Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Issa Ally Mchungahela (6 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru wewe; lakini pia niishukuru familia yangu; tatu nishukuru wananchi wa Jimbo langu la Lulindi walioniamini; nne nishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini kuwa naweza kufanya hizi kazi kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nataka nizungumzie suala la performance; nataka nijaribu kuweka wazi katika jambo hili. Wakati unapotaka kuchunguza performance ya mtu au kitu, cha msingi sana kinachohitajika kutumika pale sio percentage term, unatakiwa utumie an absolute term, maana yangu ni nini? Ni kwamba ukichukua bilioni moja ukazidisha kwa asilimia 10 unapata milioni 100, lakini ukichukua milioni 100 ukazidisha kwa asilimia 27 au asilimia 30 unapata milioni 30. Kwa hiyo, ukisema kwamba eti kwa sababu umetumia percentage kubwa wewe ume- perform, huo ni upotoshaji mkubwa, kwa hiyo nataka nieleweke hapo kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende katika utendaji wa Serikali. Hakuna hata mtu mmoja ambaye anasema kwa dhati kabisa kwamba, eti Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hakufanya vizuri kwa dhati kutoka rohoni kwake, atakuwa anatania tu. Kiuhalisia yaliyofanywa ni mengi sana, hatuwezi kuyamaliza hata tukisimulia wiki nzima maajabu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kwamba suala la maendeleo ni mtambuka. Tunahitaji kuhusisha vitu vingi na sekta mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza hayo maendeleo. Barabara za Dar-es-Salaam za mwendokasi, ni jambo zuri sana, lakini nashauri barabara hizi zizingatie pia na ukuaji wa miji ile. Nashauri kwamba barabara hizi ikiwezekana zifike hata Mkuranga kwa ajili ya ku-accommodate watu wanaoishi maeneo kama ya Mbagala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mradi wa bandari Mtwara umetumia pesa nyingi sana, takribani shilingi bilioni
157. Naomba mradi huu uunganishwe haraka sana na reli ya Standard Gauge ambayo itafika kwenye miradi mikakati ya Mchuchuma na Liganga. Tusiendelee tu kuongea mdomoni, tufanye kwa vitendo kama kweli tunataka maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mradi huu pia uunganishwe na barabara zote za kimkakati zikiwepo barabara zile za ulinzi. Kwa mfano, barabara inayotoka Mtwara – Mtawanya - Mpilipili – Chikoropola - Nanyumbu. Barabara hii nafikiri ni muhimu sana kwa ku-boost maendeleo ya watu wa Kusini na viwanda vya Kusini, hasa kiwanda cha korosho ambacho nakitegemea mimi kama mmoja wa wahamasishaji kipatikane kule lakini kiwe ni kiwanda kikubwa kabisa cha kushawishi watu wengi sana kuuza pale, kusudi tuweze kupata bei nzuri. Hali ilivyo sasa hivi hatuwezi kupata bei nzuri kwa sababu tunauza raw material. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda EPZ iwe ndio msingi wa maendeleo kwa sababu ndiyo inaweza ikasababisha watu wengine wakawekeza kikamilifu. (Makofi)

(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi, lakini niseme naunga mkono hoja kwa sababu yaliyo ndani ya Mpango ni mazuri. Nakushukuru. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nitangulize pongezi zangu kwa watu wote waliopa bahati ya kuchaguliwa kuwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwenye nafasi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nampongeza pia Mheshimiwa Rais, mama yetu kwa kuonyesha njia ya jinsi tutakavyoelekea Tanzania kwa kipindi hiki japo tulikuwa tunashaka kidogo tukifikiria kwamba itakuwaje baada ya kupata msiba mkubwa tulioupata angalau sasa hivi tunaona kidogo kuna hali tunaweza kuelekea sehemu. Nashukuru kwa hilo na tumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ametuona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, kwanza pia niwapongeze wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi kwa kunichagua nawahakikishia kwamba sitawaangusha hata mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kuangalia jinsi mwenendo mzima wa huu Mpango ulivyokwenda ni mpango mzuri sana ambao kwa muda mrefu sana tulikuwa tukiusubiri mpango wa namna hii. Kwa kweli hakuna shaka juu ya mpango huu, lakini nafikiri kwa namna moja au nyingine najielekeza katika kuchangia baadhi ya mambo katika mpango huu, hususani katika fursa ambazo kwa namna moja au nyingine tunaweza tukazitumia sisi kama Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa kusini kwa mfano, tuna fursa kubwa sana eneo lote la Mkoa wa Mtwara ni eneo la fursa ambalo tunaweza tukalitumia vizuri sana kujielekeza na kujikita kwenye biashara na nchi takribani tatu au nne. Hiyo ni advantage kubwa sana na mfano, ukiangalia kusini kule Mtwara tuna ukaribu kabisa moja kwa moja na Nchi ya South Afrika na Nchi ya Mozambique lakini pia tuna ukaribu na nchi ya Comoro, hali kadhalika tuna ukaribu na nchi ya Madagascar. Hizi nchi kwa namna moja au nyingine kama tutajikita kufanya nazo biashara, kwa sababu kwanza zenyewe zina mapungufu mengi sana ambayo wanayategema sana yanaweza yakasaidiwa na sisi uimara wetu katika kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tunayo bandari kubwa ambayo haina shida, mpaka sasa imetengenezwa kwa kiasi kikubwa kabisa lakini pale ni lango pia ambalo la kuweza kutokea nchi nyingi kwenye bandari hiyo. Kwa sababu kama unavyoangalia ile Bahari ya Hindi imeunganika moja kwa moja katika hizi nchi, lakini sisi tunazalisha vitu vingi hususani mazao ya kilimo ambayo kwa namna moja au nyingine wenzetu kule hawawezi kuzalisha kwa mfano Nchi ya Comoro. Pia tunazalisha mifugo ambayo Nchi ya Comoro hawawezi kuzalisha, sisi tunaweza kuitumia nafasi hii kwa kuwauzia kwa kiwango kikubwa kabisa tukapata pesa za kutosha. (Makofi.)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema Bandari ya Mtwara, moja kwa moja kwa makusudio yetu yale ya kuunganisha reli ya standard gauge kwenda Mbamba Bay lakini kupitia Mchuchuma na Liganga moja kwa moja, hapo tunaona kwa jinsi gani hizi products zinazozalishwa kwenye Liganga na Mchuchuma kwa mfano chuma na makaa ya mawe, tuna uwezo wa kuwauzia moja kwa moja nchi hizi ambazo nimeziataja hapa kirahisi kabisa. Kwa namna moja au nyingine pia bandari hii inaweza ikawa ni kiunganishi cha nchi nyingi sana hasa hasa zilizounganikaunganika kwa upande kwa kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naliona kwa sababu Mkoa wa Mtwara unazalisha zao kubwa la korosho ambalo kwa namna moja au nyingine siku zinavyokwenda limekuwa zao linalopendwa kwa matumizi na watu wengi sana inakuwa ni rahisi kwa namna moja au nyingine kuziuza korosho zetu katika nchi hizo ambazo nimezitaja. Kwa hiyo tunaweza kuona jinsi gani Mkoa wa Mtwara unaweza ukawa umetumika kwa namna moja au nyingine ikawa kama mkoa mkakati wakusambaza uchumi wetu, lakini na kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakua kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, naona kwamba, bado hatujachelewa, lakini kuna gesi ambayo Mtwara imekuwa ni kitovu kikubwa sana cha gesi ambayo mpaka sasa hivi haijatumika vya kutosha. Naomba Serikali ifanye jitihada ya kutosha kabisa kuhakikisha gesi Mtwara inatumika. Sijajua tatizo ni nini mpaka sasa hivi ambalo linatukwamisha. Ningeomba Wizara husika ifanye mkakati wa kutosha kabisa kuhakikisha kuona gesi hii inatumika kama vile tumetegemea itumike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo la uzalishaji katika masuala ya kilimo, Mkoa wa Mtwara hauko nyuma pia katika uzalishaji wa mazao mengine ukiachia korosho ambao ni zao maarufu. Mkoa wa Mtwara ni maarufu pia katika kuzalisha ufuta ambao ni kigezo kikubwa kabisa cha kupunguza hili gap ya matatizo ya mafuta ya kupikia kama tutaweka nguvu za kutosha kidogo kwenye ufuta, lakini korosho na mazao mengine bila shaka Mtwara itakuwa ni sehemu mojawapo inatusaidia sana kupunguza shida hasa hasa katika suala zima la kupunguza matatizo ya mafuta yanayohitajika katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niweze kuzungumzia suala la miche ya korosho ambayo ilikuwa imelimwa na wajasiriamali wadogo wadogo kwa minajili ya kwamba ilikuwa ikatumike kwenda kuwekezwa katika maeneo mengine ambayo hayalimi hiyo miche. Wawekezaji wale mpaka sasa hivi wamekuwa wakilalamika kwamba hawajalipwa stahiki zao baada ya kuwa wametumia nguvu nyingi sana, lakini pia na kutumia pesa zao katika kuwekeza hiyo miche ambayo namna moja au nyingine ilizalishwa ikaiuzia Serikali kupitia Mamlaka ya Korosho lakini mpaka sasa hivi wananchi wale wanalalamika hawajalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kwa jicho la huruma kabisa iwasaidie hawa wawekezaji wadogowadogo kwa sababu wao ni sehemu kubwa kabisa ya maendeleo ya nchi hii kama vile ilivyokuwa wawekezaji wa maeneo mengine, hususani ukizingatia kwamba hawa ni wakulima ambao hutegemea kidogo sana wanachokuwa nacho waweze kukiwekeza sehemu nyingine wajipatie mkate wa siku zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna moja ama nyingine hapo ni kama nimchomekea tu maana yake nilijua sitapata nafasi ya kulizungumza hili, nimejaribu kulizungumza kwa mara mbili, mara ya tatu, sijalipatia jibu, naomba japo sio mahali pake hapa, lakini kwa taadhima Waziri husika atuonee huruma watu wa Mtwara, aweze kuwapa wale watu waliowekeza katika ile miche ya korosho wanachostahili angalau waweze kusukuma mbele kidogo maisha yao, japo najua sio mahali pake hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, najaribu kujielekeza pia katika suala zima la gesi kwa ujumla. Gesi kwa namna moja au nyingine imekuwa ni tegemeo kubwa katika eneo la Mtwara, lakini hata kwa Tanzania kwa ujumla, nafikiri itakuwa sehemu ya mojawapo itakayotusaidia kutatua baadhi ya changamoto ndogondogo ambazo kwa namna moja au nyingine tungeweza kushindwa kuzitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nishukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuniwezesha kuwa hai hivi leo na kuchangia hoja hii ambayo ni hoja muhimu sana. Pia nawashukuru wale wote waliowezesha kwa namna moja ama nyingine kunifanya nikachangia hivi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie hali halisi ya mazingira ambayo nafikiri kwa namna moja au nyingine Serikali haijafanya jitihada za kutosha sana kuangalia hiyo halisi na kuangalia jinsi gani ya kutatua tatizo hili la mazingira.

Mheshimiwa Spika, mfano katika mji wa Dar es Salaam, tafiti zinatuonyesha kwamba tani 5,600 za uchafu zinazalishwa; na uchafu wenyewe umejikita sana kwenye takataka za plastic. Pia tafiti hizo hizo hizo zinatuonyesha kwamba asilimia 30 mpaka 40 ya taka ngumu zinakuwa ndiyo peke yake zinaweza kupelekwa maeneo ya kutupa (dump) na dampo kwa Dar es Salaam liko moja tu, Pugu Kinyamwezi. Sasa ukiangalia asilimia iliyobakia ni takataka ambazo zenyewe hazina uhakika wa kwamba zinapelekwa wapi. Unaweza ukaona kwa jinsi gani hali ilivyokuwa ngumu hapo.

Mheshimiwa Spika, hali halisi pia inaonyesha kwamba kwenye beach za Mkoa wa Dar es Salaam kuna takataka takribani mifuko 150 mpaka mifuko 200 ambazo zinatolewa kila siku, yaani wale watu wanaojishughulisha na utoawaji wa taka, kila siku wanafanya kazi ya kutoa uchafu huo. Katika hali hiyo, tunahitaji kujielekeza sana kwenye jitihada ya kuzoa takataka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jitihada ambayo nayotaka ni-stick, ziko mbili ya kwanza kabisa ni kwenye suala la elimu. Tumejikita sana katika utatuzi wa kutengeneza miundombinu mikubwa mikubwa. Tnafikiria vitu vikubwa badala ya kufikiria vitu vidogo ambavyo vitatuwezesha kufanya suala hili kwa umakini kabisa. Kama tumeamua kutoa elimu, basi tuelekeze elimu yetu kwa sehemu kubwa kabisa kwa vijana, kwenye shule za msingi.

Mheshimiwa Spika, nashauri moja kwa moja tuwe na somo la mazingira. Lichukuliwe kama ni somo linafundishwa kuanzia Darasa la Kwanza, kwa sababu tunajua vijana wadogo ndio wanaoweza ku-pick suala lolote kwa uharaka zaidi. Wanajifunza kwa uharaka zaidi na kulitendea kazi; na kwa sababu wao ndio wenye nchi yao au dunia yao ya kesho; kwa sababu siyo dunia yetu, ni dunia yao wao, kwa hiyo, tukiwafundisha wao nafikiri itakuwa vizuri zaidi. Tutumie fedha nyingi katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine nashauri tuwamilikishe uchafu wale wanaotengeneza uchafu. Kama tutafanya jitihada hii, tutahakikisha kwamba mazingira yanakuwa safi. Hapa najaribu kuzungumzia kitu gani? Kwa mfano, tunajua kuna watu wanatengeneza maji, wanatengeneza juice, lakini kiuhalisia siyo kwamba wanatengeneza maji, isipokuwa wanatengeneza uchafu wa plastic, vile vifaa wanavyovitumia katika kuweka hayo maji au kuweka hivyo vitu vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima tufanye jitihada kuwamilikisha uchafu. Katika njia gani? Kuwaambia kwamba uchafu ule ni mali yao, wahakikishe kwamba kwa namna moja au nyingine, uchafu wowote utakaonekana sehemu yoyote ile unawahusu wao. Nao lazima wawajibike katika kuhakikisha uchafu ule wanauondoa. Kwa hiyo, njia mojawapo ni kuweka bei, kwa mfano bei ya maji shilingi 600, lakini iwekwe kama shilingi 100 iwe ni pesa ku-retain ule uchafu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mtu anayekuja kununua maji, ananunua kwa shilingi 600 lakini shilingi 100 ni gharama ya kutolea uchafu pale. Kwa hiyo, nafikiri kwa namna hiyo tunaweza kuwa na uhakika wa kuondoa uchafu ambao unazagaa kiholela.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumza ni kuhusu sera. Sera zetu lazima zihakikishe zinaangalia ajira za watu wa kutoa uchafu zinathaminiwa. Tuhakikishe kwamba kwa namna moja ama nyingine watoa uchafu wanaajiriwa kwa kuwawezesha kwenye miradi midogo midogo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikushukuru wewe mwenyewe binafsi, kwa kadri jinsi unavyoiendesha taasisi yako hii ya Bunge. Lakini nimshukuru pia Naibu Spika kwa kazi hiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika sekta hii ya kilimo, Sekta ya kilimo imekuwa ni sekta nzuri ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa sana uchumi wa nchi hii. Kwa muda wote sekta ya kilimo imekuwa namba moja katika uchangiaji katika uchumi wa nchi hii. Kwa mfano, mwaka 2018 sekta hii ilichangia kwa takribani asilimia 27.9 ya bajeti nzima. Lakini pia mwaka 2019 ilichangia kwa takribani asilimia 26.6 kwenye bajeti ya nchi nzima. Lakini imeendelea pia kuchangia sekta hii katika ajira, asilimia 58 ya ajira zinazopatikana katika nchi hii zinachangiwa na sekta ya kilimo. (Makofi)

Halikadhalika asilimia 65 ya malighafi (raw materials) inachangiwa na sekta ya kilimo. Baada ya kuona umuhimu wote huu bado Serikali imeendelea kuwa na kigugumizi kikubwa katika kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inapata haki inayostahili. Serikali imekuwa haioneshi weledi wake katika kuchangia sekta hii kikamilifu. Naomba kwa namna moja au nyingine, Serikali ioneshe nguvu zake zote kwenye sekta ya kilimo kusudi tuweze kufanya mapinduzi ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi tunatumia jembe la mkono, maeneo mengi sana jembe la mkono limekuwa siyo Rafiki. Hali hii imesababisha mpaka vijana ambao ndiyo wengi katika nchi hii kushindwa kujiingiza katika sekta ya kilimo kwa sababu ya ugumu wa matumizi ya hili jembe la mkono. Kwa hiyo, naiomba Serikali itilie mkazo kwa kiasi kikubwa kuiinua sekta hii ambayo inabeba ajira za wananchi walio wengi hasa wananchi walioko pembezoni vijijini huko.

Mheshimiwa Spika, lakini Serikali pia inaona shida gani kutumia sekta zake tofauti, kwa mfano sekta ya fedha kama benki, kuyaamrisha au kuyapa taarifa kwamba wawakopeshe wananchi. Kuna ugumu gani kwa sababu hii ni sekta muhimu na kilimo kinakopesheka. Wananchi wote ambao wanashughulika na kilimo wanakopesheka.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia mfano mdogo tu wa zao la korosho limetoa dola takriban bilioni 589. Hizi ni fedha nyingi sana, ni trilioni 1.3. Nashangaa kwa nini Serikali imekuwa na kigugumizi kuwekeza katika kilimo kwa sababu hii trilioni 1.3 ni takriban asilimia 4 ya bajeti nzima. Ukiangalia ni mchango mkubwa sana, sioni sababu kwa nini Serikali haijajielekeza kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, sisi pia tumejitambulisha kuwa tunataka kuendesha uchumi wa viwanda. Uchumi wa viwanda hauwezi kufanikiwa pasipokuwa na sekta ya kilimo. Kama tulivyoona pale kwamba asilimia 65 ndiyo inapeleka pale kama malighafi, sasa ugumu uko wapi?

SPIKA: Unajua Mheshimiwa Mchungahela, Waheshimiwa tuwe tunawasikiliza Wabunge wanaochangia. Huyu ni Mheshimiwa Issa Mchungahela wa Lulindi, unajua kule Kusini zamani neno mhasibu halikuwepo walikuwa wanaitwa wachungahela. (Kicheko)

Mpaka sasa hivi Mheshimiwa hueleweki kwa kweli, yaani hujajikita moja kwa moja kujaribu kueleza kitu chako, unapiga theory. Hebu endelea kidogo lakini shuka kwenye kitu ambacho unataka kifike.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nilitaka kujikita kwenye korosho. Korosho kwa namna moja au nyingine iko wazi kabisa kwamba inachangia kiasi kikubwa kwenye uchumi lakini pia kwenye ajira ya wananchi wa Kusini kwa sababu ni pesa nyingi sana ambazo Serikali inapata kupitia kwenye korosho.

SPIKA: Yaani mtu anaweza akakuuliza swali, haijajikita vizuri kivipi, unataka kusema nini? (Kicheko)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Ahaa.

T A A R I F A

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Ndiyo, taarifa, nimekusikia.

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mchungahela, anaposema Serikali haijajikita ipasavyo kwenye kulisaidia zao la korosho, hivi tunavyozungumza hata Bodi ya Korosho yenyewe haijaundwa. Bodi ile ya Korosho kwa sasa inakaimu Mkurugenzi hamna analolifanya. Kwa hiyo, napenda kumpa taarifa msemaji anaposema Serikali haijajikita alijumuishe na jambo hilo la Bodi ya Korosho. (Makofi)

SPIKA: Yaani anasema lilelile nililokuwa nakushauri mwanzoni, unaposema kitu hebu fika mwisho.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Yes! Napokea taarifa Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nataka kusisitiza kwamba hata jitihada zinazofanyika sasa hivi za kupeleka pembejeo, hizo pembejeo mpaka sasa kuna maeneo ya Jimbo langu ambapo ndipo panapozalishwa korosho mapema sana, sasa ni kipindi cha maandalizi ambapo pembejeo zinahitajika lakini hazijafika. Kwa hiyo, nilikuwa najaribu kuonesha pia katika mazingira hayo kwamba kwa namna moja au nyingine umakini sana unatakiwa katika utekelezaji wa yale tunayoyazungumza.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Issa Mchungahela, bahati mbaya dakika zimeisha. Nakushukuru sana sana kwa mchango wako.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameniweka hai na kuweza kuchangia bajeti hii ya viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kujielekeza kwenye bajeti hii kwa kuangalia baadhi ya vitu mimi sina shaka na mipango, mipango ya Chama chetu cha Mapinduzi lakini mipango pia ya Serikali sina shaka. Tumekuwa na mipango mizuri mingi sana tangu Serikali ilivyoanza kuundwa na mpaka hivi leo, ukiangalia bajeti za kila mwaka utathibitisha hilo. Kwa miaka mitano hii inayokuja mipango yetu imekuwa mikubwa na mizuri sana na kama tunavyojielekeza kwenye bajeti ya uchumi endelevu, lakini uchumi shindani pia hili ni jambo zuri kabisa na ni jambo jema lakini tunahitaji kujielekeza nguvu zetu katika utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tuna shida sehemu katika suala hasa la bajeti kuangalia vipaumbele. Tumekuwa hatujikiti sana katika vipaumbele vya bajeti zetu, tunaongea mambo mazuri, lakini katika utekelezaji nafikiri kumekuwa na changamoto, tuangalie mfano mdogo tu katika bajeti zetu, ukiangalia bajeti ya viwanda kwa mfano bajeti hii ndio mkombozi katika uchumi wa nchi hii kwa sababu kwa kutumia bajeti hii tungeweza kwa namna moja au nyingine kufikia malengo yale ya uchumi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani kama tungeingia kwenye vipaumbele, lakini ukiangalia unakuta miradi ambayo tunajaribu kutaka kuitekeleza ambayo kwa hali halisi ndio miradi ya mkakati unakuta kitu tofauti kwa mfano Mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao ni mradi mkakati kwa mwaka 2020/2021 ulitengewa takribani shilingi milioni 120 tu, mwaka 2021/2022 umetengewa shilingi milioni 25. Kwa kweli hatuko serious kabisa kama kweli tunataka kufanya yaani kwamba kama miradi hii ni mradi mkakati tofauti tunachoongea na kile tunachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia Mradi wa Mchuchuma tumetengewa takribani shilingi milioni 120 peke yake mwaka 2020/2021 lakini mradi huo huo pia tumetengewa takribani shilingi milioni 25 katika msimu wa mwaka 2021/2022 kwa kweli hatupo serious, hatupo serious kabisa, lakini mradi wa Ziwa Natron wenyewe ulitengewa shilingi milioni 50 peke yake, hali kadhalika kwenye mwaka 2021/2022 ulitengewa shilingi milioni 24 kwa kweli haioneshi kabisa kama sisi tupo serious katika huu uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu tukitaka tuendelee kwa umakini kabisa uchumi wa viwanda lazima tufanya seriousness, ionekane kabisa kwa sababu ukiangalia kiasi kilichotengwa kwa maendeleo kwa takribani kwa miaka hii miwili haizidi bilioni 30 sasa sijui kama kweli tunataka kutekeleza maendeleo ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuzungumza ni nini; kama tutajielekeza kweli kwenye uchumi wa viwanda kikweli kweli tunaweza tukaendelea vizuri sana na tukawa tumepata tija kubwa na mafanikio makubwa sana katika maendeleo na hatuwezi kujidanganya hatuwezi kuendelea pasipo kuendeleza viwanda, kwa sababu viwanda ndio vyenyewe vinakula material, material nyingi sana ambazo sisi tunatengeneza hapa ina maana kwamba kwenye kilimo kwa mfano, lakini kwenye maeneo mengine ya uchumi kwa mfano ya madini na hali kadhalika kwenye maeneo mengine ya uchumi kwa mfano yanayotokana na bahari yaani kwenye uchumi wa blue hivi vyote vinatumika na viwanda ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo bila viwanda hivi vitu vyote tunavyovizungumza haviwezi kufanikiwa na hatutaweza kuviendeleza, kama nilivyojaribu kuangalia kwa mfano tuchukulie mfano tuone muonekano halisi wa kadri jinsi haya mambo yanavyokwenda yanavyoweza yakatupatia tija. Tuna issue ya EPZ ambaye na yenyewe hatuoni kama tuna u- seriousness.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ kwa mfano pale Benjamin William Mkapa Serikali iliwekeza pale shilingi bilioni 36.4 kwa ajili ya kufidia na kuweka miundombinu, lakini ukiangalia pale kilichotokezea tulipata tija kubwa sana kutoka kwenye hiyo shilingi bilioni 36 tuliyowekeza tija tulizozipata pale tulipata uwekezaji wa mtaji yule mwekezaji aliweka mtaji wa shilingi bilioni 134; unaweza ukaona ni fedha nyingi kuliko tulizowekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa shilingi bilioni 36 tuliyowekeza tumepata shilingi bilioni 134 kama uwekezaji wa mtaji, lakini kampuni pia ilifanya mauzo ya shilingi bilioni 385.93 na kampuni hizo pia zilifanya matumizi ya fedha ambazo takribani shilingi bilioni 2019.184 lakini pia Serikali ilipata faida kupitia kodi ya shilingi bilioni 22.67 on top of that tulipata ajira ya watu 3,156.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaweza mkaona kwa jinsi gani tija kubwa ya shilingi bilioni 36 tu imezalisha haya yote haya tumepata Watanzania, kama tungewekeza vya kutosha Benjamin William Mkapa bila shaka mngeweza mkaona tija gani mngepata hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukiangalia SEZ eneo na Bagamoyo Serikali iliwekeza shilingi bilioni 26 peke yake lakini katika kuwekeza shilingi bilioni 26 Serikali ilikuja ikapata tija kubwa sana kulikuwa na tija kwa mfano shilingi bilioni 4.8 ya uwekezaji; mwekezaji aliweka hizo fedha, lakini mwekezaji pia alifanya mauzo ya nje ya shilingi bilioni 56.2 lakini kama haitoshi kampuni pia ilipata kwa kulipa kodi shilingi bilioni 1.305. Kwa hiyo unaweza ukaangalia kwa kiasi kidogo tu cha shilingi bilioni 26 tulizowekeza Bagamoyo tumepata fedha nyingi hizi, lakini cha kushangaza hapo hapo Serikali inadai kujaribu kurudisha baadhi ya maeneo ambayo tungeendelea kuyawekeza ya SEZ kwa kweli hatupo serious na kama tupo serious kwa kweli tunatakiwa tuwekeza kikamilifu kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini naomba seriousness kwenye viwanda ifanyike, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa afya tele mpaka naweza kuchangia bajeti hii.

Pili, niishukuru familia yangu, lakini kipekee kabisa nimshukuru mke wangu aliyenipa uwezo mkubwa sana wa kuwajibika na kuweza kutimiza majukumu yangu ya kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba, bajeti hii ni bajeti ambayo itaendelea kusomwa na kusifiwa kuwa ni bajeti nzuri kabisa katika bajeti zilizowahi kujadiliwa katika Bunge hili Tukufu. Siyo nasema hivyo kwa sababu tu ya kutaka kusifia, lakini ukiangalia jinsi hii bajeti ilivyotengenezwa, unaweza ukalithibitisha hilo nia ya bajeti ukiiangalia lakini pia ukiangalia dira lakini ukiangalia dhamira na pia ukiangalia pia utayari wa Mheshimiwa Jemedari wetu Mama Samia Suluhu Hassan, hiyo inakuashiria moja kwa moja kwamba hii bajeti itakuwa bajeti nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yenyewe naanza kwa kusema kabisa kwamba itatekeleza na kusimamia mazuri yote ambayo awamu tofauti tofauti za uongozi imeyatekeleza. Mazuri katika awamu hizo yako mengi sana, kila awamu iliyopita imekuwa na jambo zuri sana la kuigwa na kulisimamia kwamba liendelee kuwepo. Hata hivyo, kwa hali jinsi ilivyo kutokana na ufinyu wa muda sitaweza kuzungumzia kila zuri la awamu iliyopita, lakini kipekee tu nitaweza kuzungumzia jinsi walivyoweza kusimamia yale waliyotaka kuyatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yeye aliamini katika Taifa lenye uchumi imara kupitia sera ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea lakini hali kadhalika nchi huru yenye fikra huru, yenye uchumi huru, yenye siasa huru bila kujifungamanisha na nchi yoyote ile. Hili lilikuwa ni jambo jema kabisa ambalo awamu hii pia italitekeleza kwa njia ya kipekee kupitia staili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu iliyofuatia ilikuwa ni awamu ya Mheshimiwa Rais Ally Hassan Mwinyi na yenyewe ilikuwa na dhamira nzuri kabisa uchumi huria, lakini yenye watu ambao wako proactive, kukimbilia fursa ambazo zitawawezesha wao kuijenga nchi yao kikamilifu hasa katika masuala ya kibiashara. Fikra hii ililenga katika kuimarisha dhana ya kuwa uchumi au suala la biashara lishughulike na watu binafsi, lakini wakati huo huo Serikali ikijikita katika kutekeleza mambo ya msingi ya kijamii na kuendeleza miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Tatu, ya Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na yenyewe ilikuja na fikra pevu, nzuri kabisa ambayo yenyewe ililenga kabisa katika utekelezaji wa uwazi, lakini seriousness katika utekelezaji huo. Lengo lilikuwa ni kuwajenga wananchi waweze kujitambua, lakini pia kuona kwamba kila wanachokifanya wanakifanya kwa ajili ya manufaa ya nchi yao na uzalendo wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia awamu iliyokuja, Awamu ya Nne ya Mheshimiwa JK. Awamu hii pia ililenga katika kutengeneza uchumi uliokuwa imara, bora kabisa, ilijihakikishia kwamba inaweka miundombinu yote ya kuchochea uchumi na maendeleo, ilijaribu kuweka mkakati pia wa mahusiano ya kimataifa ambayo yalikuwa mahusiano bora kabisa na nchi za nje. Hii yote ililenga katika kuweka uchumi uliokuwa imara uchumi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Tano, awamu ya jembe, tuliona kabisa awamu hii ilikuja kwa kasi kubwa. Hii ilikuwa ni awamu ya kazi lakini hali kadhalika ilikuwa ni awamu ya viwanda ambavyo vimejielekeza katika kutekeleza uchumi wa nchi hii. Pia awamu hii ilikuwa awamu ya uwajibikaji lakini na u-champion katika kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia awamu hizi zote zilikuwa zimefanya vizuri na kama alivyosema Mheshimiwa jembe letu, mama yetu, jemedari wetu mkubwa, kwamba atajielekeza katika kutimiza mazuri yote, tunaona mazuri haya yanajenga msingi mkubwa na imara katika kutekeleza yale yote ambayo tunayategemea katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa hayo yote, nina shaka kidogo hasa nikiangalia kwa kadri jinsi tulivyoweza kutekeleza bajeti zetu zilizopita. Ukiangalia bajeti zetu zilizopita unaweza katika hali ya ubinadamu ukaona kwamba kunaweza kuwa na shaka. Kwa mfano, kwenye kilimo kilitekelezwa kwa asilimia 13 tu ya bajeti nzima. Halikadhalika viwanda, ile dhamira ya kutekeleza uchumi wa viwanda, bajeti zilizopita zilitekeleza kwa takriban ya wastani wa asilimia 20. Kwenye mifugo, ilitekeleza kwa takriban ya asilimia 18.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mazingira hayo yanaweza yakakupelekea ukawa na wasiwasi. Hata hivyo, wasiwasi huu unatoka moja kwa moja kwangu na imani niliyokuwa nayo ni kutokana na ile hali ya utayari wa mama yetu, hapo peke yake naamini kabisa kwamba hakutakuwa na wasiwasi kila kitu kitakwenda kama vile kilivyopangwa katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusisitiza kwenye hili ni nini? Nasisitiza katika utekelezaji. Naomba utekelezaji uwe wa umakini kabisa. Tukizungumzia utekelezaji hasa hasa unajikita katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni katika kutoa pesa inayohitajika, kusudi kila sekta ambayo imeomba pesa ipewe kwa kadri ya wakati na vile inavyohitajika na kwa kiwango kinachostahili. Awamu nyingine ni awamu ya utekelezaji, ambapo Wizara husika na watendaji kupitia sekta zake binafsi pamoja na halmashauri wawe wanawajibika kikamilifu kabisa kuhakikisha kila kitu wanachotakiwa kukifanya wanakifanya kama inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nataka kulizungumzia zaidi ni eneo la usimamiaji na hilo ndiyo jukumu letu sisi Wabunge pamoja na Madiwani. Sisi kisheria tumetambulika kwamba ni wasimamiaji ambao tunatakiwa tuisimamie Serikali kikamilifu kabisa. Kazi hii haiwezi kufanyika kikamilifu kama hatutapata taarifa zinazostahili katika kusimamia mambo haya. Kumekuwa na changamoto kubwa sana katika eneo la usimamiaji hasa hasa ukiangalia kwamba watendaji wameamua kupokonya kazi hii ya kusimamia. Mara nyingi wamekuwa hawatoi taarifa kwa Wabunge ambao ndiyo wanaostahili kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya wanajikabidhi wenyewe na wewe kama Mbunge ukijaribu kufuatilia kupata taarifa stahiki kutaka kujua ili uweze kusimamia, kunakuwa na changamoto ya usiri na unaonekana kama wewe ni kama vile kizabizabina, lakini halikadhalika unaonekana kama wewe unajipendekeza, lakini pia unaambiwa kama wewe unajipa madaraka ambayo hustahili wakati hili ni suala letu au ni kazi ambayo sisi tumeambiwa kisheria kabisa tunatakiwa tuifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana Wizara, naomba sana na Mawaziri wafanye kazi ya kutupa taarifa kabla hawajapeleka pesa ya mradi wowote, sisi tunastahili kujua mapema kuliko mtu mwingine yeyote.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja, sina shaka bajeti hii itakuwa ni bajeti yenye kuzungumzwa na kutekelezwa, lakini na kusifiwa duniani kote na miaka yote. Ahsante. (Makofi)