Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Issa Ally Mchungahela (12 total)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA Aliuliza:-

Mradi wa maji wa Chipingo uliopo katika Jimbo la Lulindi ambao umegharimu Shilingi Bilioni 3.9 ni wa muda mrefu tangu mwaka 2013, lakini umekuwa hauna tija kwa kuwa hautoi maji; mabomba kupasuka mara kwa mara na mpaka sasa bado haujakabidhiwa kwa Serikali:-

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Chipingo upo katika Jimbo la Lulindi, Wilaya ya Masasi. Mradi huu ulianza kujengwa Aprili, 2013 na ni miongoni mwa miradi ambayo haikukamilika kwa wakati kulingana na mkataba. Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya jitihada za kukamilisha mradi huu na hivi sasa mradi huo unatoa maji na upo katika hatua za majaribio ambapo vijiji 6 kati ya 8 ambavyo ni Manyuli, Chipingo, Mnavira, Chikolopora, Namnyonyo na Mkaliwala vinanufaika.

Mheshimiwa Spika, Vijiji viwili vya Rahaleo na Mapiri vya mradi huo bado havijaanza kupata huduma ya maji ambapo ujenzi wa mtandao wa maji kwa ajili ya vijiji hivyo unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi, 2021.

Aidha, kuhusu suala la upasukaji wa mabomba katika kipande cha bomba kuu chenye urefu wa kilomita 1.2, Serikali inaendelea kusimamia maboresho yanayofanywa na mkandarasi kipindi hiki cha majaribio ya mradi ili wananchi waweze kupata huduma ya maji kama ilivyokusudiwa. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 90.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya mpakani kutoka Mtawanya kwenda Nanyumbu kupitia Mpilipili – Mapili –Chikoropola – Lichele – Lupaso hadi Lipumburu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mpilipili – Mapili –Chikoropora – Lichele – Lupaso hadi Lipumburu ni sehemu ya barabara ya ulinzi ya Mtwara – Madimba – Tangazo –Mahurunga – Kitaya – Namikupa hadi Mitemaupinde yenye urefu wa kilometa 365.5. Sehemu ya barabara hii yenye urefu wa kilometa 258.0 imeshafunguliwa na inaendelea kufanyiwa matengenezo ya kila mwaka na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Aidha, Serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuendelea kuifungua barabara hii kwa sehemu iliyobaki yenye urefu wa kilometa 107.3.

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) unaendelea kuiboresha barabara hii kwa kuhakikisha inapitika majira yote ya mwaka ambapo jumla ya kilometa 10.8 zimejengwa kwa kiwango cha lami katika maeneo korofi ya milima ya Mtawanya, Kilimahewa, Mdenganamadi, Mnongodi na Dinyeke. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza:-

(a) Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi wanaodai miche ya mikorosho deni ambalo ni la muda mrefu tangu mwaka 2017?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela Mbunge wa jimbo la Lulindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka 2017/ 2018 Serikali kupitia Bodi ya Korosho iliingia mikataba na wazalisahji wa miche 678 ili kuzalisha miche 13,661,433 ya korosho yenye thamani ya shilingi 5,317,107,679. Aidha, jumla ya miche 12,298,000 sawa na asilimia 92 imesambazwa kwa wakulima katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani, Tanga, Singida, Tabora, Dodoma, Kilimanjaro, Morogoro, Njombe, Mbeya, Iringa na Songwe.

Mheshimiwa Spika, malipo kwa wazalishaji hao yamechelewa kutokana na zoezi la uhakiki kuchukua muda ili kujiridhisha kabla ya kufanya malipo hayo. Kutokana na uhakiki uliofanywa katika awamu ya kwanza na timu ya wataalamu kutoka Serikalini jumla wazalishaji miche 382 waliozalisha miche milioni tano yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 wameshalipwa.

Aidha, kupitia uhakiki wa awamu ya pili uliofanyika mwezi Agosti hadi Oktoba 2020, ulibaini kuwa jumla ya miche milioni 5.8 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.660 ilihakikiwa na bado kulipwa. Aidha, Serikali inakamilisha utaratibu wa malipo kwa wazalishaji hao wa miche na watalipwa.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka Kituo cha Uhamiaji katika eneo la Chipingo ili kuondokana na vivuko bubu vilivyopo Mpakani mwa Tanzania na Msumbiji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Chipingo ni kipenyo kilichopo Wilaya ya Masasi katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji kandokando ya Mto Ruvuma umbali wa Kilomita 86 kutoka Masasi Mjini. Kwa upande wa Msumbiji hakuna ofisi za Uhamiaji wala huduma za Uhamiaji bali kuna walinzi wa mpaka wa nchi hiyo.

Mheshimiwa Spika, ufunguaji wa vituo vya mipakani hutegemea makubaliano baina ya nchi zinazochangia mpaka. Kwa upande wa mpaka wa Tanzania na Msumbiji, kumebaki kituo kimoja cha mpakani kinachofanya kazi cha Mtambaswala kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ghasia na hali tete ya usalama.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelezo hayo, Serikali inaendelea kufuatilia hali ya usalama katika mpaka huo na hali itakapotengemaa mawasiliano na Msumbiji yatafanyika ili kufungua vituo zaidi kuhudumia wananchi wanaotumia mpaka huo. Ninakushukuru.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, ni lini Vituo vya Afya vya Nagaga na Mnavira vitakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliipatia Halmashauri ya Masasi shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nagaga ambapo ujenzi umekamilika na huduma zimeanza kutolewa.

Mheshimiwa Spika, aidha, Halmashauri ya Masasi katika mwaka wa fedha 2021/2022, imetenga shilingi milioni 23 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nguzo na paa kwenye njia za watembea kwa miguu (walkways).

Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2009 hadi 2018 kiasi cha Shilingi milioni 110 kilitumika kwa ajili ya ukamilishaji wa boma la OPD la zahanati ya Mnavira. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 68 zilitolewa na Serikali na shilingi milioni 42 nguvu za wananchi. Ujenzi wa jengo hilo la Zahanati ya Mnavira umekamilika na huduma zinaendelea kutolewa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, shilingi milioni 500 zimepelekwa Halmashauri ya Masasi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Chikoropola na Chikundi ambapo ujenzi wa vituo hivi unaendelea. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha uwekezaji wa miradi 294 yenye thamani ya dola bilioni 8.04 inatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa uwekezaji wa miradi 294 yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 8.04 inatekelezwa, Serikali imeendelea kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yanaendelea kuboreshwa ili kurahisisha utekelezaji na kuvutia mitaji zaidi. Aidha, kuimarisha Kituo cha Huduma ya Mahala pamoja, kutoa huduma za mahala pamoja kwa njia ya kieletroniki lakini pia kuendelea kuwahudumia wawekezaji baada ya kukamilisha uwekezaji. Nakushukuru.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -
Je, nini kinakwamisha ujenzi wa barabara ya Mnivata – Masasi kupitia Tandahimba na Newala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepata mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara kutoka Mnivata hadi Masasi yenye urefu wa kilometa 160. Zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii zilitangazwa mwezi Julai, 2022 na kufunguliwa tarehe 18 Oktoba, 2022 na kwa sasa uchambuzi wa zabuni unaendelea. Aidha, Serikali imetoa jumla ya Shilingi bilioni 3.086 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi watakao athirika na ujenzi huo, na zoezi la kulipa wananchi hao fidia linaendelea. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwa na Chuo cha VETA katika kila Jimbo ili kuwakomboa vijana na tatizo la ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, azma ya Serikali ni kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe ambao hauna chuo cha ngazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, Serikali inaendelea kutekeleza azma hiyo na ikishakamilisha ujenzi wa VETA katika kila Wilaya itaangalia uwezekano wa kuanza kujenga vyuo hivyo katika Majimbo kulingana na uhitaji na upatikanaji wa fedha. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, lini Serikali itamaliza tatizo la umeme Mkoani Mtwara hususani Wilaya ya Masasi na Jimbo la Lulindi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Masasi inapata umeme kutoka katika Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi cha Mtwara chenye uwezo wa megawati 30.4 na pia umeme wa Gridi ya Taifa kupitia njia ya msongo wa kilovoti 33 kutokea Songea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya umeme Mkoani Mtwara, Wilayani Masasi ikiwemo Jimbo la Lulindi inatokana na Umeme mdogo usiotosheleza (low voltage) kwenye baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo kwa sababu ya umeme kusafiri umbali mrefu, uchakavu wa miundombinu hasa nguzo na vikombe pamoja na uharibifu kwenye miundombinu ya njia ya msongo wa kilovoti 132 unaotokana na watoto kupiga manati vikombe katika baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa tatizo hili Serikali kupitia TANESCO imetenga shilingi bilioni mbili ili kujenga njia ya kutoka Nanganga hadi Masasi. Aidha, ufungaji wa Auto Voltage Regulator (AVR) mpya yenye ukubwa wa MVA 20 kati ya Tunduru na Namtumbo unaendelea ili kuwezesha umeme wa kutosha kutoka Ruvuma kufika Masasi na maeneo ya jirani. Pia, kwa kutumia Shilingi Milioni 600 Serikali inaendelea kubadili vikombe vilivyopasuka na kuweka vya plastiki na nguzo za miti zilizooza zinabadilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwa na ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme katika Mkoa wa Mtwara, Serikali imepanga kuunganisha Mkoa wote na Gridi ya Taifa kupitia miradi miwili ya Gridi Imara ambayo ipo katika hatua za utekelezaji. Miradi hii ni ujenzi wa njia kuu ya umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru na kutoka Tunduru hadi Masasi. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawasaidia wanawake na vijana wa Kata za Mitesa na Nanjota wanaojihusisha na uchimbaji madini Lulindi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mtwara umebarikiwa kuwa na madini mbalimbali yakiwemo madini ya ujenzi ambayo huchimbwa zaidi na wananchi hasa wanawake na vijana. Aidha, Tume ya Madini imetoa leseni za uchimbaji madini ya ujenzi na chumvi kwa vikundi 11 vya wanawake na vijana. Vikundi hivyo ni pamoja na Mtazamo Group, Wazawa Group, Mwambani Group, Wasikivu, Songambele Group, Tusaidiane, Nguvu Kazi Youth Group katika Halmashauri ya Mji wa Masasi na Kikundi cha Kiumante kilichopo katika Manispaa ya Mtwara – Mikindani; Vikundi vya Makonde Salt Group, Mapinduzi na Umoja wa Vijana vilivyopo katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuwasaidia wanawake na vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini katika Kata za Mitesa na Nanjota, tunawashauri Wanawake na Vijana wajiunge kwenye vikundi na kusajiliwa katika Halmashauri husika. Kufanya hivyo itakuwa rahisi kuwahudumia na kuwasaidia kupatiwa leseni za uchimbaji na mikopo kutoka Halmashauri husika na hata mabenki.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kujiunga katika vikundi ili kuweza kupatiwa huduma kwa ufanisi na kwa haraka zaidi.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza:-

Je, baada ya kuporomoka kwa bei ya korosho katika msimu wa 2022/2023 Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha hali hiyo haijirudii?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya korosho Nchini hutegemea mwenendo wa bei katika Soko la Dunia. Mabadiliko ya mwenendo wa bei katika masoko hayo huchochewa na kiasi cha korosho kinachozalishwa Duniani na mahitaji kwa wakati husika. Kwa wastani katika msimu wa mwaka 2022/2023 bei ilishuka kutoka shilingi 2,150 hadi shilingi 1,850 kwa kilo kwa korosho daraja la kwanza na shilingi 1,595 hadi shilingi 1,332 kwa korosho daraja la pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea na jitihada za kuimarisha bei ya korosho nchini kwa kufufua viwanda vya kubangua korosho pamoja na kuanzisha viwanda vipya. Vilevile, Serikali itaanzisha kongani la viwanda vya kubangua korosho ili kuongeza thamani ya korosho na kuuza moja kwa moja katika nchi walaji badala ya kuuza korosho ghafi.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza:-

Je, fedha za Mfuko wa Jimbo zinaweza kutumika kununulia samani za Ofisi ya Jimbo? Na kama jibu ni hapana, samani hizi zinapaswa kununuliwa na nani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela mbunge wa Jimbo wa Lulindi kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo ulianzishwa kwa Sheria Na.16 ya mwaka 2009. Fedha za Mfuko wa Jimbo ni mahususi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kijamii iliyoanzishwa na wananchi wa Jimbo husika.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri zilielekezwa kuwapatia Wabunge Ofisi kwa ajili ya shughuli zao ikiwa ni pamoja na samani kulinganaa na uwezo wao wa ukusanyaji mapato yao ya ndani. Nachukua fursa hii kuwasihi Wakurugenzi wa Halmashauri kushirikiana na Wabunge katika kutekeleza majukumu yao.