Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jonas Van Zeeland (3 total)

MHE. JONAS V. ZEELAND: Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaondoa wanyama wakali hasa tembo katika Tarafa ya Mlali na kuwarudisha kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa kuwa wamekuwa kero kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pole kwa wananchi wote wanaokutana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo. Wizara imeendelea kudhibiti wanyamapori hawa katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kukabiliana na matukio haya, Wizara kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa iliweka mkakati wa pamoja ambapo kutakuwa na vikosi maalum vya kudhibiti tembo. Vikosi hivyo vimeendelea kutoa msaada wa haraka pale inapotokea tatizo katika Mkoa wa Morogoro na maeneo mengine ikiwemo Wilaya ya Mvomero. Vikosi hivyo vimewezeshwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu vinavyohitajika katika zoezi la kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Vifaa hivyo ni pamoja na magari, risasi za moto, risasi baridi na mabomu maalum ya kufukuzia wanyamapori hususan tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na jitihada hizo, Wizara imenunua na kusambaza simu zenye namba maalum katika maeneo 14 nchini kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanatoa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, kwa haraka bila malipo na kwa wakati ili ziweze kushughulikiwa mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mzumbe hadi Mgeta?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo: -

Barabara ya Mzumbe – Mgeta yenye urefu wa kilometa 26 ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Sangasanga – Langali – Luale hadi Kikeo yenye urefu wa kilometa 59.16 na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mzumbe - Mgeta yenye urefu wa kilometa 26 imeanza kutekelezwa kwa awamu ambapo mwaka 2020 Serikali ilikamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa kipande cha mita 400 kuanzia Mzumbe na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali inaendelea na ujenzi wa kipande kingine cha mita 700 kwa shilingi 216,800,000 na kazi ilianza Novemba, 2021 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022. Sehemu iliyobaki itaendelea kujengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi 664,557,000 kimetengwa kwa kazi hiyo. Ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kumaliza barabara ya Manyinga hadi Madizini kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland Mbunge wa Jimbo la Mvomero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 500.00 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 0.54 ambapo ujenzi huo umekamilika.

Mheshimiwa Spika, TARURA itaendelea na ukamilishaji wa kipande kilichobaki kulingana na upatikanaji wa fedha ili wananchi wa eneo la Madizini na sehemu zingine katika tarafa ya Turiani waweze kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi kwa ufanisi.