Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Francis Leonard Mtega (13 total)

MHE. FRANCIS L. MTEGA Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Rujewa – Madibira – Mafinga (kilometa 151) utaanza kwa kuwa upembuzi yakinifu umekamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Rujewa – Madibira – Mafinga yenye urefu wa kilometa 152.1 ni Barabara ya Mkoa ambayo ipo chini ya Wakala wa Barabara (TANROADS). Sehemu ya barabara hii, yani Rujewa hadi Madibira yenye urefu wa kilometa 97.1, inahudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Mbeya na sehemu iliyobaki kipande cha Madibira hadi Kinyanambo chenye urefu wa kilometa 55, kinahudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa. Barabara hii ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 na ahadi za Viongozi Wakuu wa Nchi kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii ambayo inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya mpunga na mahindi, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii. Wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi, Wizara kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea kufanya matengenezo ya barabara hii ili ipitike majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, barabara hii imetengewa kiasi cha shilingi milioni 757 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na shilingi bilioni 3,380,000,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mikakati gani wa kumaliza mgogoro kati ya Hifadhi ya Ruaha na Wakulima na Wafugaji wanaozunguka Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali iliunda Kamati iliyojumuisha Mawaziri kutoka Wizara nane kwa ajili ya kufuatilia na kutatua migogoro ya ardhi nchini. Migogoro hiyo iliyofanyiwa kazi na Kamati husika ni pamoja na migogoro kati ya wakulima na wafugaji wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Mheshimiwa Spika, Kamati hiyo imefanya tathmini ya migogoro hiyo na kutoa mapendekezo ambayo yameshatolewa maamuzi na Baraza la Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji utakaoanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine na wananchi ambao maeneo yao yana changamoto za migogoro hiyo kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji Ruduga – Mawindi ili kuwatua ndoo kichwani akina mama wa Mbarali?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Mbarali wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza, Serikali ilianza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Luduga – Mawindi kwa lengo la kuhudumia vijiji sita vya Kangaga, Mkandami, Itipingi, Manienga na Ipwani kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni. 9.66. Utekelezaji wa mradi huo umepangwa kwa awamu (lots) tano. Kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa awamu zote ni ujenzi wa banio la maji, mtandao wa bomba jumla ya kilometa 139, matanki sita yenye ujazo wa lita 150,000 moja, lita 100,000 matatu na lita 75,000 mawili na vituo vya kuchotea maji 119.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa banio la maji, mtandao wa bomba jumla ya kilometa 54 na tanki la kuhifadhia maji la lita 150,000, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 12. Kwa kazi zilizokamilika wananchi wa Kijiji cha Kangaga wameanza kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 utekelezaji wa mradi utakamilika na huduma ya maji itapatikana katika vijiji vyote na kunufaisha wananchi zaidi ya 26,000. (Makofi)
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, ni lini viongozi wa Kitaifa wataanza kutembelea nchi za nje mahsusi kwa ajili ya kutafuta masoko ya mazao hususan mpunga na mahindi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ziara za Viongozi wa Kitaifa nje zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi rafiki. Kutokana na matunda yanayopatikana kupitia ziara za Viongozi wa Kitaifa, Wizara imeendelea kushauri Mamlaka kutembelea nchi za kimkakati kwa kuzingatia maslahi ya Tanzania katika nchi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wetu wa Kitaifa tayari wamefanya ziara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na zile za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Ni katika muktadha huo, mwezi Mei, 2021, Wizara iliratibu ziara ya kikazi ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya, ambapo pamoja na mambo mengine alifanikiwa kutanzua, vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiforodha (NTBs) vilivyokuwa vikiwakabili wafanyabiashara wakiwemo waliokuwa wakisafirisha mahindi kwenda Kenya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya ni miongoni mwa wanunuzi wakubwa zaidi wa mahindi ya Tanzania kutokana na sifa zake, ubora wake na bei yake nzuri. Hali kadhalika, Wizara pia iliratibu ziara ya Mheshimiwa Rais Samia nchini Burundi, Rwanda na Uganda, ambapo pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Rais alitumia fursa hiyo kutafuta pia masoko ya bidhaa za mazao kutoka Tanzania ikiwemo mahindi, mpunga na maharage. Aidha, katika ziara ya Burundi, Mheshimiwa Rais aliongozana na ujumbe wa wafanyabiashara ambapo kulifanyika kongamano la biashara kwa lengo la kukuza wigo wa biashara kati ya Tanzania na Burundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha kuvipatia umeme wa REA Vitongoji na Vijiji vilivyobaki katika Jimbo la Mbarali?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbarali ina jumla ya vijiji 102. Ni vijiji 20 tu ambavyo bado havijapatiwa umeme. Vijiji hivyo 20 vinapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA mzunguko wa Pili awamu ya Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu unaendelea kutekelezwa na Mkandarasi ambaye ni M/S Electrical Transmission and Distribution Construction and Maintenance Co. LTD. Mkandarasi amekamilisha kazi ya usanifu wa kina, upimaji, uandaaji wa michoro na anaendelea na manunuzi ya vifaa pamoja na kusimika nguzo katika maeneo ya mradi. Gharama ya mradi ni Shilingi bilioni saba na utekelezaji unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa vitongoji, Serikali imeshaanza utekelezaji wa miradi ya ujazilizi unaolenga kufikisha umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara awamu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na Vitongoji vya Jimbo la Mbarali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine, Serikali imefanya uhakiki na kuainisha uwepo wa vitongoji takribani 37,610 visivyokuwa na umeme Tanzania Bara na inakadiriwa takribani shilingi trilioni saba zitahitajika ili kukamilisha mahitaji ya umeme katika vitongoji hivyo vyote.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuboresha Hifadhi ya Taifa Kitulo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hifadhi ya Taifa Kitulo ni hifadhi ya kipekee ambayo huwezi kuifanananisha na hifadhi nyingine hapa nchini. Hifadhi hii ina utalii wa maua, maporomoko ya maji, ndege wa aina mbalimbali na vivutio vingine. Wizara kwa kutambua hilo imeendelea kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi. Miundombinu hiyo ni pamoja na kuimarisha barabara zilizomo ndani ya hifadhi, kuanzisha huduma za malazi na chakula, kuongeza mazao mapya ya utalii ndani ya hifadhi kama vile utalii wa kutumia baiskeli, utalii wa kutembea kwa miguu na utalii wa kupanda vilima.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo maeneo ya malazi na shughuli za utalii kama vile utalii wa farasi, utalii wa kubembea na kamba na mazao mengine ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii na idadi ya siku za kukaa hifadhini na hivyo kuongeza mapato zaidi.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya maboresho makubwa ya miundombinu katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imepeleka vifaa na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 418 kwa ajili ya jengo la huduma za dharura (EMD), pamoja na mashine ya kisasa ya X-ray ya shilingi milioni 155 hospitali ya Wilaya ya Mbarali.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 69.95 katika bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Mbarali ambayo imetengewa shilingi milioni 100, ahsante.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, lini Serikali italigawa Jimbo la Mbarali na kuwa na Halmashauri mbili ili kusogeza huduma karibu na wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis leonard Mtega Mbunge wa Jimbo la Mbarali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, halmashauri huanzishwa kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa, Sura ya 287 na 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014. Mwongozo huo umeainisha vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kuanzisha Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria hii, hatua ya awali inahusisha kupata ridhaa ya vijiji, Kamati za Maendeleo za Kata, Baraza la Madiwani la Halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC). Baada ya hatua hii, maombi hayo yanawasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya uhakiki na tathmini na kuwasilishwa kwa mamlaka husika ili itoe uamuzi.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI haijapokea maombi ya kuigawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali. Hivyo, nashauri taratibu za uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala zifuatwe.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara ya mkato kati ya Wilaya za Mbarali na Chunya ili kupunguza gharama za usafiri na kukuza biashara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa umbali kutoka Wilaya ya Chunya hadi Wilaya ya Mbarali kwa kupitia Wilaya ya Mbeya ni mrefu ukilinganisha na umbali wa kupitia barabara ya mkato kati ya Wilaya ya Chunya na Mbarali. Serikali inatambua changamoto ya kutokuwepo kwa barabara hiyo na kusababisha adha ya mzunguko mrefu kwa wananchi wa wilaya hizo mbili ndani ya mkoa wa Mbeya na kusababisha gharama kubwa kwa wananchi wanaosafiri kati ya wilaya hizo mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa uhitaji wa barabara hiyo ya mkato, Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mbeya kupitia kikao chake cha tarehe 09 Januari, 2023, kilitoa mapendekezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuipandisha hadhi barabara ya Njiapanda – Sangambi – Shoga na kufungua barabara mpya kutoka Shoga Wilaya Chunya hadi Udindilwa katika Wilaya ya Mbarali inayokadiriwa kuwa kilomita 22.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mapendekezo hayo kuwasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, aliiagiza Kamati ya Kitaifa ya kupanga barabara katika hadhi stahiki (NRCC) kufika mkoani Mbeya na Kamati hiyo ilifika mnamo tarehe 24 Februari, 2023 na kutembelea barabara zilizoombwa kupandishwa hadhi ikiwemo barabara ya Njiapanda – Sang’ambi – Shoga na kipande cha Shoga - Udindilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya Kamati yaliwasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na yanachambuliwa na uchambuzi ukikamilika taarifa itatolewa. Kama barabara hiyo itakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi, itakuwa barabara ya mkoa na itahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuboresha Kituo cha Afya Igurusi ili upasuaji uweze kufanyika katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Igurusi kilijengwa mwaka 1966 na kuanza kutoa huduma katika ngazi ya zahanati hadi ilipofika mwaka 2010 kilipopandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya. Aidha, miundombinu ya kituo hiki ni michache na iliyopo ni chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imefanya uchambuzi na kupata vituo vya afya vikongwe 193 nchini kote ambavyo vinahitaji kufanyiwa ukarabati na kuongezewa majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki umefanyika kutambua vituo vya afya vikongwe na Serikali iko kwenye mchakato wa kutafuta fedha ili kuvikarabati vituo hivyo.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, lini Kata za Miyombweni, Malilo, Songwe na Luhanga zitawekwa anuani za makazi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 8 Februari, 2022 Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ufanyike kwa njia ya operesheni kwa usimamizi wa Wakuu wa Mikoa na kwamba utekelezaji wake ukamilike mwezi Mei, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ulifanyika kwa tija na ufanisi mkubwa ambapo hadi Mei, 2022 Halmashauri, Kata, Vijiji, Mitaa, Shehia zote nchini zilikuwa zimefikiwa. Aidha, utekelezaji ulifanyika kwa kuzingatia miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kutotoa anwani za makazi maeneo ambayo ni hatarishi yasiyoruhusiwa kwa makazi mfano, mabondeni, kwenye vyanzo vya maji, maeneo oevu, maeneo ya hifadhi, maeneo ya wazi na maeneo ya hifadhi ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya Kata za Miyombweni, Malilo Songwe na Luhanga zipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ahsante.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga minara ya simu maeneo yasiyo na mawasiliano hususan Kata za Ipwani, Miyombweni na Igava?

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilibaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali yakiwemo Ipwani, Miyombweni na Igava ambapo Serikali imempata mtoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata ya Ipwani kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigitali. Aidha, Kata za Miyombweni na Igava zitaingizwa katika miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ORAN M. NJEZA K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, ni lini Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rujewa inaenda kuwa Mamlaka kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mhesimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014, vigezo na taratibu zinazopaswa kufuatwa ni pamoja na maombi rasmi kuwasilishwa Ofisi ya Rais TAMISEMI. Ofisi ya Rais TAMISEMI itakapopokea maombi rasmi ya Halmashauri ya Mji Mbarali itafanya uchambuzi na tathmini ya kukidhi vigezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kumekuwa na changamoto za uendeshaji na tija za kuwepo kwa baadhi ya Mamkaka za Miji Midogo. Ofisi ya Rais TAMISEMI inafanya uchambuzi na kubaini tija ya kuendelea kuwepo au la, kwa baadhi ya Mamlaka za Miji Midogo.