Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mohammed Maulid Ali (2 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MOHAMMED MAULID ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kwa mara ya kwanza kabisa niweze kuongea kwenye Bunge lako Tukufu. Kwanza kabisa naomba niwashukuru wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki, pamoja na Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniwezesha na kuniamini kuwa Mbunge katika jimbo hilo ili niweze kuwatumikia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika hili utajikita katika mambo matatu; kwanza kilimo, pili viwanda na tatu barabara. Imeelezwa hapa kwamba zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania wanategemea kuendesha maisha yao ya kila siku kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, imeelezwa vilevile katika Mpango huu kwamba kiasi cha viwanda 8,477 vimeanzishwa ili kuchochea ajira kadhaa zilizokusudiwa katika nchi. Mchango wangu upo kwenye suala la tatu la barabara. Mambo haya matatu yaani barabara, kilimo na viwanda vinakwenda sambamba, kama kimoja kikiwa kimetetereka vingine viwili havitakwenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu vijijini haziko katika hali nzuri, wasiwasi wangu sijui kama viwanda hivi vitafanya kazi vizuri wakati malighafi au raw materials zinatoka vijijini.

Kwa hiyo, basi niungane na Wabunge wengine waliochangia kwamba TARURA iongezwe fedha ili na wao waweze kuzitengeneza barabara hizi ili huu mzunguko ambao tunauzungumzia hapa uweze kuwa vizuri, otherwise viwanda hivi vitashindwa kufanya kazi kama tulivyotoka huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mchango wangu kwa leo ni huo tu. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MOHAMED MAULID ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa ruhusa ya kuweza kuchangia siku ya leo Ijumaa, siku tukufu, asubuhi hii.

Kwanza ningependa kutoa shukrani au pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri Mdogo au Naibu Waziri Mheshimiwa Masauni pamoja na timu nzima ambayo imejikita kutengeneza bajeti hii. Kwa kweli, ni bajeti ambayo tunaweza kusema haijawahi kutokea, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu nianze kwenye TARURA. Napenda sana kuwashukuru viongozi wetu, pongezi kwa Serikali ambayo imehusisha vilio vya Wabunge moja kwa moja kuhusu fedha za TARURA, hii imetupa faraja kubwa sana. Ningependa kuwatoa hofu wananchi waelewe kwamba fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya TARURA ambayo inatoka kwenye mafuta inakwenda kutuhusisha sisi kama Wabunge moja kwa moja na kutupa ujiko kule majimboni kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningewashauri sana Wabunge wenzangu tusiingilie sana katika kuwaambia wananchi kwamba fedha hii itasumbua katika matumizi au kuongeza gharama, si kweli, fluctuations katika pesa za mafuta ni jambo la kawaida kila siku na halileti athari yoyote kwenye matumizi. Kwa hiyo, tujikite zaidi kuwaelimisha wananchi kama Serikali ilivyotusaidia sisi kutuchangia, ili na sisi twende kifua mbele majimboni na sisi tuisaidie kuwaelimisha wananchi kwamba hili jambo litatusaidia sote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa nataka kuzungumzia suala la ajira 8,000 ambazo Serikali…, samahani ni ajira milioni nane ambazo zimeainishwa kwenye ilani yetu ya uchaguzi. Kwa kupeleka fedha hizi TARURA zile ajira milioni nane ambazo zimezungumzwa katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi sasa nina hakika zitatekelezeka sawasawa. Ndani ya kipindi kifupi tutaweza kuona viwanda vyetu vipo tayari, malighafi kule vijijini kwa ajili ya viwanda hivi zitakuwa tayari, lakini hata barabara na viungo kati ya viwanda na upatikanaji wa malighafi zitakuwa tayari. Hongera sana Mama Samia kwa maono ya mbali kwa maslahi ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kulizungumza kuhusu fedha shilingi milioni 500 kwenye majimbo yetu. Fedha hizi kwa kweli, zitakwenda kusaidia tena zitakwenda kusaidia sana katika majimbo haya kwa sababu sisi kama Wabunge sasa zitatupa nguvu na zitaweza kutusaidia hata katika chaguzi zinazokuja mbele za mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Majimbo yetu yote ya Uchaguzi matatizo yake yanafanana na kilio kikubwa cha wananchi ni barabara kama yalivyo majimbo mengine yeyote Tanzania Bara na sisi tuna changamoto hii kule Zanzibar. Ningependa kuwahakikisha kwamba Halmashauri zetu na Manispaa hazina uwezo wa kutengeneza barabara hizi haitapendeka kama tutakuwa huku barabara zake zinaonekana vizuri kwetu kule hakupitiki, lakini Mbunge ni yule yule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyo Mbunge mwingine yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tunamwomba sana Mheshimiwa Mwigulu, Rais wetu ni msikivu sana na yeye ni mwelewa na viongozi wetu Mawaziri na hata hao Manaibu Waziri, nao ni wahanga vile vile wa jambo hili, ingawa midomo yao wameipiga zipu, lakini ukweli wote tunaathirika kwa pamoja lazima tuseme ukweli. Ikimpendeza Mheshimiwa Waziri suala hili nasi tuweze kusaidiwa ili twende kifua mbele. Huko majimboni kwetu wananchi wanafuatilia sana vikao hivi, tena wanavifuatilia kwa nguvu zote, wanatuuliza maswali mengi kuhusu fedha hizi ambazo kwakweli hatuna majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaamini na wao vile vile majimbo yao yatanufaika, lakini kwa kweli upande wetu ni mgumu kidogo. Nomba Serikali yetu sikivu chini ya uongozi wa Mama Samia, Waziri Mkuu, Waziri Mwigulu, Manaibu Mawaziri ambao kama nilivyosema baadhi yao ni wahanga wa tatizo hili, watufikirie sisi Wabunge wa Majimbo ya Zanzibar na sisi tuyahudumie majimbo haya ili yaweze kupitika muda wote hasa wakati wa kipindi cha mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kuzungumza…

T A A R I F A

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Karibu kwa taarifa Mheshimiwa.

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji juu ya jambo alilolizungumza, huko Majimboni kwao Zanzibar wananchi wanawauliza maswali na akasema hawana majibu juu ya hii fedha ya shilingi milioni 500 ya kila Jimbo. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji majibu ya Majimbo ya Tanzania Bara na Majimbo ya Zanzibar majibu yake ni mamoja, sote ni Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna Mbunge wa Zanzibar wala wa Bara. Ahsante.

MWENYEKITI: Unapokea taarifa Mheshimiwa Mohammed Ali?

MHE. MOHAMMED MAULID ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema nimeipokea taarifa hiyo kwa mikono na miguu pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kidogo kuhusu suala la ndugu zetu wa Bodaboda. Kwa kweli kwa nia njema kabisa Serikali imefanya kuwasaidia vijana hawa ili waweze kujikwamua kimaisha. Hii ndio nia njema kabisa ya Serikali ya Mama Samia. Tatizo moja tu ambalo ningependa kutoa tahadhari, kwanza kuna Mbunge mmoja amenifilisi kuhusu hizi bodaboda ambazo hazina makosa ya jinai. Vituo vyetu vya polisi sasa hivi havifagiliki havipitiki, kipindi cha mvua vichafu kwa sababu ya bodaboda hizi. Sasa ikiwezekana kama sheria inaruhusu maana yake siwezi kushindana na sheria…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Sasa naomba nimwite Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali.

MHE. MOHAMMED MAULID ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)