. Katika bajeti zote za miaka 10 tumetengenezewa kilometa 50. Naomba kwamba sasa kuna kila sababu, kwa kuwa barabara hii inaunganisha baadhi ya barabara zinazokwenda kwenye wilaya nyingine, pia ni barabara ya kibiashara. Kwa hiyo, tunakosa kufanya biashara zile za kisasa hasa kwa kutumia barabara hiyo kwa sababu barabara siyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara ya kutoka Mtwara kuelekea Mahurunga; barabara hii hatujaona kwenye bajeti kama imetengewa fedha. Barabara hii toka imeanza kutengenezwa sasa hivi ina kiwango cha lami kilometa ambazo hazizidi sita au saba, takribani ina miaka zaidi ya 15 na iko TANROADS. Naomba barabara hii sasa itengewe fedha za kutosha ili tuweze kupata barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kule inakokwenda ndiyo kwenye mpaka baina ya Msumbiji na Tanzania, lakini kumekuwa kuna matukio mengi ambayo yanatokea, watu wetu, watu wa Idara, watu wa usalama na watu wengine wanashindwa kufika kwa wakati kwenye maeneo hayo, kwa sababu barabara ni mbaya hazipitiki. Tunaomba Serikali mtusaidie kwenye hii barabara. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie barabara ya Kibiti – Lindi – Mtwara. Barabara hii kwa sasa hivi haipitiki, ni barabara ambayo tayari imeharibika, imekufa kutokana na malori ambayo yanabeba ufuta, korosho, na mahindi yanayopelekwa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwako, tunayo Bandari ya Mtwara; bandari hii imetumia shilingi bilioni 157 na fedha zile tumeziwekeza pale ili bandari ile ifanye kazi. Nataka nitoe angalizo, leo kuna makampuni yanayoleta mafuta, Serikali imeelekeza kwenye makampuni yanayoleta mafuta kwamba kwa watu wa mikoa ya kusini, itumike bandari ya Mtwara wa kubeba mafuta. Ni kitu gani kinashindikana sasa tukaelekeza kwamba korosho zote za Mtwara zipitie Bandari ya Mtwara; ufuta wote unaolimwa Lindi na Mtwara upitie Bandari ya Mtwara; na mahindi yote yanayolimwa yapitie bandari ya Mtwara? Kuna nini hapa? Naomba kufanya maintenance kwenye barabara yetu ya lami kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam a lot of shillings tutazitumia pale. Hivyo maintenance hizi tunazozifanya za kila siku kama tungeamua sasa fedha hizi tuzielekeze kwenye ujenzi wa barabara tungekuwa hatulalamiki hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo barabara ya Mtwara – Kibiti – Lindi, kila ukipita barabara ile, kila baada ya miezi miwili unakutana na shida. Mkandarasi yuko barabarani na anatengeneza barabara ile kwa ajili ya service. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nijumuike na wenzangu kumshukuru Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu. Lakini pia nichukue fursa nayo kumshukuru Waziri wa Ulinzi, kwa kweli nina kila sababu ya kuzungumza na Waziri wa Ulinzi jinsi anavyojiweka kwetu, tunavyozungumza naye na ni Waziri ambaye yupo tayari kuzungumza na kila Mbunge mmoja wapo iwe nje au ndani, kwa kweli ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze kwenye masuala ya barabara ya ulinzi. Katika mipaka yetu inawezekana tukazungumza suala la ulinzi kiujumla, lakini suala la ulinzi kama hatujalipa kipaumbele inawezekana majeshi yetu tukawapa kazi kubwa sana kwenye ulinzi. Mfano nataka nizungumzie mpaka wa Mtwara na Msumbiji tuna barabara hapa ya ulinzi ya kilometa 300; unatoka Mtwara hadi Tunduru. Barabara hii kwa hali jinsi ilivyo haiwezi kupitika kwa urahisi iwapo litatokea janga lolote la kitaifa au la uvamizi hawa wanajeshi wetu hawawezi kufika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu nadhani Waziri wa Ulinzi wafanye mazungumzo na Waziri wa Ujenzi barabara ile ya ulinzi ambayo iko madhubuti kabisa kwa ajili ya ulinzi wa mpaka wa kusini iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamezungumza sana kuhusu migogoro ya ardhi, kuhusu makambi ya majeshi yetu; kule kwangu ni sehemu pale Mtwara ni sehemu ya waathirika wa makambi hayo. Ukienda kwenye Kata ya Ufukoni ina watu takribani zaidi ya 12,000 lakini katika kata hiyo watu 12,000 kuna watu zaidi ya 4,000 wana mgogoro na Kambi ya Jeshi, na hili ni lazima nilizungumze kwa sababu kwenye mgogoro ule utawakuta wanajeshi/makamanda wako wana viwanja na wamejenga nyumba za kisasa. Kwa hiyo, rai yangu nataka nizungumze kwamba niombe muda wa bajeti hii ikishaisha tumemaliza hili Bunge ikimpendeza Waziri twende tukatatue mgogoro ule haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima tunaozungumza vijana wetu wa JKT; wenzangu wamezungumza sana, vijana hawa wa JKT tumekuwa tunawapa mafunzo na mafunzo haya wanayopewa ni mafunzo ya kijeshi. Lakini nataka nitoe angalizo kwa Serikali, vijana hawa tunapokwenda kuwapa mafunzo ya kijeshi na baadaye tukaendelea kuwaacha idle nje, iko siku hawa watabadilika sasa kuwa watu wabaya ndani ya Serikali yao. Kwa sababu tayari tumewapa mafunzo, lakini tunashindwa sasa kuwatumia kimafunzo sahihi. Nashauri wenzangu wamezungumza sana kuhusu viwanda, lakini wenzangu wamezungumza kuhusu activity nyingi kuhusu vijana hawa. Kama ikikupendeza na Serikali ikiipendeza naomba vijana hawa sasa waandaliwe shughuli mahususi wanapotoka kwenye mafunzo ya jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la ulinzi tukirudi nyuma kwenye historia ya nchi yetu tumepigana vita kule na Uganda, lakini wakati tunapigana vita na Uganda tulifika mahala tukaathirika kama Watanzania na Jeshi letu. Baada ya daraja letu ambalo tulikuwa tuna daraja pale Kagera halikuwa na uwezo wa kuwa na daraja kama daraja. Haya nayazungumza kwenye historia hii, natoa mfano sasa tunazungumza Mtwara na Msumbiji na nimekuwa nikizungumza sana Bunge hili, lakini nimekuwa naishauri sana Serikali juu ya kujenga daraja baina ya Msumbiji na Mtwara kwa pale ambapo tunasema barabara yetu ya ulinzi ya mpaka ule ndiyo inapoanzia basi twendeni sasa tujenge daraja ili jambo lolote litakalotokea kuwepo na unafuu wa kuweza kuboresha jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendelee kulipongeza Jeshi hili, nalipongeza Jeshi katika nchi zetu za Kiafrika ni jeshi la kwanza ambalo halijayumba na hili lazima tukubaliane kwamba tayari tuna majemedari ambao wamefika mahali wamegeuka kuwa wazalendo ndani ya nchi yao. Lakini ukiangalia kwenye nafasi zao na maudhui jinsi wanavyoishi pale kwangu Mtwara tunazo nyumba za wanajeshi nyumba zile zilijengwa takribani miaka ya 1980.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba zile ukienda kuziona siku ya leo na ukaangalia ukaona kwamba nyumba hizi wanakaa wanajeshi wetu, ni aibu kubwa sana. Niiombe na Serikali twendeni tukazikarabati zile nyumba kwa sababu ufanisi wa jeshi letu, ufanisi wa wafanyakazi wetu lazima wafike mahala wajue yale maudhui wanayoishi kwenye Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nazungumzia wanajeshi kukaa nje ya makambi; mimi nataka niishauri Serikali hawa wenzetu wanafanya mazoezi mazito sana na kwa bahati nzuri asilimia kama 20 ya mazoezi hayo mimi nayafahamu. Lakini wanapojumuika na wananchi ndiyo tunasema hawa ni rafiki sawa na wananchi lakini yako mambo ya msingi ambayo wanajeshi kama wanajeshi kwenye taaluma yao haitakiwi kujichanganya na wananchi. (Makofi)

Sasa hili natoa angalizo kwa Serikali leo tumeona maeneo mengi nasikia jeshi wamempiga mwananchi huko, jeshi wamempiga siyo kwamba wanakusudia kufanya vile kwasababu hawa wanajeshi huwezi kumpeleka jeshi aende akalinde benki siyo kazi yake na siku utakayomchukua mwanajeshi kwenda kulinda benki, inawezekana maudhui ya yeye na mteja yakawa ni mambo mawili tofauti. Kwa sababu siyo kitu ambacho wamesomea au wamejifundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi niiombe Serikali twendeni sasa tuwajengee mazingira ya kuishi kwenye makambi na wale maafisa ambao tunasema maafisa wetu hawakai kwenye makambi wanakaa uraiani, tutengeneze sasa nyumba za kisasa kwa ajili ya kukaa hawa wanajeshi wetu. Suala hili la ujenzi wa nyumba halikuanza jana wala juzi, kwa kumbukumbu zangu kabla sijaingia Bunge hili, lakini mabunge yaliyopita Wabunge wengine walizungumza sana kuhusu ujenzi wa nyumba za wanajeshi. Kwa hiyo na mimi niungane na wenzangu nikuombe Naibu Spika na Serikali kwa ujumla hebu twende sasa tuwaangalie wanajeshi wetu haswa kwenye makazi salama ambayo wanaishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanajeshi wetu wanafanyakazi kubwa sana na kama Serikali itafika mahala tukatenga bajeti leo tunazungumza kuhusu vijana hawa wanaotoka JKT, wanafanya shughuli gani tunawaacha idle, kama tumeweza kupeleka fedha tukatunga sheria, tukasema sasa tunatoa asilimia 10 kwa ajili ya wajasiriamali kwenye manispaa zetu, kwanini Serikali sasa isijiwekeze tukasema sasa tunaamua sasa tutengeneze kiwanda kimoja kikubwa ndani ya nchi yetu tutafute wabia, lakini hawa vijana wetu kwa sababu wengi wanakuwa wataalam kutoka huko jeshini waende wakafanye kazi kwenye viwanda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii rai naitoa kwasababu hawa vijana wako wengi sana na kila muda tunapowachukua kuwapeleka kule Jeshini kwenye mafunzo reaction yake inakuwa kubwa ya ukomavu wale vijana. Lakini kwenye ukomavu wao hatuwajengei sympathy ya kurudi kule kwenye maeneo wakawa wana uwezo wa kujitegemea. Tutengeneza mazingira, kama tumeelemewa basi twende na njia mbadala sasa ya kufika mahali tukasema sasa vijana wetu hawa tunawatafutia activity yoyote ile ambayo inawezekana wakaweza kuishi na kufanya shughuli zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru na niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, na mimi nichukue fursa hii kukushukuru kwa kuweza kuchangia Wizara hii ya Uvuvi na Mifugo, lakini inawezekana Wabunge tukazungumza sana humu ndani, lakini bila kuelewa au kujua kwamba tunakoelekea kwenye Wizara hii ili kuleta tija ni wapi.

Mheshimiwa Spika, tunayo bajeti ya shilingi bilioni 121 bajeti hii kama itaweza kutoka kwa wakati na ikafika kwenye maeneo husika na ikaweza kufanya kazi haya mengine ambayo ni changamoto ndani ya Wizara hii inawezekana yakapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kule kwetu Mtwara tuna bandari lakini tuna bahari kubwa mno na bahari ile takribani ndani ya miaka miwili iliyopita tumeshakamata meli zaidi ya mbili na zile meli ni meli za kigeni zinakuja kuvua kwenye eneo letu. Lakini meli ya kwanza imekamatwa ikiwa ina tani zaidi ya 150,000 za samaki, meli kubwa na samaki hawa wanavuliwa kwenye bahari za kwetu lakini kikubwa zaidi ambacho tunaweza tukapiga kelele tunao wavuvi, wavuvi hawa ni wavuvi ambao tunasema ni wajasiriamali, lakini bado Wizara haijapeleka kuwatambua hawa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa mfano leo tunazungumza kwamba mvuvi anayekwenda kuvua ambaye hana boti ana mtumbwi tu tunamwambia aende akavue mita 50. Mita 50 unazizungumzia pale Nungwi na mita 50 ili aweze kuzama mita 50 lazima awe na mtungi wa gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwangu pale Mtwara hawa wavuvi hakuna aliyeruhusiwa kuingia baharini na mtungi wa gesi. Sasa tukienda Dar es Salaam tunakuta kuna wavuvi ambao wanatumia mitungi ya gesi, sasa sielewi hizi sheria zinafanyaje na tunaangalia wapi watu wanahaki na wapi watu hawana haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna suala la uvuvi wa usiku, leo ukienda Dar es Salaam wako matajiri wakubwa wanavua mchana na matajiri wale wana maboti makubwa na wameruhusiwa, na kazi hii yote anafanya Katibu Mkuu ndiyo mwenye maelekezo ya kuwaelekeza kwamba matajiri waende wakavue mchana, maskini waende wakavue usiku, athari za uvuvi wa usiku kwasababu unapokwenda kuvua usiku, sisi ni watu wa baharini kuna maeneo yanakuwa na miamba, unapokwenda na jahazi au na chombo mwamba huwezi kuujua usiku, lazima ufike mahala uchemke ndiyo utakapojua kwamba hapa ninapoelekea pana mwamba.

Mheshimiwa Spika, Mtwara yenyewe ukizungumza Kilambo, Mtanga Mkuu, Kianga, Mikindani hapa ninapozungumza takribani ya watu zaidi ya 100 wamepotea baharini, wamefariki. Sasa huku tunakokwenda tunakoelekea Wizara yetu bado haiwawezeshi wavuvi wadogo, kinachofanya sasa hivi Wizara bado inakwenda kuwamaliza wavuvi wadogo.

Natoa mfano hawa wanaumoja wao wana asasi zao, lakini leo Katibu Mkuu unashindwa kuwaita viongozi hawa wa wavuvi mkakaa nao mkajadiliana. Lakini ukiangalia kwenye mijadala yao yote, katika paper zao zote ni za kiingereza, wale wamesoma darasa la nne hamna aliyefika hata darasa la saba wale viongozi wote wa uvuvi, wanakwenda kuelewa kitu gani? Lakini mnapitisha mle sheria, kwamba hatuwezi kuvua hapa na ring net. (Makofi)

Mheshimiwa Hayati Magufuli wakati akiwa kwenye Wizara hii alileta hapa waraka na mkakubaliana Bunge zilizopita kwamba ring net iwe sahihi kwenda kuvua sasa leo kwanini nyavu za ring net zinapigwa marufuku na wavuvi wanakamatwa? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Hassan.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niseme nikushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukizungumza suala la michezo ndani ya nchi yetu inawezekana tukazungumza kwa mapana na marefu sana kwa muda mrefu lakini bila kuelewa changamoto tulizokuwa nazo au kupata tija juu ya michezo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nianze kwenye masuala ya mchezo wa mpira. Hatuwezi kuzungumza kwamba tunakwenda kucheza mpira bila kujiandaa, lakini mara nyingi nimekuwa nasilikiza hotuba za viongozi wetu wanatueleza kwamba Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu, lakini haya yote yanakuja kwa sababu hatuna maandalizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la viwanja hatuwezi kulibeza, inawezekana tukawa na academy nyingi za kutosha, lakini kama hatuna msingi wa kutengeneza viwanja vya kutosha, hizi academy zitakwenda kuchaza wapi mipira.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunavyo viwanja vya Chama cha Mapinduzi, viwanja hivi mimi nadhani nimeshiriki wakati niko Hai nilijenga kiwanja pale kikubwa cha mpira na nadhani kiwanja sasa hivi kiwanja kile kinatumika, lakini nilivyofika Iringa niliboresha kiwanja cha Iringa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanja hivi vinahitaji kugharamiwa, lakini ukiangalia mapato yanayopatikana kwenye viwanja vile CCM nadhani inapata kwenye asilimia 20 ya mapato. Lakini tunapoingia sasa kuvikarabati viwanja vile mzigo unabaki kwa Chama cha Mapinduzi. Sasa angalizo langu tuna fedha sisi ambazo zinatoka FIFA kwa ajili ya kuboresha masuala yote ya mpira katika chama chetu cha mpira, lakini tujiangaliea na tuangalie kwamba je fedha hizi zinatumikaje kwenye suala la mpira? Lakini leo tuna vilabu timu nyingi zinakwenda kwenye awamu ya kwanza zikishapanda daraja, awamu ya pili timu zile zinatelemka daraja. Lakini timu hizi zinatelemka daraja kwa sababu tayari hatujafikia malengo ya kuzilea hizi timu kwa mfano mimi ninayo kule timu ya Ndanda, toka inacheza ligi kuu inatoka Mtwara timu ya Ndanda wanasafiri kuja Dar es Salaam lazima ungo utembee, lakini kuna wafadhili ambao wanaifadhili TFF, lakini ukiangalia kwenye kasma za fedha ambazo wanapewa kila klabu kwenda kuendeleza suala zima la mpira hawawezi ku-move kwenye suala zima la mpira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo langu leo Azam wametoa fedha nyingi sana, fedha hizi Mheshimiwa Waziri usipokuwa nazo karibu, hizi fedha zitaishia mikono ya watu, kama kuna fedha za FIFA zinakuja kwetu kwa ajili ya kuboresha mpira na fedha ni nyingi sana inayokuja Tanzania, lakini vilevile tumeshindwa kabisa hata kui-maintain timu yetu ya Taifa tutaweza haya mabilioni ya Shilingi yanayokuja, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli nikuombe kwenye suala hili la mpira kwetu Tanzania kwanza tuangalie kwenye viongozi wa TFF, hawa wanaweza wakatuvusha? Lakini la pili kuangalia mfumo wenyewe wa mpira tunaocheza Tanzania, tunazungumza kuhusu wachezaji wa kigeni, hatuwezi kuwakwepa wachezaji wa kigeni, wachezaji wa kigeni lazima waje na lazima wacheze kwa sababu hatuja waandaa wachezaji wetu humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mchezaji wa Kitanzania akishaingia amecheza Simba, amecheza Yanga na jina lake tayari limeshakuwa kuwa kubwa siku kesho anakwenda kucheza mpira leo anatafutwa yuko baa, kwa namna moja au nyingine wachezaji wetu hili lazima tulizungumze bado hawajajitambua kama mpira ni ajira. Wachezaji wa wenzetu wa kigeni wanakuja kucheza mpira Tanzania kwa sababu wanaelewa mpira ni ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Wizara ijielekeze sasa kwenye kuangalia mazingira yote ya mpira, ukiangalia pale Brazil kuna wachezaji wa zamani, lakini wale wachezaji wote wa zamani wanapomaliza muda wao wa kustaafu wanakuwa kuna chombo mahsusi ambacho kinawaweka kwa ajili ya kuwa makocha. Lakini leo ukiangalia Tanzania timu zote kubwa ukienda Namungo, Simba, Yanga na timu zingine zote kuna makocha ambao si wa zawa ni makocha wa nje, lakini timu za Brazil mnazoziona wanacheza mpira tunaziita samba wale kule kuna wazawa wenyewe ambao kuna chuo pale kinafundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi niombe tujielekeze na sisi sasa kufundisha makocha tunaposema sasa tunataka tusome lazima tuwe na walimu, hatuwezi kuzungumza kwamba tunataka tusome wakati hatuna darasa, walimu tunasema tunakwenda kusoma kusomea mpira, ni kitu ambacho hakiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wamezungumza kuhusu academy, academy hizi zina gharama kubwa sana katika bajeti hii ya Wizara niliyoiangalia sijaona sehemu ambayo Wizara inakwenda kujikita kwenda kuendesha haya madarasa ya chini ya watoto wetu ili waweze kupanda. Leo ukiangalia inawezekana tukamzungumzia Messi amekulia kwenye academy ya Barcelona na amekaa pale na wachezaji kadhaa, amelelewa, amefundishwa mpira toka akiwa na miaka mitano leo hii anaonekana mchezaji mkubwa duniani ambaye analipwa fedha nyingi duniani. Tunashindwa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ni mambo ambayo Mheshimiwa Waziri anatakiwa afanye sasa maamuzi kwamba sasa tunaingia, tutengeneze academy na vijana wetu waweze kucheza mpira. Mimi nina imani sana kubwa mtoto ukimfundisha akiwa mdogo ni mwepesi sana kushika kile kile unachomfundisha, lakini sasa sisi bado hatujajajiwekeza huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamezungumza kuhusu BASATA; kama kuna chombo ambacho kinawezekana baadaye kikaenda kuua mziki wa kitanzania ni BASATA. Hili inawezekana Wabunge tukazungumza hapa na hatuzungumzi kwa mapana na marefu sana, lakini chombo hiki hakipo kwa ajili ya kuwa-accomadate wanamuziki, lakini chombo hiki kipo kimaslahi zaidi na matendo yao wanayoyafanya, yako ambao wanayafanya hata wanamuziki wenyewe, wasanii wenyewe wamekata tamaa na chombo hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwa na chombo yaani leo tunampishi anasema anampikia Mtenga ugali, lakini Mtenga anatoka anakotoka akienda kwenye sahani anasema ugali huu mimi siwezi kula, ni vitu ambavyo haziwezekani. (Makofi)

Kwa hiyo tuangalie Mheshimiwa Waziri afike mahali aiangalie hii BASATA, lakini arudi tena kwa upande wa TFF nenda pale ukaangalie viongozi wako wengine wana miaka 20 pale TFF hawa waliokuwa miaka 20 ndio leadership, wale wanapanga viongozi, wanajua mambo yakufanya, wanajua deal ziende wapi. lakini wanajua mpira wao wanataka kuuendesha kwa namna gani, hatuwezi kumove kwa viongozi wale ambao ni watendaji pale TFF hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa tunajidanganya, hivyo leo kama tuna premier league tuna timu zaidi ya 12 au 14, lakini timu hizi kama tungekuwa tuna watu wenye uwezo wa kufikiri tungefika mahali tukasema bwana kila timu kwa mfano kwangu mimi kule tuna timu ya Ndanda pale tuna Dangote; TFF wangekwenda kuzungumza na kampuni ya Dangote, wakafanya makubaliano wakawa mdhamini namba moja, lakini kuna Breweries, sijui Kilimanjaro kuna kampuni gani; vilabu vyote tusifike mahala hapa tukamsifia Mheshimiwa Waziri Mkuu kesho inawezekana Waziri Mkuu inawezekana akasema jamani nguvu zimeniishia za kufanya hii kazi ya mpira nani anamsaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tutengeneza sasa impact ya kujua kwamba tunawatafuta wawekezaji na hili ni suala la kulibeba Serikali sio suala la vilabu hivyi, kwa sababu vilabu vinakotokea mpaka vinapanda madaraja haya wanakwenda hawa kwa kuchangishana fedha zao. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha ahsante sana.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti. Kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini niwashukuru wasaidizi wake kwa ujumla nimshukuru Waziri wa Fedha na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie dakika tano hizi kwa mambo kidogo ya msingi, tunapotaka kuzungumza uchumi wa nchi yetu lazima tujikite kwenye viwanda, lakini tunapotaka kuzungumza uchumi wa nchi yetu lazima tujikite kwenye kilimo, lazima tuwe na watu ambao wana nguvu za kutosha na watu wenye uelewa. Nini maana yake?

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu walizungumza kuhusiana hapa na vijana ambao wapo mtaani wamachinga. Genge hili la wafanyabiashara wadogo wadogo limekuwa ni kubwa mno, lakini bado sijaona kama Serikali ikiwa inajikita kuelekeza wapi iwapeleke hawa watu. Lakini nataka nitoe mfano mmoja, vijana hawa wanapanga biashara barabarani, lakini vijana hawa tayari wanafamilia zao majumbani kwao. Imetokea siku kijana huyu ambaye yupo barabarani ameumwa, kwa hali ya kawaida hawezi kumchukua mkewe aende pale barabarani akapange zile nyanya au akapange zile nguo zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa jambo lingine kwenye wamachinga hao hao kwa hali na mazingira ambayo yapo, hatuwatengenezi hawa vijana kwenda kujitegemea. Kwa sababu, kwanza hawana insurance hawakopesheki kwenye mabenki vijana hawa. Sasa, rai yangu tunayo maeneo sisi ya kutosha, maeneo haya Serikali sasa ifike mahali itambue kwamba, inaweza ikawajengea maeneo ya kisasa. Kwanza, faida yake baada ya kuwajengea maeneo ya kisasa tutaweza kupata kodi, vilevile kwenye fursa sasa ya kuwajenga vijana wetu kutoka kwenye umachinga kwenye wafanyabiashara wakubwa. Nina imani kubwa sana hata Mheshimiwa Shigongo ametokea kwenye umachinga, lakini leo amekuwa mfanyabiashara mkubwa kwa sababu yeye aliwezeshwa. Ninaiomba Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie masuala ya bandari na uchumi. Masuala ya bandari na uchumi tunazo bandari katika nchi yetu, lakini napenda sana niizungumzie bandari ya Dar es Salaam, niizungumzie bandari ya Mtwara. Ukiangalia bandari ya Dar es Salaam kwa shughuli zinazofanyika kila siku, bandari ile inaonekana kwamba iko tight. Lakini kwa nini tusifike pahali tukapanua wigo tunayo bandari ya Mtwara tunayo bandari ya Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukienda pale Dar es Salaam tunakuta zaidi ya meli 20 au 30 ziko hangar zinasubiri kupakua pale mzigo, lakini bado tunawapelekea kupata hasara kubwa jinsi meli inavyokaa kule hangar inasubiri iingie pale. Kuna service charge ambazo zinaingia kutokana na gharama za watu ambao wamekodi meli zile. Rai yangu, tutumie bandari sasa ambazo tayari zina uwezo wa kubeba hizo meli kubwa ili tupate fursa zingine za kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nizungumze Mheshimiwa Naibu Waziri leo hii tunaishukuru sana Serikali yetu, kwa kweli mimi kwangu pale Mtwara haya mafuriko yaliyotokea hali ilikuwa ni mbaya sana. Nilivyoambiwa ninapewa milioni 500, kwanza nilisali na nikasema eeeh Mama nakushukuru sana na Serikali yako. Haijawahi kutokea katika nchi yetu kwamba, Serikali imeamua kutoa package moja kwenye mzunguko mmoja kwa Majimbo yote. Kwamba leo mnapata milioni 500 kila Jimbo, kwa ajili ya matengenezo ya barabara zetu. Hongera sana Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunazungumzia zao letu la korosho la Mtwara, tulikuwa tuna Mfuko wa Export Levy. Mfuko ule ambao Serikali iliuchukua lakini mpaka leo hii kila tunapozungumza Wabunge wa Mtwara kuzungumzia juu ya fedha zetu za export levy bado hatujapata muafaka na hatujaambiwa nini kinaendelea. Rai yangu kwako Mfuko huu ndio ulikuwa unazalisha korosho kwa asilimia kubwa. Kwa sababu, ulikuwa una uwezo wa kuwenda kununua pembejeo, kwenda kuwasaidia wakulima na wakulima walikuwa hawana shida ya pembejeo kwa sababu tayari walikuwa wana mtaji wao, niiombe Serikali, nina imani Serikali yetu ni sikivu sana na inaweza kutusaidia, mfuko huu tunaomba urejeshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niishukuru Serikali, niishukuru Serikali kwa mpango ambao umeletwa wa NLG tunakwenda kujenga viwanda Lindi. Viwanda hivi ambavyo vinakwenda kujengwa Lindi, mimi niiombe tena Serikali gesi inatoka Mtwara na kama gesi inatoka Mtwara, basi kwenye Wizara ya Uwekezaji muda sasa umefika wa kuiangalia Mtwara kama Mtwara, iwe nayo ni zone ya kimaendeleo. Kwa sababu haiwezekani kwamba gesi iko Mtwara, lakini Mtwara hatuwajibiki kwenye masuala mazima ya gesi. Nilikuwa naomba, nimuombe Waziri wa Uwekezaji kwamba, hili ni jukumu lake na ana mamlaka makubwa sana ya kuweza kutusaidia wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)