Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Charles John Mwijage (7 total)

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza:-

Visiwa vilivyopo katika Ziwa Victoria, Wilayani Muleba havina usafiri salama na wa uhakika, na vilevile Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi haina miundombinu stahili.

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka kivuko ili kurahisisha usafiri kati ya Visiwa vilivyopo Ziwa Victoria na Miji ya Mwambao ya Ziwa hilo Wilayani Muleba?

(b) Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu muhimu ikiwemo maghala ya kuhifadhia bidhaa katika Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi ili kuwavutia wafanyabiashara kutumia bandari hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Uchukuzi tayari imepeleka wataalam maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, hususan Wilaya ya Muleba kufanya tathimini ya maeneo yanayofaa kuwekewa huduma ya usafiri wa vivuko. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Ujenzi, imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa maegesho ya Muleba – Ikuza na Ngara – Nyakiziba.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kwa kuuona umuhimu wa huduma hiyo kwa wananchi wa maeneo hayo, inaangalia uwezekano wa kuboresha huduma za usafiri zinazotolewa na Kivuko MV Chato II – Hapa Kazi Tu, kwa kuongeza njia (route) ya kutoka Chato hadi kwenye visiwa vinavyoweza kufikiwa na kivuko hicho katika Wilaya ya Muleba.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekamilisha zoezi la utwaaji wa ardhi katika Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi kwa lengo la kujenga miundombinu muhimu ili kuwavutia wafanyabiashara pamoja na kutoa huduma za usafiri wa kuelekea maeneo mengine ya Ziwa Victoria kupitia Bandari hiyo. Hadi sasa kazi ya kuainisha mahitaji ya miundombinu inayofaa kujengwa katika Bandari hiyo imekamilika. Miundombinu husika ni pamoja na ghala la kuhifadhia mizigo, jengo la kupumzikia abiria, kantini na chumba cha walinzi. Utekelezaji wa mradi huu unatarajia kuanza katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022. Ahsante.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: -

Nchi yetu imekuwa na mipango mkakati wa kuzalisha mafuta ya kula kiasi cha kutosheleza soko la ndani.

(a) Je, ni kwa nini Serikali isiboreshe mpango ya kuzalisha mafuta ya mawese kimkakati kwa kuhamasisha kilimo cha zao hilo katika Mikoa ya Kagera, Tanga, Pwani, Katavi na Mbeya?

(b) Je, ni kwa nini Serikali isitumie mfumo wa kilimo kikubwa cha pamoja (block farming) ambapo Serikali hubeba gharama za awali na hatimaye sehemu ya gharama hukatwa kwenye mauzo ya Mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Charles John Mwaijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa ya Kagera, Tanga, Pwani, Katavi na Mbeya na Halmashauri za Mikoa hiyo inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa zao la michikichi katika maeneo yanayofaa kuzalisha zao hilo.

Uhamasishaji huo ni pamoja na kuzitaka Halmashauri hizo kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche bora ya michikichi aina ya Tenera, kutoa mafunzo kwa wakulima na wataalam kuhusu kilimo bora cha michikichi na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata mafuta ya mawese jirani na maeneo ya uzalishaji ili kusafirisha mikungu ya michikichi kwenda viwandani.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhamasishaji huo baadhi ya Halmashauri za Wilaya zimeanzisha vitalu vya kuzalisha miche bora ambapo Ngara (Kagera) imeanzisha kitalu cha miche 100,000; Mkuranga (Pwani) miche 20,000; Tanganyika (Katavi) miche 70,000 na Kyela (Mbeya) miche 26,600.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri zenye maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo cha michikichi inaendelea kuhamasisha kilimo cha mashamba ya pamoja (Block farming) ili kuzalisha kwa tija na kurahisisha huduma kwa wakulima. Baadhi ya Halmashauri hizo ni Uvinza (Kigoma) ekari 5,000 na Uyui (Tabora) ekari 12,000. Uhamasishaji unaendelea kwa mikoa mingine yenye sifa hizo.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali isishirikishe sekta binafsi katika kilimo cha umwagiliaji ili kutimiza Ajenda 1030?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mwijage, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika utekelezaji wa miradi yake mbalimbali katika sekta ya kilimo, imeendelea kushirikiana bega kwa bega na sekta binafsi. Kwa muktadha huo, katika miradi ya umwagiliaji ambayo Serikali inatekeleza kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kuishirikisha sekta binafsi katika hatua mbalimbali za miradi hiyo ili kufikia malengo ya Agenda 10/30. Aidha, katika mwaka 2022/2023 Serikali imepanga kukarabati na kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika eneo la hekta 95,000, ambapo jumla ya kandarasi 55 zimetolewa kwa sekta binafsi. Mpaka hivi sasa jumla ya mikataba 21 ya Wakandarasi imesainiwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza: -

Je, ni kwanini katika Tarafa ya Kamachumu mlalamikaji hulazimishwa kumgharamia mahabusu kwa kumsafirisha kwenda na kurudi rumande?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Polisi (Police Force and Auxiliary Service Act) Sura ya 322 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na Kanuni 353 na 354 ya Kanuni ya Jeshi la Polisi (Police General Order) zinazosimamia watuhumiwa/mahabusu walioko kwenye Vituo vya Polisi, utaratibu wa kuwasafirisha watuhumiwa/mahabusu kwenda Mahakamani hutekelezwa na Jeshi la Polisi. Pia jukumu la kuwasafirisha watuhumiwa/mahabusu toka rumande Gerezani kwenda Mahakamani ni jukumu la Jeshi la Magereza kwa mujibu wa Kifungu cha 75 cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 ya mwaka 1967 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha mlalamikaji kulazimishwa kugharamia usafirishaji wa mtuhumiwa/mahabusu kwenda na kurudi rumande ni kukiuka Sheria na Kanuni zilizopo na kinatakiwa kuachwa mara moja. Wizara imefanya mawasiliano na Wakuu wa Vyombo vyetu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP) ili wawaelekeze wasaidizi wao ngazi za Mikoa na Wilaya kuzingatia sheria hiyo. Ninashukuru.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Meli ndogo ya abiria Muleba pamoja na kutumia meli ya MV Victoria kujaribu masoko ya nchi za Uganda na Kenya?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa ujenzi na uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua hitaji kubwa la usafiri wa wananchi Wilayani Muleba hususani waishio katika Visiwa. Kwa kutambua hitaji hilo, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imetenga meli moja iitwayo MV Clarias kutoa huduma katika Visiwa vya Godziba Wilayani Muleba na Visiwa vya Gana Wilayani Ukerewe. Meli hiyo iliyokuwa imeanza kutoa huduma katika visiwa hivyo tarehe 3 Machi, 2023 ilisimama tarehe 22 Machi, 2023 baada ya kupata hitilafu za kiufundi. Huduma hizo zitaendelea kuanza tena mwanzoni mwa mwezi Mei, 2023 baada ya matengenezo kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu huduma za safari za kwenda Uganda na Kenya, MSCL inatarajia kuanza safari hizo kwa kutumia meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu mara baada ya ujenzi wake kukamilika. Meli ya MV Victoria haitaweza kutumika kwani ndiyo meli pekee inayotegemewa katika utoaji wa huduma za usafiri kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo na ni msaada mkubwa kwa wakazi wa ukanda huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI K.n.y. MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isikae na taasisi za afya za kidini Wilayani Muleba ili kupunguza changamoto zilizopo katika kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Jimbo la Muleba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ina vituo sita vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na mashirika ya kidini. Hospitali tatu za Lubya, Ndolage na Kagondo, Kituo cha Afya kimoja na zahanati mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao utaratibu wa kukaa na hospitali teule za wilaya kupitia bodi ambazo zimejumuisha wataalam wa kutoka ngazi ya mkoa na halmashauri husika. Bodi hizo hukutana kila robo mwaka kwa ajili ya kupitia taarifa za utendaji pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wakutoa huduma.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Fibre Speed Boat mbili zilizofunikwa kama ambulance ili kusaidia Wananchi wa Visiwa 39 vya Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mhe Charles John Mwijage, Mbunge wa Jimbo la Muleba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeandaa mpango mkakati utakaowezesha maeneo magumu kufikika kama visiwani na maeneo mengine kupata huduma za usafiri wa dharura pindi utakapohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huo umeainisha vifaa vya usafiri vitakavyotumika kusafirisha wagonjwa ikiwemo usafiri wa anga yaani air ambulance na usafiri wa maji yani boat ambulance. Aidha, Mpango huo unatarajiwa kukamilika Disemba 2023 na kuanza utekelezaji katika mwaka wa fedha 2024/2025 na Wilaya ya Muleba itapewa kipaumbele, ahsante.