Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Francis Leonard Mtega (1 total)

MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na TANROADS kujitahidi kukarabati barabara ile, lakini nyakati za masika imekuwa ikikata kabisa mawasiloiano; na kwa kuwa, amekiri kwamba, ni muhimu sana kwa kusafirisha mazao na isitoshe wananchi wale wanaitegemea sana barabara ile kwa huduma mbalimbali za kijamii kupeleka wagonjwa hospitali, lakini bidhaa mbalimbali za matumizi ya kila siku. Je, Serikali haioni kwamba, sasa ipewe kipaumbele ili ujenzi wa barabara ile kwa kiwango cha lami uanze haraka iwezekanavyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mkoa wa Mbeya tuna uwanja mkubwa wa ndege wa kimataifa na Mheshimiwa Rais amenunua ndege kubwa, Dreamliner na barabara ile inapita kandokando mwa lango kuu la Kusini kuingia Hifadhi ya Ruaha (Ruaha National Park), sasa watalii wangepitia lango lile la Kusini kwa urahisi kabisa. Je, Serikali haioni kwamba inakosesha pato la Taifa hasa pesa za kigeni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwa sababu ya umuhimu wa hiyo barabara ndio maana tayari taratibu za kuanza kujenga kwa kiwango cha lami zimeshaanza na zimeshatengwa tayari bilioni 3.38 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mbarali kwamba, kwenye bajeti zinazofuata nina hakika barabara hii itatengewa fedha zaidi, ili iweze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya umuhimu huu kama alivyosema kwenye swali lake la pili kuhusu uwanja wa ndege nasema ndio maana tayari hii barabara kwa Serikali kutambua umuhimu wake ikiwa ni kupokea wageni kutoka uwanja wa Songwe, lakini na kuwapeleka kwenye mbunga, ndio maana tayari taratibu za Serikali zimeanza za kukamilisha ama kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.