Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Innocent Edward Kalogeris (16 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kwanza kumshukuru Mungu kwa mema mengi ambayo analitendea Taifa letu la Tanzania. Vile vile nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa nchi hii katika kipindi cha miaka mitano. Amekuza uchumi wan chi, ametupa ujasiri Watanzania na kubwa zaidi ametufanya tujiamini na kujitambua kwamba sisi sio masikini ni Taifa tajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii vile vile kumpongeza aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amirijeshi Mkuu wa Awamu ya Sita, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa wakati ule ya kumsaidia aliyekuwa mtangulizi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi nataka niwaambie Watanzania na wapenda maendeleo katika Taifa hili kwamba Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan anatosha kwa nafasi ambayo anayo kwa sasa na kubwa zaidi, tutarajia makubwa kwa maendeleo ya haraka na kwa kasi kubwa zaidi katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo sisi Wabunge na yeye mwenyewe na Hayati Dkt. Magufuli walipita kuwaahidi Watanzania na tukakipatia Chama cha Mapinduzi ushindi mkubwa wa kishindo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii vile vile kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye leo hii ametuletea bajeti na tunaijadili, kwa kazi kubwa ya usimamizi wa shughuli za Serikali katika Bunge na nje ya Bunge katika kipindi cha miaka mitano. Ndani ya hotuba yake kumejaa yale ambayo yametekelezeka katika kipindi cha miaka mitano na yale ambayo tunaenda kuyatekeleza ndani ya miaka mitano katika kipindi cha mwaka huu mmoja ambao tunao katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika na Spika ambaye hayupo, niwape pongezi nanyi kwa kazi kubwa ambayo mliifanya katika Bunge la Kumi katika kuisimamia Serikali na kutunga sheria ambazo zimesababisha leo tumefika tuko hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wenzangu nawaomba niwakumbushe, kazi kubwa ambayo tunayo kwa sasa, hata Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuja kufungua Bunge hili aliambia jambo moja; ana imani kubwa na Bunge hili. Sasa Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, hayupo, ametangulia mbele ya haki, tuelekeze nguvu zetu na tuonyeshe imani hiyo ambayo Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alitupa Bunge hili tujielekeze kumpa nguvu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan aweze kutekeleza yale ambayo tumewaahidi wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nianze kuchangia hoja. La kwanza, nichangie katika mipango ya miradi mikakati. Tuna Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo kwa namna moja au nyingine liko katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini na liko katika Jimbo langu la Morogoro Kusini. Ni mradi mzuri na mradi ambao kwa kweli ukikamilika utaleta mafanikio makubwa ya kujenga uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuthibitisha hilo nataka niseme tu mimi mwenyewe, ndani ya Halmashauri yetu, ndani ya kipindi hiki kifupi tumepata shilingi bilioni moja na karibu milioni 100 kama Service Levy ambapo fedha hiyo tayari asilimia 10 imekwenda kwa vijana na asilimia 40 imekwenda kwenye miradi ya maendeleo ya Halmashauri na nyingine zimeenda kufanya shughuli nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, CAG amezungumza. Kuna 4% kama huduma katika shughuli za kijamii (corporate responsibility), ambayo inatakiwa itoke katika mradi huo iende katika shughuli za wananchi. Naiomba Serikali ikasimamie hili ili kusudi tuweze kuipata fedha hii katika Halmashauri tuweze kufanya shughuli nyingi za maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna huu mradi wa Standard Gauge, ninaamini kabisa kwamba Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi zikishirikiana kwa pamoja wanaweza kutoa fursa kwa wananchi ambapo mradi huu utapita wakaweza kufanya kazi za maendeleo ambazo zitawaongezea uchumi na wakati huo huo mradi huu ukafanya katika misingi hiyo. Naomba tuangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la utawala. Katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini tuna jengo la Halmashauri. Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika mwaka wa fedha uliokwisha tumepata shilingi milioni 700. Mkandarasi yuko site, kazi inaendelea. Naomba nijue, katika awamu hii ya mwaka huu wa fedha, Halmashauri yetu imetengewa shilingi ngapi ili mradi huo uende moja kwa moja, tusije tukasimama ili tuweze kufanya shughuli za kuleta maendeleo kama vile ilivyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni afya. Katika mwaka wa fedha uliokwisha tumepata shilingi bilioni 4.3 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ambayo imekamilika na ujenzi wa vituo sita vya afya ambavyo vimekamilika. Sasa hivi kuna suala la vifaa tiba, kuna suala la dawa, ambulance na matabibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji hospitali ile ianze kazi ikiwa imekamilika, pia tunahitaji vituo hivyo vya afya vifanye kazi vikiwa vimekamilika, kufikia lengo ambalo Serikali inataka kutoa huduma kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini na Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliomba katika bajeti hii shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga wodi tatu katika Kituo cha Afya cha Mikese, Kituo cha Afya Kisaki na Kituo cha Afya cha Kisemo. Tukipata fedha hizi ni kwamba tutakuwa na uwezo wa kujenga, kukamilisha na hivi vituo vya afya vitafanya kazi na wananchi watapata kile ambacho tunakihitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, Halmashauri ya Morogoro Vijijini iko katika jiografia mbaya sana. Naiomba Serikali, pamoja na kwamba tumepata vituo vya afya sita, bado tuna uhitaji wa vituo vya afya tu. Tunahitaji Kituo cha Afya kwenye Kata ya Kasanga; Kata ya Bwakilajuu na Kata ya Singisa. Kata hizi ziko milimani na ni mbali kufikika, kwa hiyo, wananchi wetu wanapata wakati mgumu sana katika kupata huduma za afya. Tukiweza kuwafikishia huko, tutakuwa tumewasaidia sana. Naiomba Serikali ione ni jinsi gani ya kufanya na kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nizungumzie kidogo kilimo. Mkoa wa Morogoro ni mkoa ambao una ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo. Nimeona katika mpango ambao tumeletewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kuna fedha zilikwenda Njage Wilaya ya Kilombero, kuna fedha zilikwenda Mvumi Wilaya ya Kilosa, kuna fedha zilikwenda Kigubu Mvomero na kuna fedha zilikwenda Kilangazi Kilosa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na fedha hizo kwenda, lakini Mkoa wa Morogoro bado una maeneo makubwa kwa ajili ya kufanikisha kilimo cha umwagiliaji na ambacho nina uhakika ndiyo kilimo cha uhakika na cha kutusaidia. Niombe sana kuna mradi wa Kongwaturo, mradi mkubwa sana unahitaji fedha…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Niendeleze hapo hapo alipozungumza dada yangu Mheshimiwa Munde Tambwe. Mkoa wa Morogoro tunaomba ukatwe ipatikane mikoa miwili. (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Ugawanywe.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Nimeelekezwa ni ugawanywe.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Morogoro ugawanywe ipatikane mikoa miwili ambapo kutakuwa na Wilaya ya Morogoro, Wilaya ya Mvomero, Wilaya ya Gairo na Wilaya ya Kilosa; na kwingine kutakuwa na Wilaya ya Ulanga, Wilaya ya Malinyi na Wilaya ya Kilombero. Tupate mikoa miwili ili kuweza kurahisisha kupata maendeleo katika Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Ummy kwa uteuzi ambao ameupata katika Wizara hii mpya. Ni imani yangu kwamba yeye na wasaidizi wake; Manaibu wake watafanya kazi kubwa kama ile aliyoifanya akiwa Wizara ya Afya wakati wa mapambano ya Corona na tukashinda, naamini kabisa kwamba TAMISEMI atafanya vizuri zaidi. Hizi changamoto zote pamoja na mafanikio yote, lakini changamoto hizi tutakwenda kuzimaliza.

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la barabara. Mimi ni Mkandarasi. Katika uhalisia, Wilaya ya Morogoro Halmashauri yetu ina eneo la square mita 11,731, ina barabara zenye urefu wa kilometa 750, ina madaraja makubwa 29, ina ma-box culvert 74, lakini mgao wake tunapata shilingi bilioni 1.1. Ni kwamba kwa namna moja au nyingine, tunatengeneza kilometa moja tu bila kugusa makalavati wala nini kwa shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Spika, kama Mkandarasi, barabara ya changarawe ili iweze kupitika ikiwa na madaraja au box culvert, unahitaji kilometa moja kwa shilingi milioni 30. Sasa naomba tu, ndugu yangu Mheshimiwa Zungu amezungumza, Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Miundombinu Mheshimiwa Kakoso amezungumza, tuangalie jinsi gani tunaisaidia TARURA. Katika kuisaidia TARURA, naomba, hawa wenzetu wamekokotoa, wamechanganua, ni kwamba kutakuwa na uwezekano wa kila mwaka kupata shilingi milioni 500. Katika hilo suala la Mwenyekiti wangu ndugu yangu Mheshimiwa Kakoso, kila mwaka tutakuwa tunapata shilingi trilioni 2,160. Naomba Serikali ichukue mawazo haya na ikayafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika shilingi trilioni 2,160 ukizigawa kwa Halmashauri zetu, tutakuwa na uhakika wa kila mwaka kupata kila Halmashauri shilingi bilioni 11. Shilingi bilioni 11 ukipeleka kwenye Halmashauri, ndani ya miaka mitano, tatizo la TARURA litakuwa halipo tena hapa Bungeni. Kwa hiyo, naiomba Serikali tu, mama yangu Mheshimiwa Ummy, Waziri wa Fedha na wengine wote wanaohusika, lisimamieni hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakupa kichekesho kimoja, lakini siyo kizuri. Juzi mliona katika mitandao, wale watu waliokuwa wanatembea uchi, wametoka jimboni kwangu. Kilichojitokeza, watu huwa wanavua nguo wanapopita kwenye barabara za umande, wanazihifadhi nguo zao. Kwa hiyo, naomba tu, tunadhalilika. Jimbo la Morogoro Kusini eneo kubwa ni milima, kwa hiyo, shida yetu kubwa ni barabara. Tunawaomba mtusaidie katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kuna suala la maboma, ndani ya Halmashauri yetu tuna maboma 170 yanasubiri kumaliziwa, tunaiomba Serikali sijui dada yangu Mheshimiwa Ummy katika bajeti ya mwaka huu umetutengea kiasi gani? Tunaomba tufanya jambo hilo ili zile nguvu ambazo wananchi wamezitumia zikakamilike na waone faida yake. Tutaendelea kuwahamasisha kufanya mambo mengine, lakini kama haya hatujawakamilishia wataona kama vile tunawapotezea nguvu zao. Kwa hiyo, katika bajeti hii sijui Halmashauri yetu umetutengea kiasi gani, lakini tunaomba maboma yakamilike.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumza ni kwenye masuala ya madeni ya watumishi. Katika Halmashauri yetu watumishi wanadai karibu shilingi bilioni mbili. Watu hawa wanajitoa kwa hali na mali katika kufanya kazi, inapofika mahali hatuwezi kuwapatia fedha ambayo ni stahiki yao, tunakuwa hatuwatendei haki. Nawaomba katika bajeti hii, fedha zitengwe watu wapate haki zao ili waweze kututumikia vizuri vile inavyopasa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, namwomba dada yangu Mheshimiwa Ummy au wasaidizi wake, tukimaliza bajeti twende wote wakaone uhalisia wa Jimbo la Morogoro kusini na Halmshauri ya Morogoro jinsi gani ilivyo ili wakija katika bajeti ijayo wawe na mpango uliokuwa sahihi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii nyeti ambayo imegusa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika Wizara lakini vilevile kuwapa pole kwa haya ambayo yanaendelea kutokea. Yote haya naamini kabisa yanatokana na ufinyu wa bajeti ambapo kwa namna moja au nyingine kama wangeweza kupata fedha nyingi haya yasingetokea.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa ambayo Wizara inafanya, naomba niseme bado kuna kazi kubwa ambayo Wizara inaifanya katika kuinua kilimo kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, mimi nijikite kwenye eneo moja tu; naamini kabisa kilimo chenye tija na cha uhakika kwa Mtanzania ni kilimo cha umwagiliaji. Hadi hivi sasa tunavyozungumza kupitia Tume ya Umwagiliaji, tunaambiwa kwamba kuna lengo la kulima hekta milioni moja na laki mbili na hadi hivi sasa tumefikia asilimia 58 ambayo ni hekta 695. Ombi langu na ushauri wangu kwa Serikali, naomba tujikite kwenye maeneo ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nianze na moja tu, tunapoteza maji mengi ambayo yanakwenda baharini na Serikali imekaa hatuingii huko. Mfano, nataka nizungumzie kwenye Bonde la Kongwa unapoingia Kibaigwa, maji yanatiririka mwaka mzima, yanakokwenda hapajulikani lakini pale tungeweza kuchimba mabwawa watu wakafanya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Mto wa Dumila, mpaka tunaharibu barabara, zinakatika. Mimi niishauri Serikali katika maeneo kama yale ya Dumila, Ruvu, hebu tungechimba mabwawa watu waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji ambacho kitaweza kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Watanzania wanalima maeneo makubwa, dhamira kubwa ni kukusanya kidogokidogo kwenye kila hekta ili kuweza kupata tija. Nilipata nafasi ya kwenda China mara mbili, mtu analipa hekta tano, tatu analima mpunga mbili analima kilimo cha horticulture, ndani ya mwaka anapata tija kubwa kuliko Mtanzania ambaye analima hekta mia katika Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kabisa kilimo cha umwagiliaji ndicho ambacho kitamkomboa Mtanzania. Mkoa wa Morogoro umeambiwa ni FAMOGATA – Fanya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Taifa la Chakula. Ndani ya Mkoa wa Morogoro tuna eneo ambalo linatosha kwa kulimwa kwa kilimo cha umwagiliaji hekta 230,000 lakini mpaka hivi sasa tumetumia hekta 28,000 tu. Kama kweli we are serious na kilimo hebu tu-inject hela katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Morogoro Kusini tuna mradi wa Kongwa Tulo ambao una uwezo wa kulima hekta 3,000. Hadi hivi sasa zimetumika hekta 200 tu. Kuna mradi wa Mbangarawe, kuna hekta 230 tumetumia hekta 200 tu bado 30. Kuna mradi wa Lubasazi, una uwezo wa kulima hekta 120, hadi hivi sasa kuna shilingi milioni 800 imewekwa pale lakini bado mradi haujaendelea, maana yake tumeweka fedha ambazo hazitumiki. Kuna mradi wa Kirokwa ambao una hekta 105, mpaka dakika hii tunatumia hekta 40.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukijaribu kuangalia, tuna-ijnect fedha kwenye miradi lakini haifanyi kazi. Tumeomba katika mradi wa Kongwa Tulo ili tuweze kuendelea mwaka karibu wa pili huu sasa, nilikuwa Mbunge miaka mitano iliyokwisha, miaka mitano nimekwenda likizo, hakuna kilichowekwa. Sasa hivi tumeomba tena shilingi bilioni 1.4; Mbarangwe shilingi bilioni 1.5; Lubasazi shilingi bilioni 1.5; Kiroka shilingi bilioni 3, ukijumlisha ni shilingi bilioni 7. Fedha hizi tukipeleka pale nina uhakika tutanyanyua kilimo cha Watanzania na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nizungumzie suala la masoko. Kwa kweli watu wengi wamezungumzia suala la masoko; ni kero kwa wakulima wetu. Hivi ninavyozungumza kuna wakulima wangu kule mazao yako ndani na wanakaribia kuuza nyumba zao kama hatutaweza kuwasaidia kuwapatia masoko.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu ya wataalam ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kwa kuwa muda ni mchache, niombe nijikite katika maeneo kama mawili, matatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, niiombe Wizara kuna mbuga mpya ambayo imetangazwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo zamani ilikuwa ni pori la hifadhi. Niombe Wizara mbuga hii ni kubwa ina wanyama wengi, ina wanyama wakubwa na wazuri ambao inaweza kuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii katika nchi.

Ombi langu kwa Wizara ni kwamba utangazaji wa mbuga hii bado haujakuwa mkubwa kiasi cha kuwafanya watalii wengi wafike kule. Ukiangalia bado tunatangaza mbuga ambazo ziko kaskazini wakati mbuga hii ni kubwa inaweza ikaongezea mapato makubwa Serikali na kufanya kwamba mambo yawe mazuri katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naamini kabisa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linajengwa kule nalo linaweza likawa ni moja ya kivutio kikubwa cha watalii. Kwa hivyo niombe sana Wizara iangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo ningependa kuchangia na sisi Morogoro kule kuna eneo linaitwa Kisaki majimoto. Kuna maji ambayo yanachemka na mayai yanachemshwa. Niombe nacho ni kivutio ambayo Wizara kwa namna moja au nyingine watume wataalam wakaangalie jinsi gani wanaweza wakakitumia kivutio hicho kuongeza mapato kwenye Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo ningependa kuchangia katika Wizara hii, kati ya mwaka 2016 na mwaka 2021, kuna watu 46 wameuawa na mamba, kuna watu 15 katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini wamepata vilema vya kudumu kutokana na ongezeko kubwa la mamba katika Mto Ruvu na Mto Mvuha ambao unapita katika Vijiji vya Tununguo, Mkulazi, Selembala pamoja na Kijiji cha Mvuha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kwamba, idadi kubwa ambayo imetokea katika vifo kutokana na mamba imetokea katika Kata ya Selembala. Mwaka 2016 kumetokea vifo vya watu watatu; mwaka 2017 kumetokea vifo vya watu tisa; mwaka 2018 watu watano; mwaka 2019 watu sita; mwaka 2020 watu 14 na hadi Mei mwaka huu, watu tisa wameshakufa katika Kata ya Selembala. Kuna taharuki kubwa kwa watu na hasa ukitilia maanani watu wengi vijijini wanatumia maji ya mto wanashindwa kwenda kuchota kwa sababu wakienda wanakumbana na vifo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, naamini kwamba mamba wamekuwa wengi na naamini kwamba ni wakati muafaka kwa sasa kwenda kuvuna mamba hao ili tuepushe vifo vya watu, lakini wakati huo huo tukapata fedha katika kuuza ngozi za mamba hao. Sambamba na hili vile vile nikuombe kupitia Wizara kwamba, tunaomba vifuta jasho kwa watu hawa ambao wamepoteza maisha kwa mujibu wa taratibu na sheria za maliasili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe vile vile kupitia Bunge lako Tukufu, kwa Wizara ya Maliasili na Utalii isaidie Halmashauri ya Morogoro Vijijini kwa vitendea kazi vya magari, lakini vile vile Askari wa Wanyamapori ili waweze kwenda kutusaidia ongezeko la wanyama ambao wamefanya uharibifu mkubwa kwenye Kata ya Kisaki, Kata ya Bwakila Chini, kata ya Serembala, Kata ya Mvuha. Nashukuru na naipongeza Wizara katika mwaka 2019 tumelipwa kifuta jasho kwa wakulima ambao waliharibiwa mazao na wengine ambao wamepoteza maisha wamepata kifuta jasho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado katika mwaka 2020 hatujapata kifuta jasho kwa wakulima ambao ekari 572 zimeathiriwa na ongezeko la wanyama hao waharibifu na wengine ambao wameshambulia watu. Ombi langu kwa Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu, lakini kubwa zaidi nikupongeze wewe binafsi kwa kazi kubwa ambayo unaifanya hapo katika kiti katika kutuongoza. Hakika wewe ni mtoto wa nyoka na kama sio wa nyoka basi ni mjukuu wa nyoka, maana yake damu ya ukoo wa Adam Sapi Mkwawa inaonekana inafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Naibu wake na timu nzima ya wataalam kwa kutuletea bajeti ambayo kiuhakika imebeba dhana ya maelekezo ya mama yetu Samia Suluhu Hassan, lakini kubwa zaidi Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika kumsaidia Mtanzania kusonga mbele kutoka hapa tulipo na kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uthibitisho tosha umeona kila Mbunge aliyesimama anapongeza, lakini sio Mbunge kwa sababu sisi Wabunge tulichangia katika bajeti katika Wizara mbalimbali, tukieleza zile kero za wananchi wetu na wananchi wetu huko nje vile vile wamepata faraja kubwa na wanaendelea kuipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa hongera sana kwa mdogo wangu Mheshimiwa Mwigulu na timu yake kwa kufuata maelekezo ya mama, lakini kwa kufuata maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Chetu Cha Mapinduzi. Ni imani yangu kabisa tukienda hivi ndani ya miaka mitano hii tutafanya mambo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jemedari mkuu katika nchi yetu, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ndani ya kipindi cha siku 100 anakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika mama huyu ni Mama shujaa, mama shupavu ambaye kwa uhakika niwaambie Watanzania na naendelea kusema mama huyu anatosha, anatosha na atatuvusha salama Watanzania kule tunapotarajia kwenda. Hata hivyo, nitumie nafasi hii…

T A A R I F A

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa tu ndugu mzungumzaji kwamba mama huyu sio tu anatosha bali anatosha na chenji inabaki. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kalogeris, endelea na kuchangia.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nimeipokea taarifa. Ni kweli chenji bado inabaki na itatosha kufanyia mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vile vile kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndugu yetu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ndani na nje ya Bunge katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, lakini kuwa kama kiungo kati ya Mama Baraza la Mawaziri lakini na sisi Wabunge katika kuona kipi kifanyike. Ni imani yangu kwamba hata haya yaliyokuja kuna majumuisho makubwa ambayo yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vile vile kutoa pongeza za dhati kwa Serikali yangu. Hakika kauli yake Mama, anatusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi tunatakiwa kujibu kazi iendelee, kazi inaendelea tena kwa kasi kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tumepata milioni 500 kila Jimbo kwa ajili ya TARURA. Wabunge tumepiga kelele kwamba barabara mbaya, barabara mbovu, lakini mama ametusikia ametupa. Pia nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu na naamini hayo ni maelekezo ya Mama kwa kubuni vyanzo mbalimbali ambavyo tunaamini kwa mwaka huu wa fedha tutakwenda kutengeneza bilioni 300 ambayo inaonekana inakwenda TARURA. Ombi langu kwa Serikali, Halmashauri, Majiji na Manispaa tumetengwa katika fedha za Mfuko wa Barabara, wamependelewa wenzetu wa Majiji na Manispaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu fedha hizi katika mgao wake uende kwa majimbo bila kujali la Manispaa au la Jiji na kadhalika ili na sisi Halmashauri twende tukajenge barabara ambayo ukitilia maanani mtandao wa barabara kwenye halmashauri ni mkubwa kuliko kwenye majiji au manispaa. Kwa hivyo niwaombe Wabunge wenzangu katika hili tuwe pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha TAMISEMI mgao wa fedha hizi bilioni 300, zigawiwe katika majimbo, nikiamini kila Jimbo litapata karibu millioni 800 na tutaenda kufanya kazi kubwa ya barabara. Ndani ya miaka mitano nataka nithibitishe katika Bunge hili kwamba suala la barabara litakuwa ni historia katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vile vile kutoa pongezi za dhati kwa Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi tuliahidi na bahati nzuri nilikuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa mpaka naingia hapa Bungeni. Nilipita Mkoa mzima wa Morogoro tukiahidi kila kitu tutafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la REA, walipotuambia umeme tulisema mpaka kufikia 2023 tutakuwa tumekamilisha kabisa. Nataka nitoe taarifa na shukrani za dhati kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini na Mkoa wa Morogoro. Jana Mkoa wa Morogoro tumezindua rasmi REA III mzunguko wa II, vijiji vyote vinapata umeme. Hongera sana kwa Serikali yangu ya Chama Cha Mpinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru leo asubuhi katika kuuliza swali imeonekana vijiji vile ambavyo vimepungua, Wizara imesema kwamba navyo vitaingia hata kama havipo. Kwangu vimebaki vijiji vitano tu, ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niishukuru Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kazi kubwa ambayo imeifanya, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alipokuwa katika ziara yake katika siku zake za mwisho katika dunia hii, alisimama Morogoro na akasema atatoa kilometa 40 kujengwa kwa lami kutoka Mjini Morogoro mpaka tutakapoishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru katika bajeti hii tumetengewa kilometa 15 na tayari imeshatangazwa maana yake kazi inaenda kufanywa, nina kila sababu ya kuipongeza Serikali, lakini niiombe Serikali barabara hii inakwenda mpaka kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere inakwenda mpaka kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere tuendelee kutenga fedha ili tufike huko, utalii ukaendelee kuwepo kwenye Hifadhi, lakini vile vile katika hilo bwawa la Mwalimu Nyerere. Naamini bwawa hili likikamilika utakuwa ni utalii mkubwa ambao utaingiza fedha nyingi kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba nichangie kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza ni kwenye kodi; ni imani yangu hakuna Mtanzania ambaye hataki kulipa kodi, ila lipo jambo ambalo Serikali inatakiwa kufanya kupitia TRA kwamba kodi inayokadiriwa iwe na uhalisia na inayolipika. Katika maeneo mengi wafanyabiashara wanalia na ukweli usiofichika wanalia, kuna kama dhuluma ambayo inatendeka. Sasa katika hili, Mama yetu amesema hataki dhuluma, anataka watu walipe kodi kwa hiyari, naomba Mheshimiwa Waziri akasimamie hili TRA, kodi ikawe ya uwazi na iwe inayolipika kulingana na mwananchi alivyopata kipato chake, failure to that, ni kwamba watu watakwepa au tunatengeneza mianya ya rushwa kati ya watu wa TRA na walipakodi, mwisho wake kodi itakuwa haiwezi kulipika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ambalo ningependa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ili kazi iendelee, haya yote niliyosema yakamilike. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaitenda akiwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakumbuka katika Bunge lililopita nilisema kwamba mama huyu anatosha, na ni kielelezo tosha kwamba tumeshuhudia utendaji wake wa kazi uliotukuka. Sasa hivi majimboni mambo mazuri, sisi Wabunge tuko vizuri tukiamini kabisa kwamba utendaji wake wa kazi unatusaidia katika kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaitenda ndani na nje ya Bunge, akiwa kama Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Na nimpongeze kwa bajeti nzuri ambayo ameileta imesheheni katika kila sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini ikipita na tunaamini itapita, na kwamba italeta matokeo mazuri katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama changu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi nijikite moja kwa moja katika kuchangia hoja. Cha kwanza, nichangie hoja katika hotuba yake namba 57 ukurasa wa 33 ambayo inaonekana itakuwa mwarobaini wa migogoro ya wakulima na wafugaji. Tumeona hapa Serikali imepanga katika mwaka huu wa fedha kutengeneza mashamba darasa katika Wilaya ya Handeni na Longido. Niiombe Serikali, Mkoa wa Morogoro vile vile ni Mkoa ambao una migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji, lakini una ardhi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba katika mwaka ujao wa fedha au mwaka huu wa fedha wangeweka utaratibu wa kutengeneza mashamba darasa katika Mkoa mzima wa Morogoro na ikiwezekana Mkoa wa Pwani ili wale wafugaji wenyeji walioko pale wapate utaalamu wa kutengeneza haya mashamba darasa, ili wawe na utaratibu kwamba, Januari atalisha hapa, Februari atalisha hapa, Machi atalisha hapa, mpaka mwaka mzima unapita na kuacha kwenda kuzurura ovyo kuchunga na kuingia katika migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo uliifanya katika utunzaji wa mazingira Kitaifa katika Mbuga ya Ngorongoro. Ninaamini kabisa Ngorongoro ni urithi katika Taifa hili, kuendelea kuiachia watu wakaivamia, tutakuwa tunapoteza urithi huo, lakini kubwa zaidi tutapoteza fedha nyingi za kigeni ambazo zinasaidia katika kuendesha nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hili alilolifanya kama Waziri Mkuu, na ninaamini alishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Mazingira, sasa hivi tujielekeze katika kukabiliana na janga lingine la migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali katika mkoa huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kama tumeweza kupata hekta 500,000 ambazo Serikali imezipata Handeni, Tanzania bado ina maeneo makubwa ambayo tunaweza kwenda kuyapima na kuwapeleka wafugaji wakakaa huko wakanusuru mifugo yao katika kipindi cha kiangazi na tukaondokana na migogoro mikubwa ya wakulima ambayo haina sababu. Hili ni janga kubwa huko tuendako kama Serikali haitalisimamia na kulichukulia kwa umakini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini Mheshimiwa Waziri Mkuu akiamua na timu yake; Wizara ya Mifugo, Wizara ya Ardhi, wanaweza waka-allocate maeneo mbalimbali katika Tanzania yetu kama vile tulivyofanya Handeni tukapeleka huko nako wafugaji wengine wakakaa wakajengewa miundombinu ya barabara, maji na nyumba. Leo hii tunaambiwa kwamba tumepata ardhi, tumepata nyumba na tayari 101 zimeshajengwa kati ya nyumba 300; visima vinne vimeshachimbwa kati ya visima 13. Naamini Serikali ikiamua inaweza. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kama watu walivyokuwa wanapiga kelele kwamba tunafanyaje katika kunusuru mifugo? Tunafanyaje katika kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji? Naamini kama hii Serikali itashughulikia hili, itakuwa imetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikwambie, kuwaachia Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, haitawezekana kabisa kwa sababu hili tayari limeshakuwa janga kubwa na hawana uwezo nalo. Kinachotokea sasa hivi, tutakuja kufika mahali tutagombana kati ya wachuguliwa na watendaji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala la barabara. Tumefanya mambo mengi, naipongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa iliyoifanya. Kuna suala la TARURA, tulipata shilingi bilioni 1.5. Naomba na ninaielekeza Serikali, ikiwezekaa TARURA waongezewe fedha ili waweze kujenga madaraja huko vijijini. Kwa baadaye, naiomba Serikali ikiwezekana kuwe na special program kwa majimbo na wilaya zilizokuwa pembezoni ili ziongezewe fedha zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya kutengeneza barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naipongeza Serikali kwa suala la TANROADS. Tumepata lami katika Barabara ya Bigwa – Kisaki yenye kilometa 15, tunasubiri mkandarasi tu, muda wowote aanze kazi. Pia kuna barabara yenye kilometa
63 kutoka Kiloka kwenda Mvuha, tayari tunatarajia kuitangaza. Ombi langu kwa Serikali, barabara ya Bigwa – Kisaki yenye kilometa 140 kwenye mradi wa umeme, lakini vilevile kwenye hifadhi ya Mwalimu Nyerere, ni hifadhi ambayo utalii wake utaweza kuwa mkubwa kama tukifika katika kilometa zilizobakia 40. Naiomba Serikali kushughulikia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali katika suala la afya. Wilaya ya Morogoro Vijijini, hospitali yao imekamilika; vituo vya afya, sita vipo; changamoto zetu, nianze na kimkoa. Mheshimiwa Mbunge wa Morogoro Mjini amezungumzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa; Morogoro ni katikati, lakini hakuna Hospitali ya Rufaa, tuna Hospitali ya Mkoa. Tunaiomba Serikali itujengee Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro ili tuweze kunusuru maisha ya watu katika ajali za barabarani zinazotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna changamoto ya uhitaji wa vifaa tiba na dawa na majengo ya OPD katika Halmashauri ya Morogoro vijijini…

(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango mzuri wa Morogoro na maeneo mengine.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ys kuchangia Mpango wa Taifa wa maendeleo. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mama yetu, Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuiendeleza nchi yetu. Nitumie nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu kwa Taifa kwenye sekta ya utalii. Sisi wote ni mashuhuda, Mama amefanya kazi kubwa kupitia Royal Tour, watalii wamekuwa wengi na kuna kila sababu ya sasa kuelekeza maeneo mengine yenye utalii ili kusudi tuweze kuongeza pato kwenye Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi utalii upo katika Nyanda ya Kaskazini, lakini nchi yetu imepata bahati ya kuwa na vivutio vingi vya kitalii hata katika sehemu zote za Tanzania. Kuna mradi mkubwa ambao unafanyika wa kuendeleza utalii na kuendeleza rasilimali kusini ya nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbuga ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini kuna Mbuga ya Mikumi, kuna Mbuga ya Uduzungwa zipo katika Mkoa wa Morogoro. Vile vile kuna Mbuga ya Ruaha Mkoa wa Iringa na kuna Mbuga ya Katavi Mkoani Katavi. Katika mpango huu wa REGROW tuna kila sababu ya kudhani kwamba, kama Serikali itasimamia kikamilifu mpango huu tuna uhakika wa kupata mapato mengi kwenye mbuga katika Ukanda wa Kusini na kuongeza mapato makubwa katika Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe tu kupitia mpango huu Serikali isimame na ihakikishe kwamba kuna fedha nyingi, najua zimepelekwa, zikasimamiwe inavyopaswa ili ziweze kuleta matokeo chanya. Yakajengwe madaraja kwenye hifadhi zetu, zikajengwe barabara kwenye hifadhi zetu, lakini vile vile zikatumike kufanya promotion ya utalii ili kusudi tuongeze pesa katika sekta ya utalii na kuweza kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, sambamba na hilo katika mbuga ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo iko Wilayani Morogoro, niiombe Serikali, ili kuweza kuwafanya watalii waweze kufika kwa haraka lakini vile vile kwa wepesi na kwa wingi barabara ya Digwa-Kisaki iko katika mpango wa ujenzi. Bajeti iliyopita imetangazwa, tuliahidiwa mpaka kufikia Mwezi wa Tisa itakuwa tayari imeshatangazwa kwenye TANePS kwa ajili ya kumpata mkandarasi. Hata hivyo, mpaka muda huu tunaozungumza jambo hili halija-tick. Nikuombe tu Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi lakini Waziri wa Fedha najua fedha ipo basi kazi hii ifanyike ili kusudi suala hili likamilike tuweze kuongeza utalii. Tukiweza kuongeza watalii kwa upande wa kusini ni imani yangu kwamba tutakuwa tumepata fedha nyingi za utalii na tutaweza kusaidia kusukuma maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, nitumie nafasi hii kuipongeza Kamati ya Bajeti, tumeona ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa la Mwalimu Nyerere lipo katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Jimbo la Morogoro Kusini ambalo mimi nipo kule, lakini vile vile lipo katika Halmashauri ya Rufiji. Bwawa hili likikamilika litaweza kuleta matokeo makubwa sana katika uchumi wa nchi yetu. Niombe Serikali ikasimame katika mazingira yanayotakiwa kuhakikisha kwamba linakwisha kwa muda na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti imesema, mradi ulikuwa unatakiwa kukamilika tarehe 15 mwezi Juni mwaka huu, lakini wameongezewa mpaka tarehe 15 mwezi Juni mwaka unaokuja. Ombi langu kwa Serikali, wakandarasi, na mimi mwenyewe ni mkandarasi, kuna ujanja na ubabaishaji; wanaweza wakafika mahali wakataka kutucheleweshea mradi wetu ambao kwetu sisi tunauhitaji kwa kiasi kikubwa. Tuhakikishe kwamba muda huu waliopewa kwa mujibu wa utaratibu kazi iwe imekamilika; kwa sababu; moja, inaonekana, vile vile Kamati yetu imesema, wameongezewa mwaka mmoja lakini mpango kazi wa mkandarasi huyu unaonekana kwamba atamaliza kazi hiyo mwaka 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe, wenzetu ambao wanasimama TANESCO wakahakikishe kwamba wanasimama kikamilifu kuhakikisha mradi huu unakamilika ndani ya muda ili yale matumaini ya Watanzania kupata umeme wa uhakika lakini uliokuwa salama uwe umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, katika suala hili la mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kuna suala la CSR. Halmashauri ya Morogoro Vijijini na Halmashauri ya Rufiji mpaka tunafikia asilimia 75 ya ujenzi wa Bwawa hili bado hatujapata fedha yetu ya CSR kwa mujibu wa mkataba unavyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi napata mashaka, kupitia Kamati ya Bajeti, TANESCO kwa mara ya kwanza walipeleka kwa mkandarasi ujenzi wa uwanja wa michezo Dodoma. Mkandarasi akakataa kwa sababu haikidhi vigezo vinavyotakiwa. Lakini tayari katika Kamati ya Bajeti nimeona, safari hii TANESCO tena wamepeleka miradi ambayo haihusiani na wananchi wa Morogoro Vijiji na Halmashauri ya Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia kuna ujenzi ambao unaambiwa unataka kujenga chuo cha umeme na gesi asilia Lindi, sitaki wala sina mashaka na Serikali kufanya hivyo. Kuna ujenzi wa kituo cha TEHAMA – Kigoma, sina mashaka na Serikali kufanya hivyo, lakini kuna ujenzi wa kituo cha Afya au Zahanati Dodoma sina mashaka na hilo lakini vilevile Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Morogoro hata sisi Halmashauri ya Morogoro Vijijini wanahitaji huduma hizo. Kama ni suala la Chuo cha Umeme, gesi asilia, kwa nini kisijengwe Morogoro au kikajengwa Pwani? Ninaishukuru Kamati ya Bajeti imeliona hilo na imesema, tunaomba fedha ya CSR ambayo iko ndani ya Halmashauri mbili; ya Morogoro Vijijini na Halmashauri ya Rufiji ije kwetu wananchi wenye halmashauri hizo kama vile utaratibu wa mkataba unavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo na katika hili umeshuhudia hapa mchana leo kutwa nzima Waheshimiwa Wabunge wakizungumza suala la upungufu wa chakula na tatizo la mvua. Tumefanya kazi kubwa kwenye mbolea, mbegu, viuatilifu na kila kitu. Nadhani ni wakati muafaka sasa hivi tukajipanga katika bajeti yetu ijayo katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina maeneo makubwa ya kulima kilimo cha umwagiliaji. Mfano katika Mkoa wetu wa Morogoro, tuna zaidi ya hekta 2,000,000 zinazofaa katika kilimo cha umwagiliaji, lakini kila mwaka Serikali inapokuja inaendelea kuleta bajeti kwenye maeneo ya miradi midogo midogo tu ya umwagiliaji. Nadhani ni wakati muafaka kwa Serikali katika bajeti ijayo, kuangalia miradi mikubwa ambayo italeta tija na wingi wa chakula katika nchi, kitoshe nchini na ikiwezekana tusambaze kwa kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, naiomba Serikali, katika mwaka unaokuja iangalie uwezekano wa kuvuna maji ya mvua. Nilishalizungumza katika bajeti karibu mbili. Kipindi cha mvua, pale Mbande, kuna eneo linaitwa Matoroli, maji yanavuka mpaka juu ya barabara. Pia kipindi cha mvua, pale Mtanana karibu na Kibaigwa, maji yanavuka hadi juu ya barabara. Dumila vile vile mpaka yanafanya uharibifu mkubwa kwenye miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna mabwawa katika station ya reli Msaganza-Kidete. Nadhani ni wakati muafaka kwa Serikali katika bajeti inayokuja ikaelekeza kufukua mabwawa yale, lakini tukachimba mabwawa katika maeneo haya niliyoyasema ili tuvune maji ya mvua, tufanye kilimo cha umwagiliaji ambacho ndicho chenye uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la maji. Niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaifanya katika suala la maji. Karibu tumepata taarifa, maji yamefika vijijini kuna mahali asilimia 80, asilimia 75, lakini uhalisia ni kwamba bado changamoto ya maji ni kubwa katika nchi yetu. Naishauri Serikali yangu, katika bajeti inayokuja, hebu ijielekeze kwenye kufanya miradi mikubwa ya maji yenye uhakika ili iweze kusambaza maji katika maeneo mengi na tukaondokana na adha hii ya maji, kuliko hii miradi midogo midogo ya kuchimba visima, halafu ndani ya kipindi kifupi visima vimekauka; kuchukua maji kwenye mito midogo midogo wakati tuna maziwa makubwa katika nchi hii ambayo tukiyatumia yanaweza kupunguza kero ya maji nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba kwa Serikali yangu, ijitahidi kwa kiasi inachoweza kufanya kufanikisha haya yote ili kuleta tija na mafanikio kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Huo ndiyo ulikuwa mchango wangu. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako. Lakini nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpa pongezi za dhati Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika kupaisha uchumi wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vilevile kukupongeza Mheshimiwa Waziri Ndugu yangu Dkt. Mwigulu, Naibu Mheshimiwa Chande lakini watendaji wa Wizara na taasisi kupitia Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuweza kukamilisha maono yake kwa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu nianze na pongezi. Napenda nitume pongezi za dhati kwa Serikali kwa kuendelea kupeleka fedha kwenye Halmashauri ya Morogoro Vijijini na hususani katika Jimbo langu kwenye upande wa afya tumepokea fedha karibu shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga zahanati Gwata, Kisemo, Mgata na Rukulunge katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata vilevile fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya vifaatiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya na kwenye zahanati. Nimepata fedha lakini vifaa tiba vya shilingi milioni 751 kwenye halmashauri yetu kwenye Hospitali ya Wilaya. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na hata wale watu wanaosema tunaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais hakuna sababu yule mtu ambaye anaejua ukipata una kila sababu ya kushukuru na kupongeza. Kwa hiyo, sisi tutaendelea kupongeza kwa sababu Mama anafanya kazi nzuri lakini na wewe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu unafanya kazi nzuri ya kutafuta fedha kwa kumshauri Mama na kuzileta kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru vilevile kuna suala la ajira tumepokea ajira karibu watumishi 33 kwenye halmashauri yetu upande wa kada ya afya. Tuna kila sababu ya kupongeza katika hilo. Ombi langu kwako Mheshimiwa Waziri na kwenye Serikali ni kwamba pamoja na kazi hii nzuri iliyofanyika kwenye upande wa afya bado tuna changamoto. Changamoto ya kwanza ni gari la wagonjwa kwenye Hospitali ya Wilaya lakini vilevile kwenye Kituo cha Afya cha Tutume. Tungeomba Mheshimiwa Waziri katika mapitio pitio yako angalia uwezekano wa kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna changamoto za gari za hospitali kwenye idara ya afya kwa ajili ya kuweza kufuatilia shughuli za uendeshaji wa shughuli za afya lakini vilevile generator kwenye Hospitali ya Wilaya hatuna. Lakini vile vile kwenye vituo sita hivi ambavyo nimevizungumza hatuna generator, tungeomba tusaidiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile majengo ya OPD kwenye Kituo cha Afya cha Kisemo, Kisaki pamoja na Kinongo. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri utuangalie. Nitumie nafasi hii vilevile kutoa pongezi za dhati kwenye suala la elimu. Ndani ya kipindi hiki kifupi juzi tu tumeletewa shilingi bilioni tatu ambayo itajenga Shule Maalum ya Wasichana kwenye Kata ya Bwakila Chini ambayo itaanzia O level hadi A level. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais lakini tukupongeze wewe Waziri unayefanya kazi kwa dhati katika kufanya kazi hii. Lakini tulipata juzi tena shilingi bilioni 750 kwa ajili ya Mradi wa Boost katika kuendeleza shule zile ambazo zilikuwa kongwe. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri lakini vilevile kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali kwa upande wa elimu pamoja na walimu kupatikana tuendelee kupata walimu wengine. Bado tuna upungufu wa walimu kwenye maeneo hasa ya pembezoni kwenye halmashauri yetu, kata za milimani Singisa, Kisaki na kwenye maeneo mengine. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri uone jinsi gani ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi kukupongeza sana Mheshimiwa Waziri kwenye hili suala la kufuta ada kwenye vyuo vya ufundi. Nimetokea kwenye vyuo vya ufundi, nimeajiriwa railway, nilikwenda kusoma Railway Training College mpaka nimemaliza nilipofikia hapa. Sasa kwa kufuta ada kwenye vyuo vya ufundi ambavyo umevitaja DIT, MUST na Arusha Tech tunaenda kutengeneza wataalamu wengi ambao watakwenda kulisaidia Taifa lakini ombi langu kwako hebu tuviangalie Chuo cha NIT nacho tunakokwenda. Tuangalie Chuo cha Reli vilevile tunakokwenda. Kule nako tunaweza tukasaidia sana vijana wetu wakaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye suala la kilimo niipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya kwenye kuwekeza kwenye kilimo lakini ombi langu kwa Serikali kutokana na tabianchi inavyoendelea uharibifu bado kutegemea kilimo cha mvua hatutaweza kufanikisha katika dhana ya kupata chakula kingi katika nchi kwa faida ya chakula cha ndani na cha kuuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tuangalie kwenye suala la uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji. Katika yale mabonde mwaka jana nimechangia kwenye Bajeti kuna mabonde pale Kilosa, kuna mabonde hapa tukitoka hapa kuna Kibaigwa, kuna suala la Mto Dumila lakini hata Ruvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie tukachimbe mabwawa, watu wafanye kilimo cha umwagiliaji ili tutoke kwenye lile lakini kwenye suala la kilimo niombe na nadhani Ndugu yangu Bashe yupo. Mwaka huu Morogoro tumebahatika kupata ufuta mwingi sana lakini umeingizwa kwenye suala la stakabadhi ghalani wakati watu hawajajiandaa lakini vile vile hata hiyo Serikali haijajiandaa. Imeleta taharuki na changamoto kubwa. Niwaombe Wizara ya Kilimo hebu kwa mwaka huu tuacheni wananchi walime ufuta wao na wauzie watu wanaowataka ili waondokane na adha ambazo wanazipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye suala lingine Mheshimiwa Waziri nikuombe. Kuna suala la CSR la Bwawa la Mwalimu Nyerere. Nakumbuka nilikufuata uliniambia tumtafute Waziri mwenye dhamana hatukuweza kumpata lakini juzi wakati nachangia nilichangia majibu waliyonipa hayakutupa matumaini watu wa Rufiji na watu wa Morogoro Vijijini. Nikuombe wakati unachangia; je, sisi watu wa Morogoro Vijijini ambao na Rufiji ambao ndiyo tunafanya kazi kubwa ya uhifadhi lakini tunafanya kazi kubwa ya kuangalia huo mradi. Je, tunapata nini? Tuelewe ili twende tukapange na tukuleteeni kwamba tusaidieni hiki na hiki na hiki wananchi wetu wapate kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee vilevile kuzungumza kwenye suala la kodi. Mimi ni mfanyabiashara, siyo mkubwa sana lakini ni mfanyabiashara. Bado tuna changamoto kwenye sheria zetu za kodi. Mheshimiwa Waziri unazungumzia suala kwamba hakuna kufunga maduka, hakuna kufunga account, Mheshimiwa Rais alisema jambo hili. Mimi ni mhanga, mwaka huu nimefungiwa account bila sababu yoyote ya msingi. Niangalie na nikuombe lazima tukae na wafanyabiashara. Kaa na wafanyabiashara katika Sekta mbalimbali wa Kilimo, wafanyabiashara wa mahoteli, wafanyabiashara wakandarasi tuone jinsi gani tunaweza tukachangia wote kwa pamoja tutokaje hapa tulipo ili watu waweze kulipa kodi bila shuruti lakini kodi ambayo itaenda kuleta maendeleo makubwa kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii habari ya kusema tumefunga, hao watu wa TRA kupitia sheria ambazo zimetunga ukifika wanakwambia hayo ni mambo ya siasa na kwa kusema mambo ya siasa kwa kauli yako Waziri maana yake wanakufedhehesha wewe. Lakini vilevile Rais akisema kwamba hili lisifanyike watu wakifanya ukienda wanakwambia ni mambo ya kisiasa vilevile tunamvunga nguvu Rais wetu lakini tunamchonganisha Rais na wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kama kuna suala linawapa mandate watu wa TRA kufunga hizi maduka tuletee hapa tuangalie jinsi gani ya kuifanya tuondoe ili hizi kauli mnazozitoa ziende sambamba na hayo ambayo tunayataka kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikuombe kwenye suala la kupandisha cement. Naamini kabisa tutaenda kupeleka maisha magumu kwa Watanzania. Kuna maeneo mengi ya kuangalia na bahati nzuri kuna hili ambalo limezungumzwa ETS. Nilishauri siku za nyuma lilipoanza lilikuwa katika maeneo madogo lakini sasa hivi kama alivyotoka hata Engineer Chiwelesa kuzungumza limekwenda kwenye cement liende kwenye nondo, liende kwenye maeneo mengi tukajihakikishe kwamba kile kinachozalishwa kule je, kinafanana na kile tunachopewa? Tukiweza kujiridhisha matokeo yake nini? Tutaenda kuendelea kukusanya kodi nyingi ambazo upo uwezekano tusiende tukaingiza gharama kwenye cement twende kuingiza gharama kwenye nondo ambazo tutaenda kuwatilia wananchi wetu washindwe kujenga majengo mazuri vilevile washindwe kufanya mambo mengine ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye suala la kodi nakuomba sana, nakuomba sana bado kuna changamoto. Umezungumza mwenyewe wafanyabiashara ni wachache lakini mahitaji ya Serikali ni makubwa. Bado tunaweza kwenda ndani zaidi kutafuta wafanyabiashara wengine ambao watasaidia hawa ambao wamejiandikisha ambao wana mzigo mkubwa na unawaumiza wanashindwa kwenda mbele na mwisho kama tutaendelea hivi hata hawa tuliokuwa nao milioni nne tunaweza tukawapoteza na Serikali ikaingia katika wakati mgumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu, hoja ya Wizara ya Maji, Wizara yenye umuhimu mkubwa sana katika maisha ya watanzania. Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu kwa kazi kubwa ya kutoa fedha kwenda katika wizara hii ili kuweza kumtua ndoo mwanamama lakini kuhakikisha kwamba maji ni uhai yanatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza ndugu yangu Aweso msaidizi wake mama yangu Christina, Engineer Sanga Mtendaji Mkuu wa Wizara lakini kubwa zaidi Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro na Mhandisi Meneja wa Wilaya, Wilaya ya Morogoro Vijijini kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii katika kukamilisha kiu ya Watanzania katika kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, ni mtu ambaye hana akili au asiyeona, lakini kwa yoyote anayeona kazi kubwa ya mapinduzi katika sekta ya maji ndani ya kipindi kifupi anakila sababu ya kujua kwamba kuna mambo mazuri yanafanyika. Nitumie nafasi hii cha kwanza mfano kwenye jimbo langu la Morogoro Kusini kuna mradi wa Bwakila juu tumepata milioni 680, kuna mradi wa Lundi tumepata milioni 492, kuna mradi wa Mvuha huu ni mradi kupitia UVIKO tumepata milioni 680, ukijumlisha kuna bilioni 1.772. Kwakweli tunakila sababu ya kuipongeza Serikali na kuipongeza Wizara kwa kuhakikisha kwamba haya mambo ambayo Serikali inataka yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile kwenye jimbo langu kuna ukarabati wa mradi wa Singisa tumepata milioni 60 ahsante sana Mheshimiwa Waziri, lakini mradi wa Matombo
- Lugeni tumepata milioni 100 kwaajili ya kukarabati, tunakila sababu ya kupongeza.

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi nimpongeze waziri kupitia mradi wa Bonde tumejengewa mabirika 10 na vizimba zaidi ya 20 kwa ajili ya kunyweshea maji mifugo lakini vile vile wale wananchi wa jamii ya wafugaji kupata maji safi na salama tuna kila sababu ya kupongeza. Tumechimbiwa visima viwili virefu Kata ya Milengwelegwe na Mngari tunakila sababu ya kupongeza, mimi kama mbunge wao napongeza kwa kazi kubwa nakupongeza ahsante sana mdogo wangu Aweso kwa kazi kubwa ambayo unaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu pamoja na pongezi bado tunachangamoto za maji. Katika Kata ya Selembala, kuna Vijiji vya Kiganyira, Magogoni, Mji Mpya na Bwira Juu. Huko ndiko kwenye Bwawa la Kidunda tunapokwenda kujenga. Tumewatoa wananchi kwenye maeneo ambao walikuwa na maji yao sasa hivi wanakwenda mtoni kuchota maji wanakumbana na adha ya kukamatwa na mamba. Ninakuomba tupatiwe visima. Lakini vile vile Kata ya Bwakila chini kuna Vijiji vya Dakawa, Sesenga, Vigolegole, Kichangani Kata ya Kisaki na Nyalutanga tunaomba mtusaidie visima vya maji ili wananchi wetu wapate maji safi na salama na sisi tufikie azma ya Serikali ya kupata maji safi na salama tutakapofikia mwaka 2025 kama vile Serikali inavyosema.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Waziri wa Maji; kuna vijiji vya Mtombozi, Lugeni, Kisemu, Gozo Kibangile na Mtamba kuna matatizo makubwa ya maji. Idara ya Maji kupitia RUWASA na mkoa tayari walishafanya upembuzi yakinifu. Kuna mto unaitwa Kibana una uwezo wa kusababisha vijiji vyote hivi vikapata maji safi na salama. Tayari walishaandika proposal na ipo kwenye Ofisi ya Mkoa inahitaji kama bilioni tatu tu. Nikuombe Waziri angalia kwa namna moja au nyingine unaweza kutusaidia vipi tuondokane na adha hii ya maji. Mimi naamini kabisa miradi hii ikikamilika wananchi wetu watapata maji safi na salama, lakini kubwa zaidi wataweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vile vile nikuombe Mheshimiwa Waziri umetusaidia katika kupitia mradi wa UVIKO mradi wa mvua ambao ndiyo Makao Makuu ya Wilaya yetu ya Morogoro Vijijini, pale tayari kuna mradi ambao unatakiwa ufanyike lakini kama mkiweza kutuongezea fedha kiasi kama cha milioni 200 mradi ule kwa kujenga tank kubwa, ambapo lililokuwa designed ni dogo, utaweza kufanikisha maji kufika katika Kijiji cha Sangasanga, Tulo, Lukulunge na hapo tutaenda kuwasaidia wananchi wetu kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze mdogo wangu Aweso na Wizara kwa safari hii kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga Bwawa la Kidunda. Ni uhalisia suluhisho la upatikanaji wa maji wa Jiji la Dar es salaam, Pwani na hata baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Morogoro ni kujenga Bwawa la Kidunda. Bwawa la Kidunda lipo katika Jimbo la Morogoro Kusini katika Kata ya Selembali.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali, tunakwenda kujenga mradi mkubwa ambao unatakiwa ulete matokeo chanya; sijui Serikali tumejipangaje katika uhifadhi wa mazingira ili kuruhusu vyanzo vya mito ambayo inajaza maji katika Mto Mvua iendelee kuwa endelevu.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwako Mheshimiwa Waziri katika hatua za muda mfupi na katika mabonde walivyoonyesha katika jitihada za kutengeneza mabirika ili mifugo isiende mtoni tungeweza kusaidia mkachimba mabwawa ng’ombe wakaenda kupata hifadhi ya maji kwenye mabwawa badala ya kwenda mtoni kuharibu kingo za mto, lakini wakati wa kiangazi wakapanda juu kwenda kwenye vyanzo vya mito ambavyo wataenda kuharibu mazingira. Matokeo yake, nataka tu kuthibitisha, kama hatukuangalia hili hata huu mradi tutakuwa tumepoteza fedha bure ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Waziri, nimetoa angalizo kwa sababu ya uzoefu wangu kama Mbunge katika eneo lile. Na ushuhuda wewe mwenyewe unajua; mwaka huu huu Dar es Salaam walikosa maji. Lakini walikosa maji si kwa sababu Mto Ruvu ulikauka, hapana, ni kwa sababu vyanzo vya mito mitano ya Ngazi, Mto Mvua, Mto Dutumi, Mto Mgekakafa ilivamiwa na wafugaji juu kwa ajili ya kuokoa mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo Mheshimiwa Waziri nikuombe tu, katika huu mradi wa mabirika 10 karibu tunamaliza, ambao umejengwa na bonde, nikuombe wewe nawe ukipata muda twende tukazindue wote kwa pamoja ili kazi iendelee kuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho zaidi kabisa nikushukuru kwa kazi kubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Nitumie nafasi hii pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuweza kusimama nikiwa na afya tele kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu katika uwakilishi wangu kwa wananchi wangu waliopo katika Jimbo la Morogoro Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yako nzuri ambayo umeitoa hapa Bungeni ikionesha yale ambayo yalifanyika katika kipindi kilichopita lakini mwelekeo wa Wizara yako katika kuyafanyia yale yanayotakiwa kufanywa na Serikali katika mwaka huu wa fedha unaokuja. Nitumie nafasi hii vilevile kumpongeza Mama yetu Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuwaletea maendeleo Watanzania. Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano ni mashahidi, mambo ambayo yanafanyika katika Majimbo yetu ni historia ambayo kwa kweli kila Mbunge anashangaa maana ndani ya miaka miwili kuna mambo makubwa ambayo yamefanyika. Tuna kila sababu ya kumpongeza, kumpa moyo lakini kuwa sambamba na yeye katika kufanya yale ambayo anayahitaji yafanyike kwa maendeleo ya Taifa hili la Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuchangia kwenye suala la barabara. Ninaipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika ujenzi wa barabara ya Bigwa - Kisaki. Barabara ya Bigwa - Kisaki ni barabara muhimu ambayo inakwenda kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere pia inakwenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Toka tumepata uhuru ilikuwa ni historia lakini kwa mwaka huuu wa fedha Serikali yetu imetenga fedha kujenga kwa kiwango cha lami kilometa 78, tender hiyo ilitangazwa tarehe 20 Januari na juzi tarehe 5 Aprili tenda imefunguliwa wako Wakandarasi ambao wanachujwa ili kazi ianze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali lakini kubwa zaidi niiombe Serikali hasa Wizara ya Ujenzi na TANROADS waharakaishe mchakato wa kupata Mkandarasi ili kazi ianze mara moja na Watanzania ambao wako kule Morogoro Kusini, Morogoro Kusini Mashariki na Wilaya ya Morogoro na wao waone matunda ya uhuru kwa kuweza kupita kwenye barabara ya lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niishauri Serikali yangu na kuiomba Serikali tufanye upembuzi yakinifu wa barabara ya Ngerengere kwenda Mvua na Mvua kwenda Kisaki ili nayo ijengwe kwa kiwango cha lami, kwa sababu barabara zote hizi ni muhimu, ni barabara ambazo zinakwenda kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere na Bwawa la Mwalimu Nyerere, tukiweza kukamilisha kufika huko kwa kiwango cha lami tuna uhakika watalii watakwenda, tutaongeza pesa nyingi za kigeni kwenye Serikali ambazo zitasaidia kuleta maendeleo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kikubwa ambayo wameifanya katika kuleta fedha za maendeleo katika upasuaji wa barabara kwenye eneo la TARURA. Katika mwaka wa fedha uliokwisha tumepata takribani bilioni 4.13 katika utengenezaji wa barabara kazi inaendelea. Ombi langu kwa Serikali kiuhalisia jiografia ya Jimbo la Morogoro Kusini ni Jimbo ambalo liko milimani fedha hii ambayo imekwenda imetosheleza kwa kiasi lakini bado kuna uhitaji mkubwa, ninaiomba Serikali yangu ikiwezekana katika bajeti inayokuja hii kupitia TAMISEMI, TARURA waongezewe bajeti, ikiwezekana ifike hata bilioni saba tuweze kwenda kupasua barabara za milimani kama vile Singisa, Kasanga, Kolero, Bwakila Juu, Kibogwa ili barabara zifikike maendeleo yapatikane kwa urahisi. Vilevile ninaomba Serikali kuna bajeti tumeomba ombi maalum la billioni moja kwa ajili ya barabara ya Bwakila Juu - Dakawa niombe Serikali itusaidie fedha hizo ili walau tuweze kufanikisha katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwenye suala la elimu tumefanya kazi kubwa sana. Kwa mara ya kwanza nadhani Wabunge mtakuwa ni mashahidi miaka yote kila tunapofika mwishoni mwa mwaka huwa tunakuwa na operation maalum kwa ajili ya kuwachangisha wazazi ili watoto waende shule form one inapofunguliwa, ndani ya miaka miwili hii chini ya Mama Samia Suluhu Hassan hakuna mzazi ambae amebughudhiwa. Madarasa yalipelekwa na watoto wote walianza kwa mara ya kwanza wote hakukuwa na walioingia awamu ya kwanza, hakukutokea na walioingia awamu ya pili wote waliingia kwa awamu moja, tuna kila sababu ya kumpongeza Mama katika haya na tupo nyuma yake tunamuunga mkono katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali ni kwamba pamoja na mafanikio haya bado kuna changamoto, bado maboma mengi ya nguvu za wananchi ambayo yamejengwa yanahitaji kumaliziwa. Vilevile bado kuna uhitaji wa vyumba vya madarasa, ninaiomba Serikali yangu ihakikishe kwamba mambo haya yanafanyika ili watoto wetu waweze kusoma kwa nafasi na kuweza kupata elimu iliyo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika maeneo ya pembezoni kama vile kwangu Jimboni Kata ya Kolero, Kata ya Kasanga, Kata ya Kibogwa, Kata ya Singisa na Bwakila Juu, kuna uhitaji mkubwa wa mabweni kutoka katikati ya Kata kwenye shule ya sekondari mpaka kwenda kwenye vijiji kuna mwenda ambao unatumika pengine zaidi ya masaa matatu, manne watoto wetu wanashindwa kwenda na kurudi, matokeo yake nini? Wanakwenda kujipangisha kwenye vijumba ambavyo hakuna ulinzi wa watoto. Kama hivi tunavyopiga kelele maadili na nini, kwa hiyo ninaiomba Serikali ihakikishe kwamba inatutengea mabweni walau mawili mawili kwenye kila shule za sekondari katika bajeti ili watoto wetu wapate utulivu wa kusoma na kukaa katika usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala afya Serikali imefanya kazi kubwa. Ninaipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, kwenye Wilaya yangu hospitali ya Wilaya tumekamilisha, tuna kila sababu ya kupongeza katika hili. Pia Vituo vya Afya Sita vimekamiliaka, maboma Kumi yamemalizwa ya zahanati ambayo ilikuwa nguvu za wananchi zilikuwa zimetumika kulikuwa kuna uhitaji wa Serikali kuongeza, tuna kila sababu ya kupongeza Serikali katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto ambayo ninaiomba Serikali yangu ya vifaatiba vya upasuaji,majengo ya OPD kwa Kituo cha Afya cha Kisemu, Kisaki, na Mikese, vilevile Watumishi bado ni wachache, kuna hela ambazo tuliahidiwa Halmashauri ya Morogoro Vijijini milioni 500 kwa ajili ya vifaatiba kwenye Hospitali ya Wilaya, milioni 300 kwa ajili ya vifaatiba kwenye vituo hivyo nilivyovitaja vya afya na shilingi milioni 150 kwa ajili ya zahanati. Ninaiomba Serikali tuleteeni fedha hizo tukamilishe haya yanayotakiwa kupata ili Watanzania dhamira ya Serikali ya kuwapatia afya inayostahili ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwenye suala la utawala…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. INNOCENT E. KALOGERES: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia katika bajeti ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 katika Wizara hii nilikamata Shilingi, na niliahidiwa ahadi nyingi tu na Mheshimiwa Waziri aliyetangulia, lakini mdogo wangu Mheshimiwa Ulega, yeye ndiye alikuwa Naibu Waziri katika Wizara hii. Katika yote niliyoahidiwa, ni moja tu ambalo nimelipata. Bahati mbaya sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha hayupo, lakini siku hiyo yeye ndio alikuwa amenipa ushawishi mkubwa sana katika kusema kwamba, shida kubwa ya wafugaji ni malisho, shida kubwa ya wafugaji ni maji. Serikali imenunua mitambo mikubwa, adha hiyo ambayo mwaka ule ilipatikana, kwa mwaka huu haitapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliambie Bunge lako Tukufu, hadi tunapozungumza leo hii, wakulima na wafugaji bado wana migogoro mikubwa inayotokana na wafugaji katika kutafuta malisho na maji. Napata shaka, niliambiwa mwaka ule nisubiri mpaka mwaka huu. Naomba nitangaze tu, nina dhamira ya kushika shilingi ya Waziri wakati utakapofika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliahidiwa majosho kumi, mpaka dakika hii nimepata majosho manne tu. Niliahidiwa mabwawa mawili, mpaka tunazungumza dakika hii, hakuna hata bwawa moja ambalo limechimbwa. Niliahidiwa visima, hakuna hata kisima kimoja. Vilevile tuliahidiwa kupata madume bora ya nyama kwenye Halmashauri ya Morogoro Vijijini, hakuna kitu kama hicho. Ni kielelezo tosha kwamba Serikali haiwezi kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ushauri kwa Serikali. Cha kwanza, ninaamini na ninaomba, sisi Wabunge tupambane wote hapa, hasa kwenye sekta ya mifugo; wale Wabunge ambao mikoa yao wanatoka wafugaji, tuone ni jinsi gani tunaishauri na kuishawishi Serikali, katika kipindi ambacho ni cha siku zile tano, Serikali na Kamati ya Bajeti wanakaa, na bahati nzuri Mwenyekiti ambaye leo unaongoza kikao ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, tuone jinsi gani tunasaidia sekta ya mifugo kuongezewa fedha ili iweze kukabiliana na changamoto za migogoro ya wakulima na wafugaji, na changamoto wanazozipata wafugaji wetu katika kuhamahama ambapo inawaletea hasara kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, amekuja na hoja ya kusema kwamba anataka kuanzisha mamlaka maalum ambayo itashughulikia matatizo au changamoto za wafugaji na wavuvi. Kwa ushauri wangu, tulikuwa na changamoto kwenye barabara, maji, na umeme. Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri, hebu tusiende kwenye mamlaka, twende kwenye wakala. TARURA, imeondoa changamoto za barabara katika nchi yetu, lakini RUWASA imeondoa changamoto za maji, ndiyo maana sasa hivi Waziri wa Maji anatamba. Kwa hiyo, nakuomba na wewe, badala ya kwenda kwenye mamlaka, twende kwenye wakala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na changamoto kubwa za upatikanaji wa umeme katika nchi hii, vijijini hata mijini, lakini kupitia REA, leo kila Mbunge anapata faraja na wananchi wanaona kazi ambayo inafanywa na REA. Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Waziri, kwenye suala la mamlaka, tusiende kwenye mamlaka, twende kwenye wakala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuishauri Serikali yangu, hebu tuangalie, sasa hivi wafugaji wanapata wakati mgumu, na vilevile hata watumiaji wengine wa ardhi. Angalieni uwezekano wa kukutana na Wizara ya Maliasili na Utalii, na Wizara ya Ardhi, twende tukaweke mipaka kwenye maeneo ya hifadhi. Wafugaji na wakulima, hawana GPS. Utajikuta ghafla bin vup, wameingia ng’ombe kwenye hifadhi, wakulima wameingia kwenye hifadhi, wanapata fine kubwa ambazo zinawapa wakati mgumu wafugaji na wakulima wetu. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu tuangalie katika mwaka huu wa fedha, jinsi gani Wizara tatu; Ardhi, Wizara yako ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Maliasili na Utalii, mwende mkaondoe chagamoto ambazo wanapata wafugaji na wakulima wetu katika maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile namwomba Mheshimiwa Waziri, sijajua katika mwaka huu wa fedha mmetenga kiasi gani cha fedha kwenda kuendelea kutafuta maeneo ya malisho. Nimeona katika bajeti yake amesema kuna maeneo 77 yamepatikana ambapo zimepatikana hekta 994,827, lakini kuna Wilaya 14, Wizara ya Ardhi imetenga maeneo ya ardhi, naomba tuendelee kutenga kuweka fedha, ili tuendelee kutenga maeneo makubwa tuondokane na matatizo ya malisho na maji kwa wafugaji wetu na vilevile watumiaji wengine wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania bado ni kubwa. Ninaamini kabisa kwamba, tunaweza kuwa na maeneo mengine kama tulivyofanya pale Handeni, kama Serikali itajipanga vizuri. Katika hili naomba tu, Mheshimiwa Waziri, wewe ndiye mwenye dhamana hii. Waziri wa Maliasili katika kuinusuru Ngorongoro, alishirikisha Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Ardhi na wewe Waziri wa Mifugo mkaweza kupeleka kule ng’ombe. Sasa nakuomba, bado tuna changamoto, migogoro mikubwa itaendelea kutokea, lakini pamoja na migogoro tunaipeleka nchi kwenda kwenye jangwa. Lazima tuandae maeneo ambayo tutapeleka wafugaji wetu kwenda kufanya shughuli zao za mifugo bila migogoro yoyote kwa wananchi, na wao bila kupata hasara kwenye maeneo yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Innocent. Muda wako umeisha. (Makofi)

MHE. INNOCENT E. KALOGERES: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu katika Wizara ya Maji, Wizara ambayo ni muhimu katika ustawi wa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha kwamba, huduma ya maji inaendelea kuboreka nchini, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Sisi Wabunge tumekuwa mashuhuda nadhani kwamba, kila Mbunge anaponyanyuka anampongeza Mheshimiwa Aweso na wasaidizi wake na watendaji wote katika Wizara yake, nami nifanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii, cha kwanza nieleze Bunge lako tukufu kwamba, chanzo cha maji katika Mto Ruvu ambao ndio juzi katika semina tulielezwa pale na Mheshimiwa Waziri kwamba, asilimia 76 ya uchumi wa viwanda katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani unategemea Bonde la Mto Ruvu. Mto Ruvu unaanzia katika Mto unaoitwa Mbezi unaanzia katika Kata ya Kibogwa, lakini vilevile kuna Mto Mfizigo ambao unatoka kwenye Kata ya Kibungo Juu, kuna Mto Mvuha unatoka Kata ya Bungu, kuna Mto Dutumi unatoka Kata ya Kolelo, lakini kuna Mto Mngazi unatoka Singisa na kuna Mto Mgeta Kafa unaotokea huko huko Singisa. Mtiririko wa maji hayo ndio unaofanya kwamba, ustawi wa Mto Ruvu ukamilike na wenzetu wa Dar es Salaam waendelee kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina simanzi kidogo, sisi ambao ndio tunatunza vyanzo vya maji, lakini sisi tunashindwa kupata maji. Sisi tunaotunza vyanzo hivyo vya maji, sisi ndio hatupati maji, tunaendelea kupata miradi midogo midogo ya milioni mia tatu, mia nne, mia tano, mia sita, lakini unakuja kuangalia wenzetu ambao wanafaidika kwa sisi ambao tumewatunzia wanatengewa miradi mikubwa. Mheshimiwa Waziri nakumbuka alikuja jimboni nilimweleza, tuna mradi unaoitwa Kibana Group Water Project ambao ulikuwa unahitaji bilioni 7.8, aliniahidi kwa kujua umuhimu kwamba, sisi ndio tunaomtunzia maji, aliniahidi kwamba, kama tutashindwa kufanya kwa wakati mmoja, basi atanifanyia walau kwa awamu mbili, angenipa bilioni nne baadaye angenipa bilioni tatu mradi huo ukamilike.

Mheshimiwa Spika, katika kitu cha kushangaza na kuumiza sana kwa wananchi wa Morogoro Kusini, Halmashauri ya Morogoro, ndani ya bajeti tukaonekana kwamba, mradi huo haufanyiki. Nilienda ofisini kwake na watendaji wangu akaniahidi kwamba, tutaufanya na akasema twende tukaweke fedha, walau token, ili mradi ukamilike. Imewekwa milioni 200, nimwombe Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana sana tunauhitaji Mradi wa Kibana ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu ukikamilika unahitaji fedha ndogo, kama tunaweza kupeleka Dar es Salaam mabilioni kwa billions of money, juzi kwenye semina unaangalia kuna mahali kuna watu wanapata bilioni 90, kwa nini sisi watu wa Morogoro Kusini? Kwa nini sisi watu wa Halmashauri ya Morogoro tusipate mradi wetu huo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitaki kusema kwamba, nitakamata shilingi, lakini naamini Waziri ni mtu mwenye hekima, ana busara. Tumekaa na watendaji wake, lile jambo ambalo ameliahidi wakati ana-wind up naomba aje athibitishe ndani ya Bunge kwamba, tutapata maji au hatupati kupitia mradi wetu wa Kibana ili wananchi wangu wa kata nne, vijiji 12 wakapate huduma hiyo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine kuna Mradi wa E-Water, kuna wadau wamekubali kuweka bilioni 1.5 ili Vijiji vya Mirengwerengwe, Kijiji cha Mngazi na Dakawa waweze kupata huduma ya maji. Watu hawa wanachotaka ni commitment ya Serikali na kutupa kibali, ili watumbukize fedha hiyo, wananchi wapate maji na mradi huu ni mradi ambao utakuwa unarudisha fedha. Katika makubaliano na vijiji hivi ninavyovitaja na wananchi tumekubaliana kwamba, ndoo itauzwa kwa shilingi 100. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, watupe hicho kibali, hawa wadau wakatumbukize fedha za maendeleo, wananchi wapate huduma hiyo, lakini kama wanadhani kwamba, kwa mujibu wa Sera inapingana, basi tunaomba watupatie hiyo bilioni 1.5, wananchi wangu hawa wakapate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nizungumzie Bwawa la Kidunda. Niipongeze Serikali kwa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kwa sababu, ujenzi wa Bwawa la Kidunda ndio itakuwa suluhisho la uhakika wa upatikanaji wa maji safi na salama Dar es Salaam. Naomba nitoe angalizo kwa Wizara, tunaenda kutumbukiza fedha nyingi kwenye mradi huu, ni vizuri tukaangalia uhifadhi wa mazingira. Mkoa wa Morogoro una bahati ya malisho, una bahati ya maji. Matokeo yake kipindi cha kiangazi wafugaji wanavamia vyanzo hivi nilivyovitaja vya Mto Ruvu na kuweza kukausha maji katika Mto Ruvu.

Mheshimiwa Spika, sasa nimwombe Waziri kupitia DAWASA, kupitia Bonde, tukaangalie jinsi gani tunaisaidia Halmashauri ya Morogoro Vijijini na Ofisi ya DC katika kutunza vyanzo hivi vya maji. Haiwezekani tunatoa hela sisi kama Halmashauri za own source kwa ajili ya kutunza maji ambayo yanakwenda kupata uhifadhi Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna Mradi wa Umwagiliaji wa Kongwa Turo. Mwaka jana, mwaka juzi, ulifungwa wakati water right users wanalipia, lakini unafungwa kwa ajili watu wa Dar es Salaam wapate maji. Kwa hivyo, nimwombe Waziri nahitaji watu wangu wapate nao kutumia maji hayo ambayo wanayatunza, lakini vilevile tunaomba uhifadhi wa mazingira ufanyike ili kuweza kulitunza hilo Bwawa la Kidunda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, watu wa DAWASA, mwaka jana wakati tunachangia bajeti, kuna mambo ambayo ni ya msingi kwa wananchi wangu wa Kata ya Serembala, bado hawajapata toka tumekubaliana wakati tunakubali kuhama ili kupisha ujenzi wa bwawa. Kuna makaburi yao hawajalipwa, kuna Kituo cha Polisi hakijajengwa, kuna maji hayajakwenda; nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati ana- wind awaambie watu wa DAWASA, tunataka tumalizane kwa pamoja. Nilimwona Mtendaji wa DAWASA akaniambia kwamba, anasubiri tutakwenda.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 tunakabidhi Mwenge, kama Mkoa wa Morogoro. Mheshimiwa DC wangu yuko tayari, mimi Mbunge na mdogo wangu Mheshimiwa Tale tuko tayari, tunataka twende tukamalizane, ili kusudi mradi huo uanze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nimwombe Mheshimiwa Waziri, jana hapa mdogo wangu Mheshimiwa Tale alisema, sisi tunatengeneza hilo bwawa kwa wenzetu wa Pwani na Dar-es-Salaam wafaidike. Tunataka na sisi bwawa hili litusaidie kwa vijiji jirani, lakini maji ikiwezekana yafike Mvuha kwenye Makao Makuu ya Halmashauri yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara muhimu katika uchumi wa Taifa letu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kufungua uchumi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbarawa na wasaidizi wake, Naibu wa Ujenzi na Naibu wa Uchukuzi, lakini vile vile na watendaji wote ambao wapo chini ya taasisi katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii nianze mchango wangu kwa TANROADS. Nimpongeze Mtendaji Mkuu wa TANROADS lakini vile vile nimpongeze Meneja wa Mkoa wa Morogoro wa TANROADS kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika ujenzi wa barabara na madaraja yanayoendelea hapa nchini. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kujenga Barabara ya Bigwa – Kisaki kilometa 78 na madaraja mawili kwa kiwango cha lami, lakini vile vile kwa kujenga Barabara ya Ubena Zomozi – Ngerengere kilometa 11 kwa kiwango cha lami, lakini pia kufanya upembuzi yakinifu kwa ili kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Ngerengere – Mvua hadi Matemele kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kumpongeza Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi ya kuweza kujenga barabara hii. Kiuhalisia wananchi wa Morogoro, Wilaya ya Morogoro ambayo ina majimbo matatu, Jimbo la Morogoro Mjini, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na Jimbo la Morogoro Kusini. Hii ni historia toka tumepata uhuru tulikuwa tunasikia lami kwa wenzetu, lakini kwa mara ya kwanza sasa tunajenga lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ametuambia mpaka kufikia mwezi Juni, mkandarasi atatia saini ya ujenzi. Ombi langu tunaomba kazi hii ya kutia saini mkandarasi na Serikali ifanyike kwenye Wilaya ya Morogoro kwenye eneo lolote katika majimbo hayo matatu ili wananchi wajue kwamba kweli Serikali iko kazini na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vile vile kuishauri Serikali kwenye TANROADS pamoja na kazi nzuri ya ujenzi wa barabara na madaraja lakini tunahitaji vile vile kutunza barabara. Nimwombe Mheshimiwa Waziri tuangalie jinsi gani tunaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa matengenezo ya mara kwa mara kwenye madaraja yetu na barabara zetu ili hizi barabara ambazo tunazitengeneza kwa gharama kubwa ziendelee kudumu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwa TANROADS watumishi bado ni wachache, vitendea kazi bado ni vichache, lakini vile vile hata vifaa vya kupima ubora wa kazi ni vichache. Nimwombe Mheshimiwa Waziri tuendelee kutenga fedha nyingi kwa TANROADS ili watumishi wapatikane, vitendea kazi viwepo, lakini vifaa vya kupima ubora wa kazi wa fedha nyingi ambayo tunatumbukiza katika ujenzi wa barabara iwe imekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri mimi ni mkandarasi, naomba ku-declare interest. Tunatumia fedha nyingi sana kutajirisha wakandarasi wa kigeni, lakini kwa mara ya kwanza naamini ushauri wa Kamati ya Miundombinu ambayo na mimi ni Mjumbe inaoneka Mheshimiwa Waziri ameusikiliza. Nimeona katika ukurasa wa Kitabu cha Bajeti, ukurasa wa 44 kuna miradi minne ambayo imetengewa wakandarasi wazawa, lakini kuna miradi mitano ambayo imetengewa wakandarasi wazawa wa kike, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa inaonesha tunataka kujenga uchumi uendelee kubaki nchini kwetu, lakini kuwatengeneza wakandarasi wetu sasa na wao waweze kutoka hata nje ya nchi kama Wachina wanavyotoka wakafanye kazi kule wakalete fedha nchini na kujenga uchumi wa kwetu. Ombi langu, wakandarasi tuna tatizo moja Mheshimiwa Waziri, tuna tatizo wa kuwa na utaalam wa contract management, lakini tuna tatizo la utalaam wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri katika miradi hii minne ya wakandarasi wazawa, wanaume lakini hii miradi mitano ya wakandarasi wazawa wa kike, atengeneze utaratibu wa kuhakikisha kwamba kila mradi utakuwa na Mkandarasi Mshauri wa kuweza kuwasaidia wakandarasi hawa wazawa, lakini vile vile kuhakikisha kwamba fedha inapatikana wasiwe wanasuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tulijaribu kwenye Daraja la Sibiti, lakini tumejaribu kwenye Barabara ya Ludewa – Kilosa, tumewapa wakandarasi lakini wakandarasi hawa wamepata wakati mgumu katika kufanya kazi hiyo kwa sababu ya ukosefu wa utaalam katika uendeshaji wa miradi, lakini fedha za kufanya kazi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri aangalie hili alisimamie vizuri kama alivyosimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nizungumzie kwenye TPA. Wabunge wote wanaridhia, nami naridhia, hatuna sababu ya uoga katika hili la kutafuta wawekezaji katika bandari yetu. Bandari ni lango ambalo linaenda kuleta fedha nyingi katika nchi hii. Tumekwenda Dubai, wengine wamekwenda India tumeshuhudia tumeona wenzetu wanavyofanya, sasa tuna sababu gani ya kuogopa? Hatuna sababu ya kuogopa. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atuletee sheria Bungeni, tutunge sheria ili kusudi tuingize Sekta Binafsi kwenye bandari, waweze kuleta fedha na uchumi wa nchi yetu uweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie TRC, kazi kubwa imefanyika na Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Vipande vyote vya Reli vya SGR vina wakandarasi na wako kazini. Ombi langu kwa Serikali, tukikamilisha reli hii tunatarajia kusafirisha tani 17,000 kwa mwaka. Ombi langu ni moja, tukitegemea kwamba Serikali ijenge miundombinu, inunue mabehewa, inunue vichwa vya treni, ni kwamba hatuwezi kufikia lengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huu tunajenga, nimwombe Mheshimiwa Waziri atuletee sheria Bungeni tena, tutengeneze utaratibu, wawekezaji binafsi nao waweze kununua vichwa vyao vya treni, wawekezaji binafsi waweze kununua mabehewa ili tutakapokuwa tumekamilisha ujenzi wa reli, kazi ianze moja kwa moja ili fedha irudi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye suala la ATCL tuna kila sababu ya kwanza, kuishauri Serikali yangu hili shirika tunalipa wakati mgumu sana, Engineer Matindi naamini kwamba anaweza akazeeka wakati muda bado siyo wa kuzeeka kwake kwa kazi kubwa ambayo tunampa. Haiwezekani Mheshimiwa Waziri shirika linakodishwa shilingi milioni 700 kwa mwezi linalipa Serikalini, eti kwa ajili imekodisha ndege za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndege hizo zikienda nje zinakamatwa kwa sababu ya madeni ya Serikali. Mimi ninaiomba Wizara hebu liangalie hili tufute deni la ATCL ambayo ni shilingi bilioni 113. Tukifuta deni hilo ndege hizi wakabidhiwe ATCL hata ikiwezekana kwa kukopeshwa badala ya kulipa hiyo shilingi milioni 700 kwa mwezi ambayo haijulikani wanalipa nini, walau wakope baada ya muda wakimaliza madeni ndege hizi ziwe za shirika na kazi naamini itaendelea, tukifanya hivyo tutakuwa tumelisaidia shirika hilo na ninaamini kabisa tutakuwa tumefanya kazi kubwa sana katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu mimi ni faraja ni furaha, sina sababu ya kuendelea kuchangia mengi, naamini kabisa Wanamorogoro tunakwenda kuona lami sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele yetu ya kuridhia Tume ya Katiba ya Usafiri wa Anga Afrika ya 2009.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuleta Azimio hili ndani ya Bunge lako tukufu. Kubwa zaidi niseme neno moja tu kwamba naunga mkono azimio hilo lakini naunga mkono maazimio na ushauri uliotolewa na Kamati ya Miundombinu kwa Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyotangulia kusema wachangiaji waliotangulia, kwa kweli tumechelewa na katika kuchelewa kwetu naamini kabisa yako mambo mengine mazuri ambayo tumeyakosa sisi kama nchi kwa kuchelewa kujiunga na Tume hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie faida. Mojawapo ya faida kubwa ni kwamba, kama nchi tutakuwa katika mawasiliano ya uhakika ya usafiri wa anga na usalama wa anga letu kwa kujiunga na Tume hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kama nchi tutakuwa tunapata faida kwa kupata teknolojia mpya za ulinzi na usalama wa anga letu kwa kujiunga na Tume hiyo kwa sababu moja. Kama Nchi Wanachama kuna fursa nyingi za mafunzo zitakuwa zinatolewa kwa ajili ya ulinzi wa anga letu. Kwa hiyo, sisi kama nchi tunaamini kabisa tutakuwa tumepata msaada huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema ndugu yangu Mheshimiwa Mlaghila kwamba, kama nchi kupitia Tume hiyo tutakwenda kukuza Kiswahili chetu. Vijana wetu wataweza kupata ajira katika nchi hizo ambazo ni wanachama wa Tume hiyo na tutakuwa tumekuza lugha yetu ya Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, hapa tumeelezwa kwamba CAG ndiye Mkaguzi Mkuu wa Tume hiyo ya usafiri wa anga wa Afrika. Kwa hiyo, kwa namna moja au nyingine kama nchi tumepata heshima kubwa sana ya kwamba CAG wetu ameweza kutambulika katika Afrika na kwenda kukagua Tume kubwa ya Anga. Tuna kila sababu ya kukubaliana na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika faida hizo pia nizungumzie hasara. Ni kweli kwamba tunazungumza kwamba tunapofungua anga Shirika letu la Ndege linaweza likamezwa, lakini naamini kwamba kadri tunavyokuwa tunakwenda, tutakuwa tunazidi kujipanua vizuri na tutalisaidia shirika letu, kwa sababu shirika letu pia linatakiwa litoke nje ya nchi na likafanye kazi katika nchi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutokujisajili wenzangu Wanayanga waliokwenda kule Algeria, walipata matatizo makubwa...

NAIBU SPIKA: Hivi hakuna mifano mingine mpaka huo tu? (Kicheko)

MHE, INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, unajua Simba wasingepata shida hiyo kwa ajili ya uzoefu wa mechi za Kimataifa, lakini Wanayanga walipata shida kubwa sana, almost three hours walibaki pale uwanjani nchini Algeria wakifuatilia taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe tu kwamba tusije tukaingia katika shida nyingine za hapa na pale na nyingine kama hizo. Turidhie na niwaombe na niwashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba jambo hili ni jepesi wala halina mashaka yoyote. Faida ni kubwa kuliko hasara ambazo tunajaribu kuzionesha. Niwaombe na nishauri Bunge lako turidhie na tuingie katika Mkataba huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, na mimi nitumie nafasi hii vilevile kwanza kukupongeza kwa uthubutu kwa jambo ambalo liko ndani ya moyo wako na uhitaji wako. Kubwa zaidi, sisi kama Wabunge wenzako tuko nyuma yako na tunaendelea kukuombea Mungu katika dini mbalimbali Mwenyezi Mungu aweze kukamilisha hiyo azma na Taifa liendelee kung’ara kupitia wewe.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha katika maeneo mbalimbali. Sisi Wabunge ni mashuhuda, tangu tumeanza kupitisha bajeti hapa za Wizara mbalimbali, kila Wizara iliyopitishwa kuna mambo makubwa yamefanyika.

Mheshimiwa Spika, na katika hili, hata katika Wizara ya Nishati kuna mambo makubwa; trilioni tatu na pointi si jambo dogo, ni jambo kubwa ambalo linahitaji uthubutu mkubwa, na Mheshimiwa Rais amefanya. Sasa hivi kazi kuwa iko kwa ndugu yangu tu, Mheshimiwa January, kuhakikisha kwamba fedha hii inayokuja ikafanye yale matokeo ambayo yanatakiwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii vilevile kukupongeza Mheshimiwa Waziri, Niabu Waziri, management ya Wizara na watendaji kupitia taasisi zote; REA, TANESCO, EWURA na kwingineko, kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya, lakini kwa bajeti ambayo imekuja mbele ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii vilevile kutoa pongezi kwa Meneja wangu wa TANESCO Mkoa wa Morogoo, Eng. Fadhili pamoja na Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Morogoro, kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, vilevile pongezi hizi ziende kwa Mkandarasi makini Stagic International Services ambaye ndiye amefanya kazi kubwa ya kupeleka umeme wa REA katika Halmashauri ya Morogoro. Alipewa vijiji 84, tunavyozungumza sasa hivi vijiji vyote 84 vinawaka; tuna kila sababu ya kupongeza katika hili.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi, nimwombe Mheshimiwa Waziri, bado kuna vijiji vitano ambavyo havikuwepo katika ule mkataba, mkandarasi ameongezewa, tayari ameshakwenda site, anachosubiri nadhani ni kuanza kazi. Niombe, katika zile kilometa mbili mbili ambazo tumeongezewa, nikuombe mfanye kwa haraka – mkandarasi huyu yuko idle – apewe hiyo kazi afanye ili tumalize, kama vile ilani ilivyosema; mpaka kufikia 2023 tukamilishie vijiji vyote nchini. Kwetu sisi Morogoro tunaamini tutakuwa tumekamilisha; nikupongeze sana.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii vilevile kukuomba, katika suala la kwenda kwenye vitongoji. Bado tuna changamoto kubwa, vitongoji ni vingi. Tunakushukuru kwa hivyo 15 lakini nikuombe, angalia uwezekano mwingine wa kuhakikisha kwamba umeme unawafikia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wana hamu kubwa ya umeme, na umeme ni nishati kubwa sana yenye uhitaji mkubwa kwa Tanzania. Nikuombe tu Mheshimiwa Waziri, angalia namna gani – tunakushukuru kwa hivyo 15 kwa sababu tuna kila sababu ya kuanza kushukuru kwa kile tulichopata – lakini tunahitaji vingine utusaidie.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri, Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati. Kuna uhitaji mkubwa katika TANESCO wa magari na watumishi. Naomba wasaidieni watumishi wa TANESCO Mkoa wa Morogoro wapate magari mapya ili waweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kuna vyanzo vikubwa vitatu vya Kihansi, Kidatu lakini tunakwenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Lakini mkoa ni mkubwa, wana uhitaji mkubwa wa watumishi pamoja na vitendea kazi. Nikuombe unapokuja ku-wind up uone jinsi gani ya kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii vilevile kumwomba ndugu yangu, Mheshimiwa January, kwenye hili suala la vinasaba, hebu tuliache lilipotulia, tusianze mambo mengine mapya. Ninachojua nyuma kulikuwa na changamoto nyingi, lakini tulipoingia kwenye TBS changamoto zilizokuwepo tunahitaji Serikali kuisaidia TBS. TBS ni kampuni ya Serikali, ina utaalamu mkubwa, inafanya mambo makubwa katika nchi. Kwa hiyo nikuombe libakie hapohapo, hatutaki kwenda kwingine. Kwa sababu tukienda kwingine tunaanza kwenda kufukua makaburi ambayo hayana sababu.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kupongeza jitihada za dhati za Mheshimiwa Rais anazozifanya katika kuendeleza Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa hili Mheshimiwa Rais alipolichukua lilikuwa kwenye wastani wa asilimia 30/32. Lakini leo tunapozungumza mpaka kufikia Aprili tumefikia almost asilimia 88; tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa hii anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Wizara, na hasa kwako ndugu yangu, Mheshimiwa January; ndani ya mradi ule kuna kitu kinaitwa CSR ambayo tangu mradi umeanza mpaka unafikia asilimia hiyo, hakuna fedha yoyote iliyokwenda katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini au Halmashauri ya Rufiji. Nikuombe, katika Bunge lililopita ambalo tulikuwa tunapitisha mpango wa bajeti kulikuwa kunasemekana fedha ile inatakiwa ipelekwe Tanga, fedha ile inatakiwa ipelekwe Dodoma, Kigoma na Lindi. Nikuombe, fedha ile ni ya watu wa Morogoro, ni haki ya watu wa Morogoro, tunaitaka watu wa Morogoro, tuna shida nyingi Wanamorogoro ambazo kupitia fedha hii tunaamini tutaweza kuzitatua au kusaidia Serikali kufikia katika yale maendeleo tunayoyataka.

Mheshimiwa Spika, sasa kama suala ni kujenga chuo hicho cha TEHAMA ambacho mnadhani wataalamu mnakihitaji kijengwe Morogoro au kijengwe Pwani kwa sababu tuna maeneo makubwa ya kuweza kufanya jambo hilo. Lakini vilevile Morogoro juzi tuliambiwa kupitia TAMISEMI kwamba tupeleke mahitaji yetu kwenye suala la afya; tumefanya. Na hapo TAMISEMI, tunaomba yaheshimiwe.

Mheshimiwa Spika, lakini bado kuna suala la elimu, kwa sababu katika mradi huu fedha ya CSR zinakwenda kwenye elimu, zinakwenda kwenye afya. Morogoro kama Morogoro kiwilaya ina halmashauri mbili, wenzetu mjini wana VETA, sisi Halmashauri ya Morogoro Vijijini hatuna VETA; tunahitaji VETA. Tunahitaji High School, tunahitaji mabweni kutokana na jiografia ambayo tunaishi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe, Waziri anapokuja ku-wind up aje na jambo la kutueleza Wana-Morogoro na Wanapwani. Najua jambo hili Mheshimiwa Mchengerwa hawezi kulisema, yuko kwenye Cabinet; je, tufanye nini kupata haki zetu sisi ambazo ni haki ya Kikatiba na ya kimkataba?

Mheshimiwa Spika, mara ya kwanza mlipeleka Dodoma kujenga uwanja, mkabdarasi kakataa kwa sababu anajua CSR ile ni ya Morogoro na Pwani. Sasa hivi kama mtapeleka huko maana yake tunazidi kuchelewesha fedha ile, mnazidi kuchelewesha maendeleo kwa Morogoro na kwa Pwani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe sana, najua wewe ni kijana makini, na bahati nzuri umekulia Morogoro, unaijua Morogoro, unajua shida za Wana-Morogoro, nakuomba simama kuhakikisha kwamba haki ya Wana-Morogoro na Pwani ya CSR inabaki katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, sitaki kusema maneno mengi, najua Mheshimiwa January ni mchapakazi, anajua kazi. Sasa nakuomba tu utakapokuja, sitaki kushika shilingi yako lakini nataka tu unipe majibu hayo na jioni baadaye mimi ni profesa unajua, nataka tukutane baadaye ili nikupe furaha na wewe ukafurahi baada ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru; naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya na kuona umuhimu mkubwa wa kutumbukiza fedha katika Wizara hii kuweza kuboresha miundombinu katika nchi ili kuendeleza uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Manaibu wote wawili na watendaji wa taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hii, lakini kubwa zaidi naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Meneja wa TANROAD, Mkoa wa Morogoro kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuboresha miundombinu katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii vilevile kumpongeza Mheshimiwa Rais na Wizara kwa kutenga fedha ili kujenga kiwango kwa kiwango cha lami kilomita 78 barabara ya Bigwa Kisaki, lakini vilevile kutenga fedha kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 11.6 barabara ya Ubena Zamozi – Ngerengere – Mvua – Kisaki - Matemele barabara ambazo zote hizi zinakwenda katika Bwawa la Mwalimu Nyerere pia inakwenda katika hifadhi kubwa namba moja katika Tanzania ya Julius Kambarage Nyerere.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulipata fedha ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Bigwa Kisaki kilomita 15, ilitangazwa, lakini kutokana na umuhimu wa barabara hii na usikivu wa Mheshimiwa Samia Saluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliweza kuifuta tenda hiyo na sasa tunatakiwa itangazwe kilomita zote 78.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Wilaya ya Morogoro ambayo inachukua majimbo matatu Jimbo la Morogoro Mjini, Morogoro Kusini Mashariki la mdogo wangu Babu Tale na Jimbo la kwangu la Morogoro Kusini wana umuhimu mkubwa sana wa barabara hii. Hata hivyo, huko barabara inakokwenda Serikali inakwenda kuongeza mapato kupitia utalii wa Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, lakini naamini kabisa Bwala la Mwalimu Nyerere lilikikamilika linaweza kuwa nacho ni kichocheo kingine cha utalii kwa sababu ni bwawa kubwa katika Afrika. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mwaka jana tumevumilia, mwaka huu ni imani yangu kabisa atakapokuja kufunga hoja yako atatuambia ni lini barabara hii itatangazwa ili apatikane Mkandarasi na tuweze kujenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa pongezi hizo, nipende kusema neno moja TANROADS wanafanya kazi kubwa. TANROADS wako kwenye barabara, TANROADS wako kwenye madaraja, TANROADS wako kwenye viwanja vya ndege na TANROADS wako mpaka kwenye ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, nini matokeo yake? Kuna changamoto ambazo zipo kwenye ujenzi wa barabara. Niombe kuishauri Serikali, kuna fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara, ni asilimia 42 tu, nini maana yake?

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, tunatengeneza barabara kama hatutoweza kuzifanyia matengezo ya mara kwa mara, maana yake hata zile barabara tunazotengeneza zitakufa na kama zitakufa maana yake zitaendelea kugharimu fedha nyingi kwenye Serikali na matokeo tutakuwa hatuwezi kusonga mbele. Kwa hiyo ombi langu kwa Serikali katika hili suala la fedha za matengenezo ya barabara, tuangalie uwezekano wa kupandisha kutoka asilimia 42 angalau tufike asilimia 70 ili barabara ziweze kutengenezwa vizuri na zipitike mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mimi ni mkandarasi, kuna changamoto katika watumishi, watumishi wengi wa TANROADS wamegawiwa kama kuna kusema kuna usimamizi wa mabwawa, viwanja vya ndege, wa madaraja na watumishi wa TANROADS ni wachache, matokeo yake, unafika mahali kwamba Mhandisi mmoja anasimamia miradi zaidi ya 10 mpaka 15, techinician mmoja anasimamia miradi zaidi ya 10 mpaka 15, nini kinachoweza kujitokeza? Kama wakandarasi wakiwa sio makini, wanaweza kufanya kazi zikawa sio nzuri na matokeo yake fedha tunazopeleka zitapotea bure. Kwa hiyo niiombe Serikali, itengeneze utaratibu wakutoa kibali cha ajira kwa TANROADS ili wapatikane wataalam wa kuweza kusimamia hii miradi ambayo ina fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine vilevile magari ni chakavu na vifaa vya kupimia ubora wa kazi za barabara ni vibovu. Naiomba Serikali nayo iangalie jambo hili ili value of money ambayo tunaipeleka iwe katika utaratibu unaokubalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuishauri Serikali, katika upande wa mizani mimi napata uwoga na mashaka, barabara zetu tunatumia fedha nyingi kuzitengeneza, lakini watumishi wa kwenye mizani ni watumishi ambao wako katika utaratibu wa mikataba. Huyu mtu ambaye unampa kazi kubwa ya kusimamia barabara unampa kazi kwa ajira ya mikataba, anaweza kushawishika na rushwa na ndio hayo tunayaona barabara zetu zinazidi kuharibika kadri tunavyotengeneza. Namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie utaratibu mpya wa kuajiri watumishi kwenye Kitengo cha Mizani wapate ajira ya kudumu wakiwa na uhakika kwamba sasa hiyo kazi wamekabidhiwa na naamimi kwamba wataisimamia katika utaratibu unaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine niombe vilevile kupata hawa watumishi wengine wa TANROADS utakuta wanaajiriwa kwa mikataba miaka mitatu, minne, wakati zinapokuja kutangazwa nafasi za ajira na wao wanaambiwa waende wakaombe. Wanapofika kule wanakosa, hii inawavunja moyo, lakini kubwa zaidi tunaajiri wengine wapya ambao wanakuja kuanza kujifunza kazi. Ningeomba Wizara wakati wa kuajiri watumishi, tuwachukue watumishi angalau wamekaa TANROADS kwa miaka mitatu au minne wakaajiriwa moja kwa moja, waende wakafanye kazi wanaoijua. Naamini kabisa tukienda hivyo tutafanya kazi mambo mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie upande mwingine wa TRC. Nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika uwekezaji wa reli, tunaona reli ya SGR loti zote sita ziko motomoto. Tumeona ukarabati mkubwa ambao unafanyika katika reli ya kati. Ombi langu kwa Serikali, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TRC, pamoja na menejimenti yake, tumeshuhudia hapa Wabunge wanalalamika kupanda kwa miradi kupitia riba katika miradi ambayo imefungwa na TRC katika SGR hakuna kupanda kwa mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini maana yake, ni ubunifu mkubwa ambao amefanya mtendaji huyu na timu yake. Sasa ombi langu katika hili Mheshimiwa Waziri, hii ni fedha yetu tumetoa, lakini naamini hata kwenye barabara fedha zetu tunatoa, sasa tufike mahali tuje katika utaratibu waliotumia TRC katika kufunga mikataba. Tufuate utaratibu huu pia katika kufunga mikataba ya barabara zetu, isije ikajipandisha zaidi, ikawa tunalipa riba ambazo hazina sababu na tunashindwa kusonga mbele kutengeneza barabara kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna changamoto TRC pamoja na uwekezaji mkubwa, ombi langu kwa Serikali, nilikuwa mfanyakazi wa Railway. Kipindi cha nyuma kulikuwa na mabwawa matatu pale la Igandu, Kidete pamoja na Kimangia. Mabwawa yale yalikuwa yanapunguza kasi ya maji na kwenda kufanya uharibifu wa reli katika kipande cha Kilosa na Kideti, ombi langu mabwawa yale yalikuwa chini ya Railway sasa hivi yako chini ya Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji, niombe Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji yaangalie utaratibu gani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri, kengele ya pili.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga hoja. (Makofi)